Tuesday, October 28, 2014

KUMKUMBUKA ALLAH(DHIKR)PART 1

Asalaam Aleiykum

Wanasema Wanasayansi Mwanaadamu Bingwa wa Maarifa(Genious)hodari wa kupita mfano anaitumia Akili kwa uchache wa Asilimia 15 tu, Na hiyo katika jambo pengine hususia la uvumbuzi wa kitu fulani na huku akiacha mambo mengine chungu nzima yakimpita. Sasa ikiwa hali kama hiyo inatokezea kwa Bingwa kama huyo, nini habari yetu ya mimi na wewe tunatumia kiwango gani cha Akili zetu katika kujishughulisha na mambo yote yalotuzunguka?.
Inapaswa Mwanaadamu ajiulize asilimia ngapi anatumia, na katika kuzipata asilimia hizo ujitizame pia kiasi gani unatumia katika kumkumbuka Mollah wako, kama hutaki mahangaiko hayo basi nipe nafasi nikuonee mimi huruma ili nikupe kiwango chako unachotumia kwa ukamilifu kumkumbuka Mollah wako kwa masaa 24, Wallahi huzidi ila dakika 10 na nitakuonesha vipi kama angalau unazipata hizo dakika 10, Anzia wewe mwanzo unapomkumbuka Mollah wako labda tuseme kwenye Adhana unapoisikia au kipindi cha Sala kinapoingia basi muda wote huo mpaka kusali kwako labda ni dakika mbili tu ambazo pengine ndizo unazo bakia na Mollah wako, lakini mawazo yako safarini kuanzia kwenye Udhu mpaka Sala nzima, hukai hata sekunde saba katika kumkumbuka huko Mollah wako, kutwa unaendelea ku (Process)mawazo haya na yale, na ukiingia katika hiyo Sala basi unaweza hata kutukana au bure linakutoka (Fonyo)kwa ajili ya fulani alivyo kukera, hutulii kwenye Sala Abadan, unakaribia kukufuru mambo chungu nzima yanakuja katika hiyo Sala, na hapo ndio sehemu moja pekee ambayo labda unatakiwa umkumbuke Mollah wako kwa ukamilifu, lakini wapi viuno vinakuja hapo, michezo ya Tv unamalizia hapo, madeni unayalipa hapo, imekua Sala yote ni kitendo cha kupanga mambo yako na vipi utayatekeleza, ndio maana nikakupa angalau dakika mbili labda unamkumbuka uso umeumbwa na haya katika masaa 24 basi usipate hata hizo dakika 10, usishangae kuna wengine hawapati kabisa, hawajaanza safari hii ya kukumbuka hata hatua moja. Sasa wewe ulopata nafasi ukayajua haya nakuomba Jiulize hivo yule alokuumba akakupa Uhai anastahiki dakika 10 au zaidi ya dakika hizo, katika darsa hii nakufungua macho ili upate kujua vipi utamkumbuka Mollah wako, nini ufanye mpaka upate ladha ya kuwa karibu na Mollah wako.
Endelea part 2

KUMKUMBUKA ALLAH(DHIKR)PART 2

Asalaam Aleiykum

Sasa kama umeamua kwa Bidii kutaka kumkumbuka Mollah wako na uzidishe hizo dakika, basi soma maudhui hii kwa kituo ili ipate kukuonesha njia za kumkurubia Mollah wako na kumsabahi na kumkumbuka wakati bado una nguvu zako, usisubiri mpaka kuumwa au umefanya dhanmbi ndio ukakurupuka kukumbuka kuomba msamaha, au huna nguvu tena una wasiwasi karibu utakufa ndio ukaanza kazi hii, unatakiwa uianze mapema ikujae Moyoni na utapata manufaa yake makubwa baadae.
Nataka kukufahamisha kuwa ukitegemea kukumbuka ina maana wewe unaitegemea Akili, sawa, nzuri lakini inatakiwa uende (Beyond)Akili, kwa sababu Akili ina tabia ya kusahau ndio maana ukaambiwa ufikiri, lakini kuna kitu ambacho hakisahau ambacho ni huo moyo, na mifano nitakutolea hiyo sura ya (Fatiha)unaona unavyoisoma hutaki hata kuikumbuka sababu iko moyoni unaitoa (Direct)lakini zengine mpaka uzifikiri na mara unakwama, sasa nini kinachokusadia kukumbuka, kile ambacho hakikumbuki ila kinataja, moyo hausahau lakini unataka mazoea, lazima ujizoeshe ndio moyo unaweza kushika jambo, Na Mollah wako katumia mifano mingi kukupa mazoea hayo kwa kukujulisha kuwepo kwake, na kila mara anakukumbusha lakini wewe umo kuyasahau, sasa mambo hayo yepi ambayo unaishi nayo lakini hukumbuki chochote, kabla ya kuyataja mambo hayo wacha nikujulishe kitu kimoja kuhusiana na kile unachoambiwa kuona kwa moyo na kutaja kwake, moyo una uwezo wa kuona mara mbili ya mwanzo ni kuhisi(Feeling) na ya pili ni kuona kwa (Pureness)kuondokewa na pazia na unakua (Knower)unajua bila ya kuona huku kwa macho wala kufundishwa, kwa hiyo ukitia sauti ndani ya kujua huko ndio inakua sasa umetaja, na ukinyamaza kimya vilevile bado unaendelea kujua katika njia za ukimya, na yote hayo yamo katika kukumbuka, na kukumbuka huku kuna kua kila wakati na sio mara moja kama ilivyo sasa.
Sasa Ujumbe gani Mollah anatuletea ili tumkumbuke, endelea part 3.

