Wednesday, August 8, 2012

IJUWE LAYLATUL-QADIR(KUMI LA DHAMANA YA MOTO)PART 1

Asalaam Aleiykum.
Namshukru Mollah wangu kwa kuniwezesha kuandika Maudhui hizi tatu zinazohusiana na Ramadhani na kama herufi zilivopangika-Rahma-Maghfira- na leo hii tunaingia katika kumi la mwisho linalohusiana na Dhamana ya Moto, kwa wale walobahatika kupata baraka za kuzisoma zote inshaallah watapata faida japo kwa uchache kuijua Rehma na Taqwa, na leo tunamalizia kwa kuigusa maana ya (Nyota ya Jaha)au usiku wa (Laylatul-Qadir)ndani ya Dhamana ya Moto.
Hawatopata faida isipokua wale wanofatia darsa  kwa kituo na ufahamu wa ndani zaidi na sio katika kupita tu kutia macho nuru, hao watakua wameshapanda mbegu ambayo itachipua siku za mbele.
Naam sasa wacha tuingie katika mada yetu ya mwanzo(Dhamana ya Moto), na ya pili yake itakua (Laylatul-Qadir)utaona viwili hivi vyote vimo katika kumi hili la mwisho ndio maana imewajibika kuvigusa vyote viwili. Ewe Muumin umepata katika kumi la mwanzo Rehma, Umepita katika kumi la pili Maghfira, na sasa unaogelea katika kumi hili la mwisho basi hakuna jengine mja ila upewe nusura ya Moto, Na hakuna nusura nyengine unayohitaji mja ila kama hii ya kunusurika na moto, lakini jee utanusurika? huo Moto upo na vipi inakua kunusurika kwake, yote hayo inabidi tuilize Quraan na hakuna pakulipata jawabu isipokua sura ya (Maryam aya-ya-68-mpaka-72)

فَوَرَبِّكَ لَنَحۡشُرَنَّهُمۡ وَٱلشَّيَـٰطِينَ ثُمَّ لَنُحۡضِرَنَّهُمۡ حَوۡلَ جَهَنَّمَ جِثِيًّ۬ا  
"Naapa kwa Mollah, Tutawakusanya wao(Wanaadamu) pamoja na Mashetani ikisha tutawahudhurisha pembeni mwa Jahannam"
Sasa ikiwa joto huliwezi mpaka upate(Fan)moto wa bakery huuwezi una hali gani wakati umeweka pembezoni mwa Jahannam unasubiri amri ya kusukumwa wakati wowote ule,  na wewe ushalichungulia (Book)lako unaona madhanbi ulofanya ni mengi kuliko kheri ulotanguliza, jasho linakutoka wakati huo na (joshi)moshi mzito umekuzunguka Jahannam inavuma kwa ukelele leo una hali gani Mwanaadam ziwapi jeuri zako leo.
ثُمَّ لَنَنزِعَنَّ مِن كُلِّ شِيعَةٍ أَيُّہُمۡ أَشَدُّ عَلَى ٱلرَّحۡمَـٰنِ عِتِيًّ۬ا
"Ikisha tutawatoa katika kila(Kundi)taifa ambao walomuasi (Mollah)mwingi wa Rehma"
Ole wako usofunga ukawa hutii amri za Mollah wako, Tahadhari sana usiwe katika hilo kundi lilomusi Mollah wao kupita kiasi, ukaja ukashikwa bega na wewe twende huku tahadhari sana, hapa ulimwenguni ukitaka kupelekwa jela unatetemeka, unahuzunika, unaanza kuumwa, jee siku hiyo umejiuliza utaimudu vipi, sasa hivi utayaona maneno lakini ikidhihiri kwa vitendo ndio utayathibitisha maneno haya.
ثُمَّ لَنَحۡنُ أَعۡلَمُ بِٱلَّذِينَ هُمۡ أَوۡلَىٰ بِہَا صِلِيًّ۬ا
"Ikisha sisi tunafahamu wanostahili (khasa)kuunguzwa humo"
Usije mja ukanunua tiketi hii ya kuunguzwa sana, huiwezi adhabu hii ya Mwenye-enzi-Mungu, jiepushe na makosa makubwa ya makusudi, yasije mauti yakakukuta una shahada ya kukaa milele motoni kutokana na vituko ulivovifanya hapa duniani.
وَإِن مِّنكُمۡ إِلَّا وَارِدُهَا‌ۚ كَانَ عَلَىٰ رَبِّكَ حَتۡمً۬ا مَّقۡضِيًّ۬ا
"Na hakuna yoyote katika nyinyi(nyote)ila ni wenye kuifikia(kupita)katika hiyo (Jahannam)hiyo ni amri ya Mollah wako iliyokwisha hukumiwa"
Lazima wanaadamu wote wapite katika huo moto hiyo ni amri ambayo hamna pingamizi ndani yake, hapo ndipo mtu atataka amtoe mwanawe anusurike yeye, atahadhari mja katika maisha haya ya duniani anatanguliza nini huko aendako, siku hii mja ndio atajua yale makosa yake kasamehewa au Mollah hajamsamehe, chochote hapa kinaweza kutokea, ghafla unaweza kusukumwa ndani ya shimo la moto.

