Sunday, October 18, 2015

NJIA YA KUHIFADHI SALA PART 1

Asalaam Aleiykum

Nimeona kuna sababu ya kuleta darsa hii baada ya kushuhudia hasara inayopatikana juu yetu katika kusali halafu ikawa huipati sala yenyewe, Na inachangia pia Mtu kutokujua maana nzima ya hiyo Sala.
Sasa wacha tuanze kwa kujua japo kwa ufupi  Nini Sala?, Sala ni(Maombi)ya Mapenzi ya Utiifu yanotokea Rohoni, Ni kwa ajili ya Shukurani ya kujua umeumbwa na mpaka wakati huo unasimamisha sala unathibitisha kwa yakini kuwa upo uwezo wa hali ya juu ambao hauna shaka ulokufanya  na kukupa wewe na vyengine nafasi ya kuufahamu na Kuabudu, Na sasa kwa unyenyekevu wewe binafsi umesimama kutokana na Uwezo huo usio ufahamu unasema "Allah Akbar", Wewe unakiri na kutaraji alokupa neema hizo zote azidi kukupa radhi zake za kuweza kukufunulia, kukufungulia zaidi milango ya fahamu na kwa mapenzi yake akupe uwezo wa kujua yalio zaidi katika ufalme wake.
Utaona nimetaja kufahamu na kutokufahamu kwa sababu kila ukenda (Deep)kwenye Sala yako mambo mepya yanafunguka, hisia tafauti zinaongezeke.
Hiyo ndio Sala ambayo unatanguliza shukurani kwa baraka na uwezo ulopewa wa kuweza kumfahamu yeye Mollah wako na kumtii, Sasa kwanini lazima uifanyie hifadhi sala yako, kabla ya kwenda mbele itabidi ujue tafauti ya (Kuhifadhi na Kulinda).
Kulinda ni tendo la nje lenye kuhakikisha hupati dhara, huibiwi, kwa ufupi ni tendo la nje, Lakini kuhifadhi maana yake ni kutunza,kua Muangalifu hicho kitu au jambo haliharibiki, kwenye kulinda unakua mtazamaji na kwenye kuhifadhi unakua muangaliji, kwa hiyo hifadhi ina mahusiano na tendo la ndani.
Ndio maana aya ikasema(Quraa-Baqarah-238)
"حَـٰفِظُواْ عَلَى ٱلصَّلَوَٲتِ وَٱلصَّلَوٰةِ ٱلۡوُسۡطَىٰ وَقُومُواْ لِلَّهِ قَـٰنِتِينَ "
Angalieni sana Sala(Zenu)na khasa ile sala ya kati na kati, Na simameni kwa unyenyekevu katika kumuabudu Mwenye enzi Mungu.
Kwanini ikawa Hifadhi na sio Linda? kwa sababu siku hizi umezuka mtindo unaambiwa linda, na mimi napiga kelele ili usiharibikiwe nakwambia hifadhi, unatakiwa Mja ukiipeleka sala yako kwa Mollah wako uwe mnyenyekevu na mapenzi ya hali ya juu, na hilo silioni kwa Waumin wengi, Sala zimeondoka nyoyoni mwetu na kilichobaki na kupatikana ni Sala ya njia ya nje kwenye taratibu za (Viungo), ndio maana unaona akimaliza Sala anatukana, akimaliza sala anafanya mzaha, akimaliza sala anakwenda kuiba, akimaliza sala anafanya zinaa, akimaliza sala anasema uongo, sasa hapo sala ipo wapi? vipi yanaweza kuwa maneno ya Mwenye enzi Mungu hayakamatani na matendo yako, inasema Quraan sura ya (Ankabut aya ya 45)
"ٱتۡلُ مَآ أُوحِىَ إِلَيۡكَ مِنَ ٱلۡكِتَـٰبِ وَأَقِمِ ٱلصَّلَوٰةَ‌ۖ إِنَّ ٱلصَّلَوٰةَ تَنۡهَىٰ عَنِ ٱلۡفَحۡشَآءِ وَٱلۡمُنكَرِ‌ۗ وَلَذِكۡرُ ٱللَّهِ أَڪۡبَرُ‌ۗ وَٱللَّهُ يَعۡلَمُ مَا تَصۡنَعُونَ "
Soma uliyoletewa Wahyi(Uliyofunuliwa)katika kitabu, na usimamishe sala, bila shaka Sala(Ikisaliwa itakiwavyo)humzuiliya (Mtu)mambo machafu na maovu, na kwa yakini Kumkumbuka Mwenye enzi Mungu(Ndani ya hiyo Sala ni jambo)kubwa kabisa, Na Mwenye enzi Mungu anayajua mnayoyatenda.
Aya imeweka wazi hapo mwanzo yasome yale yaloletwa kwenye kitabu, nenda (Deep) kwenye hiyo aya ulochagua kuisoma wakati unasimamisha Sala,(pengine ndani ya hiyo aya utapata maana itakayofungua jambo kwenye Akili yako)lakini wapi unasoma kama kasuku, hutulii ukachambua hicho ukisomacho, unasoma aya kama mazoea huku akili inapanga mambo mengine kabisa, ifanye Sala yako(Iwe mfano kama unavocheka, jiulize wakati unacheka kuna wazo lolote linaingia hakuna, na ukenda (Deep)kwenye kucheka utaona lazima yatoke machozi, kwa hiyo jua furaha na msiba viko pamoja na hivyo hivyo elewa kwenda (deep) kwenye Sala na kuepushwa na Maasi pia viko pamoja ila tafauti yako hujenda (Deep).
Endelea part 2