KUMKUMBUKA ALLAH(DHIKR)PART 3

Asalaam Aleiykum

Tuanze na sura ya Mulk aya ya 19 ina siri ndani yake aya hii nataka tuingie ili tuitizame kwa uangalifu wa hali ya juu labda itatupa muamko fulani wa kutuwezesha kupata kitu cha kuweza kutukumbusha Ufalme wa Mollah wetu, aya inasemaje?
أَوَلَمۡ يَرَوۡاْ إِلَى ٱلطَّيۡرِ فَوۡقَهُمۡ صَـٰٓفَّـٰتٍ۬ وَيَقۡبِضۡنَ‌ۚ مَا يُمۡسِكُهُنَّ إِلَّا ٱلرَّحۡمَـٰنُ‌ۚ إِنَّهُ ۥ بِكُلِّ شَىۡءِۭ بَصِيرٌ 
Jee hawawaoni ndege walioko juu yao namna wanavyozinyoosha na kuzikunja(Mbawa zao kwa kuruka)hakuna anayewazuia(Wasianguke)ila (Mwenye enzi Mungu)Mwingi wa Rehma, Hakika yeye anaona kila kitu.
Maneno yalotajwa hapo ni makubwa sana ukiyazingatia, aya imeanza kwa sifa ya kuona aliyopewa Mwanaadamu na sifa hii ya kuona maana yake uzingatie, kama huzingatii kuona kwako hakuna maana yoyote, huna faida ya kuona, yamekua kama macho ya mnyama yanaona lakini hayajui chochote, ndio maana mkaambiwa nyinyi Wanaadamu kwa kuwa nyinyi ni (Special)wateule wa Mwenye enzi Mungu isipokua wewe Mwenyewe uamue kubakia katika unyama hilo shauri lako, lakini kama unataka upande darja katika maisha yako unaulizwa jee huwaoni hao ndege?.
Na huko kuona sio ubakie hapo hapo katika kutizama mbawa zinafunguka na kufungika lazima ujiulize imekuaje hali hii, lazima uyatizame maisha haya ya ndege,ishi japo kwa nusu saa uone ndege vipi anaishi, angalia anaishi kama wewe ila yeye ana njia mbili za kwenda angani na ardhini, yeye ana nyumba kama yako wewe yake inaitwa Mti, ndege huyu anatoka asubuhi kwenda kutafuta Riziki kama utokavyo wewe na kurudi nyumbani kwake kuviletea vitoto vyake chakula, ndege huyu ana mke kama ulivyo wewe na familia yako, anaimba na kuishi na kulala kila uingiapo usiku tafauti yake yeye hendi (Disco)hamuasi Mollah wake, na wakati mwengine hicho chakula unachotupa wewe kwa dharau yeye hushuka kutoka angani akaja kukila hicho hicho, basi jiulize nani mwenye kuwapa uwezo huo wote isipokua yeye Rahmani inatosha ukimuona ndege wakati wote akawa anakukumbusha Mollah wako, na ujumbe wa Mollah wako hauji kutoka kwa Ndege peke yake, ukiona mvua ni ujumbe wake, ukiona Jua ni ukumbusho wake, ukiona Miti ni ukumbusho wake, ukiona Mwezi ni yeye Mwenye kukumbusha kuwepo kwake, ukiona vinyama anakuonesha ufalme wake, ukiona Bahari anakujulisha kuwepo kwake,ukihisi upepo ujue huo ni Ufalme wake, ukiamka una siha nzuri huo ni katika uweza wake,ukikiona chakula mbele yako tambua mpaka unakitia mdomoni ni yeye alokuletea Riziki hiyo, ukiamka unaumwa elewa katika matakwa yake, ukisikia watu wanacheka na kufurahi elewa ni katika uwezo wake, ukisikia sauti za ngurumo za radi au umeme kutokea Mbinguni jua ni katika Mambo ya Uwezo wake, ukiamka na furaha jua Mollah wako kakutakia Furaha hiyo, ukipatwa na msiba jua hili limeandikwa na sasa wakati wake umefika na mimi sina jinsi ila  kuridhia, ukenda kusali elewa Mollah wako kakufanyia hisani ya kukuongoza umkumbuke yeye, Ukimuona Mtu kapotea basi Muombe Mollah wako amuongoze, ukiona wagonjwa wanasikitikia maradhi yao jua wao wameshughulishwa na maradhi na kumsahau yule aliyeyaleta basi waombee kwa Mollah wako, ukenda kulala kumbuka yeye Mollah wako ndio Mwenye kukuletea huo usingizi basi Muage kwa kumwambia Mollah wangu narudi katika Ufalme wako nikirimu mapenzi yako, Ukiamka sema Nashukuru kwa kunipa siku nyengine nikukumbuke wewe na Ufalme wako, basi nakuomba Mollah wangu nikukumbuke kwa kusali kutwa nzima huku nikikutaja wewe moyoni mwangu wakati naendelea na shughuli zangu, wakati naendelea na masomo yangu, kwani kila kilichomo katika Ulimwengu huu ni chako na kinanitosha mimi kukumbuka wewe, nikiona watoto Mollah wangu nakukumbuka wewe, nikiona wazee pia nakukumbuka wewe Mwenye uwezo wa kuona kila kitu, pia nashukuru ukanijaalia kunikirimu kuona huko na mimi Mja wako, basi nakuomba kila nikionacho na kusikia kinikumbushe wewe Mollah wangu uliyeumba kila kitu, nikukumbuke saa na dakika zote katika uhai huu, najua kwa sasa nimefunikwa na mambo ya dunia lakini kwa uwezo wako taratibu naanza kuyatoa na kuujaza ukumbusho wako, basi nakuomba nipe muda wa mimi kuishi mpaka nitakapo yatoa mambo yote ya dunia na ukabaki wewe Mollah wangu moyoni mwangu. 
Kwa hili najua nivigumu kulitimiza lakini kwa uwezo wako Mollah wangu hakuna kisichowezekana, Mollah wangu nakuomba nipe ukumbusho wako kwa kila ninachokiona nikukumbuke wewe na nisahau vile nivionavyo, na hiyo ndio Dhikr na ukiipata ikatulia kwenye Moyo wako basi mpaka siku ya kufa kwako wewe utakua Furahani na bila ya msukosuko wowote.Rabbi tujaalie hali hiyo Aamin.

