Asalaam Aleiykum
Kwa hiyo utaona masaa yote 24 umezungukwa na tendo hili la Sala, Na huko ndiko kumkumbuka Mollah wako, ikiwa kweli umekusudia Sala iwe Rafiki yako basi anza kuzitekeleza hizo zote nilizo zitaja na zengine ambazo sijazitaja ili nisikutie kwenye mushkeli wa kuthibiti na kutokuthibiti, Kwa ufupi Sala ni daraja baina yako na Mollah wako, Na ukiweza kulivuka daraja hili nini kinatokea? Kama utajichunguza kila ukiingia kwenye Sala yanakuja mawazo tafauti na sababu kubwa ya jambo hilo (Mind)Akili yako si kitu cha kupenda utulivu, Na Sala ni jambo la utulivu ndio maana utaona katika mataarisho yote akili inakwenda sambamba na wewe lakini ukianza Sala tu Akili inakutupa mkono na unakua hasarani si mwenye kuipata Sala, yanakuja mawazo chungu nzima, sasa ikiwa mwenye kuzoea kuzisali Sala za Fardhi na hizi za Sunna unakua unailazimisha Akili ikufate wewe, sio wewe uifate Akili, Na akili itakapofata amri yako wewe umeshafaulu, umepasi mtihani wako.
Moja kwa moja Sala zako zinakua zinatokea moyoni, na moyoni ndio kwenye nuru, moyoni ndio inapokaa Sala, na ukiwasili moyoni huwezi kukosa kipindi, huwezi kukosa Sala, wakati wote wewe ni mwenye kuikumbuka Sala na Mollah wako. Hapo tena Baraka za Mollah wako zinaanza kukushukia utaona mambo yako yanakwenda pasi wewe kuyaendesha, Na wewe unakua katika walioitikia maagizo ya (aya ya 205 sura ya Al Aaraf)
وَٱذۡكُر رَّبَّكَ فِى نَفۡسِكَ تَضَرُّعً۬ا وَخِيفَةً۬ وَدُونَ ٱلۡجَهۡرِ مِنَ ٱلۡقَوۡلِ بِٱلۡغُدُوِّ وَٱلۡأَصَالِ وَلَا تَكُن مِّنَ ٱلۡغَـٰفِلِين
Na Mtaje Mollah wako moyoni mwako kwa unyenyekevu na khofu na bila ya kupiga kelele katika kauli(Usitoe sauti, umkumbuke)Asubuhi na jioni, wala usiwe miongoni mwa waloghafilika.
Usighafilike hiyo ndio kuipata Sala, Wakati wote Sala ipo kwenye Moyo wako na ukijiona uko katika hali hiyo basi jijue wewe ushakua Rafiki wa Sala, kwani sala haishii kwenye vitendo bali inaendelea mchana kutwa na usiku kucha, Na Rafiki wa Sala ndio kipenzi cha Mwenye Enzi Mungu, Wacha wengine watoe sadaka, wafanye mema chungu nzima wewe taka au omba uwe Rafiki wa Sala utakua umefanikiwa mafanikio makubwa kabisa katika maisha yako ya Ulimwengu huu na Daraja yako itakua kama Nani?
(aya ya 206 sura hiyo hiyo ya Al Aaraf)
إِنَّ ٱلَّذِينَ عِندَ رَبِّكَ لَا يَسۡتَكۡبِرُونَ عَنۡ عِبَادَتِهِۦ وَيُسَبِّحُونَهُ ۥ وَلَهُ ۥ يَسۡجُدُونَ
Wale walioko kwa Mollah wako(Malaika)Hawajivuni(Wakaghafilika)kumuabudu(Mollah wao kwa vyeo walivyonavyo)(Bali)Wanamtukuza na kumsujudia.Na wewe utakua katika kundi hilo, Na ukiwemo katika kundi kama hilo inakuteremkia salama ya upole, hata kama ulikua mpiga makelele, mchekeshaji vyote vinaondoka unakua mpole ulojaa mapenzi, na kila wakati wewe umo kwenye Sala, ukiwa sokoni au ofisini, ukiwa kwenye TV au mkutanoni wewe umo ndani ya Sala, hata ikitokea kuota basi unaota matendo ya Sala na upo msikitini, kwakua huruhusu akili yende kwenye ndoto za kipuuzi, huo ndio Urafiki wa Sala ambao wote tunatakiwa tujitahidi tuupate, Na Inshaallah tukifanya jitihada tutafanikiwa kwa Uweza wa Allah.
No comments:
Post a Comment