Sunday, September 21, 2014

KUMBUKA UFALME WAKO PART 3

Asalaam Aleiykum

وَفِىٓ أَنفُسِكُمۡ‌ۚ أَفَلَا تُبۡصِرُونَ 
"Na katika Nafsi zenu (Alama kama hizo zimo) Jee hamzioni"
Ewe Mfalme amka umuabudu Mollah wako, Fanya mema uipate faraja ya Mwenye enzi Mungu uwe kipenzi chake cha kweli.
Ikiwa umeipata yakini ya kuviona vilivyo kwenye hii ardhi ukajiridhisha vya kutosha na kuanza kuamini kuwa kweli haya yote niloyaona katika Ulimwengu huu yamethibiti sasa Mwenye enzi Mungu anataka utizame na ndani ya nafsi yako, mwanzo ulikua unatizama nje sasa rudi kwenye Nafsi yako mwenyewe, acha kutizama (Figure) ya huyu na yule, jitizame wewe mwenyewe, kwanza tizama vipi Mollah wako alivyokuumba, akakupa kila kitu kilicho kamili, akakufanya mzuri kwa uweza wake, jiulize kwanini hayo yote huyaoni,ushawahi kutizama vidole vyako, nyayo zako, magoti yako, na kila kiungo chako ukavipenda kwa jinsi ya Mollah alivokuumba, kwanini unasubiri mpaka uumwe ndio ujiangalie, Wewe Mfalme kwanini huutizami ufalme wako, huo Mwili wako ni mji kamili na wafanya kazi wake, wewe ni mwenye kutoa Amri sasa nataka kulala usingizi njoo, sasa nataka kuamka nende kazini, leo mbona nasikia kichwa kinagonga kuna nini, mbona ulimi una hivi nimefanya nini, mguu leo umenivimba nilikanyaga nini, Mbona moyo unakwenda mbio nimepatwa na nini, jee nikapige (X-ray)nione ndani kuna usalama gani, baada ya hayo yote kuyazingatia sasa jiulize huyu anayeona Nani? Jee huyu mimi nionae ndie Mfalme mwenyewe anayezungumzwa? Halafu majibu kaa nayo mwenyewe.
وَفِى ٱلسَّمَآءِ رِزۡقُكُمۡ وَمَا تُوعَدُونَ 
"Na katika Mbingu ziko Riziki zenu na mliyohaidiwa"
Basi ukishagundua hayo yote ukawa na hakika nayo, hapo tena ndipo unaambiwa katika hiyo Mbingu unayoitizama ndiko inapotoka Riziki yako, hata uhangaike vipi kama hujapangiwa uipate huipati,Huwi tajiri hata ufanye nini,(Au uchague njia za nguvu za kukupeleka kwenye mateso)hapo utapata Riziki yako kwa njia hizo lakini utakiona cha mtemakuni,ikiwa utaridhia uondoshe matamanio(Disire)ya hichi na kile, umeridhika upewe na Mollah wako basi Riziki yako itatokea Mbinguni, lakini kama utaamua amri mkononi mwako basi subiri yale tuliyo ahidi, kama yepi ikiwa utafanya mema na kusubiri (Qadara)ya Mollah wako utapata hayo unayoahidiwa yenye kheri, na kama utatumia ujanja au mabavu ya nguvu na kufanya ufisadi wakati unaishi katika Ulimwengu huu, basi yale uloambiwa utayakuta ya adhabu za kila aina yapo yanakusubiri wala hayana shaka kama ulivyo yashuhudia hayo ya kwenye Ardhi na huko Mbinguni utakwenda kuwa Shahidi wa hayo pasi na wasiwasi.
 فَوَرَبِّ ٱلسَّمَآءِ وَٱلۡأَرۡضِ إِنَّهُ ۥ لَحَقٌّ۬ مِّثۡلَ مَآ أَنَّكُمۡ تَنطِقُونَ
"Basi Naapa kwa Mollah wa Mbingu na Ardhi, kuwa haya ni haki, kama ilivyo (Haki) ya kwamba nyinyi mnasema"
Hapa imechukuliwa uthibitisho wa haki ya hayo mambo na kuthibitishwa na kama nyinyi mlivo na haki ya kusema, Nini hicho kisemacho? na kwanini kikafananishwa na hayo mambo yalotajwa hapo juu, huo ni Ufalme ulonao wewe, hiyo ni Roho yako yenye Haki ya kuzungumza, kumbuka jambo moja ujiulize mbona ukizungumza huwezi kufikiri? na kwanini unazungumza? mamlaka haya ya kuzungumza yametokea wapi? ukilikumbuka hilo wewe utakua umeshautambua Ufalme wako, utaelewa haki yote na Amri zinatokea kwa Mwenye enzi Mungu, na huna budi ila kuishi katika Ufalme huo huku ukiwa na wewe una cheo cha Ukhalifa wa kutenda mema, Ukhalifa wa Kufanya Ibada kwa Mollah, hapo tena utafunguliwa kila lenye kheri na furaha, utazipata siri zilofichika na zilizo dhahiri kwa Uwezo wa Mollah wako. Na hiyo ni Haki yako kama utakumbuka wewe ni Mfalme.

No comments:

Post a Comment