Saturday, November 24, 2012

BALAA ZA UJANANI PART-1

Asalaam Aleiykum,

Nakushukuru Mollah wangu kwa kunipa siku nyengine ya Uhai nikaweza kukutukuza kwa zawadi hii Adhim, Nakushukuru Mollah wangu nimeamka nikiwa Hai naweza kuvuta pumzi, Naweza kutembea, Naweza kuijua Familia yangu na nikiwa mzima wa Afya.
Leo hii Mollah wangu ungetaka ningekuwepo kaburini kama walivyo tangulia walopita kabla yangu, Lakini kutokana na uweza wako bado hujanihitaji Mollah wangu, Na hayo yote si kwa mahitajio yangu mimi , Mimi sina amri kwa hilo, hichi ni kitu ulonikirimu wewe pasi mimi kuomba, Umenipa uhai huu kwa ridhaa yako na mapenzi yako juu yangu, Basi kwa hilo sina budi mimi ila ni kukushukuru na kukumbuka kila wakati Mollah wangu.
Leo tena umenipa fahamu na uwezo nitaweza kula na kunywa, Nitaweza kuwaona wanangu na wote walo wangu na marafiki zangu, Nitaweza kutoka na kurudi kwa salama nyumbani kwangu bila ya khofu yoyote ile. "Ewe Mollah wangu hakika umenipa Uhai huu wakati mimi sikua na thamani yoyote ya kupewa zawadi hii, Umenidiriki nivute pumzi hizi bila ya tabu wakati mimi nikiwa katika hali ya kukuasi Mollah wangu katika ujana wangu, Na unaendelea kunikirimu Neema hii hali naendelea kukuasi hata sasa katika uzee wangu lakini wewe upo katika hali ya kunipa nafasi labda leo au kesho nitakukumbuka Mollah wangu ili upate kunisamehe".Umenipa mimi furaha na afya wakati ule nilipo kukimbia nikawa sikukumbuki hata sekunde moja, yote hayo Mollah wangu umenisubiria, sasa sina mimi ila kujawa na shukurani katika moyo wangu na nimeridhia lolote lile litakalo nifika basi najua pengine ni mambo niliyofanya Ujanani ni makosa yangu mwenyewe ya kushindwa kujichunga wakati wa Ujana wangu ndio yalo nifikisha hapa nilipo.
Nikipata maumivu ya mwili au kero za Akili basi najua hili nimelisababisha kwa makosa yangu ya kupotea katika njia yako ya uongofu, Na mimi mwenye kukumbuka yale yote nilotenda katika Ujana wangu kama ulivosema katika kitabu chako kitukufu sura ya Qiyama aya ya 13" بَلِ ٱلۡإِنسَـٰنُ عَلَىٰ نَفۡسِهِۦ بَصِيرَةٌ۬ ""Bali mwanaadamu ni shahidi juu ya nafsi yake"
Nilikua mimi mchapaji wa mtindi (ulevi),Nilikua mimi sitoki vilabuni,Nilikua mbele ya hadhara ya watu nikipanda kwenye kiti nacheza viuno huku wengine wakinipigia makofi na wengine wakinitizama kwa matamanio sote tukitenda makosa lakini mimi ndio nilikua sababu ya kosa hilo.Nilikua nikivuta madawa ya kulevya, Nilikua nikiiba Serekalini na nikiona kama jambo la kawaida,Nilijiunga na vikundi vya uzinifu na kwangu ikawa kama jambo la kawaida, nilikua nadhulumu watu na kuwapiga nikisahau kabisa kuwepo kwako Mollah wangu, Najua yote hayo yapo hayajafutika na mengine naendelea kuyatenda sijui hali yangu itakuaje wakati utakapofika wa sasa wewe kunihitaji Mollah wangu ili nije kukutana na wewe. Na wewe utaniuliza kwani Mjumbe wangu hakusema lolote kuhusiana na Kadhia hii ya Ujana?-Endelea part-2

