Sunday, May 26, 2013

ALAMA ZA MWENYE KUIPATA SALA PART 1

Asalaam Aleiykum,

Umeshawahi kumuona Mtu kalala kwenye ngoma chini ya spika? watu wanaimba kwa mayoe, bibi harusi ndio anaingia na huku ukitizama pembeni Mtu kalala sio usingizi tu, bali anakoroma na anaweza kuota ndoto kabisa akiamka akakuhadithia, au unaingia senema unalipa pesa halafu unalala mwanzo mpaka mwisho, basi ukiyajua hayo kama yanatokea na hili jengine pia linatokea, unasimama kusimamisha Sala na  huku unaota ndoto za ajabu ajabu, umo kwenye usingizi mzito na kama utaamshwa ghafla unaweza kumpiga mtu kibao kwanini kakushitua, sisemi haya ikawa nazua, au nimeyapanga, bali itizame Sala yako ikoje, halafu ufanye hima kuzingatia haya nitakayo kufahamisha kwenye Darsa yetu ya leo ili ukurupuke utoke usingizini. Wengi katika sisi tunaitundika Sala kwa Maringo tukiwa na viburi yakwamba nisha Sali, na ishaandikwa, Nasisi tumekubali umesha sali lakini jee imekubaliwa? na Jee Mwenye enzi Mungu kataja mifano yoyote ya kukubaliwa hiyo Sala,? pata habari hii ili ujijue unasimamisha Sala au unasimama mwenyewe tu na ndoto zako.
Nini Sala?
Sala ni Maombi maalum ambayo madhumuni yake unaomba ukubaliwe kukaribishwa, kupokelewa, kuruhusiwa kuingia na kuwa karibu katika Utukufu wa Ufalme wa Mwenye enzi Mungu na ukisha kuruhusiwa katika (Matuka-Saabur)hapo tena Sala inapatikana kwa ukamilifu,( na Sala  ikipatikana kwa Ukamilifu hakuna siri tena utakua unajua ama mimi Mollah wangu anazipokea Ibadah zangu)ndio maana ikawekwa wazi kama tutavosoma huko mbele, Naam yaweza kuwa unatuma maombi haya (Sala zako mara tatu au mara tano au mara elfu kwa siku)Lakini tamaa yako unataka ukubaliwe maombi haya ili upate marejeo mazuri kwa Mtukufu Mollah wako yule aloumba Mbingu na Ardhi na yule alokukirim wewe huu Uhai wa kuweza kumkumbuka.
Nikitaja Sala au (Maombi) sina maana ya ile Sala yako ya kuomba cheo au kuomba ubunge, sikusudii yale maombi yakuomba Mke au Mume na mengineyo, laa Sala nilokusudia hapa ni ile unayokwenda kwa Mollah wako na Moyo mweupe ulojisalimisha, Hutaki Mali au kutaka Pepo, huna choyo au kuwa na wivu, hujenda na hasira wala chuki yoyote, Umekwenda Msafi hujabeba mambo ya kipuuzi, umekwenda kwa Mollah wako huna munkar wala Fawahisha kwenye kichwa chako, unasimama na kutamka Maneno ya yakini Allahu Akbar: Nani mwenye kutamka maneno hayo yatupasa tuulize Quraan sura ya Muumin aya ya (1)"
"قَدۡ أَفۡلَحَ ٱلۡمُؤۡمِنُونَ"
"Wamefuzu Waloamini"
Kwanini Wakafuzu? Sababu mwanzo walikua kama mimi na wewe, wamepita katika daraja ya kwanza ya kusikia, halafu wakapita katika safu ya pili ya kukubali, ikisha wakaingia katika hii sehemu ya tatu  yakuwa waumini, Unapewa habari kama hizi pengine mwanzo zilikua hazijakufikia, Na sasa zimekufikia ili upate kubadilisha mwenendo wa kuingia katika Sala yako, upate Imani ya kweli na upate kuipata Sala na wewe uingie katika kundi lilotajwa kwenye hiyo aya "Wamefuzu Waloamini".
Usije ukajidanganya hivi sasa kudhani umefuzu, yakupasa ujiangalie upo katika kundi gani hivi sasa ili uzidishe juhudi.Nini Kufuzu? kufuzu kuna mambo mawili lazima yatokee ndio ujue umefuzu, la kwanza ima uwe umeshindwa ukajaribu tena, na la pili ukajitahidi na kuzidisha juhudi  mpaka ukapata sifa ya kufuzu(Kufanikiwa)."Wamefuzu Waloamini" na ukifika (Stage)hii moja kwa moja unakua Muumin, na Muumin maana yake kila jambo lako linakua kwenye mstari, Muumin wa kweli hana nafasi ya makosa kwenye moyo wake.
Sasa Vipi unakua Muumin? Endelea part 2

