Wednesday, June 20, 2012
SIRI YA MAUTI-(VIPI UNAKUFA)PART 1
ASALAAM-ALEIKUM.
Hakuna kitu anacho chukia mwanaadamu na kukiogopa kama mauti au (Kifo)ndio maana mada kama hizi hazipendwi kuzungumzwa kabisa, hakuna anopendelea kuizungumza kwa undani na ufanisi japo kuwa tukio hili sote litatukabili au kuna wenzetu lishawakabili lakini tunaendelea kujifanya kama halipo au sisi halitotugusa.Ewe mwanaadamu hivo ushapata kujiuliza nini kitatokea Mauti yatakapo kuhudhuria? Wanaadamu jambo hili linavyowatisha ndio utaona hata makaburi basi yamewekwa nje ya mji sababu watu wapate kusahau tukio hili la mauti.Watu wanaweza kupata nafasi ya kuizungumzia Roho lakini hawataki kabisa kuzungumza kutoka kwa Roho, Jee basi inakuwaje pale Malaika wamehudhuria kuja kumtoa Roho Mwanaadamu, "Ewe jumba la makosa"nakuomba piga moyo konde usafiri na mimi katika maudhui hii ili upate kujua japo kwa ufupi nini hasa kinakufika wakati Roho inapotolewa kutoka katika mwili wako.Hebu acha kuizungumzia siku ya kuzaliwa peke yake pata anagalau kidogo mvinyo wa Mauti ujue ladha yake inakuaje na nini kinatokea wakati huo.
Sikusema mimi maneno haya amesema yule alotumwa kwa haki kutuletea ujumbe huu, sasa yeye kasema nini? Anasimulia "(Abdulla Ibn Umar r.a Bwana Mtume s.a.w kasema)"Moyo unaingiwa na kutu kama vile chuma kinavoingiwa na kutu kikiingiwa na maji,Alipoulizwa nini tufanye ewe Bwana Mtume s.a.w ili tuusafishe,"akasema fanyeni jitihada kubwa za kukumbuka Mauti na kusoma Quraan". Tumo katika kuyafata maagizo ya Bwana Mtume s.a.w tumeingia katika bahari hii ya Mauti ili iwe mazingatio ya ukumbusho kwetu sote.
Sasa kwanini jambo hili likawa linatuhuzunisha na kutudhoofisha, kipi hasa tunachokipoteza katika haya mauti hata ikawa hatutaki kusikia habari hii, mbona chungu sana kadhia hii, inakuaje inatisha hivi ikawa mtu akitajiwa hana raha tena ya ulimwengu huu, Tupia macho aya ya 1-2 sura (MULK-Tabarak)تَبَـٰرَكَ ٱلَّذِى بِيَدِهِ ٱلۡمُلۡكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَىۡءٍ۬ قَدِيرٌ (١) ٱلَّذِى خَلَقَ ٱلۡمَوۡتَ وَٱلۡحَيَوٰةَ لِيَبۡلُوَكُمۡ أَيُّكُمۡ أَحۡسَنُ عَمَلاً۬ۚ وَهُوَ ٱلۡعَزِيزُ ٱلۡغَفُورُ (٢)
"Ametukuka yule ambaye katika mkono(uweza wake)upo ufalme na ni mueza wa kila kitu" Ambaye ameumba mauti na uhai ili kukufanyieni mtihani (nani)atakaye fanya mema,na yeye ni mwenye nguvu na mwenye kusamehe.Ameumba mauti na uhai kwanini yameanzwa kutajwa mauti mwanzo,ukenda katika elimu ya Tawhid ndio utagundua asili yetu lazima tupitie katika mauti ndio tuzaliwe,tizama mfano wa mbengu lazima ifukiwe ardhini halafu ndio itoe mti au ichipue kuwa mmea n.k, kwa hiyo ukiangalia kwa njia ya Tawhid Mauti na Uhai ni kitu kimoja ambacho kinapita katika sehemu inayoitwa maisha, ndio maana aya ikasema tumeumba mauti na uhai ili tukufanyieni mtihani,Kutokana na sababu hii ya kukikosa kitu hichi kinachoitwa maisha ndio Binaadamu akawa anajuta,tunalia,tunahuzunika kuikosa zawadi hii njema ya Mollah wetu alotupa yakuweza kuishi, ukipewa habari tu kuwa una maradhi na yanaweza kusababisha mauti, basi jitizame vita utakayopigana hapo madawa ya kila aina dua za ajabu ili mauti yasikufike. Mollah wetu katupangia njia ya kuja katika ulimwengu huu pale wanapokutana waja wawili katika tendo la ndoa, ndani ya mkutano huu imewekwa njia ya uhai kuanza safari hii ya kuonja ladha ya Maisha. Halafu tumewekewa njia nyengine ya kuondka katika ulimwengu huu na kuicha ladha ya maisha nayo ni hichi kifo, Mwanaadamu kama ulivokuja mwanzo peke yako na kwenye njia hii ya mauti unaondoka peke yako, lakini kuna tafauti ulipoanza safari hii mwanzo ulikua huna fahamu na sasa unaondoka na fahamu zako kamili, ulikuja katika ulimwengu huu mweupe huna doa, huelewi chochote,lakini leo unaondoka umekua mjuzi wa kila kitu, basi jee katika hayo ulosomea kwenye hii University ya maisha yapo uliyoyafanyia kazi za wema, jee ule mtihani umefaulu vizuri, Na kama umefeli ulifanya jitihada za kufanya marekebisho. Basi leo unaaga dunia unayaacha maisha tunakufungulia daftari yako ili tupate kukujulisha uliyoyatenda katika ufalme huu wa Mollah wako wa haya maisha.
Mauti yanaendelea kuwa maajabu juu yetu, yanaendelea kututisha kutokana hatuko tayari kuyakabili kama walivoyakabili watendao mema. Na sababu kubwa ni ile ya kusahau kama sisi katika ulimwengu ni wageni na kuna siku tutarejea tulikotoka, sasa nini tunafanya, tunakuwa wabinafsi,mtu pengine anaabudu mali yake,au jumba lake,au mapenzi yote kayamimina kwa familia yake na kamsahau Mollah wake,hakumbuki kabisa yale maneno aloambiwa haitokufaa leo mali wala watoto wako.
