Sunday, July 26, 2015

PEPO YA DUNIA PART 1

Asalaam Aleiykum

Tumemaliza Mwezi wa Ramadhani kwa salama, tunamshukuru Mollah, Pia tunamuomba atukubalie Saum zetu na atusamehe makosa yetu atupe Rehma zake sisi na walotangulia mbele ya haki kwa jumla.
Hatuna budi na sisi kuendelea kukumbushana kwa njia ya darsa zetu kama kawaida, ama kwa wale walopata Ucha Mungu ndani ya Mwezi huo Mollah awajaalie kuendelea katika hali hiyo, Na kwa wale ambao pengine hawakubahatika, pengine (Yaum Shaka)imewafanya warejee kwenye mambo ya kula mchana, kwa sababu kuna baadhi wanasubiri wakisikia umeandama tu, Na wao hao wanapanada (Appolo)kurejea kwenye mambo walo yaacha mwezi wa kula mchana, Na ukirejea katika hali hiyo unaanza kujitia kwenye mateso tena ya miezi 11.
Sasa ufanye nini kuepuka hali hiyo? Ndio nimekuletea Darsa hii ya (Pepo ya Dunia) nisiseme hivyo ukaanza kuleta tafsiri zako za Maajabu, ukadhani na gawa viwanja vya pepo duniani, dhumuni langu ni kukufanya uishi kwa (Amani)na hiyo ndio maana ya (Pepo nilokusudia) Nakufahamisha vitu kama utavifanya basi dhiki katika ulimwengu huu zitaondoka kabisa, utaishi katika ile aya ya mawalii isemayo(Hawana hofu wala hawahuzuniki).
Nini ntakuonesha?, Ntakuonesha Njia ilonyooka na kama utaifata basi na wewe utabadilika na moja kwa moja utajikuta Mcha Mungu bila hata ya kufanya juhudi kubwa, nikisema bila ya juhudi kubwa usidhani kazi rahisi, kwa sababu nafahamu (Mahadith na Mawaidha)vyote hivyo vishagonga Ukuta, Mja hubadiliki, kwa hiyo kazi niloifanya mimi sio mpya ni kukupa kwa urahisi mambo ya kufanya ili uziwache njia 10 za vichochoroni ili uipate hiyo njia moja ilonyooka ambayo ndio kila Mwanadamu na katika Dini zote zinasisitiza kufatwa.
Mimi ninachofanya ni kukumbusha kwa Mpango maalum wa urahisi pengine ukikumbuka unaweza kuzifata, na ukizifata zote kwa ukamilifu(Automatic)unakua Mcha Mungu, kwani utakua huna pengine kwa kwenda isipokua kwa Mollah wako.
Ili kuipata njia hii moja ilonyooka, iliyo sawa wacha tuzitaje na kuzichukua njia moja baada ya nyengine ili ukifanikiwa kuziacha hizi kumi, utawashinda matajiri, utawaonea huruma maskini, utawacheka Marais na wale wote wenye kugaragara kutafuta umaarufu, na wewe pekee ndio utakua ni mwenye kufuzu.
Sasa kuipata hali hiyo itabidi uyaache mambo yafatayo kumi, na ni lazima uyaache yote ndio uipate hiyo pepo ya Dunia(Bliss).
Mambo hayo yote yametajwa katika Quraan na yana kuhusu wewe ambaye unayo mambo hayo, na kama huna hata moja basi wewe Mcha Mungu, wewe umo furahani. Sasa nayataja mambo hayo ili tupate kuyaacha na muhimu uyaache yote, kwa sababu nitataja na madhara yake kwa hiyo fatilia kwa makini sana.
endelea part 2.


