Wednesday, June 1, 2016

RAMADHAN NI VAZI LA UCHA MUNGU PART 1

Asalaam Aleiykum

Zimekufikia habari za Mwezi ambao ndani yake kuna Rehma, Kati yake kuna Maghfira(Msamaha), Na Mwisho wake kuna Dhamana.
Vipi basi yanapatikana matatu haya?, hili ndio shiko la darsa yetu ya leo, Ndio safari tutakayo kwenda mimi na wewe kama walivokwenda Nabii Musa a.s na Msaidizi wake, Nini kilitokea kwenye hiyo safari yao, na nini ilikua kusudio ya safari ile?. Quraan sura ya (Al-Kahf )kuanzia aya ya 60.
"وَإِذۡ قَالَ مُوسَىٰ لِفَتَٮٰهُ لَآ أَبۡرَحُ حَتَّىٰٓ أَبۡلُغَ مَجۡمَعَ ٱلۡبَحۡرَيۡنِ أَوۡ أَمۡضِىَ حُقُبً۬ا "
Na (Kumbukeni) Musa alipomwambia kijana(Msaidizi)wake nitaendelea kwenda (hii safari)mpaka nifike katika maungano ya bahari mbili, au niendelee kwa karne(mpaka nikutane na huyo ninayetaka kukutana naye).
Na hivyo ndio inavotakiwa katika kutafuta elimu hakuna kuchoka wala kuzeeka, vipi ilitokea safari hii, Anahadithia Ubai ibn Kaab alimsikia Mtume s.a.w akisema, siku moja Nabii Musa a.s alikua akitoa mawaidha akaulizwa swali hili, Kiumbe gani Mwenye elimu kupita wote, akajibu ni mimi, Hapo Mwenye enzi Mungu akamwambia yuko aliyekuzidi "Ewe Musa" alijibiwa hivyo kwa sababu hajarejesha jawabu hilo kwa Mwenye enzi Mungu na kwa kutaka kufahamishwa akaambiwa nenda utakutana na Mtu huyo kwenye makutano ya Bahari mbili, Sehemu hiyo haijatajwa wapi lakini wanazuoni wamekisia ilikua labda ilikua (gulf of Suez and Gulf of Aqaba) kaskazini mwisho kwenye (Red Sea) na wengine wanasema yaweza kua baina ya (Bitter lake and Timsah lake) katika eneo la (Suez Canal) Kwa hiyo fundisho hapo usijitie kiburi ukasema wewe una Elimu kushinda wenzio, wewe ndio mwenye kujua zaidi.
Unaingia katika Mwezi wa Ramadhan usione uvivu kusoma na kujifunza mambo yenye faida kubwa na wewe, wacha yapasue moyo wako utapata faida kubwa kabisa ikiwa utazingatia unachokisoma, kumbuka darsa hii inatoka moyoni kwangu kuja moyoni kwako moja kwa moja ili tupate kufanikisha Ramadhan yetu kwa uadilifu na Imani ya hali ya juu kabisa.
" فَلَمَّا بَلَغَا مَجۡمَعَ بَيۡنِهِمَا نَسِيَا حُوتَهُمَا فَٱتَّخَذَ سَبِيلَهُ ۥ فِى ٱلۡبَحۡرِ سَرَبً۬ا "
Basi walipofika wote wawili (Sehemu)zinapoungana (hizo Bahari)walimsahau samaki wao, Naye akashika njia yake kwenda baharini, hali yakuwa inafanya alama.
Hapo yanatokea mambo ya ajabu(mystical) Na ajabu yoyote haitokei mpaka uchoke, ujanja umekwisha, ukaidi huna tena ndio unatulia kufahamu mambo kwa undani kabisa, hapo tena unakua huna msimamo huna chochote ndio ukweli unadhihiri, mambo ya ajabu yanatokea Samaki kishapikwa anashika njia kurudi baharini.
"فَلَمَّا جَاوَزَا قَالَ لِفَتَٮٰهُ ءَاتِنَا غَدَآءَنَا لَقَدۡ لَقِينَا مِن سَفَرِنَا هَـٰذَا نَصَبً۬ا "
Na Walipofika mbele (Nabii Musa)alimwambia (Msaidizi)kijana wake, Tupe chakula chetu cha asubuhi, maana tumepata uchofu katika safari yetu.
Mpaka jitihada zako zimalizike, mpaka uwe ushachoka ndio ukweli unajitokeza, hiyo kufahamishwa Elimu haiji ila kutoka kwa Mwenye enzi Mungu, na wewe inakutokezea wakati mwengine unafanya kitu hupati jawabu, au jina la mtu utalifikiri haliji Akilini, mara umekaa tu na shughuli nyengine linakujia jawabu, na hivyo ni kufahamishwa Elimu zote zinatoka kwake yeye Mjuzi wa kila jambo.
" قَالَ أَرَءَيۡتَ إِذۡ أَوَيۡنَآ إِلَى ٱلصَّخۡرَةِ فَإِنِّى نَسِيتُ ٱلۡحُوتَ وَمَآ أَنسَٮٰنِيهُ إِلَّا ٱلشَّيۡطَـٰنُ أَنۡ أَذۡكُرَهُ ۥ‌ۚ وَٱتَّخَذَ سَبِيلَهُ ۥ فِى ٱلۡبَحۡرِ عَجَبً۬ا "
Akasema unaona pale tulipopumzika katika Mlima(Jabali)basi hapo nimesahau(kukupa habari)ya yule Samaki, Na hakuna aliyenisahaulisha isipokua Shetani, nisikumbuke, Naye akashika njia yake baharini kwa namna ya Ajabu. Mambo ya (mystical) lazima yawe ya ajabu, huwezi ku(Explain) na hivyo ndio inavokua katika safari zote za ajabu na kutafuta Elimu, lazima vya zamani visahaulike ili vipya vipate kuingia, usije kushangaa mbona samaki anatembea, mbona hili sijawahi kusomeshwa na Sheikh wangu, utakuja kukosa jambo la muhimu nalo la kupata ujuzi zaidi katika safari hii.
Kwa hiyo napenda kukujulisha kwenye kisa hicho msaidizi wa Nabii Musa a.s na yule samaki wote wanapotea na kusahauliwa, na mimi na maandishi yangu tutapotea katika safari hii utabakia wewe na Faida za Ramadhan na siri yake, pamoja na vazi lake,  ni kama Nabii Musa a.s alivobaki na mambo matatu ya hekima alofundishwa na (Mja Mwenye Elimu).
Popote pale inapotajwa siri napenda ufahamu ni kitu chenye kujificha au kufichwa, Kwa hiyo ukisoma kwa moyo ulotulia utapata faida kubwa ya siri hizo, Lakini ukisoma kwa akili mimi tayari najua utajikuta unakwenda safari ya tabu na siku hizi lazima uombe(Visa), utajikuta umebaki na maneno yangu lakini umekosa kile kilichomo ndani ya maneno hayo.
Kutaka kulijua vazi hili la Ucha Mungu endelea part 2

No comments:

Post a Comment