Sunday, July 27, 2014

SALAMU ZANGU ZA EID (FITR)

Asalaam Aleiykum

Shukurani zote anastahiki Mollah Mlezi wetu aliyetuwezesha kufunga na kuumaliza Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa Afya na Salama, Tarajio langu kila mmoja wetu anatoka katika kifungo hichi cha kheri kajaa mapenzi na huku akiwa na nia ya kuendelea kuenzi yale yalomfanya aweze kumtii Mollah wake kwa Mwezi Mzima, kama nilivosema katika mafundisho mengi ya huko nyuma kuwa Ramadhan inaleta (Awareness)unakua Dhahir(Alert)Mwezi mzima husahau  ukenda ukanywa maji mchana au kula chakula, basi kwa hali hiyo unapata utiifu katika mambo mengi ya kumtii Allah, kwa hiyo kinacho patikana katika Ramadhan ukaweza kukiendeleza ina maana wewe ushamshinda (Shetani) Fanya jitihada hali hiyo hiyo ulokua nayo katika Ramadhan uiendeleze kwenye miezi ya kawaida, ukiweza kufanya hivyo, wewe utakua Mcha Mungu hakuna ujanja mwengine wowote.
Ila kinachotokea ni Dhana yetu Ramadhan imekwisha na wewe unarejea kwenye usingizi wa Madhanbi, nakuomba bakia macho upate kupendwa na Mollah wako, upate kurehemewa, upate kuwa na afya katika mwili wako, Ramadhan imemaliza kazi yake, sasa unatakiwa wewe Mwenyewe uendelee na hayo matendo ya Ibada.
Vipi utakua (Alert) kuna hali mbili zinatokezea katika siku ya (Eid) Moja ya Kusheherekea na ya pili ni ya Kufurahia, Sherehe zinatokana na ushindi, zinatokana na mwisho wa jambo au mwanzo wake, lakini furaha ni ya kuendelea haina mwanzo haina mwisho, kumbuka wewe unaishi ndani ya Furaha kwa hiyo wewe huna haja ya kusheherekea siku hii ila wewe Furahia Ramadhan imekwisha lakini Taqwa inaendelea, ukiweza kufanya hivyo wewe utakua tafauti na wale wenye kusheherekea, utajihisi wale wamerudi kulala baada ya Ramadhan na wewe bado uko macho, hata ukiwa katikati ya sherehe zao wewe unamtaja Mollah wako, na ukiweza kulifanya hilo utakua unazungukwa na Malaika kwa jambo hilo na ukiweza kudumu nalo utakua unapata ishara ya mzunguko huo wa viumbe wema juu yako, na ukiligundua hilo utakwenda (Beyond)furaha nako ni kupata kitu kinachoitwa (Bliss)sasa itafute maana ya hiyo (Bliss)ukionja japo kidogo ndio utagundua Raha ya maisha.
Umepata kuingia kwenye Ibada jitahidi usitoke usiwache yale ulojifunza, yaendeleze ili upate furaha katika Dunia hii na huko Akhera uendako, Na mimi nakuambia hakuna Furaha kama kuwa Mcha Mungu, Ucha Mungu maana yake umerejea nyumbani ukiwa hai, nini Habari yako wewe siku utakapokuja kuchukuliwa na Malaika kurejea nyumbani milele? kwa hiyo sisitizo langu bakia katika Kumcha Mungu ukiwa sasa ushajua (Faida) na tafauti ya kufanya Ibada, kumbuka kabla ya Ramadhan ulikuaje, Na katika Ramadhan umeishi vipi, Na kesho siku Ya (Eid) unakwenda kuishi vipi, ukikumbuka vitatu hivyo Mwenyewe ndio utakua muamuzi unataka uishi vipi.
Namuomba Mollah wetu atudumishe kwenye Ibada, Atupe Radhi zake zenye mapenzi ili tudumu katika kumkumbuka yeye daima, atukinge na mitihani ya Dunia na Akhera, Na ikiwa kuna Maradhi ya siri ambayo bado hatujayagundua basi atuponeshe kwa uweza wake, na yale alotupangia yatufike basi atutume kwa tahfif Mollah wetu, Mollah wetu wasamehe walo wetu na waislam na viumbe wako kwa jumla uwape salama itokeayo kwenye Rehma zako, Na walofika mbele ya haki Mollah wetu wape Msamaha wako uwaepushe na adhabu zako uwatie katika pepo yako. Amin