PEPO YA DUNIA PART 2

Asalaam Aleiykum

Mwanaadamu una mambo kumi yamekuganda yanakutesa bila wewe kujijua, yamekukamata yanakuangamiza vibaya sana, tuliza akili uyafahamu ikisha yafanye kuwa Adui wako mkubwa.
Katika Mambo hayo kumi yamegawika mafungu matatu, Fungu la mwanzo lina mambo matatu ambayo yanategemea (Mwili) wako, Fungu la Pili lina mambo manne ambayo yanategemea (Mdomo) wako, na Fungu la tatu ambalo ni la mwisho linategemea (Akili)yako.
Sasa kabla ya kuyaingia mambo haya hebu tutizame sheria ya Mwenye enzi Mungu inasemaje kuhusu ukifanya katika hayo kumi, lolote lile lazima ujue utalipwa, tuhudhurie sura ya (Luqman aya ya 16)يَـٰبُنَىَّ إِنَّہَآ إِن تَكُ مِثۡقَالَ حَبَّةٍ۬ مِّنۡ خَرۡدَلٍ۬ فَتَكُن فِى صَخۡرَةٍ أَوۡ فِى ٱلسَّمَـٰوَٲتِ أَوۡ فِى ٱلۡأَرۡضِ يَأۡتِ بِہَا ٱللَّهُ‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ۬
Ewe Mwanangu kwa hakika jambo lolote liwe japo chembe ya (Atom)hardali, likawa ndani ya Jabali au Mbinguni au katika ardhi, Mwenye enzi Mungu atalileta(Amlipe aliyefanya) bila shaka Mwenye enzi Mungu ni mjuzi wa mambo yalofichikana na yalioyo dhahiri.
Kwa hiyo tumeona chochote kile kinalipwa ndio katika sheria ya Mwenye enzi Mungu na wala huna uwezo wa kuiepuka, na katika malipo hayo ndio yanakufanya maisha yako yote yawe dhiki tupu, kwa sababu unaendelea kutenda, na kifimbo cheza kinaendelea kukuchapa, ili malipo yasite basi na wewe unatakaiwa uwache matendo yako,ubadilike kabisa, kwa hiyo sasa tunaingia katika hayo mambo tupate kuyajua na kama tukiweza kuyaacha tutaishi tukiwa na furaha Duniani hapa. Kabla ya kwenda huko nataka kurahisisha mambo kwa kutaja aya zitobeba mambo hayo kwa jumla, badala ya kutaja moja baada ya jengine.
Ama yale ya Mwanzo ya Mwili(Body) yatabebwa na aya ya 68 sura ya (Furqan).
وَٱلَّذِينَ لَا يَدۡعُونَ مَعَ ٱللَّهِ إِلَـٰهًا ءَاخَرَ وَلَا يَقۡتُلُونَ ٱلنَّفۡسَ ٱلَّتِى حَرَّمَ ٱللَّهُ إِلَّا بِٱلۡحَقِّ وَلَا يَزۡنُونَ‌ۚ وَمَن يَفۡعَلۡ ذَٲلِكَ يَلۡقَ أَثَامً۬ا
"Na Wale wasiomuomba Mungu  mwengine pamoja na Mwenye enzi Mungu, Wala hawaui Nafsi aliyoiharamisha Mwenye enzi Mungu isipokua kwa haki, Wala hawazini, na atakae fanya hayo atapata Madhara.(hapa kwenye Ulimwengu)"
Ama yale ya Pili na ya Tatu ya (Mouth)Mdomo na (Thought)Dhana hayo yanatoshwa kubebwa na aya 12 ya sura ya hujurat isemayo,
يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱجۡتَنِبُواْ كَثِيرً۬ا مِّنَ ٱلظَّنِّ إِنَّ بَعۡضَ ٱلظَّنِّ إِثۡمٌ۬‌ۖ وَلَا تَجَسَّسُواْ وَلَا يَغۡتَب بَّعۡضُكُم بَعۡضًا‌ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُڪُمۡ أَن يَأۡڪُلَ لَحۡمَ أَخِيهِ مَيۡتً۬ا فَكَرِهۡتُمُوهُ‌ۚ وَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ تَوَّابٌ۬ رَّحِيمٌ۬ .
"Enyi Mloamini Jiepusheni sana na Dhana, kwani dhana ni dhambi, Wala msipeleleze, Wala baadhi yenu wasiwasengenye (wasiwaseme)wengine, Je mmoja wenu anapenda kula nyama ya nduguye aliyekufa, la hampendi,Na Mcheni Mwenye enzi Mungu, Mwenye enzi Mungu ni Mwenye kupokea toba (na)Mwingi wa Kurehemu."
Naam kama unaitaka Pepo ya dunia uishi katika Ulimwengu huu kwa furaha bila ya matatizo yoyote itabidi ujiandae kuyaacha mambo 10 nitakayo yataja(ili uziepuke dhanbi), na ukifanya hivyo utakua hulipi tena madeni, hakudai mtu(Huna Dhanmbi), na kama hudaiwi basi ushakua(Free) na hiyo ndio ile aya ya wanobashiriwa wale Marafiki wa Mwenye enzi Mungu kuwa watakua hawana khofu hapa Ulimwenguni na huko Akhera wanapokwenda, sasa ili ujiunge nao ndio unatakiwa uwache mambo hayo na ukiyawacha tu unapata(Bliss)unakua rafiki wa Mwenye enzi Mungu hakuna kinachokupa shida tena. Sasa tunayaingia mambo yenyewe ili uyapate kuyajua na madhara yake.
Endelea part 3


