Sunday, January 27, 2013

MTAFUTA DINI, DUNIA LAZIMA IMPOTEE-PART-1

Asalaam Aleiykum,

Nakuomba Mollah wangu nikurubishe mie kwako weye na unijaze fikra zako kila saa na dakika, niwe mie mwenye kukumbuka wewe mpaka muda wa uhai wangu utakapo malizika. Nirekebishe kila pale nikoseapo, Ikisha niweke katika njia ya haki iliyo katika kusudio lako, na kila nikiteleza nakuomba Mollah wangu nirejeshe katika njia yako ilonyooka, kwa kuwa najua mimi ni kinyama sichukui dhamana yakua wakati wote nitakua nimesimama imara katika njia hii, kwa hiyo naomba Mollah wangu nitoe katika daraja hii ya kua kinyama na unipeleke kuwa katika daraja ya Roho njema ilotakasika na kila baya na ovu la Ulimwengu huu.
Hayo hapo juu ni maneno anayopasa kila mtafuta dini yawemo kwenye akili yake. Nani Mtafuta Dini?
Mtafuta dini ni yule ambaye sasa ameamua kuihama dunia huku akiwa na uchu nayo, bado anaijua utamu wake, lakini sasa kimemjia kitu chengine katika moyo wake na anajiuliza hivyo hakuna jambo jengine(Beyond)badala ya mambo haya ya kidunia?, Mambo haya yote ya Ulimwengu huu hayana faida, nikimaliza hili nataka lile, nandelea kuhitaji nikiwa sina kikomo na wala faida yake siioni, sasa hebu kwa mara ya mwanzo nikitafute hicho ninachoambiwa siku zote kina faida na mimi endapo nitaamua kuwa nacho, kitu chenyewe ni hichi kiitwacho dini.
Nini Dini? Dini ni ukamilifu wa maisha, lakini sio haya unayoishi hivi sasa, kuyataka maisha haya itabidi ubadilishe mwenendo au upinde kona kabisa kuelekea katika hayo maisha ndani yake yenye dini. kwanza elewa kwa undani kabisa Maisha haya ya Dini ni tafauti kabisa na maisha ya kidunia, vitu viwili hivi tafauti yake ni kama usiku na mchana au taa na giza havikutani kabisa ima iondoke taa lije giza au uondoke mchana uje usiku, havikutani kabisa, ndio maana darsa hii kichwa chake cha habari ikawa (Mtafuta dini,lazima dunia impotee)katika kuyakinisha haya Mwenye-enzi-Mungu katwambia katika Quraan(Al-Imran-145)
" وَمَا ڪَانَ لِنَفۡسٍ أَن تَمُوتَ إِلَّا بِإِذۡنِ ٱللَّهِ كِتَـٰبً۬ا مُّؤَجَّلاً۬‌ۗ وَمَن يُرِدۡ ثَوَابَ ٱلدُّنۡيَا نُؤۡتِهِۦ مِنۡہَا وَمَن يُرِدۡ ثَوَابَ ٱلۡأَخِرَةِ نُؤۡتِهِۦ مِنۡہَا‌ۚ وَسَنَجۡزِى ٱلشَّـٰكِرِينَ "
"Na nafsi yoyote haitoweza kufa ila kwa idhini ya Mwenye-enzi-Mungu(Na)kwa ajali ilowekwa, Na anayetaka malipo ya duniani tutampa hapa hapa,Na anayetaka malipo ya Akhera tutampa huko, na kwa yakini tutawalipa wanaoshukuru"
Aya imeanza kwa kuyataja Mauti, kwanini yakatajwa mauti mwanzo, ili uwe uzinduo, ili uwe muamsho wako, halafu baada ya mauti aya ikaendelea kwa mwanzo kutaja mwenye kutaka hapa duniani tunampa, sasa tujitizame nani anotaka duniani? jee na wewe umo katika chukua chako mapema(Mwenye kutaka duniani lazima dini impotee)Naam anotaka duniani tunampa hapa hapa(Hatumdhulumu)ila tunampa tahadhari japo tunakupa hapa duniani lakini kumbuka kuna Mauti, kwanini yakatajwa Mauti sababu mauti yanakuja kukunyanganya kila kitu(Unakua muflis)mauti yanachukua nyumba yako na familia yako, mauti yanachukua utajiri wako na kila kilicho chako na kukuacha mweupe hata nguo huvai tena ila unafungwa vitambaa viwili juu na chini, halafu yanakupeleka kwenye nyumba yako ambayo ni chini ya ardhi, mwanzo ulikua unakaa juu sasa unakaa chini. Sasa ikiwa mwenye kutaka dunia ili dini ikupotee bakia hapo ulipo baada ya kusoma darsa hii, ama kama unataka kutafuta dini basi fanya kazi haraka sana ili utoke kwa wenye kutaka dunia, jee unawajua wenye kutaka dunia wanakua katika hali gani? endelea part-2

