Monday, August 1, 2016

MAPENZI NI SIRI YAKO PART 1

Asalaam Aleiykum

Umepata kujiuliza kwanini mapenzi yakawa siri?. Jee unajua sababu yake?.Basi jiulize swali hili kwa njia ya kutaka kujua na hapo utakua umepanda mbegu ambayo haina kikomo katika kukua kwake, Haina mwisho katika kutoa Miti na Matunda yake. Napenda Uelewe nikizungumza neno Mapenzi sikusudii chembe yako ya mapenzi ya matamanio, sizungumzii upya wowote wa mapenzi unayo yafahamu wewe, au kama natoa (style)upate kupendwa na wanawake au wanaume, au wengine wakadhani natoa mbinu za upatikanaji wa mapenzi ya matamanio, hilo sio kusudio langu, kusudio langu ni kukufahamisha kuwa yapo mapenzi ya aina nyengine na kama utayapata daima utakua furahani, dhiki zitakuondoka, kila siku kwako itakua siku ya (Eid).
Mapenzi ninayokufahamisha leo ni jambo la siri, Kwanini ikawa siri kwa sababu ukiizungumza tu(Ushaipoteza)  ladha yake inapotea, utamu wake unakatika, uchu wake unaondoka, kwa wale wenye kujua siri ya Mapenzi haya hawasemi chochote kwani wanajua siri ikisemwa inakua sio siri tena. Basi na mimi leo sitakwambia kwa uwazi hayo mapenzi ila ntaashiria ukakutane nayo Mwenyewe.
Basi kwanza ntakujulisha mapenzi uloyazoea ya Mwanamme na Mwanamke, au mapenzi ya kupenda nyumba yako, mapenzi ya kupenda farasi, gari na vitu vidogo vidogo ambavyo vimetajwa kwenye Quraan aya ya (14) Al-Imran.
زُيِّنَ لِلنَّاسِ حُبُّ ٱلشَّهَوَٲتِ مِنَ ٱلنِّسَآءِ وَٱلۡبَنِينَ وَٱلۡقَنَـٰطِيرِ ٱلۡمُقَنطَرَةِ مِنَ ٱلذَّهَبِ وَٱلۡفِضَّةِ وَٱلۡخَيۡلِ ٱلۡمُسَوَّمَةِ وَٱلۡأَنۡعَـٰمِ وَٱلۡحَرۡثِ‌ۗ ذَٲلِكَ مَتَـٰعُ ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا‌ۖ وَٱللَّهُ عِندَهُ ۥ حُسۡنُ ٱلۡمَـَٔابِ 
"Watu wametiwa huba(Mapenzi)ya kupenda wanawake na watoto na marundi ya dhahabu na fedha, Na Farasi wanaotunzwa vizuri, na wanyama na mashamba, Na hayo ni (kwa ajili ya)matumizi ya maisha katika dunia, Na kwa Mwenye enzi Mungu ndiko kwenye marejeo mazuri"
Mapenzi yako ya aina mbili, aina ya kwanza ndio hiyo ilotajwa hapo juu ulotiwa nayo, unayo tayari, huwezi kuikwepa ni muhimu kwa ajili ya maisha yako ya kidunia, bila ya hivyo maisha yako yatakua kama maiti, upo tu duniani unakera watu, kila kitu kwako kibaya, kutokana huna hata hayo mapenzi ambayo ni haki yako kuwa nayo, ambayo Mollah kampa kila mja wake, wewe hata hilo hukupata, ukifikia hali kama hiyo inafaa ujiulize kwanini?.
Na aina ya pili ya Mapenzi ndio hiyo siri yenyewe, sasa kabla ya kwenda mbele hebu tuirejee aya tutizame, ikisha tujiulize kwanini ikataja Wanaume na sio wanawake?. Ikiwa wewe unanifatilia vizuri utagundua ama kwa Wanawake wanayo tayari (Nature) ya (Love)Mapenzi, Mwanamke kwake rahisi ku(surrender)yuradhi kukiri na kumtii mpenzi wake, hiyo ndio hulka ya Mwanamke, anatuonesha vipi mapenzi yake yalivo katika kuwalea na kuwapenda watoto wake, Mwanamke kajaa Moyo wa mapenzi, Mwanamke hana shaka katika penzi lake, na hajui hata inakuaje ila yeye kajaa mapenzi, ndio maana kwa Mwanamke rahisi kwake kwenda kwenye hilo penzi la siri.
Kwanini ikawa hivyo?
Kwa sababu Mwanamke Mapenzi kazaliwa nayo, Mapenzi yako Moyoni, Na hiyo ni siri yake wala haisemi, anao uwezo na ujuzi wa kumpenda Mtu akanyamaza kimya, Na hiyo ndio tunapata ishara ya siri ya Mapenzi (alopewa mwanamke).
Ama kuhusu Mwanamme(Yeye alotiwa)Penzi, Penzi hilo lipo (Kichwani) na wala sio moyoni, Ndio maana "Mwanamme mara huku mara kule", Mara kapenda hichi mara kapenda kile, na hiyo ndio tafauti yao. Kwa hiyo kawaida hiyo inatujulisha Mwanamke yeye yuko tayari kuchupa kwenye Bahari ya Mapenzi ya siri, Ndio maana utaona wao hawendi vitani, (Wao sio Violence) kwa hiyo katika kwenda kwenye Penzi la siri Mwanamke yeye njia yake ni(One Way)(from the heart to the beyond). Lakini Mwanamme yeye ni (Two way)Lazima urudi chini, lazima utoke kwenye kichwa uende moyoni, lazima upate (Faminine Quality).
Ndio Maana utaona "Wacha Mungu"wapole, (Very Loving).
Kwa Mungu hakutakiwi Ujabali, Kwa Mungu hakutakiwi Kuua, Hakutakiwi(Violence)huko ni salama juu ya salama, hakutakiwi chuki, Hakutakiwi hamaki wala hasira.
Sasa leo wacha nikushike mkono labda utachupa na mimi kwenye hiyo bahari ya Mapenzi ya siri ili na wewe upate neema yake. Lakini ili usije ukaweka tamaa au kupanda kiburi kuwa utafanikiwa itabidi nikujulishe kuwa mapenzi haya wanayapata watu wa aina mbili kama ilivosema Quraan sura ya (Fussilat aya ya 34 na 35)
وَلَا تَسۡتَوِى ٱلۡحَسَنَةُ وَلَا ٱلسَّيِّئَةُ‌ۚ ٱدۡفَعۡ بِٱلَّتِى هِىَ أَحۡسَنُ فَإِذَا ٱلَّذِى بَيۡنَكَ وَبَيۡنَهُ ۥ عَدَٲوَةٌ۬ كَأَنَّهُ ۥ وَلِىٌّ حَمِيمٌ۬
Mambo mazuri na mabaya hayawi sawa, ondosha (ubaya unaofanyiwa kwa mema)tahamaki yule ambaye baina yake kuna uadui atakua kama ni jamaa (Yako)mwenye kukufia uchungu.