BALAA ZA UJANANI PART-2

Asalaam Aleiykum,

Anahadithia Ibn Abbas r.a"Kasema Bwana Mtume s.a.w""Kamilisha matano kabla hayajakufika matano"Yafanyie kazi matano hayo, kuwa makini katika mambo haya matano, jichunge sana katika kadhia hii ya mambo matano.(1)Ujana wako kabla haujakufika utu uzima,(2)Na Afya yako kabla Maradhi hayajakuvamia,(3)Utajiri wako kabla Hujafilisika,(4)Na Faragha yako kabla mambo hayaja kushughulisha,(5)Na Uhai wako kabla Mauti hayaja kuhudhuria.
Sasa hapo naya kusanya yote matano haya ili niweze kuyatia kwenye ukurasa mmoja ili upate kuyasoma kwa pamoja usije ukababaika.
Balaa za Ujana hazisemeki unaweza kuangua kilio ukikumbuka kuwa wewe ndie ulikua una andaa picknic na machupa ya ulevi, wewe ndie mwenye kuandaa ngoma za msondo na chakacha ili watu wapate kumsahau Mollah wao, wewe ndie mwenye kutembea umevaa (Backless)unaonesha watu mgongo wako. wewe ndie mwenye kuvaa kisuruali kifupi unaonesha watu mapaja yako, leo hayo yote yamepita umebaki wewe na sisi uko wapi ujana wako, Umepita kama moshi na yote ulotenda yamehifadhiwa halijafutwa hata moja, rekodi yako imetunzwa kwa umakini mkubwa na kama utabisha Viungo vitasema "Ewe kijana sisi ni mashahidi wako kwani hujaambiwa katika sura ya Yaasin aya ya 65.
" ٱلۡيَوۡمَ نَخۡتِمُ عَلَىٰٓ أَفۡوَٲهِهِمۡ وَتُكَلِّمُنَآ أَيۡدِيہِمۡ وَتَشۡہَدُ أَرۡجُلُهُم بِمَا كَانُواْ يَكۡسِبُونَ"
"Siku hiyo vitafungwa vinywa vyao, Itazungumza Mikono yao na itoe Ushahidi miguu yao kwa yale waliyokua wakiyachuma".
Ajihadhari Mwanaadamu siku ile viungo vitakapo kuwa tayari kumwaga siri zake, Vitaongea na kusema kweli mimi nilikua naishi maisha yangu kama Mcheza Cinema(Actor na Actress)Nilikua siwezi mimi kutoka katika nyumba yangu ila nijipambe, nitie piko, nitengeneze kucha,na Nywele niziachie nk, ndio nitoke, hivi hivi watu watanionaje na mimi nimeumbwa sijapendeza, Mimi nilikua nawaalika waja wako ili wanitizame mimi wapate kukuasi wewe na kukusahau Mollah wangu, hivyo ndivyo nilivoutumia Ujana wangu.(1)
Na Afya ulonipa nilikua nacheza mipira masaa mawili, Nakimbia riadha,nilikua na kula na kushiba mpaka nikawa nanyanyua vyuma nimejiunga (Gym)kwa uzima wa afya ulonipa, Lakini nyumba yako ya Ibada kwangu ilikua Marfuku, Ulikua ukiniona nikicheza pachanga (Disco)mpaka chini lakini nikiitwa kusujudu nilikua na kasirika sana hassa wakati wa Alfajiri.(2)
Na Uliponifungulia Utajiri Mollah wangu mtaa ulitingishika watu wote walijua mpaka paka wangu nilimvisha kengele, Niligeuka  mimi kuwa mcheza Senema maarufu nikiji fagharisha kwa kila aina ya starehe kuanzia ujenzi wa jumba la kifahari na magari yake sikujali chochote katika maagizo yako(3)Na Wakati ulo niruzuku ukanipa nafasi ya kuwa peke yangu ili nikukumbuke wewe, Hapo ndipo nilipotafuta (Whatsup)iko wapi, Computer iko wapi, Facebook iko wapi mchezo wangu kwenye TV utaanza saa ngapi, barazani kuna nini, hivyo ndio nilivokua natumia wakati wangu wa Faragha.(4)Na jambo la (5)ni kama ilivoanza mada kuelezea hali ya Uhai kabla ya Mauti.Basi leo uko wapi Ujana uliokua unaringia ulisahau maneno ya Mollah wako katika sura ya Yaasin aya ya 68
"وَمَن نُّعَمِّرۡهُ نُنَڪِّسۡهُ فِى ٱلۡخَلۡقِ‌ۖ أَفَلَا يَعۡقِلُونَ"
Na tunayempa Umri (mrefu)tunamrejesha nyuma katika umbo, basi jee hawayatii akilini(Kuzingatia).
Leo Ujana uko wapi huwezi hata kufanya mazoezi, Afya imekimbia umegubikwa na maradhi,Kipato sasa huwezi kukipata tena, kukaa peke yako sasa unaogopa, na pazia la Uhai lishafunikwa mgeni unae mtaraji Mauti yupo njiani, Basi yale Manne(4)umeyakosa hili lilobaki la Uhai bado unalo jitahidi katika hili kabla hujenda kukutana na Mollah wako.Zidisha Ibadah na Kuomba Maghfira Asaa Mollah wako huenda akakusamehe.

