Sunday, March 22, 2015

NDANI MCHA MUNGU NJE MCHA MUNGU PART 1

Asalaam Aleiykum

Maombi na huruma zangu Mollah wangu ni kuwaombea wale Masheikh wangu na ndugu zangu Waumini wenzangu na mimi Mwenyewe pamoja na Waislam wenzangu walokua hawafahamu maana halisi ya Ucha Mungu, Mollah wangu wafikishie Rehma ya Kufahamu wote kwa jumla.
Watu wamekua wamo katika ubabaishaji wa kudhani kuwa ukiwa unavaa vazi fulani au unatenda mambo fulani kwa ajili ya Allah basi huo ndio Ucha Mungu, Ikazama dhana hii mpaka kuwaona wale wenye kuishi maisha ya kawaida na kufata Amri za Mwenye enzi Mungu hao hawana nafasi kwa Mollah wao, mpaka uwe una kitu cha ziada cha kukuonesha wewe tafauti na wengine ndio unakua Mcha Mungu. Vimekithiri Viburi hivi hassa kwa wale wenye kudhani wako karibu na Mollah wao zaidi kuliko wengine, hivyo ndio kiburi kifanyavyo kazi yake, ikampitikia Mtu katika Akili yake kuwa yumo kwenye nyumba za Ibada, au wanatenda mambo ya Khairat basi huo ndio ucha Mungu, Shetani katumia Fursa hii kuwafunika kwa Mwanvuli wa upotofu wa Kiburi mpaka kufikia kuwatoa katika Dini pasi wenyewe kujijua.
Imefikia hali kama hii pengine kutokana na uchache wa kujua, au ubishi wa kutotaka kufahamu, au ndani ya moyo kuna mizigo mingi ndio maana Ucha Mungu hauna nafasi ya kukaa. Nawaona watu wengi sana wanasumbuliwa na hali kama hii, lakini kwa kuwa ni siri ikaayo ndani hakuna mwenye kutaka kuisema.
Kwa hiyo Mimi kazi yangu daima ni kukuonesha njia, ikisha una hiyari yako mwenyewe kuifata au kubaki kama ulivyo sasa. Kujua vipi utaupata Ucha Mungu wa ndani, halafu uupate na wa nje  inabidi nikuchukue twende tukayahudhurie maneno matatu yalosemwa ndani ya Quraan, Yamesema Nini?.
Kwanza kabisa katujua kwamba sisi sote Ima wafanya Biashara au Wanasiasa, kwa hiyo akaanza maneno yake kwa kututega, sasa kama wewe unakula pesa za Msikiti, au unakula pesa za Umma, au unavamia kufilisi mali za Yatima, au unajifanya (Tabibu) unaponesha watu kwa kuwaombea kwa kuwadanganya na kuchukua pesa zao ukiwa huna hakika na ufanyacho, Huku unajikita kuamini unafanya mambo ya kheri, basi Nabii Musa a.s kakugundua udhaifu wako huo ndio akaanza maneno yake ambayo nataka uyasikize kwa uzuri huenda yakaleta faida kubwa katika safari yako ya kuutafuta Ucha Mungu.
Endelea part 2

NDANI MCHA MUNGU NJE MCHA MUNGU PART 2

Asalaam Aleiykum

 يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ هَلۡ أَدُلُّكُمۡ عَلَىٰ تِجَـٰرَةٍ۬ تُنجِيكُم مِّنۡ عَذَابٍ أَلِيمٍ۬ 

"Enyi Mloamini Nikujulisheni Biashara mtakayofanya na Mollah wenu" Ili Muepuke adhabu iumizayo ya Mwenye Enzi Mungu.