وَمَا يُلَقَّٮٰهَآ إِلَّا ٱلَّذِينَ صَبَرُواْ وَمَا يُلَقَّٮٰهَآ إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ۬ 
Lakini (Jambo hili)hawatapewa ila wale wanaosubiri, wala hawatapewa ila wenye hadhi (Bahati)kubwa (Kwa Mwenye enzi Mungu)
Ipate maana ya maneno haya katika part 2

MAPENZI NI SIRI YAKO PART 2

Asalaam Aleiykum

Aya ya 34 inaanza hivi "Mambo mazuri na Mabaya hayawi sawa" Mambo mazuri ni nini?, ndio hayo Mapenzi ya siri, ondosha Ubaya unaofanyiwa kwa mwema, Tahamaki yule ambaye baina yake kuna uadui atakua kama ni jamaa yako mwenye kukufia uchungu.
Hiyo ndio (Power of Love) sio kuwa umempa mtu pesa au gari au nyumba. Na wewe ukigeuka panga la Mapenzi, basi yule adui yako machozi yatamiminika akikuona tu, atapigana kwa uchungu, yuko tayari kufa kwa ajili yako.
Aya ya 35 inaendelea kuwataja, "Lakini (Jambo hilo)hawatapewa ila wale wanaosubiri" (Na)Wala hawatapewa ila wenye hadhi(bahati)kubwa kwa Mwenye enzi Mungu. Sasa hawa wenye kusubiri ni wepi na wenye hadhi ni wepi, hapo ndio tunaingia katika sehemu yetu ya pili ya hilo (Penzi Lenyewe).
Nini Mapenzi?
Mpaka leo hajatokea awezaye kulijibu swali hilo, halijibiki kwa njia ya maneno, hakuna lugha inayoweza kutafsiri, ile ya Mwanzo tumepewa jawabu na Mollah wetu, lakini hili la pili ndio hiyo siri yenyewe inayokupa ladha na furaha, inakupa na utulivu, inakupa maisha, sasa shuka chini ya huo mti uoneshwe hili shina, huu mzizi, na hii ndio mbegu yenyewe, itabidi uichukue mbegu hiyo uipande mwenyewe.
Nini Mapenzi?
Mapenzi ni (Mystic Force) inayotokea kwa mollah wako na kukuvaa, ni hali unayoipata ya kukumiminia (Bliss)Raha juu ya Raha, hali ambayo haina kikomo, sasa unayapataje Mapenzi haya.
Hapo juu wametajwa watu wa aina mbili wenye kusubiri na wenye hadhi.
Ama tafauti ya wawili hawa wenye kusubiri ni wale wenye kufanya mambo kidogo kidogo, Na wale wenye hadhi ni wale wenye kuendea kheri hizo kwa haraka. Vipi inakua hali hiyo ya Mapenzi ya siri?.
Endelea part 3

