Wednesday, June 1, 2016

RAMADHAN NI VAZI LA UCHA MUNGU PART 1

Asalaam Aleiykum

Zimekufikia habari za Mwezi ambao ndani yake kuna Rehma, Kati yake kuna Maghfira(Msamaha), Na Mwisho wake kuna Dhamana.
Vipi basi yanapatikana matatu haya?, hili ndio shiko la darsa yetu ya leo, Ndio safari tutakayo kwenda mimi na wewe kama walivokwenda Nabii Musa a.s na Msaidizi wake, Nini kilitokea kwenye hiyo safari yao, na nini ilikua kusudio ya safari ile?. Quraan sura ya (Al-Kahf )kuanzia aya ya 60.
"وَإِذۡ قَالَ مُوسَىٰ لِفَتَٮٰهُ لَآ أَبۡرَحُ حَتَّىٰٓ أَبۡلُغَ مَجۡمَعَ ٱلۡبَحۡرَيۡنِ أَوۡ أَمۡضِىَ حُقُبً۬ا "
Na (Kumbukeni) Musa alipomwambia kijana(Msaidizi)wake nitaendelea kwenda (hii safari)mpaka nifike katika maungano ya bahari mbili, au niendelee kwa karne(mpaka nikutane na huyo ninayetaka kukutana naye).
Na hivyo ndio inavotakiwa katika kutafuta elimu hakuna kuchoka wala kuzeeka, vipi ilitokea safari hii, Anahadithia Ubai ibn Kaab alimsikia Mtume s.a.w akisema, siku moja Nabii Musa a.s alikua akitoa mawaidha akaulizwa swali hili, Kiumbe gani Mwenye elimu kupita wote, akajibu ni mimi, Hapo Mwenye enzi Mungu akamwambia yuko aliyekuzidi "Ewe Musa" alijibiwa hivyo kwa sababu hajarejesha jawabu hilo kwa Mwenye enzi Mungu na kwa kutaka kufahamishwa akaambiwa nenda utakutana na Mtu huyo kwenye makutano ya Bahari mbili, Sehemu hiyo haijatajwa wapi lakini wanazuoni wamekisia ilikua labda ilikua (gulf of Suez and Gulf of Aqaba) kaskazini mwisho kwenye (Red Sea) na wengine wanasema yaweza kua baina ya (Bitter lake and Timsah lake) katika eneo la (Suez Canal) Kwa hiyo fundisho hapo usijitie kiburi ukasema wewe una Elimu kushinda wenzio, wewe ndio mwenye kujua zaidi.
Unaingia katika Mwezi wa Ramadhan usione uvivu kusoma na kujifunza mambo yenye faida kubwa na wewe, wacha yapasue moyo wako utapata faida kubwa kabisa ikiwa utazingatia unachokisoma, kumbuka darsa hii inatoka moyoni kwangu kuja moyoni kwako moja kwa moja ili tupate kufanikisha Ramadhan yetu kwa uadilifu na Imani ya hali ya juu kabisa.
" فَلَمَّا بَلَغَا مَجۡمَعَ بَيۡنِهِمَا نَسِيَا حُوتَهُمَا فَٱتَّخَذَ سَبِيلَهُ ۥ فِى ٱلۡبَحۡرِ سَرَبً۬ا "
Basi walipofika wote wawili (Sehemu)zinapoungana (hizo Bahari)walimsahau samaki wao, Naye akashika njia yake kwenda baharini, hali yakuwa inafanya alama.
Hapo yanatokea mambo ya ajabu(mystical) Na ajabu yoyote haitokei mpaka uchoke, ujanja umekwisha, ukaidi huna tena ndio unatulia kufahamu mambo kwa undani kabisa, hapo tena unakua huna msimamo huna chochote ndio ukweli unadhihiri, mambo ya ajabu yanatokea Samaki kishapikwa anashika njia kurudi baharini.
"فَلَمَّا جَاوَزَا قَالَ لِفَتَٮٰهُ ءَاتِنَا غَدَآءَنَا لَقَدۡ لَقِينَا مِن سَفَرِنَا هَـٰذَا نَصَبً۬ا "
Na Walipofika mbele (Nabii Musa)alimwambia (Msaidizi)kijana wake, Tupe chakula chetu cha asubuhi, maana tumepata uchofu katika safari yetu.
Mpaka jitihada zako zimalizike, mpaka uwe ushachoka ndio ukweli unajitokeza, hiyo kufahamishwa Elimu haiji ila kutoka kwa Mwenye enzi Mungu, na wewe inakutokezea wakati mwengine unafanya kitu hupati jawabu, au jina la mtu utalifikiri haliji Akilini, mara umekaa tu na shughuli nyengine linakujia jawabu, na hivyo ni kufahamishwa Elimu zote zinatoka kwake yeye Mjuzi wa kila jambo.
" قَالَ أَرَءَيۡتَ إِذۡ أَوَيۡنَآ إِلَى ٱلصَّخۡرَةِ فَإِنِّى نَسِيتُ ٱلۡحُوتَ وَمَآ أَنسَٮٰنِيهُ إِلَّا ٱلشَّيۡطَـٰنُ أَنۡ أَذۡكُرَهُ ۥ‌ۚ وَٱتَّخَذَ سَبِيلَهُ ۥ فِى ٱلۡبَحۡرِ عَجَبً۬ا "
Akasema unaona pale tulipopumzika katika Mlima(Jabali)basi hapo nimesahau(kukupa habari)ya yule Samaki, Na hakuna aliyenisahaulisha isipokua Shetani, nisikumbuke, Naye akashika njia yake baharini kwa namna ya Ajabu. Mambo ya (mystical) lazima yawe ya ajabu, huwezi ku(Explain) na hivyo ndio inavokua katika safari zote za ajabu na kutafuta Elimu, lazima vya zamani visahaulike ili vipya vipate kuingia, usije kushangaa mbona samaki anatembea, mbona hili sijawahi kusomeshwa na Sheikh wangu, utakuja kukosa jambo la muhimu nalo la kupata ujuzi zaidi katika safari hii.
Kwa hiyo napenda kukujulisha kwenye kisa hicho msaidizi wa Nabii Musa a.s na yule samaki wote wanapotea na kusahauliwa, na mimi na maandishi yangu tutapotea katika safari hii utabakia wewe na Faida za Ramadhan na siri yake, pamoja na vazi lake,  ni kama Nabii Musa a.s alivobaki na mambo matatu ya hekima alofundishwa na (Mja Mwenye Elimu).
Popote pale inapotajwa siri napenda ufahamu ni kitu chenye kujificha au kufichwa, Kwa hiyo ukisoma kwa moyo ulotulia utapata faida kubwa ya siri hizo, Lakini ukisoma kwa akili mimi tayari najua utajikuta unakwenda safari ya tabu na siku hizi lazima uombe(Visa), utajikuta umebaki na maneno yangu lakini umekosa kile kilichomo ndani ya maneno hayo.
Kutaka kulijua vazi hili la Ucha Mungu endelea part 2

