Sunday, October 27, 2013

MAJINA YA MWENYE ENZI MUNGU(ALLAH)PART 1

Asalaam Aleiykum,

Tunaingia katika Darsa ya mzizi wa (Tawhid), Tunagusa nguzo nzima ya jengo la Dini, Tunakamata kitu muhimu sana na kama wewe utakua makini wa kufatilia na kufahamu darsa hii utatoka katika Bahari hii ya (Tawhid)huku umebeba Lulu na wala sio Chaza mwenyewe, Kwanza kabisa napenda kufahamisha hichi tunachokisoma ndio msingi mzima wa hiyo Sala unayosali, Makusudio yote ya Sala nzima yapo hapa. Kwa hiyo ukishindwa kuifahamu Darsa hii utakua umekosa kitu Adhimu sana, na vilevile ukifahamu basi usiwe mchoyo mwambie mwenzio au mfahamishe ili na yeye apate faida atakapo simamisha Sala awe na ufunuo fulani kwa ajili ya Mollah wake, kutokana na hali hiyo napenda uelewe huyo unompa taarifa hizi kila akizidi kukurubia kwa Mollah wake na wewe ukawa ndio sababu basi anazidi kukusukuma kwa darja na ujira mbele ya Mollah wako.
Katika Darsa hizi Inshaa Allah nitajaribu kuchukua majina matatu manne ili kukuonesha njia ili uifate na hayo mengine yalobakia ukayatafute zaidi, Kwa hiyo kila wiki tutakua tunalisoma jina moja na leo tunaanza Darsa hii na Jina la Allah, Katika darsa hii tunakaribishwa na aya 180 iliyomo kwenye sura ya Al-AAraf inayosema "وَلِلَّهِ ٱلۡأَسۡمَآءُ ٱلۡحُسۡنَىٰ فَٱدۡعُوهُ بِہَا‌ۖ"
"Na Mwenye enzi Mungu ana majina mazuri muombeni (Kwa)hayo"(Na mpaka mwisho wa aya inapomalizikia)
Katika hiyo aya yametajwa mambo mawili inatupasa tuyazingatie nayo la mwanzo Uzuri na la pili Ombeni, ukitumia viwili hivyo wewe mwenyewe utakua unaishi ndani ya huo uzuri ulokusudiwa, kutaka kulijua hilo kwanza tuiulize hiyo Sala, Wewe ni kitu gani, Nini Sala?.
Sala ni maombi Maalum unayopeleka kwa Mollah wako ukitumia hayo majina ya Mwenye enzi Mungu, Bila ya kutumia majina hayo utakua bado hujaitekeleza hiyo Sala, Utafanya Rukuu na Sijda lakini itakua bure mpaka upate jina zuri la kuweza kutumia katika vitendo hivyo. Na hapo ndio unakutana na majina 99 yenye (Kushubihisha)sifa za Mwenye enzi Mungu, Nimesema sifa ili usije ukaingia dhana ya kufikiri hivi ndivo alivo na haya ndio majina yake utakua umeingia hasarani, Mwenye enzi Mungu hana jina, Ila kwa kuwa anazungumza na wewe kwa kutumia lugha na kakufundisha kwa kutumia majina, basi hapana budi upewe sifa hizi nzuri(za mfano) Na imekua uzuri majina yenyewe kuwa 99, kutokana na tabia za viumbe tunajiuliza kwanini ikawa 99, lazima hesabu ikae sawa iwepo la 100, na hilo ndio lengo la kuwepo 99 ili ufanye jitihada kulifikia hilo moja ambalo halitajiki, halisomeki, halina lugha, halina mfano, na hilo ndilo lenye kuyakinisha uwepo wake Subhanna, Hilo halina(Shubiha) kama yalivyo hayo 99, huwezi kutoa mfano abadan.
Huwezi kulitamka, ila utakachoweza kufanya kutumia hayo majina 99 yakupeleke kwenye hilo moja, Na ambalo la karibu kabisa ni hili la (Allah) kama ilivotajwa katika sura ya (Ikhlas)قُلۡ هُوَ ٱللَّهُ أَحَدٌ .
"Mwenye enzi Mungu ni Mmoja" hapo limetumika neno Allah na Mmoja kwa sentensi moja kuonesha mambo mawili, ili usije ukaanza kufikiri labda yuko vile au yuko hivi, Yeye katika Ufalme wake hana Mshirika. Endelea Part 2