ثُمَّ نُنَجِّى ٱلَّذِينَ ٱتَّقَواْ وَّنَذَرُ ٱلظَّـٰلِمِينَ فِيہَا جِثِيًّ۬ا
"Ikisha tutawaokoa wale(Wano-mcha-Mungu)wafanyao Taqwa na tutawaacha  madhalimu humo wamepiga magoti"
Na hapa ndio inaingia ile ahadi ya wale walofunga wakaendelea kufanya mema basi wanapewa ahadi katika (mkusanyo)huu wao wasiwe na shaka wataokolewa, hawatosukumwa humo, itapatikana manusura juu yao wasiwe na wasi wasi, na hao madhalimu, wepi wanodhulumu masikini,wakapokea rushwa na kutoa rushwa wakafanya Dhanbi kubwa kubwa, basi wao watapiga magoti na ukiona umepiga magoti siku hiyo basi jijue umeumia hayaelezeki mambo yake mazito.
Zinatosha aya hizo tano kutujulisha hakika ya kuwepo Moto na matumaini kwa wale wano Mcha Mungu kwamba wakidumu katika hali ya (Taqwa) siku hiyo ya Masiku watapata hiyo Dhamana waloambiwa.
inaendelea part 2



IJUWE LAYLATUL QADIR(KUMI LA DHAMANA YA MOTO)PART 2

Asalaam Aleiykum.

