Sunday, June 14, 2015

KARIBU RAMADHANI PART 1

Asalaam Aleiykum

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umewasili hutopenda nikakupa kitu kipya ili ukitumie kwenye Mwezi huu upate kuiona tafauti kwenye Funga yako, Hutaki nikupe siri ya (Mawalii) wanavoishi katika Mwezi huu, basi kama unataka Fatilia Darsa hii ili ukifunga Mwaka huu uwe umeipata (Saum)yako kwa Mtazamo Mwengine kabisa.
Kwa Kukufahamisha hayo, nia yangu ni kukutaka uitizame Ramadhani kwa mtizamo wa kila Pembe. Tunaishi zama za (Google) kila mtu anataka aitizame Ramadhani kwa upande wake, kama  vile unavotizamwa mwezi wa muandamo, Na mimi ntaendelea kukuonesha pembe hizi mpaka pale utakapo ipata Ramadhani kwa ukamilifu, kwa sababu sasa hivi umegawika mapande mawili,unaweza ukaipata kwa maana, na kuna wengine wanakosa maana wanapata kwa vitendo, kwa hiyo kwenye Ramadhan lazima viwili hivi vikutane, lazima ufunge kwa Maana na vitendo, ntakuonesha vipi inafanyika.
Kufahamu kwa ufasaha wacha tuanze Darsa yetu kwa kuchemsha(Akili)sio(Bongo). Napenda kukujulisha tafauti ya Wanafunzi(Student's)na(Disciple's)Wafuasi, Wanafunzi wanaweza kuwa wengi wanakuja wanasoma wanakusanya (Information) ikisha wanakwenda zao, Wala hawakumbuki Shule(School) au Walimu wao, Kwa kuwa hawakumbuki hata akipita njiani mara chache sana kumsalimia Mwalimu. Lakini Mfuasi yeye anakua karibu na Maalim, anamshiba Sheikh wake, anakaa nae kwa karibu zaidi na mahusiano yao yanakua ya (Communion) hayakatiki ila kwa kupatikana sababu Maalum,  Anapata Mfuasi huyo mafundisho, anafundishwa mambo, anazijua kanuni ndio maana neno (Discipline) limetokana na (Disciple)Nidhamu, kwa hiyo unapoitwa Mwanafunzi jijue wewe nani, na unapoitwa Mfuasi ujijue cheo chako kikoje(Tafauti yake mmoja anasomeshwa na mwengine anafundishwa). Hayo ni ya Mwanafunzi na Mfuasi, sasa nini tafauti unapoitwa Muislam na unapoitwa Muumin.
Endelea part 2

KARIBU RAMADHANI PART 2

Asalaam Aleiykum

Ukiitwa Muislam unakua yule Mtu kakubali kusilimu, yuko tayari ku(Surrender) bado anafanya hayo mazoezi ya kua Muumin, Bado kabakia kwenye Kichwa anatawaliwa na (Mind)Akili. Lakini unapoitwa Muumin ina maana ushaingia daraja nyengine, au kwa maana nyengine ushateremka moyoni, (Kwa sababu moyo ndio wenye kuamini), Na Moyo unatawaliwa na nini?, Moyo unatawaliwa na Mapenzi tu, hakuna chengine, Na mapenzi yakikaa moyoni basi mabaya yanatoweka, na Mabaya yakitoweka unakua ni Mwenye kumpenda Mollah (automatic) na Hiyo ndio (Taqwa).
Sasa kama Muumin wa kweli umefika wakati Mwenye Kuumiliki huo Moyo anakwita.

يَـٰٓأَيُّهَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ كُتِبَ عَلَيۡڪُمُ ٱلصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى ٱلَّذِينَ مِن قَبۡلِڪُمۡ لَعَلَّكُمۡ تَتَّقُونَ 
Enyi Mloamini Mmeamrishwa kufunga(Saum)kama walivoamrishwa waliokua kabla yenu ili mpate kumcha Mungu.
Ukiangalia kwa undani Maneno kwenye hiyo aya yana sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni ile ya kufunga, hapa ni lazima ifahamike maana ya kufunga kama nilivyo sema mwanzo ili upate kuipata hiyo Ramadhani, Na sehemu hiyo ya pili ni hiyo ya vitendo(Discipiline) maalum ya kuweza kuipata hiyo (Taqwa) Na ukipata hiyo funga ndio unaweza kumcha Mungu, kama hujachanganya viwili hivyo basi itakua unapata funga lakini hupati Ucha Mungu ambao ndio sababu yenyewe ya wewe kufunga.
Sasa hebu tuanze na maana ya Funga(Saum)Nimekwambia mwanzoni ntakujulisha vipi Marafiki wa Mwenye enzi Mungu (Mawalii) wanavo funga. Nini Funga(Saum)? Nimeyasema katika darsa za nyuma, na leo nafafanua zaidi ili upate kujua kitu kwa undani, twende (Deep) kwenye (Saum) tujue dhumuni la hii Funga.
Soma kwa Makini ukifunga mwaka huu uwe umepata mabadiliko ya ukamilifu katika funga yako. Ulipoitwa Muumin umeitwa (Personal) unatakiwa ufunge, sasa kufunga kuna daraja tatu, ntazitaja daraja hizi na kukuonesha wapi mfungaji anatakiwa aishi katika daraja hizo.
Daraja ya Mwanzo ya Funga ni ile ya Mwili(Body)(Wengi wanaishia hapa)unachukua uamuzi kuwa wewe mwili wangu kwa siku ya leo hutopata chakula, Mwili una kawaida ukifika wakati wake unadai chakula, mfungaji unasema najua huu wakati wako lakini leo siwezi kutekeleza ombi lako hili utabidi usubiri mpaka magharibi.
Daraja ya pili ya Funga ni ile ya (Akili), na hii ndio ngumu kwa sababu (Brain) ina nguvu, kwa hiyo unaiambia Akili najua unatamani senema, kutizama maasi, kucheza bao, mazungumzo ya siasa na mipira, kusema watu na uongo, lakini unaiambia Akili mwaka huu mimi nafunga siwezi kutekeleza amri zako kabisa, ukiweza kuvimiliki viwili hivyo, nini kinatokea?
Endelea part 3