Mauti yanatutisha sababu kwa mara ya mwanzo inakukutanisha na hicho kitu kiitwacho Roho au kwa usemi mwengine (Your true self)Mauti yanakufanya upotee kabisa katika ulimwengu huu ndio maana khofu inakua kubwa sana, halafu napenda uwe na yakini katika safari hii ya mauti hakuna chochote kitacho kwenda na wewe isipokua amali zako, na pia jua kwa ukamilifu safari hii ni peke yako kama ulivokuja mara ya mwanzo huna jina huna nguo na mara hii unaondoka peke yako, na lengine la zaidi ni ile siri uliyoifutika ya kujiuliza hivo nitakua hai mie baada ya mauti yangu, jee vipi yale mambo ninayoambiwa kweli yapo huko niendako,basi leo ni siku ya kukutanisha na kile kilochotokea mbinguni kinachoishi ndani ya mwili wako, wengine wanapata bahati kukishuhudia wakati wapo hai kama vile ukiamka ndani ya ndoto ukawa unashuhudia kisa kinachotokea katika ndoto hiyo, ukipata nafasi ukatanabahi kujua na kuiona ndoto yako basi huyo aloona inabidi ajiulize nani huyu mwenye kushuhudia.
Ewe mwenye kuamini kwamba Mauti nikumalizika kwa kila kitu basi acha tukujulishe yakua kila chenye mwanzo elewa kina mwisho na kila chenye mwisho basi kina mwanzo wake, Jee imekufikia habari hii ya hijja yako ya akhera, basi kama huna habari au unapuuza hebu tega macho katika sehemu ya pili ya maudhui hii ujue nini kinatokea wakati Malaika wamehudhuria kuja kukuchukua, usije ukaogopa siku hii itakufika kama sio leo pengine kesho au umebakisha mwezi au mwaka lakini lazima utakutana na kadhia hii nzito isoepukika hivi karibuni.SASA VIPI MWANAADAMU UNATOLEWA ROHO,ENDELEA SEHEMU YA PILI IKIWA UNA MOYO WA KISHUPAVU.
A.BAJA
SIRI YA MAUTI (VIPI UNAKUFA)PART 2
Asalaam-Aleikum.
Ndugu yangu napenda uelewe wewe una vitu viwili vinavyo kufanya uwe mwanaadamu, kwanza mwili wako ambao huu wakati wa kufa unazikwa na kuoza na kugeuka mchanga, huo ndio mwili unarejea kuwa udongo, halafu unakitu chengine hichi ndio hicho kilotokea huko mbinguni ambacho kinaitwa (Roho)na hichi ndio kinachofanya safari ya kurejea kilopotoka. Lakini kabla ya kurejea kilopotoka hutumwa wajumbe kuja kukitenganisha na huo mwili sasa nini kinatokea wakati Malaika wamehudhuria katika (OPERESHENI)hii kubwa, Jee ushawahi kufikiria vipi itakua Mauti yakikubili, ushajua labda njia ya kufanya kupata nafuu katika tukio hili na nini Quraa'an inatwambia wakati siku hii ikidhiri na wewe upo katika godoro la mauti?."Waqiah:83-85"
(٨٢) فَلَوۡلَآ إِذَا بَلَغَتِ ٱلۡحُلۡقُومَ (٨٣) وَأَنتُمۡ حِينَٮِٕذٍ۬ تَنظُرُونَ (٨٤) وَنَحۡنُ أَقۡرَبُ إِلَيۡهِ مِنكُمۡ وَلَـٰكِن لَّ تُبۡصِرُونَ (٨٥
"Basi(inakuaje)pale roho inapofika kwenye koo, Na nyinyi wakati ule(mmemzunguka)mnamtizama,Na sisi tupo karibu naye zaidi lakini si wenye kutuona". Nini hapo kinatokea, hapo ndipo inapotokea ile operesheni kubwa kuliko zote ulimwenguni inayohudhuriwa na (Surgeon Speciality)Malaika wa Mauti,hapo unapata moja katika mawili yalotajwa katia aya ya 89 mpaka 95 katika sura hiyo hiyo ya (Waqiah)zaidi kama ni mja mwema basi unapewa anagalau dawa ya matulizo ili uepuke machungu na maumivu yanotokea hapo ulipolala kwenye godoro la mauti, na mfano mdogo walohadithia yalowakuta huku wanafahamu zao wanaelezea ni kama kuubeba mlima, usiombe ikakukuta hali hii, machungu hayo ndio anayopata yule aloishi katika ulimwengu huu kwa jeuri,au kiburi,mwenye kuwatesa wenzie au mtenda maovu,au alikua fisadi tu katika maisha alioishi na wenzie katika ulimwengu huu. Isije ikakudanganya labda ukaona mtu mwema anakufa kifo cha adhabu anateseka napenda uelewe huo ni mwili, kiroho yuko baridi hana wasiwasi na usije ukaona yule mtenda maovu kafa salama hana wasiwasi basi lau ungekua unaiona roho yake inavotolewa ungepiga kelele wewe mtizamaji, lau ingekua anaweza kuhadithia huyu asi vipi mauti yanamkuta basi hakuna hata mmoja wetu angekubali kutenda makosa tena. Sasa nini hasa kinatokea wakati huo, hakuna alokwenda akarudi na kutuhadithia nini kinatokea, lakini tunajaaliwa kupata hadithi za wale wema na wabaya wanavotoka roho wanapewa nafasi ya kusema yale wanayofanyiwa mpaka kufikia kumalizika kutoka kwa roho zao na kutokana na hadithi zao na sisi tukapata nafasi za kuhadithia ili iwe zingatio kwetu. Wagonjwa wengi husema naona mtu kanisimamia hataki kuondoka, wengine husema naona ngombe wananitizama n.k lakini kuna wengine wanahadithia process nzima tokea anapoanza kukamatwa kidole gumba mpaka roho inapofika kooni. Sasa nini walohadithia kwa ukamilifu wanasema? Jamani hali ya Mauti ni yenye kutisha ambayo haina mfano wake, Na woga unazidi kwa kuwa mwanaadamu hajui anapokwenda au vipi atapokewa, na huna kumbukumbu nini kitachotokea huko uendako, kutokana na hali hiyo mauti yanazidi kuwa magumu hususan ikiwa umeishi katika ulimwengu huu,pengine mzinifu au mla rushwa,hutaki jambo la kusali na mengine mengi ya kifisadi ambayo unayaelewa mwenyewe,unadhulumu wanyonge unatenda kikomo cha dhanbi zote kubwa hapo kwa kweli inakufika huzuni kubwa wakati kitabu chako kinapowekwa wazi ukawa unaona moja baada la jengine na kama una wasiwasi au khofu ya jambo hili muulize mwenye kuuguza wagonjwa mahtuti atakueleza huzuni zinavyowashukia wakati huo.