Vipi iwe jambo hili wameambiwa Waumini? Kwanini isiwe wasoamini, Wale wenye kutenda Dhanmbi, kwanini iwe nyie mlokwisha amini? Kwa sababu unajulikana Udhaifu wetu, tunajulikana tumevaa majuba tumo kwenye Nyumba za Ibada lakini vifuani watupu, Ndani hakuna chochote(Debe Tupu) ndio tukaambiwa Jambo la mwanzo sasa" Muaminini Mwenye enzi Mungu",(Nini Tafauti ya Imani na kuamini) Kuamini ni jambo la urahisi sana, unaambiwa kitu unakubali(Hivyo ndivyo mlivyo sasa).
Lakini Imani ni kitu chengine kabisa, lazima ufanye mambo ndio Imani ipate kukuamini, Kwa sababu Imani ni (Double Arrow) Toa upewe, Nini Imani? (Mfano wa Imani) ni mapenzi, sina shaka sote tushaonja (Ladha) ya Mapenzi, lakini mapenzi ninayozungumza hapa ni ya aina nyengine kabisa, sio yale ya kawaida ya kila siku, haya ninayozungumza mimi kama yatakushukia moyoni ndio huo (Ucha Mungu).
Sasa hivi huna kitu kama hicho, Ndio unajaribu sikatai, lakini moyoni kuna mapenzi (Fake)yamejazana, unapenda mali, umejaa kiburi na tamaa, mapenzi ya uhasidi yamo humo, mpaka usafishe moyo wako mambo yote ya ujanja ujanja ulio nao, na uwe mweupe moyoni ndio mapenzi ya Allah yanapoanza kuteremka, Ndio Ucha Mungu unachukua nafasi yake. Unakua huna haja tena ya watu wakujue una Iman, au wewe Sheikh, unakua unajijua mwenyewe kilichomo ndani ya nafsi yako.
Nini kinatokezea ukiipata hali kama hiyo? Furaha juu ya furaha, zawadi tele zinateremka kutoka kwa Mollah wako(Bashara chungu nzima unazipata kutoka kwa Mollah wako) Watu watavutika na wewe kwa kutaka kuwa karibu na wewe, lakini kwa hivi sasa bado huna Ucha Mungu wa ndani, bado haujajitokeza, bado Imani haijashuka, bado huna ukaribu na Mollah wako, hujapata kujua dalili zozote, mawazo yako na fikra zako zote zimezama kwenye mali, kwenye pesa, kwa watoto, ndugu na hivi na vile, mapenzi yako umeyagawa mafungu robo hapa, robo pale.
Hebu Jitizame kama una chembe ya Ucha Mungu, akija Mlevi kukuomba shilingi ya kula, jione unakua vipi? Unavaa taji la hakimu, unaanza hukumu zako, au akujie (Mlemavu)unasema huyu kazidi  kuomba, lakini Mcha Mungu wa kweli akiombwa anatoa halimjii wazo lolote baya au zuri, hataki hata kujua huyu nani na dini gani, Moyoni kajaa mapenzi anajua moja kwa moja mja huyu katumwa na Mollah wangu ambaye anawapa wanomuamini na wasiomuamini, walevi na wacha Mungu, wasomuabudu na wenye kumuabudu, mie kama nani nipitishe hukumu yangu.
Ikikujia hali kama hiyo na kuweza kupambambanua  na kujua Qadar ya Mollah wako za kheri au za shari, ikawa unaridhika kujaribiwa kwa Mitihani na Mollah wako, Na kila ukijaribiwa wewe unazidisha mapenzi juu yake, hulalamiki wala hununguniki, huna hasira wala kuhamaki, ndio kwanza unazidisha shukurani, hapo wewe tayari ushamiliki(A loving heart) Ucha Mungu tayari, Unayo hiyo Iman, ukishapata hilo jambo la kwanza, ndio sasa unaruhusiwa uende kwenye jambo la pili, Kwa sababu sasa hivi ushakua na mapenzi ya Mollah wako, Na Mwenye Mapenzi hamkeri mpenzi wake, huwezi kutenda kero kwa Mollah wako wala kwa viumbe wenzako, sababu ushakua Mcha Mungu.
Inakua vigumu kwako kutenda dhanmbi kwa kusudi, haiwezekani tena Mcha Mungu akatenda maasi ya jambo lolote lile.
Endelea part 3




