Sunday, March 24, 2013

FAIDA ZA IMANI-PART-1

Asalaam Aleiykum,

Kuamini na Imani ni vitu viwili tafauti, Na kama ulikua umejaa furaha ya kujinasib moyoni, au fikira zimekuingia yakwamba sasa unavuja Imani basi jaribu japo kidogo kujiangalia tena jee ni kweli mimi ninayo Imani. Jitizame kwa undani ikisha jiulize nina Imani au Na amini tu. Kama utakua na wasiwasi wa matamshi hayo yatazame hata herufi zake mwanzoni zimeanza  tafauti.
Nini Kuamini?
Kuamini ni kitu rahisi sana, kuamini daima inaishi  kwenye mdomo, kuamini haileti mabadiliko kwa mwanaadamu, kuamini ni kazi ulokwisha fanyiwa ukaambiwa sasa Amini, na wewe ukakubali, kwa hiyo kilugha kuamini haina tafauti na (Kukubali). Ni kazi nyepesi sana, ndio maana utaona ukimbana mtu kwa ufundi wa lugha, na ukamthibitishia kuwepo kwa Mwenye-enzi-Mungu na ni mmoja, basi Mja huyo anakubali mdomoni, na ukimwambia sali sala tano atafanya muhimu kutekeleza mambo hayo yote, lakini hasara yenyewe hayo yote yana malizikia mdomoni tu.
Najua nasema haya pengine yanakugusa moyoni ama iwe kwa ukweli au hamaki, sababu wewe na mimi tunasali siku zote vipi leo iwe hatuna Imani. Hiyo ndio kusudio langu katika darsa hii ya leo kugonga katika moyo wako ili upate kufanya jitihada zaidi ya kwenda huko kwenye Imani kamili.
Kusudio langu nataka tuwachie huu uzi wa kuamini ambao mara kwa mara unakwenda ukikatika, ili turukie kamba ya Imani isokatika daima. Kwani ukibakia kwenye uzi milele utakua mashakani, kwani ndani ya kuamini huwi mkweli, unaficha makucha yako, bado unabeba bango la wasio na Imani, bado upo nusu nusu, hujui kweli au unadanganywa, moto upo au wanapiga kelele tu, hizi hadith zinaweza kuwa sahihi au sio sahihi, katika kuamini umegubikwa na mashaka, japokuwa umeshapiga hatua ya mwanzo, ndio vizuri umekubali, umeshaanza kujitahidi, kuna mambo yanakupa matumaini, kuna kitu kinakuvuta kwenye Imani na sio kimoja viko vingi lakini hutaki kunyanyua mguu wa pili kwenda kwenye hiyo Imani, unaona watoto wanazaliwa, unashuhudia watu wanakufa, usiku unaona nyota mbinguni, lakini yote hayo bado hayajakufanya unyanyue hatua ya pili kuingia ndani ya Imani kamili.
Bado hujawa tayari kufanya jitihada kukipata kile kikubwa chenye thamani, ambacho kama utakipata unakua umeshakamilisha maisha, umeshafuzu katika Ulimwengu huu, umeshapata hizo (Pepo mbili)Umeshafaulu mtihani, huna dhiki tena, Maisha yako daima utaishi kwa furaha. Sasa ni kitu gani hicho chenye thamani hii lakini kila mmoja wetu hafanyi juhudi yoyote kukipata, nini hicho.
Hakuna chengine isipokua ni Imani, kutaka kujua nini Imani ?Endelea part 2

No comments:

Post a Comment