MTAFUTA DINI,LAZIMA DUNIA IMPOTEE-PART-2

Asalaam Aleiykum,

Nini Dunia? ukimuuliza Mcha Mungu atakujibu Dunia ni (A state of  Unconsciousness)hali ya mvinyo, usahulivu, au ni ulevi wa kuilaza (Roho)Nikifafanua zaidi nina maana mambo yote ya kidunia ni yenye kukusahaulisha(Akhera)ambako ndiko kwenye maisha ya Dini na kusudio zima la kuumbwa kwako. Usije ukasema nini maana ya kuletwa hapa duniani basi, wala hujaambiwa usiishi, bali unachotakiwa ukumbuke uliko toka na ndiko unako rudi, sasa kama unajikaza kuwa wewe husahau uliko toka, tembelea mifano hii, halafu mwenyewe utajijua umesahau dini au unaikumbuka, jee unataka Akhera au hapa Duniani.
Yametuzonga maisha ikisha tumetawaliwa na Shetani(Ibilis)kakaa katika usingizi wetu hatuwezi kuamka hata yakipigwa (Matarumbeta)kila mmoja wetu ni kuhitaji mali, kila mtu anapigana ajenge nyumba, kila mtu anataka apate mwanamke huyu au mwanamme yule, wengine wanahitaji dhahabu, wengine wanaabudu biashara na pesa, wengine ibada zao mipira, wengine wanasujudu kwenye muziki, wengine ndio wamejitosa katika bahari ya siasa wako tayari kuzamisha wenzao lakini wao wakae juu, kuna baadhi wamekita katika dhuluma, na wengine ni wenye kuhitaji vyeo kwa hali yoyoyte ile lazima akipate, na wako wengine ni wenye kusuguliwa roho na watoto tu, halafu na wengine maisha yao yamekua baina ya kazini na kwenye TV lazima vipindi vyake visimpite, huyu hana jengine, na haya kwa uchache ndivyo yalivyo maisha yetu na kila mmoja kazongwa na(drugs)yake hawezi kuiacha hao wote nilowataja na wengine nisowataja ni wenye kuhitaji dunia, Na Mwenye-enzi-Mungu ana wakidhia mahitajio hayo (Alhamdullillah).
Anawapa magari, na anawapa majumba na kila wanacho hitaji hao wanaendesha maisha yao(Unconscious)huku wakiwa wamelala, na kuna wengine wasopata usingizi mzuri hapo tena wanatafuta mirungi, pombe, na aina zengine za (drugs)ili wapate kukoroma vizuri.
"Enhe sasa wepi wenye kutaka Akhera"" Aya ikaendelea wenye kutaka huko Akhera tutawapa huko, ikamalizikia kwa kusema na kwa yakini tutawalipa wenye kushukuru" Nani hawa wenye Kushukuru? Na kwanini wakatajwa hapa, hawa ni wale wenye kuishi maisha yao(With-Conscious)Hadhir, wako macho, hawako ndani ya usingizi, Nini tafauti na wale walolala, Huyu kagundua kwamba dini ni maisha ya kudumu, huyu Imemjia nuru ya fahamu na kuona kwamba mauti yakija yanachukua kila kitu, lakini kuna kitu mauti hakichukui nayo ni (Life)hichi nabaki nacho, sura ya Mulk aya ya 2 "ٱلَّذِى خَلَقَ ٱلۡمَوۡتَ وَٱلۡحَيَوٰةَ لِيَبۡلُوَكُمۡ أَيُّكُمۡ أَحۡسَنُ عَمَلاً۬‌ۚ وَهُوَ ٱلۡعَزِيزُ ٱلۡغَفُورُ"
"Ambaye ameumba Mauti na Uhai ili kukujaribuni(Mtihani)ni nani miungoni mwenu mwenye vitendo vizuri, na yeye ni Mwenye Nguvu na Mwenye Msamaha".
Yeye huyu kafahamu yakuwa Mauti na Uhai ni mpito katika njia ya maisha(Life)na anajua hakuna tena kifo huko anapo rejea kama ilivyotajwa katika sura ya Ad-dukhan aya ya 56,
"لَا يَذُوقُونَ فِيهَا ٱلۡمَوۡتَ إِلَّا ٱلۡمَوۡتَةَ ٱلۡأُولَىٰ‌ۖ وَوَقَٮٰهُمۡ عَذَابَ ٱلۡجَحِيمِ "
"Humo hawataonja mauti ila mauti ya mwanzo, Na atawalinda na adhabu ya Jahanamu"
Kwa hiyo baina ya Uhai na Mauti kuna (Life)Maisha, ukigundua hili ndio umegundua dini, kwa hiyo unaweza kuishi hayo maisha hapa Ulimenguni na huko Akhera uendako, tafauti yake uelewe kuwa kumbe maisha ni safari, na wewe umo safarini na katika safari hii unaruhusiwa kufanya biashara ukachagua malipo ulipwe hapa au huko unapokwenda, uchaguzi unao mwenyewe na huo uchaguzi huupati mpaka uwe (Conscious)Hadhir, ni lazima uwe macho masaa ishirini na nne, na umacho wenyewe ni hiyo (Dhikr)Kukumbuka.
Na huku kukumbuka kuna darja zake ambazo unaendelea kuzipanda kila ukizidi kukumbuka, na kila ukipanda darja unapata ufunguo wa kujua ya kwamba hili nilochagua mimi linanipeleka katika uhai wa daima, unapata kujua pale inapotokea furaha, unapata kujua pale inapotokea afya na hapo ndipo unapoipata dini na dini haina mwisho, unaanza kuwa Mcha Mungu wa kweli na kidogo kidogo Dunia inaanza kukupotea, unakuwepo duniani lakini unaishi kidini, Mali ipo lakini haikulevi wala kukusahaulisha, dhahabu zipo huna shauku nazo, zikiibiwa sawa zikiwepo sawa, maradhi yakija sawa, afya ikiwepo sawa, kila kitu unamwachia Mollah wako.Endelea-part-3

MTAFUTA DINI,DUNIA LAZIMA IMPOTEE-PART-3

Asalaam Aleiykum,

Hapo tena unajua kumbe maisha ni kitu kinachokaa ndani, si kitu chenye kutegemea matukio ya nje, vitu vya nje vyote vinakwenda na kubadilika, isipokua nafsi yangu, Na mtu ukigundua nafsi yako unakua tajiri wa maisha, Sasa vipi inatokezea kuitambua nafsi yako?. Imehimizwa katika dini suala la kukumbuka, kwanini ikahimizwa? kwa sababu kadhia ya kukumbuka ni ngumu sana, mfano ni kama huu (ukimtizama mtoto wako basi kumbuka na wewe unotizama)fanya japo kwa saa chache tu ikiwa utaweza basi wewe rahisi kukipata hicho ninacho zungumza, lakini ni vigumu sana, ndio maana ukaambiwa Tajiri vigumu kuingia peponi kwa sababu ni vigumu kukumbuka Mollah na faida kwa wakati mmoja.
Ukiweza Kuishi hivyo ina maana wewe unaishi Hadhir(Conscious)umacho, binaadamu tuko katika shughuli ya kukumbuka kitu kimoja aidha unakumbuka mali, au hukumbuki chochote, fikra zetu ziko sana katika dunia, huwezi kuwa na mali halafu ukamkumbuka Mollah wako tabu sana, huwezi kuwa na cheo ukamkumbuka Mollah wako vigumu mno, utakwenda kutisha mara moja moja misikitini lakini hupo kabisa, unafata kundi tu huku umelala, na huwezi kuwa maskini na huku ukamkumbuka Mollah wako, sababu fikra zote ukakope wapi, utakula nini, ufanye nini, itakuaje mpaka uamue au ukujie muongozo yakua sasa nataka kuitafuta dini, na uwe tayari dunia kukupotea, na kama nani anotaka dunia impotee?.
Tizama nini imekua hali zetu, mahusiano yetu yote ni matendo ya nje. hakuna hata mmoja mwenye kutaka mahusiano ya ndani na nafsi yake, tunazihusisha furaha lazima kipatikane kitu cha nje, iwepo kitchen party mtu ndio afurahi, na kuna wengine ndio wana maradhi kama hakupata kwenda barazani anaumwa, imekua baraza muhimu kuliko familia yake, anaweza mtu kupuuza kitoto chake kinaumwa lakini lazima akahudhurie barazani, furaha yake yote inategemea baraza, na wale wagonjwa wenzie kama hawajamuona na wao hawana raha, wanakuja kumuuliza vipi leo baraza haijachangamka hujaonekana, hivi ndivyo furaha zetu zilivyo, hasara ilioje, lau tungejua furaha inatokea ndani sio nje, kama vile afya inavo tokea ndani sio nje, mwenye furaha ya kweli ni yule anayefata dini, wala hana haja ya dunia, anacheka akiona watu wanavyo hangaika kujenga majumba ikisha hao wanakufa, kukimbilia vyeo ikisha vinawatokea puani, Mtafuta dini yupo anaishi Ulimwenguni lakini dunia ishampotea zamani hana haja nayo, yeye anaishi maisha tafauti kabisa sio ya wale wenye kubadilisha tabia kabla hawajapata dini, ndio utaona maonesho makubwa lakini maskini nafsi zao hazijabadilika, nje anafata maisha ya dini, lakini ndani kajaa dunia anakaribia kuanguka, kwanza badilisha nafsi yako ikisha tabia itafatia, usipite ukasema husikilizi muziki halafu kichwani kutwa unaimba, hutizami TV story zote za michezo unazijua, usibadilishe tabia kwanza badilisha nafsi, tabia zitafatia, na tabia zikifatia unakaa katika mizani unakua kati kati huyumbi tena, unajua mali zipo nje na watoto wapo nje, lakini Mollah wangu anakaa moyoni, hapo tena unakua unaishi ndani na nje na ukianza kuishi hivyo kidogo kidogo dunia itaanza kukupotea mpaka kuna siku inabaki dini pekee hapo unakua(Wake-up)umeamka umeshahama kwenye usingizi, ndio maana utaona mambo yakiwa mengi kichwani hupati usingizi na dini ikikujaa kichwani hulali tena usingizi wa kidunia. Naumomba Mollah wetu atuamshe katika giza hili totoro-Amin.