NDANI MCHA MUNGU NJE MCHA MUNGU PART 3

Asalaam Aleiykum

Sasa ukisha kamata ngao yako ya Imani ndani ya moyo wako, Ndio unaruhusiwa nenda sasa kakamate pesa za msikiti, angalia kwa uangalifu pesa za maskini, simamia mali za yatima, tena huyo (automatic) wewe mwenyewe unaingia katika aya inayofatia ya 11 sura ya (Saff) mpaka mwisho wa aya.
"تُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَرَسُولِهِۦ وَتُجَـٰهِدُونَ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ بِأَمۡوَٲلِكُمۡ وَأَنفُسِكُمۡ‌ۚ"
Muaminini Mwenye Enzi Mungu na Mtume wake, na piganieni (kwa)Njia ya Mwenye Enzi Mungu kwa Mali zenu na nafsi zenu.
Moyo wa mapenzi desturi yake ni kutoa, Njia ya Mwenye enzi Mungu kutoa huko kuwe kwa njia ya kheri na wala sio ya shari, kutoa kwenyewe uwe hujali, au kuwa na khofu kwamba ukitoa utafilisika, Unawapa maskini,Unawapa majirani, Mayatima, wale wasojiweza wanopita njia wakakuomba.
Na kama huna basi unajitolea nguvu zako, unajitolea mawazo yako na kila ulichonacho, hiyo ndio maana ya kujitolea kwa njia ya mali, halafu tena unaingia katika hilo jambo la tatu, nalo ni hiyo Nafsi yako. Wewe unaishi kwenye jamii, Na katika Ulimwengu wa jamii kuna kila kitu ndani yake, kuna kila majambo yanatendeka, kuna kila uchafu, na wewe unajulikana unaishi humo, hujaambiwa Jiue au hama au ondoka au kimbia, umepewa (Challenge)Pigana na nafsi yako kule moyoni bakia vile vile na Ucha Mungu wako, usiteteruke, huo ndio Ucha Mungu, hiyo ndio (Jihad) ya Nafsi.
Hapa itabidi nikupe (Hadith njema) ili upate kujua vipi unabakia ndani ya nafsi yako na Ucha Mungu katika Ulimwengu huu tunaoishi hivi sasa. "Kuna Mwanafunzi Mmoja alimwambia Sheikh wake mimi nina hamu kubwa ya kumjua Mcha Mungu, naomba nifahamishe dalili zake nipate kujua yukoje,"" Sheikh akamwambia nenda kwenye Mji fulani utamkuta Tajiri katika mji huo mwambie mimi nimekutuma ukalale kwake siku moja","Akatoka yule kijana mpaka kwenye ule Mji na kumkuta yule tajiri akamwambia Sheikh kanituma nije kwako nikae siku moja na wewe""Tajiri akampokea kwa uzuri yule Mwanafunzi akaamrisha mgeni afanyiwe takrima kubwa, Ulipofika usiku watu wakaimba na kucheza, yule Mwanafunzi akashangaa sana, akawa kila saa jicho lake liko kwa yule Tajiri, ambaye anamkuta kimya na tasbih yake mkononi anavuta uradi wake. Ulipofika wakati wa kulala akapelekwa chumbani kwake katika ile njia ya (Sebule)ukumbini akakuta mapambo ya kila aina, alipofikishwa chumbani kwake hakukuta kitu chochote ila kitanda kimoja tu, alipopanda kitandani kutizama juu ya (Dari)akakuta upanga unaninginia sawa na kitovu chake, wakati wowote unaweza kuanguka, Yule Mwanafunzi hakulala usiku kucha anautizama ule Upanga usije kumuangukia,  khofu ya kufa imemtawala.
Ilipofika asubuhi akamfata yule tajiri na kumuhadithia ule mkasa wa upanga, Yule tajiri akamwambia niliona mshangao katika macho yako, na hukumu ulizokua unapitisha juu yangu, na kiburi ulichokua nacho cha kunibeza mimi na kujiuliza uwapi Ucha Mungu wangu, nikaijua akili yako inasema uwapi Ucha Mungu wenyewe, ndio na mimi nikakuwekea Alama ile ya Upanga, ili uwe macho usiku kucha, tizama ulivo (Feli)baada ya kumkumbuka Mollah wako umeukumbuka upanga, Basi kwa hiyo haya mambo uliyoyaona na ule upanga ulivokuweka macho usiku kucha ndio hali nilonayo mimi, Nilitaka kukujulisha na mimi Uradi wangu wa kunikumbusha mauti unaniweka macho siku zote simsahau Mollah wangu, Yote unayoyaona yanaendelea katika Jumba langu hili hayanishughulishi kitu, mimi ndani ya moyo wangu kajaa Mollah wangu, Na nje pia namuona Mollah wangu, tafauti yangu naishi kwenye ulimwengu wake na haya yote yanatendeka kwenye Uangalizi wake, Siri yangu kubwa mimi naishi kama sasa hivi nitakufa" Na hiyo ndio (Jihad) ya Nafsi, hiyo ndio Imani, huo ndio Ucha Mungu wa ndani na Nje.Yoyote yule anayekumbuka Mauti ndiye Mcha Mungu wa kweli, kwani kuyakumbuka Mauti ni kuwa karibu na Mollah wako, na kuyasahau Mauti ni kuwa karibu na Dunia  hii na machafu yake, na ndio sababu ya kumsahau Mollah wako.
Najua unataka kujua vipi upate hali kama hiyo, nasema tena na tena kuna mambo matatu ya kufanya ili upate huo Ucha Mungu la kwanza(1)Jishughulishe sana na (Prayers) maombi ya shukurani kwa wingi, jambo la pili(2)(Worship)tekeleza kwa wingi matendo ya Ibada na jambo la (3)(Devotion) kwa njia ya (Dhikr)kumkumbuka sana Mollah wako kila saa na dakika halafu mwachie mwenyewe atakuteremshia Ucha Mungu wa ndani na nje, lakini sio kwa kutaka wewe ila kwa kutaka yeye Mollah wako Muumba wa kila kitu. Mollah wetu tujaalie katika waloridhiwa na wewe, utukusanye pamoja na waja wema, utupe waja wako huo Ucha Mungu wa ndani na nje ili tupate kukushukuru usiku na mchana kwa uweza wako wa kila jambo na kutujaalia sisi utukufu huu wa Uhai.