Sasa Mauti yanatokea vipi, kwanza mauti yana sehemu mbili ya nje na ndani ya mwili, ama kuhusu ya nje ni pale mwili unaposimama kutenda kazi zake kiungo baada ya kiungo.
Na sehemu ya pili nayo ni ya ndani ambayo (Roho)inapotenganishwa na mwili wa mwanaadamu, na hili kwa lugha yetu yakufahamiana nitaliita ni (sense)zinapositisha kutenda kazi zake. Kuhusiana na huu mwili (Qura'aan)inasema katika sura ya (Taha-aya-ya-55) مِنۡہَا خَلَقۡنَـٰكُمۡ وَفِيہَا نُعِيدُكُمۡ وَمِنۡہَا نُخۡرِجُكُمۡ تَارَةً أُخۡرَىٰ (٥٥).
"Kutokana na hii ardhi(nyinyi)Tumekuumbeni,Na kutokana na hiyo ardhi tutakurudisheni(ikisha)kutokana na hiyo ardhi tutakurejesheni kwa mara nyengine tena,(ili muishi tena)".
Naam umbo la mwanaadamu kukamilika linahitaji mambo kama 4 ambayo ni Maji,udongo,moto,na hewa ambavyo vyote vimo katika ardhi hii, na hivi vyote vikikamilika ndio vinaunganishwa na hiyo Roho ili kiumbe kipate kuwa hai.Na hivi vyote vinakamatwa na hii Roho sasa wakati wakutolewa Roho lazima vitu hivi vitenganishwe na hiyo Roho na hapo ndipo inapopatikana(Sakaratul-Mauti),hapo ndipo safari hii nzito inapoanza na mwanzo wa safari hii dalili zake inakua wewe unaumwa watu wamekuzunguka unasikia sauti lakini hujui wanasema nini, hapo (sense)ya kusikia inaanza kupotea, Utakua unaangalia kitu umekaa kimya lakini hufahamu nini kilcho mbele yako ambacho unakitizama,kuona kunaanza kupotea sasa hali inaanza kutisha, mara inaondoka harufu huwezi kunusa tena,ulimi unapoteza ladha ndio maana utaona wagonjwa mahtuti hawataki hata maji seuze chakula, kwa hiyo msiwalazimishe mnawapa shida wakati huo.
Hayo ndio mambo ya mwanzo kabisa wa dalili za Umauti ukikufika ndio unaanza kuyaonja, Halafu tena unafatia mwili(Body)unakosa nguvu zote, huwezi sasa hata kusimama Roho ndio inaanza kutenganishwa kidogo kidogo na mwili wako. Mwanaadamu huwezi hata kunyanyua kichwa, Hata Bwana Mtume s.a.w "aliomba kitambaa akaupangusa uso wake kwa maji akasema hakika ya Mauti ni hii sakaratul-mauti". Kwenye kutenganishwa Roho na kiwiliwili ndipo mwanaadamu unahisi kama vile unamezwa na ardhi au kuna jabali linakukandamiza, na hapa ndipo kila mkao mwanaadamu unakuumiza hata mto unakukera maumivu makali mno, sasa utaona mashavu yanaanza kutumbukia ndani, Meno yanageuka rangi, macho hayafungiki tena au kama yamefungika huwezi kuyafumbua. Hapo tena mara unaanza kukoroma na unatoa sauti ya kutisha, walokuzunguka wakisikia mkoromo huu wanaanza kutaarisha mambo ya maziko, nendeni sasa katafuteni sanda, jee karafuu maiti ipo wanazungumza mbele yako na wewe unayasikia mazungumzo haya lakini huwezi kujibu, Pengine mwenye kuuliza hivyo labda mkeo au mumeo au mwanao, au hata wazee wako wote hao wanajitaarisha labda sasa hivi au halafu utazuia pumzi.