Abdulla Baja


Saturday, November 17, 2012

KIPIMO CHA IMANI-PART-1

Asalaam Aleiykum,

Hakuna jambo ambalo mwanaadamu anajihadaa kama kujinasib ana amini, ikisha ndani ya nafsi yake akawa anajua moyoni mwake hakuna hata chembe ya (Imani)Darsa yetu ya leo inagusa pahala penye uchokozi, tunakwenda kupachokoza pahala hapo ili upate kujua kumbe mimi siamini chochote, leo kamata kipimo chako ujue thamani ya Imani yako, halafu mwisho jiulize hivyo mimi naamini au nimejaa wasiwasi tu. 
Ili kukufanyia urahisi wakujua tafauti ya Mtu alokua hana Imani na Mwenye Imani nimekuchagulia visa hivi viwili ili vitufungulie darsa yetu ya leo, visome kwa umakini halafu utajiamulia mwenyewe ingekua wewe kundi lipi ungetamani kujiunga nalo. Hebu jikumbushe visa hivi viwili vimetokea katika miji tafauti, kimoja kimetokea katika mji wa (Lindi)ambapo walimaliza waumini kadhaa wakiislam kusali ikisha wakakaa Barazani, akatokea Mtu mmoja kashika panga mkononi akauliza ghafla jee hapa pana Muislam yoyote, waliopo pale barazani kwa khofu wakatingisha vichwa kuashiria hakuna Muislam huku kila mtu anatetemeka kwa khofu, yule Mtu akashika njia akenda zake, baada ya nusu saa akatokea kwa mbali huku panga lake limejaa damu anakuja haraka haraka, Barazani hakukaa mtu, walisema walokaa pale huyo yule jamaa sasa anarudi tumekwisha anarudi kuulizia kama kuna mkiristo miongoni mwetu, kumbe maskini yule Mtu alivouliza mwanzo alikua anataka akachinjiwe Ngombe wake kwa sheria za kiislam, na hii mara ya pili anarudi ili kuwaomba watu wakachukue sadaka ya nyama alipofika karibu kaikuta baraza nyeupe. Hizo ndizo zilivo Imani zetu, tukiulizwa una Amini tunatingisha vichwa kuashiria ndio, kumbe moyoni hapana kitu, Sala zote mtu anakwenda kusali kwa kuogopa moto tu, na wala si kwa ajili ya Mwenye-enzi-Mungu wake, hivyo ndio wengi Imani zetu zilivyo.
Na kisa cha Pili hiki kimetokea katika mji wa Basra kule Iraq, siku moja Darweish mmoja alikua ameketi (Zawiyyan)kwenye nyumba ya Ghorofa moja, alikua amezama katika hali ya (Wajid)kapotea kwa Mollah wake kwa ajili ya Ibadah, Darweish yule akawa anazungumza na Mollah wake "Anasema""Ewe Mollah wangu nijaribu mimi kwa chochote katika mitihani yako ili nipate kujipima mimi mapenzi yangu juu yako wewe, na mimi nafahamu mtihani wako unakuja kwa njia tafauti pasi kuwa na sababu yoyote,naomba mimi hilo ili nipate kuridhika, anamaliza kauli yake hiyo huku chini wanapita vijana na (Rika)zao wanaimba kasida hii""Kama kweli mpenzi wa Mungu chupa ujiunge nasi"(KAMA KWELI MPENZI WA MUNGU CHUPA UJIUNGE NASI)hawajamaliza mara ya tatu maneno haya mara wanamuona Darweish anazunguka na majuba hewani kutokea Ghorofani kajiachia, alipofika chini vijana wote wakakimbia Darweish huyo akakusanya majuba yake akarejea ndani ya nyumba yake bila ya kuumia hata kiungo kimoja.
Hiyo ndio Imani,. Sasa ikiwa leo na wewe mpenzi wa Mungu basi chupa ujiunge nami ili tupate kuzijua Imani zetu zikoje ili kama dhaifu tupate kuzifanyia kazi. Kumbuka katika safari hii hatakiwi mwanasiasa, au msomi, au mfanyabiashara au mpiga porojo  anotakiwa katika safari hii ni yule mpenzi wa Mungu mwenye kutaka kujua Imani yake, na huko upande wa pili kuna nini? na kwanini mimi simo kwenye kundi la wenye Imani?Endelea Part 2

KIPIMO CHA IMANI PART-2

Asalaam Aleiykum,

Nini Taqwa? Taqwa ni mapenzi, nini mapenzi, mapenzi ni njia au kivuli cha Imani, nini Imani, Imani ni msingi wa Ibadah, nini Ibadah, Ibadah ni njia au mwenendo wa kukutoa kwenye giza kwenda kwenye nuru, Kukuondoa kwenye hali ya kuto kuona kwenda kwenye kuona, Kukutoa kwenye Hamaki kwenda kwenye Huruma, Kukutoa kwenye kuadhibu kwenda kwenye kusamehe, kukutoa kwenye kusahau kwenda kwenye kukumbuka, kukutoa kwenye mazungumzo kwenda kwenye kusabihi, na mwisho kukutoa kwenye kiwiliwili kwenda kwenye Roho na hapo tena ni marejeo yetu sote kwa Mollah Muumbaji.
Sasa Ikiwa tushamaliza kuujua huo msingi hapo juu wacha tumalizie na nguzo zake ambazo sote tunazijua na kufahamu ziko sita, Katika nguzo hizi tumeambiwa tuziamini, lakini wengi katika sisi hakuna anazo ziamini ila tunazikubali, ni vizuri kukubali ndio mwanzo, lakini kinachotakiwi hapo ni kuziamini kwani kukubali tu wakati wowote unaweza kuzikataa (ndio maana wale walokaa barazani wakasema hakuna muislam hapa)ndio maana zikaitwa nguzo za Imani.Sasa chukua kipimo mwenyewe ujiulize ndani ya nafsi yako umeziamini au umezikubali ukipata jawabu ukajijua hujaamini umekubali tu Basi Nakwambia(Kama kweli mpenzi wa Mungu chupa ujiunge nami)ili utazame zaidi katika hizi Ishara ntakazo zitaja ili ujue ngapi unazo na hapo utajua kipimo cha Imani yako. Jiulize hivyo kweli mimi nina Imani?Nimeshawahi mara ngapi kuwalisha mayatima (1)Jee nimeshawahi kuwapa msaada wajane bila ya kuwatamani (2)Nini hali ya Muombaji pale anaponifata nimpe japo chakula natekeleza hilo (3)Nini hali ya Maskini jee nawafanya kuwa ndio marafiki zangu (4)Naweza kujizuia mimi nisiseme watu (5)Naweza kukaa siku mbili nisiseme uongo(6) nguzo sita namie nimetaja mambo sita lakini vipimo ni vingi sana vya hiyo Imani na kama mizani yako bado haijainuka hata kidogo kwa mambo hayo sita basi nakuomba "(Chupa ujiunge nami)"Ili tupate kuzikarabati hizo nguzo isije nyumba yako ikaporomoka kwa kukosa nguzo madhbuti.
Nguzo hizi zinafahamika uzuri kwa maandishi lakini kuna tabu kubwa kuziamini hususan kwa sisi viumbe wa kawaida ambao bado hatujaamua kuchupa, lakini kuna hii nguzo moja ambayo kidogo unaweza kujitahidi, sasa ni nguzo gani hiyo?ambayo ndio pekee inakugusa hiyo sehemu inapo kaa Imani, Nguzo yenyewe hii ya (kuamini vitabu vyake)hili la kitabu kuna wakati unachungulia ndani kutaka kujua kuna nini, angalau kidogo linakugusa pahali ukawa unakubali baadhi ya mambo, Na kama kitachomwa moto kitabu hichi unapata hasira japo kwa mbali na hamaki zinakushika, hapo angalau japo kidogo Kimizani chako kina nyanyuka, inaonesha unayo chembe ya mbegu ya Imani, Ndani ya chembe hiyo ndio mie nataka nitie mbolea ili upate kuota mti mkubwa wa Imani wenye matawi mingi.Sasa wacha tukamate nguzo hii ya kitab tutizame imesema nini na inathibitisha vipi hayo tuloyataja mwanzoni kuhusiana na kadhia hii ya Imani. Endelea-part 3

