Saturday, September 10, 2016

MAJAALIWA YA KUONA NA KUSIKIA PART 1

Asalaam Aleiykum

Zimekujia Fahamu za vitendo  viwili hivi vya kuona na kusikia,
Umepata angalau kujua kwanini unaona?, na uwezo huu unatokea wapi, unaijua fadhila ya kusikia na uzuri wa jambo hilo?, na nini habari yako wewe kama moja katika hilo litaondoshwa utakua katika hali gani, Uwe wewe (Tajiri wakupindukia) ichukuliwe tu (Jaala)hii ya kuona au kusikia ujitizame vipi unakua, ushawahi wewe kuumwa macho yakawa hayaoni au masikio yameziba ukawa husikii japo kwa siku moja unakuaje, vitu kama hivi tunavichukulia ni kama jambo jepesi sana, tunachukulia kama tuna vimiliki vitu hivi wala hatuna wasiwasi hata wakujua vinatokea wapi na kwanini tunapewa?.
Unakumbuka lini wewe umewahi kuamka bila ya kukumbushwa  ukamshukuru Mollah wako?, Ukashukuru tu Alhamdullilah(ahsante)Mollah wangu kwa kunipa tena siku hii ya leo kuona na kusikia, Imeshakufikia habari ile siku mambo mawili haya yatakapoondoshwa ukawa huoni wala husikii yaliyomo kwenye Ulimwengu huu. Basi ikiwa msahaulivu au una (Kiburi) fulani isome darsa hii upate kufungua macho yako, kwani wakati huu ulo nao  macho yako wazi lakini hayaoni.
Napenda kukumbusha uelewe jambo hili la kuona na kusikia imekua katika ihsan kubwa Mollah wako alizokufanyia  za kukufanya ukaribie Ufalme wake wakati ukiwa hai katika ulimwengu huu. Amekupa wewe (Sifat Basiran) Na akakuongezea (Wasifat Samian) Akakupa zaidi na (Sifa ya Aliim)Mwenye kujua, na pia kukupa wewe kiumbe hizo nguvu (Sifa ya Qawwiy) Amekupa mambo mengi nimeyataja hayo kwa uchache ili ujue vipi Mapenzi ya Mwenye enzi Mungu juu yako wewe Kiumbe. Kiumbe wewe huna malipo ila kumsahau, huna jengine isipokua ufisadi, Basi kabla ya kuzama kwenye Bahari hii ya kuona na kusikia wacha kwanza tuangalie nini kinatokea kabla ya kulala na kuondoshewa huko kuona na kusikia.
Endelea part 2

MAJAALIWA YA KUONA NA KUSIKIA PART 2

Asalaam Aleiykum

Nini Kinatokea?

Katika maumbile yako ya kawaida mambo haya yanatokea ikiwa hujijui au huyajui, Kimaumbile Tabia uliyoizoea ni kama ile ya taa, kuwaka na kuzimika, ila unaona ukisema hivyo watu watakushangaa kwa hiyo umechagua jina la kudumu unaita kulala na kuamka.
Lakini kama utakua Mwanasayansi wa dini basi utakuja kugundua Kulala huko na kuamka kwako kuna (Process)kubwa lazima uipitie ndio uvipate viwili hivyo na vyengine, Maajabu yanotokea hapo ni makubwa, ni taabu kuyaeleza unaweza kuyaona lakini inataka ifanyike jitihada kubwa kuyashuhudia, Inatakikana upatikane ustahamilivu wa hali ya juu kuiona hali hiyo yenye kutisha, hali ambayo ikikutokea inaambatana na khofu ya umauti.
Kuishuhudia hali hiyo kunahitaji maandalizi makubwa yenye kuambatana na ushujaa, sisemi ni rahisi yaweza kukuchukua miaka au miezi, au pengine masiku kadhaa tu ukaliona tukio hilo kwa ukamilifu, Na zaidi yategemea Majaaliwa na Ridhaa kutoka kwa Mollah wako.
Usije ukaona mbona huyu anazungumza Mambo ya ajabu, au analeta mafunzo mepya, mambo yapo, yametajwa ndani ya (Quraan fussilat aya ya 53)
سَنُرِيهِمۡ ءَايَـٰتِنَا فِى ٱلۡأَفَاقِ وَفِىٓ أَنفُسِہِمۡ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَهُمۡ أَنَّهُ ٱلۡحَقُّ‌ۗ أَوَلَمۡ يَكۡفِ بِرَبِّكَ أَنَّهُ ۥ عَلَىٰ كُلِّ شَىۡءٍ۬ شَہِيدٌ 
"Tutawaonesha (Ukweli)wa Alama zetu katika Nchi(Mbingu)za Mbali na katika Nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je haikutoshi kwa Mollah wako kuwa yeye ni mjuzi wa kila kitu".
Wanasayansi wamekwenda kwanza (Nje)Mbinguni kama ilivosema (Quraan)Na Wacha Mungu wao wamekwenda kwanza ndani kwenye Nafsi kuipata Yakini, Na wewe nenda usiogope, hee mpaka unakufa hutaki kujua chochote cha upande wa pili.
Naam hivyo ndio hali ya mambo ilivyo, Sasa turudi nyuma ili tuendelee na darsa yetu ya kuona na kusikia.
Endelea part 3