Sunday, July 20, 2014

DUA YA TOBA PART 1

Asalaam Aleiykum

Hakuna kitu ambacho Mwanaadamu anakua karibu na Mollah wake kama wakati wa kuomba Dua, Maisha yako yote yamezungukwa na Dua Tupu, na hata hiyo Sala yenyewe ni Dua. Na Jambo la Dua lina seheme mbili, Ya kwanza ni ile ulopangiwa kutoka kwenye Quraan na tulofundishwa na Bwana Mtume s.a.w, Na aina ya Pili ya Dua ni ile yako mwenyewe(Binafsi) Lazima Mja ufanye jitihada ili upate ukuruba wa kuwasiliana na Mollah wako, ufanye Ikhlas na ukweli mtupu katika maombi yako, ukileta (Carbon copy) ya Dua unakua hupati faida yoyote, unachoambulia Aamin tupu, faida anapata Sheikh na makanzu yake, sababu yeye ndio anotoa moyoni, zengine anajiombea yeye wewe unaitikia Amin sababu hujui kiarabu, na hata ukijua kiarabu unakijua kukisoma lakini hujui maana, kwenye kuomba pesa unaomba upewe elimu, kwenye kuomba pepo wewe unajiombea Moto hivi ndivo inavokua, unachukua dua za zamani kujiombea mambo mepya, unasahau kuwa Mollah wako ndio aloumba hiyo Lugha unayoongea, kwa Lugha yoyote utakayoomba yeye anakusikia na atakujibu maombi yako, huna haja tena kuomba pesa ukasoma sura ya Zil zal. Dua ni wewe na Mollah wako basi chagua kwa uzuri maneno ya kwenda kuzungumza na Mollah wako ili akuridhie ili na wewe upate kusamehewa, isipokua ile Dua ya pamoja hiyo huna haja ya kupeleka maneno yako acha msomaji akupelekee na wewe itikia Amin.
Kwa hiyo hapa nakupa mfano wa vipi utajitupa kwa Mollah yako na maneno ya unyenyekevu mpaka Malaika wajiunge na wewe kuitikia Amin.
"Ewe Mollah wangu natanguliza kwa shukurani za kuweza kunijaalia mimi mpaka leo niko Hai nikaweza kupata Muongozo huu wa kusogea kwako nikiwa na matumaini ya kupata Radhi zako ili unisamehe makosa yangu makubwa na madogo, Nilokutendea wewe Mollah wangu pamoja na viumbe wenzangu".
"Ewe Mollah Wangu hakika Wewe ni Shahid wa yote niloyatenda kwenye Umri wangu, Na mimi sasa nimefika mahali sina mategemeo yoyote ya kupata Shufaai isipokua itokayo  kwenye Dhati ya Uwezo wako, Na kama ukiniacha katika hali hii nilo nayo, basi Mollah wangu mimi sina matumaini ya kuweza kuepuka Adhabu zako, Na mimi Mollah wangu sina kifua cha kuchukua adhabu zako zenye mchungu yasioelezeka, kutokana na khofu nilokua nayo, Na ukomo nilofikia kuwa siwezi kuyatengeneza yale niloyaharibu,basi sina la kufanya ila kukuomba Rehma yako ya kusamehewa inishukie Mja wako mimi kabla ya kukabiliwa na Mauti yangu".
"Ewe Mollah wangu ulonijaalia Kuwa, ikisha Nikawa, Nakushukuru kwa Rehma hii ya Uhai, Ila nina huzuni kwenye moyo wangu ya kujua sijawa kama ulivoniamrisha niwe, Na sasa naona kila siku zikizidi Mitihani inaongezeka, Na wasi wasi wangu mimi majawabu yalo mazuri yanazidi kupungua, Basi Ewe Mollah wangu Mie Kiumbe chako Nimetenda mengi ya kukukera Wewe Mollah wangu pamoja na Viumbe Wenzangu, na kwa hilo mimi sina shaka nalo, pia mimi nimedhulumu nafsi yangu pamoja na za Wanaadamu wenzangu basi nakuomba Mollah wangu Nipe mimi zawadi ya kunisamehe kama vile ulivonipa zawadi ya Uhai".
Endelea part 2

