Sunday, September 28, 2014

SALA YA TOBA PART 1

Asalaam Aleiykum

Ushapata kujiuliza kwanini ikawa umepewa nafasi Usali Sala hii ya Toba,? Kwani si ingetosha kuomba kwa kusema ikawa mambo yamekwisha, kuna tukio gani limejificha katika Sala hii  ya toba, tumo katika maudhui ya Sala hii ya Toba ili tupate faida mbili tatu zipate kutusaidia kwa kuipata Rehma ya Mollah wetu ya kusamehewa, sasa ilikuaje mpaka tukafika katika tendo hilo la Toba, wacha nikujulishe kitu kiwe msaada katika safari yako hii ya Kusali Sala ya Toba.
Woga au (Hofu) ni (Absence) ya Utiifu, najua utashangaa lakini ndio hali ilivyo kila kitu kipya kinashangaza, Unamuogopa Nyoka sababu umempitia karibu na ushasikia ana sumu kali lakini hajawahi kukutafuna, hapo woga ushakuvaa, Unamuogopa Baba kakutisha atakupiga, Unamuogopa Mama kakwambia atakutia adabu hakupi chakula,Unaogopa Utawala sababu utakuadhibu, Unaogopa kiza hujui kitatokea nini ndani ya kiza hicho, unaogopa kufa sababu hujui kama kuna uhai mwengine kaburini au Akhera, na zaidi unaogopa kama upo uhai mwengine basi vipi utazikabili adhabu za huko, huo ni upande mmoja wa woga.
Upande wa pili wa Shilingi hii ya woga kuna Ushujaa, Ushujaa ni kama vile ulivyo woga, ila tafauti yake shujaa ni (Rebel)anaupinga huo utiifu, anaamua kuukabili, anaamua kuukabili utiifu na kupambana nao japo anajua kuna madhara, yeye anapinga kila kitu kwa kuvaliwa na jambo katika mambo mawili yaloujenga huu woga na ushujaa, na hakuna jengine ila hili la (Dark)na(Light) kusahau na kukumbuka, ukitizama kwa undani utajua anayeogopa ni Mwenye kukumbuka, na Shujaa ni Mwenye kusahau, Wawili hawa hawa wote wanapita kwenye (Usiku) na (Mchana) wa (Maasi) na (Kujuta), Mwoga akikumbuka anajuta ikisha (Anatubia)halafu anasahau, Shujaa anakumbuka lakini hajuti ikisha anaendelea kusahau, na wote wanayo ile (Nature) ya kuogopa ambayo inathibitisha kuwapo kwa adhabu za aina fulani, bila ya hivyo kuogopa kusingekuwepo.
Endelea part 2


SALA YA TOBA PART 2

Asalaam Aleiykum

Kutokana na hali hiyo ya usahaulivu Mwanaadamu anapita katika hali ya makosa kila wakati wa saa na dakika zake, hakuna anayevuka katika hilo isipokua yule ambaye amekwenda (Beyond) ya Woga na Ushujaa, ambaye sasa kwa mara ya mwanzo anaishi katika Utiifu, na ukiishi katika Utiifu Woga na Ushujaa vyote vinapotea, unakua Mja wa Mwenye enzi Mungu kama ilivyotajwa kwenye sura ya (Yunus aya ya 62-64)
أَلَآ إِنَّ أَوۡلِيَآءَ ٱللَّهِ لَا خَوۡفٌ عَلَيۡهِمۡ وَلَا هُمۡ يَحۡزَنُونَ 
"Wale vipenzi(Waja)wa Mwenye enzi Mungu hawatakua na Khofu wala hawatahuzunika"
Kwa sababu hawana woga wala ushujaa wao wanaishi kwenye Utiifu, na woga na ushujaa ni kwa wale ambao hawajafikia daraja ya kuwa vipenzi vya Mollah wao ili wapate kuondoshewa viwili hivi, sasa hawa ni watu gani?
ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَڪَانُواْ يَتَّقُونَ 
"Nao ni wale Waloamini na wakawa wanamtii(Kumcha)Mwenye enzi Mungu(Wakawa wanajiepusha na maovu)"
Ukiwa unatii huna wasiwasi maisha yako yanakua (Simple)huna haja ya kutetemeka, unaridhika na kila kitu.
لَهُمُ ٱلۡبُشۡرَىٰ فِى ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا وَفِى ٱلۡأَخِرَةِ‌ۚ لَا تَبۡدِيلَ لِڪَلِمَـٰتِ ٱللَّهِ‌ۚ ذَٲلِكَ هُوَ ٱلۡفَوۡزُ ٱلۡعَظِيمُ 
"Wao wana mema katika maisha ya dunia na katika maisha ya Akhera, hakuna mabadiliko katika maneno ya Mwenye enzi Mungu, huku ndiko kufuzu kukubwa"
Na ukisharidhika unakua ushafanikiwa kupata Mema kutoka kwa Mollah wako, maisha yako yanakua ya aina nyengine kabisa hata kuyaeleza hakuna mfano wake mpaka uishi ndio utajua yakoje maisha haya ya (Bliss)unayapata hapa Ulimwenguni na huko Akhera, Na Mwenye enzi Mungu anasema huko ni kufuzu kukubwa, lakini kufuzu huku kunatakiwa ujitolee huo (Muhanga) wa Utiifu, sasa kama huko tayari ndio unapewa nafasi ufanye japo kidogo kidogo kwa njia ya Toba.
Endelea part 3