Sunday, October 19, 2014

UFALME WA SHETANI (IBILIS)PART 1

Asalaam Aleiykum

Nakuletea zawadi nzuri ya maneno yalojaa hekima kama utayatafakari kwa makini na kuyapa uhuru maneno hayo kushuka moyoni mwako basi yatakua ndio mwanzo wa mageuzi yako ya kukufanya kuwa mtu wa Mungu, Ufahamu wako wa mambo ya maisha haya unayoishi utageuka kuwa mwengine kabisa, utakutana na ukweli uso na macho, hiyari itakua yako kuukubali ukweli au kuukataa,hapo utajijua katika falme hizi mbili wewe unaishi wapi, ukishagundua (Kukumbuka) wapi uliko itakua rahisi kwako kupata mafanikio ambayo yatafatia yenyewe baadae.
Kumbuka huwezi kugundua siri ilofichikana mpaka hayo maneno yaende (Deep)kwenye moyo wako neno baada ya neno, kwanza napenda ufahamu nilivyotaja falme mbili nilikua naelekeza Akili yako kwenye jambo fulani, Lakini haiwezekani kabisa katika Ulimwengu huu kuwepo Falme Mbili, Ufalme ni mmoja na ni wake pekee(Subbhanna Allah)Mollah wetu mlezi, ili upate kunifahamu nimekutajia huu Ufalme mwengine ambao ni (Fake) wa Uongo na ndio wengi wetu tumechagua kuishi katika kasiri hii ya (Mwinyi Ibilis).
Sasa tuingie kwenye chanzo cha Darsa yetu hii ya Ufalme wa Shetani kwa kuichukua aya iliyomo kwenye sura ya Al-Aaraf aya ya 16 mpaka 18.
قَالَ فَبِمَآ أَغۡوَيۡتَنِى لَأَقۡعُدَنَّ لَهُمۡ صِرَٲطَكَ ٱلۡمُسۡتَقِيمَ 
"Akasema Kwa kuwa umenihukumu upotofu(Kupotea kwa jeuri yangu)Basi nitawakalia(Waja Wako)Katika njia ilonyooka(Ili nipate kuwapoteza)"
Isije kutajwa njia ukaona labda kuna njia reefu ikisha pana ya kupita, Njia ilonyooka ni ile kanuni ya haki yenye kubainisha Uhalali wa kila jambo katika Dunia hii, Yeye kachukua Ahadi ya kukaa kwenye hiyo halali ambayo nyinyi mnaitaraji ikuvueni kwa usalama katika maisha haya yeye ndio anakwenda kukaa hapo, nini anafanya? kazi ni moja kukusahaulisha na kukufitini na Mollah wako ndani ya hiyo Halali, na rahisi sana kughilibiwa ndani ya huo Uhalali kuliko kwenye hiyo haramu kama tutavoona huko mbele.Kwa sababu ndani ya Halali ni vigumu kugundua kwamba unafanya makosa, ni vigumu kuona kwamba umetoka kwenye Uhalali na unaishi katika Haramu, unatenda yalo ya haramu, umezama kwenye haramu na ufisadi lakini kupitia ndani ya halali, Vipi Mfalme Ibilis Kakaa kwenye njia ilonyooka?
Endelea part 2