PEPO YA DUNIA PART 3

Asalaam Aleiykum,

Jambo la Mwanzo(1) Kuuwa:unaambiwa usiue nafsi iloharamishwa kuuwawa, na huko kuuwa kuko kwa aina nyingi unakwenda jeshini, au unamua mtu kwa makusudi au kwa kutumia sababu za uchawi na mengineyo, basi lazima adhabu ile ya kuikatili nafsi na wewe ikukute, hata kama utaishi maisha yako yatakua ya dhiki kubwa na tafrani mpaka kuondoka kwenye Ulimwengu huu, ndio maana tunapata habari idadi kubwa ya majeshi wanorudi kupigana vita hatimaye wanajiua wenyewe kwa dhiki wanayo iona, kwa hiyo elewa ukimfanyia mwenzio uadui wa kumtoa roho yake na yako itatoka kikatili tena kidogo kidogo.
Jambo la Pili(2)Zinaa. Kuzini nako kuna madhara makubwa na mateso ya Akili(utakhiyari bora upigwe mikwaju)unateseka vyengine wewe hujui kwanini, lakini sababu zake kubwa ni kuzini, unafilisika, dhiki ya maisha, maradhi na mateso ya kila aina, wewe tizama kila ukimaliza kuzini nini kinatokea baada ya siku Arobaini chunguza maisha yako utaona madhara gani yanakufika?japo maradhi basi yatakuja japo kwa njia ya siri, au matatizo nyumbani kwako, wewe fanya uchunguzi usingoje mimi nikuhadithie, mimi nakutajia moto wewe ndio unao kuunguza basi pata hisia ujiepushe nao.
Jambo la Tatu(3)Wizi: Ndio na Rushwa zote katika Dhuluma, wewe chukua pesa au mali za watu, piga mvinyo lakini hutoipata raha katika dunia hii, utakaa na mapesa yako lakini huna furaha, huwezi hata kucheka, dhiki za nafsi zinakushika unaishi kama mnyama, na wasiwasi usokwisha na mali yako wanaitafuna watu wengine, wewe umebeba gunia la dhiki lilojaa madhara, mara wewe unaumwa mara watoto wanaumwa, pesa yote inamalizika kwa waganga. hayo ni machache katika yanohusu Mwili wako.
Sasa tunaingia yenye kuhusu Mdomo, kumbuka haya yote yanakuondoa kwenye Ucha Mungu na lazima ulipwe kwa ulitendalo.
Jambo la Nne(4)Uongo: uongo una madhara makubwa kabisa ukiutumia uongo unaweza kumuangamiza mtu, ukamfanya adhurike, basi ukitenda hilo na wewe kama anavoangamia huyo(Mtu au watu) na wewe jichunguze unapata malipo yale yale ya (Mtenda akitendewa hujihisi kaonewa)na kwambia hivyo kwa sababu huna uwezo wa kuona malipo yanavotokea lakini kama ungekua unajua vipi kutizama (Mtenda na Mtendewa)ungejua nimekusudia nini, yaani wewe mwenye kutenda ujitizame wakati unatenda, halafu wakati huo huo umtizame unayemtendea ndio utajua nimekusudia nini.
Jambo la Tano(5)Kuapiza au Chuki: kuapiza unatumia (Energy) kama atumiayo (Mganga au Mchawi)kumuangamiza Binaadamu mwenzio, kwa hiyo ukifanikiwa kumdhuru jua na wewe mfano wa dhara ile itakufika, japo inachukua muda lakini inakuja.
Jambo la Sita(6)Kuhujumu:Iwe mtu au Uchumi, basi elewa na wewe hujuma zitakurejea kama ulivohujumu, ikiwa umemzulia basi na wewe itakufika dhara ya mfano uleule ulomtendea mwenzio, sawa na kula nyama ya maiti, karaha zake.