NJIA YA KUHIFADHI SALA PART 2

Asalaam Aleiykum

Unapata Darsa kama hii ili uzinduke, isifike siku ya maulizo ukashangaa unapewa Daftari lako unalikuta jeupeee, wakati mwenyewe unajijua kipindi hakikupiti. Sasa kama unataka kuijua hiyo sala basi wacha nikwambie Sala ni lile tendo zima lenye kukutanisha wewe na Mollah wako, kwa ajili hiyo haiwezekani mkutano huo ukawa kama vile unavyokutana na rafiki yako(Saboso).
Lazima uwe katika katika hali nyengine yenye matumaini na ilojaa mapenzi, usifanye jambo la Sala kwa njia ya dharau, na vilevile tambua ukiipeleka Sala yako kama ilivosemwa kwenye aya ilotangulia, ikawa ina nidhamu kamili iliyokamilika, basi kuna mambo yanapatikana kama hilo la kuepushwa na Maasi na Machafu, kupata zawadi ya kusamehewa kutoka kwa Mollah wako, Kupata zawadi za Baraka na furaha, Na utaanza kupata ishara za kuipata Sala kwa kuanza kuacha baadhi ya mambo kama, kuimba Taraab, kuangalia TV, baraza za kipuuzi, utaacha mambo mengi, na huko kuacha usije uka (Force)utapata maradhi, kwa sababu huko kuacha kuna njia mbili wacha nizitaje.
Njia ya kwanza ni ile ya (Force)kuacha jambo bado unalitaka, ndio maana utaona watu wengi wanaadhirika, Mfano unatangaza sasa hulewi tena, watoto wakikutania tu kwa ghafla unataka (beer)unaruka ile Bardii, yaani iwe (cold) Unasahau kama umeacha, au umekua Kizee mambo huyawezi. Halafu kuna huku kuwacha kwa aina ya pili nako ni (Natural) umekwenda (Deep) na mara (Prayer's happen to you) ita utakavyo umeombewa dua, siku hizi (Khamsa Salawati)la Muhimu ukenda (Deep)kwenye Sala unakua umefika kwenye (Source).
Kwa hiyo ukirudi kwenye jukwaa la Ulimwengu unakua Mtu mpya, mambo ya zamani yanaondoka, Lakini ukiacha kwa njia ya force mambo bado yanabakia kwenye Akili(Mind), lakini ukiwacha kwa njia ya (Natural)hakuna kinachobakia. Sasa ufanye nini kuitunza Sala yako?, Kuna mambo mengi yenye kukuzuia kwenda (Deep) kwenye sala yako. Sina haja ya kuvitaja vitu vyote hivyo lakini nitakwambia kwa ufupi ili uanze kuchukua tahadhari na kuweza kuitunza Sala yako.
Itabidi uanze mataarisho angalau dakika kumi kabla ya kuanza sala yako, lakini siku hizi tunaweza kufundisha vipi kujiandaa huku nje lakini mambo yanatokea Msikitini sekunde chache kabla ya kuanza Sala yenyewe, "Anasimama" Imam wetu wa leo na kuamrisha wekeni safu sawa na kuhakikisha hamuachi nafasi "Ibilis" kupita, basi muda huo huo akimaliza maneno hayo vitizame visa vinavyotokezea kwa Maamuma huku nyuma.
endelea part 3

