Sunday, April 26, 2015

SABABU ZA KUJISTIRI MWANAMKE WA KIISLAM PART 1

Asalaam Aleiykum

Mwanamke ni kiumbe alojaaliwa muujiza katika maisha yake yote, Amefanywa ndio sababu ya Viumbe kupitia kwao na kuja katika Ulimwengu huu, Yeye Mwanamke Mwili wake ndio sehemu inotumika kuumbwa mwanadamu ndani ya miezi tisa mpaka kiumbe kikaja katika dunia hii kikiwa kizima na afya na salama bila ya matatizo yoyote, sasa ikiwa Mwili huu tunao uzungumza unaweza kudhibiti tukio kama hilo na kulienzi kwa uficho na usalama mpaka baada ya miezi tisa unatutolea kiumbe aliye mzuri, nini habari yetu sisi kuhusu Mwili wa Mwanamke? Jee yeye Mwanamke anaijua thamani yake?Na kwanini akaambiwa ajifunike?.
Basi kabla ya kwenda huko wacha tupate viunganishi ili tupate kuujua ubora, na utukufu wa Mwili wa Mwanamke kama utatunzwa kama alivoamrisha Mwenye enzi Mungu. Mwenye enzi Mungu anasema nini katika sura ya (Imran aya ya 14)

زُيِّنَ لِلنَّاسِ حُبُّ ٱلشَّهَوَٲتِ مِنَ ٱلنِّسَآءِ وَٱلۡبَنِينَ وَٱلۡقَنَـٰطِيرِ ٱلۡمُقَنطَرَةِ مِنَ ٱلذَّهَبِ وَٱلۡفِضَّةِ وَٱلۡخَيۡلِ ٱلۡمُسَوَّمَةِ وَٱلۡأَنۡعَـٰمِ وَٱلۡحَرۡثِ‌ۗ
"Watu wametiwa huba ya kupenda wanawake na watoto na marundi ya dhahabu na fedha na Farasi wanotunzwa vizuri, na wanyama na mashamba,(Mpaka mwisho wa aya).
Jambo la mwanzo limetajwa Wanawake, Kwanza Wanaume wamepewa hii nyenzo ya giza wanatembea nayo ya (Huba) Mwanammke kapewa (Taa) ya kungara ya (Hubi)Kutamaniwa, (Taa) hizi zipo za aina mbili kwa Mwanammke, ipo (Nyekundu) na (Nyeupe)(Nakupeni habari hizi msianze kuwaandama wanawake na kutaka kujua wamebeba taa gani)Kumbuka Mwanamme kabeba kiza anatembea nacho, kiza hicho kinaitwa (Unconsciuos Mind) na Mwanammke kabeba taa inaitwa (Consciuos heart) Ndio maana utaona siku zote Mwanamke yuko(Alert)akiliona jicho lako anagundua mpaka nini nia yako, kwa hiyo ana uamuzi kujiepusha au kukutia Mkononi.
Sasa nini kinafanyika katika taa hizo za Mwanamke? Napenda ikumbukwe katika kila kitu kwenye Ulimwengu huu kina toa Taa(Emit Light)ndio maana ukawa unakiona, na ikiwa hukioni ina maana hiyo ni (Dark Matter) kwa hiyo wewe ukitizama unatoa (Light) na kile unachotizama kinarudisha (Light) ndio unapata kukifahamu, sasa kwenye kadhia hii ya Mwanamke nini kinatokezea mpaka akaambiwa ajisitiri, Itabidi tuhudhurie aya iliyomo kwenye sura ya Ahzab aya ya 59 tujue inasemaje?
Endelea part 2