SALA YA TOBA PART 3

Asalaam Aleiykum

Sasa kwa sie tusoyaweza Kutii moja kwa moja ndio tunapewa hii Sala ya Toba. Kutokana na hali ya makosa wakati wote viumbe tunakua tumejaza wingu hili la makosa katika nafsi zetu, kiza totoro kimetufunika Mja hapo na pale huoni, daima unakua (Guilty)huna furaha, hujui wapi unakwenda nini kitatokea dhiki tupu kwenye nafsi yako, ili kuondosha uzito huo na kuisafisha nafsi yako umepewa Sala hii ya Toba kwa kuambiwa hivi katika sura ya (Imran aya ya 135)
وَٱلَّذِينَ إِذَا فَعَلُواْ فَـٰحِشَةً أَوۡ ظَلَمُوٓاْ أَنفُسَہُمۡ ذَكَرُواْ ٱللَّهَ فَٱسۡتَغۡفَرُواْ لِذُنُوبِهِمۡ وَمَن يَغۡفِرُ ٱلذُّنُوبَ إِلَّا ٱللَّهُ وَلَمۡ يُصِرُّواْ عَلَىٰ مَا فَعَلُواْ وَهُمۡ يَعۡلَمُون
Na ambao wanapofanya uchafu(Mambo ya Zinaa)au kudhulumu nafsi zao humkumbuka Mwenye enzi Mungu na kuomba msamaha kwa Dhanmbi zao, Na nani anayeghufiria Dhanmbi isipokua Mwenye enzi Mungu, Na hawaendelei na(Maovu)waliyoyafanya hali wanajua(Kwamba haya ni Maovu).
Hakuna kitu chenye nguvu kinacho mshinda mwanaadamu kama hii (Ngono)jambo la (Sex) ndio maana hapo ikatajwa mwanzo, kwa sababu ikishaingia Akilini vigumu kutoka mpaka uzeeni mate yanakudondoka, hujiwezi, vipi utajiweza na nguvu amabazo ukizitumia kihalali zina mtengeneza kiumbe, sasa nini habari yetu tunaitumia kwa njia ya haramu? lazima itutengenezee Moto au adhabu zozote tulizoandaliwa.
Au ukidhulumu nafsi yako, vipi unaidhulumu nafsi yako kwa kutenda madhanbi na kila ukitenda dhanmbi ina maana unajitengenezea njia ya adhabu, kwa maana hiyo unaidhulumu nafsi yako mwenyewe, unautaarisha huo mwili ulokubeba kwenda kuungua kwenye moto wa Jahannam.
Sasa ufanye nini kila ukikumbuka, na hakuna kukumbuka kama kusali, kwani Sala ina kitu gani, Sala kama utaikumbuka basi inakupa (Awareness) ya kukumbuka jambo lengine kabisa la Ufalme wa Mollah wako, Sala ni (Light) kila wakati ukikumbuka Sala ina maana unawasha taa kwa kuzima giza la Akili, Jitahidi sana katika hiyo Sala usianze safari za huku na kule ikawa Sala nzima wewe umelala unakuja kuamka kwenye Salaam, Sasa kila ukikumbuka Simamisha Sala hii ya Toba na uombe (Maghfira)usichoke japo unajikwaa na kuanguka tena, hapa umetajwa wewe kwa kufanya hayo machafu na kudhulumu nafsi yako, endelea kuomba toba jizoeshe kuisali sala hii mpaka utafikia pahala taa hii ya Sala ya Toba itawaka moja kwa moja na haitozimika tena, hapo ndio utaijua tafauti ya kosa kwa undani, lakini sasa hivi unaendelea kuwa shujaa, unatubu unasahau unarejea tena, lakini utakapo pata fahamu ndani ya moyo wako na sala hii ya toba ikaingia ndani ya huo moyo hapo tena utasita wewe mwenyewe kufanya hayo makosa, mimi sikwambii kuwa ukisali mara moja ushasamehewa au ndio utaacha kabisa au kusita, ninacho kuhimiza mimi isali Sala hii kila unapohisi umetenda kosa au bila ya kutenda kosa fanya iwe ndio mazoea yako ya kuomba Toba kwa njia hii ya Sala na mwisho nakupa hakika utajikuta umeshafika kwenye Mji wa Utiifu na mapenzi ya Mollah wako.
Inasaliwa vipi Sala hii?
Anahadithia Abubakar Sadik r.a"Nimemsikia Bwana Mtume s.a.w kasema"Mtu yoyote yule ambaye katenda Dhanmbi ikisha akasimama na kutia Udhu halafu akasali Rakaa mbili na kutubu kwa Mwenye enzi Mungu basi humkuta Mwenye enzi Mungu ni Mwenye kumsamehe".
Hivyo ndivyo inavosaliwa sala ya Toba, yatizame mambo mangapi yanatokezea mpaka ukasimamisha hiyo Sala, kwanza unakumbuka, ikisha unatia Udhu, halafu tena Unasali, ndani yake unaomba Maghfira(Toba)basi ikiwa utashindwa kuacha hapo tena itabidi tukupeleke (Sober house) kama vijana wanavoita au ukajiunge (Rehabilitation clinic).Jiunge  uidumishe Sala ya Toba ipate kukuokoa na madhila haya ya Ulimwengu.