KARIBU RAMADHANI PART 3

Asalaam Aleiykum

Kwa mara ya mwanzo unakwenda (Beyond) unaishi katika hicho kinachotakiwa kifanye nacho ni(Taqwa)(Hapo ndipo wanapofunga mawalii na wacha Mungu)Funga yako itakua nyengine kabisa, ukiweza ku(control) viwili vya mwanzo unabakia (Pure Being)Muumin, hapo sasa ndio unaupata uwezo wa kubadilisha Tabia kwenye haya masiku machache, Sasa kwanini ikawa Mchana ndio unatakiwa kufunga?.
Kwa sababu Mchana ndio wakati wa Shughuli za maisha na katika wakati huu ndio una kawaida ya kila tabia imo humo, ndio wakati wakumsahau Mollah wako na vyote ulivyoamrishwa, ni wakati wa pirikapirika za maisha, Mollah wetu katujua tuna makosa yasio idadi, Sasa ili tukumbuke turejee kwenye mapenzi aliyotuamrisha ya Kumuabudu yeye, kuwatizama maskin na mayatima na wasiojiweza, ndio katuletea Ramadhani, ili tupate kuifata hiyo nidhamu ya Ucha Mungu, asaa tunaweza kuendelea nayo tukaishi hivyo hata huu mwezi utakapomalizika, na hiyo ndio ile maana ya pili ya vitendo(Taqwa).
Sasa unatakiwa ufanye nini katika Ramadhani, ikiwa umepata hiyo daraja ya tatu unatakiwa ubadilishe Tabia zako zote za mwaka mzima, vipi utabadilisha, cha mwanzo ujizuie kula na kunywa(Body)ukishajizuia mambo hayo mawili, sasa chukua (Control) ya maisha yako ili upate kubadilika kivitendo, hilo ndio la pili, acha tabia ya uchoyo Futarisha wenzio wasokua na uwezo, Ulikua huendi Msikitini sana sasa fanya hima uwepo kila wakati, Acha mambo ya kuangalia TV japo kwa Mwezi huu tu, acha kusikiliza muziki, wasamehe walokukosea, ondosha maskhara, usiseme uongo, acha kutukana,Usichukue Rushwa,usifanye biashara ya haramu,jiepushe na mikusanyiko ya jinsia tafauti, jizuie na matamanio, ondosha chuki moyoni, jilinde na kila baya na lilo haramu.
Ukiweza kufanya hivyo mchana kutwa basi wewe utakua umefunga, Na zinapofika nyakati za usiku unatakiwa uilinde Funga yako kwa mambo ya kheri na Ibada. Ukiweza kuyafanya hayo katika kumi la mwanzo uka (Master)Nidhamu hiyo utayaona mabadiliko makubwa makubwa katika funga yako ya mwaka huu.
Sasa ikiwa umedumu katika hali hiyo ndio kwa mara ya mwanzo utaona unaanza kushukiwa na Rehma za Taqwa. Mollah wako atakupa zawadi unayostahiki ya Ucha Mungu, utapewa kitu ambacho utakigundua wewe mwenyewe kwa furaha ulonayo, Ndani ya Ramadhani utaanza kupenda Ibada, Mawazo yako yote yatakua kwa ajili ya Mollah wako, zitaanza kukushukia huruma na mapenzi ya kuwapenda viumbe wenzako.
Utakua Mwenye kusikia Raha na saum yako, utakua ukitamani saa ngapi kukuche ili upate kufunga, kama una uwezo utaanza kutoa ili ufurahi na wenzio,itakua kila saa na dakika umo furahani ndani ya mwezi huu, utakua huna wasiwasi na kukubaliwa funga yako, ukiwa katika hali hiyo ndio sasa utakua umemkaribisha mgeni, na Mgeni daima analeta zawadi, na safari hii unapata zawadi za Rehma na msamaha, na pia kuepushwa na Moto wa Jahannam.
Sasa ikiwa kila mwaka unampokea Mgeni huyu kwa desturi hiyo jee utakua na haja ya kuhuzunika wakati unaondoka kwenye Ulimwengu huu. Majibu unayo mwenyewe ikiwa utaitekeleza hiyo funga ya Ramadhani.