ALAMA ZA MWENYE KUIPATA SALA PART 2

Asalaam Aleiykum,

Unaweza kuwa Muumin kwa njia mbili. ya kwanza una chupa moja kwa moja kwenye Imani, hutaki maelekezo, huna haja ya vigezo, na hiyo sana huwa zawadi kutoka kwa Mollah wako, na hii ya pili ambayo sote tupo hivi sasa ni ile ya jitihada ili tupate Kufuzu, na hii inaanzia wapi? hii inaanzia kwenye Akili(Mind) kwa hivi sasa Imani yako bado inaelea kichwani, haijaanguka Moyoni ndio maana utaona ukenda kwenye Sala hakuna unyenyekevu wowote unaoupata, vipi utaupa unyenyekevu wakati unakwenda kusali viatu umeweka (kwapani)nimetokea (Tanzania) hivi karibuni mambo niloyakuta huko imeniingia huruma sana kuziona vipi Sala za huko Nyumbani zinasaliwa, kuanzia kwenye Udhu unaanza kuvifikiria viatu, vipi leo utakua na (Unyenyekevu) katika Sala, vipi utakua na (Unyenyekevu)wakati Imam anasalisha kasujudu anasubiri watu wamalize kutia Udhu wapate kuwahi Sala, vipi utakua na unyenyekevu wakati unaingia katika Sala mawazo yote yapo kwenye (Sex), vipi  utapata unyenyekevu wakati unajiunga katika hiyo Sala umejaa hasira na hamaki na chuki vimetawala Sala nzima, madeni na mikopo yote inakuja hapo, hotuba za Siasa unaandika hapo, hesabu zote unafunga hapo, majibu ya mtihani unayapata kwenye Sala hiyo hiyo, vipi leo useme umepata unyenyekevu.
Hiyo unayofanya sasa hivi ni jitihada na ndio vizuri kufanya jitihada wakati huu umri unapotea, zidisha juhudi sana, Sasa nini ufanye ili kuipata hiyo Imani? anza kuitumia hiyo (Mind) Akili, fanya uchunguzi Mollah kakupa mifano, kama kwenye aya hii ya sura ya Dhaariyat aya ya 20 "وَفِى ٱلۡأَرۡضِ ءَايَـٰتٌ۬ لِّلۡمُوقِنِينَ"
"Na Katika ardhi zimo(dalili chungu nzima)kwa wenye yakini"
fanya uchunguzi upate hiyo yakini, ukiipata hiyo yakini ndio ushapata Imani, na ukipata Imani utaanza kujiuliza mie nani, kwanini niko hapa, vipi inakua mimi na kinyama sote tunalala usiku, kinyama kikiumwa nani anakitibu, na kwanini kinapona, na nani anawaponesha,mbona vinyama vina akili kama zetu, vinatafuta chakula na vikishiba havina hata haja ya kuweka akiba, ina maana vinyama vina Imani kuliko mimi, vina muamini Mollah kushinda mimi, na mengine kama Mollah wetu alivotuwekea Rada mbinguni za hizo nyota tukawa tunajua huku mashariki na huku magharibi, na utapata mengi ukianza kutafakari mpaka utafika ukingoni hapo Akili itasimama, na Akili ikisimama hapo ndipo pahala unapoweza kuchupa ukawa Muumin, na ukiogopa ukarejea nyuma unakua unabakia kuwa Muislam, na Sala yako inaendelea kuwa kama ilivyo hivi sasa.
Sasa ukichupa ukawa Muumin nini kinatokea?
Yanatokea mabadiliko makubwa, sababu unakuwa unaishi moyoni(Through heart) na sio akilini (Through Mind). Na unapoishi moyoni unaona mambo kwa njia nyengine kabisa, unakua katika hali mpya kabisa, na kama unataka kujua hali hiyo inakuaje basi muulize yule anopenda, yule alo (Fall in Love)au mtizame mwenye kupenda hata akipewa kikombe cha sumu na mpenzi wake, na wewe uwe shahidi umeona sumu imetiwa, na upige kelele hiyo sumu, hiyo sumu, basi utaona yule anopenda anakamata kikombe na kumimina chote mdomoni kwa ajili ya Imani aliyonayo, sasa ikiwa hilo ni penzi la kumpenda mwanaadamu mwenzio, nini habari yako wewe ukiyagundua mapenzi ya kumpenda Mollah wako, una hali gani sasa ushajitaarisha kusimama mbele ya yule umpendaye, vipi leo katika penzi hilo unatoa nafasi ya kuingia kitu chengine.
Sura ya Muumin aya ya 2 "ٱلَّذِينَ هُمۡ فِى صَلَاتِہِمۡ خَـٰشِعُونَ"
"Ambao katika Sala zao huwa wanyenyekevu"
Unaingia katika hiyo Sala kwa njia ya moyo, siyo njia ya Akili tena, kabla ya kuanza Sala lazima mambo yote yasimame, fikra zote mbaya zipotee, heshima ya Sala yako ibadilike, ukisoma aya ndani ya Quraan sio kwa kupita ni lazima uzame na huku unaifasiri taratibu huku machozi yanakutoka kwa  kuujua ukweli wa maneno hayo na kufahamu kwa  ukamilifu unachokisoma na kukiabudu. Na hapo ndipo kwa mara ya mwanzo utapata utulivu na unyenyekevu mkubwa wa hiyo Sala. Endelea part 3