SABABU ZA KUJISTIRI MWANAMKE WA KIISLAM PART 2

Asalaam Aleiykum

يَـٰٓأَيُّہَا ٱلنَّبِىُّ قُل لِّأَزۡوَٲجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَآءِ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ يُدۡنِينَ عَلَيۡہِنَّ مِن جَلَـٰبِيبِهِنَّۚ ذَٲلِكَ أَدۡنَىٰٓ أَن يُعۡرَفۡنَ فَلَا يُؤۡذَيۡنَۗ وَكَانَ ٱللَّهُ غَفُورً۬ا رَّحِيمً۬ا
"Ewe Mtume; Waambie wake zako, na Watoto wako wa kike, na wanawake wa Kiislam, Wajiteremshie uzuri nguo zao(Wajifunike)kufanya hivyo kutapelekea upesi wajulikane(Ni Wanawake wa heshima)(Ili)Wasiudhiwe, Na Mwenye Enzi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (Na) Mwingi wa kurehemu"
Kwanini Wajifunike? kwa sababu Wafunike hizo (Taa) nilizozitaja kwa vipi?Mwanamke akiacha (Maungo)yake wazi anakua anapeleka (signal) za hiyo taa nyekundu ndio maana ukaona rangi nyekundu imehusishwa na (Sex) kwa sababu imetokana na rangi ya (Damu) tulo umbwa nayo, na kutokana na (tendo hilo) sote ndio tunazaliwa, ndio utaona nguo nyekundu inahusishwa na (Sex) huoni hata siku moja Biharusi kavikwa nguo nyekundu, pia utakuta kwa wale wanawake wenye kuuza miili yao wanaweka (Taa) nyekundu au pazia jekundu kuwajulisha wateja wao hapa kuna (Bussines) sio (Love) kwa hiyo Mwanamke akenda bila ya kujisitiri utaona macho  yaso idadi yanamuangalia, na kutokana na ishara hiyo maudhi yanafatia, wanaume wanaanza kukukera, wako wanokukera kimya kimya na wale wenye kutoa sauti.
Hiyo ndio moja katika zile (Taa) mbili, Kwa hiyo Mwanamke akiamua kuzipunguza nguo ana amua akijua vizuri nataka kuwashughulisha watu(Conscious Heart) na ndio anatukuta na sisi wagonjwa maskini(Unconscious Mind)tunabubujikwa na mate, tunasahau kwamba haramu, hatukumbuki chochote tunaendelea kukodoa macho kuridhisha Mioyo yetu kwa aina ya kila mawazo, kwa hiyo muoneshaji na anaye ona wote tunaingia kwenye hasara ya nafsi zetu.
Ama akiamua Mwanamke kufata kama alivoamrisha na kufunika Mwili wake, kitu cha Mwanzo kinachotokea anawasha (Taa) nyeupe, Anaonesha Ishara ya Amani, hapo hapo anapata kuheshimiwa, anapata kujulikana yule Mke wa mtu au mtoto wa fulani, au ni Mwanamke asotaka mambo mambo ya kipuuzi, kajihifadhi, kashaleta msg usihangaike hata kutizama, hapa huoni kitu, Mimi sitibu maradhi ya watu njiani kwa kuonesha maungo yangu, lakini basi isiwe kujisitiri kwenyewe nusu nusu juu umevaa (hijab) chini Buibui limekubana, au umevaa nguo za ajabu, hapo utakua unapeleka (Wrong Msg) watu watababaika mbona kuna rangi nyeupe na nyekundu zinawaka, itakua kama (Traffic Light) ilo haribika watu watakua hawajui wavuke barabara au wasubiri, ukiamua kujifunika basi iwe Mwili mzima umejihifadhi ili upate kujulikana watu wasikuudhi.

SABABU ZA KUJISTIRI MWANAMKE WA KIISLAM PART 3

Asalaam Aleiykum
Sura ya Nur aya 31.