Friday, June 12, 2015

HAKI YA KUMUOMBEA DUA MAITI PART 1

Asalaam Aleiykum

Ipokee uisome darsa yangu ya leo iwe kama Wasia kutoka kwangu kuja kwako, Endapo utahisi hukubaliani na wasia huu basi niachie mwenyewe, na pindipo utakubaliana na wasia huu basi fanya hima uwaeleze na wengine wasije wakakosa Fadhila hii ya Dua ya Maiti, nitaeleza nini dhumuni la dua, Nitakujulisha kwanini tuombe Dua, halafu nitakupa maana ya kuomba Dua ya pamoja na sababu zake.
Ikisha ntakupa nguvu ya hoja ili na wewe ufanye uamuzi vipi utataka uombewe Dua au kumuombea Maiti wako, au utakhiyari watu wakutupe ikisha wende zao kama yanavofanyika mafundisho ya sasa hivi, Kwanini nikasema hivyo kwa sababu siku hizi mambo yamezidi, mpaka imefikia Dua marufuku, unakwenda Nyumba ya msiba unakuta watu wamejificha nyuma ya makochi kimya, hata kulia haifai, ukiuliza unaambiwa Ustaadh kasema Dua haifai, au omba kimya kimya, au omba mwenyewe, na wao wanaendelea na porojo, cha ajabu zaidi huyo Ustaadh hajaifadhi hata hadith kumi, wala hajui nini Ibada, nini Dini, ukimtizama unamuona hana isipokua katawaliwa na Kiburi, na yeye anajijua hajui chochote lakini vipi atakubali hajui wakati anadanganya wasojua.
Wanasema Maiti atajiombea Mwenyewe kwa Amali zake, na nyie mnaendelea na mazungumzo mpaka Maiti huyo anazikwa hakuna jambo la Dua, hapa ndipo tulipofikishana, Na kama hilo halitoshi Maiti huyo pia marufuku Kusaliwa Msikitini(Naeleza haya yanatokea hapa Uk) huko kwengine sina ujuzi nayo. Lakini cha kushangaza Msikiti wa Makka wakati wote tunaona Maiti wanasaliwa, Na jambo jengine ambalo linafanyiwa kazi sasa ni hili la kuombewa Dua Maiti makaburini linaondoshwa kidogo kidogo.
Basi kabla halijaondoshwa kabisa nimeona nikupeni baadhi ya faida zake labda zitakufanyeni mzinduke usingizini mkatae mchezo huu wa kutupwa Makaburini na watu wakashika njia na kwenda zao.
Ntakupa hoja halafu wewe una khiyari ukibaki katika kundi la wanotupana au la wale wano ombeana dua, utakubali au kukataa Maiti yako aombewe Dua. Na utakapo pata msiba bora utangaze toka mwanzo mimi nataka dua, asotaka ende zake, na wala usiogope watu wa kustiri Maiti yako wako wengi na hilo si tatizo kabisa.
Basi kwanza tupate taaluma ya Roho ya Mwanaadamu inapotoka kwenye Kiwiliwili, kwanza inakua (Shock) kubwa kwako kutenganishwa na Kiwiliwili chako(Body), Huo Mwili umeishi nao takriban kwa Miaka 50 au 60 leo unauona umelala pale umetengana nao, kumbuka safari yako ya (Barzak) haianzi hapo hapo, unasubiri mpaka khitimisho la Mwili wako utakapo zikwa, kwa kuwa umekua (attach) na hiyo body kwa miaka yote uloishi, ndio maana wale wenye kupata (Near death Experience) wakirudi kwenye (Body) wanahadithia nilikua niko juu nakutizameni mlivokua mnajaribu kuni (Revive)shughulikia mwanzo mpaka mwisho.
Kwa hiyo napenda uelewe Roho ni yenye kubaki mpaka yafanyike mahojiano huko kwenye Kaburi, napenda ufahamu wako Malaika wenye kuitoa Roho, wako wenye kuhoji na wako wenye kukuchukua kwenda safari ya Barzak ulikopangiwa. Katika kipindi hichi ndio tumehimizwa kuwaombea kwa wingi Maiti zetu, Na wala hakuna hata sehemu moja hata ya hadith dhaifu ilokataza jambo la Dua, au kusema ombeni lakini kimya kimya, haya yote ni mambo mepya yenye kupandikizwa katika Dini hii na watu wa Karne hii tulonayo.
Cha kusikitisha zaidi watu ni wenye kukubali hawajui kitu maskini, na wala hawaulizi yametokea wapi na kwa ushahidi gani?, ila kila Mtu anapanda gari ya kukaa kimya anaambiwa usimsalie au kumuombea Maiti yako na yeye anakubali, ikisha anajuta kwenye maisha yake, kwanini alikubali, sasa tunataka kukufahamisha hakuna kosa katika kuomba Dua, na Dua ilianza lini?.
Endelea Part 2