ALAMA ZA MWENYE KUIPATA SALA PART 3

Asalaam Aleiykum,

Ukisha kupata unyenyekevu, ndio unaweza kuyapata maneno ya Hekima ya kumuomba Mollah wako, (Mfano) Mollah wangu nikubali kuwa kipenzi chako, nifungulie mie miujiza yako niwe shahidi kwa hilo, nipe zaidi ukuruba huu katika Sala ili nipate ladha ya kumilikiwa na wewe Mollah wangu, usinijaalie mimi kukusahau na kutoka katika hali hii nilonayo ya Sala, kumbe hivi ndivyo ilivyo Sala, basi nipe mimi kila saa na dakika niwe nimo katika Sala nasali kwa ajili yako. Na huko ndiko kumkumbuka Mollah wako, ukiwa umesimama, umekaa au hata ukiwa umelala, umo usingizini(Body)Mwili umelala wewe umacho una msabahi Mollah wako, na hiyo ndio daraja ya Muumin aliyefuzu, na hapo tena ikimalizika hiyo Sala ya wakati wewe unaendelea nayo ile yako ya kudumu, na ukiipata hiyo ya kudumu unakuwa vipi? vipi inakua ukishamaliza Kusali, aya ya 3 "وَٱلَّذِينَ هُمۡ عَنِ ٱللَّغۡوِ مُعۡرِضُونَ"
"Na ambao hujiepusha na mambo ya Upuuzi"
Ukishamaliza kusali inabidi uendelee na maisha, na kuendelea na maisha inabidi ukutane na vishawishi vingi, kwa hiyo kama kweli wewe Muumin na unaipata Sala, basi unajiepusha na mambo ya upuuzi, Mollah wako hataki kipenzi chake kiwe kichepe chepe, hakuzuii usifurahi, ila anakukinga na mambo ya kijinga, sababu anajua mambo ya kipuuzi yameandaliwa na shetani ili kukusahaulisha, mazungumzo ya vibaraza, na hivi na vile, fulani kafanya hivi yule kafanya vile, yote hayo mambo ya kipuuzi hayakuhusu, na ni vitu vyenye kukupunguzia Imani, sio kwamba ukimbie watu, au uanze kupanda kiburi, umeambiwa ujiepushe, sio ujikinge, kujikinga maana yake unajilinda, hukutani nao, kujiepusha maana yake upo nao lakini wewe mizizi ya Imani imeshaota wao wanazungumza siasa wewe unamdhukuru Mwenye enzi Mungu, huko ndiko kufuzu, na huko ndiko kuipata Sala. Na mengine yalotajwa katika sura hiyo ambayo tutayazungumza siku za mbeleni za kufuzu kwa Muumin) lakini ukumbuke Muumin bado yumo kwenye Mtihani  mpaka upite katika daraja hiyo na ufike katika daraja nyengine za (Swalihina na Mukhlisina)hapo tena ushakua mtu mwengine kabisa, unaishi Duniani lakini ushawasili Akhera. Mollah wangu tujaalie tuwe katika kundi la wale wanokubaliwa Sala zao, tupe sisi faida ya Sala kuijua na kuishi nayo Daima kama walivofanya waja wako wema walotangulia, wewe Wajua Mollah wetu Dunia imetuzonga katika karne hizi tunazo ishi hivi sasa, basi tufanye wateule wa zama hizi watakaokuwa wambele katika enzi yako siku hiyo utakayo tuhitaji. Amin.