Sunday, March 15, 2015

AINA TATU ZA VIFO PART 1

Asalaam Aleiykum

Siku zote nimekua nashangazwa na jinsi gani Mawalii (Mystic)Wacha Mungu wanavo yakabili Mauti wakiwa hawana hofu, hujiuliza kuna kitu gani kinacho wapa matumaini mpaka kufikia kuaga, "anasema Mcha Mungu sasa basi msinipe dawa nimebakisha siku moja, Nyinyi msinitese tena kwa chakula kwani sina muda tena wa kuwa na nyinyi, na mwili wangu ushafungika haupokei tena hata maji, Na hadith nyingi ambazo kwa sasa ni mara chache sana kuzisikia.
Leo wako wapi wale walokua wakiaga nakwenda zangu kwenye dongo langu (Kufia)Mombasa, Wako wapi leo walofunga mizigo yao na kusema nakwenda kuzikiwa (Comoro), Wako wapi leo wale kwa makusudi anasema nikatieni (Ticket) mimi ntazikwa (Yemen).
Hakuna tunacho kiona katika (Generation) hii ila khofu kubwa ya Mauti, Nini kimetokezea?, Ni kweli isiyo shaka kwamba Mauti ni jambo zito sana, kishindo chake si kidogo, Roho haijawahi kushuhudia tukio kama hilo, Kiza kinene katika (Operation) hiyo kubwa ambayo kila mmoja wetu hana budi kupita katika (Theatre) ya Mauti.
Wengine inawachukua (Week), wengine mwezi mzima Roho kutenganishwa na kiwiliwili(Body) wale walokua hawajui kadhia hii wataona kama hadith lakini madada zetu waliopo (Hospital) manesi wanavijua vishindo hivi wanavokabiliana navyo kila siku, na yoyote mwenye kupinga na aende akashuhudie kadhia hii, atarudi na kusema kumbe kweli wanayosema si mchezo jamani Mja kutolewa Roho.
Hali hii ya kutolewa Roho imetajwa ina wakabili watu wa aina tatu katika sura ya (Waqia aya ya 88 mpaka 95)(فَأَمَّآ إِن كَانَ مِنَ ٱلۡمُقَرَّبِينَ)
Kundi la (1)
Ikiwa katika Maisha yako ulikua karibu na sisi kwa matendo mema na yaliyo mazuri, Na ukawa na mapenzi na sisi, ukajua ya kwamba yupo alokuumba na anastahili kukumbukwa na kuabudiwa na kushukuriwa kwa kila saa na dakika, Basi wewe kabla ya kufa kwako utapata Fahamu ya kujua alaa kumbe Mauti na Uhai ni kitu kimoja hakuna mushkeli, na siwajibiki mimi kuogopa, tena na siku ya kufa kwako unafurahishwa kwa manukato mazuri mazuri na pepo unaoneshwa mbele yako, unawekewa wazi kule ndipo unapokwenda, hapo unakua tayari kuondoka bila ya mashaka katika (Body) yako wala hunganganii tena kubakia katika Ulimwengu huu, unakwenda bila ya ushindani ukiwa umeridhia huku umekubali kurudi kwa Mollah wako kwenda kupumzika katika (Jannat Firdous)uko radhi sasa kwenda kukutana na wale waja wema walo kutangulia kabla yako.
Endelea part 2.