Hali kama hii ikitokea ndio udongo sasa unachanganyika na maji, mwanaadamu unaanza kuyayuka, ndio maana utaona maiti ilokufia baharini inaharibika mara moja, na akiwa ardhini bila ya kuwekwa kwenye vyombo vya baridi akagandishwa mara anavurugika na kuanza kunuka na hii inatokana na umbo letu kuwa na 85% ni maji. Hapo maji yanaanza kutokea puani au machoni, ulimi haunyanyuki tena, maji yanajaa kooni huna nguvu tena hata ya kuyasukuma, pua kutokana na kufanya kazi ya ziada inaanza kuvuta hewa ya moto ndio ile kiu ya ajabu inamshika mtu katika sakaratul-mauti,khofu kubwa inatuvaa wakati huu na ukimtizama yule atokaye roho wakati ule utaona huzuni kubwa machoni mwake, kama vile anatamani akwambie itakwisha saa ngapi kadhia ya adhabu hii kwani naona kama mwenye kuzama baharini, Hapo tena mwanaadamu anaanza kukosa fahamu zinaondoka na kurejea kwa njia ya mchanganyiko na maneno ya ajabu yanaanza kumtoka walomzunguka wanaanza kushangaa.Ghafla kauli inakatika mdomo unabadilika rangi tena kuwa wa buluu na pua nazo zinakauka kabisa, mwili unaanza kushika baridi na joto linakimbia kuanzia miguuni, sasa hata ukimpa maji ya shahada hayapiti tena kila kitu kishafungwa, Hata ukizungukwa na wanao au mkeo huwatambui tena,hata majina huyafahamu mpaka sauti zao ushazisahau, Sasa hapo unaingia katika hatua ya mwisho ambapo hata kuhema inakua matatizo makubwa, kuvuta pumzi inakua mashaka yasio mfano, na ukitoa pumzi zako zinakua reefu, ikifikia hali kama hiyo macho yanabiruka yanatizama juu na fahamu zinapotea moja kwa moja hapo hufahamu chochote kinachoendelea katika ulimwengu huu, kiza cheusi kinakuzunguka na mawasiliano yote yanakatika.Mara unaanza kupata mawasiliano ya huko unapokwenda tena kama ulikua mtu mwema ishara zinaanza kukushukia, na kama ulikua mtu fisadi unafunguliwa dalili zote wazi wazi na kama ulikua mtenda madhanbi basi unaweza kutoa ukelele waliopo wamekuzunguka wakakukimbia mara moja, lau walokuzunguka wangejua nini unakiona basi hakuna hata mmoja wao angetenda dhanbi tena baada ya siku hii.Ikisha unavuta ile pumzi moja ya mwisho na kuitoa kwa nguvu hapo tena maskini Roho hiyo Malaika wanaondoka nayo na kama umetoa macho basi yanabakia kuangalia juu, na haya yote yanatokea kwa yoyote na mauti yana njia nyingi yanavomkabili mwanaadamu lakini utaratibu ni ule ule fariki kwa accident au vyenginevyo hali hii ni lazima ukabiliyane nayo.Hivi ndivyo sote mauti yanavotukabili na hakuna njia ya kuyakimbia isipokua kuna nafuu kwa wale walorejea kwa Mollah wao kwa njia ya salama na amani, mja uko msafi umetulia huna doa pengine waweza kupata tahfif ilotajwa katika sura ya (Naaziat-aya-ya-2)"وَٱلنَّـٰشِطَـٰتِ نَشۡطً۬ا (٢ Na kwa wale wanotoa roho za (watu wema kwa (Upole)Inshaallah Mollah wetu atujaalie tuwe katika hao kwa kila takayesoma maudhui hii na asiesoma, Amin.
Mollah wangu anajua zaidi.
Monday, June 18, 2012
DAWA YA DHANBI (SOMA UTAPOA)PART 2
By-Abdulla Baja
Asalaam-Aleikum
Napenda uelewe hakuna utajiri anopata mwanaadamu hapa duniani na akhera kama kusimamisha sala na kumuabudu Mollah wake kikamilifu, watu watakua na majumba ya kifahari na magari makubwa makubwa, lakini wewe ukipata sala basi umewashinda kwa kila kitu katika ulimwengu huu, utaona watu wamefurahi nje tuu lakini mashaka walokua nayo ndani ya nafsi mfano kama milima, lakini wewe ulopata sala ni tajiri wa (kiroho)hakuna kufilisika, ndani unacheka na nje unacheka hiyo ndio siri ya Sala, huku ndiko kupewa furaha hapa ulimwenguni na huko akhera.
Mwanaadamu ni kiumbe alobahatika kwani amepewa uwezo wa kuziona dhanbi zake, simba anaua lakini hajui kama anaua yeye anafahamu kile ni chakula, lakini mwanaadamu ana uwezo wa kutokuua na kutafuta chakula kingine hiyo ndio sifa ya mwanaadamu anafahamu kila kitendo chake, ndio maana akatambua dhanbi zimemganda. Sasa tunataka uthibitisho wa jambo hili ndani ya Quraan jee sisi tuna uwezo huu?. بَلِ ٱلۡإِنسَـٰنُ عَلَىٰ نَفۡسِهِۦ بَصِيرَةٌ۬ ( وَلَوۡ أَلۡقَىٰ مَعَاذِيرَهُ
"Bali mwanaadamu ni mwenye kuiona nafsi yake(Anajua)" Japo analeta udhuru".
Vipi kuona huku na inakuaje?inakua hivi kwani ukifumba macho sasa hivi unaweza ukasafiri ukarudi iwe Pemba au Zanzibar au Daresalaam, na hivyo ndio inavokua unapotaka kutenda maovu(shari)au kheri unaona katika nafsi yako, unamsubiri mtu aondoke umsengenye, au anakuja kukuletea rushwa, au umepangana nae miadi ya kutenda zinaa, kila kitu unajua (in advance) sasa inakuaje ushajua hili ni kosa na unaendelea kutenda. Nini kinatokea hapa?, katika Gap hiyo ndogo ndipo anapoingia (SHETANI-IBILIS) kwa sababu ukibakia umacho mpaka mwisho hutendi kosa, utashtuka(utamuabudu Mollah wako hutotaka kumuasi) lazima ulale ukushike usingizi (hypnotism)hapo ndio Ibilis anafanya kazi yake, vipi anafanya hiyo kazi, wewe mwenyewe chunguza isiwe mimi nasema na wewe unakubali fanya uchunguzi, anafanya vipi, kwanza anakusahaulisha, ikisha anakutia nguvu hakuna chochote, halafu anakuhadaa unakua huna kizuizi. tizama wewe mwenyewe ikiwa mwanamme au mwanamke(akija mtu wako humuoni
yule mtu-hukumbuki kama ile Dhanbi)ila unaona mapambo yake,pengine unazama kwenye figa yake au
unakumbushwa vitu vyengine kabisa, au mtu ndio anakuletea rushwa tizama humkumbuki yule mtu bali unakumbuka kaja nazo, ngapi? atanipa vipi, au ikiwa kazi yako kusema watu unasubiri yule mtu ataondoka saa ngapi umzungumze, akizidi kukaa anakukera, hapo shetani ndio anakua kesha tawala chunguza mambo mengi kama hayo kuna kitu kinakulaza kitafute hasa kitu hichi kitu gani(mie nimekupa mifano michache), ndio maana utaona shetani hendi kwa mlevi kwa sababu yule keshajilaza mwenyewe, yeye anakutakeni nyinyi mnofikicha macho na kujitia mko macho. Sasa hapa ndio unahitaji dawa, hapa unahitaji msaada, pengine unakula mali ya Msikiti, au unadhulumu jamii, labda mali ya yatima wewe ndio huwezi kuikosa, au uzinifu ndio starehe yako kuubwa tena unaringa kwa idadi ya ulowapata, ukijiona mambo ya ufisadi kama hayo yamekuzunguka basi jijue wewe mgonjwa na kabla ya kupelekwa kwenye operesheni basi jaribu dawa hii.