RAMADHAN NI VAZI LA UCHA MUNGU PART 2

Asalaam Aleiykum

Tuanze na aya iliyomo kwenye sura ya (Aaraf)aya ya 26, tunalitafuta guo la Ucha Mungu aya hii itatufunganisha na darsa yetu ya leo ili tupate kuanza safari yetu ya uchambuzi, aya inasema nini kuhusu kadhia hii.

يَـٰبَنِىٓ ءَادَمَ قَدۡ أَنزَلۡنَا عَلَيۡكُمۡ لِبَاسً۬ا يُوَٲرِى سَوۡءَٲتِكُمۡ وَرِيشً۬ا‌ۖ وَلِبَاسُ ٱلتَّقۡوَىٰ ذَٲلِكَ خَيۡرٌ۬‌ۚ ذَٲلِكَ مِنۡ ءَايَـٰتِ ٱللَّهِ لَعَلَّهُمۡ يَذَّكَّرُونَ
Enyi Wanaadamu hakika tumekuteremshieni nguo zifichazo tupu zenu na nguo za pambo, Na nguo za utawa(Ucha Mungu)ndizo bora, hayo ni katika ishara za Mwenye enzi Mungu ili wapate kukumbuka.
Nataka uyatizame maneno mawili yaliyomo katika aya hiyo yanosema (Ishara na Kukumbuka)hayo yatakua na faida kubwa na wewe katika kuifahamu darsa hii.
Naam:tumepewa aina mbili za nguo, ama ile ya kwanza sote tunaijua ni kwa ajili ya kuhifadhi tupu zetu na kadhalika kujipamba, unalikumbuka neno (Ishara) basi inaanzia hapa, kwanini ikatajwa tupu?, kwa sababu jambo la mwanzo Mwanaadamu au tumtaje Baba yetu Nabii Adam na Mama yetu Hawa, walolipata  (Awareness)Fahamu Waligundua tupu zao. Vipi hilo linahusiana na (Saum) ya Mwezi wa Ramadhan?, endelea kusoma kwa uangalifu  ili uzipate (ishara), maana ya Ishara ni kuashiria jambo.
"Ewe Adam Msiukaribie mti huu mkala tunda lake" Pasipo na uwerevu, na ushawishi wa (Shetani)wakapinga Amri ya Mwenye enzi Mungu wakala tunda kutoka kwenye ule mti na kutolewa Peponi, Yote haya yamehusiana na hiyo (Awareness)Fahamu waloipata, ndio sasa ikaonekana itakua shida kuishi katika Ulimwengu huu, vipi tutatizamana na vizazi vyetu, vipi tutawaangalia wazee wetu ndipo Mollah akatuteremshia vazi la kujistiri, Na hii imekwenda (Deep)hata yale Makabila (Primitive)yanafunika tupu zao, kwa sababu ingekua hatari ee tunafunika hali hii(sex)imo mawazoni nyakati zote, ukiona mtu kajipamba unawacha mpaka(tasbih).
Kilichokusudiwa kuhifadhiwa Rasmi sio hiyo tupu kumbuka kuna neno ishara ambalo linaashiria kuhifadhiwa na kutulizwa ni hiyo (Mind)yako(Akili), au ita (awareness), hilo ndilo kusudio ya guo la kwanza lilotajwa kwenye hiyo aya. Kumbuka umo katika Safari ya kulijua Vazi la Ucha Mungu katika Mwezi huu wa Ramadhan, Vipi tuifunge na vipi tuipate Taqwa inokuja na hayo mambo matatu yalotajwa mwanzoni mwa Darsa hii.
Sasa Wacha tulifungue Guo la pili ambalo ndio hilo vazi la Ucha Mungu.
Endelea Part 3