DUA YA TOBA PART 2

Asalaam Aleiykum

"Ewe Mollah wangu" Wewe ni Mwenye kunijua udhaifu wangu, Wewe unayajua niloyafanya kwa Dhahir na Siri mengine nayakumbuka na mengine nimeyasahau, na wakati nikiyatenda Mollah wangu ulikua ukinistiri, lakini nina hakika yamehifadhiwa katika kitabu chako kisichofutika jambo lolote, Na mimi sasa nina khofu siku hiyo nitakaposomewa mambo yangu na yakaonekana hakika yalo mabaya yamezidi kiwango, na siku hiyo sina hukumu inayonikabili isipokua kuingia katika "Gereza" La Jahannam na kukabiliwa na adhabu yako ya Moto, ntakua na hali gani wakati "Joshi"la vuke la moto linaniziba pumzi.
"Ewe Mollah wangu" mimi sina subira kwenye machungu ya Jino linaponiuma seuze huo moto wako utakaponiunguza ikawa ngozi inakabili hasira za moto huo nitakua na hali gani Mollah wangu bila ya msamaha wako.
"Ewe Mollah wangu" Wewe ndie ulienionesha mimi katika kitabu chako kitukufu mfano wa kusamehe na ukawasamehe Mitume yako kwa makosa walokutendea, "Ewe Mollah wangu" Wewe ndie uliyempa Nabii Adam a.s muongozo wa maneno ya hekima ili kuweza kuomba msamaha utokao kwako alipopinga amri yako, na ukamjaalia moyo wa majuto ulojaa khofu na unyenyekevu, Basi na mimi Mollah wangu nimezipinga nyingi katika amri zako kubwa na ndogo na sasa umeniletea fahamu kuyajua makosa yangu nakuomba Yaa Raab nisamehe makosa yangu uniridhie kiumbe chako na uyakubali majuto yangu ya kweli, "Ewe Mollah wangu ikiwa Nabii Adam a.s kaamrishwa atoke peponi kwa kupinga amri zako, nini hali yangu mimi nisofikia hata chembe ya waja wema, kwa hilo Mollah wangu nahitaji msamaha wako, Nahitaji unijaalie  moyo wa kukuogopa na kukupenda wewe pekee Mollah wangu, Na wala usinipe mie mbadala wa mapenzi hayo nikawa napenda kitu chengine.
"Ewe Mollah wangu" hakika wewe ndie uliyemsamehe Nabii Musa a.s pale kwa bahati mbaya alipomuua mtu na ikisha ukamsamehe, Na mimi Mollah wangu pengine nimedhulumu nafsi nikiwa labda kiongozi, au kwenye madaraka yoyote au kwenye chombo chochote nikasababisha kiumbe chako kupoteza maisha yake, Mollah wangu najua labda nimeshiriki kwa njia moja ama nyengine nikiwa kwenye kundi au chama kudhulumu viumbe vyengine kwa kupoteza maisha yao au kuwakatili furaha za Roho zao,basi nanyenyekea Mollah wangu kuomba Toba itokayo kwako, nisamehe Mollah wangu.
"Ewe Mollah wangu" Ewe Mollah wangu Nabii wako Daud a.s alifanya kosa la kumpeleka Jeneral wake vitani kwa kutaraji akifa amuoe mkewe, Mollah wangu ukampelekea Malaika wawili walopindukia ukuta na kisa cha kondoo 99, alipogundua Nabii Daud kafanya makosa alianguka na kusujudu kuomba msamaha, na Wewe Mollah wangu ukamsamehe, Mollah wangu na mimi kiumbe chako nimefanya hayo na zaidi ya hayo, na sasa Mollah wangu najitahidi na mimi kusujudu nikitaraji na Msamaha utokao kwako Weye Mlezi wangu nakuomba unisamehe.
Endelea part 3