UFALME WA SHETANI (IBILIS)PART 2

Asalaam Aleiykum

Anakaa Ibilis kwenye maisha yetu na kutuzunguka katika kila nyanja ya maisha yetu kuanzia kuamka kwetu mpaka kulala kwetu, kama alivyosema.
ثُمَّ لَأَتِيَنَّهُم مِّنۢ بَيۡنِ أَيۡدِيہِمۡ وَمِنۡ خَلۡفِهِمۡ وَعَنۡ أَيۡمَـٰنِہِمۡ وَعَن شَمَآٮِٕلِهِمۡ‌ۖ وَلَا تَجِدُ أَكۡثَرَهُمۡ شَـٰكِرِينَ 
"Kisha nitawafikia kwa mbele yao na nyuma yao na kuumeni(Kulia)kwao na kushotoni kwao, wengi katika wao hutawakuta(Hutowaona)ni wenye kukushukuru(Kukumbuka)"
Wapi ntaanzia ili nipate kuwasahulisha kama wewe umewaumba na unataka kushukuriwa kwa hilo na kukumbukwa, Nimesema anaingia Shetani katika njia za halali, wala si haramu akijua yakini atakushughulisha mpaka umsahau Mollah wako,(1) kwanza anaingia katika ugonjwa wako wa kutafuta mali, huwezi kumkumbuka tena wakati duka umefungua na wateja wanamiminika hivyo kweli unadhani utaikumbuka (Subhanna)migodi ya dhahabu inapasuka unyenyembe huko utakumbuka Mollah kasema nini, Biashara zinatoka unanunua na kuuza utakumbuka kumtaja Mollah wako,uko kwenye mkutano wa siasa unaweza wewe kumsabahi Mollah wako, ofisini unafunga mahesabu unaweza kumkumbuka Mollah wako, haya umekaa barazani hufanyi chochote unaweza kumkumbuka Mollah wako,(Ibilis kazunguka kila pahala, ukiweza kumkumbuka wakati wote ambao umenasa kwenye biashara, maongezi, mikutano ya siasa,ofisini au umekaa barazani au unatizama senema basi wewe moja kwa moja ni mtu wa peponi, ndio maana vitabu vya dini zote vikahimiza kumkumbuka Mollah, vigumu sana kuupata Ufalme wa Mwenye enzi Mungu kwa kuwa Shetani anajua japokua hili ni halali lakini nitatumia njia hii kama silaha ya kuwasahaulisha Mollah wao.
(2)Pili ntawaingia hawa kwenye kadhia ya Mwanamke, kwanza ntamshughulisha huyu Mwanamke awe hana jengine isipokua kuushughulikia mwili wake kwa ajili ya kuutengeneza kwa kujipamba kwa hichi na kile mpaka atakua hamkumbuki Mollah wake kwa lolote isipokua kutaka kuwaridhisha walimwengu wamuone mzuri hususan hawa wanaume, atakua anajipamba huyu usiku na mchana, nitamtia wazimu wa (Shopping)nifisidi kipato chake awe hatoi hata ndururu ya sadaka, na kila akiangalia (TV)yangu hichi kioo ntakua na mwambia bado hujapendeza,Nguo haijabana vizuri, watasemaje kama hutingishiki, itampata shughuli atakua hana muda hata wa sekunde wa kumkumbuka Mollah wake, ikisha nahitimisha kwa Muziki ili nipate kuingia nao kwa urahisi, ndio maana utaona mwanamke akiingia katikati ya ngoma anakatika viuno basi anapata dharau kubwa, sababu hao wenye kushuhudia wanajua huyo tayari kashafukuzwa kwenye Ufalme wa Mwenye enzi Mungu. Na hawa wanaume japokua ni nyendo za halali nitawashughulisha wawe wanamsahau Mollah wao kwa ajili ya kushughulika zaidi na urembo wa mwanamke, kuangalia vifua vyao,kuangalia viuno vyao na kushughulika kuwatafuta mpaka wakawa hawana hamu tena ya kumkumbuka Mollah wao ila wanakumbuka mwanamke(Hiyvo kweli usikie mwanamke anakwita unaweza kumkumbuka Mollah wako), wanamfanyia kazi mwanamke, wanachuma kwa ajili ya mwanamke kutokana na matamanio waliyo nayo, katika viwili hivi ndio yatakua makaazi yangu makuu, nitawasahaulisha hawa hata wakenda kusali basi watakua wanakumbuka mambo yao kuliko kumkumbuka Mwenye enzi Mungu waliyekwenda kumuabudu. halafu nikisha wasahaulisha Mollah wao nitafanya nini?.
Nguvu zikimalizika kabisa,  Familia zao walizokua wanazishughulikia na kuzikumbuka wakati wana afya wakifikia uzeeni kila mmoja anamkimbia hakuna anomsikiliza, wanamuacha peke yake na hakuna hata mmoja mwenye kumthamini hiyo ndio bei tunayolipia hapa hapa Ulimwenguni kwa ajili yakumsahau Mollah wetu, Familia, ndugu, wao ndio wanakuwa wa mwanzo ukiwa unaumwa kupanga mipango yako ya mazishi, Roho hata haijatoka uzuri unaona mtu anapita na sanda, mara karafuu maiti imemdondoka, na wewe upo kitandani wamekusahau kabisa kama ndio ulochuma mali, ndio ulojenga hiyo nyumba, ndio ulokua waziri, ukawa kiongozi wajuu na mtoa hukumu wenzio wateswe,leo Shetani kakumbia kakuacha uwazi wewe na wale ulokua ukiwapa kiupa umbele na kumsahau Mollah wako, leo hawana haja na wewe, yote yale yaliyokua yanakushughulisha yametoweka umebaki wewe na Mollah wako, mpaka Shetani keshakimbia, haji tena kwani huna maana kwake, unarudi kwenye Ufalme wa kweli wa Mollah wako ukiwa Muflis, huna kitu, mali zimerithiwa, mwanamke au mwanamme kaolewa au kaoa hivi ndio sote tunavoishi katika Ufalme wa Shetani Ibilis Ufalme wa udanganyifu. Sasa ukitaka uokoke, uepuke na janga hili la kupotezwa na Ibilis ufanye nini?
Endelea Part 3