MAJINA YA MWENYE ENZI MUNGU(ALLAH)PART 2

Asalaam Aleiykum,

Sababu hana mshirika ndio ikatajwa Umoja kutokana na Allah ina mahusiano na Lugha, na neno la (Ahad)moja lina mashiko yale yale ya kwenye lugha, sasa usije kubabaika ukaona mbona kuna Allah na Ahad, kwanini ikawa viwili hivyo vipo pamoja, kwa sababu vyote vimo ndani ya hilo moja lisilo na lugha, lisoweza kutamkwa, kama Allah ilivokusanya hayo majina 99 hilo moja limekusanya vitu vyote katika Ulimwengu huu, ukiondosha hayo 99 hilo moja linabakia, Moja hili ndilo lenye(Wahid)lenye Ufalme huu wa Ulimwengu, Katika hilo moja sote ndipo tulipotokea na huko dipo tutakaporejea.
Basi kutokana na sababu hiyo, ٱللَّهُ ٱلصَّمَدُ.
"Mwenye enzi Mungu ndiye anastahiki kukusudiwa" 
Na ndio liwe kusudio lako kuyapita kwa maombi hayo yote 99 kufika kwenye hilo lenye dhati yenye yakini, Kila kusudio lako liwe kwa ajili yake, Nani Allahu Ahad? Allah Jina hili kusudio lake ni ule Utukufu Ulotawala Ulimwengu, Utukufu ulokizunguka kila kitu Mbingu na Ardhi(Allahu Akbar) kwa (Zahiri na Batini)Umefichika Utukufu huo na pia uko Wazi kwa Mwenye Akili kuona. Ahad ni Mmoja kwanini isiwe hivyo wakati unajua kila kilichomo katika Ulimwengu huu kimehusiana, wewe na Mti, wewe na Nyota na vyote vilivyomo kwenye Ulimwengu huu vina jinsi moja hakuna tafauti, Mpaka jani liloanguka kutoka kwenye mti au Ua lilochanua lina (Formula ya Dna)kama ulivo wewe, hiyo ndio Ahad, Muumbaji wake nini yeye pekee anokusudiwa na kila kilichomo kati Ulimwengu huu. Hiyo ndio Ahad au (Wahid) ilojificha, vipi sisi leo tutakijua au kulijua jambo linalo onekana na kufichikana kwa wakati mmoja, hatuwezi hata kufikiria upeo wa Allah ukoje, seuze kumfananisha na chochote.
لَمۡ يَلِدۡ وَلَمۡ يُولَدۡ
"Hakuzaa wala kuzaliwa"
Ili kuondosha zana za labda kwamba pengine ni kiumbe ama ana hivi au vile au vyenginevo ndio akatwambia (Hakuzaa wala kuzaliwa) Kilo zaa ama kuzaliwa kinategemea mambo manne, Ardhi,Hewa,Maji,Moto, na vyote hivyo kaviumba yeye Allah vipi leo atakua katika hali ya kuvitegemea vitu hivyo.
وَلَمۡ يَكُن لَّهُ ۥ ڪُفُوًا أَحَدٌ 
"Na wala hana anayefanana naye hata Mmoja" Inaweza mtu kusema ndio hakuzaa wala hakuzaliwa lakini kafanana na (Mtume Fulani) Yeye ni (Formless)hana mfano na yoyote, ikiwa hakuzaa wala kuzaliwa vipi atakua na mfano na yoyote, Anaondosha dhana zenu za kumdhania dhania, Yeye ndiye Allah ambaye mnatakiwa kumuabudu na kumuomba kwa kutumia hayo majina mazuri mazuri, usije ukataka pesa (Ukasoma Tabaytayada-Surat-Massad)utapata moto baada ya pesa, omba kwa majina mazuri upate vilivyo vizuri, na munasaba wake usije ukaishia kwenye hayo majina mkaanza kuleta (Kushubihisha)na hayo majina ukawa unafanya (Image za kila aina) unatakiwa uende (Beyond) ya hizo dhana. Tunamuomba Mollah atufikishe katika hiyo(Tawhid)ya kumjua yeye kwa uwezo  alotupangia wa kumfahamu Mollah wetu Mpenzi.Amin

Sunday, October 20, 2013

LIJUE KUNDI LAKO PART 1

Asalaam Aleiykum,

Jee unataka kujua wewe kundi gani?, Na pia unataka kuelewa ukiwemo kwenye hilo kundi nini kitakufika? Basi hudhuria darsa hii kwa uangalifu mkubwa ili upate kuchagua kundi lako kwa busara. Huna huja ya kusubiri Kiyama au mpaka ufike kaburini, hapahapa Ulimwenguni utajijua mimi ni mtu wa kundi fulani, Na katika hayo makundi yapo ya aina tatu lakini mimi leo nitayazungumza mawili lile la mwanzo la hasara, na lile la pili kundi la kheri.
Kazi yangu mimi ni kukueleza kwanini upo katika kundi fulani na kwa sababu gani, Kitu cha mwanzo unachotakiwa ukifahamu kwamba huu Uhai wako wote ni mtihani, Na hakuna mtihani mkubwa Mwanaadamu unao mshinda kama kusahau, Madhara makubwa sana yanapatikana katika kipindi hichi cha kusahau,Dhanbi zote zinafanyika katika kipindi hicho, Shida zote zipo hapo kwenye kusahau, lau Wanaadamu tungepata theluthi moja ya kukumbuka, basi ungekua wewe Walii, wewe Mcha Mungu, lakini kinyume na hivyo kundi lako litakua la balaa tupu. Na ikiwa utajikuta umo katika kundi baya basi fanya jitihada ukurupuke utoke mbio, na kama umo kwenye kundi la kheri zidi kujipigilia misumari usije ukachomoka.
Sasa kwanza acha tuingie katika kundi la hasara, Kundi la adhabu, kundi la mateso ambalo limewafunika waja kwa moshi mkubwa wa moto wa shetani, Na ndani ya kundi  hili yaweza kuwa umo mwanzoni au katikati au umezama kabisa huonekani hata kichwa. Katika kundi hili la hasara limegubikwa na Matendo ya kusahau ambayo yanapambwa na Vitendo vya Shetani kama alivoahidi mwenyewe( Sad aya ya 82)قَالَ فَبِعِزَّتِكَ لَأُغۡوِيَنَّهُمۡ أَجۡمَعِينَ 
"Akasema Naapa kwa haki ya utukufu wako, Nitawapoteza wote"
Sasa vitendo vipi Shetani anakuingia mpaka kukupoteza, ni huko kusahau, anakuondoshea kukumbuka Ufalme wa Mwenye enzi Mungu, na ukisahau Ufalme huo unaingia hasarani, Hapa inabidi kabla sijavitaja vitendo vyenyewe mnipe nafasi nifafanue kidogo, Naomba kukumbusha hujakatazwa kuishi, sio kila kitu haramu, Maisha sio uteseke, ila kinachokutia hasarani ni kitendo cha kusahau, na jambo la mwanzo katika matendo nitayoyataja utashangaa kwamba si chengine ila Taji la Pesa, Pesa ndio Baba la ushaulivu, Penye pesa Mungu hakai kabisa, penye pesa anakaa shetani na kiburi chake, Pesa ni msukosuko, lakini cha ajabu sote tunafukuzia kundi la pesa, Jee wewe kundi gani? Hili la cheo na umaarufu, Hili la (Power and Security)Hili la kunyanyasa na kuwadharau viumbe wenzio, basi ikiwa ndio hivyo fanya haraka iwezekano umlainishe ngamia wako mifupa kwani itakua tabu kubwa kupita kwenye tundu ya shindano lazima utakwama kichwa(1).
La pili(2)Linalo tusahaulisha Ufalme wa Mwenye enzi Mungu ni Matamanio(Sex), hapa tena tukifika mtu ndio hukumbuki chochote, ndio tunalala kabisa, wewe jitizame ukiwa na mpenzi wako unamkumbuka Mollah wako, Hili la (sex) lina visa chungu nzima ndio linakupofua kabisa, na kama utatajiwa mambo ya akhera wakati huo unaweza kumnasa kibao mtu anakuharibia mambo yako ya starehe, inawezekana hapo kuna watu mia mbili wanakuangalia wewe, ukaambiwa watu wanakuona, ukageuka nakujibu wote hawanioni, hao wanadhani tu, na fanya uchunguzi utaona mambo yako yote unafanya kwa ajili ya hayo matamanio, hisani zote nyuma yake imejificha (Sex) chunguza utapata jawabu la jambo hilo.
Na Jambo la(3)Kutusahaulisha ni Macho, haya ndio hatari tupu, Mimi hapa nataja mambo katika maelfu ya majambo ili nitoe mwanga wa kusahau, Basi hata wewe Macho unanisahaulisha mimi, Ndio, kupitia kwangu ndio unaona Ulimwengu, mimi ndiye ninayekuonesha mipira na senema, Ngoma Na manyama nyama yanotingishika, vipi leo wewe utaweza kumkumbuka Mollah wako.
Jambo la (4)Mdomo mimi ndio (Chifu) wa mazungumzo, mimi ndio nasababisha unazungumza mambo yote ya watu ya kweli na ya uongo, vipi uwe katika vikao na ukaweza kumkumbuka Mollah wako.
Na la (5)Ni hilo shikio, kwanini likaitwa shikio, kwa sababu linashika habari za kila mtu, linasikiliza muziki wote, hili ndilo linalo kusahaulisha kwa utamu (wa ngoma kucheza ukizunguka raha zimezidi)za kumsahau Mollah wako, na takriban kuna mambo mengi ila mimi nimeyataja haya machache makubwa  ili nikujulishe mimi na wewe tumo kundi gani. Na kazi yangu mimi na yako ni kufanya jitihada za kuweza kutoka katika kundi hili la hasara, kama alivokumbusha Mwenye enzi Mungu katika sura ya Mujaddilah aya ya 19ٱسۡتَحۡوَذَ عَلَيۡهِمُ ٱلشَّيۡطَـٰنُ فَأَنسَٮٰهُمۡ ذِكۡرَ ٱللَّهِ‌ۚ أُوْلَـٰٓٮِٕكَ حِزۡبُ ٱلشَّيۡطَـٰنِ‌ۚ أَلَآ إِنَّ حِزۡبَ ٱلشَّيۡطَـٰنِ هُمُ ٱلۡخَـٰسِرُونَ
"Amewatalia Shetani , Akawasahaulisha kumkumbuka Mwenye enzi Mungu, Hao ndio kundi la Shetani, Sikilizeni kwa hakika kundi la Shetani ndilo lenye Kuhasirika(Limo Hasarani)"
Ama kuhusu kundi la pili Endelea Part 2

