Sunday, March 24, 2013

FAIDA ZA IMANI-PART-1

Asalaam Aleiykum,

Kuamini na Imani ni vitu viwili tafauti, Na kama ulikua umejaa furaha ya kujinasib moyoni, au fikira zimekuingia yakwamba sasa unavuja Imani basi jaribu japo kidogo kujiangalia tena jee ni kweli mimi ninayo Imani. Jitizame kwa undani ikisha jiulize nina Imani au Na amini tu. Kama utakua na wasiwasi wa matamshi hayo yatazame hata herufi zake mwanzoni zimeanza  tafauti.
Nini Kuamini?
Kuamini ni kitu rahisi sana, kuamini daima inaishi  kwenye mdomo, kuamini haileti mabadiliko kwa mwanaadamu, kuamini ni kazi ulokwisha fanyiwa ukaambiwa sasa Amini, na wewe ukakubali, kwa hiyo kilugha kuamini haina tafauti na (Kukubali). Ni kazi nyepesi sana, ndio maana utaona ukimbana mtu kwa ufundi wa lugha, na ukamthibitishia kuwepo kwa Mwenye-enzi-Mungu na ni mmoja, basi Mja huyo anakubali mdomoni, na ukimwambia sali sala tano atafanya muhimu kutekeleza mambo hayo yote, lakini hasara yenyewe hayo yote yana malizikia mdomoni tu.
Najua nasema haya pengine yanakugusa moyoni ama iwe kwa ukweli au hamaki, sababu wewe na mimi tunasali siku zote vipi leo iwe hatuna Imani. Hiyo ndio kusudio langu katika darsa hii ya leo kugonga katika moyo wako ili upate kufanya jitihada zaidi ya kwenda huko kwenye Imani kamili.
Kusudio langu nataka tuwachie huu uzi wa kuamini ambao mara kwa mara unakwenda ukikatika, ili turukie kamba ya Imani isokatika daima. Kwani ukibakia kwenye uzi milele utakua mashakani, kwani ndani ya kuamini huwi mkweli, unaficha makucha yako, bado unabeba bango la wasio na Imani, bado upo nusu nusu, hujui kweli au unadanganywa, moto upo au wanapiga kelele tu, hizi hadith zinaweza kuwa sahihi au sio sahihi, katika kuamini umegubikwa na mashaka, japokuwa umeshapiga hatua ya mwanzo, ndio vizuri umekubali, umeshaanza kujitahidi, kuna mambo yanakupa matumaini, kuna kitu kinakuvuta kwenye Imani na sio kimoja viko vingi lakini hutaki kunyanyua mguu wa pili kwenda kwenye hiyo Imani, unaona watoto wanazaliwa, unashuhudia watu wanakufa, usiku unaona nyota mbinguni, lakini yote hayo bado hayajakufanya unyanyue hatua ya pili kuingia ndani ya Imani kamili.
Bado hujawa tayari kufanya jitihada kukipata kile kikubwa chenye thamani, ambacho kama utakipata unakua umeshakamilisha maisha, umeshafuzu katika Ulimwengu huu, umeshapata hizo (Pepo mbili)Umeshafaulu mtihani, huna dhiki tena, Maisha yako daima utaishi kwa furaha. Sasa ni kitu gani hicho chenye thamani hii lakini kila mmoja wetu hafanyi juhudi yoyote kukipata, nini hicho.
Hakuna chengine isipokua ni Imani, kutaka kujua nini Imani ?Endelea part 2

FAIDA ZA IMANI-PART-2

Asalaam Aleiykum,

Nini Imani?
Imani ni ukweli usokua na tafsiri, hakuna lugha yenye kuweza kufasiri nini Imani, njia moja tu inayoweza kukufahamisha maana ya Imani ni (Experience)kuishi katika hali hiyo ya Imani katika moyo wako, Hapo ndipo inapokaa Imani, na Imani au hali hiyo ya (Ukweli)ina sifa moja ikisha ingia moyoni haitoki tena, na chochote kiingiacho moyoni jua kimetokea kwa Mollah wako. Imani ni kitu kikubwa kisicho mwanzo wala mwisho, Imani ni mfano wa (Taa au Nuru) yenye kumurika yote yaliyomo kwenye ulimwengu huu, Imani ni taa popote penye giza inamurika ili vionekane vyote vilojificha, ndio utaona ukikaa na mwenye Imani aidha utamkimbia, kwanini unamkimbia kwa sababu woga unakua ushamtoka na anaweza kusema chochote kufanya chochote ambacho kinyume na matarajio yako,  au utamfata kila anapo kwenda kwa sababu na wewe ushaanza kuonja ladha ya Imani.
Sasa nini faida za Imani?
Kitu cha mwanzo(1) kuanza kujua kuwa Imani inaingia katika nafsi yako ni pale kuondokewa na Tamaa, matamanio yanakatika kabisa, nisije kusema matamanio ukaruka na kudhani nakusudia tendo la (Ndoa)laa, kusudio hapo ni tamaa ya maisha, upate hiki au upate kile, hichi unataka na kile lazima upate, kwanini tamaa inakatika, sababu tamaa ni upungufu, Na imani ni yenye kuondosha upungufu inakujaza moyo wako, na moyo ukijaa lazima vile vyote vya nje vipungue(Inaitwa kukinai), huwezi kuwa na Imani na huku unatafuta utajiri, unataka ujenge jumba la ghorofa, huwezi kuwa na Imani ukawa unapokea Rushwa, huwezi kuwa na Imani ukawa unatesa wenzio, huwezi kuwa na Imani ukawa unapita kudhulumu wenzio, huwezi kuwa na Imani bado tamaa imekushika, huwezi kuwa na Imani ukawa unapita ukizini, Imani haikai pamoja na upungufu hilo likumbuke sana, kwani Imani ni kitu chenye kutosheleza yote pasi na kuacha hata jambo moja pembeni.
Kitu cha pili(2) kujua sasa Imani inaongezeka ni kujawa na Huruma, unaonea Huruma kila chenye kuishi, kuanzia wanyama,watu, maskini na matajiri kadhalika,wagonjwa ukenda kuwatembelea machozi yanakutoka, hakupiti kizee pasi kuwa na fikra za kumsaidia, huruma zako zinaenea katika kila chenye uhai aloumba Mollah wako.
Jambo la Tatu (3) Imani inakufunika kwa guo la upole wa tabia, mazungumzo, mpaka vitendo vyako.
Jambo la Nne (4)Imani ikifurika ndani ya moyo wako, uongo unatoweka, inakuwa huwezi kudanganya tena, huwezi kusengenya, inakua vigumu kwako kumlaghai yoyote, kila ulisemalo ni kweli tupu, wasiwasi unakuondoka, macho hayachezi tena kwa sababu uongo ushatoweka, sasa ni kweli tu ndio yenye kuishi katika moyo wako, hapo ndio mwanzo wa kuona kila mtu anakukimbia, wengine wanakuona sasa huyu anaumwa, ukimgusa tu anasema ukweli, marafiki wa uongo hawakai na wewe inakua mwiko kwako kukaa nao.
Jambo la tano (5)Imani ikifika katika daraja hii sasa wewe mwenyewe unageuka kuwa Imani, unakua taa au nuru yenye muangaza wa mfano kwa wale wenye kuisaka Imani. Na Imani ikijaa katika moyo wako inageuka (kuwa Mvuto) hapo kila mtu anataka kuwa awe pamoja na wewe na hapo ndipo jambo la sita linatokezea. Endelea part 3