Saturday, January 19, 2013

SALA SIO KAZI WALA MAZOEA-PART-1

Asalaam Aleiykum,

Naanza kwa kueleza khofu kubwa nilokua nayo nikiona wengi katika wanaosimamisha (Sala) wamegeuza ama mazoea au kuitikadi nikuwa ni kazi ambapo mwisho wa kazi hii malipo yake ni thawabu, na hapo ndipo kitendo hicho cha kazi kinafikia kikomo(Mwisho). Yamekua mategemezi haya ya thawabu ndio yanamfanya mtu afanye biashara hii na Mwenye-enzi-Mungu wake ili asimpeleke Motoni, Maskini roho zetu pengine tunafanya hivyo hatujui dhumuni lenyewe la hiyo (Sala)au kwa kuzongwa na kuyakumbatia maisha tumesahau maana halisi ya kitendo hichi cha (Sala).
Nini Sala? Kwa tafsiri ya kawaida (Sala)ni kitendo cha khiyari chenye kupeleka maombi au kurejea na maombi hayo kwa (Muumba)kama alivotwambia kwenye kitabu chake kitakatifu sura ya Adh-Dhariyat aya ya 56 "وَمَا خَلَقۡتُ ٱلۡجِنَّ وَٱلۡإِنسَ إِلَّا لِيَعۡبُدُونِ".
"Sikuwaumba Majini na Binaadamu ila wapate kuniabudu mimi" Nadharia ya kuabudu kusudio lake ni baada ya kufahamu au kuamini kuwepo kwake na kukubali wewe umeumbwa ikisha ukajifunga kurejea kwa Mollah wako kwa mapenzi(Sio kwa woga au kulazimishwa au kutishwa)huku umejawa na shukurani zisizo kikomo(Hiyo ndio Sala). Utaona ufunguo huu wa hii Sala mwanzo kabisa imeanza na Shukurani(ٱلۡحَمۡدُ لِلَّهِ رَبِّ ٱلۡعَـٰلَمِينَ )"Nakushukuru Mollah wangu, Mollah wa viumbe vyote(Na kila kilichomo katika Ulimwengu)"tokea nilipomaliza kusali alfajiri niko na afya njema, nakushukuru Mollah wangu vitoto vyangu vyote vizima, kwa uweza wako Mollah wangu wewe Mlezi wa viumbe vyote vikubwa na vidogo mimi nimepata bahati ya kusikia ndege wanaitana kwa sauti zilo nzuri huku wakiwa na furaha, nimemkuta paka sikumpiga teke, nimemkuta maskini nimemsaidia kwa ajili ya mapenzi yako Mollah wangu,
"ٱلرَّحۡمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ ""Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa, na neema ndogo ndogo"
Namimi Mollah wangu nayakinisha hayo kwa sifa  hizo mbili zisizo upungufu yakua unatupa Rehma hizo kwa mimi nilokuja kukuabudu na hata yule anokuasi wakati huu, sote sisi upo katika kutusubiria labda tutarejea kwako unaendelea kutukirimu afya na mengi yalo mazuri yasiyo idadi. Sasa kwanini nikautaja (mfano)huu ndio uingie nao katika sala?, Sababu kubwa Sala yako isiwe ya (Tabia) isije ikawa kama (Kazi au Mazoea) wewe sio (Mti) au (Mlima) wewe Binaadamu na kila dakika mambo yako yanabadilika na unatakiwa kila ukenda kwa Mollah wako unakwenda na mambo mepya ya kuzungumza na Mollah wako kama alivosema Mwenyewe katika sura ya Arrahman aya ya 29,
" يَسۡـَٔلُهُ ۥ مَن فِى ٱلسَّمَـٰوَٲتِ وَٱلۡأَرۡضِ‌ۚ كُلَّ يَوۡمٍ هُوَ فِى شَأۡنٍ۬ "
"Vinamuomba yeye kila(Kitu)vilivyomo mbinguni na ardhini, kila siku(Mollah)Yeye yumo katika mambo(Mengine mapya)". Sasa leo iweje wewe Sala yako ibakie vile vile, ndio maana inafika wakati mpaka unaona Sala yenyewe inakupa udhia, unafika kusema eti wacha nisali kabisa nikikaa nipumzike, Alaa Sala leo imefikia kuwa kero? kwanini sala yako siku zote iwe vile vile wakati sala yenyewe ni maombi katika maisha yako, na maisha ni safari, sasa ikiwa unasema unasafiri halafu uko hapo hapo hiyo itakua safari?.
Sasa kwanini nikayasema hayo? Soma kwa uzuri usije ukaona huyo sasa anabadilisha Sala, laa sifanyi hivyo ninacho badilisha ni fikra zako unazokwenda nazo katika hiyo Sala, najaribu kukupa muelekeo ili ukiwepo katika hiyo Sala usizame kwenye biashara au siasa au mambo ya kipuuzi ya kidunia ikawa mpaka Sala inakwisha ndio unaamka kwenye (Tahiyyatu) Sasa ufanye nini? Endelea Part 2 upate nini cha kufanya pia ugundue nini siri ya Udhu.

