Sunday, January 15, 2017

SAFARI YA MAISHA PART 1

Asalaam Aleiykum

Maisha kitu Adhimu sana ikiwa utatuliza akili na kuzingatia, Umeshawahi kujiuliza swali hili Nini Maisha?.Kama hulijui basi utakua hasarani, inabidi ufanye bidii ili upate kuijua siri hii ya maisha wewe mwenyewe na ufurahi na baraka hii alokupa Mollah wako.
Nini Maisha? Maisha ni ule mpito baina ya Uhai na Mauti, viwili hivi vinakwenda sambamba, Unapita kiumbe wewe kwenye hali hizi mbili bila ya kujijua, Nikisema bila ya kujijua nina maana umo kwenye hali ya kusahau, Kidogo kidogo unakufa na kidogo kidogo unaishi, nikizungumzia jambo hilo nagusia huo Mwili wako, sio Roho yako, kwa sababu inayokufa sio Roho ndio maana nikasema unapita kwenye Njia ya Uhai na Mauti, Sasa ndio nikasema unajua nini Maisha. Ni kipi hicho chenye kukufanya Uishi?.
Kulijibu swali hili itabidi lazima tutafute muongozo kwenye Quraan, kwani bila ya muongozo huu nitakuacha njiani, hutoweza kunifahamu nini kusudio langu, basi kwanza kabisa hebu pata habari hii ya aya mbili zilizomo katika sura ya (Baqarah aya ya 155 na 156)uzione vipi zilivogusa kadhia hii ya Maisha.

وَلَنَبۡلُوَنَّكُم بِشَىۡءٍ۬ مِّنَ ٱلۡخَوۡفِ وَٱلۡجُوعِ وَنَقۡصٍ۬ مِّنَ ٱلۡأَمۡوَٲلِ وَٱلۡأَنفُسِ وَٱلثَّمَرَٲتِ‌ۗ وَبَشِّرِ ٱلصَّـٰبِرِينَ() ٱلَّذِينَ إِذَآ أَصَـٰبَتۡهُم مُّصِيبَةٌ۬ قَالُوٓاْ إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّآ إِلَيۡهِ رَٲجِعُون
Na tutakutieni katika msukosuko(Wa Maisha)wa hofu na njaa na upungufu wa mali na watu na wa matunda, Na wapashe habari njema wanaosubiri.
Ambao uwapatapo msiba husema Hakika sisi ni(Viumbe)wa Mwenye enzi Mungu, Na kwake yeye tutarejea.
Naam hiyo ndio kadhia ya maisha kila mmoja wetu anapitia, lakini tatizo kubwa tumeumbwa na usahaulivu, lau kama mja angeweza kuushinda usahaulivu basi moja kwa moja peponi hataki hata kushikwa mkono. 
Itabidi kabla ya kuendelea na darsa hii nifahamishe kitu, kawaida ya wanaadamu wengi wanatabia hawataki kusikia kile wanachoambiwa, kama katika hiyo aya maelezo yako wazi, ikiwa utatuliza Akili utajua Mollah wako anazungumza na nani, na kama hufahamu vipi watu hawataki kusikia wanachoambiwa, basi nipeni ruhusu  nihadithie kisa cha "Wakwe zangu" huku niwatake radhi wanisameh, kwa sababu kisa hichi kina maana lazima nikihadithie  ili upate kunifahamu nimekusudia nini?.
Nahadithia kisa hiki kwa sababu watu siku hizi tunajitia ubabaifu wa kusikiliza upande mmoja tu, watu wamefikia kuambiwa Sheikh fulani usimsikize atakupoteza, Naam  kwenye maisha hakuna Ramani kila mtu ana njia yake, na wewe ukisikiliza upande mmoja utabakia jangwani au kwenye huo msitu daima umepotea. Mimi Binafsi nafundisha Dini na Dunia, na kisa hichi kina Raha ya dunia , ukicheka hiyo ndio furaha, huo ndio uzima, utapata kujua mimi kidogo afya yangu nzuri, na ukinuna basi utakua una tatizo la ndani ya roho, kisa chenyewe "Mamdali alikua kalala kwenye (Firashi)Tandiko la Mauti, Yuko katika hali ya (Mahtuti)anakaribia kuondoka duniani, akaona bora awaite familia yote, Mkewe na wanawae ili awape wasia wa mwisho, asije akaondoka akawa amedhulumu au kadhulumiwa, Akaanza kuwaambia Karim namdai Million 20, Daramsi Namdai Million 10, Popatlal Namdai million 40, Mamdali huyoo akazama kwenye (Sakaratul Maut), Yule Mke wake akawageukia wanawe mnaona Baba yenu ilivokua jitu Mema mpaka inakufa ina akili yake, Basi Mara Mamdali fahamu zikamrejea akatoa kauli akasema na ile Lakshmi iko dai mimi Million 100, pale pale yule Mkewe akawageukia watoto na kuwaambia sasa Baba yenu mauti imemlevya ipe maji hajui inasema nini, ishachanganyikiwa".
Unaona kama jambo hutaki kusikia na wewe unakunywa maji au 
unaenda zako, na hali hiyo hiyo na wewe unaambiwa usiwasikilize wanasema nini, hali kama hiyo ndio inakufanya na wewe upewe maji. Yakatae maji kwanza upate ukweli ikisha utafanya maamuzi yako ya kimaisha, asizuke mtu akakwambia fulani hendi peponi, madhehebu fulani yamekosea hayapati salah, hakuna ajuaye siri hiyo, na wala hatojua yoyote mpaka siku hiyo ambayo Mwenye enzi Mungu kaipanga, siku ya kusimamishwa Roho zote.