FAIDA ZA IMANI-PART-3

Asalaam Aleiykum,

Kitu cha sita (6) kukutokezea katika faida za Imani ni pale yanapo ibuka mapenzi, na mapenzi ni yenye kukupeleka karibu na Mollah wako nayo ndio hiyo (Taqwa) Ucha Mungu, na elewa Ucha Mungu ni furaha, ucha Mungu ni kitendo cha kuondokewa na utendaji wa (Madhanbi) na ukiondokewa na Madhanbi hapo unakua nafsi yako imejaa vitendo vyema, na nafsi ikijaa matendo mema maisha yako yanakua ya aina nyengine kabisa, unakua ushaongozwa katika maisha ya kidini na hapo unapata faida kubwa kabisa ya Imani kama ilivyotajwa katika sura ya Yunus aya ya 9 mpaka 10.
"إِنَّ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ يَہۡدِيهِمۡ رَبُّہُم بِإِيمَـٰنِہِمۡ‌ۖ تَجۡرِى مِن تَحۡتِہِمُ ٱلۡأَنۡهَـٰرُ فِى جَنَّـٰتِ ٱلنَّعِيمِ"
"hakika wale waloamini na kufanya vitendo vizuri, Mollah wao atawaongoza kwa ajili ya Imani zao, itakua inapita mito mbele yao, katika hayo Mabustani yenye neema(Peponi)"
"Wale walokubali wakafanya matendo mema kama nilivo zitaja faida za Imani huko mwanzoni basi wao wanafunguliwa na kuongozwa katika hiyo Imani au (Taa-Nuru)maalumu inakua muono wako ni wa aina nyengine, unakua kama uliye kamata (Torch)tochi unasita kutenda (Dhanbi) kwa sababu dhanbi ni zenye kukaa kizani na wewe sasa una taa vigumu kwako kutenda maasi tena, hujikwai tena kwani unaongozwa na taa ya Mwenyewe Muumba wa Mbingu na Ardhi, sasa vipi tutajua kuona huku wakati sisi hatujafikia hiyo Imani, mifano ipo binaadamu ana njia mbili za kuona njia ya kwanza unaona kwa kutumia Akili, pale ambapo jambo unalijua na mfano wake ni huu.
Huo mfano ni Rahisi sana, Jitizame wewe ukimuona Mwizi unakuaje, vipi unabadilika, tahadhari gani unachukua, na pengine Mwizi hana hata habari kama wewe upo hapo, Na mfano wa pili jiangaliea ukimuona  au mtu mwema unakuaje. Ukisha maliza hapo sasa nenda kakitizame kitoto kichanga kilozaliwa leo au jana hapo utajua tafauti, hao wawili wa mwanzo unatumia Akili kuwatizama kutokana na uchambuzi wako, lakini hichi kitoto kichanga Akili haijui chochote kuhusu kiumbe hiki kwa hiyo hapo hutumii Akili kabisa, Akili hapo haipo, hapo upo wewe na kitoto(Pure) na hapo ndipo inapokaa Imani, unakiona kitoto kwa njia nyengine kabisa, fanya uchunguzi utayajua hayo, huwezi kuona kitoto kichanga ukaanza kufikiri atakua Rubani au atakua Mwizi, au Sheikh, unakiona kwa usafi  kitoto ni kitoto tu na hivyo ndio mwenye Imani aonavyo ila huzidi mara zisohesabika kwa mwenye Imani, ndio maana utaona mwenye Imani yuko tayari kufa kwa Imani yake, sio kama Imani yako na yangu ukisikia jiwe limeanguka kwenye Bati unataka kutoka Dini.
Sasa wakisha kupata jambo hilo la Imani, licha ya kuishi Maisha ya Salama na furaha katika Ulimwengu huu na huko wendako wanapata hayo ya kuingia (Peponi) na Mito ikipita katika Makasiri yao ya huko walikoandaliwa na Mollah wao kwa ajili ya jambo hilo la Imani, kwanini wakapata hivyo, kwa sababu hawakuijali Dunia ila walifanya jitihada ya kuipata Imani ambayo ndio ilowafanya waepukane na madhanbi,dhuluma, na maasi mengine, huku wakijishughulisha kumkumbuka Mollah wao kwa Taqwa.
Maisha yao yanakuaje huko (Peponi)?
"دَعۡوَٮٰهُمۡ فِيہَا سُبۡحَـٰنَكَ ٱللَّهُمَّ وَتَحِيَّتُہُمۡ فِيہَا سَلَـٰمٌ۬‌ۚ وَءَاخِرُ دَعۡوَٮٰهُمۡ أَنِ ٱلۡحَمۡدُ لِلَّهِ رَبِّ ٱلۡعَـٰلَمِينَ"
"Ibada yao ya (Dua)humo itakua (Utakatifu ni wako) Ewe Mwenye Enzi Mungu, Na maamkizi yao humo ni Salaamun, Na dua yao ya mwisho ya kushukuru ni Sifa zote njema anastahiki Mwenye Enzi Mungu, Mollah wa Ulimwengu wote"
Huyo ndio mwenye Imani ambayo sote tunaitamani tuwe nayo, na hilo ndio liwe  dhamira ya kila mmoja wetu mwenye kutaka kuwa karibu na Mollah wake, inataka uamuzi tu wa kunyanyua hiyo hatua ya pili kwani ya mwanzo ushanyanyua nini kinakuzuia kupiga hatua nyengine ambayo itakufikisha kwenye zawadi ya Milele.
Nakuomba Mollah wangu tuzidishie Imani, walokubali wafanye waamini, wenye kuamini wazidishie Imani na wenye Imani Yaa Rabbi wafanye tuwajue ili wawe vipenzi vyetu. Amin

Saturday, March 16, 2013

SIKU YAKO YA KUFA-PART-1

Asalaam Aleiykum,
Nakukaribisheni kwenye darsa hii "Enyi" wacheza (Birthday) Na wewe mkumbukaji wa siku yako ya harusi(Anniversery) na hata yule mpiga mayowe ya kuzaliwa kwa chama chako, Mbona umeisahau Siku ya kufa kwako, wakati unajua ipo, inakuja na ishakaribia. Nikisema ipo maana yake imetuzunguka kila siku inatokezea, lakini kusudio langu ni  ile  mnayoifahamu ya mtoto mdogo(Kichanga), Na hii ya pili yakuja, hiyo inawahusu vijana kuwa japo mmesahau lakini mgeni yuko karibu au pengine keshafika, anasubiri umkaribishe au yupo kwa jirani akitoka hapo anakuja kwako. Na ama hii  ishakaribia,  hii ni ya watu wazima  kifo kishatoa taarifa, kimeshagonga mlango, tayari kimeshatanguliza dalili, Viungo vyote sasa vinaelekea kusini, kwa sababu ulivokua mdogo vilikua vinaelekea kaskazini, ulipofika ujanani vikarejea katikati, na sasa umekua mzee vinataka kurejea vilipotoka.
Vimeshaleta ishara labda una magonjwa ambayo hayaponi tena, pengine nywele zishapiga weupe zimekua rangi ya kitambaa cha sanda, na mpaka nguvu za kukimbia zishatoweka, kutembea pia kwa mashaka, Mauti yashahudhuria na wewe huna tena amri ya kuzuia tukio hilo.
Sasa nini cha kufanya? Ukitaka kujua cha kufanya ili upate (Tahfif)siku hiyo itakapo dhihiri, basi niazime macho yako ili iwe (Tochi)yetu nikutoe kwenye kiza nikupeleke kwenye(Mwanga)Taa ya kufahamu vipi siku hiyo upate nafuu ya vishindo vyake, Na kabla hatujenda huko wacha nikujulishe nini Mauti?, Mauti ni jambo moja na Uhai vina uhusiano wa karibu, ni vitu venye kushirikiana sana katika kazi zao, najua utashangaa, ni wajibu wako kushangaa, ila kumbuka mwenye kushangaa ndie anaefahamu vizuri, mfano wa wa mtoto mwenye kuuliza hichi nini na hichi nini.
Sasa na tuanze na kuitupia macho aya inayotujulisha nini Mauti na nini Uhai, Aya ya 1-2 sura ya Mulk.
"تَبَـٰرَكَ ٱلَّذِى بِيَدِهِ ٱلۡمُلۡكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَىۡءٍ۬ قَدِيرٌ"

