Sunday, April 27, 2014

FAIDA YA SALA ZA USIKU PART 1

Asalaam Aleiykum

Tuna anza tena darsa zetu kama kawaida baada ya kusita kama jumapili mbili hivi ili tupate kusoma yalotangulia, tutaendelea na kawaida yetu ya darsa mpya Inshaa Allah kila Jumapili ikiwa Mwenyewe mwenye kutupa hekima na afya kwa uweza wake ataturidhia kwa mapenzi yake ambayo yanaendelea kumiminika juu yetu kila siku. Katika Darsa hii ya faida ya Sala za usiku dhumuni langu ni kujulisha kitu fulani ikiwa unaweza kukipata utakua umeshafuzu katika Ulimwengu huu, Nataka kujulisha kwanini hassa ikawa Sala ya usiku, lakini ntafanya hivyo kwa njia nyengine kabisa, ntakupa faida ya ndani yenye umuhimu na uhai wako katika Ulimwengu huu.
Kuna msemo wa kiswahili unasema (Jipendekeze Upendwe), 
Nini Maana ya Kujipendekeza?
Watu wengi wakiulizwa huwa wanajibu kujipendekeza ni mwenendo wa ima kujionesha unapenda au kufanya matendo ya kukupelekea uonekane mtu mzuri ili upate kupendwa, hizo ndio Fahamu za kawaida yetu ya kila siku. Lakini kuna Fahamu nyengine ya Wacha Mungu ambayo inajulikana kama kujipendekeza ni mwenendo wa kukumbusha au kujikumbusha usisahau au usisahaulike kwa mpenzi wako.
Na kwa hili la mapenzi hakuna mpenzi mkubwa aliye karibu na wewe kama Mollah wako, Yeye ndiye ambaye anakukumbuka kila sekunde na dakika katika Uhai wako wote, Hakusahau Mollah wako ukiwa kwenye Maasi au kwenye kutenda Mema daima yupo na wewe ana kukumbuka kiumbe chake. Tunaona mapenzi yetu ya kawaida vipi tunavo sahau, mpende mtu upendavo lakini , ukenda senema umemsahau, ukicheza karata umemsahau, ukenda harusini umemsahau, ukenda mpirani umemsahau na mwisho utashikwa usingizi utalala kwa masaa burdani hukumbuki chochote na ukiamka huombi hata msamaha na mapenzi yanaendelea kama kawaida, sasa baada ya kujulika udhaifu wako huo na kuonekana kama utaachiwa hivi hivi Mwanaadamu utaingia kwenye hasara kubwa, sasa ufanye nini? Endelea part 2

