Sunday, July 27, 2014

SALAMU ZANGU ZA EID (FITR)

Asalaam Aleiykum

Shukurani zote anastahiki Mollah Mlezi wetu aliyetuwezesha kufunga na kuumaliza Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kwa Afya na Salama, Tarajio langu kila mmoja wetu anatoka katika kifungo hichi cha kheri kajaa mapenzi na huku akiwa na nia ya kuendelea kuenzi yale yalomfanya aweze kumtii Mollah wake kwa Mwezi Mzima, kama nilivosema katika mafundisho mengi ya huko nyuma kuwa Ramadhan inaleta (Awareness)unakua Dhahir(Alert)Mwezi mzima husahau  ukenda ukanywa maji mchana au kula chakula, basi kwa hali hiyo unapata utiifu katika mambo mengi ya kumtii Allah, kwa hiyo kinacho patikana katika Ramadhan ukaweza kukiendeleza ina maana wewe ushamshinda (Shetani) Fanya jitihada hali hiyo hiyo ulokua nayo katika Ramadhan uiendeleze kwenye miezi ya kawaida, ukiweza kufanya hivyo, wewe utakua Mcha Mungu hakuna ujanja mwengine wowote.
Ila kinachotokea ni Dhana yetu Ramadhan imekwisha na wewe unarejea kwenye usingizi wa Madhanbi, nakuomba bakia macho upate kupendwa na Mollah wako, upate kurehemewa, upate kuwa na afya katika mwili wako, Ramadhan imemaliza kazi yake, sasa unatakiwa wewe Mwenyewe uendelee na hayo matendo ya Ibada.
Vipi utakua (Alert) kuna hali mbili zinatokezea katika siku ya (Eid) Moja ya Kusheherekea na ya pili ni ya Kufurahia, Sherehe zinatokana na ushindi, zinatokana na mwisho wa jambo au mwanzo wake, lakini furaha ni ya kuendelea haina mwanzo haina mwisho, kumbuka wewe unaishi ndani ya Furaha kwa hiyo wewe huna haja ya kusheherekea siku hii ila wewe Furahia Ramadhan imekwisha lakini Taqwa inaendelea, ukiweza kufanya hivyo wewe utakua tafauti na wale wenye kusheherekea, utajihisi wale wamerudi kulala baada ya Ramadhan na wewe bado uko macho, hata ukiwa katikati ya sherehe zao wewe unamtaja Mollah wako, na ukiweza kulifanya hilo utakua unazungukwa na Malaika kwa jambo hilo na ukiweza kudumu nalo utakua unapata ishara ya mzunguko huo wa viumbe wema juu yako, na ukiligundua hilo utakwenda (Beyond)furaha nako ni kupata kitu kinachoitwa (Bliss)sasa itafute maana ya hiyo (Bliss)ukionja japo kidogo ndio utagundua Raha ya maisha.
Umepata kuingia kwenye Ibada jitahidi usitoke usiwache yale ulojifunza, yaendeleze ili upate furaha katika Dunia hii na huko Akhera uendako, Na mimi nakuambia hakuna Furaha kama kuwa Mcha Mungu, Ucha Mungu maana yake umerejea nyumbani ukiwa hai, nini Habari yako wewe siku utakapokuja kuchukuliwa na Malaika kurejea nyumbani milele? kwa hiyo sisitizo langu bakia katika Kumcha Mungu ukiwa sasa ushajua (Faida) na tafauti ya kufanya Ibada, kumbuka kabla ya Ramadhan ulikuaje, Na katika Ramadhan umeishi vipi, Na kesho siku Ya (Eid) unakwenda kuishi vipi, ukikumbuka vitatu hivyo Mwenyewe ndio utakua muamuzi unataka uishi vipi.
Namuomba Mollah wetu atudumishe kwenye Ibada, Atupe Radhi zake zenye mapenzi ili tudumu katika kumkumbuka yeye daima, atukinge na mitihani ya Dunia na Akhera, Na ikiwa kuna Maradhi ya siri ambayo bado hatujayagundua basi atuponeshe kwa uweza wake, na yale alotupangia yatufike basi atutume kwa tahfif Mollah wetu, Mollah wetu wasamehe walo wetu na waislam na viumbe wako kwa jumla uwape salama itokeayo kwenye Rehma zako, Na walofika mbele ya haki Mollah wetu wape Msamaha wako uwaepushe na adhabu zako uwatie katika pepo yako. Amin

No comments:

Post a Comment