Jambo la Saba(7)Kujisifu:Ukisha anza tabia hii kama wewe tajiri au una mali, inabidi lazima uilinde sifa hiyo, sasa madhara yake unakwenda kukopa, unakimbia watu lakini lazima ujioneshe kuwa ni wewe tajiri au una sifa fulani,unajipa dhiki mwenyewe na hiyo inaitwa kujidhuru mwenyewe kwa Mdomo wako(Self harm).
Na tunamalizia fungu la tatu la mwisho nalo ni la Mawazo.
Jambo la (8)Choyo au Wivu: Umeuangalia vipi wivu unavokutafuna, vipi unavotaraji mwenzio labda afilisike, vipi unateseka kwanini kapata yeye, tizama vipi choyo kinavokula unga wa Roho,Umekonda wewe una nini?  kumbe nyumba ya fulani tu inakushughulisha, unakua na hali gani hata wivu wa Mke mwenzio vipi unateseka,unakua mgonjwa, jiulize ikiwa nina wivu kama huu kweli naweza kuwa Mcha Mungu.
Jambo la Tisa(9)Hamaki:itizame inavo kuangamiza siku hizi tumeibadilisha jina tunaita ana (Blood Pressure)ndio kashapata maradhi, ni hamaki kwa kuwa hatujui vipi kuifanyia kazi hamaki ili itutoke, hamaki madhara yake makubwa sana, ina mdhuru mtu na kukudhuru mwenyewe, inakuangamiza inabidi uilinde kama sifa, hata hamaki ikiondoka inabaki kovu ya madhara yake, utasikia hasemi naye kwa kuwa wamegombana, hamaki ishakwisha wewe unaendelea kulienzi kovu lake, kwa sababu hamaki haikai masaa 24 inakwisha, sasa wewe unaendelea kununa miaka miwili huoni kama ni madhara juu yako, unajinyima raha bure pengine kwa jambo la kipuuzi.
Na Jambo la (10) Hamu au Uchu:Tamaa itizame inavokupeleka mbio, vipi unavoteseka iwe ya mtu au kitu, akili yote tafrani, una hangaika, watu wanakuuliza weye una nini pengine una hamu uwe tajiri, au una uchu umpate fulani, basi ndio unakua kama umeajiriwa, akili haipo tena, hamu jamani ina matatizo, mawazo yanakuwa na mawimbi, mashaka makubwa, huna raha kwenye Ulimwengu huu ukiwa una maradhi ya hamu.
Sasa ikiwa katika mambo hayo kumi huna hata moja basi wewe ndiye Mcha Mungu, wewe ndio ushafuzu, wewe ndio katika wale Marafiki wa Mwenye Enzi Mungu, na kama bado basi fanya mazoezi uyawache mambo hayo kumi, na yakiondoka kwenye nafsi yako, basi moja kwa moja (Bliss) Furaha kila saa na dakika na hiyo ndio (Nature) yako, na ndiyo Pepo yako katika Ulimwengu huu. Tunamuomba Mollah wetu atuwezeshe katika hayo.


Thursday, July 16, 2015

FURAHA YA EID PART 1

Asalaam Aleiykum

Nakutakieni Rehma za Mollah wangu zimiminike kwa Waislam wote, Walofunga na pia wasofunga, Yeye Mollah wetu Mlezi ni Mwenye kutupenda sote viumbe vyake. Ametukuka yule ambaye kwenye Miliki yake kuna jambo la Furaha kwa ajili ya Viumbe vyake. Nini Furaha ya Eid?. Ni kujijua kwamba umeitwa na Mollah wako na wewe ukakubali mwito huo, Furaha yenyewe imo ndani ya nafsi ya kujua kwamba umeitekeleza Ibada hii kwa Uangalifu na unyenyekevu, umejizuia na yale yote aliyoamrisha Mollah wako uyawache, na wewe kwa ridhaa yako umeyaacha na mwezi mzima ukajifunga kumuabudu Mollah wako na kumkumbuka yeye, sasa kwisha kwa huu mwezi sio ndio mwisho wa kumtii Mollah wako nini unatakiwa kufanya?.