Sunday, September 21, 2014

KUMBUKA UFALME WAKO PART 1

Asalaam Aleiykum

Wanaadamu kuna hazina imetupotea siku nyingi, kuna wengine wanaijua na kuitafuta, kuna wengine wako mbioni kujitaarisha kuitafuta hazina hii, Na kuna wengine hawajui kabisa kama ipo hazina hii na ni haki yao kuitafuta, Na wako walo bahatika wachache sana wameipata hazina hii na hivi sasa wanaishi nayo wakiwa furahani katika pepo ya Dunia.
Ama kwa wale wote ambao hawajaigundua hazina hii itabidi niwachukue ili nipate kuwakumbusha njia ya kwenda ukafikia kwenye Hazina hiyo ya Ufalme wako, Wewe ni Mfalme lakini kwa sasa bado hujielewi, bado hujakumbuka japo Mollah wako anakukumbusha sana, anakwambia "Ewe Mwanaadamu" Wewe kwenye Ulimwengu huu Wewe (Khalifa) lakini unaendelea kuishi katika Umasikini, unaendelea kuishi kwenye mateso, unaendelea kuishi umo kupita kuomba hichi na kile, lini yatakwisha madhila na mateso haya.
Yatakwisha pale utakapo kumbuka kumbe hazina ipo chini ya miguu yangu, hazina imefukiwa chini ya (Ukuta) na ukifukua tu wewe ushakua (Mfalme)Tafauti yake ni kukumbuka kwa kitendo kumbe mimi (Mtawala). Sasa vipi inatokea hali hii ya kukumbuka? hali hii inatokea kwa wewe Mwenyewe kufanya kazi au kuwa karibu na watu wanofahamu, watu walokua tayari washakumbuka Ufalme huo, hao watasaidia kukumbusha kama nifanyavo mimi sasa hivi, venginevyo utaendelea kuishi kama Mtumwa hali yakua wewe ni Mfalme.
Nikitaja Ufalme tafsiri zako moja kwa moja zinakupeleka kwenye Utajiri, zinakupeleka kwenye kulimbikiza mali, hicho ndio kigezo chako ulichonacho, kwanini ikawa hivyo sababu maisha yako yote unaishi kwa vigezo vya nje, Fulani ana hichi na kile, Fulani ana Majumba makubwa ya ghorofa, Fulani ana watoto wengi, lakini hata siku moja hujapata kujiuliza hivyo Fulani ana Ufalme katika nafsi yake, anaishi Furahani na vyote alonavyo, keshajigundua yeye ni Mfalme, anaipata (Bliss)kutoka kwa Mollah wake, keshawahi ku(Test) kitu kilicho (Beyond) Furaha, vigezo hivyo huna, vigezo ulivyo navyo ni Fulani (Handsome) na Yule ana (Figure)nzuri, akitembea anapendeza umeshughulika na uonavyo nje nini habari ya Ndani kwako?.
Endelea part 2