HAKI YA KUMUOMBEA DUA MAITI PART 2

Asalaam Aleiykum

Sasa Dua tumefundishwa na nani? Dua tumefundishwa na Mwenyewe Mwenye Enzi Mungu alipompelekea Baba yetu Nabii Adam a.s maneno ya kusema katika Toba, sio kukaa kimya, maneno ambayo na wewe unayasema kumuombea Maiti wako vipi utakua unafanya makosa?, Halafu akatupa mfano mwengine wa dua ya Milele ambayo tunaisoma kila siku, Sura ya Ahzab aya ya 56.
"إِنَّ ٱللَّهَ وَمَلَـٰٓٮِٕڪَتَهُ ۥ يُصَلُّونَ عَلَى ٱلنَّبِىِّۚ يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ صَلُّواْ عَلَيۡهِ وَسَلِّمُواْ تَسۡلِيمًا"
Hakika Mwenye enzi Mungu na Malaika wake wanamsalia mtume, Basi enyi Mloamini Msalieni Mtume na Muombeeni amani.
Iliposhuka aya hii Masahaba walishtuka na kuuliza vipi Mwenye enzi Mungu anamsalia kiumbe chake, wakaambiwa hakika hiyo ilokusudiwa hapo ni Rehma, Na Sala ya Malaika ni Maghfira, na Sala yenu nyinyi Waumini kwake ni Dua ya Rehma na Amani, na hii tunaifanya kila siku na yenye kudumu milele.
Sasa la kutizamwa mwanzo katika Darsa hii jee na sisi tunapata hizo Rehma kutoka kwa Mollah wetu, jawabu ndio tunapata, Jee tunapata kuombewa Maghfira na Malaika jawabu ndio Quraan aya ya 5 sura ya Ash-Shura.
"تَكَادُ ٱلسَّمَـٰوَٲتُ يَتَفَطَّرۡنَ مِن فَوۡقِهِنَّ‌ۚ وَٱلۡمَلَـٰٓٮِٕكَةُ يُسَبِّحُونَ بِحَمۡدِ رَبِّہِمۡ وَيَسۡتَغۡفِرُونَ لِمَن فِى ٱلۡأَرۡضِ‌ۗ أَلَآ إِنَّ ٱللَّهَ هُوَ ٱلۡغَفُورُ ٱلرَّحِيمُ "
Zinakaribia Mbingu kupasuka juu yao,(Kwa kumuogopa Mollah) Na Malaika wanamtukuza Mollah wao na kumshukuru, na kuwaombea Msamaha(Maghfira) walio katika Ardhi, Hakika Mwenye enzi Mungu ni Mwingi wa Msamaha na Mwenye Huruma.
Sasa kilichopunguzwa hapo ni Dua yako na yangu, unaambiwa usimuombee mwenzio, (Wangekua na uwezo wangewaambia mpaka hawa Malaika wasituombee). Unajua kwanini imeanza kukatazwa siku hizi za karibuni, sababu kubwa kuna Dhehebu Fulani wanaomba Makaburini, kwa hiyo ikaamuliwa kwenye hili Dhehebu mnaloingia nyinyi bila ya kujijua sasa wasiombe makaburini au waombe kimya kimya, lakini dhamira iondoshwe watu kuomba Makaburini, kwa dhana yakua mtakuja kuabudu hayo Makaburi, ndio sasa ikaanza kampeni muachishwe kuombea Maiti au kama mtakua wabishi basi kila mmoja wenu akae na kuomba kimya.
Sasa Bwana Mtume s.a.w Akiwaombea Masahaba zake walipokua wanakufa kwa sauti, jawabu ndio, sio kuwaombea tu alikua akenda na kusali sala ya Maiti hapo hapo Makaburini na kuomba dua na masahaba wakaitikia Aamin. 
Sasa nini faida ya kuombewa kwenye Makaburi (Open Space) wa kwanza kabisa tumuulize Nabii Nuhu a.s nini Faida yake, Quraan As-Saffat aya ya 75 na 76.
"وَلَقَدۡ نَادَٮٰنَا نُوحٌ۬ فَلَنِعۡمَ ٱلۡمُجِيبُونَ "
Na Kwa yakini Nuhu alitwita(Katuomba Tumnusuru)Basi ni waitikiaji wema sisi.
" وَنَجَّيۡنَـٰهُ وَأَهۡلَهُ ۥ مِنَ ٱلۡكَرۡبِ ٱلۡعَظِيمِ "
Na tulimuokoa yeye na watu wake katika msiba mkubwa(Mafuriko yalogharikisha kila kitu).
Nuhu aliita kwenye (Open space) Sasa nini habari yetu sisi tukisimama Makaburini, Wakapatikana Waumin wakafata maneno ya Bwana Mtume s.a.w Muombeeni Maiti yenu kwa Ikhlas. vipi mtafanya hiyo Ikhlas mkisoma kimya kimya, wakati ikiwa hiyo Sala huipati utapata Dua kweli, (Jamani msicheze na Maiti za watu mnachukua majukumu makubwa). Sasa tunawafanyia Ikhlas vipi, kama alivofanya Bwana Mtume s.a.w Yeye anasoma Masahaba wanaitikia, na sisi Mmoja wetu anasoma na wengine tunaitikia, nini kinapatikana katika wakati ule, itizame Ikhlas inavopatikana msomaji kafungika anasoma, wakati unasoma huwezi kuwa unafikiri kitu chengine(Brain) haiwezi kuchukua mambo mawili, na wale wanoitikia wanakua wameingia kwenye (Mode) ya usikilizaji kwa hiyo wote wamefungika wanapeleka Dua yao kwa Ikhlas huku wakiitikia Aamin.
"Ndio Sasa Msomaji anasema Mollah wetu Kiumbe chako Dhaifu sasa tumesha kikabidhi kwenye ardhi yako, kiko mbele yako, Weye ni Mwenye Kujua Kheri na Shari zake, na katika hilo sisi hatuna maamuzi isipokua kumuombea Maiti wetu huyu umsamehe Makosa yake, Mnusuru na Moto wa Jahannam, Mwepushie adhabu za Kaburi, Ewe Mollah wetu Mwenzetu huyu ni mchache wa Ibada, na Mwingi wa Madhanbi, alikua dhaifu wa Dua lakini Mwoga wa Ufalme wako, basi Mollah wetu kwa kuwa wewe ni Mwenye kuwapenda Viumbe vyako, Umempa Rehma hii ya sisi kumuombea Mwenzetu huyu basi msamehe makosa yake, mkusanye na waja wema, ikisha umpe yalo mazuri katika ufalme wako". Kwa utajo wa maneno hayo Watu, Miti, ndege wanaitikia Amin.
Sasa Muujiza gani unatokea katika Dua ya Makaburini? utizame muujiza unaopatikana katika hiyo Dua mnayoomba, na ukisha kuijua una khiyari utamuombea Maiti wako au utamtupa asipate fadhila hizi, kinachotokea hapo(Nature)Ulimwengu unarekodi Dua hiyo, Kwa hiyo maombi yako yanasikika Daima(Hiyo ndio Hekima waloigundua waombaji kwa sauti Makaburini na kusoma Quraan) Wanasema Wanasayansi katika Ulimwengu huu sauti inadumu milele, haipotei kabisa,(Jee wewe hutaki kila siku linasikika jina lako unaombewa usamehewe) kama hutaki basi bakia na kiburi chako utaona faida yake.
Haiwi (Hitler) kazungumza miaka 50 ilopita na kurekodiwa kwenye karatasi tunamsikia hadi leo, nini habari yetu sisi kwa Maiti mwenye kupata dua za kheri kwenye Ulimwengu huu, Quraan pia imethibitisha hilo kwa kusema katika sura ya Maryam aya ya 80.
"وَنَرِثُهُ ۥ مَا يَقُولُ وَيَأۡتِينَا فَرۡدً۬ا"
Na tutamrithi anayoyasema, Na atatujia peke yake.
Endelea part 3