"Ametukuka yule ambaye mkononi mwake umo ufalme(Uwezo wake)Na yeye ni mwenye uwezo wa kila kitu(Yeye  ndiye alomiliki haya maisha)"
"ٱلَّذِى خَلَقَ ٱلۡمَوۡتَ وَٱلۡحَيَوٰةَ لِيَبۡلُوَكُمۡ أَيُّكُمۡ أَحۡسَنُ عَمَلاً۬‌ۚ وَهُوَ ٱلۡعَزِيزُ ٱلۡغَفُورُ"
"Ambaye ameumba Mauti na Uhai ili akujaribuni(kukufanyieni mtihani) ni yupi miongoni mwenu atakae tenda vitendo vizuri, Naye ni mwenye nguvu na mwenye kusamehe"
Naam: Aya ya pili imeanza mwanzo kwa kutaja mauti, unajua sababu gani ikawa hivyo, kwa sababu Mauti ndio mlango unaopita ukatokezea kwenye Uhai, mwanzo ulikua hupo katika maisha haya, na mfano wa hayo tizama Mti, kabla mti haujawa mkubwa inakuwepo mbegu, na hiyo mbegu lazima ife chini ya ardhi ili mti upate kuzaliwa, na wewe vile vile mfano wako ni kama huo, maumbile yako yanaanzia tokea tumboni, lazima Mauti yashirikiane  na Uhai, kwa wale wenye Elimu ya (Ukunga)au uzazi wanafahamu hilo vipi (Cells)hizi zinavofanya kazi na kufa na kujitoa (Copy) ili wengine waendelee na kazi.
Inaendelea kawaida hii katika umri mzima wa mwanaadamu mashirikiano ya Mauti na Uhai bila ya kuleta maumivu kwako, inafanyika (Process) hii ukiwa hai , hichi lazima kife ili kile kizaliwe  , yanakutokezea Mauti yakenda sambamba na uhai ndio maana unaona tafauti ulipokua mtoto, na ukawa kijana na mpaka sasa mtu mzima hiyo ni (Biological death) nilikua naitaja japo kwa ufupi kuonesha taathira za mauti, katika vazi la Umbile, Sasa hapa itabidi mnistahamilie niingie upande wa pili wa kusudio la hiyo aya ya pili  sura ya Mulk, ambayo munasaba wake ni kutujulisha(Spritual Death)Kutoka kwa Roho. kutaka kuyajua hayo Endelea Part-2

SIKU YAKO YA KUFA- PART-2

Asalaam Aleiykum,

Vipi kifo hichi kinatokea, safiri namie ili nikushike mkono tupate kuhudhuria Mauti haya ya (Final Death) Kwanza kabisa napenda uelewe Mwanaadamu ni muungano wa vitu viwili, unacho kitu cha kwanza nacho kutokana na hii ardhi(Sura ya Taha aya ya 55)
" مِنۡہَا خَلَقۡنَـٰكُمۡ وَفِيہَا نُعِيدُكُمۡ وَمِنۡہَا نُخۡرِجُكُمۡ تَارَةً أُخۡرَىٰ"
"katika(Kutokana na) hii ardhi, Tumekuumbeni, na Humo tutakurejesheni, na kutoka humo tutakutoeni mara nyengine tena"
Hiyo ndio sehemu ya kwanza ya mwanaadamu (Pande la Ardhi) lakini kumbuka uzuri una kitu  kilotokea (Mbinguni) nayo hiyo Roho ilo Tukufu, iliyo muhimu, yenye usafi ambayo ndio yenye kushereheka siku ya kuzaliwa na kuhuzunika au kufurahika siku ya kufa kwako, hiyo ndiyo (Roho) ilotoka mbinguni ikiwa safi haina doa, hiyo ndio yenye kutizamwa itafanya amali gani, hiyo ndio itakayo sutwa na ardhi kama ilivotajwa kwenye sura ya (Yaasin aya ya 65)
"ٱلۡيَوۡمَ نَخۡتِمُ عَلَىٰٓ أَفۡوَٲهِهِمۡ وَتُكَلِّمُنَآ أَيۡدِيہِمۡ وَتَشۡہَدُ أَرۡجُلُهُم بِمَا كَانُواْ يَكۡسِبُونَ"
"Siku hiyo tutaziba vinywa vyao,itazungumza mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa yale waliyokua wakiyachuma"
Naam hiyo ndio Roho inayo tajwa katika sura ya (Al-Maarij aya ya 4) "تَعۡرُجُ ٱلۡمَلَـٰٓٮِٕڪَةُ وَٱلرُّوحُ إِلَيۡهِ فِى يَوۡمٍ۬ كَانَ مِقۡدَارُهُ ۥ خَمۡسِينَ أَلۡفَ سَنَةٍ۬"
"Malaika na Roho hupanda kwake katika siku ambayo muda wake (Kwa makadirio)ni miaka elfu hamsini."
Sasa ikiwa hii ardhi na hiyo Roho zinapotaka kutenganishwa ndio linatokea hilo tukio zito(Ambalo nimelifafanua kwa urefu katika darsa yangu ya kukabiliwa na Mauti) hapa pana kazi kubwa sana , na hapa ndipo anapohudhuria yule (Surgeon Specilist)Malaika wa kutoa Roho, cha mwanzo kabisa kinachfanyika ni kukata mawasiliano inaondoshwa Sauti na macho vinakua havifanyi kazi tena, kama afanyavo operesheni Daktari wa kawaida, ila tafauti inayopatikana hii operesheni ya Kufa, inakua wale walokuzunguka wao hawaoni nini kinaendelea, lakini wewe mwenye kutolewa Roho umacho na unahisi kila kitu kinachotendeka.
Wanakwambia Malaika leo ni siku ya kutenganishwa na mwili wako uloishi nao miaka 60 mpaka 70 na machungu ya kutenganishwa huku ni makubwa sana hayana mfano, utatamani upewe Bahari yote ili ikate kiu yako, ikiwa mgonjwa wa saratani anaumwa anapewa dawa za usingizi hazifai, anapigwa shindano machungu hayaondoki nini habari yetu sisi kuja kutolewa Roho na huku una Mabegi ya Dhanbi, inapatikana nafuu kama utakua katika hawa walotajwa katika aya ya hizi ya sura ya Waqiah,
"فَأَمَّآ إِن كَانَ مِنَ ٱلۡمُقَرَّبِينَ"
"Na kama akiwa (Mtu huyo anaye kufa) ni miongoni mwa wale walokaribishwa(Na Mwenye-enzi-Mungu)"
"فَرَوۡحٌ۬ وَرَيۡحَانٌ۬ وَجَنَّتُ نَعِيمٍ۬"
"Basi ni Raha(Tupu wakati wa kutoka Roho)na Manukato(Harufu nzuri) na Mabustani yenye neema"
Na kama utakua katika kundi la Muumin wa kawaida umemtii Mollah wako, imekuingia khofu ukaanza kutenda mema basi unaambiwa,
"وَأَمَّآ إِن كَانَ مِنۡ أَصۡحَـٰبِ ٱلۡيَمِينِ"
"Na kama akiwa ni miongoni mwa watu wa kheri(Muumin)"
"فَسَلَـٰمٌ۬ لَّكَ مِنۡ أَصۡحَـٰبِ ٱلۡيَمِينِ"
"Ataambiwa ni Salama kwako, (wewe)miongoni mwa watu wa kheri"
Hapo unapata Nafuu ya kuondoshewa machungu na dhiki za utokaji wa Roho, unapewa ganzi ya kuondoshewa fahamu na unakua kama vile mtoto anavozaliwa. Lakini kama ulikua umeishi maisha yako kwa njia ya ufisadi na una mizigo ya Dhuluma, basi unaachiwa kushuhudia mambo yote (Live).
" وَأَمَّآ إِن كَانَ مِنَ ٱلۡمُكَذِّبِينَ ٱلضَّآلِّينَ "
"Na kama akiwa ni miongoni mwa walokadhibisha, wapotofu"
"فَنُزُلٌ۬ مِّنۡ حَمِيمٍ۬"
"Basi karamu(Yako) ni maji ya moto yachemkayo(ili ukate kiu).
" وَتَصۡلِيَةُ جَحِيمٍ"
"Na kuwaka (Katika)moto"
Na kama unahisi utayaweza hayo hebu jaribu japo dakika moja kuzuia pumzi uone vipi unakua, hali hiyo unokua nayo sasa igeuze mara elfu moja ndio utapata kwa uchache vipi Roho yako itatoka, kwa sababu katika kutoka Roho kuna (Vital Energy) lazima ikatwe. kutaka kuijua hiyo Energy Endelea-Part-3