LIJUE KUNDI LAKO PART 2

Asalaam Aleiykum,

Tunaingia katika kiwanja cha kundi la pili, Kundi hili lilojaa kheri tupu, Tunawauliza ili watupe habari wao wanafanya nini hata wakawemo kwenye kundi hili la kheri, Kundi liloridhiwa na Mwenye enzi Mungu.
Nini Wanafanya?
Wanafanya kitu Rahisi sana, Na wakati huo huo ni kigumu sana, Vipi kitakua rahisi na ugumu kwa wakati mmoja, wafanyacho wao ni kinyume cha kusahau, kama kundi la mwanzo wanasahau wao wanakumbuka, hiyo ndio tafauti yao, Na wewe ukifanya hilo la kukumbuka moja kwa moja unaingia katika kundi hili la kheri.
Sasa Ukumbuke Nini?
Kitu cha mwanzo kukumbuka ambacho ndio Sala yenyewe, Ndio Ibada yenyewe, Hata hao wanosali nyakati zote wanakifanya hicho hicho ni (Kulitaja Jina la Mwenye enzi Mungu) Kama alivotuamrisha katika (Sura ya Muzzamil aya ya 8)
وَٱذۡكُرِ ٱسۡمَ رَبِّكَ وَتَبَتَّلۡ إِلَيۡهِ تَبۡتِيلاً۬
"Litaje jina la Mollah wako, Na Ujitupe (Kwake)Kikweli(Kwa)(Devotion).
Kwanini ikawa Jina? Kwa sababu wewe mwanaadamu huna njia nyengine ya kumjua Mollah wako ila lazima upitie mlango huu wa jina, na Mlango huu wewe ndio ulopitia mwanzo kwa ajili ya mafundisho yako ya Majina, kutokana na Majina wewe ndio ukaona. (وَعَلَّمَ ءَادَمَ ٱلۡأَسۡمَآءَ كُلَّهَا)"Akamfundisha Adam majina ya vitu vyote"(Mpaka inapomalizikia aya) Nimesema unapitia kujua ndio ukaona, nina maana hii, Ingekua kuona ni kujua basi Malaika walipowekewa hivyo vitu wangevijua, Sasa kwanini hawakuvijua, ukijibu kwa urahisi utasema hawakufundishwa, na ukisema hawakufundishwa itabidi unipe  nafasi nifafanue zaidi.
Kutokana na Kadhia hiyo lazima kuwepo Mfundishaji, na hilo litakufanya uzame kwenye elimu ya (Tawhid)ili uweze kufahamu nasema nini kuhusiana na (Fumbo)hili la kufundishwa.
Katika kufundishwa au kujua lazima vipatikane vitu vitatu hivi: Anojua(Knower) Kinachojulikana(Known)Na Kisichojulikana(Unknowable) Hichi kisichojulikana ndio kinachokupa wewe uwezo wa kujua(Mollah wako), vipi leo utaweza kukiona hicho kisichoweza kuonekana, Ndio maana Nabii Musa a.s akaambiwa hutoweza kuniona, kwa hiyo na wewe ondoa itikadi yuko hivi au yuko vile usije ukapotosha Imani yako, Na kwa kuwa huwezi kumuona basi kwa Rehma zake kakupa Mbegu uipande ya kuweza kumjua, (Kwani hata ukipewa uwezo wa kumuona hutoweza kumjua) kwa hiyo chukua Mbegu hii ya kumjua ipande na hakuna anojua nini kitaota, unaweza kuota huo Mti wa majina 99 ambayo Insha Allah wiki zijazo nitakua nayapitia mawili matatu ili tupate maana yake na faida zake. 
Sasa Turejee nyuma katika lile kundi la kheri kundi la Mwenye enzi Mungu. Kundi hili la pili wameambiwa ili na nyinyi msisahau mkashughulika na mambo mengine basi nyie litajeni Jina la Mwenye enzi Mungu, Lishikeni kwa mtajo Jina langu, Nini kitatokea ikiwa mtadumu katika kunikumbuka kupitia moja katika majina hayo 99. Endelea Part 3