HAKI YA KUMUOMBEA DUA MAITI PART 3

Asalaam Aleiykum

Nini Kuomba?
Kuomba ni Ibada, Kwa sababu ndani ya kuomba kuna unyenyekevu(Humbleness)kuomba maana yake sasa sina uwezo tena, njia zote nishamaliza(Kiburi kishanitoka)nimeishiwa na ujuzi wote, sasa nategemea Rehma yako pekee ndio inivue kwenye matatizo yote.
Nini Kuombewa?
Kuombewa nikuwa mimi muombaji sasa sina uwezo tena wa hata kuomba, uwezo huo nimeondoshewa kwenye enzi yako, zilobaki ni Rehma zako ulizowapa viumbe kuniombea kwa niaba yangu, Na kwa Baraka zako ili uweze kunisamehe.
Hizo ndio baadhi ya ufafanuzi wa Dua mnazokatazwa msiombe, na hao wanokukatazeni walifikia hadi kutaka kuvunja Alkabba mwaka 1979 wakishirikiana na Mtu Mmoja aitwaye (Juhayman Al Otaibi) akishirikiana na Masheikh wake ambao hatimaye walifukuzwa Makka, basi ulizeni habari zao, tafuteni Akida zao na Tawhid wanayofata ikisha ndio muwafate , msisimame tu mkawa mnafata mambo hamyajui mwanzo wake wala mwisho wake.
Sasa jee kwani inaruhusiwa kuomba Dua na kusoma Quraan kwenye Makaburi.
Wacha tuwaulize Wanazuoni watupe (Fatwa)zao. Wanaanza kutufahamisha kwanza tusome sura ya Hashr aya ya 10,
"وَٱلَّذِينَ جَآءُو مِنۢ بَعۡدِهِمۡ يَقُولُونَ رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لَنَا وَلِإِخۡوَٲنِنَا ٱلَّذِينَ سَبَقُونَا بِٱلۡإِيمَـٰنِ وَلَا تَجۡعَلۡ فِى قُلُوبِنَا غِلاًّ۬ لِّلَّذِينَ ءَامَنُواْ رَبَّنَآ إِنَّكَ رَءُوفٌ۬ رَّحِيمٌ "
Na Wale waliokuja baada yao Wanasema Mollah wetu tusamehe sisi na ndugu zetu waliotangulia (Kufa) katika Uislam, Wala usijaalie katika nyoyo zetu undani kuwafanyia Waislam (Wenzetu)Mollah wetu hakika wewe ni mpole sana, na Mwenye Rehma. 
Basi Wewe endelea na jeuri za kukataa kuombewa uone kama hizo Ibada zako zinatosha, lete kiburi mbele ya Mollah wako kuwa huna haja ya wenzio kukuombea.
Aya hiyo inaonesha kuruhusiwa kwa kuombea wenzetu na jambo hilo halina mushkeli, kwani lingekua linakatazwa isingetajwa kuwaombea walotangulia mbele ya haki.Na kutajwa Mollah kuwa mpole ni Mwenye kusamehe kwa Rehma zake.
Na Bwana Mtume s.a.w kasema wasomeeni Maiti zenu Yaseen imetajwa habari  hii katika Sunan ibn Majah, kitabu Janaiz Hadith 1438.
Ibn Hibban kasema Hadith hii (sahih Hasan).
Imam Nawawi katika kitabu chake(Minhaj al Talibin) kasema yoyote yule atodhuru makaburi basi asome Quraan kidogo na amuombee dua Marehemu.
Ibn Taimiyya katika kitabu chake cha Mujmu al Fatawa pia kaandika Marehemu anapata ujira wa matendo yanayofanywa kwa niaba yake.

وذكر الخلال عن الشعبي قال كانت الأنصار إذا مات لهم الميت اختلفوا إلى قبره يقرءون عنده القرآن 
Al Shubi kasema:Ansar, Walikua yoyote yule akifa miongoni mwao, wanakwenda kwenye Kaburi lake na kusoma Quraan.
Maneno haya yamo kwenye Kitabu cha Ibn Qayyim (Kitabu Ruh-Medani page 18.
Iko mifano na Hadith nyingi tu tena kwenye vitabu vingi yakua Waislam wanaruhusiwa kuomba Dua iwe Kwenye Nyumba, Msikitini au Makaburini halijakatazwa kabisa jambo hili.
Anahadithia Abd al-Haq"Ibn al-Kharrat al-Ishbili"Walii Mmoja"akamjia kwenye Ndoto na kusema kaka yangu alipokufa wakati kashafukiwa alikua anakuja Jitu Kubwa na Mwenge wa moto, lau isingekua kwa Dua mlokua mnaniombea basi ningeangamia.
Na Masheikh wengi wametaja katika vitabu vya kila aina basi vyote hivi viwe havifai, ila kifae kimoja tu, kweli hii ni sawa hebu jiulizeni kabla ya kufata jambo. Na Nukuu vitabu ili na nyinyi mkatafute myaone kwa macho yenu.
Nawawi kataja habari hii (Kitab al-adhkar.P229).
Shawkani katika (Tahfat al-adhakirin).
Abu Daud katika Sunan(Janaiz)
Al-Nasai katika (Amal yawm wa layla)
Ibn Hibban katika Sahih(Ihsan) na wengi wa Masheikh wasokua na Idadi.
Namalizia kwa Maneno ya Mwanasayansi Mmoja Maarufu aliulizwa nini Imani yako kuhusu kuwapo kwa Mwenye Enzi Mungu akajibu "Ni Bora niamini yupo kuliko kutoamini" Sababu nikija Kufa akiwepo nitakua nimeshinda, na hata kama hayupo basi pia nitakua nimeshinda, kwa kuwa haitonifika dhara yoyote. Sasa na wewe una uamuzi wako bora usomewe au usisomewe, nani atakula hasara, walobaki Duniani au wewe ulotangulia mbele ya haki.