 يَوۡمَ يَقُومُ ٱلرُّوحُ وَٱلۡمَلَـٰٓٮِٕكَةُ صَفًّ۬ا‌ۖ لَّا يَتَكَلَّمُونَ إِلَّا مَنۡ أَذِنَ لَهُ ٱلرَّحۡمَـٰنُ وَقَالَ صَوَابً۬ا 
Siku ambayo zitasimama Roho na Malaika Safu safu, hatasema siku hiyo ila yule ambaye (Mollah) Mwingi wa Rehma amempa idhini ya(Kuzungumza)na atasema yaliyo sawa.
Na katika hiyo aya ya 155 sura ya (Baqarah) Mwenye enzi Mungu anazungumza na wewe Roho kwa kukwambia hayo mambo matano yaliyomo kwenye hiyo aya ambayo tutayapitia katika darsa yetu ya leo, nakutaka upite kama Roho, kuwa mbali na hayo maelezo (Then) utajua kumbe katika maisha haya mimi napita, na hapo litakuja swali mimi nani, utaanza kujichunguza vipi ulikuja hapa duniani?, nani alokupa jina? jee kweli mimi naitwa fulani? na kama sio fulani mimi nani? hayo ndio maswali muhimu Mja ya kuyafatilia ukajijua wewe  nani na nini wajibu wako kwenye Ulimwengu huu.
Mimi Nakushauri sikiliza pande zote, Mtume s.a.w kakwambia nenda mpaka china, chambua, tafuta halafu mwenyewe utafanya maamuzi yako na wala sio ya Sheikh fulani, au umesikia wamesema, hao walosema kina nani?.Na ukiaamua kufata utakua unafata Akili ya Sheikh na wala sio yako Mwenyewe.
endelea part 2