UFALME WA SHETANI (IBILIS)PART 3

Asalaam Aleiykum

قَالَ ٱخۡرُجۡ مِنۡہَا مَذۡءُومً۬ا مَّدۡحُورً۬ا‌ۖ لَّمَن تَبِعَكَ مِنۡہُمۡ لَأَمۡلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنكُمۡ أَجۡمَعِينَ 
"Akasema (Mwenye enzi Mungu)Toka humo(Peponi-Mbinguni)hali ya kuwa ni mwenye kudharauliwa na mwenye kufukuzwa, atakayekufata miongoni mwao(Nitamtia motoni) niijaze jahannamu kwa nyinyi nyote"
Limetumika Neno kuijaza Jahannam kwa sababu kama nilvyo sema vigumu kumshinda shetani Ibilis isipokua kama utaweza kuyafanya mambo haya, ili kuweza kumshinda Ibilis na mbinu zake za kukupoteza kwanza inabidi utumie busara yako ya muamko ambao kama utauzingatia utatambua tafauti yako ya siku za utotoni na ujanani, na huu wakati ulo nao pengine wa uzeeni ambao busara zake zinakuonesha mambo wazi wazi pasipo na kizuizi, mfano hakika upo ukijitizama pale ulivopita utotoni bila ya fahamu zozote, umepita ukiwa huna maarifa na Akili imelala kabisa, na sasa umeamka ukawa unaelewa mambo kwa upeo wa mazingatio yakua hili baya na hili zuri,umegundua kumbe mali na vyote nilivyochuma havina maana kwangu, ukagundua siku zangu zinakaribia na huko niendako sichukui chochote, ukagundua mbona moyo wangu una mazito,Na vipi nitaufanya mwepesi tena, mwanzoni ulikua huwezi kupambanua lakini sasa hivi unaweza kutenganisha baya na zuri, haramu na halali na ukitaka kuyafanya unayafanya kwa hiyari yako ilojaa kusudi, kwa hiyo ukiamua kumsahau na kutomuabudu Mollah wako sasa hivi ni kusudi si usingizi tena, ukiamua kushughulikia mali hilo ni tendo la kusudi, ukijifunga na kushughulika na maumbile ya wanawake hilo pia ni kusudio ambalo huambiwi pole na utayapata mateso ya Mwenye enzi Mungu kama alivyosema mwenyewe kuwa ataijaza Jahannam kwa yoyote yule atakayemfata Ibilis, pia na wewe unafukuzwa na kudharauliwa kama nilivosema wa mwanzo kabisa kufanya hivyo Familia yako.
Sasa cha kufanya nini?Al-shuaraa-89 إِلَّا مَنۡ أَتَى ٱللَّهَ بِقَلۡبٍ۬ سَلِيمٍ۬ 
"Isipokua mwenye kuja kwa Mwenye enzi Mungu na moyo safi"
 kupata ukumbusho wa Mwenye enzi Mungu Fanya Biashara, wapende wanawake, lakini fanya bila ya matamanio ya kudumu katika nafsi yako, Fanya Biashara ukiwa huna tamaa ya kupata utajiri, mpende mwanamke lakini usianze kumuabudu ikawa huli hulali,Elewa vitu hivi ni vya muda, halafu ielekeze daima nafasi ilobakia umkumbuke Mollah wako, hapo utakua katika njia ya kati yenye furaha na jaza njema kutoka kwa Mollah wako, hapo utakua Duniani upo na Akhera pia upo, hugandi katika kitu kimoja, ushagundua hakuna kitu cha kudumu, kama Uraisi, ubunge,uwaziri,ubalozi vyote vinapita na kuna siku vyote vitakukimbia na kimoja tu ndicho kitabaki na wewe nacho ni huyo Mollah wako, siku hiyo ikifika utakua na furaha ya kusema Mollah wangu japo nilikua kwenye Biashara, japo nilikua na Mke au Mume wangu lakini wewe ulikua hunitoki moyoni mwangu nikiamini siku hii itafika ya mimi kukutana na wewe kama vile ulivyoniumba mwanzoni, kwa hilo Mollah wangu nakuomba Nisamehe unikaribishe kwenye Ufalme wako wa Kudumu. Mollah wangu leo niko katika Ufalme wako nikiwa kimya mimi na Malaika wako, wakati Mpaka walo wangu wanaogopa hata kulala na mimi chumba kimoja kwa kuwa nimeshakufa, basi mimi sina mwenginewe isipokua wewe Mfalme wa Mbingu na Ardhi na vyote vilivyomo, na kwa hilo Mollah wangu nipokee kwenye utukufu wako hali ya kuwa nimesamehewa na nimeridhiwa kwa kuweza kumshinda Shetani Ibilis mwenye kuwapoteza waja wako.
Mollah wetu tujaalie mazingatio haya yadumu nyoyoni mwetu na tuwe wenye kufanikiwa na kupendwa na wewe Mlezi wetu. Amin