Saturday, May 11, 2013

TOBA TUBI NA MALI YA HARAMU PART 1

Asalaam Aleiykum,

Limekuja swali linasema hivi, Nini hukumu ya wale ambao wanaimba, wanocheza kamari na kufanya mengine ya haramu halafu wakatajirika kutokana na vitu hivyo(Yaani)wakapata pesa halafu ikatokea wakagundua kama walikuwa wanakosea mbele ya Allah, ikisha wakarudi kwa Mollah wao kwa dhati, vipi hapa Sheria inasemaje, Juu ya Mali zao walizozichuma huko Nyuma kwa njia ya Haramu?.
Toba Tubi yoyote anataraji jawabu iwe nzuri yenye kumridhisha, iwe inampa tamaa yeye kuwa ulivofanya sio tatizo na unaweza kubakia na Mali hizo pasi kupata tatizo lolote, kwani wanadhani haramu ni lile tendo lakini hiyo Mali ishavuka daraja ya hilo tendo, Hivyo ndio Akili zetu zinavyotutuma nipate hapa ulimwenguni raha mustarehe na huko mbinguni Akhera kadhalika niwe pia mimi Bwana, Hiyo ndio Akili ya mfanya biashara anayedhulumu, hiyo ndio Akili ya kila anopata chumo la Haramu, anafanya (Bussiness) na Mollah wake mimi nitadhulumu, halafu tene nitakula haramu, ikisha nitabakia na Mali yangu ya Haramu, na Wewe Mollah wangu upande wako fanya kimoja tu nisamehe.
Nini Anasema Mollah wako kuhusu kadhia hii ya Toba?(Al-Imran.135)
"وَٱلَّذِينَ إِذَا فَعَلُواْ فَـٰحِشَةً أَوۡ ظَلَمُوٓاْ أَنفُسَہُمۡ ذَكَرُواْ ٱللَّهَ فَٱسۡتَغۡفَرُواْ لِذُنُوبِهِمۡ وَمَن يَغۡفِرُ ٱلذُّنُوبَ إِلَّا ٱللَّهُ وَلَمۡ يُصِرُّواْ عَلَىٰ مَا فَعَلُواْ وَهُمۡ يَعۡلَمُونَ"
"Na(wale)ambao wanapofanya uchafu, au Kudhulumu nafsi zao,humkumbuka Mollah na kuomba msamaha kwa dhambi zao, Na nani anayeghufuria dhambi isipokua Mwenye enzi Mungu?Na hawaendelei na (Madhambi)waliyoyafanya, hali wanajua(Hayo ni Haramu)?"
Hapo juu swali limeanza wakagundua kama walikua wanakosea, na hapa chini aya inataja wazi, wala haikubana maneno,(Hawaendelei na Madhambi hayo)hiyo ndio kusudio la msamaha, Msamaha umekusanya mambo matatu, la kwanza (Kujuta)kwanini nikadhulumu, ilikuaje nikatenda haramu ile, sikufanya yale isipokua ama nilikua nimekusahau Mollah wangu au nilikua sijui, sasa mimi naomba Ridhaa yako unisamehe "Ewe" Muumba wa Roho yangu.
La pili Kuchukia, kwanini mimi ilinipelekea kuchukua mali ya watu kwa hadaa au kwa nguvu, kwanini nikachuma mali hii kwa njia ya Haramu na mpaka sasa naishi nayo, na kila nikiiona inanikumbusha Dhambi zako na yote niliyoyafanya, kutokana na hali hiyo mimi sasa sitaki hata kuziona mali hizi za Haramu, chukueni zote mimi hazinihusu hata chembe, sitaki kuwa Mmiliki wake abadan.
Na la Tatu kuwa hutotenda tena kosa hilo, sasa vipi utaendelea kubakia na Mali ya Haramu halafu useme umetubu, ndio maana nimekwita Toba tubi, maana yake unaitaka mali ya haramu na pepo ya halali, vipi viwili hivyo vitakaa pamoja, Madamu umechagua kubakia na mali ya haramu basi jijue umeshajiamulia wewe mwenyewe kwenda kuteseka kwenye Jela ya Mwenye enzi Mungu huko Akhera, na Kwa hilo halina mbadala kabisa, kwa yakini litatokea mapema pale utakapofunga macho tu, huku Ulimwenguni mali inaendelea kudumu, na huko Akhera wewe unaendelea kuchomeka, Shauri na uamuzi unao wewe, waachie wanao au ndugu zako mali ya haramu halafu wewe jichukulie dhamana ya moto.
Endelea Part 2