KIPIMO CHA IMANI PART-3

Asalaam Aleiykum,

"الٓمٓ (١) ذَٲلِكَ ٱلۡڪِتَـٰبُ لَا رَيۡبَ‌ۛ فِيهِ‌ۛ هُدً۬ى لِّلۡمُتَّقِينَ (٢) ٱلَّذِينَ يُؤۡمِنُونَ بِٱلۡغَيۡبِ وَيُقِيمُونَ ٱلصَّلَوٰةَ وَمِمَّا رَزَقۡنَـٰهُمۡ يُنفِقُونَ (٣) وَٱلَّذِينَ يُؤۡمِنُونَ بِمَآ أُنزِلَ إِلَيۡكَ وَمَآ أُنزِلَ مِن قَبۡلِكَ وَبِٱلۡأَخِرَةِ هُمۡ يُوقِنُونَ (٤) أُوْلَـٰٓٮِٕكَ عَلَىٰ هُدً۬ى مِّن رَّبِّهِمۡ‌ۖ وَأُوْلَـٰٓٮِٕكَ هُمُ ٱلۡمُفۡلِحُونَ ("٥
"Hiki ni kitab kisichokua na shaka ndani yake, ni uongozi kwa wanao mcha Mwenye-enzi-Mungu.Ambao huyaamini yasio onekana na kusimamisha sala na kutoa katika yale tulo waruzuku.Na ambao wanaamini yaliyoteremshwa kwako, na yaloteremshwa kabla yako na wanaimini (hiyo)Akhera.Hao wako juu ya uongozi utokao kwa Mollah wao, Na hao ndio wenye kuongoka."
"Aya hiyo ya pili imeanza kimaajabu"imesema hakika hichi ni kitabu ambacho hakina shaka ndani yake na ni muongozo(Kwa wapenzi)Wamchao Mungu,Maana yake kama utakifata kitab hichi (Quraan)basi ndani ya hiki kitab kuna muongozo na muongozo huu ni ule unao kukupeleka kwenye Imani, kwa hiyo ni vizuri kama unasimamisha Sala na kumpenda Mollah wako na Mtume wake basi umo katika (njia ya Uongofu)na ukikaa katika njia hii kuna siku utafunguliwa hiyo Imani.
"Aya ya tatu ikasema Ambao wanayaamini yasio onekana na kusimamisha sala na katika yale tunayo waruzuku wanayatoa"
Itabidi hapa mstahamili ili tupate kuchuma katika mti wa faida kuhusiana na hilo neno kuamini yasioonekana. Ina hadithiwa katika riwaya za hekima, kuna siku walikaa Mawalii wawili pamoja na wanafunzi wao, Ikawa walii mmoja anataka kumwambia mwenzie kitu lakini hawezi kufanya vile mbele ya wale wanafunzi, akaagiza aletewe karatasi nyeupe anataka kuandika kitu, wanafunzi wake wakamletea, akachukua kidole chake cha Shahada akawa anaandika kwenye ile karatasi alipomaliza akampa yule walii mwenzie yule walii aliikamata ile karatasi akaitizama kwa njia ya kusoma ikisha akaangua kicheko kikubwa, Walo hudhuria pale wakaona sasa mambo yamekua makubwa, ama walimu wagonjwa au kuna miujiza mikubwa imetendeka mbele yetu, wakashikilia sana wale wanafunzi kuwauliza walimu wao nini kilicho andikwa kwenye karatasi ile lakini hawakupata jawabu la swali lao, Baada ya muda kupita yule muandikaji wa ile barua mauti yaka muhitaji, yule mwenzie alobakia akawaita wale wanafunzi wote akawaambia leo nitakwambieni nini kilichoandikwa na mwenzangu siku ile, Alicho andika mwenzangu siku ile katika ile karatasi nyeupe na nyie mkawa hamuoni yale maandiko alisema maneno haya,"hawa wanafunzi wangu nimekaa nao sasa yapata miaka sita, hawanifahamu wala hawafahamu kitu, hawatizami dalili wala hawazioni, hawaelewi chochote ninacho wafundisha,utadhani macho yao yamepofuka au masikio kuzibwa, basi kama mauti yatanihitaji mimi mwanzo naomba uwape habari hii. Wale wanafunzi wakamuuliza vipi wewe uliweza kuisoma ile karatasi nyeupe isiyokua na maandishi, Akajibu kulikua hakuna miujiza wala makarama ila ilikua wakati anaandika anatumia ishara na alama za herufi kwa kidole chake na mimi nilikua naangalia kile kidole kinaandika herufi gani basi nikawa naunganisha neno, Na nyinyi wakati ule mlikua hamjui kuyatizama yasio onekana(yalo Ghaib).Na wewe ungekuwepo wakati ule ungebisha, ungeshangaa na kuamini makarama, lakini dunia yetu ya leo unamuona (Bubu na Kiziwi)wote wanazungumza kwa ishara na alama.Haya ndio matatizo yetu makubwa hatujui kutizama ishara zote Mollah wetu alotuwekea, sasa ikiwa umejipima na kujigundua bado Imani yako ni dhaifu jaribu kuangalia Ishara na Alama za Mollah wako asaa mizani yako ya Imani itapanda juu, pengine utafunguliwa kuona mambo ili izidi Imani yako na imani ikiingia sawa sawa basi halitoki tena jambo hilo la Imani mpaka mwisho wa Umri wako na utakua unaamini kama unavo liamini jua na mwezi kuwa vipo na hayo mengine utaamini hivyo hivyo, na ikisha kuingia Imani hiyo kwako kila wakati utakua wakati wa "(kusimamisha hiyo Sala)" na kama mtu atakutania tu, "kama kweli mpenzi wa Mungu chupa ujiunge nami"hapo hapo husiti au kusubiri chochote kile, sijui nyumba nitamwachia nani, gari atachukua nani, pesa za bank itakuaje, hufikiri mambo hayo kabisa ila unajiachia kama yule Darweish.Endelea part 4

KIPIMO CHA IMANI PART-4

Asalaam Aleiykum,

Na hapo tena  kila unacho Ruzukiwa unafanya haraka haraka kukitoa, na kumbuka kila ukitoa kwa njia ya Imani basi huku unazidishiwa kupewa ili upate kutoa tena. 
Na hao ndio walo amini yaloteremshwa kwako "Ewe Mjumbe wa Mwenye-enzi-Mungu" na yaliyo teremshwa kabla yako, yepi hayo walo yaamini ikawa ndio nguzo zao. Dalili ya nyumba, maana yake kuna mtu anaishi, Ukiona na kuutizama Ulimwengu basi una hakika yupo alouumba naye huyo Mollah wako(1)Dalili ya Hukumu ni haya matendo ya Dhanbi na Thawabu kwa hivyo ni kuamini hiyo Akhera na siku ya (Hukumu)Kiyama.(2)Kuupata huu ujumbe wa Mwenye-enzi-Mungu na ushaidi uliopo wa macho kwa kujionea na mabaki yalobakia katika historia ni kuamini Mitume yake.(3)Kuyapata maneno kama haya yenye uthibitisho na maliwazo na ukumbusho pamoja na maonyo ni kuamini Vitabu vyake.(4)Kukubali maneno ya Mollah wako na kujua kwamba utakufa na Roho yako itachukuliwa ni kuamini Malaika wake.(5)Kujua kwamba vyote viliyomo mbinguni, nyota, mwezi,jua na viliomo ardhini miti, majani, wanyama, ukiwemo na wewe mwanaadamu nyote mmekamatana ni kitu kimoja basi hiyo ndio njia ya kuamini kheri na shari vyote vinatokana na yeye Mollah wako.(6). Na huo ndio muongozo utokao kwa Mollah wako na anayepata muongozo huu unampeleka katika Imani kubwa na anakua ni mwenye kufanikiwa ndipo akiambiwa chupa kwa ajili ya Mwenye-enzi-Mungu hasubiri hata itamkwe tena ila anakua kesha hudhuria kwa Mollah wake bila ya kuchelewa.
Ukitaka kuijua Imani yako patafute wapi yanatokea machozi, wapi zinapotokea hasira,wapi inapotokea chuki, wapi zinapotokea huzuni, wapi zinapotokea huruma, wapi zinapotokea hisia ukisha pagundua hapo pahala basi subiri hapo hapo wala usichoke asubuhi na usiku wala usifanye chochote baada ya muda Mollah anajua kama kweli wewe mpenzi wake na yeye ndio atakufungulia huo mlango wa Imani, na ukiipata hiyo Imani wewe unakua hakika Miongoni mwa waloongoka.
" قَالَتِ ٱلۡأَعۡرَابُ ءَامَنَّا‌ۖ قُل لَّمۡ تُؤۡمِنُواْ وَلَـٰكِن قُولُوٓاْ أَسۡلَمۡنَا وَلَمَّا يَدۡخُلِ ٱلۡإِيمَـٰنُ فِى قُلُوبِكُمۡ‌ۖ وَإِن تُطِيعُواْ ٱللَّهَ وَرَسُولَهُ ۥ لَا يَلِتۡكُم مِّنۡ أَعۡمَـٰلِكُمۡ شَيۡـًٔا‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ غَفُورٌ۬ رَّحِيمٌ "
"Walisema Waarabu (wanaoishi majangwani)Tumeamini(Wanamwambia Mtume s.a.w)sema hamjaamini, lakini semeni tumesilimu, Maana Imani haijaingia katika mioyo yenu, Na mkimtii Mwenye-enzi-Mungu na Mtume wake, hata kupunguzieni chochote katika vitendo vyenu, Hakika Mwenye-enzi-Mungu ni mwingi wa kusamehe na Mwingi wa Kurehemu. Namalizia kwa Aya hii ili upate kujijua na kuongeza juhudi na "KAMA KWELI MPENZI WA MUNGU BASI CHUPA UANZE LEO HII KUITAFUTA NA KUIJAZA HIYO IMANI"na Mollah wako atakusaidia kwa hilo Inshaallah.

Abdulla Baja


Saturday, November 10, 2012

NANI KAMA MAMA?PART-1

Asalaam Aleiykum,

Leo wacha nikuchukue tuingie katika Dunia ya Mama, Kwanini nikasema tunaingia, nimesema tunaingia kwa sababu dunia ya mama ni ulimwengu wa ajabu, na wanaadamu desturi zetu ukishazaliwa, ukalelewa kwa mapenzi basi unakuwa huna haja ya kutizama nyuma au kwa maana nyengine hutaki kujua mahusiano yako na wazee hawa wawili. Zawadi hii adhimu hutaki kuijua, ila unaicha iendelee (Automatic), na hiyo (automatic)huenda ikafikia pahala inaharibika, inakua haifanyi kazi tena na hapo ndipo mahusiano yako na wazee wako wawili yanaanza kutetereka.
Sasa ikifikia hali kama hiyo ndio inatubidi tutembelee tena ndani ya Quraan-aya-ya-14-Luqman, ipate kutukumbusha,
"وَوَصَّيۡنَا ٱلۡإِنسَـٰنَ بِوَٲلِدَيۡهِ حَمَلَتۡهُ أُمُّهُ ۥ وَهۡنًا عَلَىٰ وَهۡنٍ۬ وَفِصَـٰلُهُ ۥ فِى عَامَيۡنِ أَنِ ٱشۡڪُرۡ لِى وَلِوَٲلِدَيۡكَ إِلَىَّ ٱلۡمَصِيرُ "
"Tumemuusia Mwanaadamu(Kuhusiana na kuwafanyia wema)Wazazi wako, Mama amechukua mimba(yako)kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha kunyonya baada ya miaka miwili,(basi)Nishukuru mimi na wazazi wako,ni kwangu mimi marejeo yenu"
Nilipoanza hapo juu nilitaja neno (Automatic)kusudio langu ni kueleza huo wasia ambao umo ndani ya jinsi(Being)yako, imeshaumbiwa ufahamu huu wa kuwafanyia wema wazee wao kama kuishi nao kwa uzuri na mapenzi, hii kwa wazee wako inakuja (Automatic)sio kwamba anakuja mtu kukuweka chini na kuanza kukupa wasia, ikiwa mtu atafanya hivyo elewa hizo ni taratibu zake au uzoefu wake, lakini wasia kutoka kwa Mollah wako unatokea ndani ya (Roho)yako ndio maana utajiona unawaonea huruma, imani, nk. Lakini aya imekwenda mbele ikakumbusha nishukuru mimi (Mollah)wako ikisha na wazee wako wawili, Hapa ndipo nikasema hebu tutizame nyuma, tuingie katika hii dunia ya Mama vipi kachukua mimba kwa udhaifu juu ya udhaifu, ukisha kuyajua hayo hapo pengine shukurani yako ya dhati itatokea moyoni.
Ili shukurani hiyo ikuporomoshe kwa maneno na vitendo, isije ukawa unaitoa shukurani hiyo huku umeshika kiuno huku unamtuma mama yako akuletee maji ya kunywa.
Nani kama Mama?
"Alikuja Mtu siku moja kwa Bwana Mtume s.a.w akamuuliza"Ewe Mjumbe wa Mwenye-enzi-Mungu, Nani Katika wanaadamu anastahiki awe kipenzi changu,(Nimfanye kuwa rafiki yangu)nimfanyie ihsani nimpe na mapenzi?Akajibu Bwana Mtume s.a.w "Mama yako,yule mtu akasema ikisha, Bwana Mtume s.a.w akasema tena Mama yako,yule mtu akasema halafu,Bwana Mtume akamwambia Mama yako, na Mara ya Nne akamwambia Baba yako.Hasemi Bwana Mtume s.a.w Ila maneno yake ni uthibitisho utokao kwa Muumba mwenyewe wa hao wanaadamu, Sasa kwanini     
Bwana Mtume s.a.w akasisitiza hususan Mama, ili upate kujua Endelea part-2