FAIDA YA SALA ZA USIKU PART 2

Asalaam Aleiykum

Na kama ukiachiwa ulale mpaka asubuhi utakua unaendelea  kulala hata ukiwa macho, najua unajiuliza vipi utalala ukiwa macho, Naam hivyo ndio sote tutendavyo, unajiuliza vipi nimeamka halafu bado niwe nimelala, yapo mambo mengi yakuuzungumzia usingizi wako lakini leo mie nataka kulitaja moja kabla ya kuendelea na darsa yetu halafu ndio utajua jee umelala au uko macho.
Wacha nigusie hili moja ili tupate kulijua, kwanza kabisa napenda uelewe kabla ya kutenda maasi yoyote pale unakua Macho, katika kipindi hicho unaweza kutenda jambo la kheri, lakini hudumu sana katika hali hiyo ya kua macho hazifiki hata dakika mbili huyo ushalala, ni muda mchache sana unakua macho wewe fikiri utalijua hilo, au lichunguze utakutana nalo hilo tendo la kuwa macho, Basi unapotaka kutenda maasi lazima uwe umelala huku umesimama vipi inatokea hali hiyo? na kwanini isitokee wakati ukilala si zinakuja ndoto? Na ukiwa macho vilevile ndoto zinakuja tafauti yake huu mchana na ule usiku, vipi inakua.
Unakua umacho saa sita ya mchana pengine umemaliza sala ya (Adhuhuri)upo kwenye baraza ya Msikiti anapita Mtoto wa Kike, Mtoto ndio Mtoto kama mnavovijua vivazi vyao unapiga Jicho hujui kama kavaa (Skati)au hakuvaa, ila ninachokijua mimi mtoto huyo anakuletea usingizi Wallahi umacho unalala huku unakoroma tena unageuka Fundi cherehani na ndoto zinafatia, utaitia zipu hiyo (Sketi)utamtilia vifungo, itakuingia mpaka khofu duh kama itamvuka itakuaje, unawapangia mpaka watu wataona nini, basi hapo unashughulika na ndoto zako mpaka unakuja kuamshwa na Muazzin wa Alasiri (Salaa Salaa)unaingia tena Msikitini na bado unaendelea na ndoto eti lakini ile (Sketi)chini haijapindwa huku unatia Udhu. 
Huo ndio usingizi niloukusudia, na ziko ndoto nyingi tena kila sehemu mwengine kutwa anafunga hesabu, unawadhuru walokukera, Nini kilitokea jana usiku, Fulani ana mpya gani leo, mambo millioni, likimalizika hili linakuja lile almuradi ndoto hazishi kichwani mwako, Na ikiwa wewe huna ndoto yoyote kichwani mwako basi wewe ushafuzu na upo katika kundi jengine kabisa, lakini ikiwa bado usiku unapata ndoto na mchana vile vile unaendelea kuota inabidi nikupe zawadi pengine ukiweza kuidumisha inaweza ndoto zikatoweka au kupungua na ukapata nafasi ya kuamka na kumpwekesha Mollah wako.
Mimi sikupi kitu kipya au ukaona nimevumbua jambo, nifanyacho mimi ni kukupa ufafanuzi wa tafsiri halisi  na wewe una hiyari kufata au kutokufata, kukubali au kukataa ni haki yako.
Ili kuifungua zawadi hii Endelea part 3

