Saturday, February 27, 2016

KISOMO CHA AROBAINI(40) PART1

Asalaam Aleiykum

Nini Arobaini? Arobaini ni nne ilofungana na sifuri, kwa wale walo bahatika kupata elimu ya hisabati wanajua nini maana ya number 4, lakini inapofatiwa na sifuri maana yote ya number 4 inabadilika, kwanini ikabadilika itabidi uhudhurie siri ya sifuri ili ujue kwanini inabadilika, sifuri siri yake ni kama daraja(Bridge)yenye kuunganisha kisicho kuwepo kukifanya kiwepo, kukionesha kilichojificha kiweze kuonekana, sifuri ni kama kiza kipo lakini hakionekani, inapotiwa sifuri ndio hesabu zinabadilika.
Leo tuko katika kisomo cha Arobaini, tunachambua uwepo wa kisomo hichi na maana yake, kwanini kikaletwa? Jee kina maana gani katika mazingira ya (Dini) kwanza kabisa napenda uelewe kisomo cha Arobaini ni sehemu ya (Dua) ya wewe kutoa Shukurani zako kwa Mollah wako, kama ilivotajwa kwenye sura ya (Al-Ahqaf)aya ya 15.

وَوَصَّيۡنَا ٱلۡإِنسَـٰنَ بِوَٲلِدَيۡهِ إِحۡسَـٰنًا‌ۖ حَمَلَتۡهُ أُمُّهُ ۥ كُرۡهً۬ا وَوَضَعَتۡهُ كُرۡهً۬ا‌ۖ وَحَمۡلُهُ ۥ وَفِصَـٰلُهُ ۥ ثَلَـٰثُونَ شَہۡرًا‌ۚ حَتَّىٰٓ إِذَا بَلَغَ أَشُدَّهُ ۥ وَبَلَغَ أَرۡبَعِينَ سَنَةً۬ قَالَ رَبِّ أَوۡزِعۡنِىٓ أَنۡ أَشۡكُرَ نِعۡمَتَكَ ٱلَّتِىٓ أَنۡعَمۡتَ عَلَىَّ وَعَلَىٰ وَٲلِدَىَّ وَأَنۡ أَعۡمَلَ صَـٰلِحً۬ا تَرۡضَٮٰهُ وَأَصۡلِحۡ لِى فِى ذُرِّيَّتِىٓ‌ۖ إِنِّى تُبۡتُ إِلَيۡكَ وَإِنِّى مِنَ ٱلۡمُسۡلِمِينَ 
Na tumemuusia Mwanaadamu afanye wema kwa wazazi wake, Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu na akamzaa kwa taabu, Na kubeba (Huko)Mimba yake hata kumuwachisha ziwa(kipimo chake)ni miezi thalathini, hata anapofikia baleghe yake na akawa Mwenye Umri wa miaka Arobaini(Alo Mwema)husema "Ewe Mollah wangu niwezeshe nishukuru neema zako ulizo nineemesha mimi na wazazi wangu, Na niwezeshe nifanye vitendo vizuri unavyo vipenda, Na unitengenezee watoto wangu, kwa yakini nina tubu kwako, Na hakika mimi ni miongoni mwa waliosilimu(Wenye kunyenyekea kwako).
Hiyo ndio Arobaini maneno yaliyomo kwenye aya hii moja ni maneno mazito na mimi nitafanya kazi ya kuyanyanyua kidogo kidogo ili tupate kuyafikisha kwenye kilele cha vichwa vyetu, umo kwenye kisomo cha Arobaini usisimame ukapinga tu bila yakua na taaluma yoyote, kwanza zama ukiona hakuna faida basi una uhuru wa kupinga.
Aya inaanza kwa wasia, Tumemuusia Mwanadamu kuhusu Wazazi wake wawili(Baba na Mama) Hususan Mama, kwanini ikawa Mama? Na Wasia huu umepewa Lini?. Yapitie maandiko haya labda yaweza kuwa na faida na wewe, Unaweza kugundua maana ya kuachiwa Radhi, ukaelewa kumbe nikienda kinyume na Wasia wa Mwenye enzi Mungu basi huenda nikakosa Radhi za Wazee wangu.
endelea part 2