SAFARI YA MAISHA PART 2

Asalaam Aleiykum

Naam tunaendelea na darsa hii ya Safari ya maisha  kusudio langu likiwa kukufahamisha wewe nani, Na hapa Ulimwenguni unafanya nini?. Soma kwa utulivu pengine utapata kujijua wewe nani na hapa ulimwenguni unafanya nini. Na ukijijua sasa hivi wakati huu unaoishi basi ni furaha kubwa ilioje, usisubiri mpaka siku ya kufa kwako ndio ukashituka kumbe huyu ndio mimi, kumbe mimi ndio nilokua naidhulumu nafsi kwa kuiamrisha itende dhanmbi, mimi ndio nilokua nashirikiana na Ibilis kufanya visa hivi vyote kwenye (Kitabu)hiki.
Aya ya mwanzo imeanza kwa kutushangaza, zama na mimi kwenye aya hizo ili uibuke na lulu, Soma Quraan kwa njia ya Kiroho upate ufunuo wake. imeanza vipi?, Imeanza na hofu (What is fear)Katika darsa hii ntakustaajabisha sana ili upate kunielewa, Nini hofu? hofu ni kitu chenye kujulikana, kitu usochikujua huna hofu nacho, wacha tulete (Mfano)Moto ukikuunguza au umemuona mtu anaungua, hapo inakua hofu imeshakuingia, unajiuliza itakuaje nikichomwa mimi, nikitiwa motoni nitakua hali gani?, Na (Mfano) Mwengine wakutokua na hofu utaona kwa mtoto mdogo, utaona hata ukimpa moto anaushika bila ya kuogopa, ukimuunguza analia na kwa mara ya pili hachezi tena karibu ya huo moto.
Ndio maana utaona hata wale wenye kutafuta watu wa kujiua kwa mabomu wanawatafuta vijana kwa sababu hawana woga. Hata jeshi linafanya ajira kwa vijana kwa sababu hiyo hiyo. Wewe Mwenyewe binafsi zamani ulikua ukikoga baharini unakwenda maji ya mbali zinapopita Meli, Leo ushazeeka maji ya kisigino unaanza kukohoa, Nini kimetokezea?.
Hofu kubwa mja inayokuvaa si nyengine ila ni hofu ya kufa, ile taarifa uliyonayo kwamba sasa ushazaliwa basi na kufa ni lazima, Na kila miaka ikizidi na huku hesabu zako zinaongezeka na hofu nayo inazidi, kila mtu au ana hofu lakini tumekua mabingwa wa kuficha hofu zetu. Unaishi katika Ulimwengu huu lazima upite katika misukosuko ya hiyo mitihani, Na ndani ya misukosuko hiyo unapewa hii (Awareness)ya jambo hilo la Umauti, tenda utendavyo elewa kuna siku utarudi ulikotokea, kutokana na ubishi na ukaidi wako ndipo na wewe hukubali unaanza kutafuta dawa  zikukinge na maradhi, lakini hiyo ni mbinu zako za kukikwepa kifo, unafanya maarifa na kupigana vita eti usife, Jitizame wewe ukifanyiwa uchunguzi hospitali unakuwaje wakati wa kusubiri majibu yako.
Kama unataka faida ya kukufanya uupate Uislam wa kweli, upate Ku(surrender)basi mtizame mnyama asiyekua na habari ya Umauti, akiumwa hata na (cancer)hashughuliki, akiumwa chochote yeye kamuachia yule aliyemuumba afanye matarajio yake, ama amponeshe au arejee Nyumbani, Na kutokana na Rehma za Mollah wake kinapona kinyama hicho bila ya dawa yoyote ya kumdhuru Afya yake, sisi wanaadamu tunapita katika maisha haya tunawakabidhi wenzetu wenye kufanya majaribio ya madawa na kutupa tutumie, huku wanatwambia zina (side affect)unapewa dawa na hofu juu yake, hizo ndio harakati za safari hii ya maisha.