FAIDA YA SALA ZA USIKU PART 3

Asalaam Aleiykum

Sura ya Muzammil aya ya Mwanzo kuna baadhi ya watu wanashikilia kuwa kakusudiwa Mtume pekee, sio hivyo Quraan imekuja kwa ajili ya Viumbe na mafundisho yote yanatuhusu na sisi.
"ـٰٓأَيُّہَا ٱلۡمُزَّمِّلُ""Ewe Uliyejifunika maguo"
Hapa imekua uzuri hakutajwa mtu kwa jina ingekua aya hii imefungika kabisa, na kama imewachwa wazi basi sote tunaingia kwa kuwa tuna tabia ya kujifunika maguo tunapolala, kama hujapata shuka japo kanga na hata kama kuna joto, sasa unaambiwa
قُمِ ٱلَّيۡلَ إِلَّا قَلِيلاً۬""Simama usiku (Kucha kufanya Ibada)ila muda mdogo(Tu ndio Ulale)
Kwanini ikawa hivyo, kwanza kabisa kuambiwa usimame usiku ni tendo la kuifanyia (Shock your system)wewe umezoea kulala, ukianza kusimama ina maana unabadilisha Tabia, na usingizi ni Tabia,(Hapa nataka uwe makini na utambue kuwa nazungumzia kiwiliwili) umeonekana kama ukiachiwa utaendelea kulala zaidi, ukiachiwa hivyo hivyo utaendelea kusahau lazima upewe nyezo ya kukuwezesha kubadilika, sasa ufanye nini acha kulala amka usiku usimamishe Sala, Sababu mchana kutwa umo katika tabia ya kusahau, sasa unaamrishwa (Disturb the System)na kama utaweza kwa muda mrefu, fanya hivyo usiku mzima, ukiendelea na Ibada hii unaizuilia (Mind)kulimbikiza ndoto na matatizo yote ya mchana kutwa, unainyima fursa ya ku (Deposit)matatizo na magonvi fikra na mbinu za kila aina kwenye (Memory)yako.
"نِّصۡفَهُ ۥۤ أَوِ ٱنقُصۡ مِنۡهُ قَلِيلاً""Nusu yake au ipunguze kidogo"
Hapa unapewa(Choice)kama huwezi fanya nusu au ipunguze kidogo, kuwa na taratibu hii isikutoke kama huwezi yote fanya nusu, huwezi nusu umeambiwa fanya japo kidogo, amua mwenyewe hicho kiasi cha udogo wenyewe.
"أَوۡ زِدۡ عَلَيۡهِ وَرَتِّلِ ٱلۡقُرۡءَانَ تَرۡتِيلاً ""Au izidishe na soma Quraan kwa (Ufasaha)ilivyo".
Ukiweza zidisha ndio uzuri zaidi, halafu isome Quraan kwa ufasaha na umakini mkubwa kwa nyakati hizi za usiku iwe unafanya vilivyo vipi, yaani wakati unasoma na uwe wakati huo huo unaisikia, kitu kizuri sana kitakutokezea ikiwa utaweza kusoma na huku unasikia kile unacho soma, utafikia kwenye sehemu ambayo (peace)inakushukia na kitu kizuri kabisa kinateremka katika kifua chako naita hiyo (Secret Energy).
"إِنَّا سَنُلۡقِى عَلَيۡكَ قَوۡلاً۬ ثَقِيلاً ""Hakika sisi tutakuteremshia kauli nzito"
Bwana Mtume s.a.w kateremshiwa Quraan, ndio hii watu wengine waloipinga wakakataa kuiamini, maneno mazito sana kifua cha mwanaadamu hakiwezi kuchukua ndio unaona mpaka leo hata mimi na wewe kuna mengine yanatuumbisha kwa uzito wake. Sasa na wewe ukidumu katika Ibada hii nini kitakuremkia, hakuna chengine isipokua hiyo hekima, na wewe ushauri wako, muongozo wako utakua mzito kila mtu atataka kukufata ili aupate, kauli zako zitakua si za ulimwengu huu bali zinatokea kwa mwenyewe Muumba Mbingu na Ardhi.
" إِنَّ نَاشِئَةَ ٱلَّيۡلِ هِىَ أَشَدُّ وَطۡـًٔ۬ا وَأَقۡوَمُ قِيلاً ""Hakika kuamka usiku(Na kufanya Ibada)Kunawafikiana zaidi na Moyo, Na maneno (yake)Yanatua zaidi"
Hapo ndio inapotajwa faida kubwa ya kunyanyuka kwako usiku, unaelezwa kuwa ukinyanyuka usiku ukadumu katika Ibada hii unapata kitu kinachoitwa (Awakening) Nini hii (Awakening)?Mwanaadamu una aina mbili unazopita katika uhai wako moja ni ya kulala ambayo ni usiku, na ya pili ni ya kuamka ambayo ni mchana, lakini kwa wakati huu wewe unaishi katika moja tu ambayo ni ya kulala usiku na mchana, hii ya kuamka huijui kabisa, mpaka uambiwe, na mimi leo nachukua hii dhamana ya kukwambia kuwa ukiwa macho unakua huzioni ndoto zako, sio kua hazipo bali unapuuza kuziangalia  vipi?
Tatizo kubwa la Mwanaadamu unatumia uhai wako wote katika kulala, Wanasayansi wanasema unatumia nusu ya Umuri wako katika usingizi, Wacha Mungu wao wanajua unatumia Asilimia 90 ya Uhai wako ukiwa Umelala, Inakuaje hali hii?
Endelea part 4