TOBA TUBI NA MALI YA HARAMU PART 2

Asalaam Aleiykum,

Wengi katika wanaadamu wanadhani mambo yapo rahisi huko kesho Akhera, wanafikiri hukumu itatolewa kutokana na muono wake unavomtuma, na wengi tushajidhulumu kutokana na dhana hizo yakuwa bakia na mali ya haramu na Mollah wako keshakusamehe, hebu itupie macho aya ya Quraan inayokuonesha vipi ukimkufuru Mollah wako na kujidhulumu nafsi yako unakuaje, hukuanza wewe fikra hizo wameanza tokea walopita kabla yako, Quraan Al Kahf 35-36,

"وَدَخَلَ جَنَّتَهُ ۥ وَهُوَ ظَالِمٌ۬ لِّنَفۡسِهِۦ قَالَ مَآ أَظُنُّ أَن تَبِيدَ هَـٰذِهِۦۤ أَبَدً۬ا"
"Na akaingia katika Bustani yake na hali yakuwa anajidhulumu nafsi yake, akasema (Mimi)sidhani abadan kuwa (Bustani-Mali)hili litaharibika"
Na hivi pia unavodhani wewe, aah si nishasamehewa, vipi tena niadhibiwe kwa sababu nakaa kwenye Nyumba ya haramu, natumia  vilivyo vya Haramu, muda wake ushapita mie sifanyi haramu tena, sasa itakuwaje nipewe adhabu.

"وَمَآ أَظُنُّ ٱلسَّاعَةَ قَآٮِٕمَةً۬ وَلَٮِٕن رُّدِدتُّ إِلَىٰ رَبِّى لَأَجِدَنَّ خَيۡرً۬ا مِّنۡهَا مُنقَلَبً۬ا "
"Wala sidhani kuwa kiyama kitatokea, na kama (kitatokea hicho Kiyama)nikarudishwa kwa Mollah wangu, bila shaka nitakuta kikao chema kuliko hiki(Nilichopata Ulimwenguni)(huku nipate na kule nipate)"
Hivi ndio sote tunavodhani, kula rushwa, chuma haramu, nyanganya hapa, kaibe kule, kwani hicho kiyama kipo, mbona mpaka leo hakijatokea, na hata kikitokea wewe ushasamehewa na huko utakuta (Jumba la Ghorofa na Swimming Pool)pembeni. Hasara kubwa na jambo zito sana unalofikiria, Shetani anakupigia muzeka wa usahaulivu, nyimbo inazidi kukupepea ulale uzuri, nasikia unakoroma mpaka huku nilipo, hebu acha kunifanyia zogo kwa usingizi usofaida, jaribu kujikumbusha nini Toba?
Wakiristo wanaita (Born Again)hawajakosea ni kama Mimba, hakuna anoendelea kubakia na Mimba lazima izaliwe, na uchungu wa kuzaa anaujua mwanamke, na wewe lazima upitie uchungu huo, lazima kama mali hiyo kachuma mzee wako au wewe mwenyewe basi lazima upate uchungu wakuitoa kama ulivopata Raha ya kuichuma, Usimame useme Mali hii si haki yangu na mimi naitoa yote kwa ajili ya Mollah wangu yeye ndio atakua Hakimu wa jambo hilo, majumba chukueni, magari chukueni, mapesa (bank yote yenu)mimi nataka niwe msafi kama siku nilozaliwa, au kama nguo nyeupe isiyokua na doa.
Hiyo ndio Toba wala sio Tubi, itamke sawa sawa upate kutubu kikweli, upate kutubu moja kwa moja haifai kubakia na chochote kile cha Haramu, Toba maana yake kujitua mizigo, sasa vipi leo umebakia umeibeba, halafu unasema nimetubu, Nini Toba?
Toba lazima upate uchungu, unaachia huku mate yanakutoka, kama unakula shubiri, upande chungu upande dawa, Toba lazima umungunyuke kama udongo ubakie mchanga, Toba lazima upotee ndani ya Nafsi yako, ikisha uzaliwe mwengine ndani kwa ndani, alotubia, hana tamaa, alotubia hafanyi tena, alotubia hadumu na kumbukumbu, anafuta vyote kama ulozaliwa Zanzibar, Ukaishi China, jee utaikumbuka Zanzibar, hiyo ndio maana ya Toba potea kabisa kazaliwe Dubai Rasulhema, hiyo ndio Toba ya Kweli na kama unazuia Mali yako ya haramu, wewe utakua Shahidi kwa hilo Mbele ya Mollah wako. Namuomba Mollah atukinge na yote ya Haramu.