LIJUE KUNDI LAKO PART 3

Asalaam Aleiykum,

Litaje jina la Mollah wako, nini kimo ndani ya hilo jina, Elewa ndani ya hilo jina yamefichwa mambo, Ndani ya hilo jina utapata kumjua Mollah wako, Sio Kumuona, Na siri ya kujua haina mwisho, daima utaendelea kufunguliwa maajabu yaliyomo kwenye Ulimwengu huu kama wanasayansi wanavoendelea kuvumbua kila siku mambo mepya mepya, Basi na wewe kama umo katika kundi la Mwenye enzi Mungu unayo nafasi hiyo ikiwa utadumisha kulitaja na kulikumbuka jina la Mollah wako.
Kwani ikiwa utakua unalitaja pekee utaingia katika kusahau, utakua kama kasuku, inatakiwa lazima ulikumbuke kwa hamu kubwa na Shauku, kama unavokumbuka mbona sijasali, ni kitu kimoja ila umebadilisha jina, Sababu unakwenda kutaja hilo hilo jina la Mwenye Enzi Mungu. Jitupe kikamilifu, vipi kujitupa kikamilifu(Devotion) Unakumbuka wakati unashida au jambo baya litakutokea unavomuomba Mollah wako akuvue, hivyo ndio kujitupa, Na huko kujitupa isiwe kwa ajili ya kuonesha watu iwe siri baina ya wewe na Mollah wako, Na Mollah wako ni mwenye kukujua vipi ukweli wa mapenzi yako juu yake, usijali wengine kama wanajua wewe Mcha mungu au sio usiwajali kabisa hawapunguzi wala kuongeza chochote katika dini yako, Kujitupa kwenyewe lazima kuwe kwa Roho yako, Akili yako, na kila tendo lako kwa ajili ya kumkumbuka Mollah wako.Na hiyo ndio maana halisi ya( وَتَبَتَّلۡ إِلَيۡهِ تَبۡتِيلاً۬).
Na hayo ndio makundi mawili ama utakua kushoto au kuliani, lipo la tatu lakini nimeamua nisilizungumze kwa sababu watu wachache sana wanofanikiwa kubakia katika hilo kundi la katikati la (Ashab-Aaraf)ambalo hili kwa viumbe haliko na kwa Mollah wao halitaki.
Inshaa Allah tutalizungumza siku za mbele penye majaaliwa tukipata nafasi. Na mpaka sasa ushapata nafasi ya kujijua wewe mtu wa kundi gani, Basi ikiwa la hasara fanya haraka utoke kwani muda ushamalizika, umekaa siku nyingi katika kundi hilo la hasara, huna faida unayopata ila kuzidi kumsahau Mollah wako.
Na kama umo katika kundi la kheri basi zidisha mapenzi yako kwa Mollah wako na yeye atafungua pazia lake uone mambo hujapata kuyaona ya furaha katika Ulimwengu huu, Hapo utajua Mollah wako kakuridhia na wewe umemridhia, Na kuwemo katika kundi la Mwenye enzi Mungu ni mafanikio yasioelezeka.
Namuomba Mollah atujaalie sote tuwemo katika kundi la kheri aliloliridhia kwa uwezo wake Rahman. Amin.



Sunday, October 13, 2013

MUALIKO WA IMANI PART 1

Asalaam Aleiykum,

Kubali kuna kitu kinakusumbua, Kuna jambo hutaki kulisema, mbona umenyamaza kimya, unadhani nani atakusemea, Na hofu sasa imekuzidi Umri unasonga mbele, Na ndani ya moyo wako una yakini Imani haipo, hujui ufanye nini, Moyo unakutu, kipande hicho cha nyama umekijeruhi kwa mambo chungu nzima ya maasi nk, ndio maana Imani haina nafasi ya kukaa kabisa, Na una wasiwasi pengine hiyo ndio sababu dua hazipokelewi, unakhisi katika mambo ya Dini umekua muflis, hali hiyo inakufanya uwe dua zako mfano wa(Mtu aliye kwenda kwa Tajiri akaomba akopeshwe pesa ya kiwanja, na huyo tajiri akashangaa hii huyu utajenga vipi hiyo nyumba) Na hivi ndivo sote tunavo shangaa  katika jambo hili la Imani, Mbona kwangu haitokezi Imani hii, Hali yangu mimi najijua sina chochote moyoni, Nasoma Quraan, Nasali sana lakini ndani Kifuani(Empty).
Na baya zaidi nikishikwa na dhiki ima namtegemea Mganga au binaadamu mwenzangu kunitatulia matatizo yangu, sasa hapo iwapi Imani yangu, Na kibaya zaidi nakwenda kwa mganga eti kutafuta Utajiri hali najua huyo Mganga mwenyewe anataraji mie ndio nimpe pesa ili apate chakula chake, Inakua vipi namuamini Mganga kuliko Mollah wangu. Haya yote yanatukuta na tumo tunajiuliza lini na mimi nitaipata hiyo Imani niachane na mambo haya, lini nitaipata Imani iwe napeleka sala yangu kikamilifu, Nini tufanye tupate kutoka madhila, Tupate kusafisha Nyoyo zetu ili ije kukaa hiyo Imani.
Midamu umeuliza swali hili unajibiwa kuwa zipo mbinu na njia ukifanya unaweza kuipata hiyo Imani na zaidi ya Imani, ukifanya utafunguliwa mambo ambayo hujayategemea katika maisha yako, basi kama uko tayari chukua Zawadi ya aya iliyopo kwenye sura ya Rad aya ya 28. Inasemaje kuhusiana na kuipata hiyo Imani
Endelea Part 2