SIKU YAKO YA KUFA PART-3

Asalaam Aleiykum,

Kwenye hii (Vital Energy) inataka ufafanuzi wa ziada, sote tunaelewa kwa lugha ya sayansi wakati tunavuta hewa tunaambiwa tunavuta(Oxygen) huo ndio ufahamu wetu, lakini wale walo karibu na Mollah wao wanaelewa(Oxygen) ni gari tu ya kubeba na kukichukua hicho kilofichika ndani ya (Oxygen)kuna kitu maalum chenye kukufanya Uishi, hicho kinabebwa na hiyo (Oxygen) na kuingia katika Mwili wako, ukitaka kugundua hilo fanya ufike kujikurubisha na Mollah wako utapata kukijua nini hicho.
Naam kutoka kwa Roho ndugu zangu ni jambo kubwa na si la kufanyiwa maskhara kabisa, Nini habari yetu sisi tulozama kwenye maasi, itakuaje siku hii ikitukuta bado tumo kushughulika na dunia, vipi itakua tuje kutolewa Roho mbichi ilochafuka na madhanbi, ilokua ina ishi miaka nenda miaka rudi ikichuma na kufurahikia Maasi, vipi utakua utokaji wa Roho zetu.
Sasa ikiwa ndio Roho ishakata Tamaa, na matumaini hakuna tena na dhanbi ndio ushatenda na wala hazifutiki tena, nini cha kufanya? Jee kipo cha kufanya ili kupita katika daraja hili la Uhai na kwenda katika huo mji wa Mauti kwa salama. Naam la kufanya lipo na tena upande mmoja rahisi sana na upande wa pili mgumu sana, shauri ni kwako wewe kama utaweza, Jambo la kwanza ni lazima ukumbuke dhanbi zako zote ulofanya, kwanini nikakwambia ukumbuke kwa sababu nikikwambia ujute au utubu hutoweza kufanya  hivyo, ndio itakua unakwenda na kurudi pale pale, unatubu unajuta uongo halafu unaendelea tena, lakini nikikwambia ukumbuke madhanbi yako yote wakati unayakumbuka moja baada ya moja yatakupeleka katika hisia za makosa na hisia hizo zitakupeleka kwenye kujuta na ukianza kujuta basi jua ushaanza kutubu, na ukianza kutubu kinakuteremkia kilotajwaa katika Sura ya Zumar aya ya 53
" قُلۡ يَـٰعِبَادِىَ ٱلَّذِينَ أَسۡرَفُواْ عَلَىٰٓ أَنفُسِهِمۡ لَا تَقۡنَطُواْ مِن رَّحۡمَةِ ٱللَّهِ‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ يَغۡفِرُ ٱلذُّنُوبَ جَمِيعًا‌ۚ إِنَّهُ ۥ هُوَ ٱلۡغَفُورُ ٱلرَّحِيمُ"
"Sema Waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu, msikate tamaa na Rehma ya Mwenye-enzi-Mungu, Bila shaka Mwenye-enzi-Mungu husamehe dhanbi zote, hakika yeye mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu"
Hapo kwenye Moyo wako itaanza kuingia tamaa ya kusamehewa, anakutia Mollah wako Rehma zake na kukubadilisha kama ulikua unakwenda mwenendo wa kushoto unabadilika unaanza kwenda kulia, kama ulikua (Over-sex)itaanza kupungua na (Sex)matamanio yakipungua Taqwa(Ucha Mungu)unazidi na Taqwa ikizidi (Attachement)inapungua kama ulikua unapenda Mali, unakua hupendi tena, kama ulikua umezama katika mabiashara sasa unakua hupendi tena, kama ulikua unapenda watoto huwachukii lakini mapenzi yako yanahamia kwa Mollah wako, unapata kujijua kumbe mimi hapa Ulimwenguni(I belong to no one, and no one Belong to me)Nimekuja peke yangu, na nitaondoka peke yangu.
Na mapenzi yakihamia kwa Mollah wako hapo tena unapata kufahamu kwa undani  kumbe mimi sitoguswa na Mauti, ila mauti yanatendeka kwenye kiwiliwili changu, hapo ndipo yanapokutana baina ya Mauti na Uhai, na tabu zote nazipata wakati wa kutoka Roho yangu sababu kubwa kungangania hivi vilivyomo ulimwenguni, Unatolewa Roho yako huku huzuni imekushika umeacha mapesa mengi Bank, nyumba zako tano atarithi nani, hivyo ile gari wataitunza, wewe unaitwa Akhera hutaki kwenda unakwenda shingo upande, kuna mambo hujamaliza ndio maana mnagombeana Roho na Malaika, lakini ukiacha (Attachement) ukaridhika nini kinatokezea siku hiyo. unatolewa Roho huku umeridhika hupati uchungu hata chembe na huku unaambiwa.Al fajr-27-30
"يَـٰٓأَيَّتُہَا ٱلنَّفۡسُ ٱلۡمُطۡمَٮِٕنَّةُ"
"Ewe nafsi yenye kutua(Na matumaini)"

"ٱرۡجِعِىٓ إِلَىٰ رَبِّكِ رَاضِيَةً۬ مَّرۡضِيَّةً۬"
"Rudi kwa Mollah wako, hali ya kuwa umeridhika, na Mwenye-enzi-Mungu aridhike na wewe"

" فَٱدۡخُلِى فِى عِبَـٰدِى"
"Basi ingia katika (Kundi)la waja (Wema)

"وَٱدۡخُلِى جَنَّتِى"
"Uingie katika pepo yangu"
Hapo khofu  inakutoka, unakua si moga tena wa kukabiliana na siku hiyo, nini woga? woga ni sehemu katika sehemu za Mauti, ndio maana unakua na khofu kubwa, nini Ushujaa? ushujaa ni sehemu katika sehemu za Uhai, na tafauti yake moga kajaa khofu, na shujaa hana khofu kabisa, ndio maana ukiumwa unaogopa kufa, na ukiwa mzima huogopi kutenda dhanbi.
Namuomba Mollah wangu atuweke katika utulivu wa kuikumbuka siku hii inayomkabili kila mmoja wetu, atupe takhfif itakapofika kila mmoja zamu yake, atukurubishe katika enzi yake ya kusubiri ili tupate shufaa ya tukio hili la siku ya kufa, atujaalie tupokewe kwa salama na amani katika Miliki yake ya Milele kama isemavyo aya hii ya Naziat" وَٱلنَّـٰشِطَـٰتِ نَشۡطً۬ا"  Na kwa wale wanotoa Roho (Za watu wema)kwa taratibu. Amin