AINA TATU ZA VIFO PART 2

Asalaam Aleiykum

(وَأَمَّآ إِن كَانَ مِنۡ أَصۡحَـٰبِ ٱلۡيَمِينِ )
Na kama Ulikua Mwenye (Imani) basi salama itakua juu yako, kwa sababu (Imani) ni (Mapenzi) na mwenye mapenzi hatendi mabaya abadan, Lakini kuamini kwenyewe isiwe umekubali kwa kuwa umezaliwa ndani ya (Uislam) basi iwe umeamini, sio kwa kufata kundi kwenda Msikitini, Kuamini kwenye kunatakiwa kuwe katika Uhai wako, ushapata kitu katika moyo wako tayari kina kuongoza kwa Mollah wako.
Sio Imani ile ukiguswa ukucha ushamsahau Mollah wako, Mambo yakenda vibaya unatafuta Mtu akusafishie nyota, ukipatwa na misukosuko mara ushatoka dini, Imani inayotajwa hapo ni ile ya juhudi uliyoifanya kuwa karibu na Mollah wako, vipi ulikua unaubeba ukumbusho wa Mollah wako wakati wa kula na kunywa, jee ulikua ukimtaja wakati wa kulala na kuamka kwako, Jee alikuwepo moyoni Mollah wako wakati ukizungumza na kukaa kwako kimya?, Jee Imani hiyo ilikutupa kwenye kuwakumbatia Mayatima na Maskini, ilikua nini tabia yako pale alipokujia muombaji ukitoa kwa unyenyekevu au ulikua ukinyanyua midomo kwa dharau.
Imani yako hiyo ilikupelekea kuwasaidia Wajane, kuzishukuru neema zetu, vipi hali yako ilikua wakati ule tulipokupa Baraka za afya ulifanya vitendo gani vya kheri vyenye kuhusiana na Imani, Jee uliwasaidia wazee na watoto, ulijitolea nguvu zako kuinufaisha jamii ilokua karibu yako, Imani yako ilikufanya uishi vipi na Walimwengu wenzio, ulijua kwamba wanastahiki heshima, huruma na haki ya Ulimi wako, kutowasingizia mambo ya uongo ili waadhibike, Na kama uliyaamini maneno yetu tuliyoteremsha katika kitabu basi leo yakabili Mauti kwa salama, ondoka katika Mwili wako bila ya matatizo au mashaka yoyote.
Endelea part 3.

AINA TATU ZA VIFO PART 3

Asalaam Aleiykum

(وَأَمَّآ إِن كَانَ مِنَ ٱلۡمُكَذِّبِينَ ٱلضَّآلِّينَ )
Ama kama ulikua katika wale walokadhibisha, ukawa kwenye udhalimu, basi leo hasara ilioje, waliokuzunguka kitandani wanaona uko salama, kumbe ndani una jungu la maji ya moto kidogo kidogo umepewa ulimalize ndio Roho itoke, Kama itatokea uachwe peke yako japo kwa muda kidogo watu waende nje kwa mapumziko, wakirudi wanaweza kurejea wakakukuta ushameza shuka ya kulalia yote. 
Utatamani wakati huo itolewe (Pipe) ikatiwe baharini ili upate kuikata (Kiu) Na kama hakuna maji basi unaweza kumeza (Jora) zima la kitambaa upate japo ubaridi kwa wakati ule, Wakati ule hata ukikamata chuma basi kwa machungu yake unaweza kukipinda kwa jinsi ya machungu ya Roho inavotolewa, Macho yanakaribia kuruka kwa jinsi yalivotoka na dhiki unayoonjeshwa kuondoka kwako Ulimwenguni, Walokuzunguka machozi yanawatoka kwa taabu inayokufika, huku wanamaliza (Doti) za khanga kukufuta majasho yanomiminika kama mvua, na kama umeachwa peke yako wanakukuta chini ya uvungu wa kitanda unamkimbia (Malaika wa Mauti)
 قُلۡ يَتَوَفَّٮٰكُم مَّلَكُ ٱلۡمَوۡتِ ٱلَّذِى وُكِّلَ بِكُمۡ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمۡ تُرۡجَعُونَ 
(Sema; Atakufisheni Malaika wa Mauti aliyewakilishwa kwenu, ikisha mtarejeshwa kwa Mollah wenu).
Yote haya yanakukuta kwa sababu ulipokua na Afya na nguvu zako ulikua hutaki mambo ya Mungu, hutaki kusikia hadith za Akhera, ukitajiwa mambo ya Dini unakunja uso au unacheka kuona upuuzi gani huu, pesa zako hazitoki ila kwenye mipira na pombe na anasa zengine, maskini hawana haki katika kipato chako, Mayatima hata nyuso zao huzitizami, maskini wanalala na njaa huku wewe ukinunua nguo mpya, dhahabu hazikutoshi, unapita kubadilisha na kuongeza magari, akikuuliza hali maskini unakereka, ulikua katika hali ya kuwafitini wenzio, kuwadhulumu na kuwasingizia mambo yasio ukweli, ulikua ukidhulumu nafsi za wenzio ili upate mafanikio ya kidunia, leo hii Hakimu wa Haki anaamrisha uyakabili mauti ukiwa katika hali ya mateso makubwa ili iwe ishara yako ya hayo makubwa zaidi unayokwenda kukutana nayo, ingia katika shimo lenye kiza kinene ukiwa huna muokozi, na hiyo ni yakini isiyo na Shaka. Tunamuomba Mollah wetu atunusuru na hali kama hiyo kwa kutusamehe na kutupa uongofu kabla ya kukutana na siku hii.