Sunday, June 7, 2015

TAWI LA TAQWA PART 1

Asalaam Aleiykum

Taqwa ni Mti Mkubwa wenye jina la Mapenzi, Kwenye Mti huu kuna matawi mengi yenye kutoa matunda ya kila aina, leo hii mimi nimekuchumia Tunda la (Zaka) ili upate kuonja Ufahamu wake.
Nisiseme Mti watu wakataka kufunga safari ya kuutafuta Mti huu wakidhani labda uko Makka, kule utakutana na Mitende mitupu, Mti niloukusudia hapa ni ule unao ota ndani ya nafsi yako, mimi hapa nimetumia mfano ili uweze kunifahamu nini hiyo Taqwa ya (Zaka).
Basi kwanza wacha tujue tafauti usije ukavamia matawi ukawa hujui unachuma nini?, Watu wengi wanababaika kwenye mambo mawili haya baina ya Sadaka na Zaka. Unaingia kwenye Mwezi wa Ramadhani, Mwezi wenye kulea Roho na kufundisha mambo mazuri yenye faida na wewe hapa Ulimwenguni na kesho huko Akhera uendako kwenye safari ya ulazima.
Nini Sadaka?, Sadaka ni tendo la hiyari ambalo hulazimishwi, kiumbe ana uchaguzi kwa hilo, atoe au asitoe, lakini Zaka ni kitendo cha Amri ya maelekezo kutoka kwa Mollah wako, unatizamwa utaitekeleza au kuipinga, ukitekeleza Malipo yake hayana mfano, na ukiyapinga madhara yake pia makubwa ambayo wengi wetu hatuyatambui.
Zaka ziko za aina nyingi lakini kwa kuwa tunaingia katika Mwezi wa Ramadhani, Ni wajibu wangu kukumbusha zaka hii ambayo takribani wengi wetu tunaiweza, nayo ni zaka hii ya (Vitendo) wengi hatuna uwezo wa kutoa hiyo (Zaka) ya Mali, au ya Fedha, au ya Mazao, ili tusilalamike Mollah wetu katupa zaka ya nguvu za uwezo ili tuitekeleze.
ipi Zaka hiyo?
Endelea part.

TAWI LA TAQWA PART 2

Asalaam Aleiykum

Zaka yenyewe ni hii ilotajwa katika sura ya Muuminun aya ya (4)
"وَٱلَّذِينَ هُمۡ لِلزَّكَوٰةِ فَـٰعِلُونَ"
Na ambao (Nguzo ya)Zaka wanaitekeleza.
Hapo ni kufanya matendo ya Zaka, na hayo matendo yako mengi,na ikiwa Muislam ataishi katika matendo ya Zaka akawa hamshirikishi Mollah wake na kitu chochote basi hana sababu za kuadhibiwa kwa kuingia Motoni,lazima tukumbushane kwamba sadaka ni tendo la nje (Outer) na Zaka ni tendo la ndani (Inner) Wenzetu wengine wanafanya matendo kama haya lakini kwa kuwa hayana mashiko wanaita matendo hayo (Volunteer), Kwa hiyo Zaka ninayo izungumza leo ni ile Zaka ya matendo, Na huwezi kuifanya Zaka hii ya Matendo mpaka kwanza uwe karibu ya Mollah wako.
Itabidi ujitizame kwanza kama upo Karibu na Mwenye enzi Mungu, Na nini kipimo cha kuwapo karibu na Mollah wako ni (Humble) Unyenyekevu, na hilo kwa binaadamu wa kawaida sio jambo rahisi, Jitizame wewe kwanza nyumbani kwako unavotangaza ufalme, kila mtu mpaka mkeo lazima atetemeke juu yako, ndio maana utaona katika Ulimwengu wa sasa hivi utaona Mtu anawaibia Maskini Million mia, halafu anatangaza anawapa sadaka ya Million moja, Lakini kwenye Zaka ya vitendo unatakiwa uteremke kutoka wapi?. 

TAWI LA TAQWA PART 3

Asalaam Aleiykum

Unatakiwa uteremke kutoka kwenye kiti chako cha Ufalme wa Kiburi uje chini kunyenyekea, Sababu kwenye Ku(Surrender) Kiburi lazima kipotee, Sasa ufanye nini ili kupata matendo na vitendo hivi vya zaka, ambavyo ni bora zaidi hata kuishinda hiyo Sadaka, Unatakiwa ujihusishe kwenye shida na matatizo ya watu kwa njia ya huruma,pia kuhusika kibinafsi katika matendo ya kuwasaidia watu, kama vipi?Nenda katoe huduma zako za nguvu Kwenye nyumba za wazee, kwenye nyumba za yatima, kwenye Mahospital.
Ramadhani inakuja pita Majumbani uulize watu wanashida gani uwasaidie, katafute watu wazima uwasaidie matatizo yao, pengine watoto hawana baba au mama na kwao hakuna uwezo, basi watafutie njia za kuwakwamua ili watoke kwenye matatizo yao, hayo yote ni matendo ya Zaka uyafanyao, hata ukiwapa ushauri yakamuondoka Mtu matatizo kwenye Akili yake, basi wewe umeshatenda tendo la zaka ya vitendo, Husika kwenye Misiba yao, pita ukihimiza watu kwenye uadilifu, fanya jitihada ili walogombana wapatane, wasaidie walemavu na wasojiweza, shiriki katika kuwajengea watu makaazi, huku kaa ukijua vitendo vyote uvifanyavo ni Zaka, na fadhila za malipo ajuae ni yule mlipaji wa matendo hayo ambaye ndie Mollah wako mlezi alokupa nguvu hizo na hekima za kuyatekeleza hayo, sifa zote na shukurani anastahiki yeye pekee Mwenye uweza wa kila jambo.