Saturday, March 9, 2013

ELIMU YA UCHAWI NA MASHETANI-PART-1

Asalaam Aleiykum,
Leo tunaligusa somo lenye kuwagusa wengi katika jamii kuhusiana na kadhia hii ya (Uchawi na Mambo ya Mashetani)si dhumuni langu kufundisha au kutilia nguvu jambo hili, lakini nia yangu kufahamisha chanzo na madhara ya wenye kushiriki katika jambo hili hususan tukiwa tumebeba (Mabango ya  kujiita sisiWaumini)Nitaanza maudhui hii kwanza kuzungumzia (Uchawi)halafu nitagusia (Mashetani), Kwanini nikafanya hivyo, Sababu kubwa (Shetani)ni Mwalimu wa huu uchawi, kwa hiyo kwanza nimeona nitaje somo halafu ndio nimtaje (Mwalimu)wa somo hilo.
Nini Uchawi?
Kwa ujuzi wangu Uchawi ni (Inner-Science)Sayansi ya Ndani ya Upande wa pili tusiouona, Katika sayansi hii isiyo onekana ina mrengo wa kushoto ya (Ufisadi na uharibifu)na Kuna Mrengo wa kulia ambao huu ndio huo wa (Tabibu nk), Inapatikana Elimu hii kwa njia mbili ya mafundisho au ya kuingia mwenyewe kwa taaluma makhsusi ambayo inachukua muda kufanikiwa kuingia katika hii (Psychic-World)katika dunia hiyo ya sayansi ya (Uchawi),kuna dhamana maalum ya yoyote mwenye kuingia basi itabidi ajiandae kwenda (Motoni-Jahnnam)kwa sababu vishawishi vilivyomo ni vikubwa sana mwanaadamu wa kawaida ukiingia lazima upotee, na Dalili mnaziona kwa wale wenye kupata tone la elimu hii vipi wanakua katika shughuli zao za kila siku zenye kuambatana na (Shirk na Uharibifu)"Ameangamia yule anokwenda kwa wanoitwa Mganga akataka cheo au fulani adhurike".
Elimu hii ya Uchawi inaandamana na mambo mengi, makubwa katika hayo ni (Mind-Elecricity-Sound)Ukiingia katika Elimu hii unakutana na utawala au uwezo wa (Control-other's mind)unakua na uwezo wa elimu ya kuharakisha maradhi kwa wanaadamu wenzio, unakua na uwezo wa kuchezea akili za wenzio, na katika kuzidi elimu hiyo unapata sasa uwezo wa kutumia (Electricity and Air)Umeme na hewa kwa njia za kuruka, kupeleka ujumbe wako, kufanya vitu kuonekana na kupotea, na kwa ajili ya (Sound) Sauti unapata uwezo wa kuwatia maradhi wenzio kubadilisha matukio nk, hayo yote ni mambo yenye kukupeleka (Motoni).
Sasa nilipoita Sayansi ya ndani nilikua na maana ya mifano hii, kama vile vifanyavyo kazi vitu hivi, (Mind)Akili Ukiingia katika (Field)uwanja  huu jambo la mwanzo lazima ufanye ni (Shirk) kwa sababu kama unataka fulani adhurike, au yamkute mauti, au mke na mume waachane lazima ufanye (Connection)Mawasiliano na (Cosmic Mind) ambapo unatumia mawasiliano ya (Energy) nguvu maalum kusafirisha (Madhara au maradhi)yende kwa fulani, ndio maana Waganga wanataka jina na mambo mengine ili wapate kumshirikisha Mwenye-enzi-Mungu kutumia hiyo (Energy)yao ndogo kusafirisha au kugeuza mambo kutumia (Special Power)sitaki kueleza vipi na wapi hiyo (Specia Power) ipo ili asije kila mmoja wenu akataka kuwa Mganga, kwani kila Mganga mwenye kuleta madhara kashachukua dhamana ya kukaa motoni pamoja na huyo alokwenda kufanyiwa hiyo haja yake. Sasa kutokana na Ufundi huo wa uchawi anatumia mtumiaji nyenzo maalumu ya hii (Electricity signal)kusafirisha matakwa yake hata kwa mtu aliye mbali ili adhurike, sote tunajua katika Sayansi ya nje kuna kitu kinaitwa (Electrical Ray's) au mionzi inavo mponesha mtu kwa magonjwa mbali mbali, na pia sasa tunaelewa Akili (Mind)inafanya kazi kutumia hizo (Electrical-signal) kwa hiyo Wachawi wamegundua zamani elimu hiyo na wakawa wanaitumia kwa matakwa yao ya uharibifu na ufisadi.
Na hili la Tatu la (Sound) hili nalo lina mfano ule ule wa (Elecricity signal) hakika sauti ina mambo mengi mengine wenyewe mnayaona mtoto akiimbiwa nyimbo analala kwa nguvu za sauti, Wale watu wa dhikr wanajua kama likitajwa neno la (Allahu-Allah)kwa sauti moja  na kwa muda mrefu, basi inapatikana harufu ya (Ubani) na hapo ndipo ilipogundulika mti huu wa (Ubani)ikawa mpaka leo watu wakifanya visomo wanachoma ubani, kwa sababu hawana wakati wa kudhikr mpaka ikapatikana hiyo harufu ya ubani, Na ubani pia umegunduliwa una (Connection) na (Mind) unaleta utulivu, unaondosha tafrani (Dipression au stress)wewe jaribu kama una (maudhi yako fukiza ubani na moshi vuta kwenye pua utaona manufaa yake)kwenye (Brain) yote hayo yamegunduliwa kutokana na (Sound) Naitaja (Sound) kwa njia ya kheri kwa sababu katika njia ya shari ina balaa kubwa na siwezi kuzitaja hadharani, wazee wangu wa kingazija walikua na elimu hii ya (Sound)wakiita (Burdai)sijui kama mpaka leo ipo au vipi? ilikua elimu hii kama kuna mgonjwa taabani wakukatiwa tamaa basi huja wasomaji wa dua hii ya (Burdai)ilopangwa kwa mpango maalum, wanasoma wakimaliza basi ama mgonjwa anapona au ana ana aga dunia na (Kufariki), kitizamo hapo sio kisomo ni ile (Sound) au sauti wanayoitoa wasomaji ndio inayoleta matokeo, walikuwepo watu miaka ya nyuma wenye kujua elimu hii ya (Sound)wakafanya utafiti, alichukuliwa ndege akawekwa mbele ya huyu mwenye elimu hii ya kichawi, yule bwana akafanya sauti fulani ndege akaanguka na kuzimia na akafanya tena yule ndege akaamka na kuruka. hii kwa uchache ni kuonesha vipi huo Uchawi unafanya kazi zake, sasa nini Quraan inasema kuhusu kadhia hii.
Endelea Part 2

ELIMU YA UCHAWI NA MASHETANI-PART 2

Asalaam Aleiykum,

Quraan Baqarah aya ya 102.