Kwanini usipate dhamana na wewe umeamrishwa na Mollah wako na umetii amri yake, lakini sasa linalofatia ni tatizo ulokua nalo mwanaadamu,  Tatizo ulokua nalo huitaki dhamana hii alokupa Mollah wako unaivunja hata husubiri siku ya pili, pengine siku ile ile umeandama tu unapiga simu kwa hawara, au umo katika (Yaum-shaka)ushaupiga mvinyo chopi umelewa,huna haja ya kujua umeandama au haujaandama hilo sio tatizo lako, Muumin unaanza kupanga mambo ya ufisadi hata mwezi haujaonekana.
"Enyi Waumin Dhamana hii mmepewa lakini hamdumu nayo kabisa hata wiki moja haifiki meshaivunja, Unajikuta mja ushachafua Book lako na hivi ndivo tulivo Mollah wetu katukirimu zawadi hii ndani ya kumi hili la mwisho akatupa zaidi nayo ni hii Laylatul Qadir kuwamo katika kumi hili lakini wapi.
Na ajitizame kila mtu vipi anaivunja Dhamana hiyo pengine huko kuitambua yaweza kuwa ndio dawa yako. Na kama huwezi kuitambua dawa yako basi wacha nikupe mimi dawa yangu ninayo ijua labda yaweza ikakutibu, Kwanza napenda uelewe kila mtu anaipata na kuwemo katika (Laylatu-Qadir)lakini inategemea inakukuta katika hali gani, kabla ya kuigusa hiyo Nyota ya jaha(Laylatul-Qadir)au kuipata hiyo Dhamana ni lazima kwanza ufe, yakukute mauti ungali (Hai),kwanini unaogopa kufa hali unajua kuna siku utafariki na wala hamna shaka katika hilo, Jee ushawahi kufikiri siku utayokufa? huku watu wameuchukua mwili wako, wengine wanalia, imeshakujia habari wakati mwili wako unapokoshwa na watu wengine ikisha wakauvika sanda halafu wakautia kwenye jeneza, wakawa wanaupeleka makaburini huku unapitishwa pengine kwenye baraza yako au mtaani kwako, na walokua marafiki zako wengine watakuja mazikoni kwako na wengine wanaendelea na biashara zao kama kawaida.
Watakapo kufikisha makaburini watakufukia haraka haraka ikisha hao wanashika njia na ndugu na marafiki zako wanaendelea na biashara zao kama kawaida wewe utabakia sehemu ilo kimya, hapiti mtu peke yako unasubiri siku ya kuhukumiwa na hapo huna dhamana tena.
Basi kabla ya kukuta Mauti hayo nakutaka ufe ungali hai ili upate ladha ya maisha yenye dhamana, Vipi sasa huko kufa ukiwa hai?.
Endelea part 3

