Asalaam Aleiykum
mambo yanaendelea kutajwa katika kuupanda mti wa Ibada kama?
وَلَا يَحُضُّ عَلَىٰ طَعَامِ ٱلۡمِسۡكِينِ
Wala hajihimizi kuwalisha Maskini (Sio yeye wala kuwahimiza wenzie) hakuna faida inayopatikana kwa urahisi kama ukawa na uwezo ikisha ukailisha Roho ya Maskini, lau ungekua unajua fadhila zake basi ungewatafuta maskini kwa magoti ili upate kuwalisha na kula nao.
فَوَيۡلٌ۬ لِّلۡمُصَلِّينَ
Basi adhabu itawapata wanosali.
vipi itawapata adhabu wakati wao wanasali, kwa sababu sala zao ni bure, ndani ya moyo hakuna kitu, amri za kuifanya hiyo sala wanaipinga, vipi uvae kanzu, usujudu, ufunge halafu uwache viumbe wenzio wateseke, nani anakutaka kwenye mti wa Ibada, hufai hata kukamata tawi.
ٱلَّذِينَ هُمۡ عَن صَلَاتِہِمۡ سَاهُونَ
Ambao wanapuuza Sala zao.
hufati maamrisho, Sala haitokei katika moyo wako, huna huruma huna mapenzi, unafata kundi, lakini mwenyewe umefungika ndani na chuki ubaghili na kila kasoro, nini unacho fanya?
ٱلَّذِينَ هُمۡ يُرَآءُونَ
Ambao hufanya riyaa.
maonesho matupu, vipi utakwenda kusali Tarawih wakati unajua fika Jirani yako hajafuturu, una hakika mayatima nyumba ya tatu hawana chakula wala nguo za sikukuu.
وَيَمۡنَعُونَ ٱلۡمَاعُونَ
Nao hunyima misaada.
hata watu wakikujia na shida hutoi kitu unasema wamezoea, kama nani anazoea shida, shida haizoeleki kabisa.Sasa jikumbushe maskini wangapi umewapita, vipi utaweza kupanda Mti wa Ibada, mzizi unakushinda halafu unafikiri kufikia kileleni, na huko kileleni ndio kwenye hiyo Taqwa, basi kama hujui vipi unaweza kuupanda Mti huu wacha tukujulishe mengine zaidi yanoweza kukupandisha Mti huu.
Sasa umefika wakati wa kutoa yale alokupa Mollah wako(Pay Back) "Na kwa yale tunowaruzuku wanayatoa" Sasa unatakiwa kuanza kupanda Mti huu kwa Kusali sana, Kumsabahi Mollah wako kwa wingi, wasaidie wasojiweza, kawasafishie majumba yao wazee, nenda kacheze na mayatima, si unasema huna uwezo basi tumia nguvu zako, nazo umeruzukiwa , basi zitumie ili zikudondoshee matunda kwenye mti huu wa Ibada, una ndugu zako wengine wagonjwa ikiwa utakwenda kuwatizama tu watafurahi na wakifurahi matunda yanakuangukia kwako wewe, na unakua umeshafanya Ibada, una nguo za zamani umeziweka huna haja nazo basi zitoe upesi, upande Mti huu kwa kutoa, namie leo nakwambia siri ya kutoa ni kuongezewa, hakuna yoyote mwenye kutoa akafilisika, sababu Ulimwengu huu ukiuchunguza daima Mollah wako ni mwenye kutoa vipi leo wewe uwe na hofu ya kutoa, kama vile Ulimwengu utafilisika, umepewa toa, na ukifilisika basi Mollah wako anajua umefilisika kwa ajili yake na atakutengea matunda yasiyo kwisha kwenye Mti wa Ibada.
Kufanya Suluhu na Mtu mlogombana nayo pia ni Ibada, nenda katake usuluhisho akikufukuza wewe utakua umeshatenda Ibada, vipi ikawa Ibada? sababu hiyo ni Amri ya Mwenye enzi Mungu imo ndani ya Quraan, na wewe utakua ushaitekeleza, jitolee nguvu zako na Akili, wewe si mwalimu wasomeshe watoto wa kimaskini na yatima bure, utumie ujuzi wako kwa kuwanufaisha Watu.
Huna vyote hivyo basi jitolee hata Damu, hata hiyo pia huna mwilini? kumbuka kila kitu kinalipwa katika Mti huu wa Ibada, na usifanye mambo hayo yote ukasubiri matunda yaanze kuanguka moja kwa moja, wacha yawive, bakia unategemea unaweza kuyala ukiwa hai au umekufa hakudhulumu mtu kabisa.
Hata kuufanyia Ihsan huo Mwili wako pia hiyo Ibada, ukawa hujiangamizi kwa Ulevi wa aina yoyote, hujitii maradhi kwa kushiriki uzinifu(Kwa sababu kama hupigwi makwaju thamanini na viumbe wenzio, Mollah wako anakupiga mkwaju wake, unajikuta una maradhi, unafilisika, huna Raha Nk)acha kujichubua uso kwa (Powder)za (Chemical) wewe mzuri hivyo hivyo alivokuumba Mollah wako na wala hajakosea, Mshukuru kwa kusema shetani ananidanganya kwa kuninongoneza eti mimi mbaya, basi mie nashukuru kwa huu ubaya wangu nikiwa na Imani wewe Mollah wangu unanijua mimi mzuri, na kuanzia leo sina haja ya kuvaa mawigi wala kutia (Kal Kit).
Na hizo Nguvu alizokupa Mollah wako ni kwa ajili ya Ibada, basi mpaka hiyo kazi uifanyayo pia ni Ibada, Mollah kakupa majukumu ili uupande Mti wa Ibada, Kakupa watoto ufanye kazi kuwatizama, kakuwekea wazee wako washakua watu wazima dhamana wewe ili upate matunda ya Ibada, jitizame wewe unafanya nini?.
Huwakuti watu ila ni wenye kukataa kazi kwa viburi na kugeuka (Mission in Town)unamfanyia Mollah wako alokuumba ujanja, unaishi kwa mali za haramu, unageuka bosi wa mitaani,kazi hutaki maguvu unayo ukiulizwa nguvu hizo unazifanyia nini eti wewe dalali? sio tu hutaki kazi bali wewe hutaki kuupanda Mti wa Ibada ulioko mbele yako, namalizia kwa kukwambia kila kitu chako ni Ibada kichunguze ukione vipi kimezungukwa na Mti huu wa Ibada, Na ukisha ugundua upande Mti kwa haraka kwani kileleni kuna Furaha isiyoelezeka, kuna maajabu yasiyomalizika, lakini huwezi kuyaona ukiwa chini mpaka upande juu, ndio maana hata haya maisha unapozaliwa unakua mdogo, mfupi halafu unaanza kukua na kurefuka mpaka unaiona raha ya maisha, na Mti wa Ibada una mifano hiyo hiyo lakini mpaka ufike juu ndio utaijua, na hakuna wakati mzuri wa kujizoesha kuupanda Mti huu kama wakati huu wa Ramadhani.
No comments:
Post a Comment