FAIDA YA SALA ZA USIKU PART 4

Asalaam Aleiykum

Najua utasema huyu anasema nini hali yakua mimi niko macho, Nakwambia wewe huko macho, ila hayo macho yako wazi wewe mwenyewe unaendelea na ndoto unazipanga hizi za mchana na hizi za usiku na zote ukitaka unaweza kuziona, lakini za usiku unaziona uzuri sababu umetulia. Na mchana unaendelea kuona ndoto zako, mara umejenga nyumba, pengine unaota mpaka ushatajirika au uko (Beach una Enjoy)au unamuota mwanamke au mwanamme huku umetulia na ukishtuka duh kumbe hizi ndoto unakurupuka usingizini na kuona huu ni ujinga, unajibabaisha kidogo ikisha huyoo unaendelea na ndoto nyengine na hiyo ndio hali ya kila saa na dakika zetu tulizojaaliwa.
Na usiku ni hivyo hivyo ila umekua hodari wa lugha usiku unaziita ndoto na mchana unaita fikira ni kitu kimoja kama utakichunguza kwa makini, Lakini kutokana na uweza wako wa kushuhudia hayo yote ya usiku na mchana lazima ipatikane hali nyengine ambayo inaitwa (Awakening State) Hali hiyo ndio inayopatikana kutokana na hizo Ibada za usiku.
Nini(Awakening)? Ni hali ya kuwa macho wakati wote na watu hao wametajwa katika sura ya (Al-Imran aya ya 191)"(Ambao humkumbuka Mollah wao wakiwa wima wamesimama, na wakikaa na hata wakilala)"Hali hiyo inatokea kwenye (Mind)ndio ukaambiwa hali hiyo inawafikiana sana na Moyo, kwa hiyo kwenye (Mind)Akili inatokezea (Awakening)Muamko na kwenye Moyo ndio inatokezea hiyo (Laylatul Qadir) kwa hiyo maana ya kuwafikiana sasa unakua tayari ushafanya mataarisho ya kujiandaa na hiyo (Laylatul Qadir) Akili ushaiweza sasa huna nafasi tena ya kutenda dhanmbi, kwani sasa uko macho, na Shetani hapati nafasi ya kukushawishi na kukulaza.
Sababu kubwa Shetani anayoweza kukufitini na Mollah wako shuruti lake lazima uwe umesahau au umelala, ndio anakuletea firimbi na wewe unatoka kama nyoka wa kihindi kwenye kikapu, hapo unavamia chochote, unaletewa nyimbo, au ngoma au senema au watu wanatembea uchi, anakupa mambo chungu nzima ili upate kukoroma, na ukikoroma umekwisha, unatenda kila maasi, lakini ukiwa macho mwizi hawezi kuja kukuibia mema yako, na afanyacho Shetani hataki jambo moja tu la wewe kuwa karibu na Mollah wako, ndio maana utaona ukisali siku mbili ushachoka au unasubiri mpaka Ramadhani ije.
