Wednesday, June 20, 2012

SIRI YA MAUTI (VIPI UNAKUFA)PART 2

Asalaam-Aleikum. Ndugu yangu napenda uelewe wewe una vitu viwili vinavyo kufanya uwe mwanaadamu, kwanza mwili wako ambao huu wakati wa kufa unazikwa na kuoza na kugeuka mchanga, huo ndio mwili unarejea kuwa udongo, halafu unakitu chengine hichi ndio hicho kilotokea huko mbinguni ambacho kinaitwa (Roho)na hichi ndio kinachofanya safari ya kurejea kilopotoka. Lakini kabla ya kurejea kilopotoka hutumwa wajumbe kuja kukitenganisha na huo mwili sasa nini kinatokea wakati Malaika wamehudhuria katika (OPERESHENI)hii kubwa, Jee ushawahi kufikiria vipi itakua Mauti yakikubili, ushajua labda njia ya kufanya kupata nafuu katika tukio hili na nini Quraa'an inatwambia wakati siku hii ikidhiri na wewe upo katika godoro la mauti?."Waqiah:83-85" (٨٢) فَلَوۡلَآ إِذَا بَلَغَتِ ٱلۡحُلۡقُومَ (٨٣) وَأَنتُمۡ حِينَٮِٕذٍ۬ تَنظُرُونَ (٨٤) وَنَحۡنُ أَقۡرَبُ إِلَيۡهِ مِنكُمۡ وَلَـٰكِن لَّ تُبۡصِرُونَ (٨٥ "Basi(inakuaje)pale roho inapofika kwenye koo, Na nyinyi wakati ule(mmemzunguka)mnamtizama,Na sisi tupo karibu naye zaidi lakini si wenye kutuona". Nini hapo kinatokea, hapo ndipo inapotokea ile operesheni kubwa kuliko zote ulimwenguni inayohudhuriwa na (Surgeon Speciality)Malaika wa Mauti,hapo unapata moja katika mawili yalotajwa katia aya ya 89 mpaka 95 katika sura hiyo hiyo ya (Waqiah)zaidi kama ni mja mwema basi unapewa anagalau dawa ya matulizo ili uepuke machungu na maumivu yanotokea hapo ulipolala kwenye godoro la mauti, na mfano mdogo walohadithia yalowakuta huku wanafahamu zao wanaelezea ni kama kuubeba mlima, usiombe ikakukuta hali hii, machungu hayo ndio anayopata yule aloishi katika ulimwengu huu kwa jeuri,au kiburi,mwenye kuwatesa wenzie au mtenda maovu,au alikua fisadi tu katika maisha alioishi na wenzie katika ulimwengu huu. Isije ikakudanganya labda ukaona mtu mwema anakufa kifo cha adhabu anateseka napenda uelewe huo ni mwili, kiroho yuko baridi hana wasiwasi na usije ukaona yule mtenda maovu kafa salama hana wasiwasi basi lau ungekua unaiona roho yake inavotolewa ungepiga kelele wewe mtizamaji, lau ingekua anaweza kuhadithia huyu asi vipi mauti yanamkuta basi hakuna hata mmoja wetu angekubali kutenda makosa tena. Sasa nini hasa kinatokea wakati huo, hakuna alokwenda akarudi na kutuhadithia nini kinatokea, lakini tunajaaliwa kupata hadithi za wale wema na wabaya wanavotoka roho wanapewa nafasi ya kusema yale wanayofanyiwa mpaka kufikia kumalizika kutoka kwa roho zao na kutokana na hadithi zao na sisi tukapata nafasi za kuhadithia ili iwe zingatio kwetu. Wagonjwa wengi husema naona mtu kanisimamia hataki kuondoka, wengine husema naona ngombe wananitizama n.k lakini kuna wengine wanahadithia process nzima tokea anapoanza kukamatwa kidole gumba mpaka roho inapofika kooni. Sasa nini walohadithia kwa ukamilifu wanasema? Jamani hali ya Mauti ni yenye kutisha ambayo haina mfano wake, Na woga unazidi kwa kuwa mwanaadamu hajui anapokwenda au vipi atapokewa, na huna kumbukumbu nini kitachotokea huko uendako, kutokana na hali