Wednesday, June 1, 2016

RAMADHAN NI VAZI LA UCHA MUNGU PART 5

Asalaam Aleiykum

Mapenzi hayajulikani, lakini vitendo vyake vinajulikana ndio watu wakasema fulani anapenda, Na kama wewe ni kweli mpenzi wa Mungu basi matendo yako yatakua kulisha maskini, Kuwaangalia mayatima, kuwapa haki ndugu jamaa na marafiki, kujishughulisha kuwasaidia hata wapita njia, na kuwatunza mpaka wanyama wenye kuishi katika Ufalme wa Mwenye enzi Mungu.
Kujiepusha na kila jambo baya ambalo Mwenye enzi Mungu amelikataza, pia kujielewa miezi yote kumi na moja ulikua hujavaa guo la Ucha Mungu, ona haya Mollah wako anakuona, Malaika wanakuona kua huna cha kukusitiri, upo Mtupu, sasa umekujia Mwezi huu Mtukufu omba sana kwa Mollah wako akuvike guo hili la mapenzi, Sema nitie mapenzi niwe nakuabudu japo sikuoni, hakika mimi mapenzi siyajui, ila nasubiri kutoka katika enzi yako unipe mapenzi kama ulivonipa (awareness)Fahamu.
Basi nipe mapenzi ya kukupenda wewe niwe Rafiki yako wa (kimya), Nipe mapenzi nivipende viumbe vyako na kuwa karibu na wewe, Nitie matumaini ya kupata Rehma zako kwenye kumi hili la mwanzo, nipe mapenzi yako unisamehe kwenye kumi lako la pili, Nifanye niwe katika waja wako walio karibu na wewe, Ikisha nichukulie mimi dhamana ya kutoingia motoni.
Mollah wangu Najua Mwenye kulivaa guo lako la Ucha Mungu hapati tabu kwenye maisha, hana mahuzuniko wala shida katika Uhai wake, Na daima yumo Furahani kwa kupata Rehma, Kheri, Na Neema zako wewe Subhanna.
Basi na Mimi ntakapolivaa guo hili la Ucha Mungu nijaalie nidumu nalo kwa Rehma zako, isije ikawa ikisha Ramadhan nalivua tena kwa kulichana chana guo hili. Niepushe mimi na kuvaa nguo za chuki, dhulma na balaa za ujambazi wa Kiroho.
Mollah wangu wewe ni mwenye kuona na kusikia basi natuma maombi yangu nikitaraji utanikubalia. Ipate hali hiyo utakua umeipata Saumu, ipate hali hiyo utayapata mapenzi ya Mwenye enzi Mungu.



No comments:

Post a Comment