MUALIKO WA IMANI PART 2

Asalaam Aleiykum,

 ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَتَطۡمَٮِٕنُّ قُلُوبُهُم بِذِكۡرِ ٱللَّهِ‌ۗ أَلَا بِذِڪۡرِ ٱللَّهِ تَطۡمَٮِٕنُّ ٱلۡقُلُوبُ 
(Wao)Ni wale waloamini na zikatulia Nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenye enzi Mungu, Kwa kumkumbuka Mwenye enzi Mungu nyoyo hutulia.
Maneno yaliyotajwa hapo juu ni makubwa ikiwa unayajua maana yake kwa undani, lakini kama utapita juu juu hupati kitu, maana imefichika mpaka uwe katika wale wanotaka kujishughulisha kuitafuta.
Kwa wale wanotaka kujua maana basi nitafafanua kidogo ili nikujuze japo kwa uchache maana hiyo, Pata faida mbili hizi uzitumie kuipata hiyo Imani katika moyo wako ugeuke kuwa mtu mwengine kabisa.
Aya Imeanza kwa wale waloamini. Nini Kuamini? Kuamini ni kukubali bila ya pingamizi yoyote kwa lile uliloambiwa, Lakini hiyo haitoshelezi haja, ukikubali bila ya ushahidi (Shaka inabakia) Kwa sababu umeambiwa tu, inaweza kuwa kweli au uongo, unakua na mashaka huna utulivu, mara unafanya makosa, mara unatubu, mara unajiuliza pepo ipo, mara unajipa tamaa moto hakuna, hali hiyo inatokea moyoni mwako kila siku, Ndio maana mtu akikwambia katokea mjini unakubali, unamuamini, lakini ikiwa umemuagizia kitu hajakuletea unabaki na wasiwasi sijui kenda kweli au ananidanganya, lakini wakati huo ushaamini, inakua nusu umeamini nusu una shaka, kutokana na hali hiyo moyo wako unakua (Split)umegawika hauko kwenye Imani wala kwenye kukanusha.
Na unajiona hivi sasa Unakubali Mwenye enzi Mungu yupo, unaogopa adhabu zake, lakini bado unachungulia dirishani huku shaka imekushika, inaweza kuwa kweli inaweza kuwa uongo, Na kama kweli wacha Nisali, Na ikiwa uongo sijapata hasara yoyote, hivi ndio fikra zetu zilivo, zimejaa kila shaka, zimejaa mambo chungu nzima, Unapeleka dua bila ya tamaa, Sala yako inakua kama ya kulazimishwa.
Sasa kwenye aya hii unakumbushwa kitu muhimu sana na kama utakifanyia kazi unaweza kupata manufaa makubwa ya kuipata hiyo Imani. Wale wenye kuamini wanapata utulivu kwa kumkumbuka Mollah wao, Kukumbuka kuko kwa aina mbili, aina ya kwanza hii ni ngumu sana, wachache sana wanoweza kuipata hiyo Imani kupitia njia hii, na hiyo njia ya pili ni rahisi wengi wanaweza kuipata hiyo Imani kama watafata maelekezo yake.
Ama hii ya ugumu unatakiwa Uweke uwepo wa Mwenye enzi Mungu wakati wote (Presence) kila unapokuwepo fikra zako, na wewe mwenyewe uwe kwa Mollah wako, Ukiona Mti, Ukiona Ndege, Ukiona Mbingu, Ukiona Jua, Ukiona mwezi iwe unaviona vyote hivyo na huku unamkumbuka Mollah wako ndie aliyeviumba, ni Vigumu sana huwezi kumkumbuka Mollah kwenye Sala yako, utamkumbuka ukiona Mti, ndio maana nikasema hii ni ngumu wacha sasa tuitizame hiyo ilo rahisi ili tupate kuona kama tutaipata hiyo Imani.
Endelea Part 3

