Asalaam Aleiykum
Zipate darsa zenye kufungua maono yako ili usije kushangaa katika mambo usoyajua yakakuletea balaa za ubishi, Soma kwa uangalifu ili upate maelekezo yatoridhisha nafsi yako kuhusiana na huo upande wa pili unaokwenda kuishi. Pia napenda uelewe hayawafiki mafunzo haya Matajiri wala Wanasiasa kwa kuwa hawana haja nayo, Na pia ukiwa na uchu wa kutafuta mali inakua vigumu mafunzo kama haya kukufikia.
Kwanini ikawa hivyo?(Quran-145-Al-Imran)
وَمَا كَانَ لِنَفْسٍ أَنْ تَمُوتَ إِلاَّ بِإِذْنِ الله كِتَابًا مُّؤَجَّلاً وَمَن يُرِدْ ثَوَابَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَن يُرِدْ ثَوَابَ الآخِرَةِ نُؤْتِهِ مِنْهَا وَسَنَجْزِي الشَّاكِرِينَ
"Na Nafsi yoyote haitoweza kufa ila kwa amri ya Mwenye enzi Mungu(na) kwa ajali iliyowekewa, Na Anayetaka malipo ya duniani tutampa hapa (hapa), Na anayetaka malipo ya Akhera tutampa huko (huko), Na kwa yakini tutawalipa wanaoshukuru".
Kwanini aya imeanza na kutajwa mauti? kwa sababu humkuti tajiri au mtu yoyote mwenye harakati nyingi za maisha akataka kujua habari hizi, akajiuliza kwanini kaumbwa, lini atakufa? upande wa pili ukoje, nini wajibu wake, ajabu gani za maisha, kwanini anaishi, na akimaliza maisha haya itakuaje, hataki kabisa maswali haya yamzonge katika shughuli zake za utafutaji wa mali.
Mtu kama huyu utakua naye Msikitini, kipindi cha Sala hakimpiti lakini hana akifanyacho ila mazoea ya mazoezi ya viungo, Sala haipatikani kabisa. Kutokana na hali hiyo Mtu huyo awe wewe au mimi anajiweka mbali na pepo.
Sasa wepi watakayoipata hiyo pepo, zama katika hii darsa angalau uchungulie mfano wa pepo au maana yake ikoje. Naam nani wanoingia? aya hapo juu imeanza vizuri sana imetaja "hakuna Nafsi itokufa ila kwa Idhini ya Mwenye enzi Mungu" Hapo ni kuoneshwa yupo Mfalme Mwenye kukumiliki na hufi hata ujitupe ghorofa mia ila atake yeye, na si hivyo tu bali umeshapangiwa kifo hicho na kimo ndani ya Kitabu kilichohifadhiwa.
Watakao ingia katika hiyo Pepo ni Maskini, Nisije kusema Maskini ukaanza kushangiria na kujiona namie nimo sababu sina nyumba, sina pesa, sipati chakula kwa kawaida, Maskini Mwenyewe sio wewe, kwa sababu wewe na Tajiri hamna tafauti, nyote mkenda kusali maombi yenu yaleyale, Mmoja anaomba apewe utajiri, na Mwengine anaomba azidishiwe utajiri, mali yake isipungue, Mwanawe apasi Mtihani, anaomba asitumbuliwe jipu, apandishwe cheo, Mkewe au Mumewe asichepuke, jirani anyimwe bahati, wewe itizame sala yako utadhani unakwenda kwa (Mganga wa Kienyeji) Kumbe umehudhuria kwa Yule alokupa uhai.
Sasa basi Masikini wepi walokusudiwa hapo, itabidi hapa tuvuke bahari twende ngambo ya pili tukaazime maneno yalotamkwa na Nabii Isa a.s au (Yesu)ndani ya (Injili) pale aliposema:
(Bless are the poor in spirit:for theirs is the kingdom of heaven-Matthew:5:3).
Wamebarikiwa wale masikini wa Kiroho:Kwao wao upo(Urithi) Ufalme wa Mwenye enzi Mungu.