KUMBUKA UFALME WAKO PART 2

Asalaam Aleiykum

Hata siku moja hujakaa ukatizama kitu ambacho kitakukumbusha Ufalme wako, kitu gani hicho kiwezacho kukumbusha Ufalme wako? kama nilivyosema huko nyuma Ufalme wako umefunikwa na usingizi wa mambo mengi ya tamaa za kidunia kwa hiyo ili kupata huo ukumbusho, ili ujijue wewe Mfalme basi itakubidi jambo la mwanzo usamehe Usingizi, kwa sababu hivi sasa wewe mvivu unalazwa mchana na mambo ya kidunia, ikisha unalala usiku na mambo ya (akhera) kinachotakiwa wewe Mwenyewe ujikaze kwanza kupigana na usingizi wa Usiku kwa kufanya (Ibada)    كَانُواْ قَلِيلاً۬ مِّنَ ٱلَّيۡلِ مَا يَہۡجَعُونَ 
"Walikua wakilala kidogo(Nyakati za)Usiku"
Kugundua Ufalme huu lazima ufanye jitihada ya kuondosha mazoea ya usingizi, masaa manne yanakutosha huna haja ya kukoroma mpaka majirani wakasikia, ukipata mazoea haya kidogo kidogo uvivu utaanza kuondoka, ndoto za kiajabu ajabu zitaanza kupotea, usingizi wako utakua(Light)utakua una mazoea ya kumkumbuka Mollah wako kwa Ibada, na utakua japo umelala lakini upo (Alert)huhitaji (Alarm)tena unaamka kwa kutegesha (alarm)yako ya (Awareness).
 وَبِٱلۡأَسۡحَارِ هُمۡ يَسۡتَغۡفِرُونَ 
"Na Wakiomba Msamaha Nyakati kabla ya Alfajiri"
Ukiwa (Alert)kumbukumbu za mwanzo kuhudhuria ni zile za makosa zilojaa katika Akili yako, hapo Mja alokwisha anza kukumbuka Ufalme wake hana budi ila kujitupa kwa Mollah wake na kuomba Msamaha, na hakuna nyakati nzuri kama zile za karibu ya Alfajiri, kuna siri kubwa katika nyakati hizo ambazo nitazizungumza siku za mbele.
 وَفِىٓ أَمۡوَٲلِهِمۡ حَقٌّ۬ لِّلسَّآٮِٕلِ وَٱلۡمَحۡرُومِ 
"Na katika mali zao ilikuwa haki ya kupewa maskini aombaye na ajizuiaye kuomba"
Wao washagundua hii Mali imepitia tu katika mikono yao, wamepewa na Mollah wao ili waifikishe kwa wale waombao na pia wasioomba, wao washajua haina faida yoyote kwao, ikiwepo au isiwepo mali hiyo, washagundua kuwa kuna siku watafukiwa chini ya Ardhi na mali yote ibaki juu ya Ardhi na kutafunwa na watu wengine, sasa kuna faida gani ya kuichunga na kuumia kwa kuishughulikia huku unasahau Ufalme ulio nao, itoe kwa njia za kheri ili ipate mali hiyo kukumbusha Ufalme wako, kwani kila ukiweka matamanio ya ulimbikizaji yanazidi, lakini ukitoa na matamanio yanaondoka(Unless)uwe mgonjwa wa kutafuta mali, lakini siku zote kutoa kunakuletea Faraja fulani inayotokea kwenye huo Ufalme ninaozungumza.
وَفِى ٱلۡأَرۡضِ ءَايَـٰتٌ۬ لِّلۡمُوقِنِينَ 
"Na katika Ardhi zimo alama(Za kuonesha Ufalme wa Mwenye Enzi Mungu")kwa wenye yakini.
Pita kwenye Ardhi utizame uhai uloanzia kwenye vidudu mpaka vinyama, ukafikia mpaka Baharini tukawa tunaona vyote vilo hai, mpaka miti na ndege wanavoishi, kaa uwatizame ndege wendavyo kwenye nyumba zao magharibi, na panapo pambazuka alfajiri uone vipi wanavotoka kwenda kutafuta Riziki zao, umewatizama ngombe na farasi wanavokula majani yao, umejiuliza kwanini wakiwekwa kwenye msitu hawali majani yote bali wanachagua baadhi ya majani kuyatafuna, nini kimefichwa kwenye majani hayo hata ikawa Ngombe lazima ayapate hayo, Umeichunguza miti inapokua na furaha vyote hivyo vina uhai kinachotakiwa  wewe tu kuyagundua hayo yote yalo wazi mbele yako na yenye yakini, basi itafute hiyo yakini ikuvae kwenye ujuzi wako na ukipata uhakika sasa wewe utakua tayari kukumbuka kwamba, daah, kama mimi nimeweza kuyajua haya basi mimi ni Mfalme, kwa vipi?
Endelea part 3