Sunday, March 1, 2015

FUNGUO 99 ZA IMANI PART 1

Asalaam Aleiykum

Utakapo kaa peke yako usione haya hebu jiulize Imani ni kitu gani?, Jee mimi ninacho kitu hicho kiitwacho Imani?, Angalia sana kifuani mwako useme mbona mimi Nasimamisha(Sala)siku zote, Najaribu kuwa msafi nisifanye Dhanmbi, lakini hayo yote nayatenda huku moyoni nikiwa mtupu, Hata nikitoa sadaka natoa ima nipate picha au watu wanishuhudie kuwa mimi mtoaji na mimi ni mfanya mema, lakini hakuna chochote chenye kutokea katika nafsi ya moyo wangu.
Walisema Waarabu tumeamini, Wakajibiwa(Quraan sura ya Hujraat aya ya 14)
"قَالَتِ ٱلۡأَعۡرَابُ ءَامَنَّا‌ۖ قُل لَّمۡ تُؤۡمِنُواْ وَلَـٰكِن قُولُوٓاْ أَسۡلَمۡنَا وَلَمَّا يَدۡخُلِ ٱلۡإِيمَـٰنُ فِى قُلُوبِكُمۡ‌ۖ وَإِن تُطِيعُواْ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُ ۥ لَا يَلِتۡكُم مِّنۡ أَعۡمَـٰلِكُمۡ شَيۡـًٔا‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ غَفُورٌ۬ رَّحِيمٌ"
"Walisema Waraabu(Wakao Majangwani)Tumeamini, Sema (Uwaambie)Hamjaamini, Lakini semeni tumesilimu, Maana Imani haijaingia vyema Nyoyoni mwenu bado, Na mkimtii Mwenye Enzi Mungu na Mtume wake, hatakupunguzieni chochote katika vitendo vyenu, kwa yakini Mwenye Enzi Mungu ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa Kurehemu".
Wewe hujasema lakini bado uko kwenye Jangwa la saruji, Umekubali leo pengine mwaka wa arobaini bado Imani haijaingia, usije ukanyanyuka na kusema mimi nishaamini, Imani ni kitu chengine kabisa ambacho kinatokezea kwenye Moyo.  Utajiri uko wa aina mbili wa kwanza ni ule wa Nje ambao kila mtu anauona wa magari, majumba, dhahabu na kadhalika, na ule wa pili ni wa ndani ambao ni wa thamani zaidi na huo ndio hiyo Imani.
Na dalili za hiyo Imani zina mfano kama wa (Mapenzi na Afya), sasa kama unajua nini Mapenzi na nini afya basi utakua tayari kujua nini Imani, Napenda kukufahamisha ikiwa utaupata utajiri huu wa Imani basi hakuna chengine chochote chenye kuweza kukushughulisha, hata mtu awe na utajiri wa aina gani wa mali basi utachofanya kikubwa ni kumcheka. Lakini kwa sasa bado usihangaike huna hicho kitu kiitwacho Imani, wewe umezaliwa tu kwenye dini umekuta watu wanafata na wewe umefata, umesomeshwa umejua kidogo kusali lakini huna taaluma ya hiyo Imani, ipo kwako kwa njia ya maandishi na bado haijafika moyoni.
Sasa umefika wakati na wewe kukipata kitu hichi ndio maana nakuletea funguo hizi 99 ili upate kuzitumia kuufungua huo moyo wako.
endelea part 2