DUA YA TOBA PART 3

Asalaam Aleiykum

"Ewe Mollah wangu" Nabii Yunus a.s aliyakimbia majukumu yake ukamtia kwenye Tumbo la Chewa kwa siku tatu tu, akawa anaita na kuomba atolewe, akakubali makosa yake na ukamsamehe na kumtoa kwenye tumbo la Chewa, Nini habari yangu mie ambaye nakwenda kukaa kwenye tumbo la Ardhi mpaka siku ya Kiyama, Mollah wangu na mie kiumbe chako nimeyapuuza majukumu yangu mengi uliyonipa, nimeshindwa mimi hata kuitizama Familia yangu na kuwahimiza wakutii Wewe Mollah wangu, Marafiki wangu wanatenda maasi namie nimo kuwapigia makofi, Nashindwa hata kuhimiza kizazi changu kukuabudu Wewe Mollah wangu, itakuaje hali yangu mimi nitakapokamilisha Umuri wa kuishi hapa ulimwenguni, Mollah wangu mimi siziwezi adhabu zako, Nauomba msamaha wako, nisamehe kiumbe chako, niepushe mimi na Moto wa jahannam na adhabu zengine ulizowaandalia wafanyao maovu wasokuogopa Wewe Muumba wa kila kitu.
"Ewe Mollah wangu" Wewe ndiye uliyemnyanganya Nabii Suleiman a.s Ufalme kwa ajili ya kukusahau Wewe mara moja tu, ikisha akaomba Toba na Wewe ukamsamehe, Basi nina hali gani mie nisie kukumbuka kabisa, Yaa Raab mimi nimeshughulika kutafuta cheo na Utajiri kwa waganga na majini, nakushirikisha Wewe katika Shirk kubwa kabisa, Basi Sasa nakuomba Mollah wangu nisamehe usinijaalie tena kurejea makosa hayo makubwa, Nakuomba Mollah wangu niridhie niipate Toba itokayo kwako, nipe mimi Faraja ya kusamehewa na Wewe na uniepushe na Adhabu za siku ya kufa, adhabu za kaburi, adhabu za siku ya kufufuliwa, adhabu za siku ya hukumu, niepushe na adhabu za Ulimwengu huu na Adhabu za Akhera, Nijaalie afya unishushie mapenzi ya kukuabudu wewe kila saa na dakika, Mollah wangu wasamehe Wasilam wenzangu na viumbe wako kwa jumla walo hai na walotangulia mbele ya haki. AAMIN.