Naam dawa yenyewe sharti lake usije ukasoma kama nyimbo mdomoni mwako, au fikira zako ziko kwengine ni lazima uwe hufikiri chochote wakati unasoma dawa hii, Utasoma mara tatu, kumbuka kabla ya kufanya hilo tendo lako labda kupokea rushwa, au kumsema mtu, au kumtukana mtu, kumbuka kabla hujaanza kwanza soma(aya hii sura ya Anbiyaa-aya ya 87)"وَذَا ٱلنُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَـٰضِبً۬ا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقۡدِرَ عَلَيۡهِ فَنَادَىٰ فِى ٱلظُّلُمَـٰتِ أَن لَّآ إِلَـٰهَ إِلَّآ أَنتَ سُبۡحَـٰنَكَ إِنِّى ڪُنتُ مِنَ ٱلظَّـٰلِمِينَ"
(Na Dha-Nun, (Nabii yunus)alipondoka hali yakua ameghadhibika, akadhani labda hatutokuwa na uwezo juu yake, basi aliita akiwemo kwenye giza, hapana Mollah isipokuwa wewe Subhanna, Hakika mimi nilikuwa katika wenye kudhulumu)
Sasa wewe huna haja ya kuisema aya nzima, ila tumia neno alotumia Nabii Yunus a.s, alosema (LAA-ILLAH-ANTA-SUBHANNAKA-INNIY-KUNTU-MINNA-DHAALIMINA)kumbuka kabla ya kutenda hilo kosa,ndi usome dawa hii, sasa nini kinatokezea nitakupa kwa undani japo kidogo hicho kinotokezea, Kwa sababu umelala umo gizani, nini neno hili tukufu linafanya katika nafsi yako, kidogo kidogo linasafisha moyo wako ,kidogo kidogo unaanza kupata nuru na hiyo nuru iking'ara katika moyo wako basi, mapesa yatakua mbele yako huna haja nayo, wanawake au wanaume wako mbele yako huna haja nao, utakua humsemi mtu, hutaki mambo ya watu, hufanyi dhuluma ya aina yoyote utaridhika na ulokua nacho hapo unakua mweupe, na ukianza kuwa mweupe basi Sala inapatika bila ya taabu, bila ya vishindo, unaweza kujikuta umesimama mbele ya Mollah wako machozi yanakutoka (Mbele ya matuka-Sabur)hujijui kwanini, unajuta kwa uliyoyatenda zamani. Hapo unakua ushatoka gizani umeokoka kama aya ya (88)ya sura
hiyo hiyo, Inavomalizia (Hakika na
hvi ndivo tunavyo waokoa Waumini.
Hiyo ndio dawa nilokuletea jaribu ili upate kupona, kwa sababu hapo juu tumeambiwa nafsi zetu tunaziona japo tunaleta udhuru, basi kwa hiyo dawa hii ni ya kukumbuka huwezi kuendelea(kuleta udhuru) na kutenda dhanbi wakati unamtaja Mollah wako kutokea moyoni hiyo ni (Awareness), masisitizo yote ni katika(ZIKR)kukumbuka, huwezi kumkumbuka Mollah wako huku unamtii shetani, ukiona unasoma na chochote hakibadiliki, hee wewe tena unataka operesheni tena kubwa.Na tilia wasi wasi Imani yako.
Mollah wangu anajua zaidi.
A.Baja
DAWA YA DHANBI (SOMA UTAPOA)PART 1
By-Abdulla Baja
Asalaam-aleikum.
Limekuja swali, muulizaji anasema, Sheikh mimi nina matatizo kwanza nasumbuliwa moyoni mwangu halafu nina mashaka na aya ya quraan,mimi nasimamisha sala tano kipindi hakinipiti, mambo yote ya kheri mimi nipo mstari wa mbele, lakini matatizo yangu yanakuja katika swala la wanawake wananisumbua sana, siwezi kuacha vitendo hivi vya haramu, halafu tena mimi nafanya kazi serekalini watu wanapokuja nawasaidia sana, nikimaliza hunipa zawadi kwa msaada wangu, hayo ndio matatizo yangu, sasa mushkeli wangu unakuja katika hii aya inosema(hakika ya sala inakuepusha na mambo machafu na mabaya yanochukiza)sasa mimi najitahidi kusali lakini siachi vitendo viovu,nipe maarifa nini kimenisibu.
Kwanza kabisa jawabu lako ni rahisi lakini maelezo yake ni magumu, ama kuhusu jawabu lako kuwa unasali vipindi vitano havikupiti jijue huna sala hujawahi kupata sala.
Sasa tuje kwenye maelezo yake na uchambuzi, Kwanini huipati hiyo sala? sijibu mimi, inajibu aya katika Quraan sura ya (muumin-aya-1-2)anasemaje huyo mwenyewe mwenye kukubali hizo sala."قَدۡ أَفۡلَحَ ٱلۡمُؤۡمِنُونَ (١) ٱلَّذِينَ هُمۡ فِى صَلَاتِہِمۡ خَـٰشِعُونَ (٢) "wamefuzu"(wamepata-wamefanikiwa)"wale ambao katika sala zao wanaleta unyenyekevu.