MUALIKO WA IMANI PART 3

Asalaam Aleiykum,

Kwanini utulivu haupatikani kwa sababu huna Imani, Na kama Imani haipo ndio utaona kila ukianza Ibada huyoo unatoka arijojo hurejei mpaka pale Ibada inapotaka kwisha, Sasa hii aina ya Pili ni ya Kutamka iwe taratibu au kwa sauti, hii kidogo ni Rahisi nikisema rahisi nina maana kama utaifanyia mazoezi labda unaweza kuipata hiyo Imani kwa kutumia njia hii ya kukumbuka Majina ya Mwenye enzi Mungu, Na majina hivyo hivyo yako mengine ni magumu kujihusisha nayo kwa njia ya kukumbuka, mie nimekuchagulieni jina hili la Rahisi pengine mtu anaweza kulizoea nalo ni kalima ya Tawhid(Laa Illa Illah Allah) Lifanyie mazoezi ya kulitaja na kulikumbuka Jina hili japo kwa siku nzima uone faida zake, na ukiweza kufanya kwa miezi mitatu utaona faida zake kubwa kubwa zinazopatikana katika jina hili la Mollah wako.
Nini Kinatokea?
Ukiweza kufanya moja katika mawili hayo nilokueleza utaanza kuona Utulivu unakushukia katika Moyo wako, Na huo Utulivu ukija unafatana na hiyo Imani,Na kwa ajili gani ukaja huo utulivu, kwa sababu Fikra zako haziwezi kumudu mambo mawili, Fikra zako zina (Focus)katika jambo moja tu, kwa hiyo Unapo mkumbuka Mollah wako una (Block) vyengine vyote, na ukivizuia hivyo vyengine ndipo unapata huo Utulivu,  Na utulivu ukija unageuka na kuwa Imani, Na Ukiipata Imani unakua ushafanikiwa, watu wanaweza kuchukua utu wako, wanaweza kuchukua heshima yako, wanaweza kuchukua cheo chako na mali yako, Lakini kitu kimoja hawawezi kukichukua ni hiyo Imani yako Adhimu uliyonayo. Na huo utulivu unatokea vipi, kihudhurie kisa hiki cha Mke na Mume(Walipokua wamepanda Jahazi wanasafiri mara kukazuka Kimbunga kikubwa, Yule Mke akaanza kupiga mayowe na kelele huku akimwambia Mumewe fanya maarifa tuokoke au tutakufa, Yule mume alipoona makelele yamezidi alichomoa jambia lake akamuekea mkewe shingoni, yule mke akanyamaza kimya, baada ya muda kupita yule bwana akaondosha kile kisu shingoni, Ikisha akamuuliza Mkewe nini kimetokea mbona umenyamza kimya, Yule bibi akajibu umenijia Utulivu sijapata kuuona, hofu yote ya kimbunga iliniondoka, ikawa naona kwa kimbunga nitakufa na kwa jambia nitakufa sasa kelele za nini. Yule Mume akasema na mimi  nimetulia moyo wangu nikawa najua aloleta Kimbunga hichi yeye ana uwezo akitaka tutakufa na akitaka tuokoke basi atakiondosha kimbunga kama alivofanya sasa hivi).
Na hiyo ndio Imani na utulivu ulokusudiwa, sio ya matatizo kidogo kukimbilia kwa waganga kuomba ufanikiwe, Unamtegemea Mtu mpaka unamuasi Mollah wako, Na sasa turejee nyuma katika yale mambo mawili ya (Dhikiri) au kukumbuka, Nini Kinatokezea?
Ukiweza kudumu kukumbuka, unakua unatumia (Energy)nguvu ambayo inatumika ukiwa kimya au ukitoa sauti, yote hayo ni sawa.
Unapotumia hizo nguvu unakutana na Sheria mbili moja hii inojulikana ya Ulimwengu ambayo inaitwa (Gravitation) na ile ya Pili ya Dunia ya pili ambayo ni ya (Sipiritual)inayoitwa(Levitation) pengine mtu ishawahi kukutokezea lakini huijui, na inatokezea mara nyingi kama umedumu kwenye Ibada au unasoma Quraan utahisi kama unapaa au unanyanyuka kutoka katika ardhi wakati umekaa, Na kama haijakutokezea fanya ujaribu upate faida ya kuijua hiyo (Levitation).
Aya Imesema wale wenye kuamini wanapata utulivu kwa kumkumbuka Mollah wao, Wanapoanza kukumbuka wanakua wanapeleka nguvu hizo za kukumbuka Moyoni, na kama kweli Mja anafanya kwa Ikhlas na kumuhitaji Mollah wake na kumkumbuka kila mara, Basi Mollah wao huwapa nguvu hii ya (Levitation)ikatokea Moyoni na kuwa utulivu wa Imani, Na ukipatikana huo utulivu nguvu hiyo haibakii hapo moyoni bali inapanda juu, Na hapo ndio unapatikana Ucha Mungu, Kwenye moyo umetulia haikubabaishi mali ya mtu, anotaka kukuroga, anotaka kukudhulumu,vyote hivyo havikushitu kabisa, Na  juu kwenye kichwa utaona furaha na mapenzi yanotokea kwenye huo moyo, na hapo tena ndio unaanza kutoa nuru moyoni mwako, wale wanofahamu wanajua sasa ushapanda daraja, unageuka wewe kuwa (Light)Laa illa illlah Allah inakungarisha mbali ya kukupa utulivu, na yoyote atokua karibu na wewe anapata hiyo nuru, macho yako yatakua yanangara kwa nuru ya Mwenye enzi Mungu.
Huo ndio Utulivu ambao unaambatana na Imani, Na hakuna kitu kizuri katika Ulimwengu huu kama Imani, Imani haibadiliki, Imani haisemi uongo, siku zote inatoa uhakika, siku zote iko vilevile haibadiliki, Na ikiingia Imani unakua ushashinda, usha (Surrender) na huo ndio Uislam, kwa hiyo fanya hima ujitahidi kualika hiyo Imani ije kwenye Moyo wako ili upate utulivu, fanya sana bidii ya kukumbuka, kwani ushasikiliza Mawaidha chungu nzima mambo yako vile vile, ushasomewa hadith mabuku kwa mabuku bado hujabadilika, basi hebu jaribu dawa hii yaweza kuwa ndio ponyo lako ukapata hiyo Imani, kinachotakiwa ni kukumbuka tu, sikwambii ni rahisi lakini inawezekana, na Imani ikiingia Moyoni kwako hapo ndio unaipata Sala sawasawa, Dua zako zinapokelewa kwa uhakika. Naomba Baraka za Mollah zitushukie sote tuwe na Imani.