وَقُل لِّلۡمُؤۡمِنَـٰتِ يَغۡضُضۡنَ مِنۡ أَبۡصَـٰرِهِنَّ وَيَحۡفَظۡنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبۡدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنۡهَا‌ۖ وَلۡيَضۡرِبۡنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِہِنَّ‌ۖ وَلَا يُبۡدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوۡ ءَابَآٮِٕهِنَّ أَوۡ ءَابَآءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوۡ أَبۡنَآٮِٕهِنَّ أَوۡ أَبۡنَآءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوۡ إِخۡوَٲنِهِنَّ أَوۡ بَنِىٓ إِخۡوَٲنِهِنَّ أَوۡ بَنِىٓ أَخَوَٲتِهِنَّ أَوۡ نِسَآٮِٕهِنَّ أَوۡ مَا مَلَكَتۡ أَيۡمَـٰنُهُنَّ أَوِ ٱلتَّـٰبِعِينَ غَيۡرِ أُوْلِى ٱلۡإِرۡبَةِ مِنَ ٱلرِّجَالِ أَوِ ٱلطِّفۡلِ ٱلَّذِينَ لَمۡ يَظۡهَرُواْ عَلَىٰ عَوۡرَٲتِ ٱلنِّسَآءِ‌ۖ وَلَا يَضۡرِبۡنَ بِأَرۡجُلِهِنَّ لِيُعۡلَمَ مَا يُخۡفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ‌ۚ وَتُوبُوٓاْ إِلَى ٱللَّهِ جَمِيعًا أَيُّهَ ٱلۡمُؤۡمِنُونَ لَعَلَّكُمۡ تُفۡلِحُونَ
"Na Waambie Waislamu wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa vinavyo dhihirika,Na waangushe shungi zao mpaka vifuani mwao,Na wasionyeshe mapambo yao ila kwa wanaume zao, au baba zao, au baba za waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao,au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenziwao, au wale iliyowamiliki mikono yao ya kiume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio, au watoto ambao hawajajua mambo yalohusu uwana uke, Wala wasipige miguu yao ili yajulikane wanayoyaficha katika mapambo yao, Na tubieni nyote kwa Mwenye enzi Mungu Enyi Waumini ili mpate kufaulu."
Nini kuinamisha?
Kuinamisha macho kwa Mwanamke ni kuenzi (Hayya) ya Mwanamke, kuwa siku zote unaona aibu, hiyo ndio silaha ya Mwanamke, daima macho yako chini, na macho yakiwa chini nini kinatokea? siku zote unaendelea kuwa (Biharusi), kila mtu anatamani ulinyanyue jicho la (Ghazzala) lakini halinyanyuki, kuinamisha macho siku zote unabakia na bashasha za mtoto mdogo, macho daima meupe yanangara kwa utiifu, na ukiwa hutizami ovyo ovyo ndipo unapata neema na nguvu ya kulinda(Kasha lako la dhahabu).
Halafu wasidhihirishe viungo vyao, kwa sababu maungo ya Mwanamke yote ni mapambo kwa wanaume, kwa hiyo ukidhihirisha ina maana umeweka (Window shopping), kila mtu atizame mimi niko hivi, na hapa kuko vile, inakua watu wanakujua kama (Map) ya dunia, wanajua kasoro na ukamilifu wako, halafu unauliza mbona wanashangilia wakati wewe ndio(Actress). Yote haya unafundishwa heshima na adabu ya kujilinda, ili ujijue thamani yako, ujijue wewe na wanawake wengine tafauti, wewe bakia na (Uharusi) wako daima, wewe kuwa Mwanamke usishindane na Wanaume.
Halafu tena kwa kuenziwa na Quraan unaambiwa wewe (Mwana kinda kindaki) Teremsha shungi lako mpaka kifuani, kwa sababu kifua chako kina (Madhara) kwa Wanaume, kuna wengine wamekatishwa (Kunyonya) walipokua wadogo kwa hiyo wakikiona kifua cha Mwanamke wanakua hawajiwezi, wanaweza kukufata njia nzima huku wamefadhaika na kifua cha Mwanamke, na hayo yatakuletea udhia, kwa sababu yanawapendezesha baadhi ya wanaume na unakua kivutio(Senema) ya siku nzima kwa ajili ya kifua chako, kwa hiyo utaona kifua chako wewe lakini wanakikatia (Ticket)watu wengine bila ya wewe mwenyewe kujijua, sasa ufanye nini? Hifadhi kifua chako usitoke kama una nyanyua vyuma, kuwa na aibu, wewe Malkia, angusha shungi lako na useme hapa hamuoni kitu, mimi Mwanamke wa Kiislam na hili ndilo vazi langu.
Na Mapambo yenu hizo (Piko na Hina) na mengineo msioneshe kwa sababu katika hayo kuna siri kubwa inayo kwenda (Deep) kwa wale wenye kujua mambo, ama kwa wasojua wanaona maandishi, lakini kwa wenye kujua (Siri) ya maandishi na hizo (Tatoo) za (Hina na Piko) wanajua na (Msg) zilizomo katika michoro hiyo, wanajua Mwanamke anasema nini? kwanini akachora hivyo, na anakusudia nini? kumwambia huyo alo mchorea kama anafahamu, Ntakupeni mfano mmoja(Kama yamechorwa Mawaridi kwenye Mwili)basi unaambiwa sasa acha kutizama Bustani nitizame mimi)sasa una hiyari yako kama utatizama ua moja moja au kwa jumla, halafu aya inaendelea kukufahamisha kwa watu gani unaweza kuyadhihirisha mapambo hayo ambayo hayataleta tafsiri nyengine kama walivotajwa watu hao wa aina gani.
Na Wala msipige miguu yenu ili kudhihirisha mapambo yenu, Mpaka mwendo unafundishwa kama utakua umevaa vitendea kazi, yaani hayo mapambo, sasa mapambo yepi yalotajwa hapa?(Ni yale yanotoa sauti)(Na sauti ina athari ya kila aina kwa mwanaadamu) siku hizi nadhani sio sana, katika karne hizi (Art) hii nadhani imepotea, siku hizi kuna watu wanajichora (Nyoka mara simba)(Art)ya mapenzi imepotea, kuna msemo mmoja kama mnausikia(Nani atomvika paka kengele) kwanini paka akavikwa kengele, paka anavikwa kengele kwa sababu anakamata ndege sana katika mawindo yake, kwa hiyo kwa kufanya hivyo wanashituliwa ndege wakisikia kengele wanajua paka huyo anakuja, kwa hiyo wanaruka, kwa hiyo zamani Wanawake walikua wakivaa kengele kwenye miguu yao si kwa ajili ya kumfanya Mwanamme akimbie laa, ni kwa ajili ya kuamsha au kushitua hisia fulani lakini kwa njia za mapambo, na hutungwa kengele hizi kwa milio tafauti kwa ajili ya mwendo wake wa haraka haraka na mwendo wa taratibu, (Vibration) za kengele hizo zina athari yake kwenye (Akili) ya Mumeo,ndio maana mkaambiwa msipige miguu (hatari kubwa) kuna watu waso husika watapata (taarifa) zisizo wahusu, msidhihirishe mapambo yenu na hizo ndizo sababu za kuambiwa mjisitiri, lakini Mwenye enzi Mungu anakujueni, anajua mtateleza ndio akakwambie katika aya ilotangulia mkiteleza mkaponyoka basi yeye atakusameheni, na atakushushieni Rehma ya kuweza kujistiri ili msije kuudhiwa na kuwashawishi watu kuanza kukuvunjieni heshima zenu, hayo yote ni kwa ajili yenu nyinyi kwa heshima na uzuri na adabu na aibu na kulinda enzi ya Malika za nafsi zenu.

