Tuesday, June 5, 2012

FAIDA ZA NDOA

Asalaam-Aleiykum. Ndugu zangu Waislamu Bwana Mtume s.a.w ametamka maneno makubwa kuhusiana na ndoa basi kabla ya kuingia katika darsa hii ya ndoa kwanza kabisa wacha tuyaangalie tafsiri ya maneno yenyewe ili tupate kuyafanyia kazi neno baada ya neno. يا معشرا اشبا ب من استطاع منكم ا لباءت فليتزؤج فاءنه اغض للبصر و احصن للفرج~ ومن لم يستطع فعليه با لصوم فاءنه له و جاء "Enyi vijana mtakapofikia umri wa baleghe basi oweni(fungeni)ndoa, Hakika hayo yatakufanyeni muangushe macho,na muhifadhi sehemu zenu za siri (tupu)" "Na kwa wale wasokua na uwezo basi kwao iwe nikufunga na hiyo ni yenye kukata matamanio" Sasa kwanini Bwana Mtume s.a.w kwanza akawataja vijana, ikisha akataja watakapobaleghe tu wafunge ndoa, na nini hekima ya kuangusha macho na kuhifadhi sehemu za siri, hayo ndio tutayaangalia ili tupate kuchuma hapa na pale tupate faida mbili tatu tuweze kuzitumia katika maisha yetu ya kila siku katika kuzitunza ndoa zetu. NINI NDOA: Ndoa ni muungano baina ya watu wawili. NINI MUUNGANO: Muungano ni kitendo cha kufuta chengine kisiwepo kabisa, ndio maana mtaona Mume anaacha familia yake na Mke anaacha familia yake wawili hawa wanaungana nakua kitu kimoja hakuna nafasi ya kuingia baina yao shoga ama rafiki, Ukiona bado kuna shoga au rafiki ni muhimu kwako, basi itilie shaka ndoa yako na uanze kufanya marekebisho ili yasije kukuta matatizo katika maisha yako ya ndoa. Naam sasa kwanini? Bwana Mtume s.a.w akaanza kuwataja vijana katika kadhia hii ya ndoa, sababu kubwa itabidi tuitupie macho mbegu ya uzazi, Binaadamu anazaliwa na kuishi na mbegu hii kwa muda wa miaka takriban 14 anayo katika mwili wake lakini imelala haitumiki haiko (Active)ndio maana utaona nguvu hizo (Energy)zinatumika kwa aina nyengine vile kama michezo na kadhalika, ndio utaona mtoto ancheza kutwa hachoki sababu (Energy)inafanya (Re-cycle)lakini inapofikia umri wa Baleghe mambo yote yanaanza kubadilika ghafla tu fahamu zinapata upeo mwengine. Kwa kuwa Bwana Mtume s.a.w anaijua siri hii akasema "Mtakapofika katika umri wa Baleghe basi sasa oweni" akaendelea kusema huko kuoa kunakupelekea kuangusha macho", Sababu Bwana Mtume s.a.w anawapenda vijana wa umma wake na anawatakia wahifadhi nguvu zao (Energy)kama pale walipokua bado ku-baleghe hutizami matamanio yoyote nguvu zako zote zaishia kwenye michezo na bado zinabakia kwa wingi na sasa umeoa unatakiwa uendelee kuzihafadhi mwenyewe, Kwanza kabisa Mollah wako alikua anakusaidia sasa umepewa uhuru kazi hiyo ifanye mwenyewe. Kwanini ikawa hivo?uangushe macho yako, sababu kila ukitizama matamanio hususan ya wanawake basi inakua kama ulofanya kitendo chenyewe, Ndio maana Nabii Isa a.s akasema yoyote yule mwenye kumtizama mwanamke kwa matamanio basi kesha zini, Mtume s.a.w anatwambia inamisheni macho yenu usitizame hifadhini nguvu zenu, nini kinatokea ukihifadhi nguvu zako au kuinamisha macho yako, sio nakwambia kwa kubahatisha fanya majaribio utaona faida zake dondosha macho chini kutwa usitizame utaona huna machofu,uko imara,sala zako zinapata (Quality)nyengine, utaona mapenzi yanazidi kwa mkeo na watoto wako sababu hazitumiki kutizama migongo ya wake za watu au vifua vyao hayo yote sasa yanatumika kumtizama mkeo, utazidi kumsaidia mkeo nyumbani, utapenda kubakia nyumbani,nyumba itakua na furaha tupu, lakini tizama ukirudi ushatizama filamu tupu za mambo Machafu huko nje hali inavokua, ukiingia ushachoka unaanza kukunja uso watoto baada ya kufurahi wanamuogopa mzee wao, na wewe kwenye kichwa chako