Unaendelea kuambiwa Nyakati hizi za usiku "Maneno yake yanatulia kwenye moyo"yanateremka vizuri, unajua kwa sababu gani (Ndio maana unaambiwa ulale kidogo)sababu ukiamka unakua (Empty Mind) kwa muda ule hakuna mawazo, umeamka ghafla ndoto zimesita, na mfano mzuri hivi sasa pengine umekuja na tafsiri za (Sheikh)wako huwezi kukubaliana na mimi mpaka uje bila ya Tafsiri, au utakua unasoma maneno yangu lakini anatafsiri (Sheikh) wako kichwani(Amka)hata niseme nini huwezi kukubaliana na mimi moyo wako hauafikiani na maneno yangu mpaka uipate hiyo (Awakening) kwa hiyo ukija na (Mind iko full) unakua umo hasarani.Aya inayofatia inasemaje kuhusiana na kuja kwako na mizigo kichwani. "إِنَّ لَكَ فِى ٱلنَّہَارِ سَبۡحً۬ا طَوِيلاً۬ "Hakika mchana una shughuli nyingi"
Vipi utapata Muamko(Awakening)kwenye jiji kama la Daressalaam haiwezekani kabisa au uwe umedumu kwenye Ibada hizi za usiku kwa muda mrefu, kwa sababu shughuli zake nyingi, kelele ndio usiseme, nyimbo ndani ya vilabu vya pombe mpaka asubuhi, biashara honi za magari, kelele za binaadamu zinakuzuilia kupata (Awakening)Muamko kabisa, akili haiwezi kutulia.
Namalizia darsa ya leo kwa hii aya ya 8 sura ya Muzammil
"وَٱذۡكُرِ ٱسۡمَ رَبِّكَ وَتَبَتَّلۡ إِلَيۡهِ تَبۡتِيلاً۬ "
Na litaje jina la Mollah wako na ujitupe kwake kwa kweli(Mapenzi)
kwanini ikawa ulitaje jina la Mollah wako, kwa sababu unaweza kushikwa na usingizi ukalala tena kwa kuwa umekaa macho na huna la kufanya, (Kwani hujawahi kumuona mtu kalala chini ya Speaker na Muziki unaendelea na yeye anakoroma)sasa na wewe unaogopewa ndio unaambiwa litaje jina la Mollah na ujitupe kwake kwa mapenzi ya kutaka kumjua, mapenzi ya kutaka uwe karibu naye, na katika hayo majina kuna siri kubwa.
Na ukimtaja kwa ukweli mara nyingi unakua muda wote unamkumbuka na ukimkumbuka sana unakua katika waja waliyo karibu yake, Na waja wote walo karibu na Mwenye enzi Mungu wanaipata Nuru yake, Na nuru ya Mwenye Enzi Mungu ikikuwakia ukaanza kungara watu wataanza kukupenda na kukuogopa, sio kukuogopa na kukuchukia, huo uadui, hayo maradhi, lakini kuogopewa na kupendwa mfano vile wa watoto wako wanakuogopa na kukupenda, na kama sisi tunavyo muogopa Mollah wetu na kumpenda, hiyo ndio kheri, hiyo ndio neema itokayo kwa Mollah wako, na huko ni kufanikiwa kukubwa katika upeo wa kibinaadamu, ama kwa upeo wa upande wa Mollah wako utaujua mwenyewe utakapoipata hiyo (Awakening)vipi anavokufungulia zawadi zake zisizokua na Mwisho kwa ajili ya kisimamo chako cha usiku.
Nakuomba Mollah wetu tuwezeshe kuifanya na kudumu katika Ibada hii ya Usiku ili utupe fadhila zake na Rehma zako. Amin