Sunday, April 12, 2015

MAISHA NI KITU GANI ? PART 1

Asalaam Aleiykum

Nilimuuliza Rafiki yangu mmoja wa Dhehebu la (Kikatoliki) katika Dini ya (Kikiristo)akiwa katika (Kabila) la (Kizungu) nini Maisha ?
Akanijibu kwa lugha ya (Kabila) yake kama hivi,
(Life is those a few year's between Birth and Death).
Jawabu zuri, lakini halijakamilika, tena limejibiwa kwa urahisi sana kama kwamba hiyo miaka michache haina thamani yoyote, Lakini ukweli halisi hilo ndilo jawabu la watu wengi wenye kuishi katika Ulimwengu huu. Dhana hiyo ndio inayo tupelekea tukaona maisha si chochote, (One Life) endelea kuchapa maji, endelea kufanya uharibifu, endelea kudhulumu, endelea kumsahau huyo alokupa maisha haya.
Kama utasoma vizuri utaona mwanzoni nimesema jawabu la swali hili ni zuri, lakini sio sahihi kwa kuwa halijakamilika. Kwanini likawa zuri kwa sababu Mwenye kujibu kagundua hiyo miaka michache baina ya kuzaliwa na kufa, Mtu kama huyo kaonesha dalili kama akifanyiwa kazi ya kujulishwa zaidi anaweza kupata matumaini ya kuokoka. Lakini kwa watu wengine haoneshi hata dalili, moyo ushakufa na moyo ukifa ina maana moja tu kuwa (connection) na Mungu wako ishakatika, na hapo hakuna matumaini tena.
Ndio Utakuta Baadhi ya watu wanaishi mpaka kufariki kwao hawaupati ukombozi wa Roho zao, na kama hupati ukombozi huo ni vigumu kukijua kitu hichi muhimu kiitwacho maisha.
Nakuchukua katika safari hii ya maisha ili nipate kuwasiliana na Roho yako tuweze kulizungumza tukio hili la maisha, Nini Maisha?. Watu wengi wana (Confused) baina ya (Life and Living) ndio Waingereza wanamsemo huu (One life Live it) Hawajakosea katika msemo wao, ila wamekosea katika ufahamu wao, Maisha (Life) ni kitu cha Kudumu ila kuishi ndio kitu cha muda (Temporary), Kwa sababu ingekua (Life) yenyewe ni ya muda vitabu vingesema zamani, lakini vitabu vyote vya (Haki) vinasema Maisha ni Milele iwe kwenye (Pepo au Moto) kwa  hiyo kaa 
ukijua wewe ni wa kudumu kwa sababu umetokana na hiyo (Life).
Ama tukizungumza kuishi ndio tunazungumza hicho kipindi unachopita baina ya kuzaliwa na kufa kati kati yake ndio kuna hiyo fahamu ya kuishi ambayo ina mpito wa matendo yako katika Ulimwengu huu. Sasa tujiulize kwanini kwetu sisi kikawa kipindi hichi cha mpito kikawa muda mfupi sana.
Ndio nimeamua kukuchukua katika safari hii ili na wewe upate kugundua jambo ambalo pengine litakufanya uweze kuishi japo muda mchache ulobakisha katika Ulimwengu huu.
Endelea part 2.

MAISHA NI KITU GANI ? PART 2

Asalaam Aleiykum

Basi kwenye Safari hii ya (Maisha ni Kitu gani) Nataka nizindue Akili yako kwa kukujulisha jambo ambalo huenda likawa msaidizi wako huko mbele katika somo hili, Nataka wewe Mwenyewe ufanye uchunguzi wa mambo mawili haya ambayo pengine yanaweza kukujulisha aina gani ya maisha unayoishi hivi sasa.
Angalia wakati wa dhiki au maradhi, Wakati wa shida au matatizo kwanini wakati yaani(Muda) unakwenda taratibu, unakua mrefu, miaka inakua mingi. Na wakati wa furaha au Raha (Muda) au wakati unapotea, au unakwisha haraka, kama unajua siri ya viwili hivi basi huna haja ya kusoma darsa hii ya nini maisha?.
Lakini kama hujui basi wacha nikuchukue katika dunia ya ufafanuzi wewe mwenyewe ili uwache kusubiri nani kasema, nani katoa (Fatwa) ili upate ufafanuzi wa kufahamu na uweze kuishi hiyo miaka michache ilobakia, kwanini nikasema hivyo pengine siku zote ulikua unaishi(Dead man walking).
Kuna Msemo wa (Waingereza)wanasema kwa lugha yao kama hivi "Inasemwa sana kabla ya kufa Maisha yako yanapita mbele ya macho yako, Kitu hicho ni kweli kinaitwa kuishi"(Mwisho wa kunukuu), Sasa wacha tuitizame jee kauli hii ina ukweli ndani yake?."Kwanini kabla ya kufa kwako ndio maisha yanapita mbele ya macho yako?" Na maisha kupita mbele ya macho yako ni kitendo cha majuto kama kilivotajwa kwenye Quraan aya ya 10 sura ya (Munafiqoon)