NJIA YA KUHIFADHI SALA PART 3

Asalaam Aleiykum

Sala nzima inageuka (Break Dance) utaona Mtu anahangaika lazima vidole vyako na vyake vigusane, akikukosa vidole analifata goti, akikosa goti anayumba kwenye Bega lazima akuguse, nyote wawili mnakua hamna sala ila mnakazi ya kukimbiana na "Ibilis" kakaa nyuma hana haja hata ya kupita anakuchekeni kwa mambo ya kipuuzi.
Sasa nini umeamrishwa ufanye ukiingia ndani ya hiyo Sala(Kumbuka mwanzo imetajwa uhifadhi) Na sasa aya iliyomo kwenye sura ya (Muuminoon aya 2)inasema
"ٱلَّذِينَ هُمۡ فِى صَلَاتِہِمۡ خَـٰشِعُونَ"
Ambao katika Sala zao huwa ni wanyenyekevu.
Unyenyekevu ulotajwa hapo ni ule wa mazingira ya sala yako, inatakiwa katika muda wote wakati umo katika hiyo Sala matendo yako yote yadumu ndani katika hiyo Sala, Bila ya kuwachia wazo lolote kuingia na kukutoa katika hali hiyo ya Sala yako, Ukiwa kwenye Kisimamo, kwenye Rukuu au Sijda uwe unamkumbuka Mollah wako kwa Tasbih zote.
Kwanini ujizoeshe hali hiyo kwa sababu ukichunguza utaona kila kitu kinakuja wakati wa kuanza sala,kwa sababu wakati ule unapata utulivu,na huo ndio wenye kutakiwa ukikurubia kwa Mollah wako, sasa cha kufanya kwanza ni kuizoesha hiyo (mind) au Akili izoee hali ya kumsabahi Mollah wako, usivunjike moyo mwanzoni itashindikana, huwezi kuishinda akili mara moja, na wala usibishane nayo kwa sababu ukifanya hivyo kushindana na Akili ndio utakaribisha magazeti kwenye Sala yako, vyama vya siasa vitakuja hapo, lakini ukifanya kwa taratibu zake za kuizoesha Akili Tasbih za kumkumbuka na kumtaja Mollah wako utaanza kuona kichwani hakuji tena mambo machafu, hukumbuki biashara wala madeni, hapo tena utakuwa tayari kuleta unyenyekevu na utulivu ndani ya Sala yako, Utaona Mwenyewe Kisimamo chako kimeanza kuwa kirefu, Rukuu zako na Sijda zako zinakua ndefu zenye utulivu, Na ukiipata hali hiyo ndio unakua ushaanza kwenda (Deep) na ukenda (Deep) kuna mambo mengi yanatokezea ndani ya hiyo Sala.
Kumbuka Sala ni Maombi, siku utakayoipata sala yako vema utanyamaza kimya, Na siku hiyo ndio utaacha kupeleka maombi yako ya Biashara, sijui ushinde kesi, mwanao apate visa, afanye uzuri mtihani wake, kazini upande cheo,Jirani aharibikiwe, vyote hivyo vitasimama kwa sababu siku hiyo utanyamaza kimya kwa kuwa umegundua kile ambacho  Akili (Mind)yako ikiongea, hicho kitu kinanyamaza, Wewe ukinyamaza hicho kitu kinaongea, kuanzia hapo kila ukiingia kwenye sala na kutoka utakua ukisema "kile nilokipoteza miaka yote nimekiona ndani ya Sala", sasa sitaki maasi, sasa sitaki machafu ila nasadikisha Mollah wangu pekee ndie anostahiki kuabudiwa, na kuanzia hapo utaanza kuhifadhi kila kipindi cha Sala zako.