Nini maana ya maneno haya? na upi huo Ufalme wa Mwenye enzi Mungu?, Na kwanini Ufalme huo utakua wao?, Basi kwanza kabla ya kugusa mambo hayo itatubidi tuujue Ufalme wenyewe ulokusudiwa ni upi?, Umo katika darsa ya Wafalme wa Pepo nakutaka uilekeze Akili yako katika kitabu Kitukufu chenye ukweli ndani yake ili kikujulishe vipi utakua Ufalme huo.
Endelea part 2
Asalaam Aleiykum
Sura ya Maryam aya (61,62,63).
"جَنَّـٰتِ عَدۡنٍ ٱلَّتِى وَعَدَ ٱلرَّحۡمَـٰنُ عِبَادَهُ ۥ بِٱلۡغَيۡبِۚ إِنَّهُ ۥ كَانَ وَعۡدُهُ ۥ مَأۡتِيًّ۬ا"
Pepo za milele ambazo (Mollah)Mwingi wa Rehma amewaahidi waja wake katika siri, Bila shaka ahadi yake ni yenye kuja.
"لَّا يَسۡمَعُونَ فِيہَا لَغۡوًا إِلَّا سَلَـٰمً۬اۖ وَلَهُمۡ رِزۡقُهُمۡ فِيہَا بُكۡرَةً۬ وَعَشِيًّ۬ا"
Hawatasikia humo upuuzi ila Salama, Na watapata humo riziki yao asubuhi na jioni.
"تِلۡكَ ٱلۡجَنَّةُ ٱلَّتِى نُورِثُ مِنۡ عِبَادِنَا مَن كَانَ تَقِيًّ۬ا "
Hiyo ndio pepo tutakayowarithisha katika waja wetu wale ambao (Walikua)ni Wanamcha Mungu.
Aya tatu lakini zina tafsiri kubwa kabisa inataka siku nzima kuichambua tafsiri hiyo, lakini kwa ufupi tukio hilo linaashiria kwenye aya ya mwanzo kuwepo kwa uendelevu wa maisha,Maisha ambayo wewe utakua ni "Bwana" Utakua ni Mfalme, Jee wewe huitaki ahadi hii ya siri ya Mollah wako, kama ninavosema, (nasema kila mara)uhai ni kitu cha kudumu, ila maisha ndio kitu cha (Mpito)au(Temporary). Kwa hiyo hichi kitu kinachoitwa Pepo ni ahadi ya siri, Lakini daima ahadi ya Mwenye enzi Mungu ni yenye kutimia, kwa hiyo kaa ukijua utakapomaliza muda wa kuishi hapa Ulimwenguni kuna maisha mengine.
Na Maisha ya huko hayana porojo za wanasiasa, hakuna uongo wa wafanya biashara, mambo ya kipuuzi yote yana katika katika dunia hii, huko unakutana na hali ya usalama(Peace)tupu, hakuna chuki wala uhasama, na humo wewe ni Mwenye kuhudumiwa kila kitu chako unaishi maisha ya Kifalme, Sasa hivi unaona kwenye TV tu lakini huko na wewe utayapata, utakua Mwenye kupata riziki yako asubuhi na jioni, hakuna tena shida ya kutafuta wala kuhangaika.
Hiyo ndio hiyo pepo watakayorithi wale walokua na Mapenzi na Mollah wao, wakakubali yupo na kumtii kwa ajili ya Ibada na kufata amri na sheria zake. Lakini uingiaji wake una shuruti lazima uwe Maskini, Sasa Umasikini huu ukoje? (Quraan imeashiria jambo kwenye sura ya Ash-Shuura aya ya 20) inasemaje?.
مَن كَانَ يُرِيدُ حَرۡثَ ٱلۡأَخِرَةِ نَزِدۡ لَهُ ۥ فِى حَرۡثِهِۦۖ وَمَن كَانَ يُرِيدُ حَرۡثَ ٱلدُّنۡيَا نُؤۡتِهِۦ مِنۡہَا وَمَا لَهُ ۥ فِى ٱلۡأَخِرَةِ مِن نَّصِيبٍ
"Mwenye kutaka jaza ya Akhera tutamzidishia katika Jaza yake hiyo, Na anayetaka Jaza ya Dunia tutampa, Lakini Akhera hatakuwa na sehemu yoyote ya kheri".