KUMBUKA UFALME WAKO PART 3

Asalaam Aleiykum

وَفِىٓ أَنفُسِكُمۡ‌ۚ أَفَلَا تُبۡصِرُونَ 
"Na katika Nafsi zenu (Alama kama hizo zimo) Jee hamzioni"
Ewe Mfalme amka umuabudu Mollah wako, Fanya mema uipate faraja ya Mwenye enzi Mungu uwe kipenzi chake cha kweli.
Ikiwa umeipata yakini ya kuviona vilivyo kwenye hii ardhi ukajiridhisha vya kutosha na kuanza kuamini kuwa kweli haya yote niloyaona katika Ulimwengu huu yamethibiti sasa Mwenye enzi Mungu anataka utizame na ndani ya nafsi yako, mwanzo ulikua unatizama nje sasa rudi kwenye Nafsi yako mwenyewe, acha kutizama (Figure) ya huyu na yule, jitizame wewe mwenyewe, kwanza tizama vipi Mollah wako alivyokuumba, akakupa kila kitu kilicho kamili, akakufanya mzuri kwa uweza wake, jiulize kwanini hayo yote huyaoni,ushawahi kutizama vidole vyako, nyayo zako, magoti yako, na kila kiungo chako ukavipenda kwa jinsi ya Mollah alivokuumba, kwanini unasubiri mpaka uumwe ndio ujiangalie, Wewe Mfalme kwanini huutizami ufalme wako, huo Mwili wako ni mji kamili na wafanya kazi wake, wewe ni mwenye kutoa Amri sasa nataka kulala usingizi njoo, sasa nataka kuamka nende kazini, leo mbona nasikia kichwa kinagonga kuna nini, mbona ulimi una hivi nimefanya nini, mguu leo umenivimba nilikanyaga nini, Mbona moyo unakwenda mbio nimepatwa na nini, jee nikapige (X-ray)nione ndani kuna usalama gani, baada ya hayo yote kuyazingatia sasa jiulize huyu anayeona Nani? Jee huyu mimi nionae ndie Mfalme mwenyewe anayezungumzwa? Halafu majibu kaa nayo mwenyewe.
وَفِى ٱلسَّمَآءِ رِزۡقُكُمۡ وَمَا تُوعَدُونَ 
"Na katika Mbingu ziko Riziki zenu na mliyohaidiwa"
Basi ukishagundua hayo yote ukawa na hakika nayo, hapo tena ndipo unaambiwa katika hiyo Mbingu unayoitizama ndiko inapotoka Riziki yako, hata uhangaike vipi kama hujapangiwa uipate huipati,Huwi tajiri hata ufanye nini,(Au uchague njia za nguvu za kukupeleka kwenye mateso)hapo utapata Riziki yako kwa njia hizo lakini utakiona cha mtemakuni,ikiwa utaridhia uondoshe matamanio(Disire)ya hichi na kile, umeridhika upewe na Mollah wako basi Riziki yako itatokea Mbinguni, lakini kama utaamua amri mkononi mwako basi subiri yale tuliyo ahidi, kama yepi ikiwa utafanya mema na kusubiri (Qadara)ya Mollah wako utapata hayo unayoahidiwa yenye kheri, na kama utatumia ujanja au mabavu ya nguvu na kufanya ufisadi wakati unaishi katika Ulimwengu huu, basi yale uloambiwa utayakuta ya adhabu za kila aina yapo yanakusubiri wala hayana shaka kama ulivyo yashuhudia hayo ya kwenye Ardhi na huko Mbinguni utakwenda kuwa Shahidi wa hayo pasi na wasiwasi.
 فَوَرَبِّ ٱلسَّمَآءِ وَٱلۡأَرۡضِ إِنَّهُ ۥ لَحَقٌّ۬ مِّثۡلَ مَآ أَنَّكُمۡ تَنطِقُونَ
"Basi Naapa kwa Mollah wa Mbingu na Ardhi, kuwa haya ni haki, kama ilivyo (Haki) ya kwamba nyinyi mnasema"
Hapa imechukuliwa uthibitisho wa haki ya hayo mambo na kuthibitishwa na kama nyinyi mlivo na haki ya kusema, Nini hicho kisemacho? na kwanini kikafananishwa na hayo mambo yalotajwa hapo juu, huo ni Ufalme ulonao wewe, hiyo ni Roho yako yenye Haki ya kuzungumza, kumbuka jambo moja ujiulize mbona ukizungumza huwezi kufikiri? na kwanini unazungumza? mamlaka haya ya kuzungumza yametokea wapi? ukilikumbuka hilo wewe utakua umeshautambua Ufalme wako, utaelewa haki yote na Amri zinatokea kwa Mwenye enzi Mungu, na huna budi ila kuishi katika Ufalme huo huku ukiwa na wewe una cheo cha Ukhalifa wa kutenda mema, Ukhalifa wa Kufanya Ibada kwa Mollah, hapo tena utafunguliwa kila lenye kheri na furaha, utazipata siri zilofichika na zilizo dhahiri kwa Uwezo wa Mollah wako. Na hiyo ni Haki yako kama utakumbuka wewe ni Mfalme.