Sunday, July 13, 2014

BARAKA TANO ZA RAMADHAN PART 1

Asalaam Aleiykum

Mwezi wa Ramadhan ni mwezi wenye kuja na zawadi nyingi sana ambazo hazina idadi maalum, Miongoni mwa zawadi hizo zimo hizi za Baraka tano ambazo wanapewa Umma huu wa Kiislam (Special) kwa sababu moja tu nayo ni ile kuitikia kwa pamoja wito wa Mwenye enzi Mungu na kukubali kufunga mwezi huu wa Ramadhan, Basi kwa ajili hiyo mnapewa na kuongezewa Baraka hizi Tano ambazo ukizipata Mja unakua umeshafanikiwa mafanikio makubwa katika uhai wako na mauti yako.
Napenda uelewe Baraka ziko chungu nzima, lakini hizi tano ni (Special)kwa ajili yenu Mlofunga. Nini Baraka?
Baraka ni ngumu kufasirika kilugha ya kawaida, lakini midamu tuko katika Darsa ya kuichambua Baraka basi itabidi nijitahidi kuileza ili tupate kuifahamu, lakini elewa hata sifiki karibu na kuifasiri Baraka, kwa sababu baraka haina tafsiri, naweza kuileza baraka kwa neno moja tu nikaita Baraka ni Furaha kwa anaeijua, Na ama kwa yule asiyeijua kwake yeye Baraka ni kitendo, vitu viwili tafauti huyu kwake ni furaha na yule kwake ni kitendo, ndio maana yule asiyejua husema (I'm counting my blessing).
Huyu yeye tayari akipata Mali anasema kabarikiwa, ndio sawa, wala sio kosa, lakini huyu anakua kabakia kwenye kitendo na anasahau maana yenyewe ya Baraka, na kuakiangalia kitendo ni sehemu ya chini kabisa na yenye mtihani mkubwa.
Lakini mwenye kujua yeye akipewa Furaha tu anajua kapewa Baraka kubwa kabisa, kwani unaweza kupewa hiyo Mali (Utajiri)ukanyimwa Baraka za Furaha, kwa hiyo ndio maana nikasema Baraka ni Furaha, bila ya furaha huo ni mtihani wa Baraka, sasa vipi ikawa Furaha jitizame wewe ukipewa Watoto unafurahi (Hiyo Baraka) Ukipewa Afya unafurahi, angalia unakuwaje yakikufika maradhi, mambo yote yanomalizikia kwenye furaha jua hiyo ni (Baraka). Sasa kama ushalijua hilo Mwenye enzi Mungu mwenye kutoa hizo Baraka kwa viumbe vyake kawashushia ndaniya mwezi huu Tano rasmi kwa wale wenye kufunga kweli, na pia napenda uelewe Baraka huwezi kuilazimisha, unachoweza kufanya usubiri ikushukie ndio tunajikuta katika mwezi huu wa Ramadhan Baraka zinamiminika.
Baraka ya Mwanzo(1) "Anasema Bwana Mtume s.a.w" Umma wangu umepewa Mambo matano hawajapata kupewa Umma zengine kabla ya hapo, Jambo la mwanzo ikiwa utatia nia kwa mapenzi ya kufunga Ramadhan kwa ajili ya Mollah wako, ukanuia  kuwa utaifanyia ihsan funga yako iwe ya haki na Iman ya kweli, "Basi Mwenye enzi Mungu ule usiku wa mwanzo wa Ramadhan anakuangalia na mwenye kuangaliwa na Mollah wake basi haitomfika adhabu, (Hayatomkuta mateso) .
Endelea part 2

BARAKA TANO ZA RAMADHAN PART 2

Asalaam Aleiykum,

wengine wakisikia kuangaliwa wanaanza kuleta ishara zao za maajabu, labda jicho kubwa linangara, au hivi na vile wanaleta mifano ya ajabu ajabu, Mollah wako hana haja hata ya kukuangalia yeye ni mwenye kujua na anaelewa kuwa Mja wake kaingia katika bahari ya kujulikana, Na ile dhamira au (Nia) uliyoiweka ndio inakufanya uchukuliwe dhamana ya kutokupewa adhabu yoyote, ni kwa ajili ya Nia tu na wala si jengine, Na hata ukifa usiku huo basi wewe ushasamehewa Dhanmbi zako, Na Mja ukijua umesamehewa Dhanmbi zako furaha iliyoje kwako wewe Kiumbe.
Baraka ya Pili (2)"Kila siku katika Mwezi huu Malaika wanawaombea Msamaha walofunga" Wenye Akili za ubishi wanaweza kuuliza mbona mambo yanajichanganya, huku hutoadhibiwa, hapa unaombewa msamaha inakuaje, Inatakiwa ujijue katika Maumbile yake wewe Binaadamu una (Past) na (Future) ambayo ukiambiwa huadhibiwi kwa yale yalopita, lakini haya yajayo ambayo unaendelea kuyatenda ndani ya Mwezi wa Ramadhan Mamia ya madhanbi, basi haya ndio hao Malaika wamewekwa kazi yao kukuombea Maghfira, Na kwa hilo basi zidi kuingia Furahani kwa kuijua Baraka hii ya kuombewa na Malaika.
Baraka ya Tatu (3) Hakika Mwenye enzi Mungu anaiamrisha Pepo na kuiambia," Ewe Pepo Mpambie Mja wangu mwenye kufunga aje kustarehe kwa zile taabu alozipata kwenye dunia ili apate yalo mazuri yaliyopo kwenye Nyumba ya peponi".
Asije kushangaa Mtu akaona mbona inasemezwa Pepo, kwani Pepo ni yenye kufahamu, Naam kila kilichoumbwa na Mollah kina (Degree of Consciousness).
Baraka ya Nne (4) Na harufu zao zitokazo vinywani mwao zinakua nzuri kuliko hata hiyo Misk(Manukato)
Na Baraka ya tano (5) Na kila ufikapo mwisho wa usiku  Mwenye enzi Mungu husamehe wote walofunga, na vile vitendo vyao walivyotenda, vitawafaa katika malipo ya ujira wao.
Hizo ndio Baraka tano zilizomo kwenye mwezi huu unazitaka zifanyie kazi, ondosha uvivu wa Ibada upate yalo mema, jitahidi kufunga uwe karibu na Mollah wako.

