Sunday, July 26, 2015

PEPO YA DUNIA PART 3

Asalaam Aleiykum,

Jambo la Mwanzo(1) Kuuwa:unaambiwa usiue nafsi iloharamishwa kuuwawa, na huko kuuwa kuko kwa aina nyingi unakwenda jeshini, au unamua mtu kwa makusudi au kwa kutumia sababu za uchawi na mengineyo, basi lazima adhabu ile ya kuikatili nafsi na wewe ikukute, hata kama utaishi maisha yako yatakua ya dhiki kubwa na tafrani mpaka kuondoka kwenye Ulimwengu huu, ndio maana tunapata habari idadi kubwa ya majeshi wanorudi kupigana vita hatimaye wanajiua wenyewe kwa dhiki wanayo iona, kwa hiyo elewa ukimfanyia mwenzio uadui wa kumtoa roho yake na yako itatoka kikatili tena kidogo kidogo.
Jambo la Pili(2)Zinaa. Kuzini nako kuna madhara makubwa na mateso ya Akili(utakhiyari bora upigwe mikwaju)unateseka vyengine wewe hujui kwanini, lakini sababu zake kubwa ni kuzini, unafilisika, dhiki ya maisha, maradhi na mateso ya kila aina, wewe tizama kila ukimaliza kuzini nini kinatokea baada ya siku Arobaini chunguza maisha yako utaona madhara gani yanakufika?japo maradhi basi yatakuja japo kwa njia ya siri, au matatizo nyumbani kwako, wewe fanya uchunguzi usingoje mimi nikuhadithie, mimi nakutajia moto wewe ndio unao kuunguza basi pata hisia ujiepushe nao.
Jambo la Tatu(3)Wizi: Ndio na Rushwa zote katika Dhuluma, wewe chukua pesa au mali za watu, piga mvinyo lakini hutoipata raha katika dunia hii, utakaa na mapesa yako lakini huna furaha, huwezi hata kucheka, dhiki za nafsi zinakushika unaishi kama mnyama, na wasiwasi usokwisha na mali yako wanaitafuna watu wengine, wewe umebeba gunia la dhiki lilojaa madhara, mara wewe unaumwa mara watoto wanaumwa, pesa yote inamalizika kwa waganga. hayo ni machache katika yanohusu Mwili wako.
Sasa tunaingia yenye kuhusu Mdomo, kumbuka haya yote yanakuondoa kwenye Ucha Mungu na lazima ulipwe kwa ulitendalo.
Jambo la Nne(4)Uongo: uongo una madhara makubwa kabisa ukiutumia uongo unaweza kumuangamiza mtu, ukamfanya adhurike, basi ukitenda hilo na wewe kama anavoangamia huyo(Mtu au watu) na wewe jichunguze unapata malipo yale yale ya (Mtenda akitendewa hujihisi kaonewa)na kwambia hivyo kwa sababu huna uwezo wa kuona malipo yanavotokea lakini kama ungekua unajua vipi kutizama (Mtenda na Mtendewa)ungejua nimekusudia nini, yaani wewe mwenye kutenda ujitizame wakati unatenda, halafu wakati huo huo umtizame unayemtendea ndio utajua nimekusudia nini.
Jambo la Tano(5)Kuapiza au Chuki: kuapiza unatumia (Energy) kama atumiayo (Mganga au Mchawi)kumuangamiza Binaadamu mwenzio, kwa hiyo ukifanikiwa kumdhuru jua na wewe mfano wa dhara ile itakufika, japo inachukua muda lakini inakuja.
Jambo la Sita(6)Kuhujumu:Iwe mtu au Uchumi, basi elewa na wewe hujuma zitakurejea kama ulivohujumu, ikiwa umemzulia basi na wewe itakufika dhara ya mfano uleule ulomtendea mwenzio, sawa na kula nyama ya maiti, karaha zake.
Jambo la Saba(7)Kujisifu:Ukisha anza tabia hii kama wewe tajiri au una mali, inabidi lazima uilinde sifa hiyo, sasa madhara yake unakwenda kukopa, unakimbia watu lakini lazima ujioneshe kuwa ni wewe tajiri au una sifa fulani,unajipa dhiki mwenyewe na hiyo inaitwa kujidhuru mwenyewe kwa Mdomo wako(Self harm).
Na tunamalizia fungu la tatu la mwisho nalo ni la Mawazo.
Jambo la (8)Choyo au Wivu: Umeuangalia vipi wivu unavokutafuna, vipi unavotaraji mwenzio labda afilisike, vipi unateseka kwanini kapata yeye, tizama vipi choyo kinavokula unga wa Roho,Umekonda wewe una nini?  kumbe nyumba ya fulani tu inakushughulisha, unakua na hali gani hata wivu wa Mke mwenzio vipi unateseka,unakua mgonjwa, jiulize ikiwa nina wivu kama huu kweli naweza kuwa Mcha Mungu.
Jambo la Tisa(9)Hamaki:itizame inavo kuangamiza siku hizi tumeibadilisha jina tunaita ana (Blood Pressure)ndio kashapata maradhi, ni hamaki kwa kuwa hatujui vipi kuifanyia kazi hamaki ili itutoke, hamaki madhara yake makubwa sana, ina mdhuru mtu na kukudhuru mwenyewe, inakuangamiza inabidi uilinde kama sifa, hata hamaki ikiondoka inabaki kovu ya madhara yake, utasikia hasemi naye kwa kuwa wamegombana, hamaki ishakwisha wewe unaendelea kulienzi kovu lake, kwa sababu hamaki haikai masaa 24 inakwisha, sasa wewe unaendelea kununa miaka miwili huoni kama ni madhara juu yako, unajinyima raha bure pengine kwa jambo la kipuuzi.
Na Jambo la (10) Hamu au Uchu:Tamaa itizame inavokupeleka mbio, vipi unavoteseka iwe ya mtu au kitu, akili yote tafrani, una hangaika, watu wanakuuliza weye una nini pengine una hamu uwe tajiri, au una uchu umpate fulani, basi ndio unakua kama umeajiriwa, akili haipo tena, hamu jamani ina matatizo, mawazo yanakuwa na mawimbi, mashaka makubwa, huna raha kwenye Ulimwengu huu ukiwa una maradhi ya hamu.
Sasa ikiwa katika mambo hayo kumi huna hata moja basi wewe ndiye Mcha Mungu, wewe ndio ushafuzu, wewe ndio katika wale Marafiki wa Mwenye Enzi Mungu, na kama bado basi fanya mazoezi uyawache mambo hayo kumi, na yakiondoka kwenye nafsi yako, basi moja kwa moja (Bliss) Furaha kila saa na dakika na hiyo ndio (Nature) yako, na ndiyo Pepo yako katika Ulimwengu huu. Tunamuomba Mollah wetu atuwezeshe katika hayo.


No comments:

Post a Comment