hiyo mauti yanazidi kuwa magumu hususan ikiwa umeishi katika ulimwengu huu,pengine mzinifu au mla rushwa,hutaki jambo la kusali na mengine mengi ya kifisadi ambayo unayaelewa mwenyewe,unadhulumu wanyonge unatenda kikomo cha dhanbi zote kubwa hapo kwa kweli inakufika huzuni kubwa wakati kitabu chako kinapowekwa wazi ukawa unaona moja baada la jengine na kama una wasiwasi au khofu ya jambo hili muulize mwenye kuuguza wagonjwa mahtuti atakueleza huzuni zinavyowashukia wakati huo. Sasa Mauti yanatokea vipi, kwanza mauti yana sehemu mbili ya nje na ndani ya mwili, ama kuhusu ya nje ni pale mwili unaposimama kutenda kazi zake kiungo baada ya kiungo. Na sehemu ya pili nayo ni ya ndani ambayo (Roho)inapotenganishwa na mwili wa mwanaadamu, na hili kwa lugha yetu yakufahamiana nitaliita ni (sense)zinapositisha kutenda kazi zake. Kuhusiana na huu mwili (Qura'aan)inasema katika sura ya (Taha-aya-ya-55) مِنۡہَا خَلَقۡنَـٰكُمۡ وَفِيہَا نُعِيدُكُمۡ وَمِنۡہَا نُخۡرِجُكُمۡ تَارَةً أُخۡرَىٰ (٥٥). "Kutokana na hii ardhi(nyinyi)Tumekuumbeni,Na kutokana na hiyo ardhi tutakurudisheni(ikisha)kutokana na hiyo ardhi tutakurejesheni kwa mara nyengine tena,(ili muishi tena)". Naam umbo la mwanaadamu kukamilika linahitaji mambo kama 4 ambayo ni Maji,udongo,moto,na hewa ambavyo vyote vimo katika ardhi hii, na hivi vyote vikikamilika ndio vinaunganishwa na hiyo Roho ili kiumbe kipate kuwa hai.Na hivi vyote vinakamatwa na hii Roho sasa wakati wakutolewa Roho lazima vitu hivi vitenganishwe na hiyo Roho na hapo ndipo inapopatikana(Sakaratul-Mauti),hapo ndipo safari hii nzito inapoanza na mwanzo wa safari hii dalili zake inakua wewe unaumwa watu wamekuzunguka unasikia sauti lakini hujui wanasema nini, hapo (sense)ya kusikia inaanza kupotea, Utakua unaangalia kitu umekaa kimya lakini hufahamu nini kilcho mbele yako ambacho unakitizama,kuona kunaanza kupotea sasa hali inaanza kutisha, mara inaondoka harufu huwezi kunusa tena,ulimi unapoteza ladha ndio maana utaona wagonjwa mahtuti hawataki hata maji seuze chakula, kwa hiyo msiwalazimishe mnawapa shida wakati huo. Hayo ndio mambo ya mwanzo kabisa wa dalili za Umauti ukikufika ndio unaanza kuyaonja, Halafu tena unafatia mwili(Body)unakosa nguvu zote, huwezi sasa hata kusimama Roho ndio inaanza kutenganishwa kidogo kidogo na mwili wako. Mwanaadamu huwezi hata kunyanyua kichwa, Hata Bwana Mtume s.a.w "aliomba kitambaa akaupangusa uso wake kwa maji akasema hakika ya Mauti ni hii sakaratul-mauti". Kwenye kutenganishwa Roho na kiwiliwili ndipo mwanaadamu unahisi kama vile unamezwa na ardhi au kuna jabali linakukandamiza, na hapa ndipo kila mkao mwanaadamu unakuumiza hata mto unakukera maumivu makali mno, sasa utaona mashavu yanaanza kutumbukia ndani, Meno yanageuka rangi, macho hayafungiki tena au kama yamefungika huwezi kuyafumbua. Hapo tena mara unaanza kukoroma na unatoa sauti ya kutisha, walokuzunguka wakisikia mkoromo huu wanaanza kutaarisha mambo ya maziko, nendeni sasa katafuteni sanda, jee karafuu maiti ipo wanazungumza mbele yako na wewe unayasikia