Sunday, July 6, 2014

MTI WA IBADA PART 1

Asalaam Aleiykum

Unaijua tafauti ya watu wa Ulaya na Africa katika kupanda Mti? Ni ile ya Watu wa Ulaya kuupanda Mti kwa kutumia Ngazi na kuvaa makofia ya kuwakinga na Ajali, Lakini Africa wao wanaupanda bila ya kutumia chochote, hawaogopi hata Ajali, wakivunjika mguu kwao sawa, hata wakifa pia kwao sawa, sasa kwanini ikawa hivyo kwa sababu bado wanaishi kwa Imani iwe yoyote ile lakini (Still) wana Imani fulani inayowafanya hawataki (Gurantee) hawataki(Insurance) na kwa Imani yangu mie nahisi hivyo ndivyo unavotakiwa kupandwa mti, lazima uhisi umekuchuna mapaja, umekukwaruza kwaruza damu zinakutoka, halafu ukisha uzoea mti unakua rafiki yako, hata Tawi likitaka kukatika linakupa taaria mapema, na hivyo ndio ulivo Mti wa Ibada lazima upate tabu, lazima uhangaike, uamke Alfajiri, ufunge Ramadhan ukumbatie mayatima, utumie kilicho chako kwa kukitoa buree umemkuta mtu kakaa unampa, na huku huna (Gurantee)kama ukifika kileleni utachuma matunda au itatokea nini? lakini ukianza kuvaa makofia na ukaweka ngazi ina maana unataka uhakika usianguke na hivi na vile.
Elewa Ulimwengu huu umeumbwa na Athari za Ajali, wewe mwenyewe huna (Gurantee) unaweza kuwa umeficha maradhi, unaweza kufa wakati wowote, Ndio maana unatakiwa ufanye juhudi ya kuupanda Mti huu wa Ibada, Na huu ndio wakati mzuri wakuuzungumza Mti huu wakati umo katika tawi moja wapo la kufunga mwezi wa Ramadhan.
Mti wa Ibada Ukoje?
Mti wa Ibada ni mkubwa sana na hauna kikomo kwa urefu wala mapana, Sababu Mti huu una matawi mengi na matunda mengi, Na hapo ndio unatizamwa mpandaji unataka kupanda kufikia Tawi gani, jee una (Stamina) ya kuupanda Mti huu. (Stamina) utaipata wapi wakati unaogopa kupanda Mti huu wa Ibada, unataka uwekewe ngazi iwe ushafika Juu bila ya tabu yoyote, na huku  unauliza mti wenyewe unaitwaje, na sisi kila ukituuliza tunakwambia Mti wenyewe ni unaitwa (Mdini) Dini, usije ukadhani nimesema (Mdimu).
Na cha kusikitisha zaidi wengine wanaukimbia Mti huu hata kwenye mwezi wa Ramadhan, tumo ndani ya Uislam na kanzu zetu nyeupe, na saum zetu tunajidai zinapanda, vipi saum hizo zitapanda wakati tunasutwa, tunaambiwa kwenye sura ya (Maun)
أَرَءَيۡتَ ٱلَّذِى يُكَذِّبُ بِٱلدِّينِ 
Je Umemuona yule anayekadhibisha Dini.
Aya imesema vizuri sana, kwani ingesema unamjua ungekua ubishi mkubwa, utajuaje kama mtu anatoa au hatoi, ana amini au haamini kama akhera ipo? ndio ikasemwa umemuona, kwa sababu unasali nae, pengine jirani yako, mnakwenda darsa pamoja, kila siku mnaona, wewe unamuangalia na yeye anakuangalia, nini kinatokea katika hicho unacho kiona.
 فَذَٲلِكَ ٱلَّذِى يَدُعُّ ٱلۡيَتِيمَ 
Huyo ni yule anomsukuma yatima.
Vipi anamsukuma yatima? kukisukuma kitu lazima uwe karibu nacho, mayatima wapo mitaani tunaishi nao, maana yakua yatima wako chini ya uwezo hawana wazazi, zaidi ya hilo wewe mwenye uwezo unawasukuma kwa kuwaacha usiwasaidie, wanakukera kwa hiyo unaamua kuwasukuma shimoni wazidi kuteseka kwa dhiki na madhila ya Roho, kwa sababu wanawaona watoto wako mara wana baskeli, mara wana gari, mara wana suruali mpya mara wanakula (Ice Cream)huko ndiko kuisukuma Roho ya Yatima
Endelea part 2