Sasa kwanini ikawa moja utazidishiwa, na nyengine utapewa, kuna mambo yamejificha wewe huyajui, maana ya kusemwa hivyo kuna kitu wewe unacho tayari lakini hukijui, na kitofanyika ni kuzidishiwa, unaweza kukipata hapa hapa na ndio haki yako ikiwa utamcha Mwenye enzi Mungu, lakini kupewa ni kwa muda unaweza ukapoteza, unaweza kunyanganywa au kukupotea. Kwa hiyo tabia ya Mwanaadamu ni vigumu sana kuvitaka vyote vilotajwa kwenye aya hiyo.
Ni watu wachache sana wanoweza kufanikiwa, Na sababu kubwa viumbe hatuna (Balance), Ndio maana tukapewa uhuru wetu kwa yule Mwenye kutaka Dunia anapewa, na Mwenye kuitaka Akhera pia anapewa. Sasa Maskini yupi Mwenye kurithi huo Ufalme?, Usikilize ukweli unapo dhihiri, Yasome Maneno ya Mwenye enzi Mungu kupitia katika vinywa vya Mitume wake wanasemaje.
Anasema Isa a.s "Wamebarikiwa Maskini kwani wao ndio watorithi Ufalme wa Mwenye enzi Mungu" Kwanini likatajwa neno kubarikiwa(Blessing)Kwa sababu hao wamechagua kitu kizuri sana, Wao wamechagua (Both) wako kwenye (Balance) (Irejee aya juu imetaja kuzidishiwa na kupewa) maana ya kuzidishiwa tayari unacho, na kupewa ndio hicho cha ziada, ukichagua (Both) unakuaje? na ukichagua kimoja unakuaje?.
Ukichagua Dunia na ndio wengi tunaichagua unakua unajishughulisha sana na kutafuta mali, mashamba, ufakhari, Na ukichagua Akhera pekee unakua Mwenye kutaka kufa, ushachoka na maisha, kila kitu haramu, muradi wako unakua (Neurotic) kwa sababu huna (Balance). Sasa uchague vipi? chagua kama ilivosema katika Quraan, imesemwa vipi?
Endelea part 3
Asalaam Aleiykum
(Quraan Baqarah aya ya 201)
وَمِنۡهُم مَّن يَقُولُ رَبَّنَآ ءَاتِنَا فِى ٱلدُّنۡيَا حَسَنَةً۬ وَفِى ٱلۡأَخِرَةِ حَسَنَةً۬ وَقِنَا عَذَابَ ٱلنَّارِ
"Na Miongoni mwao wako wasemao Mollah wetu tupe mema duniani na (Tupe)Mema Akhera, Na utulinde na adhabu ya moto".
Kauli ni ile ile Mollah wangu nibariki kwa mambo mazuri hapa duniani(Blessing)na huko Akhera, Ikisha niepushe na adhabu ya moto, na unapoepushwa na adhabu ya moto kinachofatia ni kupewa au kuingizwa kwenye huo ufalme wa Mwenye enzi Mungu. Hao ndio watorithi Ufalme wa Mwenye enzi Mungu.
Sasa tuwatizame warithi wenyewe ni Maskini wa aina gani?, (Usije ukadhani ni wale omba omba) Walotajwa ni wale Maskini wa Roho wenye kutafuta utajiri wa kumjua na kumpenda Mollah wao, Hao ni Maskini wa Ibada, Maskini wa kufanya mambo ya kheri, maskini wa Mapenzi, Maskini wa Huruma, Maskini wenye Uchu wa Kumkumbuka na kumtii Mollah wao, Maskini walokua hawana Kiburi, Maskini wenye hamu kubwa ya kumjua Mollah wao, Maskini ambao wakati wote wamo kwenye Dunia lakini mawazo na fikra zao zote wamejishughulisha kumkumbuka Mollah wao.