mazungumzo haya lakini huwezi kujibu, Pengine mwenye kuuliza hivyo labda mkeo au mumeo au mwanao, au hata wazee wako wote hao wanajitaarisha labda sasa hivi au halafu utazuia pumzi. Hali kama hii ikitokea ndio udongo sasa unachanganyika na maji, mwanaadamu unaanza kuyayuka, ndio maana utaona maiti ilokufia baharini inaharibika mara moja, na akiwa ardhini bila ya kuwekwa kwenye vyombo vya baridi akagandishwa mara anavurugika na kuanza kunuka na hii inatokana na umbo letu kuwa na 85% ni maji. Hapo maji yanaanza kutokea puani au machoni, ulimi haunyanyuki tena, maji yanajaa kooni huna nguvu tena hata ya kuyasukuma, pua kutokana na kufanya kazi ya ziada inaanza kuvuta hewa ya moto ndio ile kiu ya ajabu inamshika mtu katika sakaratul-mauti,khofu kubwa inatuvaa wakati huu na ukimtizama yule atokaye roho wakati ule utaona huzuni kubwa machoni mwake, kama vile anatamani akwambie itakwisha saa ngapi kadhia ya adhabu hii kwani naona kama mwenye kuzama baharini, Hapo tena mwanaadamu anaanza kukosa fahamu zinaondoka na kurejea kwa njia ya mchanganyiko na maneno ya ajabu yanaanza kumtoka walomzunguka wanaanza kushangaa.Ghafla kauli inakatika mdomo unabadilika rangi tena kuwa wa buluu na pua nazo zinakauka kabisa, mwili unaanza kushika baridi na joto linakimbia kuanzia miguuni, sasa hata ukimpa maji ya shahada hayapiti tena kila kitu kishafungwa, Hata ukizungukwa na wanao au mkeo huwatambui tena,hata majina huyafahamu mpaka sauti zao ushazisahau, Sasa hapo unaingia katika hatua ya mwisho ambapo hata kuhema inakua matatizo makubwa, kuvuta pumzi inakua mashaka yasio mfano, na ukitoa pumzi zako zinakua reefu, ikifikia hali kama hiyo macho yanabiruka yanatizama juu na fahamu zinapotea moja kwa moja hapo hufahamu chochote kinachoendelea katika ulimwengu huu, kiza cheusi kinakuzunguka na mawasiliano yote yanakatika.Mara unaanza kupata mawasiliano ya huko unapokwenda tena kama ulikua mtu mwema ishara zinaanza kukushukia, na kama ulikua mtu fisadi unafunguliwa dalili zote wazi wazi na kama ulikua mtenda madhanbi basi unaweza kutoa ukelele waliopo wamekuzunguka wakakukimbia mara moja, lau walokuzunguka wangejua nini unakiona basi hakuna hata mmoja wao angetenda dhanbi tena baada ya siku hii.Ikisha unavuta ile pumzi moja ya mwisho na kuitoa kwa nguvu hapo tena maskini Roho hiyo Malaika wanaondoka nayo na kama umetoa macho basi yanabakia kuangalia juu, na haya yote yanatokea kwa yoyote na mauti yana njia nyingi yanavomkabili mwanaadamu lakini utaratibu ni ule ule fariki kwa accident au vyenginevyo hali hii ni lazima ukabiliyane nayo.Hivi ndivyo sote mauti yanavotukabili na hakuna njia ya kuyakimbia isipokua kuna nafuu kwa wale walorejea kwa Mollah wao kwa njia ya salama na amani, mja uko msafi umetulia huna doa pengine waweza kupata tahfif ilotajwa katika sura ya (Naaziat-aya-ya-2)"وَٱلنَّـٰشِطَـٰتِ نَشۡطً۬ا (٢ Na kwa wale wanotoa roho za (watu wema kwa (Upole)Inshaallah Mollah wetu atujaalie tuwe katika hao kwa kila takayesoma maudhui hii na asiesoma, Amin. Mollah wangu anajua zaidi.

1 comment: