Asalaam Aleiykum
Binaadamu katika kadhia hii ya Talaka anakutana na fimbo mbili, Anachapwa viboko viwili pasi mwenyewe kujielewa kutokana na makosa ya kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenye-enzi-Mungu, Anasema Mwenye-enzi-Mungu katika sura ya (Talaq)aya ya kwanza kabisa anachanganywa na Bwana Mtume s.a.w,"
"ـٰٓأَيُّہَا ٱلنَّبِىُّ إِذَا طَلَّقۡتُمُ ٱلنِّسَآءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِہِنَّ وَأَحۡصُواْ ٱلۡعِدَّةَۖ وَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ رَبَّڪُمۡۖ لَا تُخۡرِجُوهُنَّ مِنۢ بُيُوتِهِنَّ وَلَا يَخۡرُجۡنَ إِلَّآ أَن يَأۡتِينَ بِفَـٰحِشَةٍ۬ مُّبَيِّنَةٍ۬ۚ وَتِلۡكَ حُدُودُ ٱللَّهِۚ وَمَن يَتَعَدَّ حُدُودَ ٱللَّهِ فَقَدۡ ظَلَمَ نَفۡسَهُ ۥۚ لَا تَدۡرِى لَعَلَّ ٱللَّهَ يُحۡدِثُ بَعۡدَ ذَٲلِكَ أَمۡرً۬ا"
"Ewe Nabii, Mtakapo wapa talaka wanawake(wake zenu)basi wapeni talaka katika Eda zao, Na fanyeni hisabu za Eda, Mcheni Mwenye-enzi-Mungu, Mollah wenu mlezi, Msiwatoe(Wanawake)katika nyumba zao, wala (Wao)wasitoke wenyewe, ila(Kama)watafanya jambo la uchafu ulio wazi(Kama vile mtu kafumaniwa kitandani nk)Hivyo ndiyo mipaka ya Mwenye-enzi-Mungu, msiivuke, na mwenye kuivuka mipaka ya Mwenye-enzi-Mungu, basi amejidhulumu nafsi yake, (Huwezi kujua)Hujui, labda Mwenye-enzi-Mungu ataleta jambo jengine baada ya haya."
Kuna makosa matatu yanatokea katika kupeana Talaka kwa karne hii tulonayo na hilo ndio linalo tupelekea kupata hizo fimbo za Mollah wetu. Amri ya kwanza kabisa ambayo hatuitekelezi(1)Hakuna anojali kabisa habari hii ya eda, si anosali au Sheikh au Ustaadh, jambo la mwanzo wanakimbilia katamka, na ukitamka umeumia, ndio kutamka kupo, lakini jee mlikaa mkahesabu miezi mitatu?.
Kosa la Pili(2)Msiwatoe au wao kutoka katika majumba yao, jee nyinyi mlikaa miezi mitatu mfululizo katika nyumba yenu ya ndoa?
Na kosa la tatu(3)Na hili ndio la kusikitisha zaidi linapita tendo la ndoa eti na huku eda inaendelea, hapo tena mtu anakua hajijui anapotoka na anapokwenda, hivi ndivo tulivofikia. Na hapa UK tunaachwa wanaume (Kama alivosema Mollah nyumba zao)basi hapa tunakiona cha-mtemakuni, unaweza kushtukia umefungiwa fuko lako la rambo(Black-bin-Bag)halafu linarushwa kutokea ghorofa ya kwanza, na ndani pengine umetiliwa na viatu vyako, fuko lile likifika chini linachanika kwa aibu unafanya haraka kuokota ili majirani wasione ikisha huyo unakimbilia kwa rafiki, hiyo ndio hali tulofikia sisi tunojiita waumini.
Basi msivuke mipaka ya Mwenye-enzi-Mungu, hapo sisi mipaka yote tunavuka na tuko tayari kwa chochote, tumeadhimia kumtii bwana wetu Ibilis hatusikii wala kuona, na huku tunaambiwa yoyote yule atokwenda kinyume na hayo basi amejidhulumu nafsi yake. Kwanini anajidhulumu nafsi? Sababu Mollah kakupeni Hekima zake, anakujueni viumbe vyake, na sababu ni zile zile nilizo zitaja mwanzoni, nyie mna (Magnet)menasana baina yenu na mkitaka kuinasua kwa nguvu basi mtajidhulumu, basi kwa hiyo kaeni kwanza miezi mitatu, huku mnapishana bila ya kufanya tendo lolote, huyu anapita huku kanga zinamuanguka na yule anapita kule anapiga ujicho, ikiwa kweli nyie mtafikisha miezi mitatu hamjapatana au hamaki hazijaondoka au hamjavamiana basi hapo rejeaneni kwa wema au tokaneni kwa wema. Nyinyi sasa mshaweza kuachana, kweli itakua Ibilis kamudu kukaa na nyinyi kwa miezi mitatu, kavunja kazi zake zote ili kukushughulikieni nyinyi tu, lakini pia eleweni Ibilis hatupi muda wote huo kukusubirini nyinyi, ndio maana mkapewa miezi mitatu, Haiwezekani mkakaa miezi yote hiyo mna hasira, hiyo ni (Cooling-off-Period)ilotoka kwa Mollah wenu. Eda ina hekima zake msiifanye Talaka ya kiislamu kuwa rahisi hata kupita bei ya (Njugu)watu wengi wanatizama ugonvi kuliko zile sheria za Mwenye-enzi-Mungu wanojinasib wanazifata, sasa ikiwa mshakaa hiyo miezi mitatu mkafata amri ya Mwenye-enzi-Mungu, basi tafuteni mashahidi wawili wa kuaminika na muwaeleze sisi tunarejeana kwa wema au tunaachana kwa wema na hapo Mwenye-enzi-Mungu anakufanyia urahisi njia ya (Move-on)kutokea, kama alivyoitaja kwenye aya ya pili ya sura hiyo hiyo.
Sasa kama unaenda kinyume cha hayo nini kinatokezea, vipi unayapata machungu na hizo bakora? kutokana na talaka zetu za siku hizi. Endelea-Part-3
No comments:
Post a Comment