IJUWE LAYLATUL QADIR(KUMI LA DHAMANA YA MOTO)PART 3

Asalaam Aleiykum,
Vipi sasa huko kufa ukiwa hai, mfano wake kama vile mbegu unavoitia ndani ya ardhi ikisha unakaa kwa muda mpaka mmea unaanza kuchipua(kutokeza)lakini mwanzo lazima mbegu ife ndio uchomoze huo mti uchipue, na wewe umeshatupa mbegu ya Taqwa katika ardhi ya Ramadhani unayo nafasi  sasa uipalilie mbegu yako au usubiri Ramadhani ya 29 uikate kate, uamuzi ni wako wewe, kwa lugha ya ufupi nilivosema ufe nime maanisha ubadilike kabisa katika mwenendo wa Tabia zako ufanye u-turn, upotee kabisa chukua ahadi Ramadhani inakwisha lakini kwangu itaendelea mwaka mzima, nitadumu na mwezi huu katika nyanja zote za maisha yangu, kila siku kwangu mimi itakua Ramadhan, Uchukue ahadi yakua utawakimbia Marafiki zako wenye tabia mbaya na mbovu kabla wao hawajakukimbia wewe ikiwa umekufa au umepata maradhi, Na wale Marafiki zangu wema nitabakia nao kama kawaida lakini ndani mie nitakua kiumbe mwengine kabisa.
Uache mambo ya ulevi, ujizuie na mambo ya uzinifu, uwache kula mali ya haramu na rushwa, ujiepushe na mambo ya kipuuzi puuzi, fikra mbovu,tamaa ya utajiri,uridhike na alicho kukadiria Mollah wako,usipite ukawa unasengenya wenzako,uondoshe husda katika nafsi yako, na kiburi kikuondoke kabisa, ukikuta maskini unakaa nao na kula nao, ndio maana nikasema ufe kwani hivo vichache tu nilivovitaja vyote ni vifo ambavyo mwanaadamu itabidi upite unakufa kidogo kidogo unakufa taratibu ni lazima tabia zote hizi ziyayuke isibaki hata moja zikimalizika wewe utakua mtu wa aina nyengine hapo utakapo kuwepo hapo ndipo pana dhamana ya pepo na hapo tena utaiona (Nyota ya Jaha)kama unavo uona mbaa mwezi ingaravo.
Nini Laylatul Qadir?Jee ipo?Jee inaonekana?.
Jawabu wewe upo tayari kuiona,
إِنَّآ أَنزَلۡنَـٰهُ فِى لَيۡلَةِ ٱلۡقَدۡرِ 
"Hakika tumeiteremsha ndani ya usiku(Maalum)ulio mtukufu wa kadir"
Hebu tutizame nini kiza(usiku)ni(absence of light)au kutokuwepo kwa taa au (muangaza)ndio maana utaona mchana nyota hazionekani lakini zipo pale pale, lakini kilichoondoka ni kiza(usiku)kwa maana hiyo katika ufalme wa Mwenye-enzi-Mungu hakuna usiku wala mchana ila katika Ulimwengu wetu huu ndio kuna huo usiku na mchana, akauteua Mollah wako katika usiku huu wa (Qadir)kuiteremsha hii (Quraa'n)kwanini ikawa katika usiku huu kwa sababu hii Qura'an yenyewe ni (Nuru)na usiku huu ndani yake inatokea kuwa na utukufu wa hiyo (Nuru)ya Mwenye-enzi-Mungu yanachanganyika Mawili haya kupatikana huo ukweli wa Taa ya muongozo.
وَمَآ أَدۡرَٮٰكَ مَا لَيۡلَةُ ٱلۡقَدۡرِ
"Nini kitachokujulisha hiyo Laylatul Qadir"
Ndio mwanzo wa darsa hii nikasema itabidi kwanza yakukute mauti (ungali-hai)ili uijue hiyo maana yenyewe na uione kama unavotaraji, na vipi waloiona wakawa wanahadithia inagara sana na wewe miaka yote umesubiri hata siku moja hujaiona, mambo haya yakoje, napenda uelewe hayasemwi maneno yanohusiana na Mwenye-enzi-Mungu yakawa ndani yake hayana ukweli, wapo walouona usiku huu ndio wakahadithia, na wewe unayo nafasi hiyo lakini uko tayari kujitoa muhanga, kama nilivosema (Nuru)hii inataka mataarisho ambayo machache nimeyataja huko mwanzoni, sasa ikiwa jua huliwezi kulitizama vipi utaweza kuitizama hiyo (nuru)iliyomo katika hii Laylatul-Qadir, walipo ona (watawa wa Kikiristo)iliwafanya upofu, ikawa kiza wao wakaita(The dark night of the soul)Walipoona wacha Mungu wa Kiislamu wao wakaita(The light night of the soul)au nyota ya jaha, Nakujulisha yakuwa kila mtu anapita au anakuwemo katika usiku huu, lakini yategemea umekukuta katika hali gani?.

