Asalaam Aleiykum,
Kitu cha sita (6) kukutokezea katika faida za Imani ni pale yanapo ibuka mapenzi, na mapenzi ni yenye kukupeleka karibu na Mollah wako nayo ndio hiyo (Taqwa) Ucha Mungu, na elewa Ucha Mungu ni furaha, ucha Mungu ni kitendo cha kuondokewa na utendaji wa (Madhanbi) na ukiondokewa na Madhanbi hapo unakua nafsi yako imejaa vitendo vyema, na nafsi ikijaa matendo mema maisha yako yanakua ya aina nyengine kabisa, unakua ushaongozwa katika maisha ya kidini na hapo unapata faida kubwa kabisa ya Imani kama ilivyotajwa katika sura ya Yunus aya ya 9 mpaka 10.
"إِنَّ ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ يَہۡدِيهِمۡ رَبُّہُم بِإِيمَـٰنِہِمۡۖ تَجۡرِى مِن تَحۡتِہِمُ ٱلۡأَنۡهَـٰرُ فِى جَنَّـٰتِ ٱلنَّعِيمِ"
"hakika wale waloamini na kufanya vitendo vizuri, Mollah wao atawaongoza kwa ajili ya Imani zao, itakua inapita mito mbele yao, katika hayo Mabustani yenye neema(Peponi)"
"Wale walokubali wakafanya matendo mema kama nilivo zitaja faida za Imani huko mwanzoni basi wao wanafunguliwa na kuongozwa katika hiyo Imani au (Taa-Nuru)maalumu inakua muono wako ni wa aina nyengine, unakua kama uliye kamata (Torch)tochi unasita kutenda (Dhanbi) kwa sababu dhanbi ni zenye kukaa kizani na wewe sasa una taa vigumu kwako kutenda maasi tena, hujikwai tena kwani unaongozwa na taa ya Mwenyewe Muumba wa Mbingu na Ardhi, sasa vipi tutajua kuona huku wakati sisi hatujafikia hiyo Imani, mifano ipo binaadamu ana njia mbili za kuona njia ya kwanza unaona kwa kutumia Akili, pale ambapo jambo unalijua na mfano wake ni huu.
Huo mfano ni Rahisi sana, Jitizame wewe ukimuona Mwizi unakuaje, vipi unabadilika, tahadhari gani unachukua, na pengine Mwizi hana hata habari kama wewe upo hapo, Na mfano wa pili jiangaliea ukimuona au mtu mwema unakuaje. Ukisha maliza hapo sasa nenda kakitizame kitoto kichanga kilozaliwa leo au jana hapo utajua tafauti, hao wawili wa mwanzo unatumia Akili kuwatizama kutokana na uchambuzi wako, lakini hichi kitoto kichanga Akili haijui chochote kuhusu kiumbe hiki kwa hiyo hapo hutumii Akili kabisa, Akili hapo haipo, hapo upo wewe na kitoto(Pure) na hapo ndipo inapokaa Imani, unakiona kitoto kwa njia nyengine kabisa, fanya uchunguzi utayajua hayo, huwezi kuona kitoto kichanga ukaanza kufikiri atakua Rubani au atakua Mwizi, au Sheikh, unakiona kwa usafi kitoto ni kitoto tu na hivyo ndio mwenye Imani aonavyo ila huzidi mara zisohesabika kwa mwenye Imani, ndio maana utaona mwenye Imani yuko tayari kufa kwa Imani yake, sio kama Imani yako na yangu ukisikia jiwe limeanguka kwenye Bati unataka kutoka Dini.
Sasa wakisha kupata jambo hilo la Imani, licha ya kuishi Maisha ya Salama na furaha katika Ulimwengu huu na huko wendako wanapata hayo ya kuingia (Peponi) na Mito ikipita katika Makasiri yao ya huko walikoandaliwa na Mollah wao kwa ajili ya jambo hilo la Imani, kwanini wakapata hivyo, kwa sababu hawakuijali Dunia ila walifanya jitihada ya kuipata Imani ambayo ndio ilowafanya waepukane na madhanbi,dhuluma, na maasi mengine, huku wakijishughulisha kumkumbuka Mollah wao kwa Taqwa.
Maisha yao yanakuaje huko (Peponi)?
"دَعۡوَٮٰهُمۡ فِيہَا سُبۡحَـٰنَكَ ٱللَّهُمَّ وَتَحِيَّتُہُمۡ فِيہَا سَلَـٰمٌ۬ۚ وَءَاخِرُ دَعۡوَٮٰهُمۡ أَنِ ٱلۡحَمۡدُ لِلَّهِ رَبِّ ٱلۡعَـٰلَمِينَ"
"Ibada yao ya (Dua)humo itakua (Utakatifu ni wako) Ewe Mwenye Enzi Mungu, Na maamkizi yao humo ni Salaamun, Na dua yao ya mwisho ya kushukuru ni Sifa zote njema anastahiki Mwenye Enzi Mungu, Mollah wa Ulimwengu wote"
Huyo ndio mwenye Imani ambayo sote tunaitamani tuwe nayo, na hilo ndio liwe dhamira ya kila mmoja wetu mwenye kutaka kuwa karibu na Mollah wake, inataka uamuzi tu wa kunyanyua hiyo hatua ya pili kwani ya mwanzo ushanyanyua nini kinakuzuia kupiga hatua nyengine ambayo itakufikisha kwenye zawadi ya Milele.
Nakuomba Mollah wangu tuzidishie Imani, walokubali wafanye waamini, wenye kuamini wazidishie Imani na wenye Imani Yaa Rabbi wafanye tuwajue ili wawe vipenzi vyetu. Amin
No comments:
Post a Comment