Asalaam Aleiykum
Tuanze na sura ya Mulk aya ya 19 ina siri ndani yake aya hii nataka tuingie ili tuitizame kwa uangalifu wa hali ya juu labda itatupa muamko fulani wa kutuwezesha kupata kitu cha kuweza kutukumbusha Ufalme wa Mollah wetu, aya inasemaje?
أَوَلَمۡ يَرَوۡاْ إِلَى ٱلطَّيۡرِ فَوۡقَهُمۡ صَـٰٓفَّـٰتٍ۬ وَيَقۡبِضۡنَۚ مَا يُمۡسِكُهُنَّ إِلَّا ٱلرَّحۡمَـٰنُۚ إِنَّهُ ۥ بِكُلِّ شَىۡءِۭ بَصِيرٌ
Jee hawawaoni ndege walioko juu yao namna wanavyozinyoosha na kuzikunja(Mbawa zao kwa kuruka)hakuna anayewazuia(Wasianguke)ila (Mwenye enzi Mungu)Mwingi wa Rehma, Hakika yeye anaona kila kitu.
Maneno yalotajwa hapo ni makubwa sana ukiyazingatia, aya imeanza kwa sifa ya kuona aliyopewa Mwanaadamu na sifa hii ya kuona maana yake uzingatie, kama huzingatii kuona kwako hakuna maana yoyote, huna faida ya kuona, yamekua kama macho ya mnyama yanaona lakini hayajui chochote, ndio maana mkaambiwa nyinyi Wanaadamu kwa kuwa nyinyi ni (Special)wateule wa Mwenye enzi Mungu isipokua wewe Mwenyewe uamue kubakia katika unyama hilo shauri lako, lakini kama unataka upande darja katika maisha yako unaulizwa jee huwaoni hao ndege?.
Na huko kuona sio ubakie hapo hapo katika kutizama mbawa zinafunguka na kufungika lazima ujiulize imekuaje hali hii, lazima uyatizame maisha haya ya ndege,ishi japo kwa nusu saa uone ndege vipi anaishi, angalia anaishi kama wewe ila yeye ana njia mbili za kwenda angani na ardhini, yeye ana nyumba kama yako wewe yake inaitwa Mti, ndege huyu anatoka asubuhi kwenda kutafuta Riziki kama utokavyo wewe na kurudi nyumbani kwake kuviletea vitoto vyake chakula, ndege huyu ana mke kama ulivyo wewe na familia yako, anaimba na kuishi na kulala kila uingiapo usiku tafauti yake yeye hendi (Disco)hamuasi Mollah wake, na wakati mwengine hicho chakula unachotupa wewe kwa dharau yeye hushuka kutoka angani akaja kukila hicho hicho, basi jiulize nani mwenye kuwapa uwezo huo wote isipokua yeye Rahmani inatosha ukimuona ndege wakati wote akawa anakukumbusha Mollah wako, na ujumbe wa Mollah wako hauji kutoka kwa Ndege peke yake, ukiona mvua ni ujumbe wake, ukiona Jua ni ukumbusho wake, ukiona Miti ni ukumbusho wake, ukiona Mwezi ni yeye Mwenye kukumbusha kuwepo kwake, ukiona vinyama anakuonesha ufalme wake, ukiona Bahari anakujulisha kuwepo kwake,ukihisi upepo ujue huo ni Ufalme wake, ukiamka una siha nzuri huo ni katika uweza wake,ukikiona chakula mbele yako tambua mpaka unakitia mdomoni ni yeye alokuletea Riziki hiyo, ukiamka unaumwa elewa katika matakwa yake, ukisikia watu wanacheka na kufurahi elewa ni katika uwezo wake, ukisikia sauti za ngurumo za radi au umeme kutokea Mbinguni jua ni katika Mambo ya Uwezo wake, ukiamka na furaha jua Mollah wako kakutakia Furaha hiyo, ukipatwa na msiba jua hili limeandikwa na sasa wakati wake umefika na mimi sina jinsi ila kuridhia, ukenda kusali elewa Mollah wako kakufanyia hisani ya kukuongoza umkumbuke yeye, Ukimuona Mtu kapotea basi Muombe Mollah wako amuongoze, ukiona wagonjwa wanasikitikia maradhi yao jua wao wameshughulishwa na maradhi na kumsahau yule aliyeyaleta basi waombee kwa Mollah wako, ukenda kulala kumbuka yeye Mollah wako ndio Mwenye kukuletea huo usingizi basi Muage kwa kumwambia Mollah wangu narudi katika Ufalme wako nikirimu mapenzi yako, Ukiamka sema Nashukuru kwa kunipa siku nyengine nikukumbuke wewe na Ufalme wako, basi nakuomba Mollah wangu nikukumbuke kwa kusali kutwa nzima huku nikikutaja wewe moyoni mwangu wakati naendelea na shughuli zangu, wakati naendelea na masomo yangu, kwani kila kilichomo katika Ulimwengu huu ni chako na kinanitosha mimi kukumbuka wewe, nikiona watoto Mollah wangu nakukumbuka wewe, nikiona wazee pia nakukumbuka wewe Mwenye uwezo wa kuona kila kitu, pia nashukuru ukanijaalia kunikirimu kuona huko na mimi Mja wako, basi nakuomba kila nikionacho na kusikia kinikumbushe wewe Mollah wangu uliyeumba kila kitu, nikukumbuke saa na dakika zote katika uhai huu, najua kwa sasa nimefunikwa na mambo ya dunia lakini kwa uwezo wako taratibu naanza kuyatoa na kuujaza ukumbusho wako, basi nakuomba nipe muda wa mimi kuishi mpaka nitakapo yatoa mambo yote ya dunia na ukabaki wewe Mollah wangu moyoni mwangu.
Kwa hili najua nivigumu kulitimiza lakini kwa uwezo wako Mollah wangu hakuna kisichowezekana, Mollah wangu nakuomba nipe ukumbusho wako kwa kila ninachokiona nikukumbuke wewe na nisahau vile nivionavyo, na hiyo ndio Dhikr na ukiipata ikatulia kwenye Moyo wako basi mpaka siku ya kufa kwako wewe utakua Furahani na bila ya msukosuko wowote.Rabbi tujaalie hali hiyo Aamin.
No comments:
Post a Comment