NANI KAMA MAMA?PART-2

Asalaam Aleiykum,

Uhusiano wako  na mama yako mpaka leo unabaki miujiza ambayo hatuwezi kutambua undani wake, kwanza kabisa huyu Mama akizaliwa tu anakuja na mayai yake kamili ndani ya tumbo lake, na katika mayai hayo moja wapo ndio hilo lilo kuzaa wewe, jee mapito yako kwa mama huyu ni bahati au kitu kilichopangwa?Kaa ufikiri kadhia hii halafu ujue kwanini ikatokea hivyo, mtizame Mama yako kwa jicho la huruma ujue kutokana na kudra ya Mwenye-enzi-Mungu yeye karidhia sababu ya uhai wako ianzie kwenye kiwili wili chake, yuko tayari achukue machungu yote na taabu zote ili na wewe upate ladha hii ya maisha ya kidunia.
Na muujiza mwengine ambao unadumu mpaka ya wawili nyie kuondoka katika Ulimwengu huu ni ule unao anzia tumboni katika kiunganishi chako wewe na Mama yako yaani kwenye (kitovu)Hapo katika miezi yote tisa yakuumbwa kwako ndio unapata huduma ya uhai wako, zinapita hapo (Electric-Transfer)baina yako na mama yako, ikawa aanchokila na wewe unapata faida zake, akihema kwa kupokea nguvu za uhai na wewe unapata kuishi(Umo tumboni umelala masaa ishirini na nne)kila kitu unafanyiwa, nje kukitokea msuko suko na wewe unashtuka mule ndani, kila kitu kimeambatana na Mama yako huku wewe umetulia unaendelea kuumbwa, na kila hatua ya kuumbwa kwako basi matatizo,magonjwa na shida zote zinamfika Mzazi wako huku yeye anastahamili na kumuomba Mwenye-enzi-Mungu "Ewe Mollah wangu nijaalie nikitoe kiumbe hichi kwa salama, hayo ndio maombezi ya Mama kwa mwanae ambae hata hajamuona au hamjui atakua kiumbe wa aina gani?.
Mapenzi ya Mama yanaanzia ungali tumboni, na inapotimia miezi tisa unazaliwa na kitu cha mwanzo kinofanyika unapewa uhuru wako ili uweze kuishi mwenyewe unakatwa ile(Life-support)Kitovu ,ile kamba ya uhai ikisha katwa baina yako na Mama yako sio mwisho wa wewe kumuhitaji Mzazi wako, ila baada ya muda mfupi tu una muhitaji huyu Mama aendelee kukupa huduma hii ya Uhai ili upate kuishi, hapo tena mahusiano ya tumboni yamekatika yanaanza ya kwenye (Kifua)kunyonyeshwa.Unaendelea kuwa muhitaji, unaendelea kumtegemea Mama takriban kwa miaka miwili au karibu na hapo, Na kama Mama atakua katili au hana huruma au ujana unamtesa akakudhulumu kukunyonyesha katika kipindi hichi basi maisha yako yote yatakua na matatizo ya hapa na pale kuhusiana na mapenzi au mahusiano yako na watu wengine.
Lakini Mama mwema ni yule apendaye kumnyonyesha mwanae na huku akimuombea Taufik kwa Mollah wake,Mjaalie mwanangu akue bila ya matatizo mpe afya njema na lau kama Mama huyu ataulizwa ghafla baina yako na mwanao nani unataka afe mwanzo, basi bila ya kusita au kujishauri atasema bora afe yeye ili huyu mtoto abaki.
Nani kama Mama? Huyu ndie leo wewe mtoto eti unaomba atakufa lini, mbona anateseka na anakutesa na wewe.Huyu ndie Mama mwenye kupokea machungu yote unayomletea au yanayokupata, huyu ndie mama mwenye kukupa mapenzi bila ya masharti yoyote.Huyu ndie Mama mwenye kusamehe kabla hata hujaomba hiyo samahani, Wallahi hakuna shaka ya mapenzi yako isipokua mfano wa miujiza,Hata watu wote wakikuchukia yeye anabakia kukupenda,yuko radhi akae na njaa ili upate kula wewe,yuko tayari akae macho ili wewe upate kulala,"wewe Mama mimi nikiumwa wewe unahangaika usiku kucha huku watu wote wamelala", uko radhi uteseke ili mimi nifurahi, wewe ndie unaenijua naumwa nini wakati hata siwezi kujieleza,Na sifa yako nyengine halipungui penzi lako hata tukiwa kumi unatupenda sote katika hali ilo sawa.
Nani kama Mama?endelea part-3

