Sunday, January 15, 2017

SAFARI YA MAISHA PART 1

Asalaam Aleiykum

Maisha kitu Adhimu sana ikiwa utatuliza akili na kuzingatia, Umeshawahi kujiuliza swali hili Nini Maisha?.Kama hulijui basi utakua hasarani, inabidi ufanye bidii ili upate kuijua siri hii ya maisha wewe mwenyewe na ufurahi na baraka hii alokupa Mollah wako.
Nini Maisha? Maisha ni ule mpito baina ya Uhai na Mauti, viwili hivi vinakwenda sambamba, Unapita kiumbe wewe kwenye hali hizi mbili bila ya kujijua, Nikisema bila ya kujijua nina maana umo kwenye hali ya kusahau, Kidogo kidogo unakufa na kidogo kidogo unaishi, nikizungumzia jambo hilo nagusia huo Mwili wako, sio Roho yako, kwa sababu inayokufa sio Roho ndio maana nikasema unapita kwenye Njia ya Uhai na Mauti, Sasa ndio nikasema unajua nini Maisha. Ni kipi hicho chenye kukufanya Uishi?.
Kulijibu swali hili itabidi lazima tutafute muongozo kwenye Quraan, kwani bila ya muongozo huu nitakuacha njiani, hutoweza kunifahamu nini kusudio langu, basi kwanza kabisa hebu pata habari hii ya aya mbili zilizomo katika sura ya (Baqarah aya ya 155 na 156)uzione vipi zilivogusa kadhia hii ya Maisha.

وَلَنَبۡلُوَنَّكُم بِشَىۡءٍ۬ مِّنَ ٱلۡخَوۡفِ وَٱلۡجُوعِ وَنَقۡصٍ۬ مِّنَ ٱلۡأَمۡوَٲلِ وَٱلۡأَنفُسِ وَٱلثَّمَرَٲتِ‌ۗ وَبَشِّرِ ٱلصَّـٰبِرِينَ() ٱلَّذِينَ إِذَآ أَصَـٰبَتۡهُم مُّصِيبَةٌ۬ قَالُوٓاْ إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّآ إِلَيۡهِ رَٲجِعُون
Na tutakutieni katika msukosuko(Wa Maisha)wa hofu na njaa na upungufu wa mali na watu na wa matunda, Na wapashe habari njema wanaosubiri.
Ambao uwapatapo msiba husema Hakika sisi ni(Viumbe)wa Mwenye enzi Mungu, Na kwake yeye tutarejea.
Naam hiyo ndio kadhia ya maisha kila mmoja wetu anapitia, lakini tatizo kubwa tumeumbwa na usahaulivu, lau kama mja angeweza kuushinda usahaulivu basi moja kwa moja peponi hataki hata kushikwa mkono. 
Itabidi kabla ya kuendelea na darsa hii nifahamishe kitu, kawaida ya wanaadamu wengi wanatabia hawataki kusikia kile wanachoambiwa, kama katika hiyo aya maelezo yako wazi, ikiwa utatuliza Akili utajua Mollah wako anazungumza na nani, na kama hufahamu vipi watu hawataki kusikia wanachoambiwa, basi nipeni ruhusu  nihadithie kisa cha "Wakwe zangu" huku niwatake radhi wanisameh, kwa sababu kisa hichi kina maana lazima nikihadithie  ili upate kunifahamu nimekusudia nini?.
Nahadithia kisa hiki kwa sababu watu siku hizi tunajitia ubabaifu wa kusikiliza upande mmoja tu, watu wamefikia kuambiwa Sheikh fulani usimsikize atakupoteza, Naam  kwenye maisha hakuna Ramani kila mtu ana njia yake, na wewe ukisikiliza upande mmoja utabakia jangwani au kwenye huo msitu daima umepotea. Mimi Binafsi nafundisha Dini na Dunia, na kisa hichi kina Raha ya dunia , ukicheka hiyo ndio furaha, huo ndio uzima, utapata kujua mimi kidogo afya yangu nzuri, na ukinuna basi utakua una tatizo la ndani ya roho, kisa chenyewe "Mamdali alikua kalala kwenye (Firashi)Tandiko la Mauti, Yuko katika hali ya (Mahtuti)anakaribia kuondoka duniani, akaona bora awaite familia yote, Mkewe na wanawae ili awape wasia wa mwisho, asije akaondoka akawa amedhulumu au kadhulumiwa, Akaanza kuwaambia Karim namdai Million 20, Daramsi Namdai Million 10, Popatlal Namdai million 40, Mamdali huyoo akazama kwenye (Sakaratul Maut), Yule Mke wake akawageukia wanawe mnaona Baba yenu ilivokua jitu Mema mpaka inakufa ina akili yake, Basi Mara Mamdali fahamu zikamrejea akatoa kauli akasema na ile Lakshmi iko dai mimi Million 100, pale pale yule Mkewe akawageukia watoto na kuwaambia sasa Baba yenu mauti imemlevya ipe maji hajui inasema nini, ishachanganyikiwa".
Unaona kama jambo hutaki kusikia na wewe unakunywa maji au 
unaenda zako, na hali hiyo hiyo na wewe unaambiwa usiwasikilize wanasema nini, hali kama hiyo ndio inakufanya na wewe upewe maji. Yakatae maji kwanza upate ukweli ikisha utafanya maamuzi yako ya kimaisha, asizuke mtu akakwambia fulani hendi peponi, madhehebu fulani yamekosea hayapati salah, hakuna ajuaye siri hiyo, na wala hatojua yoyote mpaka siku hiyo ambayo Mwenye enzi Mungu kaipanga, siku ya kusimamishwa Roho zote.

 يَوۡمَ يَقُومُ ٱلرُّوحُ وَٱلۡمَلَـٰٓٮِٕكَةُ صَفًّ۬ا‌ۖ لَّا يَتَكَلَّمُونَ إِلَّا مَنۡ أَذِنَ لَهُ ٱلرَّحۡمَـٰنُ وَقَالَ صَوَابً۬ا 
Siku ambayo zitasimama Roho na Malaika Safu safu, hatasema siku hiyo ila yule ambaye (Mollah) Mwingi wa Rehma amempa idhini ya(Kuzungumza)na atasema yaliyo sawa.
Na katika hiyo aya ya 155 sura ya (Baqarah) Mwenye enzi Mungu anazungumza na wewe Roho kwa kukwambia hayo mambo matano yaliyomo kwenye hiyo aya ambayo tutayapitia katika darsa yetu ya leo, nakutaka upite kama Roho, kuwa mbali na hayo maelezo (Then) utajua kumbe katika maisha haya mimi napita, na hapo litakuja swali mimi nani, utaanza kujichunguza vipi ulikuja hapa duniani?, nani alokupa jina? jee kweli mimi naitwa fulani? na kama sio fulani mimi nani? hayo ndio maswali muhimu Mja ya kuyafatilia ukajijua wewe  nani na nini wajibu wako kwenye Ulimwengu huu.
Mimi Nakushauri sikiliza pande zote, Mtume s.a.w kakwambia nenda mpaka china, chambua, tafuta halafu mwenyewe utafanya maamuzi yako na wala sio ya Sheikh fulani, au umesikia wamesema, hao walosema kina nani?.Na ukiaamua kufata utakua unafata Akili ya Sheikh na wala sio yako Mwenyewe.
endelea part 2

No comments:

Post a Comment