Sunday, October 12, 2014

NINI MAPENZI ?TAQWA PART 1

Asalaam Aleiykum

Nimetakiwa nitoe ufafanuzi  kuhusu darsa zilizopita niliposema (Taqwa) ni Mapenzi nilikua nina maana gani? kuihusisha (Taqwa)na Mapenzi, Ingekua rahisi kwangu kumjibu muulizaji kwa ufupi swali lake hili, lakini kanifunga aliponambia nilete ufafanuzi, sasa pakitakiwa ufafanuzi inakua pengine muulizaji pamoja na wale wengine wasouliza labda hawajui nini Mapenzi?, ndio maana ukatakiwa ufafanuzi ili wajue yana mahusiano gani na (Taqwa).
Sasa nakuchukua katika safari hii ili upate muangaza japo kidogo ikitokea siku nyengine unamwambia mtu neno la kupenda angalau uwe karibu japokua kwa neno, sababu sasa hivi unalitamka hujui hata maana yake, hujui hata kusudio, Nini Mapenzi?.
Mapenzi hayana Tafsiri ila yana ufafanuzi, na ufafanuzi wake ni kama hivi, Mapenzi ni Muujiza unaotoka(Mbinguni)unakuja na (Quality of your Being) au niseme mwenendo wa nafsi yako, na kila kiumbe anayo haki hii ya mapenzi, anaishi katika mapenzi na kinachotizamwa hapo ni hiyo (Quality)ya Mapenzi yake kayaelekezea wapi, tukijua yalipoelemea ndipo tutapata kufahamu ni mahusiano yepi yaliyopo baina ya Mapenzi na (Taqwa).
Mapenzi yanatokana na Mwenyewe Mwenye enzi Mungu, sisi hatuna uamuzi katika jambo hilo, tunachoweza sisi kufanya ni kulikataa hilo penzi kwa njia tunazochagua sisi wenyewe, Nini Mapenzi? Mapenzi ni (Sharing of your Being)ni nafsi ilojitolea kwa njia ya (jihad)ukiniuliza mimi nitakwambia soma sura ya (Baqarah aya 2 na 3)
 ذَٲلِكَ ٱلۡڪِتَـٰبُ لَا رَيۡبَ‌ۛ فِيهِ‌ۛ هُدً۬ى لِّلۡمُتَّقِينَ 
"Hicho ni Kitabu kisicho na shaka na Muongozo kwa wamchao Mungu"(Wenye Mapenzi)
Kitabu hichi wameletewa wale wenye mapenzi ili uwe muongozo wao wa kuepuka maovu(Mabaya)watu hawa kwani wana mapenzi ya aina gani?
ٱلَّذِينَ يُؤۡمِنُونَ بِٱلۡغَيۡبِ وَيُقِيمُونَ ٱلصَّلَوٰةَ وَمِمَّا رَزَقۡنَـٰهُمۡ يُنفِقُونَ 
"Ambao huamini yasoonekana na husimamisha Sala na kutoa katika yale tuliyowapa"
Hiyo ndio (Quality of your Being) imejaa mapenzi ya kile kisichoonekana, Nafsi yako iko kwa ukamilifu wa kile unachoamini kipo na ndicho chenye kukuongoza katika maisha haya na hayo ya baadae,ndio maana Walimwengu wakasema(Love is Blind)kisichoonekana(Usilaumu macho kwa kuwa hakioni jambo hili ulaumu Moyo kwanini mpaka leo haujapenda hichi kisichoonekana, Juta sana kukosa kitu adhimu kama hicho, Ndio maana ukiangalia kwa yule aliyekuwemo kwenye mapenzi kikweli anakua haoni kitu, mnayeona nyinyi watazamaji, mbona anafanya hivi, mbona kaacha kila kitu, hivyo hajui kama anapoteza mali yake, hizo zinakua shida zenu nyinyi lakini yeye kwa wakati ule ana(Enjoy)mapenzi yake(Love is from Beyond)linachukua Mamlaka