وَأَنفِقُواْ مِن مَّا رَزَقۡنَـٰكُم مِّن قَبۡلِ أَن يَأۡتِىَ أَحَدَكُمُ ٱلۡمَوۡتُ فَيَقُولَ رَبِّ لَوۡلَآ أَخَّرۡتَنِىٓ إِلَىٰٓ أَجَلٍ۬ قَرِيبٍ۬ فَأَصَّدَّقَ وَأَكُن مِّنَ ٱلصَّـٰلِحِينَ 
Na toeni katika yale tuliyokupeni, kabla mmoja wenu hayajamjia mauti, ikisha akasema, Mollah wangu huniakhairishi muda kidogo, nikatoa sadaka, na nikawa miongoni mwa watendao mema.
Mauti yakishawasili ndio unaanza kukumbuka kuishi, unabubujikwa na machozi lau ningehairishiwa muda ningefanya hivi na vile, sasa swali la kujiuliza kwani siku zote ulikua wapi? kwani sasa hivi unafanya nini? wapi tena, wakati huu hufanyi unasubiri karibu ya kufa unasema ningejua ningetoa mali yote kwa yatima, ningejua ningekua siku zote nasafisha Msikiti, ningejua kuwa maisha yana umuhimu huu ningefanya ihsani kwa kila mtu, ningekua mtu mwema.
Swali la kujiuliza kwani ulikuwa wapi? huo ndio msemo wa maisha yanakupita mbele ya macho yako, ulikua unaishi lakini ndani ya (Memory) umelala katika godoro la kumbukumbu, kila kitu chako kimo kwenye ndoto, kama sizo zilopita unaota zijazo, ndio maana hata siku moja huoti kitanda ulicholalia, ushapata kujiuliza kwanini?
endelea part 3