FUNGUO 99 ZA IMANI PART 2

Asalaam Aleiykum

Kitu hichi Imani ndicho alokitaja Nabii Issa a.s  kama utakipata ndani ya moyo wako "Basi unaweza kuwambia Mlima sogea ukasogea" Unaweza kumwambia mtu pona akapona, "unaweza kusema leo hapa Meli haiondoki na haitoondoka" Hiyo ndiyo Imani kama utakua nayo watu wengi watavutika kwako, kwanini nikasema wanavutika kwa sababu pia wanavutika kwa tajiri wa Mali, kwa hiyo na wewe kwako watavutika kwa sababu ya utajiri ulio nao ndani ya nafsi yako, kila mmoja ataona yeye unampenda zaidi kuliko mwenzake, Sasa vipi kinapatikana kitu hichi ikiwa una haja nacho?.
Ndio unakutana na hizo funguo 99 za Imani ili uchague mwenyewe ipi ita (Unlock) moyo wako, funguo gani inafaa ili uitumie, Nilipoandika darsa ya (Uradi wa Dhikr ya kumtaja Mollah) wengi hawakufahamu nini ilikua makusudio yangu, sasa nimeleta hizi funguo 99 ili na wewe upate kuwasha hiyo Taa ilozimika Moyoni. Mimi nina hakika baada ya kuzijaribu funguo hizi 99 lazima iko moja itafungua moyo wako, iko hiyo moja itawasha Taa katika nafsi yako, Na taa ikiwaka baada ya hapo wewe ndio utakua shahid, wewe ndio utajua faida yake lakini kikubwa kinachotakiwa ni hio juhudi na bidii ya kukumbuka hilo jina ambalo litakua ndio ufunguo wako.
Na hiyo Imani ikishajaa Moyoni mwako wewe ushakua tajiri mkubwa kuwapita matajiri wote walokuzunguka, ndio maana utaona "Alexander the Great" alipokua kalala kwenye kitanda na Mauti yashamsogelea akawaambia wasaidizi wake nataka nitakapo kufa mkanitia kwenye jeneza muache mikono yangu inaninginia na kuonekana nje ili halaiki ya watu waione hata "Alexander" na Mali zote na kuiteka kila nchi anaondoka mikono mitupu.
Kaa ukijua hayo ma(Plastic)unayo kusanya, hizo Funiture na makaratasi unayo rundika (Bank) vyote ni vya kupita kwenye Ulimwengu huu havina maana kabisa, Na siku ya kuondoka kwako na wewe utachagua ama utudanganye mikono ifichwe ndani ya jeneza au na wewe utaomba ininginizwe kama "Alexander" chaguo ni lako.
Lakini utakapo pata utajiri huo wa Imani basi mara moja utakuachisha Rushwa, dhuluma, tamaa ya mali, choyo na uchu wa cheo, sasa kitu chenye kukuachisha hayo yote kinakupa nini badili yake?.
Endelea part 3