Sunday, September 14, 2014

URAFIKI WA SALA PART 1

Asalaam Aleiykum

Umeshawahi kujiuliza urafiki wako na huyo mwenzio ulianza vipi? Jee mahusiano yenu yana mapenzi au makubaliano?Na kwanini Jambo dogo tu linavunja urafiki huo, ukiangalia kwa makini mahusiano hayo ya Urafiki wenu yamekamatana na makubaliano ya hiyari, ndani ya hiyo hiyari imejificha chembe ya mapenzi, kwenye hiyari kuna mbegu na kama mbegu hiyo itachanua Urafiki wenu unakua wa kufa na kuzikana, Mnakua kama ndugu wa tumbo moja, huo ni urafiki wa Binaadamu kwa Binaadamu, Mimi leo nataka kukujulisha vipi unapatikana Urafiki baina ya Mwanaadamu na Sala na nini kinatokezea Urafiki huo unapokuwa wa kweli, Wapi Rafiki yako Sala anakupeleka.
Sala ni sehemu maalum unayoingia na kutoka kwa njia ya Siri na Dhahiri, Dhahiri ni Msikitini au Nyumbani watu wote wanakushuhudia, halafu unaingia kwenye siri ambapo moyoni mwako wewe pekee na Mollah wako mnakutana katika njia zako maombi, Na katika hiyo siri wewe hukai moja kwa moja, mara umehamia kwenye akili na akili inakupeleka inapojua yenyewe, ndio maana unaingia msikitini lakini unajikuta upo senema, au upo dukani au unafunga hesabu na kuamua mambo haya na yale, Unatoka kabisa katika sehemu takatifu uliyosimama, sehemu ya unyenyekevu uloingia ukawa huna kusudio lolote ila ni kusali kwa kumuomba na kumsabahi Mollah wako.
Sasa nini kitakujulisha kuwa ushaanza kuipata Sala? Vipi utajua ushaanza kuwa wewe na Sala ni marafiki? Jambo la Mwanzo kabisa Rafiki wako huyu anakukinga na (Machafu na Maovu)
(إِنَّ ٱلصَّلَوٰةَ تَنۡهَىٰ عَنِ ٱلۡفَحۡشَآءِ وَٱلۡمُنكَرِ‌ۗ)
Na moja kwa moja ukiepushwa na mambo hayo Sala inakupeleka kwenye Jambo la pili ambalo kubadilishwa au kugeuzwa khofu yako kuwa mapenzi, maisha yako yote yanabadilika kwa Jambo la kuipata Sala, Na jambo la tatu unakua huondoki tena kwenye hiyo sala na kwenda kutalii. Hapo tena Sala inakuondoshea khofu ya kufa, khofu ya Akhera unakua tayari kukutana na Mollah wako Mpenzi, wakati wote wa Sala na hata kurejea huko Akhera.
Lakini huwezi kuyapata hayo mpaka ufanye mazoea ya hiyo Sala, mpaka umuombe urafiki hicho kitendo kiitwacho Sala, mpaka mzoeane ndio utakua mwenye kusimamisha Sala, vipi unafanya mazoea haya, ni lazima kwanza uishinde Akili, halafu? .endelea part 2