MAISHA NI KITU GANI ? PART 3

Asalaam Aleiykum

Kwa sababu pale kwenye kitanda ndipo penye ukweli, kwenye kitanda ndio kwenye maisha, pale ndipo ulipo lala, ndipo ilipo (Body) yako imepumzika, Roho yako imetulia, lakini yenye kuhangaika ni hiyo Akili yako, ambayo inahangaika usiku na mchana wewe ukiamka unafatisha amri zake, siku utakayo amka na kuacha kusikiliza akili yako siku hiyo ndio utaanza kuishi, utaanza (Jihad Nafsi) kwa sababu Nafsi ikitawaliwa na Akili huna maisha mpaka Nafsi itawale Akili ndio hapo utakua unaishi.
Nini Maisha?
Maisha ni hali hiyo ulo nayo sasa hivi, zengine zote ulo nazo ni ndoto, na tafauti yake unaishi kwenye ndoto unayasahau maisha,
Maisha naweza kuyafananisha na neno moja nalo ni kuridhika na (Qadar) ya Mwenye enzi Mungu, Vipi kuridhika huko?(Mfano) Umepangiwa maisha yako pengine uko (Dubai), au Upo (Muscut) au uko Canada au unaishi Uingereza, ikawa katika moyo wako imekujia fahamu ya kuridhika Mollah wangu kanichagulia katika Ardhi hii ndio  nifanye maisha, na kazi hii japo ya Cleaner ndio iwe pato langu la halali, na mimi  kwa hilo nimeridhika, kwa hili nimekubali kwa Roho ya ukunjufu, na niko nasubiri na yale mengine ulo nipangia ambayo mimi sina uwezo wa kuyajua ila kwa kutaka wewe, Mimi nafurahi kila leo kwa neema za afya, na kipato ulichoniruzuku, ukanifanya pia niweze kusaidia wengine, ukanilinda mimi na ufisadi wa dini yangu na dunia hii ambayo wewe ni mfalme wake, Mollah wangu naishi kwa ajili yako kila siku ulonipangia niwepo katika Ulimwengu huu, nipo mimi katika kukumbuka wewe, kuyakumbuka Mauti, kukumbuka Ibada, kukumbuka kila kinachotokea siku nzima hii ya leo, natulia katika enzi yako nikishukuru pumzi zako ulizonijaalia, afya njema ulonitunikia, Mke au Mume mwema ulonipa niishi naye, pamoja na kizazi chema ulichonijaalia, basi nijaalie mimi niishi sasa hivi badala ya kutegemea ndoto za utajiri au kuwa nakhofu kesho itakuaje, na chochote kile utakacho nipa basi nipe na nguvu za moyo nikitoe kuwapa wengine, Pia Mollah wangu usininyime mimi Roho ya Imani na Wema na Ihsani kwa Binaadamu wenzangu, nijaalie mimi niwe Mwenye kuzikhofia kuja kuzikosa Pepo  mbili moja hii ya Duniani ninayo ishi na nyengine hiyo ya Enzi yako ya Akhera nitakayokuja ishi.
Sasa kama hujaridhika ndio unatoka kwenye Maisha na unaingia kwenye (Plan B) ambayo ndio yako Mwenyewe unayoishi nayo hivi sasa, sasa hapo unataka Ujenge Jumba la ghorofa (Tanzania) au Kenya, unataka na Biashara na kuongeza Mke wa Pili, unataka ununue Shamba, upeleke gari, Ewe ndugu yangu Kichwa chenyewe kimoja utaweza vipi kuyakidhi mahitaji hayo yote bila ya kuhangaika? Lakini siku utakayosema maisha yangu hapa hapa nilipo, na kazi yangu ndio hii nilonayo hapa, moja kwa moja nafsi yako itakushukuru (Alhamdullilah) sasa ndio tunaishi, sasa ndio tunaanza kufurahia maisha, Lakini kinyume cha hayo ni kualika matatizo, Na ukiamua kuikubali (Qadar) ya Mwenye enzi Mungu ukaanza kuishi kihalali na kama alivoamrisha Mollah wako katika muongozo wake alokuletea hapo maisha yatakua hayapiti mbele ya macho yako, ila utakua unapita nayo kila sekunde na dakika zilizomo kwenye maisha yenyewe.
Kuishi sasa hivi ni kama (Hivi)"Unajua mwenyewe kwa yakini sasa hivi ni msimu wa Kiangazi wakati wake umefika, sio mpaka(Gazeti liandike mazao yaathirika kwa Jua kali) Na wewe ndio unanyanyuka usingizini(Kiangazi hicho) Ishi ndani ya Kiangazi, furahia neema ya Jua, ona Mollah wangu ananipa (Vitamin D na K) Na kupitia Majani wanayokula wanyama ananipa mengine ya siri nisiyoyajua, Wakati wenzangu kule Ulaya wamevaa (Bag) zima Barabarani kwa ajili ya Baridi, Mie nimevaa fulani (Bukheir wa Afya). Hayo ndio maisha unayotakiwa uishi lakini tafauti yake wewe jitizame maisha yako yote unaishi kwenye jana, au kesho, lakini kwenye leo hupo kabisa, na matokeo yake unakosa kuishi kwa ukamilifu, na maisha yanakupita mbele ya macho yako huku ukiwa umelala, ukiamka unauliza kimetokea nini, utadhani ndio kwanza umekuja Ulimwenguni.
Maana ya Maisha ni  kuwa Furahani hiyo ndio (Nature) yako, ukiona humo furahani basi jijue huishi vizuri, kuna tatizo fulani, pahala fulani, Maisha ni kuridhika na hali uliyonayo, kuridhika na ulichonacho, Maisha ni kuamini na kujua kila jambo limekuja na kutokea kwa Mwenyewe Mwenye enzi Mungu na wewe kazi yako ni kupokea, lakini ukenda kinyume na maelekezo na muongozo wa Mwenye enzi Mungu ndio utakua unaishi huku umetawaliwa na Akili.
Vipi kutawaliwa na Akili? 
Kutawaliwa na Akili ndio huko kuishi na Tamaa za ndoto, haikatazwi kutamani, ila inakatazwa kuzifanya hizo tamaa ni kweli na kuanza kuzifatilia, hapo ndio utakua unaingia hasarani, inakua hamna maisha tena, unahangaika pengine Family yako iko mbele yako huwezi hata kufurahi nayo, kila kitu mateso kwako, inakua mchana kutwa unapita na ndoto juu ya ndoto, unapita mjini huoni unakoroma, unakwenda Msikitini umejaa njozi tupu, unashindwa hata kusali mambo yanakujia kwenye Sala, Unakwenda Nyumbani usingizi hupati  umo katika mbinu za kesho, wakati leo hujaimaliza, Na hivyo ndivyo maisha yanavo kupita mpaka pale Mauti yanavokaribia ndio unakumbuka lahaullah sijatoa sadaka, hujapata ku(Enjoy)hujapata ku(Spend time with family) wewe ulikua unaishi kwenye ndoto mwanzo mpaka mwisho.
Na ukiacha Maamrisho ya Mwenye enzi Mungu kuna mambo matatu lazima yakufikie mapema, sababu huna maisha, hujui thamani ya maisha haya, umeamua unavotaka wewe,  ukawa unatenda mambo machafu basi ima Maradhi yanakushukia mapema, ukiacha kumuabudu Mollah basi dhiki za Roho zinakutawala, na kama huwatendei wema wanaadamu wenzio basi mashaka ya Akili yanakuzonga unakua huna furaha daima.
Lakini ukiwa katika njia ya Mwenye enzi Mungu Basi Furaha na Afya njema ndio vinafatia, Maisha ya salama na Roho inapata starehe za maisha, na utulivu kama ule wa utotoni, Ndio maana siku zote unakumbuka utotoni, kwa sababu ndio (Time) pekee uliyopata kuishi, Basi fanya mema, muabudu Mollah wako, kuwa msafi urejee utotoni upate kujua nini Maisha, na ukiyajua hivi sasa ni vizuri zaidi kwani utotoni ulipita na sasa hivi unakaribia kufika, basi ikiwa utaonja ladha ya utoto uzeeni ukaona raha yake, utawacha tabia yako ya hivi sasa kuwa kama (Robot) Kazini, nyumbani,kula,kulala,kazini tena. Utaanza kubadilisha mwenendo utaichukua siku kama inavokuja, kila siku itakua mpya kwako, (Walking)harusini, Msikitini, Darsani. Mpirani, Shamba, Baharini, kila siku utakua unapanga na Ku(Experience) mambo mepya, lakini ukiona umo kwenye tabia isobadilika basi pata wasiwasi nini kimekusibu, na jiulize mimi naishi au nasindikiza wenye kuishi.