Sunday, April 6, 2014

NGAZI SABA ZA ROHO PART 1(NGAZI 7)

Asalaam Aleiykum

Leo tumefikia kilele cha hitimisho la Darsa zetu za Ngazi saba za Roho, Hii leo tupo kileleni mwa hiyo Ngazi, sote tukiwa hatujui nini kitatokea? Mimi msimulizi na wewe msimuliwa darsa hii hatujui kwenye ngazi hii kuna nini, Tunachokifahamu Watu wengi wanaipanda ngazi hii wakati wa Mauti yao, Wachache sana wanofika wakapanda wakiwa hai. Na yule afikae akirudi anakua hana lugha ya kuhadithia mambo yaliyopo kwenye ngazi hii ya Saba.
Wanofanikiwa kuhadithia ni wachache  mno,Na sisi ndio tunapata kutoka kwa hao wachache habari za ngazi ya saba jinsi ilivyo, Unaweza Mwanaadamu ukajikaza ukazipanda mpaka ngazi ya sita lakini ngazi ya saba huna cha kufanya huwezi kupanda kwa uwezo wako, mpaka upewe mualiko, au labda utaraji maneno yaliyomo kwenye aya hii Sura ya Fussilat (35)
وَمَا يُلَقَّٮٰهَآ إِلَّا ٱلَّذِينَ صَبَرُواْ وَمَا يُلَقَّٮٰهَآ إِلَّا ذُو حَظٍّ عَظِيمٍ۬
"Lakini hawatapewa (Jambo hili) ila wale wanosubiri, wala hawatopewa ila wale wenye hadhi kubwa.(Mbele ya Mwenye enzi Mungu).
Wale wanosubiri kwa kufanya Ibada bila ya kuyumba, Na wale Wacha Mungu walojitupa kwa Mollah wao hao ndio watoifikia Ngazi hii(Soma Uzuri kuanzia aya ya 30 mpaka 35)ndio utajua kusudio la ngazi ya saba. Katika ngazi hii kinachotokea  ni kitu cha ajabu kabisa ikiwa utalifahamu tafsiri ya neno hili (Dis-Appear)maana yake unatoweka halafu unarejea, lakini marejeo yako ya pili sio ya kawaida, hurejei yule yule wa mwanzo, (Wenzetu Wakiristo wameita marejeo haya (Born Again) sio hivyo, uhakika ni kuwa umetoweka ikisha ukarejea, lakini marejeo haya unapata ladha ile ile kama utakumbuka ya utotoni (Innocent) kila kitu kwako ni (Bliss)kwa hiyo huwezi kuita kuzaliwa tena kwa sababu kuzaliwa (Complete) hujui lakini sasa hivi unajua lakini si kwa kutumia (Brain) ila kwa kutumia Roho yako.
Endelea part 2

