Asalaam Aleiykum,
Itafute harufu uijue mahusiano yake na yako, fanya bidii uzinduke uifate, kaipekue hivi sasa huna haja ya kuvunja Ukuta, harufu itakuonesha Mlango, itakufahamisha kuwa Bwana wee, mie natokea huko kwenye kutokea usingizi, kwenye kutokea kuona, kwenye kutokea kusikia na mengi mengineyo ya siri ambayo nyinyi hamshughuliki kuyatafuta ila mnashughulika na mambo ya Kidunia, Rumi aya ya (7)"يَعۡلَمُونَ ظَـٰهِرً۬ا مِّنَ ٱلۡحَيَوٰةِ ٱلدُّنۡيَا وَهُمۡ عَنِ ٱلۡأَخِرَةِ هُمۡ غَـٰفِلُونَ ".
"Wanajua hali ya dhahiri(Wazi)ya Maisha ya Dunia, Na wameghafilika na akhera"
Hamtaki kabisa kujua akhera kuna nini, Na wala hamtaki kuwauliza wanojua wakufahamisheni, Watu wameshika kupangiana na atokwenda peponi na nani anopata Sala sawa sawa, hiyo sio kazi yako wala haijakuhusu, na ukiona unajishughulisha sana na hilo basi jitilie wasiwasi kwanza wewe mwenyewe, yaweza kuwa umekua (Muflis)na shetani anakujengea cheo cha kujiona wewe tayari ushafanikiwa, tahadhari sana. Sasa wewe ufanye nini? nini kazi yako wewe, unatakiwa ujishughulishe sana na kupekua na kuyajua mambo ya akhera, si kwambii ni rahisi, bali yanawezekana kuyajua, na wewe kuwa Mwana sayansi wa Kidini, ufanye nini? likamate Ua ikisha zungumza nalo, Kumbe wewe Ua uko kama mimi, wewe una (DNA) na mimi ninayo, wewe una harufu na mimi nina sauti vyote hivyo vimetokea kwenye hiyo (Siri ndani ya Siri) Na baina yetu tunaweza kuipata (Communion)ikawa baina yako na Ua mnakutana (Sirini)Chuma ni vigumu wewe kukutana nacho lakini Ua ni rahisi kukutana nalo, kwa sababu baina yenu inapatikana nipe nikupe,(Ua linatoa harufu na wewe unatoa harufu)mnakutana katikati wewe ndio unatafsiri hili la waridi, lakini ukiweza kupata harufu hiyo ukawa hujafasiri chochote ndio hapo mnakutana kwenye Siri, Ua linapotea na wewe unapotea kinachobaki (Kakitafute mwenyewe)Siri ndani ya Siri.
Na ukiigundua hiyo siri na ukaamua kuifata basi hakuna kwengine itakapo kupeleka ila kwa Mwenye enzi Mungu wako, Sisemi habari za harufu wengine mkanifahamu vyengine na kuanza kunusa mabaibui ya watu na kanga zao, atanaswa mtu kibao mie(Simo) Lazima ujue dhumuni na kusudio la harufu ilokusudiwa, Na hiyo harufu imetumika kama alama na ukiifata hupotei, lakini vipi utaijua harufu wakati Ua lenyewe hulijui, basi kama ushafahamu maana ya harufu ifate ukapate chakula na kinywaji cha
خِتَـٰمُهُ ۥ مِسۡكٌ۬ۚ
Mwisho wake(kinaleta harufu ya)Misk,
وَفِى ذَٲلِكَ فَلۡيَتَنَافَسِ ٱلۡمُتَنَـٰفِسُ
"(Basi) na katika (kuyapata) haya washindane wenye kushindana", na kushindana kwenyewe ni kuipata hiyo harufu inayo kujulisha mambo mema ili uyafanye, na ukiinusa hiyo harufu kweli kweli basi huokoki tena, daima utanasa kwenye (Ulimbo) wa harufu na kwa njia hiyo tunapata siri iliyomo kwenye harufu na nguvu ya harufu hii ilofanya mpaka watu wakavunja kuta za watu, mpaka hii leo harufu imebaki inawashangaza wengi, wapi inatokezea na wapi inakwendea, na huko inapokwenda na sisi tutafika, na kwanini hassa inatuvutia, na ukitizama kila mtu ana hamu ya kuvunja huo Ukuta apate hiyo harufu lakini si kitu chenye kupatikana kwa urahisi, ndio maana tukaambiwa washindane wenye kushindana kwa ajili ya hayo mambo ya Akhera.
Sasa kwanini Mvunjaji akavunja Ukuta wa watu kwa harufu ya chakula kitamu?, Inaonesha Mvunjaji lazima aliwahi kukionja au kukila chakula kitamu ndio maana akaijua harufu yake.
Endelea Part 3
No comments:
Post a Comment