Sunday, April 5, 2015

HAKI YA MWANAMKE KUTOA TALAKA PART 1

Asalaam Aleiykum

Uislam ni Dini ya haki na Mollah Muumbaji ni Mwenye kuhakikisha haki inatendeka na hayo ndio maamrisho ya kisheria katika Ulimwengu huu, hakuna yoyote Mwenye kulazimishwa jambo kinyume na matakwa yake, Sasa kuna haki moja ambayo mwanamke anateseka sana ambapo  ikiwa ataamua kuidai kutoka kwa Mumewe au katika mamlaka ya Dini yake ya Kiislam, katika kadhia hii ya Talaka Mwanamme katawala mpaka kudhani ana Mmiliki mwanamke katika nyanja zote za maisha ya Kidini na kidunia hassa ukizingatia Mamlaka haya ya Talaka katajiwa Mwanamme ndie awezaye kuitoa, basi swali la kujiuliza jee haki hii kapewa mwanamme peke yake, katika maudhui hii tutalitizama hilo ili tupate kujua jee Mwanamke na yeye anayo haki hiyo.
Kwa kuwa Wanaume wamepewa haki ya kuwaongoza Wanawake basi imekua desturi hata mwanamme akiwa mkosa basi kesi nzima inatizamwa na kufanywa mwanammke ndio (Guilty Part)hata kama ana sababu za kimsingi za kumaliza mahusiano na mwanamme husika ambaye itakua kachoka kustahamili au mapenzi yameondoka kutokana na sababu anazo zifahamu Mwenyewe.
Basi atakapoamua sasa anahitaji Talaka au anataka kumaliza mahusiano hayo kwa njia ya salama kabisa ndio huwa sababu ya magonvi na kuteseka kuipata haki yake hiyo ya kimsingi, Pengine itambidi aangukie masheikh labda wamsaidie kuipata haki yake hiyo, mpaka wamwambie sasa uko huru umeeachika, sio (Guilty)tena tumekubali unaweza kuolewa, basi inapaswa Wanawake wajiulize jee kuna haja ya Mateso haya?.
Kabla ya kujiuliza huko wacha kwanza tuguse hiyo ndoa yenyewe ikoje mpaka ikaitwa ndoa, Ndoa ni maridhiano ya nyoyo ya kukubali kwa ridhaa ilo Barikiwa na Mwenye enzi Mungu wako, Kuwa wewe na fulani Muanze mahusiano ambayo yataleta Mapenzi na Rehma ya kizazi na Riziki njema katika maisha yenu ya kidini na dunia baina ya wawili nyinyi, katika mahusiano haya napenda uelewe mnokutana ni wawili nyinyi wenye tabia tafauti ambazo mnatakiwa kuziunganisha ziwe kitu kimoja, ziwe zilofungana nyoyoni ikawa akipigwa (Amin anaumia Amina).
Endelea part 2..

HAKI YA MWANAMKE KUTOA TALAKA PART 2

Asalaam Aleiykum

Katika Mahusiano hayo kama kutatokea khitilafu ikawa hamkuweza kuishi pamoja basi hapo hakuna ndoa, ila kilichobaki ni ugonvi na kuwekwa kwa ndoa hiyo kwa kipande cha karatasi, Mnasahau kabisa kuwa nyinyi ndoa yenu mmefunga kwa Rehma ya Mwenye enzi Mungu, kwa upendo na makubaliano ya pande mbili za familia.
Sasa kinachobaki hapo ndoa inasahauliwa na unabaki ugonvi wa Talaka, Mwanamke anataka Talaka Mwaname hataki kutoa karatasi, na hapo inampelekea Mwanamke kujihisi ana makosa ya kujitenga na Mwanamme huyo, anazidi kumpa nguvu kwa kudhani Amri hiyo lazima itoke kwa Mwanamme, anasahau kabisa kwamba na yeye ana uwezo wa kutoa Talaka.
Vipi ana Uwezo huo?
Mwanamme kapewa nafasi chungu nzima za kutekeleza tendo la Talaka, Na Mwanamke kapewa(Chance)yake japo mara moja lakini yenye nguvu ya hoja pale ambapo jitihada zote zimefanyika za kuinusuru Ndoa hiyo zimeshindikana, yakatizamwa matatizo yote husika yanayoikabili ndoa hiyo ikawa hakuna uwezekano tena wa wawili hawa kukaa pamoja, Na mpaka ikapatikana taarifa sasa hata vitanda wanalala tafauti mwezi wa sita huu, hapo inaashiria mahusiano yameshakatika na ndoa ishavunjika, na hakuna haja ya mmoja wao kubakia mahabusu(Kinyume chake ni jela unayoichukia ya Ndoa).
Na ikiwa Wawili hawa ndio hawakutani Kindoa na mwanamke anasisitiza kutokana na vitendo viovu vya mumewe au Rehma ya mapenzi imemuondokea na hawezi tena kuishi na Mume huyo basi sheria inampa haki ya kutoa Talaka kama ilivyoamrisha Quraan na Hadith ya Bwana Mtume s.a.w inavosema..