SALA SIO KAZI WALA MAZOEA-PART-2

Asalaam Aleiykum,

Sasa kamatana na mimi mkono kwa mkono twende kwa daktari wa Akili zetu halafu tukifika tujiulize nini kinatokea wakati tumesimama tuna Sali, ukitaka usitake kuna mambo matatu yanatokea, Jambo la kwanza unasoma sura ndani ya Quraan kwa njia ya (Automatic)(1)halafu Akili iko kwengine kabisa, pengine unafikiri nitakula nini, au kama unakwenda harusini ndio manyago matupu, au mpira umeanza unasikia watu wanashangiria itizame sala yako inakuaje(2)na la Tatu ambalo hilo ndio linalotakiwa litende hicho kitendo chenyewe cha Sala ni pale unaporejea kwa ghafla ukajisuta mwenyewe kuwa ulikua umesafiri, kuna kitu kinakukumbusha ewe mja we, wewe unasali, upo mbele ya Mollah wako wewe, hapo unarejea na inakutoka (Allahu-Akbar)kubwa ikisha huyo (Una-Rukuu)hapo unaporejea huyo ndio wewe na huyo ndio hili jambo la (3)ambalo unatakiwa uwepo kwenye Sala nzima katika hiyo namba(3)lakini hukai hata sekunde (10)mara huyo ushakimbilia kwengine.
Inapatika hali hii ya fungu la tatu(Mfano)pale Sheikh anaposoma ukalia, au ukicheka au ukirejea mwenyewe katika hizo sekunde chache, ninacho himiza hapa basi ikiwa wewe ndio mbovu wa mawazo hayo, basi tafuta mawazo yenye kheri na dua zilizo nzuri, ili kila ukenda kwa Mollah wako uwe umejitahidi mpaka pale utakapofika kutekeleza Sala kwa ukamilifu isiyo na mawazo wala mahitaji, pale ambapo Mtume s.a.w alipomrejesha yule kijana asali tena mara tatu, pahala pale ambapo Nabii Isa a.s. alipoulizwa na wanafunzi wake vipi unasali alianguka moja kwa moja na kusujudu.
Sala ni mapenzi makubwa juu ya Mollah wako, uwe tayari kuvikosa vyote iwe mali yako au watoto wako au mkeo, uvikusanye vyote kwenye gunia uwe tayari kuvitosa baharini kwa ajili ya Mollah wako, uwe unajua hivi vyote wewe ndie muumba wake namie niko tayari kuvikosa au vinikose kwa ajili yako Mollah wangu. Kumbuka kisa cha Nabii Ibrahim a.s sura ya As-Saffat-102-112"Alipoota kumchinja mwanawe hakusita kwa mapenzi ya Mollah wake mpaka ilipoletwa fidia ya mnyama ili atoe sadaka"Muumin ndio unatakiwa uwe katika hali kama hiyo kwa ajili ya Mollah wako, wewe hujaambiwa kuchinja ila unatakiwa uende kwenye hiyo sala japo kidogo umejawa na mapenzi, japo kidogo kila kipindi cha sala uwe na hamu ya kukutana na kuzungumza na Mollah wako, uwe na shauku ya kumhadithia yalo kukera na kukufurahisha na yupi alokukosea umemsamehe kwani na wewe kila kipindi cha hiyo sala unasamehewa kutokana na mapenzi ya Mollah juu yako, vipi unasamehewa? pata maana ya udhu kwa undani ili sasa ukenda kutia udhu uwe muangalifu, uache maneno ya kipuuzi, uwache habari zote za kidunia.
Nini Udhu?
Udhu una (Symbol)alama mbili kwako Binaadamu, kama ilivyo nguo, ukivaa ya kike na ya kiume unavo tafautisha tabia zako, au Nurse akivaa nguo za kawaida na akivaa (uniform) yake anavobadilika na shindano lake mkononi, au Mwanajeshi akiwa na nguo za kawaida au za kazini tabia inabadilika kabisa. Sasa ikiwa nguo zinakwenda (Deep) na kumbadilisha mtu tabia, nini habari yetu sisi kuhusiana na (Udhu)Alama hii ya udhu inaashiria mambo mawili, yepi endelea-part-3

