Sunday, October 27, 2013

MAJINA YA MWENYE ENZI MUNGU(ALLAH)PART 1

Asalaam Aleiykum,

Tunaingia katika Darsa ya mzizi wa (Tawhid), Tunagusa nguzo nzima ya jengo la Dini, Tunakamata kitu muhimu sana na kama wewe utakua makini wa kufatilia na kufahamu darsa hii utatoka katika Bahari hii ya (Tawhid)huku umebeba Lulu na wala sio Chaza mwenyewe, Kwanza kabisa napenda kufahamisha hichi tunachokisoma ndio msingi mzima wa hiyo Sala unayosali, Makusudio yote ya Sala nzima yapo hapa. Kwa hiyo ukishindwa kuifahamu Darsa hii utakua umekosa kitu Adhimu sana, na vilevile ukifahamu basi usiwe mchoyo mwambie mwenzio au mfahamishe ili na yeye apate faida atakapo simamisha Sala awe na ufunuo fulani kwa ajili ya Mollah wake, kutokana na hali hiyo napenda uelewe huyo unompa taarifa hizi kila akizidi kukurubia kwa Mollah wake na wewe ukawa ndio sababu basi anazidi kukusukuma kwa darja na ujira mbele ya Mollah wako.
Katika Darsa hizi Inshaa Allah nitajaribu kuchukua majina matatu manne ili kukuonesha njia ili uifate na hayo mengine yalobakia ukayatafute zaidi, Kwa hiyo kila wiki tutakua tunalisoma jina moja na leo tunaanza Darsa hii na Jina la Allah, Katika darsa hii tunakaribishwa na aya 180 iliyomo kwenye sura ya Al-AAraf inayosema "وَلِلَّهِ ٱلۡأَسۡمَآءُ ٱلۡحُسۡنَىٰ فَٱدۡعُوهُ بِہَا‌ۖ"
"Na Mwenye enzi Mungu ana majina mazuri muombeni (Kwa)hayo"(Na mpaka mwisho wa aya inapomalizikia)
Katika hiyo aya yametajwa mambo mawili inatupasa tuyazingatie nayo la mwanzo Uzuri na la pili Ombeni, ukitumia viwili hivyo wewe mwenyewe utakua unaishi ndani ya huo uzuri ulokusudiwa, kutaka kulijua hilo kwanza tuiulize hiyo Sala, Wewe ni kitu gani, Nini Sala?.
Sala ni maombi Maalum unayopeleka kwa Mollah wako ukitumia hayo majina ya Mwenye enzi Mungu, Bila ya kutumia majina hayo utakua bado hujaitekeleza hiyo Sala, Utafanya Rukuu na Sijda lakini itakua bure mpaka upate jina zuri la kuweza kutumia katika vitendo hivyo. Na hapo ndio unakutana na majina 99 yenye (Kushubihisha)sifa za Mwenye enzi Mungu, Nimesema sifa ili usije ukaingia dhana ya kufikiri hivi ndivo alivo na haya ndio majina yake utakua umeingia hasarani, Mwenye enzi Mungu hana jina, Ila kwa kuwa anazungumza na wewe kwa kutumia lugha na kakufundisha kwa kutumia majina, basi hapana budi upewe sifa hizi nzuri(za mfano) Na imekua uzuri majina yenyewe kuwa 99, kutokana na tabia za viumbe tunajiuliza kwanini ikawa 99, lazima hesabu ikae sawa iwepo la 100, na hilo ndio lengo la kuwepo 99 ili ufanye jitihada kulifikia hilo moja ambalo halitajiki, halisomeki, halina lugha, halina mfano, na hilo ndilo lenye kuyakinisha uwepo wake Subhanna, Hilo halina(Shubiha) kama yalivyo hayo 99, huwezi kutoa mfano abadan.
Huwezi kulitamka, ila utakachoweza kufanya kutumia hayo majina 99 yakupeleke kwenye hilo moja, Na ambalo la karibu kabisa ni hili la (Allah) kama ilivotajwa katika sura ya (Ikhlas)قُلۡ هُوَ ٱللَّهُ أَحَدٌ .
"Mwenye enzi Mungu ni Mmoja" hapo limetumika neno Allah na Mmoja kwa sentensi moja kuonesha mambo mawili, ili usije ukaanza kufikiri labda yuko vile au yuko hivi, Yeye katika Ufalme wake hana Mshirika. Endelea Part 2


No comments:

Post a Comment