MAPENZI NI SIRI YAKO PART 3

Asalaam Aleiykum

Mapenzi hayo ya siri yanapatikana kwa jitihada, kwa sababu yale ya aina ya kwanza umepewa na Mwenyewe, haya ya pili inatakiwa uyatafute Mwenyewe, Na hiyo ndio maana ya (Ibada)umepewa nusu na nusu uitafute, kwa sababu sasa hivi penzi lako ni (Fragment) vipande vipande, unatakiwa ufanye juhudi uliunganishe, kwanini ikawa vipande vipande, wacha nikujulishe ili upate kulijua penzi la siri likoje, na ukiliunganisha lina faida ipi. Ntakuonesha kwa mfano wa Quraan Al-Ahzab(35)
 إِنَّ ٱلۡمُسۡلِمِينَ وَٱلۡمُسۡلِمَـٰتِ وَٱلۡمُؤۡمِنِينَ وَٱلۡمُؤۡمِنَـٰتِ وَٱلۡقَـٰنِتِينَ وَٱلۡقَـٰنِتَـٰتِ وَٱلصَّـٰدِقِينَ وَٱلصَّـٰدِقَـٰتِ وَٱلصَّـٰبِرِينَ وَٱلصَّـٰبِرَٲتِ وَٱلۡخَـٰشِعِينَ وَٱلۡخَـٰشِعَـٰتِ وَٱلۡمُتَصَدِّقِينَ وَٱلۡمُتَصَدِّقَـٰتِ وَٱلصَّـٰٓٮِٕمِينَ وَٱلصَّـٰٓٮِٕمَـٰتِ وَٱلۡحَـٰفِظِينَ فُرُوجَهُمۡ وَٱلۡحَـٰفِظَـٰتِ وَٱلذَّٲڪِرِينَ ٱللَّهَ كَثِيرً۬ا وَٱلذَّٲڪِرَٲتِ أَعَدَّ ٱللَّهُ لَهُم مَّغۡفِرَةً۬ وَأَجۡرًا عَظِيمً۬ا 
Bila shaka Wanaume wenye kuufata (vizuri) Uislam, na wanawake wenye kuufata (vizuri) Uislam, Na Wanaume wanoamini (vizuri), Na Wanawake wanoamini(Vizuri), Na wanaume wanotii, Na wanawake wanotii, Na Wanaume wasemao kweli, Na wanawake wasemao kweli, Na wanaume wanosubiri, Na wanawake wanosubiri, Na wanaume wanonyenyekea, Na wanawake wanonyenyekea, Na wanaume wanotoa sadaka, Na wanawake wanotoa sadaka, Na wanaume wanofunga, Na Wanawake wanofunga, Na wanaume wanaojihifadhi tupu zao, Na wanawake wanaojihifadhi, Na wanaume wanomtaja Mungu kwa wingi, Na wanawake wanomtaja Mwenye enzi Mungu kwa wingi, Mwenye enzi Mungu amewaandalia Msamaha na ujira mkubwa.
Hapo utaona wametajwa wale wenye mapenzi lakini ya tafauti tafauti, huyu anatoa sadaka, huyu anatii, huyu anaamin, huyu anahifadhi tupu, wote hao wanafanya hayo kwa ajili ya mapenzi. Nini habari yako wewe kama utachanganya mambo hayo yote, siri yake ni kupata msamaha, na tunza yake ni kupata huo ujira mkubwa, ukisamehewa unaipata (Pepo), Na hapo ndio utakapo ipata (Mapenzi ni siri yako)jaribu kukusanya uone inakuaje, ipate hali kama hiyo ukutane na mambo ya ajabu.
Na hapo ndio unapata kujua kumbe Uislam ni Dini ya Mapenzi na amani, kwa vipi na imesemwa wapi.Siku zote si Mnasema (Love is Blind)kweli hamjakosea, lakini kwenye Uislam Mwenye enzi Mungu kayafanyia nini hayo mapenzi?. 