SALA SIO KAZI WALA MAZOEA-PART-3

Asalaam Aleiykum,

Mambo yenyewe la kwanza ni ile (Tohara)inayopatikana kutokana na usafi wa viungo kama ilivo taja aya ya sita ya surat Maidah halafu kuna la pili lake karibu na mwisho wa hiyo aya ambalo ulikua hulijui limo katika (Udhu)"  مَا يُرِيدُ ٱللَّهُ لِيَجۡعَلَ عَلَيۡڪُم مِّنۡ حَرَجٍ۬ وَلَـٰكِن يُرِيدُ لِيُطَهِّرَكُمۡ وَلِيُتِمَّ نِعۡمَتَهُ ۥ عَلَيۡكُمۡ لَعَلَّڪُمۡ تَشۡكُرُونَ
"Mollah wenu hataki kukutieni kwenye taabu, bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu,ili mpate kushukuru"
Ipi neema hiyo, ni ile neema ya kusamehewa kila ukitia udhu wakati unaenda kusali kabla hata ya kuanza huko kusali basi Mollah wako kwa Rehma zake anakufutia madhanbi kwa udhu huo, lakini Udhu wenyewe lazima utimie wende kwa adabu na unyenyekevu, ukikosha viganja vyako na mikono(labda)kuna vijidhanbi vya mkono umevifanya katika wakati ule tambua unavifuta, Ukikosha uso labda kuna dhanbi za macho unafutiwa, ukitia maji mdomoni kusukutuwa labda kuna uongo au jambo umesema la dhanbi unafutiwa,ukitia maji masikioni pengine umesikiliza mambo maovu unafutiwa dhanbi zake,  ukitia maji kichwani labda ulikua na mawazo mabaya unafutiwa dhanbi zake, ukitia maji miguuni pengine ulikwenda pahala penye maovu kwa hiyo unafutiwa hiyo dhanbi, hii ndio Neema ya Mollah juu yako.Usije ukashtuka hee mbona huyu anasema hivi(Kwanza katafute asili ya neno Tawba)toba utalikuta maana ya asili yake kurejea na wewe unarejea kwa siku mara tano huo ndio Udhu nje Tohara ndani maghfira)na aya inamalizikia ili mpate kushukuru ndipo unaingia katika Sala mwanzo unaanza," ٱلۡحَمۡدُ لِلَّهِ رَبِّ ٱلۡعَـٰلَمِينَ".
Hapo ndipo Bwana Mtume s.a.w alipomuuliza Bilal "Ewe Bilal r.a mimi nasikia nyayo zako peponi una matendo gani unafanya hata ukapata hayo" akajibu Sayyidna Bilal r.a haunitoki Udhu sala mpaka sala.
Sasa ikiwa Udhu unatia kila mara iweje Sala yako kila wakati ni vile vile, itizame sana sala yako isije kuwa mazoea au tabia, ifanye kila wakati kama unavotia Udhu na sala yako vile vile iwe nyengine, kumbuka wakati unabadilika basi na wewe fanya sala yako ibadilike, kama ulikwenda na maombi ya dhiki basi wakati mwengine pia nenda na salamu za shukurani. Usije ukawa kama wale walotajwa katika sura ya (Maun) aya ya 4"فَوَيۡلٌ۬ لِّلۡمُصَلِّينَ"
"Wataona wale wenye kusali(Sala za kinafik)unakwenda tu kupachika sala ikisha huyo unatoka mbio,(5)"ٱلَّذِينَ هُمۡ عَن صَلَاتِہِمۡ سَاهُونَ""Ambao wanapuuza sala zao"(Maamrisho yake).(6)
"ٱلَّذِينَ هُمۡ يُرَآءُونَ""Ambao hufanya(Sala na Amali)zao kwa riyaa(ili kuwaonesha watu namie nasali)(7)"وَيَمۡنَعُونَ ٱلۡمَاعُونَ"Na hunyima misaada"(haitakua na faida sala hiyo) ikiwa maamrisho ya Mwenye enzi Mungu huyatekelezi na huku unataraji kurejea kwa Mollah wako, hata ukirejea ni bure, hata huo Udhu hupati kitu kwa sababu inayosamehewa ni Roho si mwili na ikiwa Roho yako ngumu basi jijue na huko kwa Mollah wako hupati kitu, Sala ikipatikana sawa sawa kwako inakua furaha, sala ikipatikana mazito yanakua mepesi, sala ikipatikana mpaka mwenyewe unajua Mollah ana mapenzi na mimi, sala ikipatikana mpaka khofu ya kufa inaondoka na khofu hiyo ikiondoka kwa mara ya mwanzo ndio unaanza kuishi, huogopi tena kufilisika, huogopi tena umaskini, huogopi tena maradhi ukiwa katika hali hiyo jua sala zako zinafika-Mollah atujaalie kabla ya umauti wetu tupate daraja hiyo sisi na familia zetu.Amin

Saturday, January 12, 2013

MADHARA YA DHULUMA-PART-1

Asalaam Aleiykum,

Anasema Mwenye enzi Mungu "Enyi viumbe mimi nimejiharamishia kudhulumu, Ikisha nikajaalia baina yenu haramu kudhulumiana", Msifanye kabisa vitendo vya kudhulumiana. Na huku kudhulumiana kuko kwa aina nyingi na mbolea yake kubwa ya Mti huu wa dhuluma ni Uongo na Mateso, Waweza kumdhulumu mtu kwa kumdanganya na kuchukua Mali yake, waweza bure ukamsingizia mambo ya uongo au ukampiga ukachukua kilicho chake, Na pia unaweza kuleta visingizio vya ajabu na sababu zisizohusu ukamtia Gerezani pengine kulinda maslahi yako na hilo ni dhanbi kubwa katika dini hii ya Kiislam.
Nini anasema Bwana Mtume s.a.w katika Hadith iliyosimuliwa na (Muslim na Tirmidhy)kutoka kwa Abu Huraira r.a"Kasema Bwana Mtume s.a.w Jee mnamjua Muflis(Yule alofilisika)?""Wakajibu Masahaba muflis ni yule ambaye hana (Dirham-Pesa)wala starehe yoyote ile, Akasema Bwana Mtume s.a.w "Alofilisika katika umati wangu ni yule atakae kuja siku ya Kiyama na Sala zake, na Zaka zake na Funga yake na pia Hijja yake, Ikisha na huku anakuja kachukua Mali ya huyu, Kamshtumu (Kumsingizia)huyu, Kampiga huyu, Kamwaga Damu ya huyu, Basi yatachukuliwa yale Mema yake wapewe wale alowadhulumu na ikisha kama hayajatosha basi atapewa maovu ya wale walotenda alowadhulumu halafu achukuliwe huyo kupelekwa Motoni".
Hizo ndio hali zetu Waislam wa leo hao ndio alowataja Bwana Mtume s.a.w, Leo tunakua Mbele kusheherekea Dhuluma na huku tukiendelea kudhulumu na Ibilis anatwambia hapana neno mko wengi kila mtu ana sheherekea kwanini na wewe upitwe jiunge na kundi, na kitu kikifanywa na wengi wasiwasi unaondoka kabisa imekua sasa dhuluma kitu cha kawaida. Na sasa tumefikia Waislamu wenyewe kwa wenyewe tunaadhibiana eti kwa kuwaridhisha watu fulani kwamba sisi tuna uwezo hata wakukamata Waislam wenzetu na kuwaweka Gerezani(Jela) Na hakuna jambo zito katika dini hii kama mwenzio uliyekua unasali naye ukamsingizia uongo au ukamdhulumu kwa kumuweka Gerezani(Mahabusu)Tambua haipatikani nusura kwako wala usamehevu ikiwa kwa mbinu au mipango umempeleka Muislamu mwenzio ndani hususan ukijua hana kosa.
Sasa kwanini Ikawa hivyo? Tunaingia katika maudhui ya Dhuluma safiri na mimi ili upate kujua dhuluma ilivo na athari zake halafu ufanye bidii kuiepuka, Kwanza kabisa katika Uislam hakuna (Jela au Mahabusu) Nitataja sababu zake na hukumu mbili ili na wewe upate kutumia Akili yako kama unakubaliana nazo au unapinga.
Hukumu ya Jela Mwenye-enzi-Mungu kawatengea wanaadamu huko Akhera kama ilivosema Quraan sura ya (Mulk aya ya 7-8)
"إِذَآ أُلۡقُواْ فِيہَا سَمِعُواْ لَهَا شَہِيقً۬ا وَهِىَ تَفُورُ"
"تَكَادُ تَمَيَّزُ مِنَ ٱلۡغَيۡظِ‌ۖ كُلَّمَآ أُلۡقِىَ فِيہَا فَوۡجٌ۬ سَأَلَهُمۡ خَزَنَتُہَآ أَلَمۡ يَأۡتِكُمۡ نَذِيرٌ۬ "
"Watakapotupwa humo watasikia(sauti)ya Ngurumo(Kishindo cha Moto)lake na hali yakuwa unafoka(Mfano wa Volcano)".
"Unakaribia kupasuka kwa hasira(Kwa ajili ya wafungwa wanotumbukizwa humo)kila mara linapotupwa kundi, walinzi wake watawauliza jee hajakufikieni Muonyaji".
Naam hiyo ndio Jela Mollah kaiweka siku ya malipo hapa Ulimwenguni katupa adhabu za kufanya lakini tusifungane(Jela)ambazo nitazitaja kwa uchambuzi huko mbele, sasa kwanini tusipelekane (Jela) hapa duniani? Hakuna Shari kubwa ya Roho kama ukiinyima Uhuru wake, na kama unataka kuyajua hayo-Endelea Part-2