URAFIKI WA SALA PART 2

Asalaam Aleiykum

Ndio nakutajia Sala ambazo zitakuwezesha kufikia lengo lako la kuwa Rafiki wa Sala na ukageuka kuwa Kipenzi cha Mollah wako,
Nakupa utangulizi wa maneno kuna vitabu vyengine vinasema hizi Sala hazijathibiti, Sasa wewe una hiyari yako kama alivyosema Mwanasayansi mmoja alipoulizwa kwanini unaamini Mungu? akajibu Majuto ya kutoamini makubwa pale ambapo ntakapokufa ikisha Mungu akawa yupo, nini hali yangu itakua wakati huo, basi bora Imani yangu itanitetea na kama hayupo basi vilevile sijapata hasara yoyote.
Basi na wewe hali kama hiyo kama utaamini hazijathibiti sawa, na kama itakua zimethibiti nini habari yako wewe katika hayo mapokezi kwa Mollah wako, Ama kwa hapa Ulimwenguni dalili ninazokupa mimi ni huo Urafiki, sasa una uamuzi wako kuzisali au kuziacha, sasa kwanini nikakukumbusha sababu kubwa watu wameacha hata Sala za sunna siku hizi wameziacha, hawajui kipi kinaruhusiwa na kipi kinakatazwa, misingi ya dini yote imevunjwa, na sisi wengine kazi yetu ni kutafuta (Vifusi) vilobakia ili tujaribu kujenga tena kama tutaweza, ziko wapi zile zama ambapo unakwenda Msikitini robo saa kabla ya Sala ya Fardhi ili upate kutanguliza Sunna zako, uko wapi Urafiki wa Sala siku hizi.
Sala ya Dhuhaa
Kwanini nikaanza na Sala hii kwa sababu nakutaka uwe mwenye kujizoesha kumsabahi Mollah wako baada ya kumalizika ile fardhi ya alfajiri, jipangie uwe mwenye kuipata sala hii ukiwa ofisini, ukiwa kwenye biashara, ukiwa darasani popote kuwa mwenye kukumbuka uipate sala hii kwani anasema Abuu Hurairah r.a "amenihusia Bwana Mtume s.a.w" kufunga siku tatu kila mwezi, kusali Rakaa za sala ya Dhuhaa, na kusali sala Witr kabla ya kulala.
Anahadithia Bibi Aisha r.a Alikua Mtume akisali Rakaa nne za Sala hii ya Dhuhaa na kuzidi.
Na fadhila zake Sala hii ya Dhuhaa kama vile uliyetoa sadaka, pia ni yenye kukuamrisha mema na kukuepusha na mabaya na mengine yalotajwa katika hadith, na Rakaa zimetajwa nyingi tu ikiwa utaweza kuziendeleza na umehimzwa kusoma sura ya (Fatiha na kufatiwa na Washamsi, na sura ya Dhuhaa.
Sala ya Istikhara(Maombi)unaweza kuisali wakati wowote uloruhusiwa sala za sunna, lakini ikiwa unataka upate ishara za maombi yako basi unaweza kusali usiku Rakaa zako mbili na kutaka kujulishwa maombi yako.
Sala ya Haja.
Utasali Rakaa mbili nakuomba haja yako.
Sala Ya usiku, soma mada ya (Faida ya Sala za usiku).
Na zengine zinofatia Sunna za Kabliya na Baadiya na pia usisahau rakaa mbili za Tahiyatul Masjid uingiapo msikitini. endelea part 3