KISOMO CHA AROBAINI(40) PART 2

Asalaam Aleiykum

Naam, Tumemuusia mwanadamu kuhusu wazee wake wawili, wasia huu umetokea wapi? Wasia huu unapewa kwa njia ya ufunuo, ni neema ya fahamu(Knowing) inokujia mara tu unapofikia Umri fulani, na hususan una shikana sana na Mama yako kutokana na ile (Bond) yako ya kukaa tumboni mwake kwa muda wa miezi (9) Mama yako kachukua Mimba hiyo kwa Tabu na misukosuko mizito, kwa vile (Body Chemical)yake inavobadilika kutokana na kukubeba wewe ndio Mara katamani (Mbirimbi) mara anaomba apewe(Udongo)siku katamani (Papa)alooza na kesho lazima apewe achari ya (Ndimu) na Tafrani zikizidi anaomba bora aletewe (Mavi ya Kuku)yatamsaidia kukata kichefuchefu, hivyo ndivyo Mama anavoteseka kwa ajili yako, na wewe uko (Bukheir)umetulia tumboni.
Tumboni huko kila kitu unafanyiwa, Mpaka pumzi unavutiwa. Huku nje Mama yako mzigo unamtesa takriban kwa muda wa miezi tisa, leo ukiombwa (Shilingi unakunja Uso)Tahadhari sana, ikisha zinafatia pirika za kuushusha mzigo, Machungu na dhiki anazozipata ndio kila kitu kinachafuka, mpaka Roho yake inatetemeka kwa juhudi za kukuzaa wewe.
Sasa Nini Arobaini? Arobaini kwa njia ya maneno ni Kisomo cha mzee yule kutoa Shukurani kwa kuvuka Salama kwenye (Daraja). Lakini zile siku zenyewe za Arobaini ndizo zilobeba maana ya hiyo (40).Wazee wenye Elimu ya Hisabati waligundua kwamba (Number 4)ni Namba ilobeba Furaha, Walipoichunguza sifuri(Zero O)wakagundua imejaa (Nothingness), Nikisema (Nothing) Nakusudia Nini?, Nakusudia Sifuri Peke yake inakua imetulia haina kitu, haina papara, haina thamani lakini imebeba kitu kikubwa chenye hazina ya utulivu, Kumbuka kwenye utulivu ndiko kwenye kutokea kila kitu.
Sifuri mpaka ikatulia ndio inaleta maana ya (Full circle)kukamilika, ndio maana utaona kwenye masahihisho ya Mitihani Mwanafunzi anatiliwa (Zero) unajua maana ya (Zero) Zero maana yake Mwanafunzi hajafahamu, baada ya jitihada zetu zote za kumsomesha tumeshindwa kumtoa kwenye Kiza (Sifuri)kumpeleka kwenye Nuru, kwa hiyo kwa ufupi sifuri inabeba utulivu na kwa Mwanafunzi ina maanisha hakushughulika au kuchangamsha Akili yake kuwa (Active)katika kusoma, lakini kwenye (Currency) ikiongezwa (Zero) mambo yanakua mengine, hesabu zinabadilika, au mfano mwengine mwanzo ulikua huna kitu(Sifuri)sasa umetajirika(From nothing to something) hayo ndio maelezo ya sifuri kwa ufupi ukitumia njia ya maneno.
Tumeizungumza Number 4 na number Zero O sifuri tumeziunganisha tumepata Arobaini(40)ndani yake tumepata Furaha na Utulivu, Ama Arobaini kwa vitendo siri yake ni Utulivu, inachukua siku Arobaini Roho na Mwili(Body)kuwa (Stable)kutulizana katika harakati za kimaumbile. Vipi?
Tuanze na Mama, Imetajwa kuwa anabeba Mimba kwa Tabu na anazaa kwa Tabu, (Chemical)Mwilini zinachafuka, Roho inatikisika, kila kitu kwenye mwili wa huyo Mama kinapepesuka, Akili inakua katika msukosuko mkubwa, hali hii inachukua siku (40) mambo hayo yote kutulia. Ndio maana wazee wetu wa (Africa) wakawa wanawapumzisha wazazi kwa siku (40) hapo zamani, na kama hajapumzika ndio siku hizi imegundulika anapata kitu kinaitwa(Post Natal depression).
Ndio Maana kama mzazi hajapumzika baadae matatizo yanajitokeza, Mara utasikia chumbani kabeba mtoto anambembeleza mwanae mwenyewe mara unasikia "Ntamtupa chini"kumbe maskini ana tafrani za Akili, Wenzetu wameligundua hilo wanawapa watu wao matibabu, lakini katika jamii yetu toka tulipoondosha Arobaini tumekula hasara, ndio utasikia Mke wangu toka kazaa kabadilika, kumbe Mtu ana Tafrani za (Mind) yake hapati msaada, hujamsaidia, maskini ana hangaika hajui afanye nini, Hiyo ndio Arobaini kwa Mama, Nini Habari ya Arobaini kwa Mtoto? Hapa kuna Siri itabidi uijue!!
Endelea Part 3