Sunday, October 4, 2015

MATIBABU YA ROHO PART 1

Asalaam Aleiykum

Naanza Darsa yangu ya leo kwa maneno yalotamkwa na (Professor)mmoja kwenye (University)nilohudhuria sherehe za kuhitimu (Graduation)Mahafali ya Mwanangu hivi karibuni,"Professor" huyo alisema hivi "Na nukuu""Tumefanya uchunguzi na sasa tumegundua kuwa Ukisoma au Ukipata Elimu kuna mambo kadhaa unaepukana nayo, akayataja baadhi ya mambo hayo na kusema, "Unaepukana na mambo ya ukhalifu(Criminal activity)akataja jengine na kusema unaepusha mzigo kwa serekali ya kukutibu, akimaanisha unajiepusha na maradhi,(Unaishi vizuri)katika kuchunga Afya yako, kutokana na hilo jambo la elimu pia unakua na Maisha bora katika uhai wako.
Mimi Nakubaliana na (Professor) huyo katika suala la Mtu kukusanya (Information), unakua unajua na unafahamu kuwa ukivuta sigara utakufa na Cancer, kwa hiyo unaacha kuvuta, lakini tukumbuke maneno haya ya (Elimu)au kujua yalitamkwa ndani ya (Quraan)miaka kama 1400 ilopita kwenye sura ya (Az-Zumar-39.9)
قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الَّذِينَ يَعْلَمُونَ وَالَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ
Sasa cha kushangaza zaidi kwanini wenye kujua ndio wanateseka?,Nini kinawaponza?,Mbona imekua tafauti inaonekana wasojua ndio wanastarehe, wasojua hawana wasiwasi wanafurahia maisha haya kama vinyama vinavyofurahi. Sasa kwetu sisi kimezidi nini mpaka hatuna furaha, Majumbani hakuna mapenzi, kila mtu kachoka anaona bora aende barazani, au aende (disco)kuliko kukaa ndani, ana khofu mara mwenzie atamparura, basi ikiwa imefikia hali hiyo lazima kuna mambo ambayo yanasababisha hali hiyo.
Sasa Ingia kwenye Darsa hii ya (matibabu ya Roho)ili upate kumeza kidonge chako na kupata nafuu ya maradhi hayo, Kumbuka vizuri hakuna chenye kuigusa Roho yako, lakini hiyo Roho imeponzwa na jambo moja tu nalo hiyo uwezo wa kujua, nikiwa na maana wewe Mwenye kusoma sasa hivi, ndio Mwenye na hiyo Asili ya kujua ambayo hatimaye unaweka hizo (Information)katika kumbukumbu ya Akili yako. Japokua yenye kushikwa na maradhi ni Mwili(Body)na Akili(Mind)Lakini huwezi kuvitibu viwili hivyo mpaka kwanza uifanyie marekebisho ya matibabu Roho yako, ndio Maana Mwenye enzi Mungu akasema kutumia (Jumla)katika sura ya (Anfal aya ya 53)
ذَٲلِكَ بِأَنَّ ٱللَّهَ لَمۡ يَكُ مُغَيِّرً۬ا نِّعۡمَةً أَنۡعَمَهَا عَلَىٰ قَوۡمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُواْ مَا بِأَنفُسِہِمۡ‌ۙ وَأَنَّ ٱللَّهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ۬ 
Hayo (yakuawafikia hizo Balaa za kukosa Raha) ni kwa sababu Mwenye enzi Mungu habadilishi kabisa neema alizo waneemesha watu, hata(mpaka)wabadilishe wao yaliyomo nyoni mwao, hakika Mwenye enzi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye Kulijua kila jambo.
Kwa hiyo Nyoyoni kwenye hiyo Roho kuna Maradhi na hiyo ndio kazi ninayo ifanya ili na wewe urejeshe na kurejeshewa Furaha yako. Lakini kwanza lazima ujijue unaumwa Nini?
Endelea Part 2