"وَٱتَّبَعُواْ مَا تَتۡلُواْ ٱلشَّيَـٰطِينُ عَلَىٰ مُلۡكِ سُلَيۡمَـٰنَ‌ۖ وَمَا ڪَفَرَ سُلَيۡمَـٰنُ وَلَـٰكِنَّ ٱلشَّيَـٰطِينَ كَفَرُواْ يُعَلِّمُونَ ٱلنَّاسَ ٱلسِّحۡرَ وَمَآ أُنزِلَ عَلَى ٱلۡمَلَڪَيۡنِ بِبَابِلَ هَـٰرُوتَ وَمَـٰرُوتَ‌ۚ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنۡ أَحَدٍ حَتَّىٰ يَقُولَآ إِنَّمَا نَحۡنُ فِتۡنَةٌ۬ فَلَا تَكۡفُرۡ‌ۖ فَيَتَعَلَّمُونَ مِنۡهُمَا مَا يُفَرِّقُونَ بِهِۦ بَيۡنَ ٱلۡمَرۡءِ وَزَوۡجِهِۦ‌ۚ وَمَا هُم بِضَآرِّينَ بِهِۦ مِنۡ أَحَدٍ إِلَّا بِإِذۡنِ ٱللَّهِ‌ۚ وَيَتَعَلَّمُونَ مَا يَضُرُّهُمۡ وَلَا يَنفَعُهُمۡ‌ۚ وَلَقَدۡ عَلِمُواْ لَمَنِ ٱشۡتَرَٮٰهُ مَا لَهُ ۥ فِى ٱلۡأَخِرَةِ مِنۡ خَلَـٰقٍ۬‌ۚ وَلَبِئۡسَ مَا شَرَوۡاْ بِهِۦۤ أَنفُسَهُمۡ‌ۚ لَوۡ ڪَانُواْ يَعۡلَمُونَ "
"Wakayafata yale (walozua)kuyafata mashetani, Katika ufalme wa (Nabii) Suleiman (a.s) Na hakukufuru Suleiman, bali Mashetani ndio walokufuru, Wakiwafundisha watu Uchawi(Walokuwa wanaujua toka mwanzoni) Na (elimu ya Uchawi)ulioteremshwa kwa Malaika wawili Haruta na Maruta, katika mji wa Babil(Babiloni)(Malaika hao)hawakumfundisha yoyote mpaka wamwambie, Hakika sisi ni mtihani(wa kutizamwa kwenu)basi usikufuru, Wakajifunza kwao ambayo (Katika elimu hiyo)waliweza kumfarakisha mtu na mkewe (Na mambo chungu nzima). Wala hawakua wenye kumdhuru yoyote kwa hayo ila kwa idhini ya Mwenye-enzi-Mungu. Na wanajifunza ambayo yatawadhuru wala hayatawafaa, Na kwa yakini wanaju kwamba aliyeridhi haya hatakuwa na sehemu yoyote katika Akhera, Na bila shaka ni kibaya kabisa walichouzia nafsi zao laiti wangalijua."
Naam, Nabii Suleiman a.s yeye alipewa Elimu hii lakini kupitia Mrengo wa kulia, akawa mwenye kusikia sauti, kuumiliki upepo na majini, ndipo walipomzulia kuwa yeye si mtume bali ni mchawi, ndio wakajibiwa alikua anajua elimu hiyo lakini hakukufuru, lakini walo kufuru ni Majini na watu wenyewe kwa kuwafundisha watu uharibifu na ufisadi mwengine kama vile kuchezea akili ya Mke na Mume na kuwagombanisha, wanatumia ile (Method) ya (Mind elecritical signal) na kuisambaratisha na kama kumtia mtu chuki nk, Malaika wale walotumwa walifundisha watu kwa masharti, kwanza wakiwaambia sisi tumekuja na (Mtihani)hii elimu tulo nayo ni Mtihani kwenu ukiingia umeumia, wachache sana wanovuka wakaamua kuwa (Matabibu)wa huo Uchawi, lakini wengi wenye Elimu hii lazima wakufuru, ndio maana ukiigusa elimu hii basi jiwekee wewe mtu wa  Motoni, sababu vishawishi vyake ni vikubwa na hapo ndio unapokutana na mwalimu wako Shetani.
Shetani anafanya nini? Shetani yuko jirani na elimu hii japokua si wenye kuimiliki kikamilifu lakini wanachangia sana katika kumkufurisha Mwanaadamu, Wanapendelea sana Mashetani kuwaandama wanawake kutokana na wanawake kuwa na (Energy)ya (Nagative) ya kukubali, kupokea, ukiona mtu kapanda shetani na anasema lugha nyengine basi hapo kwa wenye kujua elimu ya (Hypnotism)watanielewa na kujua nini Shetani kafanya, Wale wenye kumjua (Hypnotist)wanajua vipi anavoweza kukuamrisha ufanye kitu na ukafanya bila ya ridhaa yako, basi na Shetani hutumia njia hiyo hiyo akaanza kuwakufurisha watu na hata kuwafitini.
Usidhani Shetani pekee ni mwenye kupasua ukuta akaingia hata wanaadamu wanazo elimu hizo pale wanapofanya kitu kupotea, na wala usidhani ni uzushi wa Mtu kuonekana sehemu mbili kwa wakati mmoja hayo yote ni katika elimu hizo nilozitaja huko nyuma ni vitu vinavyo wezekana na bado vipo. Shetani anayo vile vile elimu ya kuingia na kukaa katika mwili wa binaadamu na kuupoteza kabisa katika njia za haki, na nyinyi mnoshuhudia mkawa mnastaajabu nini kimetokezea kwa mwenzetu huyu. Lakini katika yote hayo Mwenye-enzi-Mungu hakutoa elimu ya kukiangamiza kiumbe(Kufa) isipokua kwa Idhini yake, hakuna jini wala binaadamu atakae kudhuru ikiwa wewe utajitupa katika elimu ya (Qadir)ya Mollah wako, katika Elimu hii hakuna chochote chenye kudhurika au kuguswa na dhara.Yoyote yule  Anaengia katika elimu hii ya Kichawi ni lazima anakutana na Bahari ya (Numerology)au Ramli, ambayo inamuangamiza kabisa, kuna wengine wenye kutizamia kwenye maji au kioo, bahari ya elimu hii ni kubwa na mimi sina wino wa kuimaliza, dhamiri yangu ilikua ni kuonesha japo kwa uchache vipi inakua na vipi Makosa yanopatikana kwa yule anofanya na anaeomba kufanyiwa, na yule mwenye kushiriki katika Imani za mashetani ajue huko ni kuangamia kukubwa, wala hakuna msamaha, na kwa utendaji wa mambo hayo umejiharamishia mwenyewe Pepo huko Akhera, kwa hiyo kama una jamaa au rafiki au Muislam mwenzio anaeshiriki mambo haya muonee huruma na umfahamishe simambo yenye manufaa kwa maisha haya ila ni vishawishi vya kukupeleka Motoni. Namuomba Mollah atuepushe na kupenda na kuyafata mambo haya, na wenye nayo Mollah awashushie muongozo na kuwacha itikadi hizi za Kishetani na elimu isiyo na manufaa.
Amin.