Haiwezekani kabisa maneno ya Mollah wako yakawa na khitilafu ndani yake, haitokei kabisa kukawa na batili ndani yake, pengine mja labda hujui nini huo unyenyekevu? hujawahi kufanya unenyekevu au moyo ushakufa haukai unyenyekevu, umo katika kupata dawa usijali dawa kakupa nani, wewe chukua ujaribu asaa yaweza kukuponesha, pengine watu wakuona wewe Sheikh mkubwa au Maalim mwenye elimu iso na mfano lakini maskini hujawahi kupata sala.
Sasa inakuwaje huo unyenyekevu, isikudanganye (hali ya nje)sijui watu wanakuona wewe mtu wa msimamo ibada hazikupiti, kumbe maskini moyoni wewe fakiri mkubwa ndani huna kitu hujawahi kukutana na Mollah wako."umeisoma ile hadith inosema muabudu Mollah wako kama unamuona", Huo ndio unyenyekevu unotakiwa, Iwe ukiingia katika Sala unaingia kwa mapenzi makubwa na kama huwezi mapenzi basi uingie kwa (ghushui)hofu ya aina gani? unakumbuka ulivokua mtoto umefanya kosa, ukiambiwa utasemewa kwa mzee wako hali yako inavokua(khofu na mtetemko)ulopata, Au sasa hivi umeshakua mtu mzima ukiambiwa chukua hii mihadarati(madawa ya kulevya) uipitishe(Uwanja wa ndege)unavokua ile khofu na mtetemeko unokupata umeambiwa maneno tu, basi yale ni maneno unakua katia hali hiyo,(na mifano iko mingi)z jee nini hali yako wewe yakwenda kukutana na Mollah wako, jee jiulize unapata hisia za (unyenyekevu na utiifu na mapenzi na hofu)ya kukutana na mollah wako, jee unaingia katika kila
Sala katika hali kama hiyo. Sio utegemee unakwenda kwenye Sala
umebeba makapo ya maudhi kichwani mwako halafu utaraji juu yake uipate hio Sala.
Elewa sala ina mafungu matatu(3)la kwanza mahusiano ya viungo, la pili mahudhurio yako kiroho, na la tatu faida zake baada ya hiyo sala.Na hapo ndio inaingia hiyo aya(Hakika sala inakuepusha na machafu na mambo ya munkari)lazima sala yako iwe kama alivosema:Mshairi;"Nilipogundua mimi ndani ya moyo wangu anakaa asokua wewe, nilifanya jitihada ya kuweka uongofu ulotoka kwako, mpaka ikawa hakai katika moyo wangu asokua wewe.Sasa ukiingia ndani ya hiyo sala kwa mifano niloitaja hapo juu, basi tambua hata ukimaliza kusali hisia hizo zinaendelea kuwepo, unyenyekevu huo unaendelea kuwepo sala hadi sala, hapo tena ndipo inaanza kukuepusha na kila maovu na machafu na mambo ya kipuuzi.Hivi ndivo muumin unavotakiwa kusimamisha sala, isije ikawa siku zote kazi yako kusindikiza watu wanosali na ikawa unasubiri wanosali wakipewa zawadi, wewe unasubiri ziwadondoke ili upate japo moja, fanya jitihada na wewe uwe kati ya hao wanosimamisha Sala.
Sasa ikiwa sala haifanyi kazi, ndio huipati, unaendelea kutenda dhanbi, sasa unahitaji dawa na dawa zipo za aina nyingi, bahari ya dawa ni kubwa, mwengine anaweza kuchota kigamboni, na mwengine akachota mangapwani, lakini bahari ni moja(sehemu ya kuchota hiyo dawa)ndio tafauti, kwa hiyo zisikushike ghaddhabu kwanini Sheikh wako kakupa dawa nyengine na mimi nakupa nyengine. Sasa kachukue dawa kwenye toleo la pili.
Mollah wangu anajua zaidi.
A.baja
Tuesday, June 5, 2012
FAIDA ZA NDOA
Asalaam-Aleiykum.
Ndugu zangu Waislamu Bwana Mtume s.a.w ametamka maneno makubwa kuhusiana na ndoa basi kabla ya kuingia katika darsa hii ya ndoa kwanza kabisa wacha tuyaangalie tafsiri ya maneno yenyewe ili tupate kuyafanyia kazi neno baada ya neno.
يا معشرا اشبا ب من استطاع منكم ا لباءت فليتزؤج فاءنه اغض للبصر
و احصن للفرج~ ومن لم يستطع فعليه با لصوم فاءنه له و جاء
"Enyi vijana mtakapofikia umri wa baleghe basi oweni(fungeni)ndoa, Hakika hayo yatakufanyeni muangushe macho,na muhifadhi sehemu zenu za siri (tupu)"
"Na kwa wale wasokua na uwezo basi kwao iwe nikufunga na hiyo ni yenye kukata matamanio"
Sasa kwanini Bwana Mtume s.a.w kwanza akawataja vijana, ikisha akataja watakapobaleghe tu wafunge ndoa, na nini hekima ya kuangusha macho na kuhifadhi sehemu za siri, hayo ndio tutayaangalia ili tupate kuchuma hapa na pale tupate faida mbili tatu tuweze kuzitumia katika maisha yetu ya kila siku katika kuzitunza ndoa zetu.
NINI NDOA:
Ndoa ni muungano baina ya watu wawili.
NINI MUUNGANO:
Muungano ni kitendo cha kufuta chengine kisiwepo kabisa, ndio maana mtaona Mume anaacha familia yake na Mke anaacha familia yake wawili hawa wanaungana nakua kitu kimoja hakuna nafasi ya kuingia baina yao shoga ama rafiki, Ukiona bado kuna shoga au rafiki ni muhimu kwako, basi itilie shaka ndoa yako na uanze kufanya marekebisho ili yasije kukuta matatizo katika maisha yako ya ndoa.