Sasa nini kinachokufanya uwe na hofu, kama nilivosema mwanzo ile desturi tulo nayo ya kujuwa (knowing) jee na Mauti tunayajua?, inawezekana kuwa jawabu ndio tunayajua, na inawezekana kuwa sio, mie nakita ushahidi wangu kwenye neno la mwanzo ndio tunayajua, kwa sababu mwanzo tumepita kwenye hali hiyo ya Umauti, sasa kwanini hofu imetushika kwa sababu Roho ni yenye kujua ilipotoka na wapi itarejea, Sasa kwanini tunasahau kule (original)tulipotokea, sababu kubwa ni mazingira yetu ya safari hii ya maisha yanatufanya tushughulike na mambo ya nje kupita kiasi, (Mfano)Macho yanaona Nje, Mdomo unaonja vya nje, Masikio yanasikiliza Nje,Pua inanusa vya Nje, Mikono imeshughulika na kazi za nje, miguu nayo ni yenye kutembea nje, Akili inawaza mambo yalopita na kupanga yajayao, hakuna hata kimoja chenye kushughulika na mambo ya ndani, (Wizara hii imewachwa bila ya muangalizi)Na ndio wizara muhimu sana, mambo ya ndani ya kiharibika (Automatic) na nje kunaharibika.
Sasa ili ukumbushwe kama kuna mambo ya ndani, ujue kuwa yupo mwenye kuongoza hivyo vyote vyenye kushughulika na nje, Ndio Bwana Mtume s.a.w akaamrisha waislam wende kudhuru "Makaburi, Wahudhurie shughuli za maziko wasikose, na huo ni muongozo wenye hekima kubwa kutoka kwa Mtume s.a.w..  Najua siku hizi kumezuka watu wanakukatazeni msende kudhuru makaburi, na nyie bila ya kuuliza sababu mnakubali, lakini bora walivosema msende, haijambo kuna kitu kimebakia, nacho huo wasia wa Bwana Mtume s.a.w wa kuhudhuria, wangekwambieni msihudhurie ingekua balaa, wangeondosha kitu adhimu kwenye dini hii, kwanini nikasema hivyo, (Kumbuka tuko kwenye safari ya maisha ni wajibu kuchambua mambo yanohusu),Kwa sababu kwenda na kuhudhuria ni vitu viwili tafauti, Najua utashangaa lakini wacha nikufafanulie. Unaweza kwenda lakini usihudhurie, na unaweza kuhudhuria lakini usende, Inakujia habari kama hii unatakiwa uitie Akilini ili upate kurekebisha (safari yako ya maisha).
Vipi inakua hali hiyo? Utaona Watu wanakwenda Mazikoni pengine na wewe umo, Kwa ile hofu ya Umauti walonayo wanaanza kuchat kwenye simu, au mazungumzo ya kipuuzi, au ndio wanakwenda kukutana na watu ambao hawajaonana siku nyingi. Lakini yule alohudhuria pale makaburini anakua hataki kuchat, wala mazungumzo wala kukutana na mtu ila chenye kumshughulisha pale kuona vipi umauti unavokua, vipi analitizama dongo linavorejea kwenye dongo lenzie chini ya Ardhi, au anaweza kupata fahamu ya vipi alivyoumbwa kwa udongo na sasa anarejeshwa kuwa udongo, Mtu huyu ikiwa bahati yake kahudhuria kikweli anaweza kwenda (Beyond death)au akazingatia kuwa karibu zamu yake itafika na aanze kuifanya mizigo yake iwe mepesi.Anaweza Mtu huyo kuhudhuria mazikoni akiwa Moga na hofu imemjaa, na kurejea akiwa shujaa hana hofu tena kakutana na Umauti yungali akiwa hai.
Endelea part 3