Quraan (Baqarah aya ya 2 mpaka ya 3) Ipate siri hii ya Mapenzi ili na wewe ufanikiwe.
 ذَٲلِكَ ٱلۡڪِتَـٰبُ لَا رَيۡبَ‌ۛ فِيهِ‌ۛ هُدً۬ى لِّلۡمُتَّقِينَ
"Hiki ni kitabu kisichokua na shaka ndani yake, ni uongozi kwa (wapenzi)wamchao Mwenye enzi Mungu".
Ukishampenda Mollah wako ni lazima upate uongozi ili usije ukapotea, usije ukajigonga na makuta, usije ukachaniwa majuba ndio unapewa hichi kitabu ili kikuongoze, Kwa sababu hayo wayafanyayo hao walotajwa hapo juu yote ni kwa ajili ya mapenzi.
Sasa wamefanyaje hata wakayapata mapenzi hayo.
ٱلَّذِينَ يُؤۡمِنُونَ بِٱلۡغَيۡبِ وَيُقِيمُونَ ٱلصَّلَوٰةَ وَمِمَّا رَزَقۡنَـٰهُمۡ يُنفِقُونَ
Ambao huyaamini  ya (Siri)yasionekana Na husimamisha Sala na hutoa katika yale tuliyowapa.
Kuamini ni jambo rahisi sana, kuamini ni kazi mtu mwengine kakufanyia wewe unakubali, lakini tafsiri sahihi ni lazima uende (deep)ukatafute siri za huo upande wa pili, lazima ujishughulishe sana kutaka kujua kuna nini kwa Mollah wako, ufanye jitihada zako ukipata uthibitisho wa mambo yalofichwa huko japo chembe hapo utakua huzini tene, hudhulumu tena, hupiti kuua, unachorudi nacho kutoka upande wa pili ni kusimamisha Sala, kumbuka kuna kusali na kusimamisha sala, Kwanini ikawa hivyo?, kilosimamishwa lazima kwanza kilikua kimekaa au kulala, sasa wewe kwanini unakisimamisha? kwa sababu Wingi wa Wanaadamu siwenye kusimamisha sala, Maana ya kusimamisha Sala kujaa na mapenzi kwa ajili ya Mollah wako, huwezi kuiba ikisha ukenda kusali, huwezi kupokea rushwa halafu ukasali, huwezi kuzini ikisha ukasimamisha sala, haiwezekani ukaweka mapesa (Bank)huku unasimamisha sala. Utakua unamdanganya Mollah wako,(Bado Umelala) Mwenye kusimamisha sala amejaa mapenzi na akimaliza sala anatoa kile alichopewa na Mwenye enzi Mungu, Unaona Mollah wetu alivojaa mapenzi anatupa uhuru, anatupa uhai, anatupa mali na mengi mengineyo, kwa hiyo yoyote yule Mwenye mapenzi lazima awe na athari ya kutoa, tena athari hiyo haihitaji maonesho ni siri yake na kila akitoa anasikia furaha ya mapenzi kwa wale awapao. Na hiyo ndio siri ya mapenzi unasisitizwa uipate. hapo utaona vipi (Mapenzi yanavo miminika kutoka Mbinguni).