Naam sasa kwanini? Bwana Mtume s.a.w akaanza kuwataja vijana katika kadhia hii ya ndoa, sababu kubwa itabidi tuitupie macho mbegu ya uzazi, Binaadamu anazaliwa na kuishi na mbegu hii kwa muda wa miaka takriban 14 anayo katika mwili wake lakini imelala haitumiki haiko (Active)ndio maana utaona nguvu hizo (Energy)zinatumika kwa aina nyengine vile kama michezo na kadhalika, ndio utaona mtoto ancheza kutwa hachoki sababu (Energy)inafanya (Re-cycle)lakini inapofikia umri wa Baleghe mambo yote yanaanza kubadilika ghafla tu fahamu zinapata upeo mwengine. Kwa kuwa Bwana Mtume s.a.w anaijua siri hii akasema "Mtakapofika katika umri wa Baleghe basi sasa oweni" akaendelea kusema huko kuoa kunakupelekea kuangusha macho", Sababu Bwana Mtume s.a.w anawapenda vijana wa umma wake na anawatakia wahifadhi nguvu zao (Energy)kama pale walipokua bado ku-baleghe hutizami matamanio yoyote nguvu zako zote zaishia kwenye michezo na bado zinabakia kwa wingi na sasa umeoa unatakiwa uendelee kuzihafadhi mwenyewe, Kwanza kabisa Mollah wako alikua anakusaidia sasa umepewa uhuru kazi hiyo ifanye mwenyewe.
Kwanini ikawa hivo?uangushe macho yako, sababu kila ukitizama matamanio hususan ya wanawake basi inakua kama ulofanya kitendo chenyewe, Ndio maana Nabii Isa a.s akasema yoyote yule mwenye kumtizama mwanamke kwa matamanio basi kesha zini, Mtume s.a.w anatwambia inamisheni macho yenu usitizame hifadhini nguvu zenu, nini kinatokea ukihifadhi nguvu zako au kuinamisha macho yako, sio nakwambia kwa kubahatisha fanya majaribio utaona faida zake dondosha macho chini kutwa usitizame utaona huna machofu,uko imara,sala zako zinapata (Quality)nyengine, utaona mapenzi yanazidi kwa mkeo na watoto wako sababu hazitumiki kutizama migongo ya wake za watu au vifua vyao hayo yote sasa yanatumika kumtizama mkeo, utazidi kumsaidia mkeo nyumbani, utapenda kubakia nyumbani,nyumba itakua na furaha tupu, lakini tizama ukirudi ushatizama filamu tupu za mambo Machafu huko nje hali inavokua, ukiingia ushachoka unaanza kukunja uso watoto baada ya kufurahi wanamuogopa mzee wao, na wewe kwenye kichwa chako kimejaa (figure)ya fulani na nguo yake nani kapendeza nani ilo mbana, hata ukiambiwa chakula tayari unajibu nasoma gazeti, imehusiana nini chakula na gazeti hii ndio hali inayotukuta kwa kusimamisha macho yetu, ndani ya nyumba ugonvi mtupu sababu huthamini yale unayofanyiwa ndani ya nyumba yako mwenyewe.
Nakuomba Ndugu yangu ufate wasia wa Mtume s.a.w angusha macho yako uone mabailiko yake, mtizame mkeo tu uone penzi linavoongezeka, jee unajua kama unatupa nguvu zako ukiwa umacho hata wakati umelala kwa sababu mambo mengi umetizama umeijaza akili na (information)nyingi kwa hiyo akili nayo inataka ipunguze mzigo kwa hiyo unaanza kupoteza nguvu mpaka kwenye usingizi wako halafu unashangaa umeamka bado umechoka.
Na hali hii ukizoea nyumbani hukai utakua unataka utoke mbio ukisha kula hapo hapo lazima uende barazani, ushatia nguvu zengine sasa unataka ukazitupe tena ndani hakukuweki ushakua mteja hata mkeo umbo lake hulijui sababu humtizami kabisa.
"Enyi vijana angusheni macho yenu"hifadhini nguvu zenu, kaaeni na wake zenu, wapendeni wake zenu muone ladha ya ndoa, Hakika ladha ya ndoa ni mapenzi,na mapenzi ni kitu chenye kutaka mbolea, Hebu jiulize siku gani ulimtizama mkeo kwa jicho la mapenzi, jee mara ngapi umemtamkia japo moyoni unampenda?mtupie macho japo kwa siri ili uondoshe mazoea kuwa mimi naishi naye tu kwa ajili ya kipande cha karatasi kiloandikwa ukawa nacho usifanye hivyo yageuze mapenzi yako katika njia ya (sipiritual-love)yalete kwenye hisia,hiyo ndio mbolea niloikusudia. Isiwe unamtizama mkeo lakini fikira zote ziko kwa kimada utakua hasarani ndugu yangu, tuliza macho kwa mkeo au mumeo na kidogo kidogo utaona mabadiliko baada ya kufikiri mambo ya nje (Energy)yote inarejea kwa mwenzio na hapo ndio unapatikana mripuko wa mapenzi na hilo ndio kusudio la kuangusha macho.
Ama kuhusu kuchunga tupu zenu: Amesema Bwana Mtume s.a.w "Na hilo linakupelekeeni kuhifadhi tupu zenu"
Napenda uelewe jambo la kwanza kabisa Baba yetu Nabii Adam a.s na Bibi Hawa walipopata fahamu (Awareness)kitendo cha kwanza kabisa walichofanya walifunika tupu zao kwa majani, kwanini walitenda hivo sababu walijitafautisha na wanyama wengine walowazunguka, wao wamejitoa katika wanyama wakagundua Mollah wetu katupa fahamu yakujua tafauti baina yetu na wanyama na hapo ndipo tukaanza kuitwa wanaadamu na hicho ni kitendo cha kwanza kufanywa na viumbe ni kujitafautisha wewe na wanyama.