Sunday, May 5, 2013

BARUA YA UKUMBUSHO PART 1

Asalaam Aleiykum,

Leo pokea bahasha ndani yake utaikuta Barua Adhimu ya Ukumbusho, fungua uisome Barua hii kwa utaratibu wa fikra ili umalizapo kusoma na wewe upate kuijibu kwa shauku na hamu kubwa, na ipe umuhimu wa pekee kwani utaulizwa jee hukuisoma Barua ya Ukumbusho?. Jee kwani wewe ilikua haikuhusu barua hiyo? mbona basi mliachia watu wachache kuandika barua hiyo.
Barua hii inatoka wapi na inakwenda kwa nani? Barua hii Inatoka kwa Mpenzi Mollah wako kwenda kwa vipenzi waja wake wakiwemo mimi na wewe, Anakuagiza Mollah wako wapelekee vipenzi vyako wote wakaribu ujumbe huu wakiwemo, wa kwanza mkeo au mumeo, kama kweli unampenda, ikisha wanao damu yako unayo ionea huruma, halafu tena wazazi wako wawili, na baada ya hapo wote walo karibu katika familia yako.
Anza kwa kuwaandikia barua hii au wasomee njia zote mbili zinafaa, na wa mwanzo muanze mkeo au mumeo na hao wawili imewahusu sana kwa sababu wao wako karibu sana mpaka malazi yao yako pamoja. Halafu tena wanafatia watoto wako au wazazi wako wawili, yaweza kuwa makaka zako au madada zako na pamoja wote walio karibu yako katika mahusiano ya kiroho, wote hao wasomee barua hii.
Naanza Barua hii kwa Jina la Mwenye enzi Mungu mwingi wa Rehma Mwenye kurehemu, Naandika Barua hii nikiwa na hisia za mapenzi kifuani mwangu,(Kwanini zikawa hisia?)kwa sababu mapenzi ushayamaliza kabla hayajaanza katika hiyo(Ndoa)ndio maana kutwa mnaparurana, imekuaje hali hiyo, imekua hivi, unampenda Sharbanu unamuoa Shabira, umeolewa na Abdulla unampenda Baja, hizo ndio hali zetu tulivyo, mume au mke anakua (Mfano)tu uko naye lakini unamungunyika ukimuona yule ulomtia moyoni, vipi leo utaruhusu mapenzi yatokezee kwenye moyo wako, wakati moyo wenyewe ushaufunga, na ungekua wazi moyo wako na mapenzi yametokezea basi (Wallahi)ungekua ushaandika Barua hii siku nyingi au ushaisoma maneno yake tokea kitambo huko nyuma, na kama hujaandika basi pia hujachelewa anza leo, Vipi?.
Naam: Mimi zimenijia hisia za mapenzi kifuani mwangu, halafu nikafunikwa na khofu kichwani mwangu ya kwamba mimi nimo hasarani ya kukukosa  wewe hapa Ulimwengu na kesho huko Akhera, na nimekubali kustahamili kukukosa hapa Ulimwenguni, kwani unaishi katika jumba la damu, jumba la usaha, jumba la wadudu, mkusanyiko wa mifupa na nyama na ndio maana unapokufa naufanyia ukarimu mwili wako kwa heshima ya kukuzika haraka sana, mpelekeni ataharibika, atatoa harufu msimweke muda mrefu, yote hayo nayasema mimi mwenyewe, na nimekubali kuyavumilia hapa Ulimwenguni, Lakini nisichoweza kukisubiri na kukinyamazia kimya ni ile hukumu ya Roho yako itakapoamuliwa sasa ikaishi na kuteseka Motoni, ama kwa hilo nimeshindwa kuvumilia ndio maana hii leo nakuletea Barua hii nikitumai utaipa zingatio la umuhimu wa kipekee ikiwa wewe ni mwenye kumogopa Allah na kufahamu umeumbwa na leo au kesho unaweza kuondoka katika Ulimwengu huu bila ya taarifa yoyote ile.
Kwanini nikayasema hayo?Endelea Part 2