Sunday, October 6, 2013

SIRI NDANI YA SIRI PART 1

Asalaam Aleiykum,

Katika Ulimwengu wa Elimu zipo za aina mbili, ya kwanza ni hii ya Dhahiri, na ya pili ni ile ya siri ilofichika ambayo leo tunaingia japo kidogo tupate kuchungulia tujue faida mbili tatu ambazo zitaweza kutujulisha mambo ya upande wa pili katika hiyo elimu isiyo onekana, Twende tukapajue pahala panapotokea  hiyo siri.
Nitaanza darsa yetu ya leo kwa msemo wa hekima ulo maarufu unaosema hivi"(KAVUNJA UKUTA WA WATU KWA HARUFU YA CHAKULA KITAMU)"
Msemo huu kwa nje unaonekana ni wa kawaida lakini ukizama ndani ya maana ya maneno haya utakutana na Siri kubwa ilofichika ndani ya Ukuta huo.(Kavunja Ukuta wa Watu) tujiulize kwanini akavunja?. Inaonesha labda hajui Mlango ulipo, Na hivi ndivo sote tulivo, hatujui mlango uwapi na kila mtu anapita akivunja ukuta wa mwenzie bila ya faida yoyote. 
Sasa Ukuta kwani una siri gani? Ukitaka kujua siri ya Ukuta kihudhurie kisa cha Msemezwa na Mwenye enzi Mungu Nabii Musa a.s na yule Mja alopewa elimu na Mollah wake kwa jina anaitwa Al Khidhir, Kisa chenyewe kilianzia pale walipofika katika mji wakaomba wapewe chakula na wale watu wa ule mji wakakataa, Ndipo Al Khidhir alipoukuta Ukuta unataka kuanguka akaujenga, Na Nabii Musa a.s akamwambia kwanini umeujenga, Al Khidhir akamjibu.
 وَأَمَّا ٱلۡجِدَارُ فَكَانَ لِغُلَـٰمَيۡنِ يَتِيمَيۡنِ فِى ٱلۡمَدِينَةِ وَكَانَ تَحۡتَهُ ۥ كَنزٌ۬ لَّهُمَا وَكَانَ أَبُوهُمَا صَـٰلِحً۬ا فَأَرَادَ رَبُّكَ أَن يَبۡلُغَآ أَشُدَّهُمَا وَيَسۡتَخۡرِجَا كَنزَهُمَا رَحۡمَةً۬ مِّن رَّبِّكَ‌ۚ
"Na ama(ule)Ukuta, Ulikuwa wa watoto wawili mayatima katika huo mji, Na chini yake(Ya Ukuta)kulikuwa na Hazina yao, Na Baba yao alikuwa (Mtu)mwema, kwa hivyo Mollah wako alitaka wafikie baleghe yao (Ili)wajitolee hazina yao, Hiyo ni Rehma inayotoka kwa Mollah wako" Mpaka inapomalizikia aya.
Naam hizo ndizo habari ya siri za Ukuta, Ukuta ni wenye kuficha Siri na Hazina za kila aina, Sasa huo wa kwenye Quraan ulikua ndio unaanguka ukajengwa, lakini kinyume na Ukuta wetu kenda mtu kuuvunja makusudi, Na sababu yake kubwa kuvunjwa ukuta huu ni hiyo harufu.
Nini Harufu? Nipeni nafasi nifanye ufafanuzi mdogo wa harufu ili tujue Harufu ina mahusiano gani na (Siri ndani ya Siri)pata faida hii uitie kibindoni iwe manufaa  kwako. Harufu kwa upande wa sayansi inapatikana kwenye pua na lazima ipatikane(molecules)kutoka katika hicho kitu ili upate kunusa hiyo harufu, lakini upande wetu wa (Mystic)katika fani ya Dini tunatambua harufu inatokea kulekule inapopatikana hizo (Senses)tano kubwa ikiwemo na kunusa, zipo za ziada lakini leo tutazitaja hizi tano ili kufupisha uchambuzi, nazo ni (Kuona, Kusikia, Kunusa, Kugusa na Kuhisi) yote hayo yanamilikiwa na hiyo Siri, Na hiyo Siri inakaa kwenye huo Mwili lakini cha ajabu haigusani na huo Mwili(Siri ndani ya Siri) Na kwenye hiyo siri ndipo inapopatikana Harufu, Na hiyo harufu yenyewe inaendelea kuwa siri, Mwana sayansi anaweza kulikamata Ua akatwambia kuna kitu kinatoka katika hilo ua kinaitwa (esters)kinatokea kwenye Ua ukimuuliza afafanue hajui ni kitu gani, au akujibu nini,ila atakwambia livamie upate (DNA)zake, lakini utapata (DNA)huwezi kupata harufu na hiyo ndio haja yako, kwa hiyo Utavunja ukuta wake lakini hupati harufu yake, Sasa ufanye nini kuijua hiyo harufu? Endelea part 2

SIRI NDANI YA SIRI PART 2

Asalaam Aleiykum,

Itafute harufu uijue mahusiano yake na yako, fanya bidii uzinduke uifate, kaipekue hivi sasa huna haja ya kuvunja Ukuta, harufu itakuonesha Mlango, itakufahamisha kuwa Bwana wee, mie natokea huko kwenye kutokea usingizi, kwenye kutokea kuona, kwenye kutokea kusikia na mengi mengineyo ya siri ambayo nyinyi hamshughuliki kuyatafuta ila mnashughulika na mambo ya Kidunia, Rumi aya ya (7)"يَعۡلَمُونَ ظَـٰهِرً۬ا مِّنَ ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا وَهُمۡ عَنِ ٱلۡأَخِرَةِ هُمۡ غَـٰفِلُونَ ".
"Wanajua hali ya dhahiri(Wazi)ya Maisha ya Dunia, Na wameghafilika na akhera"
Hamtaki kabisa kujua akhera kuna nini, Na wala hamtaki kuwauliza wanojua wakufahamisheni, Watu wameshika kupangiana na atokwenda peponi na nani anopata Sala sawa sawa, hiyo sio kazi yako wala haijakuhusu, na ukiona unajishughulisha sana na hilo basi jitilie wasiwasi kwanza wewe mwenyewe, yaweza kuwa umekua (Muflis)na shetani anakujengea cheo cha kujiona wewe tayari ushafanikiwa, tahadhari sana. Sasa wewe ufanye nini? nini kazi yako wewe, unatakiwa ujishughulishe sana na kupekua na kuyajua mambo ya akhera, si kwambii ni rahisi, bali yanawezekana kuyajua, na wewe kuwa Mwana sayansi wa Kidini, ufanye nini? likamate Ua ikisha zungumza nalo, Kumbe wewe Ua uko kama mimi, wewe una (DNA) na mimi ninayo, wewe una harufu na mimi nina sauti vyote hivyo vimetokea kwenye hiyo (Siri ndani ya Siri) Na baina yetu tunaweza kuipata (Communion)ikawa baina yako na Ua mnakutana (Sirini)Chuma ni vigumu wewe kukutana nacho lakini Ua ni rahisi kukutana nalo, kwa sababu baina yenu inapatikana nipe nikupe,(Ua linatoa harufu na wewe unatoa harufu)mnakutana katikati wewe ndio unatafsiri hili la waridi, lakini ukiweza kupata harufu hiyo ukawa hujafasiri  chochote ndio hapo mnakutana kwenye Siri, Ua linapotea na wewe unapotea kinachobaki (Kakitafute mwenyewe)Siri ndani ya Siri.
Na ukiigundua hiyo siri na ukaamua kuifata basi hakuna kwengine itakapo kupeleka ila kwa Mwenye enzi Mungu wako, Sisemi habari za harufu wengine mkanifahamu vyengine na kuanza kunusa mabaibui ya watu na kanga zao, atanaswa mtu kibao mie(Simo) Lazima ujue dhumuni na kusudio la harufu ilokusudiwa, Na hiyo harufu imetumika kama alama na ukiifata hupotei, lakini vipi utaijua harufu wakati Ua lenyewe hulijui, basi kama ushafahamu maana ya harufu ifate ukapate chakula na kinywaji cha 
 خِتَـٰمُهُ ۥ مِسۡكٌ۬‌ۚ
Mwisho wake(kinaleta harufu ya)Misk, 
وَفِى ذَٲلِكَ فَلۡيَتَنَافَسِ ٱلۡمُتَنَـٰفِسُ
"(Basi) na katika (kuyapata) haya washindane wenye kushindana", na kushindana kwenyewe ni kuipata hiyo harufu inayo kujulisha mambo mema ili uyafanye, na ukiinusa hiyo harufu kweli kweli basi huokoki tena, daima utanasa kwenye (Ulimbo) wa harufu na kwa njia hiyo tunapata siri iliyomo kwenye harufu na nguvu ya harufu hii ilofanya mpaka watu wakavunja kuta za watu, mpaka hii leo harufu imebaki inawashangaza wengi, wapi inatokezea na wapi inakwendea, na huko inapokwenda na sisi tutafika, na kwanini hassa inatuvutia, na ukitizama kila mtu ana hamu ya kuvunja huo Ukuta apate hiyo harufu lakini si kitu chenye kupatikana kwa urahisi, ndio maana tukaambiwa washindane wenye kushindana kwa ajili ya hayo mambo ya Akhera.
Sasa kwanini Mvunjaji akavunja Ukuta wa watu kwa harufu ya chakula kitamu?, Inaonesha Mvunjaji lazima aliwahi kukionja au kukila chakula kitamu ndio maana akaijua harufu yake.
Endelea Part 3