MATIBABU YA ROHO PART 2

Asalaam Aleiykum

Ugonjwa ulo nao ni hatari, na kama haujatibiwa basi mpaka utaondoka kwenye Dunia hii utakua unaumwa na Ugonjwa wa (usununu)hali yakua huna Furaha, Sasa Magonjwa gani ya Roho yanotusumbua? huwa nashangaa sana nikipata mashtaka au malalamiko ya Watu wengi husikii kabisa kutajwa Maradhi yanomsumbua Mtu bali hutajwa sababu nyengine, kama Mume wangu hanisaidii chochote, au Mke wangu kawa kisirani hatizami watoto ipasavyo, au Watoto wamekua (Manunda)wajeuri ndani ya nyumba, sina masikilizano na Mke wangu, au siku hizi sina furaha kabisa kwa kila nitendacho, au bure namchukia fulani, nasikia kero tu kwenye maisha yangu na ndani ya nafsi yangu, au jambo dogo tu nahamaki,Nikisikia Asalaam Aleiykum Bwana nasikia nimeitwa Mtwana naanzisha ugonvi.
Kwa Muono wangu takriban Maisha yako yote yamekua ya Chuki,Visasi, Ghadhabu, Pengine unakerwa kazini ukirudi nyumbani mtoto kamwaga maji unampiga kama vile unaua nyoka, nini kimetokezea Majumbani kwa ujumla na hata kwa kila mmoja wetu.Jee tuseme hiyo Rehma na Baraka imeondoka kile kipindi cha (Honey Moon)ilipokwisha?halafu cha ubaya zaidi Mtu akisha choka huku nje anakusanya mambo yake yote halafu anaigeukia Dini, hapo inapatikana hatari kubwa, bora ageukie mambo mengine kuliko kuvaa joho la dini, hupati isipokua chuki tupu, unamuona hana furaha kwa sababu kachanganya (Madawa).Utaona anaanza kufukuza mpaka wale wanaotaka kujisalimisha kwa Mollah wako. kwanini ikawa hivyo? kwa sababu Dini yake, Matendo yake yanakua ya Maradhi matupu tuko nao na tunawaona wanavyoteseka ,kwa kuwa hawajapata dawa ya kuitibu Roho yake.
Sasa ukitaka matibabu ufanye nini?, hapa kuna uchaguzi wa aina mbili, Ima uendelee na Maradhi ya Roho, au utafute Dawa, ambayo wengi wanakwenda kwa (Doctor)atibiwe maradhi ya Roho, (Doctor)au Mganga wa kienyeji hatibu maradhi ya Roho, wao wanasaidia kukupa nafuu ya Mwili(body) na Akili(Mind)anafanya nini?anakupa matibabu ya aina tatu, anakupa Vidonge, anakupeleka kwa (Therapist) au (Counselling)sikatai vitu hivyo vinasaidia kuleta Nafuu kwenye (Body) na (Mind) lakini hakuna manufaa kwenye Ulimwengu wa Roho, Katika kuhangaika huko kidogo wamegundua kwa mbali kuwa kuna kitu nje ya viwili hivyo ambacho hakipo kwenye uwezo wao ambacho kama utakifanyia (therapy au counselling) unaweza kupata nafuu, ndio unaona watu wengi wanaishi kwenye nafuu tu, kwa wale wenye kupata angalau hayo matibabu ya kisayansi, Wengi wanataka kupona lakini masikini hawaijui dawa, hawajui wafanye nini.
Leo unapewa muelekeo wa hiyo Dawa ili maradhi yako yapone, ili na wewe uweze kuishi Furahani.
Endelea part 3