Friday, March 1, 2013

BARUA YA MCHA-MUNGU-PART-1

Asalaam Aleiykum,

Katika darsa yetu ya leo tunasoma Barua ya Mcha-Mungu, Basi nakuomba kama una Phd, au Master's au Degree yoyote ile basi iweke pembeni, Soma Maudhui haya ukiwa mweupe moyoni(Absent)hakuna kitu, hapo unaweza kuifahamu barua hii, lakini ukija umejaa mizigo ya elimu kichwani, hapo utakosa kumfahamu Mcha-Mungu na kusudio la maneno yaliyomo kwenye barua hii. Halafu kumbuka utakapoisoma usije ukafanya makosa ya (Kutuwama)kubakia kwenye maneno, bali fanya bidii na jitihada uyapasue hayo maneno ili upate ujumbe(Massage) iliyomo kwenye hayo maneno.
Inaanza Barua hii kwa mshangazo na maajabu makubwa, Anauliza Mcha-Mungu!! Jee ushawahi kujiuliza kwanini Mlevi akilewa Anayumba(Anapepesuka)? anaendelea kwa kusema lazima iko sababu, Na tayari kila mmoja wenu ana jawabu alilo taarisha kujibu, lakini subirini na hizo jawabu ili tupate nafasi ya kuendelea na Barua ya Mcha-Mungu. "Mwenye-enzi-Mungu katuumbia waja wake kitu kiitwacho (Sense) na hizo ziko tano ambazo tulokua tunazijua, Nazo ni (1)Kutokana na ngozi tunapata hisia ya kugusa(2)Kwa ajili ya Macho tunapata kuona, (3)Kutokana na masikio tunapata kusikia,(4)Na kwa njia ya ulimi tunapata kuonja Ladha,(5)Na la Tano ni hili la pua tunapata kunusa vilo vizuri, hizo ndizo tano tunazozijua na zenye kujulikana tokea hapo kale na wagunduzi wa majambo.
Ikatajwa ndani ya kitabu kitukufu chenye maneno ya ukweli mtupu ya kwamba  "وَٱلَّذِينَ إِذَآ أَنفَقُواْ لَمۡ يُسۡرِفُواْ وَلَمۡ يَقۡتُرُواْ وَڪَانَ بَيۡنَ ذَٲلِكَ قَوَامً۬ا" sura ya Furqan aya ya 67," Na Wale ambao wanatoa(Kutumia)hawafanyi israf(fujo-Ovyo) Na wala (hawazuii kabisa)hawafanyi Ubakhili, Bali wanakuwa kati kati baina(Balance) ya hayo".
Utakapo toa usifanye israf au kuzuia kabisa ila unatakiwa uwe umekaa katikati, umefanya (Balance)ya mizani usije ukayumba, usije ukatoa sana ukafilisika au kuzuia kabisa ukawa Bakhili, Hapo Mwenye-enzi-Mungu anaitaja (Balance)ambayo tumekuja kuigundua kupitia wana sayansi miaka ya karibuni kumbe kuna (Sense)ya sita inayomuweka Binaadamu kuwa (Balance) ili asiyumbe, Na nyinyi mnalishuhudia hilo kwenye mapigano ya Masumbwi kama atapigwa mmoja wao konde la sikio likampata utamuona mpiganaji huyo anavoyumba na hana tena (Balance).
Au kama mtu atafanyiwa Operesheni ya masikio akakosewa kidogo inakua hata kusimama hawezi keshakosa (Balance)Hiyo ndio hisia ya sita katika Umbile la Mwanaadamu, hilo ndilo alotuchagulia Mcha-Mungu kutuonesha kupitia mfano wa Mlevi, tumeoneshwa mfano huo kwa sababu hiyo (Balance) ipo kwenye (Physical na Mental) na Mcha-Mungu kagundua  sisi sote tunalewa ila tunabadilisha aina ya Mvinyo, Mlevi yeye kaamua kuyumba dhahir, lakini sisi wengine tunaamua kunywa siri siri, na sote tumetajiwa ulevi wetu na mtu ajitizame yeye anakunywa nini na kama hayumbi kwa siri, kuna wengine wana chupa ya Kiburi, hebu mtizame wewe vipi mwenye kiburi anavoyumba, wengine ulevi wao zinaa, wengine mvinyo wao Mali, wengine wamelewa chopi katika kutafuta pesa, wengine wanachupa za kula Rushwa, wengine wana ulevi wa maharusi Nk, na mambo mengi ambayo yanatufanya maisha yetu iwe mfano kama vile tupo Baharini, kila mtu anayumba na atizame mtu nini yeye kinamyumbisha hata ikawa hakai katika hiyo (Siratul-Mustakim).
Jitizame kwanini (Sense)yako ya sita inakutesa, nini khasa tatizo lako, mbona huna furaha, wapi chanzo chake kinatokea na upande gani nimeelemea jee niko katikati au nimezidi sehemu nyengine,  Mbona siwezi kuweka mizani yangu ya maisha sawasawa.
Jaribu kujifanyia mitihani midogo midogo upate kujua (Balance)yako iko wapi, angalia kama mtu atakupa Msahafu na pesa nini kina kufurahisha, ukiona pesa ndio inakufurahisha basi ushajua upande gani unakuyumbisha na pata wasi wasi mkubwa, na ikiwa umepewa vyote viwili na furaha yako ikawa iko kawaida na vyote umeviridhia basi wewe ushaipata (Balance) na hapo uko sawa ikija pesa sawa, ukija Msahafu sawa basi jijue huyumbi na tayari ushaanza kupiga hatua za Ucha-Mungu, na kama hayo yote yamekushinda sasa unataka msaada endelea na Barua ya Mcha-Mungu sehemu ya Pili ili ukaone msaada gani unapewa ili upate kuweka (Sense)yako ya sita katika mstari ulonyooka na ukisha kuwa huyumbi basi hapo safari ya Ucha-Mungu ndio imeshaanza.
Kuyajua hayo Endelea-Part-2