MADHARA YA DHULUMA-PART-2

Asalaam Aleiykum,

Ukachukua Roho ya mwenzio na kuifunga pahala pamoja ikawa haina Uhuru, hilo ni Dhuluma kubwa kwa Binaadamu mwenzio ndio maana utaona Nabii Yunus a.s alipowekwa ndani ya tumbo la chewa kwa siku tatu tu akawa anaomba usiku na mchana anusuriwe
"وَذَا ٱلنُّونِ إِذ ذَّهَبَ مُغَـٰضِبً۬ا فَظَنَّ أَن لَّن نَّقۡدِرَ عَلَيۡهِ فَنَادَىٰ فِى ٱلظُّلُمَـٰتِ أَن لَّآ إِلَـٰهَ إِلَّآ أَنتَ سُبۡحَـٰنَكَ إِنِّى ڪُنتُ مِنَ ٱلظَّـٰلِمِينَ "
"Na Dha-Nun(Yunus)(Mtaje)alipoondoka huku amechukia, na akadhani ya kwamba hatutamdhikisha, basi (uzito wa Roho ulipomzonga)aliita katika giza(ndani ya tumbo la chewa)(Akasema)Hakuna aabudiwaye isipokua wewe, (uliye) mtakatifu, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu".
Sasa huyo ni nabii kakaa siku tatu tu na inatajwa hali hiyo ni ya (Kumdhikisha)akakiri mwenyewe kadhulumu kwa hiyo anaomba atolewe nini hali yetu sisi tunowekana ndani bila ya kuwa na uyakini kama kweli hao tunao waweka ndani wana hatia au wamesingiziwa tu, Mambo ya kuwekana ndani ni dhuluma kubwa watahadhari wale wenye kufurahikia wenziwao wanoteseka hapa Ulimwenguni basi wajiandae wao kuteseka huko Akhera, mambo ya ndani ni magumu ndio maana hata mtoto akifika miezi 9 hakai tena tumboni  anapiga mateke ili apate kutoka.
Sasa kwanini dini ya kiislam haikuweka (Jela)kisome kitabu cha haki na Umsikilize nini anasema Hakim wa siku ya Mwisho adhabu gani peaneni hapa Ulimwenguni ili matatizo yote yaondoke, kwani huko kuwekana (Jela)Takwimu zinasema wezi wanaendelea kuwa wezi wakitoka, majambazi wanaendelea na kazi zao zile zile hakuna mafunzo yoyote yanayo wageuza wakitoka humo ndani, sasa nini habari yetu sisi wale walotiwa ndani bure tunajenga au tunabomoa kabisa, isome kwa ufanisi Hukumu ya Mwenye-enzi-Mungu, ambazo baadhi ya watu wanazitilia mashaka na kuzishtumu katika dini hii:Anasema Mwenye enzi Mungu katika Quraan sura ya Maidah aya ya (38).
"وَٱلسَّارِقُ وَٱلسَّارِقَةُ فَٱقۡطَعُوٓاْ أَيۡدِيَهُمَا جَزَآءَۢ بِمَا كَسَبَا نَكَـٰلاً۬ مِّنَ ٱللَّهِ‌ۗ وَٱللَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ۬"
"Mwizi mwanamme na Mwizi mwanamke, Ikateni mikono yao, malipo ya yale waliyoyachuma, ndio adhabu itokayo kwa Mwenye enzi Mungu na Mwenye enzi Mungu ni Mwenye nguvu na Mwenye Hekima"
Sasa kwanini ikabidi akatwe kiganja chake? hapa pana hekima gani? pata maalumati haya ujuwe kwanini Mollah wako akatoa adhabu hiyo, Wallahi hakuna (Profession)kazi yenye kulaza na kuwa na Raha na iliyo rahisi na utamu kama wizi, Ndio maana utaona mwizi hawachi kazi yake, midamu kiko cha kuiba iwe serekalini au dukani au kwenye nyumba basi hawachi abadan.
Sababu ya wizi unaingia (Deep)kwenye Roho ya mwanaadamu na hakuna kiingiacho (Deep)ndani ya Roho ila kinakwenda kukulaza sasa kuamshwa kwa Roho lazima kipatikane ama machungu au mshituko au muamko(Awaken)ili apate kuzinduka, na vipi atazinduka basi akatwe kiganja chake na ili wengine wapate hiyo (Awaken)muamko, ukiona mwenzio hana kiganja hata ukitaka kuiba utafikiri mara mbili uchukue au uache, hiyo ndio hekima ya Mwenye-enzi-Mungu. Na pia tambua kulala kuko kwa aina mbili aina ya kwanza ni kulala kwa (Body)mwili na kulala kwa aina ya pili ni kulala kwa Roho ndio maana ukitaka kumumsha alo lala unamtingisha amka amka, sasa ukikatwa kiganja ndio unaamka moja kwa moja hulali tena kwa maana (utaogopa kuiba).
Na Wazinifu pia Roho haziamki mpaka apigwe mijeledi mia, na mpigaji lazima apatikane Baba kubwa la miraba sita litumie nguvu zote ili kuiamsha Roho, na watakao shuhudia hukumu hiyo kila mtu akili yake itakaa sawa, atajua nikikamatwa nimeumia, Hiyo ndio hukumu ya aliyetuumba. Sasa wanaadamu wakikataa hukumu hii nini kinafatia, Wanamchukua mzinifu wanampamba kwa mashada ya maua na cheo na sifa nyingi pamoja na mazawadi, halafu maskini wanamchukua mwizi wanamdhulumu Roho yake, Mwenye enzi Mungu kasema mkateni mkono nyie mnaua na kila anoshiriki kumpiga mwizi akasababisha kifo chake basi ajijue kadhulumu na yeye atahukumiwa kwa kosa hilo. 
Sasa kuna wengine watasema hee mbona adhabu yenyewe kali hakuna ya Tahfif, nyepesi kidogo ya kuweza kuwacha huu wizi, mbona hukumu kali mno, basi kulala huku hakuna njia nyengine ya kuamshwa ndio lazima upigwe mikwaju na ukatwe mkono?
Naam ukitaka kujua njia nyengine-Endelea-part-3