IJUWE LAYLATUL QADIR(KUMI LA DHAMANA YA MOTO)PART 4

Asalaam Aleiykum,
Wengine unawakuta wakiwa katika hali ya maasi, wengine unawakuta wakiwa wamelala, na wengine umewakuta wako katika hali ya kufanya Ibada, Ndio maana kwa wale utakao wakuta wamo kwenye Ibada hii ya saum basi wao wanapata moja kwa moja dhamana ya kunusuriwa na Moto, na hususan katika kumi hili la mwisho.
 لَيۡلَةُ ٱلۡقَدۡرِ خَيۡرٌ۬ مِّنۡ أَلۡفِ شَہۡرٍ۬
"Hakika ya usiku huu ni bora kuliko miezi elfu"
Ukiupata usiku huu kweli kweli ikisha ukaamua sasa unakufa ukiwa hai, basi ubora wake ni kupita hiyo miaka 83 ya umri wako unao ishi, sababu dhanbi zote zinafutwa, maisha yako yote yanabadilika kuwa(Blissful)furaha tupu, unaridhika na kila kadara alokupangia Mollah wako na wala hutaki zaidi,huwi tena kama matajiri wetu wa kileo eti anaomba dua Mungu niongezee utajiri, hii wewe ushapewa basi unaomba uongezewe nini tena,mapesa yote, mali zote bado unaomba upewe zaidi, basi hujatosheka tu, ndio maana unaona ukiumwa jipu tu unaanza kuhuzunika unaona kifo hicho kinakuja kukutenganisha na mali yako.
Ukiiona au kuipata hiyo Qadir unakua huna khofu tena, inakuwa kwako ukifa sawa au ukiwa hai kwako sawa. Ukipewa umaskini sawa, ukishushiwa maradhi sawa, lakini ukiona mwezi wa Ramadhan umekwisha na wewe unaendelea kupigana na kadara za Muumba wako, unashindana kutafuta utajiri kwa nguvu zako basi jijue umo hasarani.
 تَنَزَّلُ ٱلۡمَلَـٰٓٮِٕكَةُ وَٱلرُّوحُ فِيہَا بِإِذۡنِ رَبِّہِم مِّن كُلِّ أَمۡرٍ۬
"Huteremka Malaika(kwenye usiku huu)na Roho za (Wanaadamu)kwa idhini ya Mollah(wako)na kila amri (ya mambo yake)"
Huko ndiko kusafishwa, huku ndiko huko kuiona na ukawa umetakasika, msafi kwa kila hatua unayopiga mpaka mwisho wa umri wako,Mweupe unakua na (aura)fulani kila anaekuona au kukusikia anatamani awe karibu na wewe, dua zako hazirudi, mwenendo wa maisha yako unakua mfano wa Quraan unasikia tabu hata kutamka neno la uongo, unakuwa nuru tupu kuanzia tabia mpaka umbile lako lakini watu wakawaida hawawezi kuijua siri hiyo.
سَلَـٰمٌ هِىَ حَتَّىٰ مَطۡلَعِ ٱلۡفَجۡرِ
"Na ni salama(usiku)huu mpaka inapo pambazuka alfajiri"
Linapotamkwa neno salama basi jua ndani yake limebebwa neno la amani, na maana ya neno la amani ni (utulivu)ukimya ndio maana hata utaona vazi la kiislamu limekua rangi nyeupe, kumaanisha utulivu, utaratibu,utiifu,upole,uangalifu,ukimya na uvumilivu, Na hiyo ndio itakua hali ya wacha Mungu huko peponi ambayo sote tunatakiwa tuitarajie.
Naam hiyo ndio nyota ya (Jaha)unayoitaka timiza masharti yake ili upate kuiona, na ukiiyona mambo mawili yanaweza kutokezea nayo ima utahadithia au utanyamaza kimya kama wengine walochagua kufanya hivo.
Namalizia kwa kukupa habari kuwa hiyo Laylatul Qadir haionekani kwa haya macho ya kawaida, ikiwa wanaadamu hatujui nini umeme vipi leo unaweza kuijua nuru kwa macho ya kawaida. Jitupe kwa Mollah wako na Mollah wako ni mwenye kujua kama umejitupa kweli au unasubiri mwezi upite uanze visa vyako, na ukiwa umejitupa kweli basi Wallahi kuna siku utaondolewa pazia ili uone maajabu hayo ya Laylatul Qadir.
Sasa naomba dua, kwa kukutakieni kheri na mema kutoka kwa Mollah:Inshaallah darsa zitaendelea kama zilivo anza:
Mollah atujaalie Saum hii makbul na nyengine zinazofatia panapo majaaliwa.
"Ewe Mollah wangu kwa dhati ya uwezo wako niteremshie Nuru ninayoweza kuipokea, ambayo katika uwezo wako imeweza kuondoa kiza kilonizunguka,Ewe Mollah wangu nijaalie Nuru itakayongarisha mwili mzima ili yakinikuta marejeo katika ufalme wako niwe katika walofunikwa na nuru yako".
"Ewe Mollah wangu najikinga kwako na maneno yoyote ambayo yataleta usumbufu, maharibiko, au shaka kwa wale watokua hawajanifahamu, Kwako wewe Mollah wangu ndiko inapotokea hekima na mimi sina la zaidi ila kumuombea Bwana Mtume s.a.w na masahaba zake baraka zitokazo kwako. Amin

Abdulla Baja