SIRI NDANI YA SIRI PART 3

Asalaam Aleiykum,

Kwanza kabisa napenda nifahamishe harufu yenyewe ilokusudiwa kushindaniwa ni hiyo ilotajwa katika aya ya 21 mpaka ya 28 ya sura ya Al Mutaffifyn, Harufu yenyewe ya kushindaniwa ni hiyo Ibada, harufu yenyewe ya mambo mema, na harufu ya Ucha Mungu ili uyapate hayo yalotajwa nyuma katika hiyo sura.
Kavunja ukuta wa watu kwa harufu ya (Chakula kitamu)Kajuaje kama hiyo alonusa ni ya chakula kitamu, lazima mwanzo iwe kakaribishwa, lazima alialikwa na kukila chakula hicho, ndipo aliposikia harufu akakumbuka ni ya chakula kitamu, hakusema chakula pekee bali kaongeza na utamu.
Nini Utamu? Utamu ni wenye kukaa kwenye ulimi, nikisema kukaa sina maana uko hapo, ila unapitia hapo kama harufu inavopitia puani, na unafanya kazi zake kwa mashirikiano ya pamoja na harufu, ndio maana mvunjaji akavunja ukuta kwa harufu ya chakula kitamu. Na inavoelekea sote tushaonja chakula hichi na bado tuna hamu ya chakula kitamu, ila upo wetu umetufikisha katika kukijua tu na bado hatujakifahamu, Na tafauti ya kufahamu na kujua ni kubwa sana, kwani kufahamu kunatokana na (Roho) na kujua kunapatikana kwenye (Akili), Kwa hiyo aliponusa harufu akafahamu ni ya Biriani, alipokiona chakula akajua ni kitamu,( au mfano mwengine wa maneno unaambiwa Mgonjwa anafahamu zake anamjua anoingia na kutoka)ukizama kwenye maneno hayo utajua nimekusudia nini.
Usije ukakurupuka ukanusa vitunguu ukadhani Biriani, kumbe ni wali wa Ki Iran, Naam kwanini chakula , katika mambo yote mwanaadamu anaweza kuyakana isipokua chakula.Anao uwezo mwanaadamu wa siku 90 tu, baada ya hapo bila ya chakula anakufa, watu wanapigana vita kwa ajili ya chakula, Binaadamu anaweza kukamilisha kila kitu lakini akifika kwenye chakula anashangaa, anatoa macho, anajiuliza kama kikikosekana au ikawa Mollah kazuia kisiote chochote nini utakua mwisho wetu.
Ndio tunaambiwa msitoe macho kwenye hicho chakula kuna ushahidi wa kutosha kuonesha kuwapo kwa Mwenye enzi Mungu na mambo ya Akhera, Inatosha kukufahamisha kama Muumbaji yupo na kama unavo kitizama chakula chake na yeye anakutizama wewe, Na huyo Mollah wako alokuumba sasa anakwambia huna haja ya kuvunja ukuta, kwanza kitizame chakula chenyewe upate kukifahamu, فَلۡيَنظُرِ ٱلۡإِنسَـٰنُ إِلَىٰ طَعَامِهِۦۤ,(Abbasa 24)
"Na Atazame mwanaadamu chakula chake"
Siri ndani ya Siri, Sisi ndio yulomuoteshea, tukaifungua ardhi na kuotesha vyote vilivyomo na kutajwa katika sura hiyo na venginevyo visivotajwa.
 مَّتَـٰعً۬ا لَّكُمۡ وَلِأَنۡعَـٰمِكُمۡ
Kwa ajili ya kukustarehesheni nyinyi na wanyama wenu(Abbasa 32) Itizame siri ilofichikana kwa upande wa nje kukustarehesheni(Kavunja ukuta wa watu kwa harufu ya chakula kitamu) lakini kwa upande wa ndani chakula hicho hicho ni dawa kinatibu maradhi haya na yale, ndani ya chakula inapatikana Vitamin, ndani ya chakula inapatikana hizo nguvu unazoringia, Kitizame chakula chako ikisha jiulize nani alotia maji kwenye Dafu, Nani aloufanya mua kutoa sukari ukakutia nguvu, Nani aloweka sukari kwenye Tende, Ndizi, na Zabibu, Jee ushawahi kuzijua ladha yake kwa undani, au unakula zikujaze tumbo, Ushawahi kula chakula bila ya mazungumzo wala tafsiri yoyote ikawa wewe na chakula mnatafutana maana laa bado, basi hebu fanya japo siku moja amua kula chako mwanzo mpaka mwisho bila ya kuzungumza au kutizama TV na kadhalika, iwe wewe na chakula tu uone ladha yake itakuaje, kitafute chakula siri yake na ukiijua hutotaka tena kula huku unazungumza, utakua mwenye hamu ya kujua ikiwa Duniani nahisi ladha hii huko Akhera itakuaje nikipewa(Fresh)Zama kwenye vyakula utapata siri hizo ndogo ndogo zitakuchukua kwenye hiyo siri kubwa, na ukiweza kufika kwenye siri hiyo ndio unakua huna haja ya kuvunja ukuta wa watu, Unaingia kwenye Siri ndani ya Siri, Na utakayo yakuta huko ni Siri yako huna haja ya kuhadithia kama nilivofanya mimi.
Nakutakieni siku kumi njema za Dhul-Hijja.