Sunday, February 9, 2014

KUFA HUKU UMEFURAHI PART 3

Asalaam Aleiykum,

ٱرۡجِعِىٓ إِلَىٰ رَبِّكِ رَاضِيَةً۬ مَّرۡضِيَّةً۬
Rejea kwa Mollah wako Mlezi umeridhika, Na Umemridhisha,
Vipi utaridhika, utaridhika pale utakapokua umeshajisafisha kikamilifu, vipi utajisafisha kikamilifu, inabidi uende ndani kwanza kujutia moja baada ya jengine yale uloyafanya, na utake Maghfira(Msamaha)kwa kila kosa ulolitenda, yale unoweza kuyasawazisha, basi yasawazishe, na yale usoweza basi egemea kwa Mollah wako kwa maombi ya msamaha na Ibada za kila wakati na huko ndiko kumridhisha, na ukifanya hivyo sasa utakua tayari wewe kurejea kwa Mollah wako kwa Usalama na bila ya shaka yoyote.
فَأَمَّآ إِن كَانَ مِنَ ٱلۡمُقَرَّبِينَ
Basi ikiwa huyo (Anofariki)ni miongoni walokaribishwa(Na Mollah wao). Basi hapo furaha tupu, Roho inatoka huku unahadithia kama kisa cha mzee wetu huyu wapili ambaye yeye wakati wa kifo chake alikua yumacho, na hakuna kifo kizuri kama hicho, inaonesha umeridhika kwenda kukutana na Mollah wako, Huyu yeye alikua anakufa huku anaona Roho yake inavotolewa, akawa anahadithia bila ya machungu wala woga, na wala hakuchagua kufa huku kalala, au kufa huku kazimia, yeye aliamua kufa huku anahadithia Roho inavotolewa, akisema nini? "Hao wameanza kunitoa kwenye kidole, wananitoa taratibu sasa washafika miguuni sina hisia tena, akasema sasa wanapanda kidogo kidogo sehemu ya kiunoni sina nguvu tena, akaendelea kusema wamefikia kwenye mbavu wanaivuta Roho taratibu, akasema sasa wacheni nikuageni wanakaribia kwenye moyo, nahisi watakapofika kwenye ulimi nitashindwa kuhadithia, akamwambia mwanawe nipe mkono nikuage kabla nguvu hazijaniishia kabisa, Mwisho akasema hao wanaipandisha mabegani, akatizama juu kimya, ikisha hayo macho yake yakabiruka na kuondoka katika Ulimwengu huu.
فَرَوۡحٌ۬ وَرَيۡحَانٌ۬ وَجَنَّتُ نَعِيمٍ۬
Basi ni Raha(ilioje)na Manukato na mabustani yenye neema.
Hicho ndio kifo cha Shahada unakufa hakuna machungu wala woga, hakuna kuteseka wala vitisho na cha zaidi unahadithia mambo yanavotokea, Wanayapataje haya hao wanofurahi katika vifo vyao(Usije ukaona furaha wanapiga makofi)kusudio lake wameridhika, ni bora waihame Dunia waende kwa Mollah wao, na ukitamani kurudi kwa Mollah wako ni furaha kubwa Mwanaadamu huwezi kuilinganisha na jambo lolote.
Sasa nini ufanye ukipate kifo hiki?
Unatakiwa uwe Mtu mwema sana, Uwe Mcha Mungu mwenye kuyatafuta mapenzi ya Mollah wako kikweli kweli,unatakiwa uanze kubadilika sasa hivi, Na kubadilika kwenyewe ni huko kujiuliza hili Swali?
Wapi nimetokea? Na nini nilifanya ili kuibebesha Roho yangu mizigo hii nilonayo. Wapi ninapokwenda na nini itakua khatima yangu? siku yangu ya kutolewa Roho, zikikujia hisia hizo anguka kwa Mollah wako na umuombe "Ewe Mollah yabadilishe mabaya yangu kuwa mema"na hayawezi kubadilika mpaka uonekane kweli sasa huna haja ya Ulimwengu huu, nikimaanisha chochote kile unamwachia Mollah wako ndie awe muamuzi na ukifikia daraja hiyo unakua (Non-Attachment) hapo unaishi katika maisha ya kutulia, kila kitu umekiridhia, Mauti yakija sawa, maradhi yakija sawa, mvua ikinyesha kwako sawa, jua likitoka kwako sawa, unakua ni mwenye kumtegemea Mollah wako nakuridhia kila alokupangia, ndio hata wakati wa kufa kwako unakua na furaha unajua sasa wakati umefika wa mimi kwenda kwa Kipenzi Mollah wangu, na kama nani mwenye  kuhamaki kukutana na kipenzi chake, Usiwe na Woga na hamaki za  kukataa kwenda kukutana na mpenzi mollah wako.
Na  Fahamu kumbe Maisha yameumbwa na kifo kimeumbwa, vyote ni njia lazima nipite, lazima niridhie ni mambo katika jambo la uhai.
Mollah wetu tujaalie mwisho mwema. Amin.

No comments:

Post a Comment