MADHARA YA DHULUMA-PART-3

Asalaam Aleiykum,

Ipo njia nyengine lakini wewe upo tayari kuamka kwa njia nyengine, basi kama uko tayari kisome kisa cha Mcha Mungu Bolkiyah aliyemuachisha mwizi kuiba, ilikuaje?. Siku moja katika mji wa Asia mtoto wa Mtawala alikua anaumwa, alimaliza dawa zote Mfalme yule lakini hakupata matibabu ya mwanawe, Mmoja katika washauri wake akashauri wamfate Mcha Mungu Bolkiyah aliyekua anaishi kwenye pango msituni, wakatumwa watu wende kumleta bwana huyo, alipofika Mtawala akamwambia nimepewa habari ya kuwa wewe uko karibu na Mungu, naomba uniombee ili mwanangu apate kupoa, Bolkiyah akasema nitakuombea kwa Mungu lakini shuruti langu ni moja tu sitaki kushukuriwa, Mtawala akasema kwa hilo umepata, Bolkiyah akamuombea yule mtoto kabla hata hajaondoka kitoto kikaanza kurukaruka, alipotaka kuondoka Mfalme akamwambia umesema hutaki kushukuriwa na pia najua hutaki chochote katika mali wala chenye thamani , basi naomba mimi uniridhie nikupe bakuli la kuombea chakula. Bolkiyah akakubali akafungiwa lile bakuli alipotoka nje kulifungua akakuta bakuli la dhahabu na nje wezi wakamuona Bolkiyah ana bakuli la dhahabu mwizi mmoja akawa anamfata nyuma ili apate kuliiba, Bolkiyah alipofika msituni akaingia pangoni mwake ikisha akalirusha lile bakuli nje, mwizi akashangaa sana akaokota lile bakuli na kuingia pangoni akamwambia "Ewe"Bolkiyah mbona leo umenishangaza mie nilikua nasubiri upitiwe na usingizi ndio niingie niibe lakini leo umeniistaajabisha umenirushia nje ili nisipate hata shida ya kukusubiri, inaonesha umekinai huna haja na chochote cha Ulimwengu huu, basi nakuomba nifundishe na mimi niondoke katika hali hii ya kudhulumu mali za watu, niwache mimi hii tabia ya wizi, Bolkiyah akamwambia nitakufundisha lakini itabidi uendelee kushangaa , nitazidi kukushangaza akamwambia nifundishe sasa sishangai tena.
Bolkiyah akamwambia kuanzia leo nenda kaendelee kuiba kwa muda wa mwezi mmoja, lakini kila ukitaka kuiba fanya jambo moja, kumbuka sasa naiba, Yule mwizi akaondoka baada ya siku kumi karudi kwa Bolkiyah machozi yanamtoka anamwambia umenifanyia (Trick)gani sasa siwezi kuiba tena(Nishaamka)kila nikitaka kuiba nakumbuka, na kila nikikumbuka ina nijia fikira yakua nadhulumu, na ikija fikira hiyo nakua siwezi tena dhuluma ya wizi, basi kuanzia hapo yule mwizi akawa mwanafunzi wa Bolkiyah na akawa Mcha Mungu na mji mzima ukapata habari na kushangaa kwa ghafla jambazi lile kubadilika, hiyo ndio njia alotumia Bolkiyah kumuamsha huyo mwizi, sasa kama na wewe itakufaa itumie kabla hujadhulumu au kwenda (Jela kwa sheria za siku hizi).
Na huo uzinifu vilevile unaweza kuamka, kwa kuwa  sasa hivi umelala na umebadilisha mwenendo mwanzo matamanio yalikua (Nature)lakini umeyabadilisha kuyapeleka Akilini sio (nature) yamezama kwenye (Mind)unafikiri wakati wote ukipewa salamu aleiykum unatafsiri anataka, ukikosa mwanaadamu unakimbilia magazetini, ukikosa kwenye magazeti mbio kwenye video, sasa nini ufanye amka na wacha (Nature)ifanye kazi tena, utaona umerejea kuwa binaadamu mwenye akili timamu na afya iliyo nzuri, kila yakikujia mawazo machafu kuwa (Alert)matamanio hayo, ukiwa unayagundua pale yanapokuja au ukazuia pumzi ghafla utaona yanapotea, au pitia maudhui zilizopita ili upate dawa ya kadhia hii.
Nini Dhuluma?Endelea-part-4

