Friday, February 15, 2013

SHUKURANI ZA UHAI-PART-1

Asalaam Aleiykum,

Namuomba Mollah wangu niepushe na kupenda ufakhari, Ama kujulikana au kujijulisha mimi yakua Mcha Mungu au Sheikh, Ninyime mimi nafasi ya kujulikana kuwa najua, halafu nifiche mimi katika lile kundi la wasofahamu, usinipe nafasi ya kuhifadhi Msahafu wote, au Hadith chungu nzima ikawa nimevaa joho la Uanazuoni wakati nikijua Bahari ya Ulimwengu huu ni kubwa namie sina uwezo wa kuikoga nikaimaliza, Nakuomba nipe japo aya moja, niifahamu kiundani maana iliyofichikana kwa wale wengi wasofanya jitihada za kukumbuka wewe na kuzijua Rehma zako. Haina haja mie kupiga kelele kuamsha wenzangu wakati mie nimelala fofoo, Naam anaishi Mwanaadamu mpaka anaondoka katika Ulimwengu huu hajapata kutoa Shukrani za dhati kwa Mollah wake.
Umetukuka Mollah wangu kwa kutujaalia hisia hizi za Uhai, kutupa Baraka hii ya Uhai na thamani yake, Ikisha ukawajaalia baadhi ya waja wako kufahamu haki hii walonayo ikawaingia khofu na utiifu pasi na kutishwa wakaamua kukuabudu na kufata amri zako, hao ndio Waumini wa kweli kama ulivo wataja mwanzoni mwa sura ya (Baqarah-aya-ya-3)"ٱلَّذِينَ يُؤۡمِنُونَ بِٱلۡغَيۡبِ وَيُقِيمُونَ ٱلصَّلَوٰةَ وَمِمَّا رَزَقۡنَـٰهُمۡ يُنفِقُونَ "
"Ambao wanaamini yasiyo onekana na wanasimamisha Sala na kutoa yale Tuliyowapa"
Hawa ndio waloamini pasi na uthibitisho wowote, kabla ya kupata ushahidi wao wame(Surrender to Islam)wamekua Waumini, Ikisha wakaingia katika kundi la wale ulo waruzuku wakawa wanatoa kwa Shukurani kubwa, wanaona furaha kuvitoa hivyo ulivowapa, Na huku wanashukuru kwa zawadi hii ya Uhai ulowapa, Sasa vipi utasema Ahsante ?, kila kiungo chako kina fursa ya kusema Ahsante(Kutoa shukurani kwa Uhai huu)Kulea yatima hiyo shukurani, kutizama wagonjwa hiyo shukurani, kutoa damu pia shukurani, kulisha maskini nayo pia shukurani, kumsomesha mtu pia shukurani, kujenga zahanati pia kutoa shukurani, kuangalia wajane pia ni shukurani kila jambo la kheri ulifanyalo ni shukurani, lakini sharti lake ni moja nalo usitake malipo au kushukuriwa na binaadamu wenzio, anasema Mollah wako wale wanotoa shukurani wamo katika aya hii ya 9 ya sura ya (Insaan)"إِنَّمَا نُطۡعِمُكُمۡ لِوَجۡهِ ٱللَّهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمۡ جَزَآءً۬ وَلَا شُكُورًا"
"Ambao wanatoa kwa ajili ya Mollah wao, hawataki wao malipo wala kushukuriwa"
Wanayafanya hayo kwa kutambua thamani hii ya Uhai na hiyo ndio njia yao pekee ya kutoa shukurani kwa Mollah wao, huku wakiwa na uhakika wa jambo ulolisema katika aya ya 10 ya sura hiyo hiyo
"إِنَّا نَخَافُ مِن رَّبِّنَا يَوۡمًا عَبُوسً۬ا قَمۡطَرِيرً۬"
"Hakika sisi tunaiogopa (Kwa ajili)ya Mollah wetu hiyo siku yenye shida na Taabu"
Jee siku hii ipo, inakuja, itatokea, nitaijuaje? Itabidi uwe mstahamilivu nikuchukue katika Ngarawa ya Wacha Mungu, Panda na mimi katika Mashua ya Mawalii(Mystic) ili nikupeleke katika kisiwa cha Ajabu sana cha Taaluma ya Tawhid, ukakutane na mambo yatakayo kukujulisha kuwepo kwa siku hiyo, ukitaka kuyajua hayo Endelea-Part-2

No comments:

Post a Comment