Sunday, March 1, 2015

FUNGUO 99 ZA IMANI PART 3

Asalaam Aleiykum

Kabla ya kukufahamisha nini ufanye, kwanza wacha nikupe mfano wa matumaini ili usije kuona kazi ambayo utaifanya haina faida na wewe, Faida ipo tena kubwa sana ambayo ukiipata utadumu nayo mpaka mwisho wa uhai wako. Wacha tutoke kidogo kwenye darsa hii ya Imani na tuhudhurie jambo la kina(Mama)linalohusiana na (Eda), Nini Eda kwa lugha ya urahisi wa kufahamu eda ni (Cooling off period)ambayo ina maana mbili moja ya nje ni ile ya kujua tukio la Uja uzito, na maana ya pili ni ile ya ndani ya (Communion)ambayo ni ya (Let it go) au kipindi cha mpito wa pozo la moyo(Kusahau)au kitu kukutoka kwenye moyo wako.
Ndio maana utaona inapatikana katika mambo mawili moja ni la kufiwa au kupewa talaka, na haya kapewa Mwanamke sababu yeye Mwanamke mambo yake yote anapeleka moyoni tafauti na Mwanamme ambaye mambo yake yote yanabakia kichwani,( ndio maana utaona hata akiambiwa tufunge macho tuchukue ahadi kama tutakua pamoja daima, basi mkifunga macho Mwanamme haamini anafungua jicho moja, lakini mwanamke yeye anaamini moja kwa moja hana sababu yakuweka jicho moja wazi, litakalo tokea mbele lolote atalikabili) kwa hiyo kapewa muda wa eda kama nafasi ya kuupoza moyo wake.
Kwa hiyo utaona (Eda) ni (Method) ya kukitoa kilichomo moyoni, sasa sisi tunarudi kwenye funguo zetu 99 ambazo kazi yake ni kutia kitu ndani ya huo moyo, Pengine iko moja itafungua moyo wako, iko moja itawasha Taa ndani ya moyo wako imurike hazina ya Imani iko wapi, na ukisha kuona Utajiri wa Imani utakua umegundua faida kubwa kabisa, utapata Rafiki ndani ya Moyo wako na hutojiona maskini tena katika maisha yako.
Elewa kama kwenye tukio la (Eda)linavo mtoa mpenzi wako mpaka ukamsahau, na tukio hili jengine ni la kumtia Mpenzi Mollah wako kwa mapenzi makubwa mpaka na yeye akajua kweli mja wangu kanihitaji, Kweli mja wangu anastahiki zawadi ya ukarimu wangu wa Imani, Na ukipewa kitu hicho unageuka kuwa kiumbe mwengine kabisa, Mpaka Sala yako itakua ya aina nyengine sio ya hivi sasa yakupeleka maneno, na masikitiko matupu, mpaka unasujudu eti unaomba jirani yako avunjike mguu, mke mwenzio apate maradhi hiii, hivyo hiyo inaweza kuwa sala kweli(Unaleta ujambazi mpaka kwenye Ibada)unasimama kwenye sala nzima ya Fardhi unaomba mtoto wako apasi mtihani, au ashinde match ya mpira, halafu unasema umesali laa umepeleka maneno tu.
Na unafanya hayo yote sio makosa kwa sababu Imani haijakugusa, Siku imani itakaposhuka Moyoni mwako Sala yako itageuka na kuwa ya Shukurani, Sala yako itageuka na kuomba Msamaha kwa yale yote ulokua ukienda kwa Mollah wako na kutaka uongezewe kipato, utakua Mwenye kuridhika(Complete Surrender)utakua Mwenye kushukuru mwanzo wa Sala mpaka mwisho wake, na kuanzia siku hiyo maisha yako yatabadilika na kuwa yenye furaha na matumaini matupu, utakua mwenye kuhisi nikiachwa duniani sawa, nikichukuliwa Akhera sawa kote ni nyumbani aliko nikirimu Mollah wangu, Sasa ufanye nini kujaribu kuipata hiyo Imani.
Utachukua Majina ya Mwenye Enzi Mungu yote 99, Utaanza kulisoma kila jina siku nzima(kumbuka ni jina moja)na siku ya pili utachukua jina lengine kwa utaratibu huo, sio wakusoma yote 99 mara moja ikisha unafunga kitabu unasahau, inatakiwa uchukue siku jina moja na uishi nalo masaa 24(Tuseme Sala ya Alfajiri mpaka Alfajiri Nyengine)utakua ukilitaja(Jina la Mwenye Enzi Mungu) wakati unakula, unazungumza, ukiwa ofisini au unatizama Tv, hali yoyote ya harakati uwe unalikumbuka jina hilo, na siku ya pili ikifika unakamata jina linalofatia, utafanya hivyo ukipata nafasi kwa njia ya sauti na kama hujapata nafasi utalikumbuka kwa njia ya ukimya moyoni mwako, lakini uendelee kulitaja Rohoni mwako kila wakati, inachukua kazi hiyo miezi mitatu na siku tisa.
Baada ya kipindi hicho mimi nakuachia mwenyewe, wewe ndio utakua shahidi wa hilo tukio, utajijua kama sasa umeipata hiyo Imani au bado, utajua kama kweli sasa unaishi na Rafiki kwenye Moyo wako au bado, utajua kama kitu kimefunguka katika moyo wako au bado, utajua kama kweli mapenzi ya Mollah wako yameingia au bado.
Ninacho kwambia mie inawezekana jaribu lakini kwa bidii kubwa sio unakumbuka kwa siko mara tano unataka moyo ufunguke(Hii sio funguka sesame ya Pango la Ali Baba) hichi ni kitu kikubwa chenye mahusiano na Mollah wako, ndio maana ukapewa majina kwa sababu vitu vyengine vyote huwezi kujihusisha navyo kwa karibu isipokua majina.

 قَالَ يَـٰٓـَٔادَمُ أَنۢبِئۡهُم بِأَسۡمَآٮِٕہِمۡ‌ۖ فَلَمَّآ أَنۢبَأَهُم بِأَسۡمَآٮِٕہِمۡ قَالَ أَلَمۡ أَقُل لَّكُمۡ إِنِّىٓ أَعۡلَمُ غَيۡبَ ٱلسَّمَـٰوَٲتِ وَٱلۡأَرۡضِ وَأَعۡلَمُ مَا تُبۡدُونَ وَمَا كُنتُمۡ تَكۡتُمُونَ
"Akasema (Mollah) Ewe Adam waambie majina yake, alipowaambia majina yake alisema(Mollah) sikukwambieni kwamba mimi ninajua siri za Mbinguni na za Ardhi, tena najua mnayo ya dhihirisha na mliyokuwa mnayaficha".
Basi kwa hiyo tumia hayo majina yatakua na faida na wewe ambayo siri yake itakufikia katika kipindi hicho nilichokwambia lakini ikiwa utaifanya kazi ya haki ya kulikumbuka kikweli jina moja moja la Mollah wako kwa muda huo nilio kwambia kwa masaa nilokutajia inshaa Allah Molla atakushushia Imani itokayo kwake.


No comments:

Post a Comment