MAJAALIWA YA KUONA NA KUSIKIA PART 3

Asalaam Aleiykum

Siku zote nasisistiza uielewe sifa ya Jaala ni yenye kuja na kuondoka, Na sifa hii inatosha kukuthibitishia kuwa Kiama kipo na kinakuja, ima utakua hai siku hiyo au utafufuliwa lakini siku hiyo ipo na inathibitishwa na sifa hii ya Jaala. Basi yachunguze wewe mambo makubwa makubwa kuhusishwa na sifa ya (Temporary).
sifa kama zipi?(1)sura ya Nabaa,
 أَلَمۡ نَجۡعَلِ ٱلۡأَرۡضَ مِهَـٰدً۬ا
Je hatukuifanya ardhi kuwa (kama)Tandiko. Sasa kwanini likaitwa tandiko, kwa sababu wakati mwengine tandiko linaondoshwa au kuwekwa pembeni, na hayo yanafanyika katika ardhi ima kwa kudidimia au kwa mtetemeko wa ardhi.
وَجَعَلۡنَا نَوۡمَكُمۡ سُبَاتً۬ا 
Na tukaufanya usingizi wenu kama kufa. Na aya hii ndio inaigusa aya yetu moja kwa moja kwa kuondoshwa hayo majaaliwa ya kuona na kusikia.Ikisha unarejeshewa mambo hayo.
وَجَعَلۡنَا ٱلَّيۡلَ لِبَاسً۬ا
Na tukaufanya Usiku kama guo(Mnalofunikwa)kama utazingatia nyakati za kuzama jua utaona vipi kiza kinavo kuvaa na kukuondoshea nuru ya kuona. 
وَجَعَلۡنَا ٱلنَّہَارَ مَعَاشً۬ا 
Na Tukaufanya mchana Kama kufufuka. Hayo yanataka mazingatio pale mwanzo unaporejeshewa kuona na kusikia ndio utajua vipi inakua huko kuona na kusikia.
وَجَعَلۡنَا سِرَاجً۬ا وَهَّاجً۬ا 
Na Tukaifanya taa ingarayo na yenye joto kubwa.hilo ndio Jua lenye kutupa vitamin na nyenzo zengine za maisha, kama chakula na kadhalika. Hayo ni machache ambayo ni (Temporary)huja na kuondoka kutokana na anavopanga Mollah wako.
Ukichunguza maneno yangu utagundua siku zote nasisitiza kuwa sifa hii ya jaala ni yenye kuja na kuondoka, Na ikiwa umepewa Akili ya mazingatio basi pia litakuongezea nguvu za imani yako pale utakapoona kumbe sifa hii pia imo kwenye nafsi yangu, Ukajua kumbe yupo Mwenye kunipa sifa hii ya kuona na kusikia.
إِنَّا خَلَقۡنَا ٱلۡإِنسَـٰنَ مِن نُّطۡفَةٍ أَمۡشَاجٍ۬ نَّبۡتَلِيهِ فَجَعَلۡنَـٰهُ سَمِيعَۢا بَصِيرًا 
Hakika tumemuumba Mwanaadamu kutokana na mbegu ya Uhai iliyochanganyika,( ya Mwanamme na Mwanamke)ili tumfanyie mtihani, kwa hiyo tukamfanya Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
Sasa inakuaje majaaliwa haya, Nini kinatokezea?.
Wacha nikuchukue kwenye safari hii ambayo unaiogopa sana lakini huna budi ni lazima uende, si umeambiwa tukaujaalia huo usingizi wao kama kufa, Basi wacha na sisi tuanzie hapo kuhusu yale mambo niloyataja huko mwanzo ambayo yanaondoshwa taratibu(Slow motion)au labda uwe umechoka ndio unazimika ghafla. Lakini (Process)za kawaida ziko, wacha nikupe mfano ili uone jambo gani la mwanzo hilo lenye kuondoshwa taratibu?kwenye hiyo (Process).