Ilikuaje hata kufanya hivyo, upo katika maudhui ya ndoa pata faida ujue vipi unarejea katika ile jinsia ya mnyama wakati unapomvulia nguo yule asokua halali yako:Itupie macho Al-Arraf-aya-ya-27: ـٰبَنِىٓ ءَادَمَ لَا يَفۡتِنَنَّڪُمُ ٱلشَّيۡطَـٰنُ كَمَآ أَخۡرَجَ أَبَوَيۡكُم مِّنَ ٱلۡجَنَّةِ يَنزِعُ عَنۡہُمَا لِبَاسَہُمَا لِيُرِيَهُمَا سَوۡءَٲتِہِمَآۗ إِنَّهُ ۥ يَرَٮٰكُمۡ هُوَ وَقَبِيلُهُ ۥ مِنۡ حَيۡثُ لَا تَرَوۡنَہُمۡۗ إِنَّا جَعَلۡنَا ٱلشَّيَـٰطِينَ أَوۡلِيَآءَ لِلَّذِينَ لَا يُؤۡمِنُونَ
"Enyi wanaadamu asikufitinini(akakutieni kwenye mashaka) shetani, kama alivowatoa wazee wenu katika pepo,(alifanya nini?)akawavua nguo zao ili kuwaonyesha tupu zao, hakika yeye pamoja na kabila lake wanakuoneni, na hali ya kuwa nyinyi hamuwaoni,hakika sisi tumewajaalia mashetani ni marafiki kwa wale wasoamini".
Naam ukiivua nguo moja kwa moja unampa shetani nafasi ya kukaa katika mwili wako na nguo ilokusudiwa hapo nitaizungumza katika darsa ya (vazi la ucha Mungu)lakini nguo zetu hizi tulokua nazo sasa hivi ukivua umeumia shetani ana uhuru wa kukuingia na kutoka kama nyumbani kwake huna kinga tena, anakaa kwenye akili yako ndio maana unakwenda kwenye sala unakua na mawazo matupu ya wanawake, na shetani akikuingia jambo la mwanzo kabisa huondoka ni Imani utaona mwenyewe unakwenda msikitini kufanya mazoezi ya viungo, ukirukuu mwanamke,ukisujudu mwanamke hasara tupu, hata mara moja humkumbuki mkeo hiyo ndio hali inayokukuta ikiwa utazivua nguo zako na kuacha kuhifadhi tupu yako. Ndio maana Bwana Mtume s.a.w akahimiza kuhifadhi tupu zetu mkisha kuoa na kabla ya kuoa, usije ukampa nafasi shetani akakufanya mteja(wala usiwacheke wale walopata madhara ya kutumia drugs)na wewe pia mteja lakini katika fani tafauti nyote hamuwezi kuwacha.Hiyo ndio hali inayokukuta ukiamua kurejea katika jinsia ya unyama, unaondoshewa imani,aibu na mengi katika jamii hata kwa Mollah wako malaika wanakulaani kila upitapo(mbinguni unajulikana kwa jina la fisadi)sababu wewe mwenyewe umekataa kuwa mwanaadamu,basi ukitaka utu wako ubinaadamu wako hifadi tupu yako na kama ushafanya makosa hayo basi bado una wakati rejea kama alivorejea Baba yetu Adam a.s "omba maghfira-vaa tena nguo zako).
Nini kitatokea ukianza kuvaa tena nguo zako?
Utaona maisha yako yanaanza kubadilika, nguvu zote unazozitupa nje zitaanza kurejea nyumbani utaanza kuona unampenda mkeo au mumeo na yeye anakupenda,riziki yako inaongozeka utaanza kuwapenda wanao na kama hujapata mtoto basi (chance)kubwa ya kupata mtoto inazidi hizo ndio siri chache za kuhifadhi tupu yako japo ziko nyingi lakini wakati ni finyu kuzitaja zote.Na vijana wanahimizwa unapotaka kuoa ujue kwanza madhumuni ya kwanza ya ndoa ni kupata kizazi, halafu mahusiano yasikwamie kwenye kiwiliwili,bali yawe ni ya Akili na kidini ndio ndoa itakwenda kupata furaha, lakini mkianza ndoa na mambo ya kubishana mbele za watoto au wageni au majirani basi ndoa hiyo itakua na matatizo makubwa, Isiwe hasira za kazi au biashara za nje unakuja kumalizia mwenzio nyumbani hayo yote yanachangia kuharibu ndoa yako.
Pia naomba unielewe yakua ndoa ni maabara(laboratory)ya kutiwa sumu zote za hamaki,ubinafsi,na tabia mbaya ili ziingizwe kwenye machine ya kuchunguzwa inayoitwa subira ili mpate majibu ya mafanikio. Na mkisha kuoana fanyeni mazoezi ya mapenzi kukumbushana mambo mazuri mazuri yalopita,semeni mambo mazuri ya mapenzi,tokeni safari za pamoja,kamataneni mikono nyie sio haramu feeling zenu ni muhimu sana msione haya,peaneni zawadi, oneaneni huruma, msaidie mwenzio hata kazi za nyumbani na wewe ni nyumba yako eti si ya mtu mmoja, najueni huruma na kuoneana imani kutamvutia kila mtu kwako kila mtu atakupenda kwa jambo moja tu la kumpenda mkeo au mumeo au wanao.Na kumbukeni ndoa ikishikamana na dini basi jua umekutana na (soulmate)wako na hakuna safari nyengine isipokua ya peponi. Usije ukaharibu ndoa yako kwa kutumia wakati mwingi na marafiki zako au mashoga zako, au kukaa mabarazani kutwa kucha n.k jiepushe ili upate mapenzi nyumbani, pia napenda uelewe katika umri wako unakutana na marafiki (300) lakini wote wanakukimbia wanabaki mkeo na wanao tu na ndugu zako tu, kwa hiyo usiwape marafiki umuhimu kuliko familia yako.
Ama kuhusu fungu la wale wasoweza kuoa Bwana Mtume s.a.w amesema "Juu yao wamepangiwa saum ambayo ni yenye kukata matamanio", Hili nitalizungumza kwenye darsa yangu ya (VAZI LA MCHA MUNGU)ambayo nitaandika Inshaallah ukikaribia mwezi wa Ramadhani na kusudio langu nataka Saum yako ya mwaka huu iwe ya aina nyengine kabisa ili upate siri ya saum ikupeleke katika darja nyengine kabisa.
Mollah wangu anajua zaidi.
A.Baja
Subscribe to:
Posts (Atom)