Wednesday, August 8, 2012

IJUWE LAYLATUL-QADIR(KUMI LA DHAMANA YA MOTO)PART 1

Asalaam Aleiykum.
Namshukru Mollah wangu kwa kuniwezesha kuandika Maudhui hizi tatu zinazohusiana na Ramadhani na kama herufi zilivopangika-Rahma-Maghfira- na leo hii tunaingia katika kumi la mwisho linalohusiana na Dhamana ya Moto, kwa wale walobahatika kupata baraka za kuzisoma zote inshaallah watapata faida japo kwa uchache kuijua Rehma na Taqwa, na leo tunamalizia kwa kuigusa maana ya (Nyota ya Jaha)au usiku wa (Laylatul-Qadir)ndani ya Dhamana ya Moto.
Hawatopata faida isipokua wale wanofatia darsa  kwa kituo na ufahamu wa ndani zaidi na sio katika kupita tu kutia macho nuru, hao watakua wameshapanda mbegu ambayo itachipua siku za mbele.
Naam sasa wacha tuingie katika mada yetu ya mwanzo(Dhamana ya Moto), na ya pili yake itakua (Laylatul-Qadir)utaona viwili hivi vyote vimo katika kumi hili la mwisho ndio maana imewajibika kuvigusa vyote viwili. Ewe Muumin umepata katika kumi la mwanzo Rehma, Umepita katika kumi la pili Maghfira, na sasa unaogelea katika kumi hili la mwisho basi hakuna jengine mja ila upewe nusura ya Moto, Na hakuna nusura nyengine unayohitaji mja ila kama hii ya kunusurika na moto, lakini jee utanusurika? huo Moto upo na vipi inakua kunusurika kwake, yote hayo inabidi tuilize Quraan na hakuna pakulipata jawabu isipokua sura ya (Maryam aya-ya-68-mpaka-72)

فَوَرَبِّكَ لَنَحۡشُرَنَّهُمۡ وَٱلشَّيَـٰطِينَ ثُمَّ لَنُحۡضِرَنَّهُمۡ حَوۡلَ جَهَنَّمَ جِثِيًّ۬ا  
"Naapa kwa Mollah, Tutawakusanya wao(Wanaadamu) pamoja na Mashetani ikisha tutawahudhurisha pembeni mwa Jahannam"
Sasa ikiwa joto huliwezi mpaka upate(Fan)moto wa bakery huuwezi una hali gani wakati umeweka pembezoni mwa Jahannam unasubiri amri ya kusukumwa wakati wowote ule,  na wewe ushalichungulia (Book)lako unaona madhanbi ulofanya ni mengi kuliko kheri ulotanguliza, jasho linakutoka wakati huo na (joshi)moshi mzito umekuzunguka Jahannam inavuma kwa ukelele leo una hali gani Mwanaadam ziwapi jeuri zako leo.
ثُمَّ لَنَنزِعَنَّ مِن كُلِّ شِيعَةٍ أَيُّہُمۡ أَشَدُّ عَلَى ٱلرَّحۡمَـٰنِ عِتِيًّ۬ا
"Ikisha tutawatoa katika kila(Kundi)taifa ambao walomuasi (Mollah)mwingi wa Rehma"
Ole wako usofunga ukawa hutii amri za Mollah wako, Tahadhari sana usiwe katika hilo kundi lilomusi Mollah wao kupita kiasi, ukaja ukashikwa bega na wewe twende huku tahadhari sana, hapa ulimwenguni ukitaka kupelekwa jela unatetemeka, unahuzunika, unaanza kuumwa, jee siku hiyo umejiuliza utaimudu vipi, sasa hivi utayaona maneno lakini ikidhihiri kwa vitendo ndio utayathibitisha maneno haya.
ثُمَّ لَنَحۡنُ أَعۡلَمُ بِٱلَّذِينَ هُمۡ أَوۡلَىٰ بِہَا صِلِيًّ۬ا
"Ikisha sisi tunafahamu wanostahili (khasa)kuunguzwa humo"
Usije mja ukanunua tiketi hii ya kuunguzwa sana, huiwezi adhabu hii ya Mwenye-enzi-Mungu, jiepushe na makosa makubwa ya makusudi, yasije mauti yakakukuta una shahada ya kukaa milele motoni kutokana na vituko ulivovifanya hapa duniani.
وَإِن مِّنكُمۡ إِلَّا وَارِدُهَا‌ۚ كَانَ عَلَىٰ رَبِّكَ حَتۡمً۬ا مَّقۡضِيًّ۬ا
"Na hakuna yoyote katika nyinyi(nyote)ila ni wenye kuifikia(kupita)katika hiyo (Jahannam)hiyo ni amri ya Mollah wako iliyokwisha hukumiwa"
Lazima wanaadamu wote wapite katika huo moto hiyo ni amri ambayo hamna pingamizi ndani yake, hapo ndipo mtu atataka amtoe mwanawe anusurike yeye, atahadhari mja katika maisha haya ya duniani anatanguliza nini huko aendako, siku hii mja ndio atajua yale makosa yake kasamehewa au Mollah hajamsamehe, chochote hapa kinaweza kutokea, ghafla unaweza kusukumwa ndani ya shimo la moto.

ثُمَّ نُنَجِّى ٱلَّذِينَ ٱتَّقَواْ وَّنَذَرُ ٱلظَّـٰلِمِينَ فِيہَا جِثِيًّ۬ا
"Ikisha tutawaokoa wale(Wano-mcha-Mungu)wafanyao Taqwa na tutawaacha  madhalimu humo wamepiga magoti"
Na hapa ndio inaingia ile ahadi ya wale walofunga wakaendelea kufanya mema basi wanapewa ahadi katika (mkusanyo)huu wao wasiwe na shaka wataokolewa, hawatosukumwa humo, itapatikana manusura juu yao wasiwe na wasi wasi, na hao madhalimu, wepi wanodhulumu masikini,wakapokea rushwa na kutoa rushwa wakafanya Dhanbi kubwa kubwa, basi wao watapiga magoti na ukiona umepiga magoti siku hiyo basi jijue umeumia hayaelezeki mambo yake mazito.
Zinatosha aya hizo tano kutujulisha hakika ya kuwepo Moto na matumaini kwa wale wano Mcha Mungu kwamba wakidumu katika hali ya (Taqwa) siku hiyo ya Masiku watapata hiyo Dhamana waloambiwa.
inaendelea part 2



No comments:

Post a Comment