kimejaa (figure)ya fulani na nguo yake nani kapendeza nani ilo mbana, hata ukiambiwa chakula tayari unajibu nasoma gazeti, imehusiana nini chakula na gazeti hii ndio hali inayotukuta kwa kusimamisha macho yetu, ndani ya nyumba ugonvi mtupu sababu huthamini yale unayofanyiwa ndani ya nyumba yako mwenyewe. Nakuomba Ndugu yangu ufate wasia wa Mtume s.a.w angusha macho yako uone mabailiko yake, mtizame mkeo tu uone penzi linavoongezeka, jee unajua kama unatupa nguvu zako ukiwa umacho hata wakati umelala kwa sababu mambo mengi umetizama umeijaza akili na (information)nyingi kwa hiyo akili nayo inataka ipunguze mzigo kwa hiyo unaanza kupoteza nguvu mpaka kwenye usingizi wako halafu unashangaa umeamka bado umechoka. Na hali hii ukizoea nyumbani hukai utakua unataka utoke mbio ukisha kula hapo hapo lazima uende barazani, ushatia nguvu zengine sasa unataka ukazitupe tena ndani hakukuweki ushakua mteja hata mkeo umbo lake hulijui sababu humtizami kabisa. "Enyi vijana angusheni macho yenu"hifadhini nguvu zenu, kaaeni na wake zenu, wapendeni wake zenu muone ladha ya ndoa, Hakika ladha ya ndoa ni mapenzi,na mapenzi ni kitu chenye kutaka mbolea, Hebu jiulize siku gani ulimtizama mkeo kwa jicho la mapenzi, jee mara ngapi umemtamkia japo moyoni unampenda?mtupie macho japo kwa siri ili uondoshe mazoea kuwa mimi naishi naye tu kwa ajili ya kipande cha karatasi kiloandikwa ukawa nacho usifanye hivyo yageuze mapenzi yako katika njia ya (sipiritual-love)yalete kwenye hisia,hiyo ndio mbolea niloikusudia. Isiwe unamtizama mkeo lakini fikira zote ziko kwa kimada utakua hasarani ndugu yangu, tuliza macho kwa mkeo au mumeo na kidogo kidogo utaona mabadiliko baada ya kufikiri mambo ya nje (Energy)yote inarejea kwa mwenzio na hapo ndio unapatikana mripuko wa mapenzi na hilo ndio kusudio la kuangusha macho. Ama kuhusu kuchunga tupu zenu: Amesema Bwana Mtume s.a.w "Na hilo linakupelekeeni kuhifadhi tupu zenu" Napenda uelewe jambo la kwanza kabisa Baba yetu Nabii Adam a.s na Bibi Hawa walipopata fahamu (Awareness)kitendo cha kwanza kabisa walichofanya walifunika tupu zao kwa majani, kwanini walitenda hivo sababu walijitafautisha na wanyama wengine walowazunguka, wao wamejitoa katika wanyama wakagundua Mollah wetu katupa fahamu yakujua tafauti baina yetu na wanyama na hapo ndipo tukaanza kuitwa wanaadamu na hicho ni kitendo cha kwanza kufanywa na viumbe ni kujitafautisha wewe na wanyama. Ilikuaje hata kufanya hivyo, upo katika maudhui ya ndoa pata faida ujue vipi unarejea katika ile jinsia ya mnyama wakati unapomvulia nguo yule asokua halali yako:Itupie macho Al-Arraf-aya-ya-27: ـٰبَنِىٓ ءَادَمَ لَا يَفۡتِنَنَّڪُمُ ٱلشَّيۡطَـٰنُ كَمَآ أَخۡرَجَ أَبَوَيۡكُم مِّنَ ٱلۡجَنَّةِ يَنزِعُ عَنۡہُمَا لِبَاسَہُمَا لِيُرِيَهُمَا سَوۡءَٲتِہِمَآ‌ۗ إِنَّهُ ۥ يَرَٮٰكُمۡ هُوَ وَقَبِيلُهُ ۥ مِنۡ حَيۡثُ لَا تَرَوۡنَہُمۡ‌ۗ إِنَّا جَعَلۡنَا ٱلشَّيَـٰطِينَ أَوۡلِيَآءَ لِلَّذِينَ لَا يُؤۡمِنُونَ "Enyi wanaadamu asikufitinini(akakutieni kwenye mashaka) shetani, kama alivowatoa wazee wenu katika pepo,(alifanya nini?)akawavua nguo zao ili kuwaonyesha tupu zao, hakika yeye pamoja na kabila lake wanakuoneni, na hali ya kuwa nyinyi hamuwaoni,hakika sisi tumewajaalia mashetani ni marafiki kwa wale wasoamini". Naam ukiivua nguo moja kwa moja unampa shetani nafasi ya kukaa katika mwili wako na nguo ilokusudiwa hapo nitaizungumza katika darsa ya (vazi la ucha Mungu)lakini nguo zetu hizi tulokua nazo sasa hivi ukivua umeumia shetani ana uhuru wa kukuingia na kutoka kama nyumbani kwake huna kinga tena, anakaa