HAKI YA MWANAMKE KUTOA TALAKA 3

Asalaam Aleiykum

Talaka hiyo kwa jina la (Sheria) inaitwa (Khul). Nini maana ya Talaka, kwa lugha ya kiarabu neno hili limehusiana na kumpa mnyama uhuru wake(To set animal free). Sasa hii Talaka ya (Khul) imetokana na neno la (Khul-al-Thaub) na tafsiri yake ni kuvua nguo kutoka kwenye mwili, na asili yake imehusiana na aya katika Quraan inayosema "Hao Wanawake ni nguo zenu na nyinyi ni nguo zao kwao. Sasa kama wewe unavua na yeye pia ana uwezo wa kuvua, hapana maonevu haki sawa kwa nyote wawili.
Kama sheria inavoamrisha Mwanamme kuacha na Mwanamke kapewa uwezo huo wa Kisheria ikiwa itakua Mwanamme anamfanyia mateso ambayo hayasthamiliki, Uislam umefanya hivi ili isije kuwa mateso kwa (Family) nzima ikawadhuru mpaka watoto kwa magonvi na mapigano. Wanazuoni wa Madhehebu zote wameitaja Talaka hii ni kama tendo la kurejesha Mahari na kutamka neno hilo la (Khul). Quraan na Hadith imeweka muongozo wa jambo hili kama aya ilivosema (128 sura ya An-Nisaa)
"وَإِنِ ٱمۡرَأَةٌ خَافَتۡ مِنۢ بَعۡلِهَا نُشُوزًا أَوۡ إِعۡرَاضً۬ا فَلَا جُنَاحَ عَلَيۡہِمَآ أَن يُصۡلِحَا بَيۡنَہُمَا صُلۡحً۬ا‌ۚ وَٱلصُّلۡحُ خَيۡرٌ۬‌ۗ وَأُحۡضِرَتِ ٱلۡأَنفُسُ ٱلشُّحَّ‌ۚ وَإِن تُحۡسِنُواْ وَتَتَّقُواْ فَإِنَّ ٱللَّهَ كَانَ بِمَا تَعۡمَلُونَ خَبِيرً۬ا 
Na ikiwa kama Mwanamke akiona kuwa Mume wake kugombana(Kumezidi)au Anatekelezwa(anatupwa na Mume hatizamwi), Basi si vibaya kwao wakitengeneza baina yao Suluhu, maana Suluhu ni kitu bora, Japokua Nafsi za (Wanaume) zimewekewa ubakhili mbele, Na kama mkifanya mema na kumcha Mwenye enzi Mungu, Kwani Mwenye enzi Mungu anazo khabari za yote mnayoyatenda.
Wengine wakasema ama aya hiyo inamtaka Mwanamke asubiri afanye Suluhu, sasa suluhu ya nini? wakati anapigwa, mume ana mwanamke nje, anatengwa hatizamwi, anapata shida na watoto, hatimiziwi haki zake, mateso na matusi yamezidi, nini afanye? Suluhu yenye ndio hiyo (Khul) Amwite ewe Bwana fulani kutokana na hivi tunavoendelea mimi siwezi tena, kwa hiyo shika mahari yako niwachie mie huru(Ukitaka usitake) ndio Maana aya ikataja hapo (Wanaume kwa hamaki wanaweza kukutajia mapesa chungu nzima kutokana na Ubakhili wa Roho na hamaki za kupewa Talaka) Na kama ikiwa Mwanamme anajua haki na yeye Mcha Mungu basi anaridhia ombi hilo la Mwanamke.
Na Hadith iliyomo katika Sunnan al- Baihaqq "Inasema"
Mwanamke  alikuja kwa Bwana Mtume s.a.w akamwambia"Namchukia Mume wangu nataka aniache" Bwana Mtume s.a.w "Akamuuliza jee utamrejeshea shamba alokupa kama Mahari yako"Yule Mwanamke akajibu Naam na hata zaidi ya hayo" Bwana Mtume s.a.w akasema usirejeshe zaidi ya hayo.
Na kesi ya Mwanzo ya Khul katika Uislam imehadithiwa na Imam Bukhari kama hivi "Mke wa Thabit bin Qais kenda kwa Mtume s.a.w akasema""Ewe Bwana Mtume s.a.w"Mimi sijamkasirikia Mume wangu Thabit, kwa ajili ya mahamaki yake au dini yake, Lakini nakhofia kuna kitu kinaweza kutokea kwangu mimi kinyume na dini ya Mwenye Enzi Mungu, kutokana na sababu hiyo nataka niachike kutoka kwa mume wangu, Bwana Mtume s.a.w akasema jee utamrejeshea Thabit shamba lake alokupa kama mahari ili uachike, akajibu naam, akamwambia Thabit chukua shamba lako na mpe Talaka yake.
 hivyo ndivyo mambo yanavokwenda hakuna kuteseka kwenye ndoa ila kinachotakiwa ufate hiyo sheria ya (Khul) katika mahakama za (Qadhi) ili ipate kuthibitishwa, lakini huna haja ya kuteseka na jambo usilolipenda, kuvumilia madhila na kero na machungu Dini imekupa nafasi na wewe Mwanamke kuamua jambo hili, na huo ndio usawa na hiyo ndio haki aliyokutakieni Mollah wenu. Lakini ole wako usije kufanya mambo haya ukawa nyuma yake kumbe kuna (Kicheki Bobi) kinakusubiri uwachwe, uharibu maisha yako na ya watoto kwa ajili ya mambo machafu, utatiwa machungu na adhabu mpaka mwisho wa umri wako, hiyo ndio tahadhari ninayokupa, lakini kama hakuna sababu za udanganyifu ila humpendi mumeo, au mateso yamezidi, au kakutupa basi kamata peni na karatasi umalize udhia huo na Mungu atakusaidia.