yote ya kiumbe akawa hana uwezo wowote wa maamuzi, Na ukipata mapenzi ya kumpenda Mollah wako ukapenda dini yako wewe ndio umepata (Taqwa), baada ya kulijua hilo basi wewe huna linalo kushughulisha isipokua kusimamisha Sala, kuwasiliana na Mollah wako asiyeonekana, Na Mollah wako kama utampa mapenzi yako kwa ukamilifu basi atakuonesha Ufalme wake bado ukiwa Hai, Na watu hao kwa kuwa wamejaa Mapenzi basi wao hawana haja tena ya kuvizuia vile wanavopewa na Mollah wao, wana (Share)na yoyote yule iwe mali au nafsi zao kwa kujitolea, hilo ndio penzi (First class)Namba moja, halafu kuna penzi namba mbili(Second Class) Endelea part 2

NINI MAPENZI ?TAQWA PART 2

Asalaam Aleiykum

Al Imran 14
زُيِّنَ لِلنَّاسِ حُبُّ ٱلشَّهَوَٲتِ مِنَ ٱلنِّسَآءِ وَٱلۡبَنِينَ وَٱلۡقَنَـٰطِيرِ ٱلۡمُقَنطَرَةِ مِنَ ٱلذَّهَبِ وَٱلۡفِضَّةِ وَٱلۡخَيۡلِ ٱلۡمُسَوَّمَةِ وَٱلۡأَنۡعَـٰمِ وَٱلۡحَرۡثِ‌ۗ ذَٲلِكَ مَتَـٰعُ ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا‌ۖ وَٱللَّهُ عِندَهُ ۥ حُسۡنُ ٱلۡمَـَٔابِ 
"Watu wametiwa Huba(Mapenzi)ya kupenda wanawake na watoto na mirundi(wingi)wa dhahabu na Fedha, na Farasi wanaotunzwa vizuri, na wanyama na mashamba, na hayo ni matumizi ya maisha katika dunia, na kwa Mwenye enzi Mungu ndiko kwenye marejeo mazuri".
Niliposema tumezungukwa na mapenzi nilikua namaanisha zilivyofanywa Nafsi zetu ni kuishi katika hayo mapenzi, hakuna kosa kabisa, ukiwa hupendi wewe utakua na matatizo, ukiwa hutaki wenzio wapende wewe ndio kabisa unaumwa, hayo mambo yamewekwa na Mwenye enzi Mungu mwenyewe ili mpate kufurahi katika Dunia hii, na ikisha mnapewa taarifa kuwa yapo mazuri zaidi huko Akhera mnaporejea.
Sasa ukiyatizama mapenzi hayo ni (Vipande vipande)umependa hiki au kile, umpenda gari, umependa nyumba, umependa chakula, huko ni kugawika kwa mapenzi, na mapenzi ukiyagawa ndipo yanapatikana matatizo makubwa, mara unampenda huyu mara akipita yule ushampenda huyu umemsahau, kwa hiyo unakwenda na tabia hiyo mpaka mapenzi ulopewa na Mwenye enzi Mungu yanageuka kuwa (Desire) unakua mwenye kutaka kitu kufa kupona, na jambo hilo linakusahaulisha kila kitu, na hapo unakua mwenye kuharibikiwa kabisa, kwa hiyo hilo (Penzi)la (Second Class)huwezi kuliita (Taqwa) kwa sababu lishakuondoa katika kumpenda Mollah wako, unamshirikisha na vitu vyengine, unapenda kila unachokiona, na (Quality)yako inakua (Fragment).
(Taqwa) ni (Unity of Love)ukimpenda Mollah wako vyote vinafatia bila kipingamizi, unakua unapenda kila kitu kwa pamoja, lakini kwa sasa hivi wewe ulivyo unachagua, na kuchagua ndio matatizo yanokufanya usiipate (Taqwa)sasa kama huipati Taqwa, hupati kuyakamilisha mapenzi yako unaamua kufanya nini mpaka kufa kwako? Endelea part 3.