Hao ndio walochagua (Both) Dunia na Akhera, na ndivo inavotakiwa, ndivo ilivosema Quraan, ukiweza kufanya hivyo nini kinatokezea? (Quraan Ahqaf aya 13-14)
"إِنَّ ٱلَّذِينَ قَالُواْ رَبُّنَا ٱللَّهُ ثُمَّ ٱسۡتَقَـٰمُواْ فَلَا خَوۡفٌ عَلَيۡهِمۡ وَلَا هُمۡ يَحۡزَنُونَ "
Hakika wale waliosema Mollah wetu ni Mwenye enzi Mungu kisha wakatengenea(Kusimama kwenye kufanya yalo haki)hawatakua na hofu na wala hawatahuzunika.
"أُوْلَـٰٓٮِٕكَ أَصۡحَـٰبُ ٱلۡجَنَّةِ خَـٰلِدِينَ فِيہَا جَزَآءَۢ بِمَا كَانُواْ يَعۡمَلُونَ "
Hao ndio watu wa Peponi, watakaa humo (daima)ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyatenda.
Sasa hapa duniani unapata nini?
Unapewa na Mwenye enzi Mungu mambo mawili hapa hapa duniani iwe mfano wa mambo yatakavokua huko Akhera kwenye Ufalme wenyewe. Jambo la Mwanzo Unateremshiwa (Body Guard) Malaika wawe na wewe popote uendapo, unapata ulinzi(Ukitaka kuwaona niandikie pembeni ntakufundisha vipi uwaone?, Najua utashangaa ndio maana ya kukwambia, kumbuka unakoga katika bahari usishangae maji kugusa)Naam na Jambo la pili ndio huo mfano wa pepo unapewa kitu adhimu sana, kitu hichi ukikipata ukaweza kudumu nacho basi kiumbe unakua ushafuzu katika maisha yako ya Ulimwenguni na huko akhera, Kitu gani hichi cha pili?, hakuna chengine isipokua kupewa (Control) ya (Mind) Akili yako, hapa itabidi nieleze vizuri ili upate kujua maana ya atakua hana khofu wala huzuni ikoje?.
Hali hii anaipata kila mtu lakini inakujia mara chache sana, kwa mimi naita hali hiyo (To make contact with your being) unapata baadhi ya Nyakati pale unapokua (Total engaged)Mfano, kama wewe mcheza mpira au unatizama kipindi chako kwenye TV, au unapozungumza hapo Akili au (Mind)inapotea, hakuna mawazo, unakua hufikiri chochote, kwa sababu Akili haiwezi kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja, basi hapo unakua (full Being)huna huzuni, huna khofu na ukiwa katika hali hiyo unakuwa huwezi kutenda kosa.
Hivyo ndio wanavokua "Hao Maskini walotajwa" wenye kurithi huo Ufalme, Wanakua ni wenye kudumu katika hali hiyo, sio kwamba hawana Akili ila ana uwezo wa kuitumia wakati anaotaka Mwenyewe kwa hiyo muda wote ulobakia yuko kwenye (Being)yake na hapo ndio kwenye hiyo (Bliss), Kwa hiyo tafauti yako na yeye wewe unatumia nyakati maalumu za kucheza mpira, kutizama TV, kuzungumza na yeye anaendelea kuwa nayo (Being)yake wakati wote, kwa hiyo hapo mambo yanakua (Vice Versa), Wewe unatumia (Mind)Akili wakati wote na yeye anatumia(Being) wakati wote. Na kama utakua na ubishi kwenye Nafsi yako basi jiangalie mara chache sana unaipata hiyo (Being)lakini muda wote umetawaliwa na mafikra, mawazo juu ya mawazo(Stress)zimekujaa, dhana za kila aina, wanawake au wanaume wanaishi humo, madeni yanaishi humo, chuki zinaishi humo binaadamu huna mapumziko, huzuni juu ya huzuni, mashaka na khofu chungu nzima, Na hiyo ndio Akili uliyoibeba na ndio ilokufanya uchague dunia dhidi ya Akhera.