Monday, June 1, 2015

KIKAO CHA MSIKITINI PART 1

Asalaam Aleiykum

Mwezi wa Ramadhani unakaribia, Mwezi ulo Mtukufu na kwa sababu hiyo na sisi inatubidi ndio uwe wakati muafaka wa kuanza mataarisho ya kuelekeza darsa zetu kwenye mwezi huu ambao ndio (Ustaadh wa kuzilea Roho zetu). Mwezi huu dhamiri yake kubwa ni kukumbusha kama yupo alokuumba na wewe unatakiwa uwe karibu nae.
Kutokana na sababu hiyo ndio ukaambiwa jizuie kula, kwani ukizuia kula kinatokea nini?, Unapo jizuia kula jambo la mwanzo lenye kutokezea unapata (Separation) tafauti baina yako na huo Mwili, siku zote ulikua hujui nini Mwili(Body), hebu Ramadhani hii jitizame, utaanza kujua nini njaa, miezi yote kumi na moja unakula hujui una njaa au umeshiba, unatia tumboni bajia, chauro, juice, keki, huangalii na wala hujui una njaa au umetamani, mara tangawizi, mara kahawa, (Ice cream) twende vyote vinaingia tumboni, lakini ukianza kufunga kwa mara ya mwanzo njaa inahudhuria, unaanza kupata mawasiliano na (Body)mwili wako, mwaka mzima hujawahi kushikwa na (Kiu) unaanza kujua nini kiu, kwa mara ya mwanzo unatamani (Juice) unatamani maji ya madafu, tumbo linaanza kunyonga, unajisikia uchovu. hayo ndio mawasiliano ya mwili yako ambayo unayapoteza mwaka mzima.
Na Dalili ya mwanzo utaona unaanza kuupenda mwili wako, kwenye njaa (hata tendo la ndoa) hutamani, hutaki mapenzi na mtu unajipenda mwenyewe, mpaka upate shibe ndio unajisahau na kuanza kupenda nje, (Maajabu makubwa yapo kwenye funga).
Lakini katika siku za kawaida mpaka ukucha ukuume ndio unashituka kumbe nina mwili(Body).Sasa ukiweza kujua hiyo (Separation)unapata kufahamu kumbe mimi na (Body) ni vitu viwili tafauti, ukiwa mtulivu ukaujua ukweli huo wa tafauti, ndio hapo inaanza hiyo funga ya Ramadhani.
Elewa kwamba hicho kilicho tafauti na mwili wako ndicho kinachotakiwa kufunga, ndicho kinachotakiwa kiwe karibu na Mollah wako, ndicho chenye kutarajiwa kufanya (taqwa), Usije kuona rahisi kwa kuwa nimehadithia, ukaona Ramadhani hii na mimi ntakipata, vizuri kujitahidi lakini weka mbele kukuponyoka kila mara kutokana na mazoea ya tabia yako, mara utakua umehamia kwenye njaa, mara kwenye fikira za mikungu ya ndizi, lakini usivunjike moyo jitahidi ukiweza kuishi nacho hata kwa nusu siku utaona raha ya funga yako.
Lakini kina masharti kitu hichi nacho usile sana, na hapo ndio matatizo yanapoanzia, kwani ukishiba tu unakipoteza ima kwa usingizi au usahaulivu, kwa hiyo unatakiwa ubakie kwenye hali ya katikati, ili uweze kuidhibiti hali hiyo, kwani ukiwa katika funga ya kweli ni vigumu kwako kutenda dhanmbi, uzito kwako kusengenya, huwezi kwenda kucheza bao na karata, hutaki hata kwenda barazani, sasa yote hayo ukisha yakataa nini kinafatia?, hapo ndipo unaambiwa nenda kwenye kikao cha Msikitini.
endelea part 2