NINI MAPENZI ? TAQWA PART 3

Asalaam Aleiykum

Al-Fajr aya ya 20
وَتُحِبُّونَ ٱلۡمَالَ حُبًّ۬ا جَمًّ۬ا 
Na Mnapenda Mali Pendo la kupita kiasi.
Kitizame kinyanganyiro kinacho kukumba, Mollah anakwita kwenye mapenzi yake, jitizame vipi unavo mjibu, bila kutoa sauti unamuonesha kwa ishara, mimi bado niko kwenye siasa, mimi bado nashughulika kutafuta mali,mimi niko nafanya maarifa vipi nitayamaliza mambo ya watu, mimi najenga majumba, mimi natafutia wake zangu na wanangu Mali, niko mbioni kusimamia mashamba, nakwenda kazini asubuhi mpaka jioni vipi nitakukumbka Mollah wangu, Fulani anaumwa mimi namshughulikia sipati wakati wa kuabudu, nasimamia jengo sina nafasi.
Mapenzi yakuchuma Mali yamekushughulisha huwezi kuyawacha ndio maana ukaambiwa bora "Ngamia ataweza kupita kwenye tundu ya shindano"kuliko wewe afadhali ngamia atakua anafafanya jitihada za kujikunja ili apite, lakini wewe kwanza utatafuta uzi uko wapi uuze kwanza ikisha ndio upite kwenye tundu ya shindano, Mali imekushughulisha sana, hujui tena hata maana ya kupenda, hata penzi likiwa mbele yako unauliza hichi nini?. Kila mmoja wetu kashughulika na utafutitaji wa Mali ikisha ikisha nini? unaziacha Ulimwenguni huendi hata na karatasi ya kusema mimi nilikua na Mali, Mimi nilikua na Majumba na magari, mimi nilikua na viwanja na mashamba, yale yote uliyokua unayashughulikia unayawacha unakwenda mikono mitupu, huja starehe kabisa sababu siku zote ulikua unatafuta na kuilinda mali yako, huku mapenzi yapo pembezoni mwako yanakwambia geuka unipende wewe upate furaha, acha na mambo ya kidunia hayana maana, ukiandikiwa uyapate utayapata, na kama hujaandikiwa basi utahangaika bure, na hayo ndio mapenzi ya hali ya chini kabisa, mapenzi ya mateso, na mifano ipo tazameni matajiri wenu hawana furaha kabisa, sikatai wana (Security)lakini furaha haipo, hawajui kupenda wala kupendwa, na wakipendwa wanadhani huyoo anataka mali yangu, hayo ndio mateso kila mmoja wetu anashindwa kuyaepuka.
Sasa jiulize wewe Mwenyewe ukoje katika kadhia hii ya mapenzi unapenda nini? Unampenda Mollah, au Mpira, Unawapenda watu au kikundi, unapenda Nyumba zako au Mashamba yanakusumbua na faida zake, au una maradhi ya pesa uzione tu ukishajigundua wewe mapenzi yako yamehimili wapi basi anza taratibu kuya(Mix)na kumpenda Mollah wako ili upate hiyo (Unity)ya mapenzi nayo ndio hiyo (Taqwa) na ukipata hiyo ndio umefanikiwa kukubwa na Raha na Furaha zilizopo hapo unatakiwa lazima wewe Mwenyewe upate (Exeperience)hiyo, hutoelewa mtu akikuhadithia, hayo ndio mapenzi katika kipimo chake cha juu kabisa.