FURAHA YA EID PART 2

Asalaam Aleiykum

Unachotakiwa kufanya hivi sasa ni kuilinda hali hiyo ulonayo ili isikuponyoke, Sasa hivi wewe unangara Taa, basi usiruhusu kiza kikafunika kwa miezi mengine 11, jitahidi uendelee na hali hiyo ulonayo ya Ucha Mungu na hivyo ndio utakua siku zote umo ndani ya Furaha ya Eid, usiruhusu kughafilika kwa siku hizi za mwanzoni ndio maana ukapewa sunna ya (Kufunga)sita, siku saba za mwanzo zinakua ngumu kuiweka hali yako ya Ucha Mungu, vishawishi vyote vinakuvutia urejee katika hali ya zamani, kila aina ya matamanio inafunguka tena kukutizama kama kweli wewe Mcha Mungu, au unatania, basi Mwenye kuutaka Ucha Mungu na ailinde hali ya (Taqwa) ili apate kufanikiwa.

FURAHA YA EID PART 3

Asalaam Aleiykum

Tunakuomba Mollah wetu tudumishe katika kukumbuka wewe, tupe mazuri kama ulivyowapa walo wema walotangulia, Tukinge na Shari za Ulimwengu, tunusuru na Balaa za maangamizo, tuondoshee dhiki za Roho, tupe Riziki za Halali, tulinde na uadui na wafanyao uwadui, tunusuru na majanga yaangamizao, tukirimu kheri zisizokua na mwisho, tumiminie neema zisizokatika, Ewe Mollah wetu tukirim tahfif kwenye Maradhi yetu, tuponeshe magonjwa makubwa na madogo, tuondoshee dhiki za Nafsi, tuondoshee hamaki na chuki, Ewe Mollah wetu tuoneshe njia za kheri ili tuzifate, tunusuru na adhabu zako za Dunia na Akhera.
Ewe Mollah wetu tusamahehe makosa yetu, tunusuru na Moto wa Jahannam, utupe Pepo yako ulotuahidi Mollah wetu. Tupunguzie Mollah wetu adhabu za kutoka Roho, tujaalie kivuli kitokacho kwako ambacho wanakipata waja wako wema, Mollah wetu zikubali Saum zetu, zipokee Ibada zetu, na utufutie makosa yetu.
Mollah wetu wasamehe walo wetu walotangulia mbele ya haki yako, waondoshee adhabu, uwakirimu msamaha wako na uwape pepo yako ya Allah. Yarabi tuongozee vizazi vyetu viwe katika waja wema, wanasuru na upotevu unozidi kuvumbuliwa, wape Elimu ya manufaa itokayo kwako wewe Mollah wetu, tujaalie kwa uwezo wako tuifunge Ramadhani yako ya mwakani kwa Radhi zako Yaa Subhanna, na kama ukituhitaji mbele ya haki basi Mollah wetu tusamahehe kwa kila Mja wako atakaesoma na asiesoma Dua hii, hakika wewe ni mueza wa kila jambo, basi tunakuomba kwa wale walozama kwenye matatizo ya madawa ya kulevya Yaa Rabbi waondoshee mtihani huo waweze kuuwepuka kwa uwezo wako, wenye mataizo ya ulevi, kamari, na majanga mengine yenye madhara ya Akili Yaa Rabbi wewe ndio Mwenye Kuwamiliki hizo Akili zao, basi tunakuomba uwageuzie ili yawaondoke mashaka hayo, wenye dhiki na umasikini waondoshee dhiki zao, na kila mwenye shida yake Yaa Rabbi Mtatulie kwa uwezo wako Mollah wetu, Tunakuomba tuwe waja wako wakaribu kwa mapenzi na Ibada na kutaka kukujua wewe na njia zako Subhanna. Amin.