BARUA YA UKUMBUSHO PART 2

Asalaam Aleiykum,

Sababu kubwa imetuhusu mimi na wewe, na mimi nadhani mahusiano yetu si ya nyama na mifupa bali yamekwenda mbali(Deep)Kiroho, na nimetambua mimi mahusiano yetu haya ni ya (Thamani)kubwa na yatakayo endelea kuishi milele,  Na kutokana na uhusiano huu ndio imekua sababu ya mimi na wewe kukutana hapa Ulimwenguni, na kutokana na sababu hiyo mimi sina shaka makutano yetu yatatokezea tena huko Akhera tuendako, napenda uelewe yametukutanisha Mapenzi yake Mollah wetu, wewe ulikua haupo katika Ulimwengu huu wala mimi sijaumbwa. sote sisi  tukapita katika Mlango wa Rehma wa Mwenye enzi Mungu ikisha tukazaliwa katika nchi moja ama tafauti, hapo tena tukaja kuungana na kuunganisha Udugu ulio imara kabisa, ikawa huyu mtoto, wewe dada, yule kaka, hawa wajomba, shangazi nk, sasa kilicho nipelekea kuandika Barua hii ni muono wangu mimi juu ya matendo yako, naona si ya kumridhisha Mwenye enzi Mungu.
Na mimi nina khofu kubwa ya wewe kwenda kuwekwa kwenye Jela(Shimo)la Jahannam, Na ninayo yakini kwa kuwepo kwa Moto huo kwa sababu Mitume yoote wametaja kuwepo kwake Jela hii, na mimi sina shaka kwamba woote wawe wenye kusema jambo ambalo halipo. Na Mollah katuhimiza katika sura ya At-Tahrim aya ya 6 "يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ قُوٓاْ أَنفُسَكُمۡ وَأَهۡلِيكُمۡ نَارً۬ا وَقُودُهَا ٱلنَّاسُ وَٱلۡحِجَارَةُ عَلَيۡہَا مَلَـٰٓٮِٕكَةٌ غِلَاظٌ۬ شِدَادٌ۬ لَّا يَعۡصُونَ ٱللَّهَ مَآ أَمَرَهُمۡ وَيَفۡعَلُونَ مَا يُؤۡمَرُونَ"
"Enyi Mloamini jiokoeni Nafsi zenu na watu wenu(Wakaribu)na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe, Wanousimamia(Walinzi wake)Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mollah (Wao)kwa amri zake, na wanatenda wanayo amrishwa".
Nimehimizwa nikupe ujumbe huu na yule anokujaalia kulala ikisha akakuamsha kwa Uwezo wake, anokujaalia kuhema bila ya kufanya juhudi yoyote upande wako, na akizuia pumzi kidogo tu unapaparika, huyo ndio alonipa mimi nguvu za kuandika Barua hii kukumbusha ujitahidi sana kama unampenda Mollah wako na mie mwenzio, basi sasa nakwambia acha kulewa, acha kuvuta bangi, acha mambo ya mirungi, jiepushe na kudhulumu, jizuie na kuzini, na ikisha nakutaka ujiepushe na mambo yote ya haramu, halafu najitolea mimi mwenyewe muhanga acha kuninunulia dhahabu au majumba na hizo pesa au mali ulonayo tulee mayatima, tuwatizame wajane,tuwalishe maskini, tukifanya hivyo jambo la kwanza hapahapa Ulimwenguni Mollah wetu atatueremshia mapenzi, atatupa baraka, tutapewa tahfif za maradhi, atatufanya wafalme kwa walotuzunguka, kwa hayo yote sijioni kuwa mimi mkosa katika kukuandikia barua hii Adhimu ambayo nataraji itakufika katika hali ya kuufahamu ujumbe huu wa kheri.
Nakwita mwenzangu urudi kwa Mollah wetu, mimi nishatangulia kamata mkono wangu tuwe pamoja, usiniache nikazama kwenye Nuru wewe ukabakia kichochoroni kwenye kiza totoro nini itakua hali yako,  Na kumbuka hakuna yoyote anorejea kwa Mollah wake ila hufunguliwa Neema zote na Rehma za Mwenye enzi Mungu, na kwa ushahidi wa hilo tujikumbushe barua ya Nabii Suleiman a.s alyomuandikia (Malkia Bilkis)kumwita kwenye Uislam. alifanya nini? sura ya Naml aya ya 28 mpaka 31.