RAMADHAN NI VAZI LA UCHA MUNGU PART 3

Asalaam Aleiykum

Tumekwisha kuona au kusoma au kujua vipi (awareness)Fahamu zetu zinavokua zikikutana na jambo la (tupu), vipi akili ina haribika, uharibifu gani unatokea, na sasa tunajua nini kinatokea kama kitu hicho kitafunikwa. Sasa ni wakati wa kulihudhuria Vazi la pili la Ucha Mungu, lile la mwanzo ni Vazi la (Mind)Akili na Utupu, Na hili la Pili ni la (Roho)na Ibada.
Kazi yetu kubwa hapa ni kujua vipi tutalivaa, basi kama aya ilivosema vazi hilo ni bora kwenu na hizo ni (alama)kutoka kwa Mollah wetu ili tupate "kukumbuka". Naendelea kukuonesha tena neno "(kukumbuka)", nakutaka ukumbuke lile vazi la kwanza Nje ni Guo na ndani ni utulivu, Na hili la Pili Nje (Action) ndani Mapenzi, Nini Utulivu? Utulivu ni (Peace)Islam(Surrender), Nini Mapenzi? ni (Bliss).
Kutokana na hayo Mapenzi wewe ndio umeumbwa, kutokana na hayo mapenzi wewe ndio unaishi, kutokana na hayo mapenzi wewe Unaruzukiwa, kutokana na hayo mapenzi Ulimwengu huu unamsabahi Mwenye enzi Mungu, Sasa na wewe unakumbushwa jiunge na Mapenzi hayo ili upate Furaha, upate afya na uipate Pepo ya Mollah wako, Na sharti lenyewe la kujiunga ni lazima uvae hili vazi la Ucha Mungu, unatakiwa bila ya kulazimishwa Umpende Mollah wako, uwapende viumbe wenzako, na utende yalo mema.
Ikiwa utafanya hivo kwa uadilifu kwa upande wake Mwenye enzi Mungu atakupa hayo mambo matatu ambayo yamo katika hiyo Ramadhan,  Rehma, Maghfira na Dhamana ya kutoingia motoni.
Vipi tutalivaa Guo hili la Taqwa?
Kumbuka bado tumo kwenye safari yetu ya kutafuta vazi la Taqwa na sasa tunachukua aya hususia iloamrisha kufunga Ramadhan(Baqara 183).
"يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ كُتِبَ عَلَيۡڪُمُ ٱلصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِڪُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَتَّقُونَ "
Enyi Mloamini Mmelazimishwa kufunga(saumu)kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu.
Kabla ya kuendelea mbele wacha turudi nyuma tukalihudhurie lile tukio maarufu la mwanzo waloambiwa wazee wetu Bwana Adam na Bibi Hawa walipokatazwa wasile tunda kwenye ule mti, Nini kiliwatokezea walipokwenda kinyume na Amri ya Mwenye enzi Mungu? walipata (Awareness)Fahamu.
Basi Napenda utambue na hivi sasa mnaamrishwa tena msile(Fungeni) Nini Kinapatikana?, Hapa itabidi mnipe nafasi nifafanue japo kwa ufupi ili mpate kunifahamu, Napenda kufahamisha kuwa kuna vitu vitatu vinatokea kwa Mollah wetu navyo ni hivi(From awareness to intelligence from intelligence to love) Na hayo Mapenzi ndio zawadi ya juu Mja kushushiwa kutoka kwa Mollah wako, Nisiseme Mapenzi watu  (Wakaanza kuchemsha Supu za Pweza, wengine wakatafuta uji wa kungu manga, na wengine kumtafuta ndege kisiji)sio aina hiyo ya mapenzi, Mapenzi yalokusudiwa hapo yale yanokuja bila sababu, yale unatoa huhitaji malipo, yale ambayo uko radhi kulala na njaa mwenzio apate kula yeye, mapenzi ya mfano wa Mama hatarajii hata kama utampenda kama anavokupenda yeye, yeye anafanya (for the sake of Love)Sasa nini unapata kama utafunga kikweli kweli kwa Imani ya juu kabisa? hapa inabidi ukumbuke tena ulipokula tunda ulipata (Awareness)Fahamu, na sasa kitu cha mwanzo unapata nini?