BARUA YA MCHA-MUNGU-PART-2

Asalaam Aleiykum

Haitakiwi katika maisha haya kufanya jambo ukayumba upande mmoja kama vile baadhi yetu tunavo jilazimisha tuonekana Wacha Mungu, Mtu asivae (Joho)la Plastic ikawa yeye aonekana Mcha Mungu mkubwa kumbe akifanyiwa mtihani mdogo kayayuka, kipitie kisa cha Sheikh mmoja wa (Plastic)na mwenzie walivofanyiana mtihani "Masheikh hawa wawili walikua na kawaida ya kuvipitia vitabu vya wanazuoni, leo nyumba ya huyu kesho ya yule mwenzie, kwa bahati wote wawili wakajifunga hawana haja ya kuoa, ila wanashughulika na mambo ya kutafuta Ilmu, baada ya miaka michache kupita yule Sheikh mwenye kuaminika kwa Ucha Mungu akaamua kuajiri Msichana wa kufagia na kumpigia pasi nk, Yule mwenzie akamwambia mbona unajipa mtihani asije shetani akakushika ukaja kulala na huyu msichana, yule Sheikh akahamaki sana, akamwambia mwenzie mimi na heshimika katika jamii na sikudhani nitasikia maneno kama haya kutoka kwako, kuanzia leo urafiki wetu umekwisha na nakuomba uondoke kwenye nyumba yangu sasa hivi, natoka nje nikirudi uwe ushaondoka,  baada ya muda Yule Sheikh akafunga vitabu vyake huyo akaondoka".
"Baada ya siku tatu akapokea barua kutoka kwa yule mwenzie anamwambia hivi""Sithubutu kusema kama wewe mwizi, ila ikiwa kwa bahati mbaya umeondoka na kitabu changu basi naomba unirudishie"Akakamata kalamu huyu mwenzie na yeye akaandika""Na mimi vile vile Sina dhamiri ya kukuita wewe Muongo, lakini ikiwa ungekua unalala kwenye chumba chako basi ungekiona kitabu chako" hiyo ndiyo Plastic ilivyo kuna wakati lazima inayayuka, kumbe Sheikh kafanyiwa mtihani kitabu kimewekwa kwenye kitanda chake, kumbe halali pale, ana lala chumbani kwa mfanyakazi wake, usivae juba la uongo, Ucha Mungu unakuja (Natural) huna haja ya kujilazimisha, usifanyie watu mfanyie Mollah wako na yeye atakuondoshea tabia ya kuyumba.
Mcha-Mungu ana tunongoneza tufungue Quraan sura ya Al-Hashir aya ya 18"
"يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱتَّقُواْ ٱللَّهَ وَلۡتَنظُرۡ نَفۡسٌ۬ مَّا قَدَّمَتۡ لِغَدٍ۬‌ۖ وَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ خَبِيرُۢ بِمَا تَعۡمَلُونَ "
"Enyi mloamini Mcheni Mwenye-enzi-Mungu na kila Mtu aangalie anayo tanguliza kwa ajili ya kesho(Akhera) Na Mcheni Mwenye-enzi-Mungu, hakika Mwenye-enzi-Mungu anazo habari mnayoyatenda"
Atizame Mja asiwe anayumba anapoteza muelekeo, yupo na kushughulika na mambo ya kipuuzi, umepewa (balance) ili uweze kushi katika ulimwengu huu katikati ya njia alokuwekea Mollah wako, ukianza kuyumba ushapoteza (Dira)na ukipoteza dira basi malipo yana anza hapa hapa Ulimwenguni, na kama unabisha hayo weye yumba ukione cha mtema-kuni. Tuna nongonezwa tena aya ya 19 " وَلَا تَكُونُواْ كَٱلَّذِينَ نَسُواْ ٱللَّهَ فَأَنسَٮٰهُمۡ أَنفُسَہُمۡ‌ۚ أُوْلَـٰٓٮِٕكَ هُمُ ٱلۡفَـٰسِقُونَ"
"Wala msiwe kama wale walomsahau Mwenye-enzi-Mungu, na (Mollah) Akawasahaulisha nafsi zao, hao ndio maasi wakubwa"
Hii (Sense) ya sita ndio inokufanya usahau, ukipenda mali lazima umsahau Molla wako, ukiwa na kiburi lazima wakati wote ukumbuke kiburi chako, kama unapenda maharusi saa zote unafikiri sijui ntaalikwa au sialikwi, hivi ndivo ilivo hiyo hali ya kuyumba, kama mlevi asivo kumbuka sala kasahau na wewe vile vile, jipime wewe mchezo wako unaanza na wakati wa sala umefika, Jaalia ndio unakwenda kusali, tumekubali, basi sala yako mwanzo mpaka mwisho anatawala (Actor)na nini kitatokea katika hiyo story, au kama mfanya biashara ndio unahesabu faida au khofu ya kuibiwa imekujaa, hivyo ndio maana ya kusahaulishwa nafsi zao, ikiwa wewe unamsahau Mungu na yeye anakusahaulisha kabisa, na huko kusahau ndio huku kuyumba, kwanini ikawa kuyumba, kwa sababu kuna wakati unakumbuka kumbuka mara moja moja.
"Basi nyinyi waumini msiwe kama wale walosahahu, usiwaonee choyo wale walokwenda kwenye Taarab, ila waonee huruma, usiwaone wanafaida walokwenda vilabu vya pombe, ila waombee dua wawache kumuasi Mollah wao, na wewe unaambiwa usiwe kama wao, kwani hao ni maasi makubwa wanayofanya,  wewe kuwa tafauti nao, na ukiwa tafauti basi jambo la mwanzo unasita kuyumba, na ukisita kuyumba hapo unaanza safari ya Ucha-Mungu.
Ananongoneza tena Mcha-Mungu tizameni aya ya 20:Endelea-part-3

BARUA YA MCHA MUNGU-PART-3

Asalaam Aleiykum,

" لَا يَسۡتَوِىٓ أَصۡحَـٰبُ ٱلنَّارِ وَأَصۡحَـٰبُ ٱلۡجَنَّةِ‌ۚ أَصۡحَـٰبُ ٱلۡجَنَّةِ هُمُ ٱلۡفَآٮِٕزُونَ"
"Hawawi sawa watu wa Motoni na Watu wa peponi, Watu wa peponi ndio wenye kufuzu".
Kwanini sasa ukatajiwa tafauti ya watu wa motoni na peponi na wewe huwajui, umetajiwa watu hao kwa sababu ushapewa ishara zao katika aya ilopita ukaambiwa wewe usiwe kama hao, hakika hao ni wenye kutenda Maasi, basi kuwa tafauti nao, usikubali kuyumba wala kuyumbishwa, na watu wa peponi ni wenye kufuzu, basi na wewe anza kuonja matunda ya peponi ungali hai kabla hujafika, ishi katika hiyo (Balance)usikope, usiibe,usizini,usiseme uongo,usidhulumu jiepushe na kila aina ya dhanbi, jikurubishe sana kwa Mollah wako hapo utapata mambo mawili la kwanza itakuteremkia (Dhikr) wakati wote utakua unamkumbuka Mollah wako na la pili itakushukia(Bliss) au (To live happy ever after).
Na aya ya 21 inatukumbusha kuhusu hii Quraan na ukweli wake na thamani ya maneno haya kwa kutwambia,
"لَوۡ أَنزَلۡنَا هَـٰذَا ٱلۡقُرۡءَانَ عَلَىٰ جَبَلٍ۬ لَّرَأَيۡتَهُ ۥ خَـٰشِعً۬ا مُّتَصَدِّعً۬ا مِّنۡ خَشۡيَةِ ٱللَّهِ‌ۚ وَتِلۡكَ ٱلۡأَمۡثَـٰلُ نَضۡرِبُہَا لِلنَّاسِ لَعَلَّهُمۡ يَتَفَكَّرُونَ"
"Lau kama tungeiteremsha hii Quraan juu ya Mlima, ungeliona ukinyenyekea (na)Kupasuka kwa khofu ya Mwenye-enzi-Mungu, Na hii ni mifano tunawapigia watu(wanaadamu)ili wafikiri".
Hapa limetajwa jambo la kushangaza, kuwa mlima ungenyenyekea na kupasuka kwa khofu ya (Mollah)wake, sasa swali la kujiuliza kwanini ukatajwa mlima, Umetajwa mlima kwa sababu kila chenye kuishi katika Ulimwengu huu basi kiko hai na kina ufahamu wake, utizame mti unaota ikisha unachomoza mizizi, ile mizizi kazi yake kupata (Nutrition)na maji kwa umbali ulokadiriwa, milima hali kadhalika, ina mungunyika na kujitengeza upya ili kuweka hiyo(Balance)(Kama nilivotaja katika mada ya Shukurani ya Uhai)tizama weye kila kiumbe kiwe kidogo au kikubwa kinavofanya kazi ya kutafuta Riziki yake kama alivo ipangia Mwenye-enzi-Mungu.
Basi Unaambiwa Utukufu wa hii Quraan, na uzito wa maneno haya lau ungejua thamani yake ungekwenda kwa tumbo kuyakiri na kuyatii maneno haya na maamrisho yake, na hiyo ndio mifano tunayopigiwa ili tupate kufikiri, Mollah wako hana haja ya kukitesa kiumbe chake, analo taka ni jambo moja fikiri tu, na ukiweza kufikri maane yake ushakumbuka, na ukikumbuka ina maana ushasita kuyumba, na ukisita kuyumba funga barua ya Mcha-Mungu sasa andika yako ili watu wapate kuisoma. Kwani na wewe Mungu kashakujaalia kuwa Mcha-Mungu.
Namuomba Mollah atuondoshee usahaulivu wa hii (Sense)ya sita na tukaanza kuyumba, atupe utulivu tusiyumbe mpaka tukawa hata katika huo Ucha-Mungu tunaongeza na (Riah)kujionesha, au tukayumba upande wa pili kuwa katika kundi la walomsahau Mollah wao na Mollah akawasahaulisha. Amin.