Basi Jitizame katika kusinzia utaona nguvu zinakuishia, ndio maana utaona kama umekaa unataka kama kuanguka,(Balance)huna, nguvu zinachukuliwa taratibu, Na Jambo la pili kuondoshwa ni huo uwezo wa kuona kidogo kidogo huo unaondoshwa mpaka kupotea.
Na jambo la tatu uwezo wa kusikia nao unaondoshwa ndio maana utaona chakacha au disco inapigwa yeye kalala anakoroma, "Wewe unashangaa sauti hii huyu anakoroma" kumbe mwenzio pale kama maiti, (Tukaujaalia usingizi wao kama kufa)unaendelea kushangaa ngoma hizi na sauti hii na huyu kalala chini ya (speaker)bado hasikii kitu huyu.
Na Jambo la Mwisho kuondoshwa ni hiyo (Knowing) au ita (consciousness), hapo tena Mwanaadamu unakua kama maiti. Sasa kwa wale Wacha Mungu au wanasayansi wa ndani wao wanafanya maandalizi na kuomba ridhaa ya Mollah wao ili wapewe uwezo wa kushuhudia (Process) yote hii huku wamebakishiwa hiyo (Knowing) au (Consciousness)vile vitatu vinatoweka hichi kimoja kinabakia na hiyo ni Fadhila kubwa kutoka kwa Mollah wao.
Ukijaaliwa kuipata hali kama hiyo unakua umefuzu katika Ulimwengu na huko uendako kwa Mollah wako.
Sasa nini Habari yetu sisi viumbe wa kawaida ukipata bahati ya kushuhudia, kama utakua makini ni rahisi kwako kushuhudia kuamka kwako, (Process) ni ile ile, ila sasa inakuja kinyume chake, katika kuamka lile liloondoka mwisho ndio lenye kuja mwanzo, Yaani hiyo (Knowing) au (Consciousness)au (Fahamu) Napenda uelewe wewe upo ila viloondoshwa ni hivyo vitendea kazi vya kuona na kusikia, kwanini nikasema wewe upo, kwa sababu jiulize nani Mwenye kuona ndoto, ukipata jawabu endelea kusoma ili upate faida zaidi, niliposema hili la (Kufufuliwa) ni rahisi kulipata nimekusudia wakati mwengine inakutokezea lile jambo la mwanzo la kujua(Knowing)linapokuja unazinduka ukawa hujui uko wapi, wewe nani?, Halafu jambo la pili linafatia ni kusikia, unasikia watu wanazungumza kwa mbali, halafu hapo tena inakuja kuona ikifatiwa na nguvu, ukiyapata hayo kama mja Mwema unaamka na Alhamdullilah, Nakushukuru Mollah wangu kwa kunijaalia uhai baada ya Mauti yangu.Kuna mambo mengine yenye faida nitayazungumza nini ufanye wakati unapata Rehma hii ya kuamka, huko siku za mbele nikijaaliwa.