MTI WA IBADA PART 2

Asalaam Aleiykum

mambo yanaendelea kutajwa katika kuupanda mti wa Ibada kama?
 وَلَا يَحُضُّ عَلَىٰ طَعَامِ ٱلۡمِسۡكِينِ 
Wala hajihimizi kuwalisha Maskini (Sio yeye wala kuwahimiza wenzie) hakuna faida inayopatikana kwa urahisi kama ukawa na uwezo ikisha ukailisha Roho ya Maskini, lau ungekua unajua fadhila zake basi ungewatafuta maskini kwa magoti ili upate kuwalisha na kula nao.
فَوَيۡلٌ۬ لِّلۡمُصَلِّينَ
Basi adhabu itawapata wanosali.
vipi itawapata adhabu wakati wao wanasali, kwa sababu sala zao ni bure, ndani ya moyo hakuna kitu, amri za kuifanya hiyo sala wanaipinga, vipi uvae kanzu, usujudu, ufunge halafu uwache viumbe wenzio wateseke, nani anakutaka kwenye mti wa Ibada, hufai hata kukamata tawi.
ٱلَّذِينَ هُمۡ عَن صَلَاتِہِمۡ سَاهُونَ 
Ambao wanapuuza Sala zao.
hufati maamrisho, Sala haitokei katika moyo wako, huna huruma huna mapenzi, unafata kundi, lakini mwenyewe umefungika ndani na chuki ubaghili na kila kasoro, nini unacho fanya?
ٱلَّذِينَ هُمۡ يُرَآءُونَ 
Ambao hufanya riyaa.
maonesho matupu, vipi utakwenda kusali Tarawih wakati unajua fika Jirani yako hajafuturu, una hakika mayatima nyumba ya tatu hawana chakula wala nguo za sikukuu.
وَيَمۡنَعُونَ ٱلۡمَاعُونَ 
Nao hunyima misaada.
hata watu wakikujia na shida hutoi kitu unasema wamezoea, kama nani anazoea shida, shida haizoeleki kabisa.Sasa jikumbushe maskini wangapi umewapita, vipi utaweza kupanda Mti wa Ibada, mzizi unakushinda halafu unafikiri kufikia kileleni, na huko kileleni ndio kwenye hiyo Taqwa, basi kama hujui vipi unaweza  kuupanda Mti huu wacha tukujulishe mengine zaidi yanoweza kukupandisha Mti huu.
Sasa umefika wakati wa kutoa yale alokupa Mollah wako(Pay Back) "Na kwa yale tunowaruzuku wanayatoa" Sasa unatakiwa kuanza kupanda Mti huu kwa Kusali sana, Kumsabahi Mollah wako kwa wingi, wasaidie wasojiweza, kawasafishie majumba yao wazee, nenda kacheze na mayatima, si unasema huna uwezo basi tumia nguvu zako, nazo umeruzukiwa , basi zitumie  ili zikudondoshee matunda kwenye mti huu wa Ibada, una ndugu zako wengine wagonjwa ikiwa utakwenda kuwatizama tu watafurahi na wakifurahi matunda yanakuangukia kwako wewe, na unakua umeshafanya Ibada, una nguo za zamani umeziweka huna haja nazo basi zitoe upesi, upande Mti huu kwa kutoa, namie leo nakwambia siri ya kutoa ni kuongezewa, hakuna yoyote mwenye kutoa akafilisika, sababu Ulimwengu huu ukiuchunguza daima Mollah wako ni mwenye kutoa vipi leo wewe uwe na hofu ya kutoa, kama vile Ulimwengu utafilisika, umepewa toa, na ukifilisika basi Mollah wako anajua umefilisika kwa ajili yake na atakutengea matunda yasiyo kwisha kwenye Mti wa Ibada.