URAFIKI WA SALA PART 3

Asalaam Aleiykum

Kwa hiyo utaona masaa yote 24 umezungukwa na tendo hili la Sala, Na huko ndiko kumkumbuka Mollah wako, ikiwa kweli umekusudia Sala iwe Rafiki yako basi anza kuzitekeleza hizo zote nilizo zitaja na zengine ambazo sijazitaja ili nisikutie kwenye mushkeli wa kuthibiti na kutokuthibiti, Kwa ufupi Sala ni daraja baina yako na Mollah wako, Na ukiweza kulivuka daraja hili nini kinatokea? Kama utajichunguza kila ukiingia kwenye Sala yanakuja mawazo tafauti na sababu kubwa ya jambo hilo (Mind)Akili yako si kitu cha kupenda utulivu, Na Sala ni jambo la utulivu ndio maana utaona katika mataarisho yote akili inakwenda sambamba na wewe lakini ukianza Sala tu Akili inakutupa mkono na unakua hasarani si mwenye kuipata Sala, yanakuja mawazo chungu nzima, sasa ikiwa mwenye kuzoea kuzisali Sala za Fardhi na hizi  za Sunna unakua unailazimisha Akili ikufate wewe, sio wewe uifate Akili, Na akili itakapofata amri yako wewe umeshafaulu, umepasi mtihani wako.
Moja kwa moja Sala zako zinakua zinatokea moyoni, na moyoni ndio kwenye nuru, moyoni ndio inapokaa Sala, na ukiwasili moyoni huwezi kukosa kipindi, huwezi kukosa Sala, wakati wote wewe ni mwenye kuikumbuka Sala na Mollah wako. Hapo tena Baraka za Mollah wako zinaanza kukushukia utaona mambo yako yanakwenda pasi wewe kuyaendesha, Na wewe unakua katika walioitikia maagizo ya (aya ya 205 sura ya Al Aaraf)
وَٱذۡكُر رَّبَّكَ فِى نَفۡسِكَ تَضَرُّعً۬ا وَخِيفَةً۬ وَدُونَ ٱلۡجَهۡرِ مِنَ ٱلۡقَوۡلِ بِٱلۡغُدُوِّ وَٱلۡأَصَالِ وَلَا تَكُن مِّنَ ٱلۡغَـٰفِلِين
Na Mtaje Mollah wako moyoni mwako kwa unyenyekevu na khofu na bila ya kupiga kelele katika kauli(Usitoe sauti, umkumbuke)Asubuhi na jioni, wala usiwe miongoni mwa waloghafilika.
Usighafilike hiyo ndio kuipata Sala, Wakati wote Sala ipo kwenye Moyo wako na ukijiona uko katika hali hiyo basi jijue wewe ushakua Rafiki wa Sala, kwani sala haishii kwenye vitendo bali inaendelea mchana kutwa na usiku kucha, Na Rafiki wa Sala ndio kipenzi cha Mwenye Enzi Mungu, Wacha wengine watoe sadaka, wafanye mema chungu nzima wewe taka au omba uwe Rafiki wa Sala utakua umefanikiwa mafanikio makubwa kabisa katika maisha yako ya Ulimwengu huu na Daraja yako itakua kama Nani?
(aya ya 206 sura hiyo hiyo ya Al Aaraf)
إِنَّ ٱلَّذِينَ عِندَ رَبِّكَ لَا يَسۡتَكۡبِرُونَ عَنۡ عِبَادَتِهِۦ وَيُسَبِّحُونَهُ ۥ وَلَهُ ۥ يَسۡجُدُونَ 
Wale walioko kwa Mollah wako(Malaika)Hawajivuni(Wakaghafilika)kumuabudu(Mollah wao kwa vyeo walivyonavyo)(Bali)Wanamtukuza na kumsujudia.Na wewe utakua katika kundi hilo, Na ukiwemo katika kundi kama hilo inakuteremkia salama ya upole, hata kama ulikua mpiga makelele, mchekeshaji vyote vinaondoka unakua mpole ulojaa mapenzi, na kila wakati wewe umo kwenye Sala, ukiwa sokoni au ofisini, ukiwa kwenye TV au mkutanoni wewe umo ndani ya Sala, hata ikitokea kuota basi unaota matendo ya Sala na upo msikitini, kwakua huruhusu akili yende kwenye ndoto za kipuuzi, huo ndio Urafiki wa Sala ambao wote tunatakiwa tujitahidi tuupate, Na Inshaallah tukifanya jitihada tutafanikiwa kwa Uweza wa Allah.