MADHARA YA DHULUMA-PART-4

Asalaam Aleiykum,

Nini Dhuluma? Dhuluma ni Dhanbi ya ziada, dhanbi lazima apatikane wapili wake ndio iwe dhanbi, lakini kama utajiua(Kutoa Roho yako) haitwi dhanbi inaitwa kajidhulumu, Kwa hiyo elewa ukidhulumu unakuwa umetenda mambo mawili yaani dhanbi na dhuluma, dhanbi ina mahusiano na (Body)mwili na dhuluma ina mahusiano na (Soul)Roho, Ama kuhusiana na dhanbi Mollah wako anasema "atasamehe yale ulomfanyia yeye lakini yale ulowafanyia watu ni lazima mpaka wakusamehe wenyewe""Atakuja mtu siku hiyo aseme Mollah wangu nihukumie huyu alinidhulumu duniani"Mollah atawaambia Malaika chukueni mema yote mumlipe alodhulumiwa ikisha mtieni peponi huyu alodhulumiwa"Ama huyu alo dhulumu makaazi yake moja kwa moja motoni.
"Enyi Madaktari(Doctor)na nyie Manesi(Nurse) nyie Makachero(Polisi)na Nyie Wake kwa Waume, wenye kuwadanganya wenzio jueni hiyo ni dhuluma kubwa, Mna wadanganya wagonjwa, na kuwatesa Raia, mna danganya mpaka nyumbani wake zenu na waume zenu zote hizo ni dhuluma na mtaulizwa siku ya (Kiyama)kwa matendo hayo.(Mfano)Daktari  anakuja mwanamke kamleta mumewe mgonjwa anaumwa anataka matibabu pengine maradhi yake dawa elfu 15 unamwambia laki mbili na wao hawana uwezo huo, inabidi atoke yule mwanamke maskini aende kukopa kwa (Kibosile)huko hapewi mkopo mpaka azini, akisha kuzini anapata mimba, akipata mimba inabidi aitoe, au isiwe hivyo, mume anashindwa kupata matibabu huyo anarudi nyumbani na kukata Roho, anawacha vitoto vidogo yatima jueni (Doctor na Nurse)nyote mmo mwanzo mpaka itakapoishia, na mmedhulumu na mtaulizwa siku ya siku au mtaanza kulipwa hapa hapa duniani.
Na kama (Kachero)Polisi umetumwa kwenda kumpiga mtu ukamvunja miguu au kumuua basi mwanzo wa dhiki ya familia ile mpaka mwisho wake wewe unaendelea kuandikiwa dhanbi ya dhuluma mpaka dhiki ile iwaondoke, Na wewe Mume na mke mnopita mkadanganyana jueni pia mnadhulumiana dhuluma ilo kubwa, nyinyi mpewa amana ya maisha yenu, inakuaje leo huyo apite kule na yule apite huku eti kutafuta riziki, eti anafanya biashara hakuna chochote isipokua dhuluma na unaandikiwa dhuluma hiyo labda mpaka mtakapo achana, leo inafikia mtu anazaa vitoto, unaulizwa pesa ya kula unajibu huna ikisha huyo unatoka kwenda kutumia na kimada, atahadhari sana mtu na dhuluma hizi adhabu zake nyinyi hamziwezi, na wameumia wale wenye kuuzaa madawa ya kulevya wao pamoja na familia zao, kwani yule unayemuonjesha unga tokea siku ile alipokuwa mteja mpaka anaingia kaburini dhanbi zake zote unaandikiwa wewe umemdhulumu. 
Sasa kama umezinduka kidogo rejea kwa (Boss)Mkubwa wako wa kazi kamwambie leo nimeoneshwa aya ya Quraan imeniamsha sitaki tena kudhulumu nishachoka naomba maghfira kwa Mollah wangu, mwambie nimesoma mimi sura ya Ibrahim aya ya 42-49-50 inasema:" 
"وَلَا تَحۡسَبَنَّ ٱللَّهَ غَـٰفِلاً عَمَّا يَعۡمَلُ ٱلظَّـٰلِمُونَ‌ۚ إِنَّمَا يُؤَخِّرُهُمۡ لِيَوۡمٍ۬ تَشۡخَصُ فِيهِ ٱلۡأَبۡصَـٰرُ"
"Wala msidhani Mwenye enzi Mungu ameghafilika na (haya)wanayofanya Madhalimu, Hakika amewakhairishia tu mpaka siku ambayo macho yatatoka(Kwa khofu)"
" وَتَرَى ٱلۡمُجۡرِمِينَ يَوۡمَٮِٕذٍ۬ مُّقَرَّنِينَ فِى ٱلۡأَصۡفَادِ"
"Na utawaona wakosa siku hiyo wamefungwa katika minyororo"
"سَرَابِيلُهُم مِّن قَطِرَانٍ۬ وَتَغۡشَىٰ وُجُوهَهُمُ ٱلنَّارُ"
Nguo zao (siku)hiyo zitakua za lami na Moto utazijia nyuso zao(Kuziunguza).
Hayo ni baadhi ya mambo yatakayo wapata wenye kufanya dhuluma ya aina yoyote ile, siku hiyo ya kiyama, na ukitaka kujua duniani kinawafika nini-Endelea-part-5


MADHARA YA DHULUMA PART-5

Asalaam Aleiykum,

Nini kinawifika hapa Ulimwenguni wale walo zama katika dhuluma, wenyewe hawajioni lakini wakitizama kwa makini wanaweza kugundua mambo mengi yanayo wafika katika nafsi zao mpaka familia zao na kama aya ilivosema wanapururiwa, lakini mifano ni mingi madhara yanopatikana ni makubwa, kwa sababu sheria ya Ulimwengu huu chochote unachotenda kiwe kibaya au cha kheri basi kuwa na hakika utalipwa hapa duniani na huko akhera uendako, ukidhulumu wewe basi ujue chaweza kulipa kizazi chako midamu kama wameshiriki katika dhuluma hiyo Mollah lazima apitishe hukumu yake na mfano wa kwanza utaupata katika sura ya Kahf aya ya 79-82.
(79)"Ama ile jahazi, ilikua ya maskini wanofanya kazi zao baharini, na nilitaka kuharibu, kwani mbele kulikuwa na Mfalme(anayedhulumu)anakamata kila jahazi(nzuri)kwa jeuri."
(80)"Ama yule kijana, wazazi wake walikuwa Waislam kamili, tukahofia kwamba asije akawapeleka(Wazee wake)katika uasi na ukafiri.
(81)"Basi tulitaka Mollah wao awabadilishie mtoto aliye bora kuliko yeye kwa kutakasika, na aliye karibu zaidi kwa huruma".
(82)Na ama ukuta, ulikuwa wa watoto wawili mayatima katika mji ule, na chini yake kulikuwa na hazina yao, na baba yao alikuwa(Mja) mwema, kwa hivyo Mollah wako alitaka wafikie baleghe yao wajitolee khazina yao, Hiyo ni Rehma inayotoka kwa Mollah wako, nami sikuyafanya haya kwa amri yangu, hayo ndio katika yale ambayo hukuweza kuyavumilia.
Ukisoma kwa makini utaona vipi Madhara utakayoyapata kama wewe utakua mtu wa dhuluma, Ama kuhusu hii safari alokwenda yule msemezwa na Mwenye-enzi Mungu Nabii Musa a.s na yule alopewa ilmu Nabii Hidhr a.s, Ilikua lengo lake kuonesha vipi dhuluma ilivokua mbaya na vipi Mollah wako anavo ikinga kwa wanyonge na anavoangamiza wabaya, Na vipi ukiwa mtu mwema malipo yake yanavoendelea hata ukiondoka katika Ulimwengu huu Mollah anahifadhi mpaka familia yako. Ili kutoonesha sisi vipi dhuluma ilivyo mbaya na madhara yake, Mtawala anadhulumu Raia wake basi bora Jahazi izamishwe, Mtoto atawadhulumu wazee wake kwa kuwatia kwenye maasi basi bora afe, atakuja mtoto mwengine,Na wale watoto mayatima wawili kwa kuwa baba yao alikua mtu mwema tu, basi umejengwa ukuta ili wasije kudhulumiwa hazina yao, Kwa hiyo hata kulinda kipande chako cha ardhi usidhulumiwe ni haki yako, na umehalalishiwa simama katika haki hiyo kama walivyo simama walio wema kupigania haki. Sasa nawaombea dua wale walokuwemo katika dhiki Mollah awaondoshee na awape subira kama alivompa Nabii Yusuf a.s, Na wale walopata madhara ya maradhi au majeraha basi Mollah awape shifaa na subira ya Nabii Ayub a.s, Mollah tujaalie ulowapa Uweza juu yetu sisi basi watie huruma na Imani watutendee haki katika matakwa yetu ya kidunia, na wakishindwa basi sisi tunarejea kwako kwa muongozo wenye kheri.Amin.