FUNGUO 99 ZA IMANI PART 3

Asalaam Aleiykum

Kabla ya kukufahamisha nini ufanye, kwanza wacha nikupe mfano wa matumaini ili usije kuona kazi ambayo utaifanya haina faida na wewe, Faida ipo tena kubwa sana ambayo ukiipata utadumu nayo mpaka mwisho wa uhai wako. Wacha tutoke kidogo kwenye darsa hii ya Imani na tuhudhurie jambo la kina(Mama)linalohusiana na (Eda), Nini Eda kwa lugha ya urahisi wa kufahamu eda ni (Cooling off period)ambayo ina maana mbili moja ya nje ni ile ya kujua tukio la Uja uzito, na maana ya pili ni ile ya ndani ya (Communion)ambayo ni ya (Let it go) au kipindi cha mpito wa pozo la moyo(Kusahau)au kitu kukutoka kwenye moyo wako.
Ndio maana utaona inapatikana katika mambo mawili moja ni la kufiwa au kupewa talaka, na haya kapewa Mwanamke sababu yeye Mwanamke mambo yake yote anapeleka moyoni tafauti na Mwanamme ambaye mambo yake yote yanabakia kichwani,( ndio maana utaona hata akiambiwa tufunge macho tuchukue ahadi kama tutakua pamoja daima, basi mkifunga macho Mwanamme haamini anafungua jicho moja, lakini mwanamke yeye anaamini moja kwa moja hana sababu yakuweka jicho moja wazi, litakalo tokea mbele lolote atalikabili) kwa hiyo kapewa muda wa eda kama nafasi ya kuupoza moyo wake.
Kwa hiyo utaona (Eda) ni (Method) ya kukitoa kilichomo moyoni, sasa sisi tunarudi kwenye funguo zetu 99 ambazo kazi yake ni kutia kitu ndani ya huo moyo, Pengine iko moja itafungua moyo wako, iko moja itawasha Taa ndani ya moyo wako imurike hazina ya Imani iko wapi, na ukisha kuona Utajiri wa Imani utakua umegundua faida kubwa kabisa, utapata Rafiki ndani ya Moyo wako na hutojiona maskini tena katika maisha yako.
Elewa kama kwenye tukio la (Eda)linavo mtoa mpenzi wako mpaka ukamsahau, na tukio hili jengine ni la kumtia Mpenzi Mollah wako kwa mapenzi makubwa mpaka na yeye akajua kweli mja wangu kanihitaji, Kweli mja wangu anastahiki zawadi ya ukarimu wangu wa Imani, Na ukipewa kitu hicho unageuka kuwa kiumbe mwengine kabisa, Mpaka Sala yako itakua ya aina nyengine sio ya hivi sasa yakupeleka maneno, na masikitiko matupu, mpaka unasujudu eti unaomba jirani yako avunjike mguu, mke mwenzio apate maradhi hiii, hivyo hiyo inaweza kuwa sala kweli(Unaleta ujambazi mpaka kwenye Ibada)unasimama kwenye sala nzima ya Fardhi unaomba mtoto wako apasi mtihani, au ashinde match ya mpira, halafu unasema umesali laa umepeleka maneno tu.
Na unafanya hayo yote sio makosa kwa sababu Imani haijakugusa, Siku imani itakaposhuka Moyoni mwako Sala yako itageuka na kuwa ya Shukurani, Sala yako itageuka na kuomba Msamaha kwa yale yote ulokua ukienda kwa Mollah wako na kutaka uongezewe kipato, utakua Mwenye kuridhika(Complete Surrender)utakua Mwenye kushukuru mwanzo wa Sala mpaka mwisho wake, na kuanzia siku hiyo maisha yako yatabadilika na kuwa yenye furaha na matumaini matupu, utakua mwenye kuhisi nikiachwa duniani sawa, nikichukuliwa Akhera sawa kote ni nyumbani aliko nikirimu Mollah wangu, Sasa ufanye nini kujaribu kuipata hiyo Imani.
Utachukua Majina ya Mwenye Enzi Mungu yote 99, Utaanza kulisoma kila jina siku nzima(kumbuka ni jina moja)na siku ya pili utachukua jina lengine kwa utaratibu huo, sio wakusoma yote 99 mara moja ikisha unafunga kitabu unasahau, inatakiwa uchukue siku jina moja na uishi nalo masaa 24(Tuseme Sala ya Alfajiri mpaka Alfajiri Nyengine)utakua ukilitaja(Jina la Mwenye Enzi Mungu) wakati unakula, unazungumza, ukiwa ofisini au unatizama Tv, hali yoyote ya harakati uwe unalikumbuka jina hilo, na siku ya pili ikifika unakamata jina linalofatia, utafanya hivyo ukipata nafasi kwa njia ya sauti na kama hujapata nafasi utalikumbuka kwa njia ya ukimya moyoni mwako, lakini uendelee kulitaja Rohoni mwako kila wakati, inachukua kazi hiyo miezi mitatu na siku tisa.
Baada ya kipindi hicho mimi nakuachia mwenyewe, wewe ndio utakua shahidi wa hilo tukio, utajijua kama sasa umeipata hiyo Imani au bado, utajua kama kweli sasa unaishi na Rafiki kwenye Moyo wako au bado, utajua kama kitu kimefunguka katika moyo wako au bado, utajua kama kweli mapenzi ya Mollah wako yameingia au bado.
Ninacho kwambia mie inawezekana jaribu lakini kwa bidii kubwa sio unakumbuka kwa siko mara tano unataka moyo ufunguke(Hii sio funguka sesame ya Pango la Ali Baba) hichi ni kitu kikubwa chenye mahusiano na Mollah wako, ndio maana ukapewa majina kwa sababu vitu vyengine vyote huwezi kujihusisha navyo kwa karibu isipokua majina.

 قَالَ يَـٰٓـَٔادَمُ أَنۢبِئۡهُم بِأَسۡمَآٮِٕہِمۡ‌ۖ فَلَمَّآ أَنۢبَأَهُم بِأَسۡمَآٮِٕہِمۡ قَالَ أَلَمۡ أَقُل لَّكُمۡ إِنِّىٓ أَعۡلَمُ غَيۡبَ ٱلسَّمَـٰوَٲتِ وَٱلۡأَرۡضِ وَأَعۡلَمُ مَا تُبۡدُونَ وَمَا كُنتُمۡ تَكۡتُمُونَ
"Akasema (Mollah) Ewe Adam waambie majina yake, alipowaambia majina yake alisema(Mollah) sikukwambieni kwamba mimi ninajua siri za Mbinguni na za Ardhi, tena najua mnayo ya dhihirisha na mliyokuwa mnayaficha".
Basi kwa hiyo tumia hayo majina yatakua na faida na wewe ambayo siri yake itakufikia katika kipindi hicho nilichokwambia lakini ikiwa utaifanya kazi ya haki ya kulikumbuka kikweli jina moja moja la Mollah wako kwa muda huo nilio kwambia kwa masaa nilokutajia inshaa Allah Molla atakushushia Imani itokayo kwake.