Sasa Wacha nikuchukue kwenye mfano wa Ufalme wa vinyama hususan ndege uone wanaishi vipi?.
Endelea Part 4
Asalaam Aleiykum
Ipate japo siku moja hata nusu saa, kuwa (Mad)kama (Shk Baja)kakae kwenye Bustani au kwenye(Garden) au nenda (Park)au hata shamba asubuhi na mapema, halafu kashuhudie vipi(Unconscious Being)wanavoishi, Wanaishi kama unavoishi, Wana Nyumba zao tena wamezijenga wenyewe, wana watoto wao na wake zao, wanatafuta chakula kama mfanyavo nyinyi, wanalala na kuamka, wanakwenda huku na kule kwenye bustani, mara kwenye mti huu mara kwenye mti ule, mara kwenye maji wanakunywa, mara kwenye mti wanapumzika, Na mara wanaimba kwa furaha na baraka alizowapa Mollah wao.
Wao katika Ufalme huo wanaishi kwa mapenzi kama utayafahamu, mara wanaruka mara wametulia wanatizama neema walizopewa na Mollah wao, Na wakishikwa na maradhi wao wako kwenye subra wanajua Mollah wao anawaponesha daima. Basi wao wapo kwenye (Mfano)wao wa pepo na ikifika wakati wanajifia na kurejea kwa Mollah wao(Blissful), Viungo vyao vinaanguka na kugeuka Mchanga kama wewe utakavogeuka wakati wa kifo chako.
Naam unapewa mifano hii ya pepo ili na wewe uchague vipi unataka. Na ukiwa utaridhia huo umasikini ukaipata hali hiyo niloitaja kwenye (Part 3)basi Ufalme gani utakaoupata wewe?
Quraan Waqiah aya ya 10.
"وَٱلسَّـٰبِقُونَ ٱلسَّـٰبِقُونَ"
Walioko mbele(Kwenye Ucha Mungu)nao ndio wlioko mbele
"أُوْلَـٰٓٮِٕكَ ٱلۡمُقَرَّبُونَ"
Hao ndio watakaokaribishwa(Kwenye Ufalme wa Mwenye enzi Mungu)
"فِى جَنَّـٰتِ ٱلنَّعِيمِ"
Katika Mabustani yenye Neema
" ثُلَّةٌ۬ مِّنَ ٱلۡأَوَّلِينَ"
Sehemu kubwa ni miongoni mwa (watu)wa mwanzo(Zamani)
Kwani ikawa zamani kwa sababu walikua wakiishi kwenye (Being)zao, wanaishi kwa (Feeling)kutumia moyo sio kwa njia za (Mind)Akili .
"وَقَلِيلٌ۬ مِّنَ ٱلۡأَخِرِينَ"
"Na sehemu ndogo ni miongoni mwa watu wa mwisho
Huu wakati tulonao ni mashaka makubwa ya kurithi au kuyapata au kupata kuwa karibu na Mollah wetu kutokana na ujanja tulonao, kila mtu kabeba mzigo wa mawazo machafu, mawazo mabaya, dhuluma, magonvi, hasada, chuki, viburi. Na maelezo yanaendelea mpaka aya ya 26 kuwaeleza hao watakaorithi huo Ufalme wa Mwenye enzi Mungu.
Ama wale waloshindwa kuupata huo umasikini lakini wakafanya kheri, na walotubia makosa yao nao imetajwa sehemu watakayokua wao nayo inaanzia aya ya 27 mpaka aya ya 40. Kwa hiyo bidii yako ndio itakayokufanya ima uwe Mfalme au Mtu wa kawaida, zisome hizo aya halafu utafanya uamuzi unataka vipi. Na kama umeshindwa kabisa basi jitaarishe na kundi la tatu ambalo litakua makaazi yako Motoni, Na kumbuka hiyo ni ahadi ya Mwenye enzi Mungu.