Endelea part 4 

RAMADHAN NI VAZI LA UCHA MUNGU PART 4

Asalaam Aleiykum

Kitu cha Mwanzo safari hii upatacho ni (awareness of Love) vipi inakua, pengine Mja siku zote mambo haya yanakutokezea huyajui, basi anza kuyajua mambo haya kwenye Ramadhan yako ya mwanzo ili usikose makusudio na faida ya Ramadhan. Kitu cha mwanzo kama utachunguza wakati unavaa guo hili la (Taqwa) ni njaa, wewe umezoea wakati wote unakula asubuhi, mchana na usiku, leo umefika ule wakati hujatia chakula, hapo mazoea yanaondoka inakuja(1) (Awareness of Body)Fahamu ya mwili wako, unahitaji chakula wakati wake ushafika na wewe huupi chakula, Na vyakula vyote vimo kwenye nyumba na Mahotelini na madukani vinauzwa, lakini wewe kwa Mapenzi tu ya kufata amri ya Mollah wako leo Umefunga hugusi chakula.
(2)(Mind)Akili inataka mambo yake ya kusema watu, kuzini, kudhulumu,wizi,rushwa,mazungumzo yasofaa, kutizama mambo machafu, wewe umekazana hutekelezi amri za akili, ukiweza kwenda (Beyond) vitu viwili hivyo ndipo unapojikuta wewe ni (Pure Soul)Roho safi, hapo ndipo yanapokaa ita(Mapenzi)(Dhikr)(Watch)(Witness)(Remember)(Kukumbuka)(Mindful)ita jina lolote lakini hapo ndipo kwenye kusudio la (Saumu)hapo ndipo kwenye hiyo(Itikaf)unakua huna fikra chafu ila kumkumbuka Mollah wako, una (Watch)kila kitu lakini hushiriki, njaa inakuja,watu wanaendelea na upuuzi wao wewe unabaki kuwa shahidi tu, unaishi katika hali ya kusikia na kuona mambo yote yanatokea lakini wewe hayakugusi, Unaishi kwenye (Roho)uko (Alert)wakati wote unakumbuka unamtaja Mollah wako ukiwa katika hali ya (Full Aware).
Napenda nikumbushe tena wakati ule wa mwanzo Mzee wetu Adam alivopata (Awareness) kapata katika hali ya kuasi kutokana na (kutokujua). Lakini safari hii wewe umo kwenye werevu(Awareness)Fahamu yenye kutii, umejaa mapenzi ya Mollah wako, umejifunga kutekeleza amri yake, umevijua kua Mwili una njaa, na Akili ina mshipa wa Maasi vyote hivyo umeweza kuvimudu na kuvishinda, sasa umefika wakati wa kusema Mollah wangu nimeyefanya haya kwa ajili yako Mollah wangu.(Quraan Al-Anaam-162)
"قُلۡ إِنَّ صَلَاتِى وَنُسُكِى وَمَحۡيَاىَ وَمَمَاتِى لِلَّهِ رَبِّ ٱلۡعَـٰلَمِينَ "
Sema,Hakika Sala yangu, Na Ibada zangu, na Uzima wangu, Na kufa kwangu ni kwa ajili ya Mwenye enzi Mungu Muumba wa walimwengu wote.
Kutokana na Uwezo huo mimi nasimama kutekeleza vitendo vya mapenzi Mollah wangu, kama vipi?
Endelea part 5