KISOMO CHA AROBAINI(40) PART 3

Asalaam Aleiykum

Pata habari hii ili iweze kukusaidia katika safari yako ya kujitambua wewe nani?, Umetokea wapi?, Na unakwenda wapi?.
niliposema ijue siri nilikusudia kukufahamisha (Daraja)lenye kuunganisha (Body)Mwili wako na Roho yako.Daraja lenyewe ni hiyo (Hewa)yako unayovuta yaani (Oxygen)Nyuma ya hiyo (Oxygen)ndio kuna hiyo Roho(Nisiseme nyuma ukaanza kufasiri nyuma ya ukuta, nyuma ya kichwa)nimetumia neno hilo kuashiria jambo ambalo pengine utaligundua ukishajitambua (wewe nani).
Sasa inapoungana Roho hiyo na (Body)ndio inaitwa Uhai, Na ikiachana na huo Mwili inarejea katika hali yake ya mwanzo Mauti na baina yake ndio kuna kitu kinaitwa(Life)au kuishi milele, Tafauti ya viwili hivyo kimoja kinaoza(Body)na cha Pili (Roho) ni yenye kubaki daima(Eternal).
Sasa hivi huwezi kutafautisha lakini kuna wakati au siku ya kufa kwako ndio utakuja kujua alaa kumbe mimi sio (Body) ila mimi ni ile Roho ilokua ikizungumzwa, wakati huo unatenganishwa na (Body)wakati huo utaona (body)yako kumbe mimi nilikua miaka yote (70)nikiishi kwenye nyumba ile(Body), Naam ndio maana utakuta kitu cha mwanzo mtoto akizaliwa anatizamwa jee anavuta pumzi(Daraja analo)kalia japo kidogo, katoa sauti huyu, lakini kinachotizamwa zaidi ni (Breath)Pumzi au hiyo(Oxygen), Mtoto huyu anaweza kuhema Mwenyewe.
Na vilevile siku ya kufa kwako wanakuja kutizama jee kashabomoa (Daraja)huyu, tegemeo zima la Uhai ni hiyo (Hewa)ndio yenye kusema bado nipo au nishatoweka(Daraja lishavunjika)na sasa niko upande wa pili. 
Ama kuhusiana na huyo Mtoto mpaka daraja kuwa madhubuti yaani (Chemical) zake kutulia inachukua siku hizo (40). Wacha sasa tukuguse wewe Mtu mzima(Baba au Mama la Miraba saba)wewe umehusiana vipi na hii (40). Tumeona kwa Mama ni kitulizo, Kwa Mtoto ni ku(Solidify with the Body), Sasa kwako wewe vile vile ni kama ulivopewa taarifa kwenye hiyo (aya) nilotaja mwanzo, unapofika Umri wa miaka (40)unategemea utulie, (Unaondoshewa Dhamana)mpaka hapa sasa ukiendelea itakua ni jeuri, Sasa hivi huna sababu tena za kukufanya uendelee kucheza, (Nature)inakusuta(Chemical)zishatulia, ujana ushatoweka, nikisema ujana ushatoweka itabidi nifafanue kidogo, kwenye (Bible)kuna msemo huu (Three scores and ten)maana ya (score) ni kumi mbili, kwa hiyo (score) maana yake ni (20) kwa hiyo (Score)tatu ni sitini(60)na ile kumi ndio unapata (70), kwa hiyo kama umefika miaka (40)ina maana ushakula nusu na ushei hivi(Score)Mbili, umebakisha hiyo (30) tu, hata nusu huna tena.
Mwanzo vitu vyote vilikua vinakwenda (North) na sasa vinashuka (South)wakati unazidi kukuacha, ikiwa bado hujazinduka unaendelea kukera mbinguni na huku ardhini unaendelea kutia wanaadamu tafrani, watu wakikuona wanasema Baba yake fulani bado hajatulia, ukijikuta katika hali hiyo ndio unatakiwa ujisomee mwenyewe kisomo cha Arobaini ili upate kuzinduka.
Arobaini maana yake zinduka, kuwa na Furaha ya maisha na utulie, sasa turejee kwenye Tafsiri. 
Inaendelea aya ya (15)sura ya (Ahqaf)kwa kusema."Hata anapofikia Umri wa miaka (40)husema(Mja Mwema)Niwezeshe" Limetumika neno niwezeshe, ili uondoshewe jeuri ya kuji nasib kuwa kila kitu umefanya kwa uwezo wako, umepata kwa nguvu zako, "Niwezeshe nishukuru Neema zako ulizo ni neemesha" Neema hazihesabiki, (Pengine umenipa neema kuwa wazee wangu wa hai na afya zao)umenipa mali na watoto. Sasa wakati huu nilofikia niwezeshe nifanye matendo mazuri unayoyapenda, Na pia sasa nishapata watoto basi naomba kama ulivo niongoza mimi kwenye kheri, na Wanangu Mollah wangu niongozee, Na mimi  sasa natubu kwenye Enzi yako Mollah wangu, na kwako wewe na (Surrender)na kuwa Muislam kamili.
Hiyo ndio Arobaini kwa mtu mzima, unatakiwa utulie uwache ulo nayo ya ufisadi, balaa na mijidhanbi ili upate kuwa Muislam kamili. Na ukifa pia Imani zetu zina matumaini kuwa baada ya siku arobaini Roho yako ndio imepata utulivu na sisi huku tunasoma na kukuombea dua upate Shufaa kutoka kwa Mollah wako, akipokea Mollah wetu sawa na kama hakupokea pia hiyo ni uwezo wa khiyari yake. Hiyo ndio maana ya Kisomo cha Arobaini kwa hiyo watu wakisoma huna sababu ya kuwashangaa au kuwakataza tena, Kwani wanaomba dua na kumshukuru Mollah wao.