Asalaam Aleiykum,
Naanza kwa kueleza khofu kubwa nilokua nayo nikiona wengi katika wanaosimamisha (Sala) wamegeuza ama mazoea au kuitikadi nikuwa ni kazi ambapo mwisho wa kazi hii malipo yake ni thawabu, na hapo ndipo kitendo hicho cha kazi kinafikia kikomo(Mwisho). Yamekua mategemezi haya ya thawabu ndio yanamfanya mtu afanye biashara hii na Mwenye-enzi-Mungu wake ili asimpeleke Motoni, Maskini roho zetu pengine tunafanya hivyo hatujui dhumuni lenyewe la hiyo (Sala)au kwa kuzongwa na kuyakumbatia maisha tumesahau maana halisi ya kitendo hichi cha (Sala).
Nini Sala? Kwa tafsiri ya kawaida (Sala)ni kitendo cha khiyari chenye kupeleka maombi au kurejea na maombi hayo kwa (Muumba)kama alivotwambia kwenye kitabu chake kitakatifu sura ya Adh-Dhariyat aya ya 56 "وَمَا خَلَقۡتُ ٱلۡجِنَّ وَٱلۡإِنسَ إِلَّا لِيَعۡبُدُونِ".
"Sikuwaumba Majini na Binaadamu ila wapate kuniabudu mimi" Nadharia ya kuabudu kusudio lake ni baada ya kufahamu au kuamini kuwepo kwake na kukubali wewe umeumbwa ikisha ukajifunga kurejea kwa Mollah wako kwa mapenzi(Sio kwa woga au kulazimishwa au kutishwa)huku umejawa na shukurani zisizo kikomo(Hiyo ndio Sala). Utaona ufunguo huu wa hii Sala mwanzo kabisa imeanza na Shukurani(ٱلۡحَمۡدُ لِلَّهِ رَبِّ ٱلۡعَـٰلَمِينَ )"Nakushukuru Mollah wangu, Mollah wa viumbe vyote(Na kila kilichomo katika Ulimwengu)"tokea nilipomaliza kusali alfajiri niko na afya njema, nakushukuru Mollah wangu vitoto vyangu vyote vizima, kwa uweza wako Mollah wangu wewe Mlezi wa viumbe vyote vikubwa na vidogo mimi nimepata bahati ya kusikia ndege wanaitana kwa sauti zilo nzuri huku wakiwa na furaha, nimemkuta paka sikumpiga teke, nimemkuta maskini nimemsaidia kwa ajili ya mapenzi yako Mollah wangu,
"ٱلرَّحۡمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ ""Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa, na neema ndogo ndogo"
Namimi Mollah wangu nayakinisha hayo kwa sifa hizo mbili zisizo upungufu yakua unatupa Rehma hizo kwa mimi nilokuja kukuabudu na hata yule anokuasi wakati huu, sote sisi upo katika kutusubiria labda tutarejea kwako unaendelea kutukirimu afya na mengi yalo mazuri yasiyo idadi. Sasa kwanini nikautaja (mfano)huu ndio uingie nao katika sala?, Sababu kubwa Sala yako isiwe ya (Tabia) isije ikawa kama (Kazi au Mazoea) wewe sio (Mti) au (Mlima) wewe Binaadamu na kila dakika mambo yako yanabadilika na unatakiwa kila ukenda kwa Mollah wako unakwenda na mambo mepya ya kuzungumza na Mollah wako kama alivosema Mwenyewe katika sura ya Arrahman aya ya 29,
" يَسۡـَٔلُهُ ۥ مَن فِى ٱلسَّمَـٰوَٲتِ وَٱلۡأَرۡضِۚ كُلَّ يَوۡمٍ هُوَ فِى شَأۡنٍ۬ "
"Vinamuomba yeye kila(Kitu)vilivyomo mbinguni na ardhini, kila siku(Mollah)Yeye yumo katika mambo(Mengine mapya)". Sasa leo iweje wewe Sala yako ibakie vile vile, ndio maana inafika wakati mpaka unaona Sala yenyewe inakupa udhia, unafika kusema eti wacha nisali kabisa nikikaa nipumzike, Alaa Sala leo imefikia kuwa kero? kwanini sala yako siku zote iwe vile vile wakati sala yenyewe ni maombi katika maisha yako, na maisha ni safari, sasa ikiwa unasema unasafiri halafu uko hapo hapo hiyo itakua safari?.
Sasa kwanini nikayasema hayo? Soma kwa uzuri usije ukaona huyo sasa anabadilisha Sala, laa sifanyi hivyo ninacho badilisha ni fikra zako unazokwenda nazo katika hiyo Sala, najaribu kukupa muelekeo ili ukiwepo katika hiyo Sala usizame kwenye biashara au siasa au mambo ya kipuuzi ya kidunia ikawa mpaka Sala inakwisha ndio unaamka kwenye (Tahiyyatu) Sasa ufanye nini? Endelea Part 2 upate nini cha kufanya pia ugundue nini siri ya Udhu.
No comments:
Post a Comment