"ٱذۡهَب بِّكِتَـٰبِى هَـٰذَا فَأَلۡقِهۡ إِلَيۡہِمۡ ثُمَّ تَوَلَّ عَنۡہُمۡ فَٱنظُرۡ مَاذَا يَرۡجِعُونَ"
Nenda na Barua yangu hii na (Wadondoshee)uwafikishie, kisha uwaache, na utazame watarudisha(Maneno) gani"
Na wewe kama unaogopa kumpa mkononi barua yako Ipost au weka kwenye mto usiku halafu kimbia ukalale ukumbini.

Endelea Part 3

BARUA YA UKUMBUSHO PART 3

Asalaam Aleiykum,


" قَالَتۡ يَـٰٓأَيُّہَا ٱلۡمَلَؤُاْ إِنِّىٓ أُلۡقِىَ إِلَىَّ كِتَـٰبٌ۬ كَرِيمٌ "
"Akasema (Yule Malkia kuwaambia washauri wake)hakika nimeletewa Barua Tukufu"
Namkumbushe yoyote kuhusu barua yako Tukufu, kwani ukimkumbusha umemwita kwenye utiifu, na ukimwita kwenye utiifu maana yake umemleta kwenye Taqwa, na ukimleta kwenye Taqwa inakua Roho mbili zimependana kwa ajili ya Mwenye enzi Mungu.

"إِنَّهُ ۥ مِن سُلَيۡمَـٰنَ وَإِنَّهُ ۥ بِسۡمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحۡمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ "
"Imetoka kwa Suleiman a.s, nayo ni kwa jina la Mwenye enzi Mungu mwingi wa Rehma Mwenye Kurehemu"
Na hii imetoka kwangu, na Barua yoyote ikianza kwa Jina la Mollah wako inakua Tukufu, na ndani ya Utukufu huo ndio unazikuta hizo Wingi wa Rehma na Wingi wa Kurehemu, akiikamata Barua hii Tukufu yoyote yule ikiwa mja mwenye Fahamu basi pale pale Rehema zinaanza kumshukia na anakua Mwenye Kurehemewa, na kama akipuuza basi ujue huyo kesha, huyo kamalizika subiri muda mdogo utaona yepi yatakayo mfika, lakini na wewe usiwache kumuombea dua.

" أَلَّا تَعۡلُواْ عَلَىَّ وَأۡتُونِى مُسۡلِمِينَ"
"Wala msinifanyie Jeuri, na fikeni(Njooni)kwangu na hali ya kuwa mumekwisha kusilimu"
Wala usiifanyie mzaha Barua yangu hii, Ikiwa Mtume Suleiman a.s kamuandikia mtu aliyekua anasujudia Jua kumwita arejee kwa Mollah wake, vipi mimi leo nitakua mkosa kukwita wewe kwenye njia ya kheri, wewe ni Muislam huna haja ya kunijia, ila unachotakiwa uzinduke kutoka usingizini, ibadilishe nafsi yako, kamata Barua hii enyi vipenzi vyangu, isomeni kwa shauku, inatosha hayo mlotenda, sasa Rejeeni kwa Mollah wenu mtamkuta mwenye kusubiri na Mwenye kusamehe, Nakala ifike kwako enyi wanangu, kwako wewe mshirika wangu, pamoja na nyote mlo karibu na mimi kwa mahusiano ya Udugu, napenda pia kuwafikishia  wote ndugu zangu katika Uislam.