SAFARI YA MAISHA PART 3

Asalaam Aleiykum

Jambo la pili kutajwa kati aya hiyo ni Njaa, Kwanini ikatajwa njaa, kwa sababu baada ya hofu kinachofatia ni Njaa, tizama mahusiano haya mawili yalivyo, ukiwa na hofu wakati wote unakua unafikiri, na ukiwa na njaa hali ni hiyo hiyo vipi utapata chakula uhifadhi tumbo lako, unajua kama sikula nitakufa, Njaa pia inahusiana na Mauti, Kama hujala kwa miezi mitatu unakufa, (Body)haiwezi ku(survive) zaidi ya hapo.
Ndio maana Makureish wakaambiwa kwenye sura ya (Quraysh)"Wakaambiwa wanachukuliwa dhamana ya janga la njaa halitowafika, Na kuwa hapo pamejengwa Nyumba Tukufu basi pia imepatikana dhamana ya hofu haitowafika kwa kushambuliwa kivita na kupoteza maisha yao".  Ndio maana na hata serekali zenu zina kitu kinaitwa (food security)wanapita watu kutizama hali ya ukame ikoje, mazao yamepungua, mvua za kutosha, akiba ya chakula ipo, kwa sababu njaa ikikithiri watu na Taifa zima liko hatarini, watu watashindwa kutekeleza wajibu wao.
Na ukiutizama huo Mwili unategemea chakula ili uweze kuendelea kuishi katika safari hii ya maisha. 
Jambo la tatu kwenye Mtihani wa safari hii ya mwanaadamu ni kupungukiwa na mali, Mali ulochuma inaanza kupunguzwa kwa njia usizozifahamu, Ukiangalia utaona watu wengi walikua na mali lakini kidogo kidogo wanaanza kufilisika, sasa kwa yule Mwenye Akili anajua Mwenye enzi Mungu ndie aliyenipa na haina haja mimi kuteseka na kuanza kuitafuta kwa nguvu zangu, huu mtihani na mimi nauridhia.
Na jambo la Nne utalishangaa mali ikipungua na watu wanaanza kupungua, Marafiki wanakimbia, sasa huna kitu, wote walikusanyika sababu ya mali yako, wengine wanakufa, wengine wanatoweka, na wewe afya yako inaanza kupungua, kutokana na kuegemea kwako kwenye mihimili ya mali na watu huwezi kuchukua sasa unaanza kuumwa, afya yako inadhurika.
Na jambo la Tano, kama ulikua na mashamba vitu havioti kikawaida, Hapo tena ndio furaha inapungua, biashara hazendi, ulowakopa wanataka walipwe madeni yao, hapo ndipo kila kitu kinakuja juu mara (Blood Pressure)mara una (stress)mara Bul sukari(Diabetic), Nini sababu yake umeshikamana na mali, unaipenda pesa, unapenda mali huwezi kuzikosa, hapo tena na maradhi yanakupenda wewe yanaanza kukupa (sign)jirekebishe, mara (Minor stroke)mara hichi mara kile unapunguzwa kidogo kidogo kwanza Nje halafu kwenye Nafsi yako.
Unajikuta umebaki peke yako na hiyo ndio safari ya Maisha, hiyo ndio njia anayopita kila mmoja wetu kwenye Ulimwengu huu. Lakini kwa kuwa Mwenye enzi Mungu anawapenda Viumbe vyake kaamua kuwapa siri wakiweza kuisikiliza na kuijua maana yake basi watakua wamegundua kitu Adhimu sana, watakua wameikomboa nafsi yake kutoka kwenye mitihani hii ya safari ya maisha.
Kawaambia nini?, Kasema kwenye mwisho wa  aya Wabashirie Wenye Kusubiri, Nini subira?. Subira (Sabr)ni katika majina ya Mwenye enzi Mungu, Nini kinapatikana kama utaingia katika Ufalme wa Subira, Ndani ya Subira hakuna siku wala saa, hakuna Mchana wala usiku wewe umo katika hali ya subira, ikiwa unaumwa unaweza kupona au usipone, inaweza ukapewa au usipewe, wewe upo katika hali ya ku(surrender)Ndani ya subira ndio unafunguliwa ukweli wa mambo, kama kweli umejifunga katika subira, huna shaka hata chembe, hutaki hirizi wala kafara, unaacha itokee kama ilivoandikwa, inakua umejikabidhi kwenye Ufalme ulokuumba, sasa huna madaraka yoyote, kama maradhi ndio yapo, kama shida ndio zipo, kama Mauti ndio yapo, na ndio haki ya Mwanaadamu, sasa wewe ushajijua huna la kufanya, Na umeamua kukaa kwenye shimo la (Abyss)ya subira unasubiri. Na ikiwa kweli ni Mwenye kusubiri basi ndani ya hiyo subira utafunguliwa kitu, kitu hicho ukikijua wakati uko hai inakua faraja, unajua kumbe huyu ndio mimi, Mimi ndio Roho, ndio nilokua nasikia hadith zake, ndio mimi nasubiri, kumbe mimi tafauti na hayo mambo yanaonikuta katika hii misiba mitano ya misukosuko.
Basi hapo ndio utaweza kutamka kwa Ukweli hayo maneno ya yaliyomo katika aya inayofatia ya (156) "Ambao uwapatapo Msiba husema""Hakika sisi ni wa Mwenye enzi mungu"Na kwake yeye tutarejea".
Ukiweza kutamka maneno hayo Kiroho, hapo utakua na Mamlaka ya kujiita "Walii" au jina lolote jengine, kwa sababu kuanzia hapo wewe ni kiumbe mwengine kabisa, hivi sasa unajijua wewe binaadamu unatamka maneno hayo kila siku, akifa mtu unasema lakini huyajui maana yake, Lakini ukishajijua Kwamba wewe ni Roho, basi kila msiba unao kufika katika dunia hii utalisema neno hilo lilokuwemo kwenye hiyo aya huku umehudhuria, akifa mtu utakua unajua khalifa karudi Nyumbani.
Na ukifikia hali hiyo ukajigundua kuwa wewe ni Roho basi Sala yako itakua ya aina nyengine, vitendo vyako vitabadilika, utakua mwenye (control) ya maisha yako mpaka kuondoka kwenye Ulimwengu huu, hapo tena utakua huna haja ya kupenda mali, kupenda majumba, kupenda mapesa, kupenda watoto, unakua huna haja hiyo, unakua ushajijua kumbe mimi hapa napita tu, kama nilivokuja sina kitu, kumbe duuh mpaka hili jina wamenipa nilipowasili hapa duniani, kuanzia leo sitaki tena Kumuasi Mollah wangu Mpenzi alonikirimu maisha haya ya Ulimwenguni, Na kuanzia sasa nitafanya kazi ya kuwaonea huruma wageni wenzangu, kuwafanyia mema walo karibu yangu, huku nikitaraji kurejea nyumbani wakati wowote alonipangia Mollah wangu.
Kila mmoja yupo Safarini tufanye hima ya kupunguza mizigo tulobeba ili   safari ya maisha isizidi kuwa nzito.
Jifahamu wewe nani utapata raha ya maisha ya hapa duniani na huko nyumbani unakorejea.