MATIBABU YA ROHO PART 3

Asalaam Aleiykum

Sasa ukitaka hiyo Dawa lazima ukijue hichi cha Nne ambacho si (Madoctor)wala(Waganga)wenye kukijua, hukipati kitu hicho ambacho ndio dawa yenyewe kwa kutoa Rushwa wala kujidai kwa cheo chako ulo nacho, Dawa hii au kitu hicho anatoa Mwenyewe alokupa hiyo (Roho), Akikupa dawa hii wewe unakua Furahani, sasa dawa gani hii yenye kutakiwa na kila mtu.
Dawa hii hapewi ila Mtu ila wachache wenye kutimiza masharti yake, ita Dawa hii au kitu hichi upendavyo, Kiite (Taqwa) au Mapenzi, kiite Utiifu au Ucha Mungu lakini Muhimu ukipate kama alivosema Mwenye enzi Mungu wakati anazungumza au kumpelekea (Wahyi) Nabii Musa a.s kwa kumwambia(Mwisho wa aya ya 39)" ۥ‌ۚ وَأَلۡقَيۡتُ عَلَيۡكَ مَحَبَّةً۬ مِّنِّى وَلِتُصۡنَعَ عَلَىٰ عَيۡنِىٓ (٣"
Na Nimekutia Mapenzi yanotokana na Mimi, Na ili ulelewe machoni mwangu(Katika uangalizi wangu )
Hapo kumetajwa mambo makubwa yanataka siku nzima kuchambuliwa ila kwa haraka nakufahamisha hivi, huna furaha katika Dunia hii isipokua uteremkiwe na mapenzi ya Mwenye enzi Mungu, na yakisha teremka ndio unaweza (Kushare)na wenzio kama alivofanya Nabii Musa a.s baada ya kuwaona watu wake wanateseka ndio yakamunigia mapenzi ya kuwavua kutoka kwenye mateso hayo.
Tunaendelea na sisi kutafuta hali kama hiyo ya mapenzi na Furaha, kukitafuta hicho cha nne, huwezi kukipata lazima urejee au niite (repentance)uondokane na tabia ya uasi wowote ule ulo nao, pengine umeacha tu lakini (Inward)kwenye nafsi yako hujabadilika, kwa hiyo kama unaendelea na jeuri na (punishment)adhabu inaendelea unafanywa uwe huna furaha kwa kila ambacho hujakitakia msamaha au kutubu kama mnavyoita, au kusamehe na kusamehewa.
Sasa ufanye nini kuyapata hayo Mapenzi? kuna Masharti yake lazima yatimizwe ndio uwe unaishi kwenye Furaha, kumbuka mapenzi ndio yalobeba hiyo Furaha, kwa hiyo lazima uyapate mapezi ndio uwe furahani kama dunia hii ilivozungukwa na mapenzi matupu ikiwa utafungua macho yako na kuona hilo. Sasa ikiwa hivyo lazima ujiulize mbona wewe unaishi na maradhi? ya Chuki,Hamaki,Hasira,Wivu,na Choyo na mengineyo, daima huko Furahani.
Inatakiwa jambo la mwanzo ulitizame kwenye Ulimwengu huu kila kitu kwenye Ulimwengu huu kimeumbwa kwa Mapenzi ya Mwenye enzi Mungu kuanzia kuumbwa kwako na kila kilichomo, sasa nini kosa lako, Kosa lako wewe umetoka kwenye njia ilonyooka kutokana na mambo mengi sio ya haki na sheria uliyoyafanya ili kuipata hiyo Furaha na mapenzi ndio unatakiwa urejee au urudi ujisafishe. Na hapo ndio unakutana na tafsiri yangu ya neno (Love), maana yake kutokana na mimi ni hii.
(Look Over and View your Emptiness).
Na hiyo pia ndio maana ya yale maneno (Yafanyie wepesi Mizigo yako).
Endelea part 4