kwenye akili yako ndio maana unakwenda kwenye sala unakua na mawazo matupu ya wanawake, na shetani akikuingia jambo la mwanzo kabisa huondoka ni Imani utaona mwenyewe unakwenda msikitini kufanya mazoezi ya viungo, ukirukuu mwanamke,ukisujudu mwanamke hasara tupu, hata mara moja humkumbuki mkeo hiyo ndio hali inayokukuta ikiwa utazivua nguo zako na kuacha kuhifadhi tupu yako. Ndio maana Bwana Mtume s.a.w akahimiza kuhifadhi tupu zetu mkisha kuoa na kabla ya kuoa, usije ukampa nafasi shetani akakufanya mteja(wala usiwacheke wale walopata madhara ya kutumia drugs)na wewe pia mteja lakini katika fani tafauti nyote hamuwezi kuwacha.Hiyo ndio hali inayokukuta ukiamua kurejea katika jinsia ya unyama, unaondoshewa imani,aibu na mengi katika jamii hata kwa Mollah wako malaika wanakulaani kila upitapo(mbinguni unajulikana kwa jina la fisadi)sababu wewe mwenyewe umekataa kuwa mwanaadamu,basi ukitaka utu wako ubinaadamu wako hifadi tupu yako na kama ushafanya makosa hayo basi bado una wakati rejea kama alivorejea Baba yetu Adam a.s "omba maghfira-vaa tena nguo zako). Nini kitatokea ukianza kuvaa tena nguo zako? Utaona maisha yako yanaanza kubadilika, nguvu zote unazozitupa nje zitaanza kurejea nyumbani utaanza kuona unampenda mkeo au mumeo na yeye anakupenda,riziki yako inaongozeka utaanza kuwapenda wanao na kama hujapata mtoto basi (chance)kubwa ya kupata mtoto inazidi hizo ndio siri chache za kuhifadhi tupu yako japo ziko nyingi lakini wakati ni finyu kuzitaja zote.Na vijana wanahimizwa unapotaka kuoa ujue kwanza madhumuni ya kwanza ya ndoa ni kupata kizazi, halafu mahusiano yasikwamie kwenye kiwiliwili,bali yawe ni ya Akili na kidini ndio ndoa itakwenda kupata furaha, lakini mkianza ndoa na mambo ya kubishana mbele za watoto au wageni au majirani basi ndoa hiyo itakua na matatizo makubwa, Isiwe hasira za kazi au biashara za nje unakuja kumalizia mwenzio nyumbani hayo yote yanachangia kuharibu ndoa yako. Pia naomba unielewe yakua ndoa ni maabara(laboratory)ya kutiwa sumu zote za hamaki,ubinafsi,na tabia mbaya ili ziingizwe kwenye machine ya kuchunguzwa inayoitwa subira ili mpate majibu ya mafanikio. Na mkisha kuoana fanyeni mazoezi ya mapenzi kukumbushana mambo mazuri mazuri yalopita,semeni mambo mazuri ya mapenzi,tokeni safari za pamoja,kamataneni mikono nyie sio haramu feeling zenu ni muhimu sana msione haya,peaneni zawadi, oneaneni huruma, msaidie mwenzio hata kazi za nyumbani na wewe ni nyumba yako eti si ya mtu mmoja, najueni huruma na kuoneana imani kutamvutia kila mtu kwako kila mtu atakupenda kwa jambo moja tu la kumpenda mkeo au mumeo au wanao.Na kumbukeni ndoa ikishikamana na dini basi jua umekutana na (soulmate)wako na hakuna safari nyengine isipokua ya peponi. Usije ukaharibu ndoa yako kwa kutumia wakati mwingi na marafiki zako au mashoga zako, au kukaa mabarazani kutwa kucha n.k jiepushe ili upate mapenzi nyumbani, pia napenda uelewe katika umri wako unakutana na marafiki (300) lakini wote wanakukimbia wanabaki mkeo na wanao tu na ndugu zako tu, kwa hiyo usiwape marafiki umuhimu kuliko familia yako. Ama kuhusu fungu la wale wasoweza kuoa Bwana Mtume s.a.w amesema "Juu yao wamepangiwa saum ambayo ni yenye kukata matamanio", Hili nitalizungumza kwenye darsa yangu ya (VAZI LA MCHA MUNGU)ambayo nitaandika Inshaallah ukikaribia mwezi wa Ramadhani na kusudio langu nataka Saum yako ya mwaka huu iwe ya aina nyengine kabisa ili upate siri ya saum ikupeleke katika darja nyengine kabisa. Mollah wangu anajua zaidi. A.Baja

No comments:

Post a Comment