RAMADHAN NI VAZI LA UCHA MUNGU PART 5

Asalaam Aleiykum

Mapenzi hayajulikani, lakini vitendo vyake vinajulikana ndio watu wakasema fulani anapenda, Na kama wewe ni kweli mpenzi wa Mungu basi matendo yako yatakua kulisha maskini, Kuwaangalia mayatima, kuwapa haki ndugu jamaa na marafiki, kujishughulisha kuwasaidia hata wapita njia, na kuwatunza mpaka wanyama wenye kuishi katika Ufalme wa Mwenye enzi Mungu.
Kujiepusha na kila jambo baya ambalo Mwenye enzi Mungu amelikataza, pia kujielewa miezi yote kumi na moja ulikua hujavaa guo la Ucha Mungu, ona haya Mollah wako anakuona, Malaika wanakuona kua huna cha kukusitiri, upo Mtupu, sasa umekujia Mwezi huu Mtukufu omba sana kwa Mollah wako akuvike guo hili la mapenzi, Sema nitie mapenzi niwe nakuabudu japo sikuoni, hakika mimi mapenzi siyajui, ila nasubiri kutoka katika enzi yako unipe mapenzi kama ulivonipa (awareness)Fahamu.
Basi nipe mapenzi ya kukupenda wewe niwe Rafiki yako wa (kimya), Nipe mapenzi nivipende viumbe vyako na kuwa karibu na wewe, Nitie matumaini ya kupata Rehma zako kwenye kumi hili la mwanzo, nipe mapenzi yako unisamehe kwenye kumi lako la pili, Nifanye niwe katika waja wako walio karibu na wewe, Ikisha nichukulie mimi dhamana ya kutoingia motoni.
Mollah wangu Najua Mwenye kulivaa guo lako la Ucha Mungu hapati tabu kwenye maisha, hana mahuzuniko wala shida katika Uhai wake, Na daima yumo Furahani kwa kupata Rehma, Kheri, Na Neema zako wewe Subhanna.
Basi na Mimi ntakapolivaa guo hili la Ucha Mungu nijaalie nidumu nalo kwa Rehma zako, isije ikawa ikisha Ramadhan nalivua tena kwa kulichana chana guo hili. Niepushe mimi na kuvaa nguo za chuki, dhulma na balaa za ujambazi wa Kiroho.
Mollah wangu wewe ni mwenye kuona na kusikia basi natuma maombi yangu nikitaraji utanikubalia. Ipate hali hiyo utakua umeipata Saumu, ipate hali hiyo utayapata mapenzi ya Mwenye enzi Mungu.