MATIBABU YA ROHO PART 4

Asalaam Aleiykum

Binaadamu hapo ulipo una mizigo mingi, dawa haiwezi kufanya kazi kirahisi mpaka uipunguze ili uwache nafasi (empty)mapenzi yaje kukaa sio kupita kwenye moyo wako, Utafanyaje?.Cha kwanza kukumbuka wewe ni (Kinyama)Niseseme hivyo ukaona natukana, ikisema (Biology)ndio inafundisha, Kumbuka sote ni Vinyama, tafauti yetu sisi tumepewa mitihani, na makosa  au kutofaulu katika Mtihani huo ndio kuna kunyima mapenzi na furaha.
Sasa ikiwa umewakosea Viumbe wenzio basi jambo la mwanzo kulifanya kaombe msamaha kwa kila ulomkosea unayemkumbuka , kumbuka mwanzoni mwa Darsa tumezungumzia jambo la (Kujua) kwa hiyo ukenda kwa Mtu kwa moyo mkunjufu, ikawa (sincere and humble)bila ya jeuri, ukakiri kwa kujua kosa lako na yeye alokukosea akajua kwa njia ya haki kweli umekuja kuomba msamaha hapo inakua kazi imemalizika, mzigo umeshatua,(Kujua inageuka kujulikana)na tatizo hilo linamalizika nafasi inakua(Empty).
Ikifikia hali kama hiyo basi jua kama atakusamehe sawa na kama hajakusamehe huo unakua ugonjwa wa Roho yake, Ikisha geuka nyumbani kwako kwa Mkeo au Mumeo huko ndiko kwenye shina la matatizo yote ya kukunyima Raha, fanya siku maalum ugeuke Babu jinga umuweke kitako Mwenzio umuombe Samahani, mwambie macho yameniponza lakini kuanzia leo sitizami nje ntakua naangalia ndani, nilikua nakupuuza wewe (soul mate)wangu kwa hilo nisamehe, Mpaka watoto waombe samahani usipande Kiburi ndicho chenye kukuzuia usiyapate mapenzi na Furaha ya Roho, anza kutumia wakati wako na Mkeo, Wanao, cheza na familia yako, msaidie watoto na kazi za nyumbani, usione aibu ukiambiwa kupiga deki piga, fanya chai mfanyie chai,zoa taka zizoe, Wallahi ukiwa unafanya kwa Ridhaa yako kidogo kidogo kuna mambo yataanza kukushukia moyoni mwako utashangaa yanatokea wapi, ifanye siri yako, ukibubujikwa na machozi usijizuie yaache yatoke.
Basi zidisha furaha na watoto wako, usiwafanye wakuogope, kuwa nao karibu, wafanye marafiki zako, kidogo kidogo utaanza kuona unapona Furaha inarudi kwenye Roho yako, alama za kukunja uso zinapotea, utaanza kujua nini maana ya Samahani, Samahani haina maana yoyote huku nje, lakini ndani ina thamani kubwa, Samahani ndio hiyo (Emptiness)nini kinyume cha (Emptiness)ni hiyo (Fullyness)Samahani imejaa mapenzi ndani mwake, kwani hujawahi kusamehewa ukajiona unakuwaje?.
Mwalimu akikusamehe au mzazi unahisi nini?, Jee Mtu akikusamehe Deni unakua katika hali gani, sasa ikiwa Mwanaadamu mwenzio anakupa furaha ya dharura kama hiyo nini habari yetu sisi unaposamehewa na Mollah wako?.
Mollah ambaye amewapa mapenzi yake wanomuasi kuliko wewe, anawapa majambazi na wahalifu, anawapa wauaji na wanaodhulumu, hali gani inakua inakua kama wewe utakaa msikitini au nyumbani kwako chumbani ikawa unakumbuka Dhanmbi moja baada ya nyengine na kila ukikumbuka basi unasali Rakaa mbili za Sala ya Toba, usifanye uvivu kabisa, na kila ukisimama Utamuomba Mollah wako kama hivi "Ewe Rabbi Mollah wangu hakika mimi kwa yakini nimefeli Mtihani wako, Na najua kwa yakini nimefanyaa jinsi kadhaa wa kadhaa, basi kwa dhati ya uwezo wako uloniumbia mimi nakuomba Mollah wangu unisamehe", utaomba hivyo ndani ya kila sijda.
Baada ya kufanya hayo kwa kadir ya uwezo wako wa kukumbuka makosa yako, na ikiwa maombi yako ilikua ya Ikhlas basi baada ya siku chache au hata zisifike utajikuta umerejea kwenye(Emptiness)kama (Mtoto)huna mzigo, na hapo tena ndipo utajua (Kilichofanyika kimefanyika)huwezi ku-(reverse)na ukijua hivyo muda huo huo ushapata matibabu(Depression)zinaondoka kwenye Roho.Furaha inaanza kukuteremkia na furaha ikiteremka wakati wowote mapenzi yanaweza kukushukia, unachotakiwa hivi sasa usubiri kwa kusali, Usubiri kwa kuwakumbatia na kuwasaidia mayatima,usubiri kwa kuwalisha masikini, na ghafla utajikuta umejaa mapenzi na huo ndio Ucha Mungu, na huyo ndio Mja Mwema, na hayo ndio matibabu ya Roho ambayo ukiyapata utakua na furaha mpaka siku yako ya kuondoka kwenye Ulimwengu huu.
Tunamuomba Mollah wetu atujaalie tuyapate mapenzi na Furaha zitokazo kwake na zidumu kwenye Roho zetu.