NGAZI SABA ZA ROHO PART 2 (NGAZI 7)

Asalaam Aleiykum,

Kwa hiyo huwezi kuita umezaliwa tena, alozaliwa tena anakua yule yule, ndio maana Shetani (devil) rahisi kumuingia tena, ana uwezo wa kumtawala, lakini ukitoweka na kurejea unakuja na mambo mapya huku ukiwa unazijua mbinu za kale za shetani. Na hivyo ndivyo inavotokea kwa Wacha Mungu wengi walofanikiwa kupanda na kuchungulia katika ngazi hii, waliporejea  ndio baadhi yao wakahadithia  waloyaona huko mfano kama Bibi Rabbiya bin Adwiyya, Jalaludin Rumi, Mansour Bin Khalaj, kina Ibn Arabi na wengi wengineo, Na kila mmoja kahadithia kwa njia yake ili na wewe uweze kupata hamu na shauku ya kupanda ngazi hii ya saba.
Nini Walichokutana nacho?
Jambo la Mwanzo wanakutana na Nuru ya Mwenye Enzi Mungu, hivi ndivo Wacha Mungu wote wasemavyo kiwatokeacho katika ngazi hii, sio kuwa wamekutana na Mwenye enzi Mungu kwani jambo hilo haliwezekani, na wala halitotokea, unaweza kuhisi lakini sio kumjua au kumuona(Never)kwani Mollah wako (Si kitu kinachoweza kujulikana. Kwa hiyo Roho inachopata kuona ni hiyo Nuru.
ٱللَّهُ نُورُ ٱلسَّمَـٰوَٲتِ وَٱلۡأَرۡضِ‌ۚ مَثَلُ نُورِهِۦ كَمِشۡكَوٰةٍ۬ فِيہَا مِصۡبَاحٌ‌ۖ ٱلۡمِصۡبَاحُ فِى زُجَاجَةٍ‌ۖ ٱلزُّجَاجَةُ كَأَنَّہَا كَوۡكَبٌ۬ دُرِّىٌّ۬ يُوقَدُ مِن شَجَرَةٍ۬ مُّبَـٰرَڪَةٍ۬ زَيۡتُونَةٍ۬ لَّا شَرۡقِيَّةٍ۬ وَلَا غَرۡبِيَّةٍ۬ يَكَادُ زَيۡتُہَا يُضِىٓءُ وَلَوۡ لَمۡ تَمۡسَسۡهُ نَارٌ۬‌ۚ نُّورٌ عَلَىٰ نُورٍ۬‌ۗ يَہۡدِى ٱللَّهُ لِنُورِهِۦ مَن يَشَآءُ‌ۚ وَيَضۡرِبُ ٱللَّهُ ٱلۡأَمۡثَـٰلَ لِلنَّاسِ‌ۗ وَٱللَّهُ بِكُلِّ شَىۡءٍ عَلِيم 
Mwenye Enzi Mungu ni Nuru ya Mbingu na Ardhi, Mfano wa Nuru yake, ni kama Shubaka ndani yake Taa, (Imo)katika Tungi(Kama Chemni)tungi (hilo ni)kama nyota ingarayo, inayowashwa(Taa hiyo kwa mafuta yatokeayo)katika mti ulobarikiwa wa mzeituni, usio wa (Upande)wa Mashariki wala wa Magharibi, Yanakaribia mafuta yake kungaa (wenyewe)ingawa moto haujayagusa, Nuru juu ya Nuru Mwenye Enzi Mungu humuongoza katika Nuru yake amtakaye, Na Mwenye enzi Mungu hupiga mifano kwa watu, Na Mwenye enzi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.
Mambo mengi yanataka kuzungumzwa katika aya hii lakini leo si siku yake, Inshaa Allah siku za usoni penye uhai tutaizungumza aya hii kwa undani zaidi ila leo ni kuonesha nini hicho wanachokutana nacho wale wanofikia ngazi hii ya saba, hicho ndio wanachokikuta cha mwanzo kabla ya kitu chochote kile.
Na mwanzo kabisa Nuru hii inavokumurika unaingiwa na khofu kubwa kabisa mpaka unapoteza fahamu, unaweza kushikwa na homa hata kuishinda ya (Malaria), Na inaweza kuchukua tukio hili ukawamo katika hali hiyo kwa masiku au siku kutokana na kupanda kwako katika ngazi hii. Hofu ikimalizika ukakaa sawa ndio kidogo kidogo unarejea katika hali ya kawaida lakini sasa ukiwa Mtu mwengine kabisa, Na hivyo ndivyo inavotokezea kadhia hii katika ngazi hii ya Saba kwa kila apandae, Na kizuri zaidi kinachotokezea ukiteremka lazima upewe zawadi kama vile (Mfano) wa Imam Ghazzali aliposhuka kutoka ngazi ya Saba akatuletea zawadi ya kitabu chake maarufu (Uhiyya Ullumu Diin) basi na wewe fanya jitihada upande ili upate kutuletea zawadi yako.
Endelea part 3 