KIKAO CHA MSIKITINI PART 2

Asalaam Aleiykum

Sasa unapata nafasi ya kujiuliza kwanini umeambiwa ukakae msikitini?.Na wapi umeambiwa maneno haya?.Quraan sura ya Baqarah aya ya 187 mwanzo mpaka mwisho wa aya na hapo unakutana na neno hili, وَلَا تُبَـٰشِرُوهُنَّ وَأَنتُمۡ عَـٰكِفُونَ فِى ٱلۡمَسَـٰجِدِ‌ۗ 
"Na hali (yakua) mnakaa itikafu(Devotion)Msikitini".
Ikiwa umefahamu kilichosemwa mwanzoni sasa unatakiwa ukakae msikitini ukilinde, kalinde (Saum) yako japo kwa siku moja, chukua japo likizo(off work)ili upate mawasiliano na Mollah wako kwa kukaa Msikitini, kwanini ikawa hivyo, kwa kuwa huu ni mwezi maalum wa viumbe kuwa karibu na Mollah wao, pia kukumbuka ulipotoka, kujua dhumuni la kuumbwa kwako, kuzungumza na Mollah wako,Kuwapenda viumbe wenzio kwa misaada ya hali(Dua) na Mali, vipi utayapata mambo hayo kakae Msikitini.
Miezi kumi na moja zinaingia fujo tupu Kichwani mwako, Siasa zimo humo, Nyimbo zinaishi humo ndani, humo kuna magonvi, umerundika visasi, kila kitu kichafu unatupa ndani ya nafsi yako, Sasa ikiwa (Body) Mwili unapona kwa ajili ya Funga ya Ramadhani, Basi na Akili (Mind) inatakiwa kupumzishwa ndio unaambiwa (Kakae Msikitini), sio kuanzisha Baraza Msikitini na vikao vya siasa na masikhara katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Vipi Kukaa huku?
Watu wengi wamekua na fikra tafauti na kikao hichi cha Msikitini, Kwa sababu kelele nyingi na mambo mengi yameingia Akilini, unaogopa kukaa kimya, ndio utaona unataka labda uvute uradi au ufanye mambo mengine, kikao hichi hakijataja hayo, wewe umeambiwa ukakae tu Msikitini, nini kitatokea ukiwa na Subira?. (Mfano)unaona ukikaa kimya unatizama mchezo wako kwenye TV ama taarifa ya habari, hufikiri kitu chochote chengine, na hali kama hiyo ndio unatakiwa ukae nayo Msikitini, ukiweza kufanya hivyo moja kwa moja na wewe utapata, au kukujia ile hali au daraja ya wale (Wanomkumbuka Mollah wao wakiwa wamesimama, au wamekaa, au kulala) na ukiipata hali hiyo wewe ushafuzu na ushaipata funga ya Ramadhani.
Aya haijasema ukadhikiri, wala kuvuta uradi, aya imekwambia kakae Msikitini (Just sit) Wafuasi wa Dini ya (Kikiristo) waliambiwa katika maandiko yao maneno mfano wa haya"(Kuwa Mtulivu na ujue mimi ni Mungu wako)"Wafasiri wakatafsiri kuwa mkimya ujue mimi ni Mungu wako, hapo wakafanya makosa makubwa sana, kwani ukimya siku zote unafatiwa na Makelele, na Binaadamu siku zote anaongozwa na utamaduni wake, ukichanganyika na Dini ndio unaona vipi unapata mseto wa kelele na kutupwa kwa Ibada, kwa sababu Binaadamu anaogopa kukaa kimya, ndio maana kaamua kuimba, kupiga miluzi, na firimbi, ngoma, ili iwe sehemu ya Ibada na kuondosha ukimya, lakini wangefasiri (Be still and know I'm your God) basi wangepata utulivu, na utulivu mwenzie harakati, kwa hiyo ukiambiwa tulia ina maana acha harakati, na kuacha harakati maana yake kaa kitako utulie, na hiyo ndio maana ile ile na maneno ya kikao cha msikitini, kakae utulie(Do Nothing)kuwa mtulivu, maneno ni yale yale lakini walipoonekana wameyatia mkono wanaadamu ndio Waislam wakaambiwa kakaeni Msikitini, itakujieni fahamu ya kumjua Mollah wako kwa njia anazozijua yeye Mollah wako.
Kwani nyakati nyengine si unakujia mfano unakutana na mtu humjui jina lake, una hangaika kutwa nzima hulipati lakini ukikaa ukatulia kimya mara linakujia, basi na Msikitini kakae utulie kuna faida chungu nzima utazipata zikiwamo na zile za kuepukana na machafu na maasi.

KIKAO CHA MSIKITINI PART 3

Asalaam Aleiykum

Hakuna tatizo gumu kama kukaa usifanye jambo, Jaribu uone kama unaweza kukaa usifanye chochote, yatakujia mambo hayapungui mia moja, hiyo ndio hulka ya mwanaadamu, utaanza kuwashwa, mara umejikuna, fujo tupu huwezi kukaa ukatulia.
Wewe umepewa nafasi hii kwa sababu za msingi ili upunguze mambo kwenye (Mind) ukifunga viungo vinafanyiwa ukarabati, na huku kukaa kimya Akili inapunguzwa mizigo usije ukapata matatizo baadae, ukikaa Msikitini mawazo yatakujia ya kila aina usiogope hiyo ndio (Process) ya kuondoshewa mazito yaliyomo kwenye (Mind) yako.
Ukitoka katika (Funga) unakuwa mweupe chuki, hasada, choyo,uadui vyote vinakuondoka na unabaki wewe kuwa Mcha Mungu. Umeambiwa ukakae Msikitini lakini hujaambiwa nini kitatokea, Kwa sababu ukiambiwa utaanza shughuli ya kungojea na kusubiri hicho kitakacho tokea, lakini umeambiwa kakae, kimetokea kitu shukuru, hakikutokea shukuru, lakini katika kikao hicho kuna faida kubwa utayoipata, Napenda ukumbuke chochote kile kitokacho kwa Mollah wako ni chenye Faida kubwa juu yako.
Sasa wacha nikupe dalili labda utazinduka na hii faida ya kukaa kimya Msikitini, Basi huoni wewe ukitulia kimya usingizi ndio unakuja?, Huoni wewe ukitulia ukasikiliza kwa utulivu ndio unafahamu vizuri?, Hivyo hujui kama ukitulia hata jambo ulilosahau linakujia na unalikumbuka, Basi kwa hayo machache nenda sasa na Saum yako kakae kimya peke yako Msikitini asaa kuna mambo au shufaa utaipata kutoka kwenye Dunia ya miujiza na kukufikia Mja wewe ukiwa umekaa kwenye Msikiti, Najua na wanawake watauliza na sisi jee, na nyie ndio mshaondoshewa Jinsia ya Kiume mbele yenu, basi kwa hiyo kaeni na nyinyi katika zile sehemu zenu mnazofanyia Ibada na nyinyi mtayapata yale yale wanayopata wenzenu wa Kiume, kwani Mwenye enzi Mungu, hambagui kiumbe wake katika kumpa Rehma zake, mbele ya Ufalme wake nyinyi nyote mko sawa. Na hicho ndio kikao cha Msikitini kama utakipata ipasavyo utaona Raha na furaha ya Funga yako ilo jaa tafauti mwaka huu.