Sunday, January 27, 2013

MTAFUTA DINI, DUNIA LAZIMA IMPOTEE-PART-1

Asalaam Aleiykum,

Nakuomba Mollah wangu nikurubishe mie kwako weye na unijaze fikra zako kila saa na dakika, niwe mie mwenye kukumbuka wewe mpaka muda wa uhai wangu utakapo malizika. Nirekebishe kila pale nikoseapo, Ikisha niweke katika njia ya haki iliyo katika kusudio lako, na kila nikiteleza nakuomba Mollah wangu nirejeshe katika njia yako ilonyooka, kwa kuwa najua mimi ni kinyama sichukui dhamana yakua wakati wote nitakua nimesimama imara katika njia hii, kwa hiyo naomba Mollah wangu nitoe katika daraja hii ya kua kinyama na unipeleke kuwa katika daraja ya Roho njema ilotakasika na kila baya na ovu la Ulimwengu huu.
Hayo hapo juu ni maneno anayopasa kila mtafuta dini yawemo kwenye akili yake. Nani Mtafuta Dini?
Mtafuta dini ni yule ambaye sasa ameamua kuihama dunia huku akiwa na uchu nayo, bado anaijua utamu wake, lakini sasa kimemjia kitu chengine katika moyo wake na anajiuliza hivyo hakuna jambo jengine(Beyond)badala ya mambo haya ya kidunia?, Mambo haya yote ya Ulimwengu huu hayana faida, nikimaliza hili nataka lile, nandelea kuhitaji nikiwa sina kikomo na wala faida yake siioni, sasa hebu kwa mara ya mwanzo nikitafute hicho ninachoambiwa siku zote kina faida na mimi endapo nitaamua kuwa nacho, kitu chenyewe ni hichi kiitwacho dini.
Nini Dini? Dini ni ukamilifu wa maisha, lakini sio haya unayoishi hivi sasa, kuyataka maisha haya itabidi ubadilishe mwenendo au upinde kona kabisa kuelekea katika hayo maisha ndani yake yenye dini. kwanza elewa kwa undani kabisa Maisha haya ya Dini ni tafauti kabisa na maisha ya kidunia, vitu viwili hivi tafauti yake ni kama usiku na mchana au taa na giza havikutani kabisa ima iondoke taa lije giza au uondoke mchana uje usiku, havikutani kabisa, ndio maana darsa hii kichwa chake cha habari ikawa (Mtafuta dini,lazima dunia impotee)katika kuyakinisha haya Mwenye-enzi-Mungu katwambia katika Quraan(Al-Imran-145)
" وَمَا ڪَانَ لِنَفۡسٍ أَن تَمُوتَ إِلَّا بِإِذۡنِ ٱللَّهِ كِتَـٰبً۬ا مُّؤَجَّلاً۬‌ۗ وَمَن يُرِدۡ ثَوَابَ ٱلدُّنۡيَا نُؤۡتِهِۦ مِنۡہَا وَمَن يُرِدۡ ثَوَابَ ٱلۡأَخِرَةِ نُؤۡتِهِۦ مِنۡہَا‌ۚ وَسَنَجۡزِى ٱلشَّـٰكِرِينَ "
"Na nafsi yoyote haitoweza kufa ila kwa idhini ya Mwenye-enzi-Mungu(Na)kwa ajali ilowekwa, Na anayetaka malipo ya duniani tutampa hapa hapa,Na anayetaka malipo ya Akhera tutampa huko, na kwa yakini tutawalipa wanaoshukuru"
Aya imeanza kwa kuyataja Mauti, kwanini yakatajwa mauti mwanzo, ili uwe uzinduo, ili uwe muamsho wako, halafu baada ya mauti aya ikaendelea kwa mwanzo kutaja mwenye kutaka hapa duniani tunampa, sasa tujitizame nani anotaka duniani? jee na wewe umo katika chukua chako mapema(Mwenye kutaka duniani lazima dini impotee)Naam anotaka duniani tunampa hapa hapa(Hatumdhulumu)ila tunampa tahadhari japo tunakupa hapa duniani lakini kumbuka kuna Mauti, kwanini yakatajwa Mauti sababu mauti yanakuja kukunyanganya kila kitu(Unakua muflis)mauti yanachukua nyumba yako na familia yako, mauti yanachukua utajiri wako na kila kilicho chako na kukuacha mweupe hata nguo huvai tena ila unafungwa vitambaa viwili juu na chini, halafu yanakupeleka kwenye nyumba yako ambayo ni chini ya ardhi, mwanzo ulikua unakaa juu sasa unakaa chini. Sasa ikiwa mwenye kutaka dunia ili dini ikupotee bakia hapo ulipo baada ya kusoma darsa hii, ama kama unataka kutafuta dini basi fanya kazi haraka sana ili utoke kwa wenye kutaka dunia, jee unawajua wenye kutaka dunia wanakua katika hali gani? endelea part-2

No comments:

Post a Comment