Sunday, March 22, 2015

NDANI MCHA MUNGU NJE MCHA MUNGU PART 3

Asalaam Aleiykum

Sasa ukisha kamata ngao yako ya Imani ndani ya moyo wako, Ndio unaruhusiwa nenda sasa kakamate pesa za msikiti, angalia kwa uangalifu pesa za maskini, simamia mali za yatima, tena huyo (automatic) wewe mwenyewe unaingia katika aya inayofatia ya 11 sura ya (Saff) mpaka mwisho wa aya.
"تُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَرَسُولِهِۦ وَتُجَـٰهِدُونَ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ بِأَمۡوَٲلِكُمۡ وَأَنفُسِكُمۡ‌ۚ"
Muaminini Mwenye Enzi Mungu na Mtume wake, na piganieni (kwa)Njia ya Mwenye Enzi Mungu kwa Mali zenu na nafsi zenu.
Moyo wa mapenzi desturi yake ni kutoa, Njia ya Mwenye enzi Mungu kutoa huko kuwe kwa njia ya kheri na wala sio ya shari, kutoa kwenyewe uwe hujali, au kuwa na khofu kwamba ukitoa utafilisika, Unawapa maskini,Unawapa majirani, Mayatima, wale wasojiweza wanopita njia wakakuomba.
Na kama huna basi unajitolea nguvu zako, unajitolea mawazo yako na kila ulichonacho, hiyo ndio maana ya kujitolea kwa njia ya mali, halafu tena unaingia katika hilo jambo la tatu, nalo ni hiyo Nafsi yako. Wewe unaishi kwenye jamii, Na katika Ulimwengu wa jamii kuna kila kitu ndani yake, kuna kila majambo yanatendeka, kuna kila uchafu, na wewe unajulikana unaishi humo, hujaambiwa Jiue au hama au ondoka au kimbia, umepewa (Challenge)Pigana na nafsi yako kule moyoni bakia vile vile na Ucha Mungu wako, usiteteruke, huo ndio Ucha Mungu, hiyo ndio (Jihad) ya Nafsi.
Hapa itabidi nikupe (Hadith njema) ili upate kujua vipi unabakia ndani ya nafsi yako na Ucha Mungu katika Ulimwengu huu tunaoishi hivi sasa. "Kuna Mwanafunzi Mmoja alimwambia Sheikh wake mimi nina hamu kubwa ya kumjua Mcha Mungu, naomba nifahamishe dalili zake nipate kujua yukoje,"" Sheikh akamwambia nenda kwenye Mji fulani utamkuta Tajiri katika mji huo mwambie mimi nimekutuma ukalale kwake siku moja","Akatoka yule kijana mpaka kwenye ule Mji na kumkuta yule tajiri akamwambia Sheikh kanituma nije kwako nikae siku moja na wewe""Tajiri akampokea kwa uzuri yule Mwanafunzi akaamrisha mgeni afanyiwe takrima kubwa, Ulipofika usiku watu wakaimba na kucheza, yule Mwanafunzi akashangaa sana, akawa kila saa jicho lake liko kwa yule Tajiri, ambaye anamkuta kimya na tasbih yake mkononi anavuta uradi wake. Ulipofika wakati wa kulala akapelekwa chumbani kwake katika ile njia ya (Sebule)ukumbini akakuta mapambo ya kila aina, alipofikishwa chumbani kwake hakukuta kitu chochote ila kitanda kimoja tu, alipopanda kitandani kutizama juu ya (Dari)akakuta upanga unaninginia sawa na kitovu chake, wakati wowote unaweza kuanguka, Yule Mwanafunzi hakulala usiku kucha anautizama ule Upanga usije kumuangukia,  khofu ya kufa imemtawala.
Ilipofika asubuhi akamfata yule tajiri na kumuhadithia ule mkasa wa upanga, Yule tajiri akamwambia niliona mshangao katika macho yako, na hukumu ulizokua unapitisha juu yangu, na kiburi ulichokua nacho cha kunibeza mimi na kujiuliza uwapi Ucha Mungu wangu, nikaijua akili yako inasema uwapi Ucha Mungu wenyewe, ndio na mimi nikakuwekea Alama ile ya Upanga, ili uwe macho usiku kucha, tizama ulivo (Feli)baada ya kumkumbuka Mollah wako umeukumbuka upanga, Basi kwa hiyo haya mambo uliyoyaona na ule upanga ulivokuweka macho usiku kucha ndio hali nilonayo mimi, Nilitaka kukujulisha na mimi Uradi wangu wa kunikumbusha mauti unaniweka macho siku zote simsahau Mollah wangu, Yote unayoyaona yanaendelea katika Jumba langu hili hayanishughulishi kitu, mimi ndani ya moyo wangu kajaa Mollah wangu, Na nje pia namuona Mollah wangu, tafauti yangu naishi kwenye ulimwengu wake na haya yote yanatendeka kwenye Uangalizi wake, Siri yangu kubwa mimi naishi kama sasa hivi nitakufa" Na hiyo ndio (Jihad) ya Nafsi, hiyo ndio Imani, huo ndio Ucha Mungu wa ndani na Nje.Yoyote yule anayekumbuka Mauti ndiye Mcha Mungu wa kweli, kwani kuyakumbuka Mauti ni kuwa karibu na Mollah wako, na kuyasahau Mauti ni kuwa karibu na Dunia  hii na machafu yake, na ndio sababu ya kumsahau Mollah wako.
Najua unataka kujua vipi upate hali kama hiyo, nasema tena na tena kuna mambo matatu ya kufanya ili upate huo Ucha Mungu la kwanza(1)Jishughulishe sana na (Prayers) maombi ya shukurani kwa wingi, jambo la pili(2)(Worship)tekeleza kwa wingi matendo ya Ibada na jambo la (3)(Devotion) kwa njia ya (Dhikr)kumkumbuka sana Mollah wako kila saa na dakika halafu mwachie mwenyewe atakuteremshia Ucha Mungu wa ndani na nje, lakini sio kwa kutaka wewe ila kwa kutaka yeye Mollah wako Muumba wa kila kitu. Mollah wetu tujaalie katika waloridhiwa na wewe, utukusanye pamoja na waja wema, utupe waja wako huo Ucha Mungu wa ndani na nje ili tupate kukushukuru usiku na mchana kwa uweza wako wa kila jambo na kutujaalia sisi utukufu huu wa Uhai.


No comments:

Post a Comment