Kufanya Suluhu na Mtu mlogombana nayo pia ni Ibada, nenda katake usuluhisho akikufukuza wewe utakua umeshatenda Ibada, vipi ikawa Ibada? sababu hiyo ni Amri ya Mwenye enzi Mungu imo ndani ya Quraan, na wewe utakua ushaitekeleza, jitolee nguvu zako na Akili, wewe si mwalimu wasomeshe watoto wa kimaskini na yatima bure, utumie ujuzi wako kwa kuwanufaisha Watu.
Huna vyote hivyo basi jitolee hata Damu, hata hiyo pia huna mwilini? kumbuka kila kitu kinalipwa katika Mti huu wa Ibada, na usifanye mambo hayo yote ukasubiri matunda yaanze kuanguka moja kwa moja, wacha yawive, bakia unategemea unaweza kuyala ukiwa hai au umekufa hakudhulumu mtu kabisa.
Hata kuufanyia Ihsan huo Mwili wako pia hiyo Ibada, ukawa hujiangamizi kwa Ulevi wa aina yoyote, hujitii maradhi kwa kushiriki uzinifu(Kwa sababu kama hupigwi makwaju thamanini na viumbe wenzio, Mollah wako anakupiga mkwaju wake, unajikuta una maradhi, unafilisika, huna Raha Nk)acha kujichubua uso kwa (Powder)za (Chemical) wewe mzuri hivyo hivyo alivokuumba Mollah wako na wala hajakosea, Mshukuru kwa kusema shetani ananidanganya kwa kuninongoneza eti mimi mbaya, basi mie nashukuru kwa huu ubaya wangu nikiwa na Imani wewe Mollah wangu unanijua mimi mzuri, na kuanzia leo sina haja ya kuvaa mawigi wala kutia (Kal Kit).
Na hizo Nguvu alizokupa Mollah wako ni kwa ajili ya Ibada, basi mpaka hiyo kazi uifanyayo pia ni Ibada, Mollah kakupa majukumu ili uupande Mti wa Ibada, Kakupa watoto ufanye kazi kuwatizama, kakuwekea wazee wako washakua watu wazima dhamana wewe ili upate matunda ya Ibada, jitizame wewe unafanya nini?.
Huwakuti watu ila ni wenye kukataa kazi kwa viburi na kugeuka (Mission in Town)unamfanyia Mollah wako alokuumba ujanja, unaishi kwa mali za haramu, unageuka bosi wa mitaani,kazi hutaki maguvu unayo ukiulizwa nguvu hizo unazifanyia nini eti wewe dalali? sio tu hutaki kazi bali wewe hutaki kuupanda Mti wa Ibada ulioko mbele yako, namalizia kwa kukwambia kila kitu chako ni Ibada kichunguze ukione vipi kimezungukwa na Mti huu wa Ibada, Na ukisha ugundua upande Mti kwa haraka kwani kileleni kuna Furaha isiyoelezeka, kuna maajabu yasiyomalizika, lakini huwezi kuyaona ukiwa chini mpaka upande juu, ndio maana hata haya maisha unapozaliwa unakua mdogo, mfupi halafu unaanza kukua na kurefuka mpaka unaiona raha ya maisha, na Mti wa Ibada una mifano hiyo hiyo lakini mpaka ufike juu ndio utaijua, na hakuna wakati mzuri wa kujizoesha kuupanda Mti huu kama wakati huu wa Ramadhani.