NGAZI SABA ZA ROHO PART 3 (NGAZI 7)

Asalaam Aleiykum,

Sasa na wewe pia unaweza kuipata hiyo Nuru hapa hapa chini lakini iliyo (Hafifu) ikiwa utafanya Ibadah kwa muda wa miezi mitatu mfululizo na bila ya kufanya makosa makubwa, utaanza kutoa Nuru fulani ambayo watakua wanahisi lakini hawajui kitu gani, mtu akikaa na wewe tu atakua anasikia furaha kwa ajili ya hiyo (Energy)inayotoka katika mwili wako.
Naam katika ngazi hii baada ya hiyo Nuru ndipo unakuja kuona vipi Dunia mbili zinavokutana ile Dunia ya (Spirit)na Dunia ya (Matter), Nuru hiyo inakusaidia kuona mambo yalivyo kwa uwazi kabisa, kwa mara ya mwanzo unajua alaa kumbe haya ndio yalosemwa kwenye aya ya mwanzo sura ya (Nisaa)mpaka mwisho wa aya.
يَـٰٓأَيُّہَا ٱلنَّاسُ ٱتَّقُواْ رَبَّكُمُ ٱلَّذِى خَلَقَكُم مِّن نَّفۡسٍ۬ وَٲحِدَةٍ۬ وَخَلَقَ مِنۡہَا زَوۡجَهَا وَبَثَّ مِنۡہُمَا رِجَالاً۬ كَثِيرً۬ا وَنِسَآءً۬‌ۚ 
Enyi Watu Mcheni Mwenye Enzi Mungu  wenu ambaye amekuumbeni katika Nafsi moja, akamuumba mkewe katika nafsi ile ile na akaeneza wanaume wengi na wanawake(Mpaka mwisho wa aya).
Unapata kuona kumbe kilichomo kwenye Nafsi yangu ndio hicho hicho kilichomo kwa Mke wangu, au wanangu au majirani au hata mpita njia, hapa ndio unagundua lile Daraja la mmoja kwa wengi na wengi kurejea kuwa mmoja (Nafsi Wahida), na ukiyajua hayo kama wewe Shujaa wa kweli unachupa, na huko uchupapo hakuna (Gurantee)unaweza kurudi Akili imeharibika, unaweza kurudi ukakaa kimya mpaka kufa kwako.
Kumbuka Nasema ukirejea kutoka Ngazi ya saba unakua mtu mwengine kabisa kutokana na mabadiliko ya matendo yako, kama tuonavo mfano huu ulomtokea "Ibn Arabi" siku moja alikuja maskini kuomba ikawa Ibn Arabi hana cha kumpa basi akatoa Nyumba yake,(Unajua kwanini?)(kwa sababu ukipanda huko unatambua kuwa haya mambo yote ya Ulimwengu ni Temproray, hayadumu kwa hiyo unakua huna shughuli nayo) Sasa wewe huko tayari hata kutoa chakula hivyo kweli utafika ngazi ya Saba. Alisimama siku moja Ibn Arabi msikitini  akanadi kwa kupiga makelele na  kuwaambia waliyomo msikitini enyi mliyomo ndani "Mollah mnaye muabudu yupo chini ya miguu yangu"wakatoka watu ndani wakampiga vibaya sana kwa hasira, lakini kwa kuwa wanajua Ibn Arabi katokea ngazi ya Saba wakaona bora wachunguze kwanini kasema vile na yeye ni mtu wa Mungu, na hivi ndivyo walivyo wanasiasa misikitini na wafanya biashara wanasubiri tu wapate (Chance) ya kufanya (Bussiness) au kudhulumu watu haki zao, "kweli walipochimba ile sehemu wakakuta Dhahabu nyingi"wakagundua nini alikua anakusudia Ibn Arabi.
Na hivyo ndivyo tufanyavyo Misikitini mtu anaomba mpaka mechi ya mpira timu ishinde, au uchaguzi wa diwani eti ashinde yeye, tumegeuza misikiti sehemu ya biashara na siasa hakuna ibadah tena, na naogopa kama kuna mtu atakua anarekodi mawazo yetu wengi tutakua hatuna (Stara)wakati wa Sijjida zetu, itakua aibu tupu.
Naam: (Ahmad Ibn Hanbal) Anahadithia hadith ya Bwana Mtume s.a.w "Kasema"Hakika Mwenye enzi Mungu Kaumba Ulimwengu kwa kutumia Kiza,(Na sasa Inajulika kama Dark Matter)Ikisha akaumurika kwa Nuru yake, Na yoyote yule Mwenye kumurikwa na Nuru hiyo basi atapata baraka za kuongozwa kwenye njia iliyonyooka, Na yoyote yule ambaye Nuru hii haitompata basi huyo ndio alopotea".
Basi namie nakuomba panda ngazi hizi saba ili upate kufanikiwa na uzipate hizo Baraka za Mollah wako.
Mimi sitoendelea sana kuhadithia mambo ya ngazi ya saba,kuna mengi mno mpaka ya kuonana na Majini na Malaika lakini nafata wasia wa Bwana Mtume s.a.w katika hadith ilo hadithiwa na (Bukhari)"Kasema Bwana Mtume s.a.w" "Usizungumze sana mwishoe utasema uongo"Yafanye mawaidha yako mafupi"ili uwafanyie watu wepesi na sio uwatie dhiki""Na wape habari njema""Na wala usiwape vitisho vya Adhabu".
Na mimi nakutakieni kheri na kufahamu niliyoyaandika.Mollah atupe Fahamu ya kuyajua mambo mengi yaliyomo kwenye Ufalme wake. Ikisha aturuzuku msamaha kwa Radhi zake. Amin