NANI KAMA MAMA?PART-3

Asalaam Aleiykum,

Mama ni wewe mpaka nikiwa mtu mzima mapenzi yako yanaendelea kama yalivo mwanzo, Leo hii nimekua mkubwa ukaja kuniozesha sasa niko na mke wangu au mume wangu eti nakukejeli mbele yake, Mimi nakupuuza na huku namuamini mume wangu au mke wangu na kukukadhibisha wewe, Mimi nina hali gani kama ghafla nitahudhuria kwa yule aloniumba. Leo imefikia eti nakutuma unikoshee vyombo, au uende dukani, na hivi ndivo jeuri ziliponifikisha.Nimefikia hali nayapuuza Maneno ya Bwana Mtume s.a.w alosema "Hakika ya hiyo pepo ipo chini ya nyayo za Mama zenu",Kwanini Bwana Mtume s.a.w akasema maneno haya na nini alikua anakusudia,"Kusudio hapo lilikua kukufahamisha ni lazima ujitupe, urejee katika hali ya chini kabisa mbele ya Mama yako, sio wewe umtume maji ya kunawa mkono Mama yako,ila unatakiwa wewe ukachukue hayo maji umnawishe Mama yako halafu usimame mpaka amalize kula hiyo ndio heshima na huko ndio kunyenyekea kwa mzee wako, wangapi katika sisi leo tunatenda hayo, leo akikuomba pesa ya kula  tu majibu yanayokutoka mpaka Malaika wanaogopa. Leo unasahau kama Mama yako alikua akienda msitu na nyika ili atie tonge kinywani mwako, yeye ndio kila akikaa anakuombea dua kwa siri na dhahir ili ufanikiwe.
Nani kama Mama?
Sasa kama unayatilia wasiwasi Maneno hayo ya Bwana Mtume s.a.w "Basi jikumbushe kisa cha kijana Alqamah"Yeye alikua  ni mwenye kujitahidi kufanya mambo mengi ya Ibadah, alikua akisimamisha Salah, (kipindi hakimpiti)akifunga sana(Saum ni kawaida yake)na katika mambo ya kutoa sadaka yeye alikua mbele sana katika kutoa, Yakaja kumpata maradhi na maradhi yale yakawa yanazidi, akamtuma mkewe akampe habari Bwana Mtume s.a.w"Akenda yule Mke kwa Bwana Mtume s.a.w "Akamwambia mume wangu Alqamah anaumwa Taabani Yaa Rasullallah"kanambia nije kukufahamisha. Bwana Mtume s.a.w akatuma Masahaba zake akiwemo Syd Bilal r.a wende nyumbani kwa Alqamah mkamtoleshe Shahada, wakenda Masahaba  wakamkuta Alqamah makhtuti, wakamwambia "Ewe Alqamah sema"(Laaillah-illa-Allah)Lakini ulimi wa Alqamah haukuweza kutamka, wakarejea kumpa habari Bwana Mtume s.a.w na akasema jee wazee wake Alqamah wa hai, akajibiwa Mama yake yupo hai lakini ni mtu mzima sana, akamtuma mtu akamwambie mama yake Alqamah kama ataweza kutembea na kuja kwa Bwana Mtume s.a.w laa kama hawezi basi Bwana  Mtume s.a.w atakwenda yeye.
Akainuka Mama yake Alqamah na fimbo yake akenda kwa Mtume s.a.w akamsalimia na Bwana Mtume s.a.w akarudisha salam ikisha akamwambia "Ewe Mama wa Alqamah niambie ukweli na kama ukidanganya basi utakuja wahyi kutoka kwa Mwenye-enzi-Mungu" ilikuaje hali ya Mwanao Alqamah(wakati yuko mzima)Akajibu Mama yake Alqamah alikua mwenye kusali sana, na akifunga sana, na akitoa sadaka sana, Akamuuliza tena Bwana Mtume s.a.w jee yalikua vipi mahusiano yako na mwanao Alqamah, yule mama akasema "Ewe Mjumbe wa Mwenye-enzi-Mungu, Hakika mimi nimefungika moyo wangu juu ya mwanangu"kwani alikua akimsikiliza Mkewe na akiniasi mimi(akinikadhibisha)Akasema Bwana Mtume s.a.w kufungika kwa Mama yake Alqamah ndio sababu mwanae hawezi kutoa Shahada, ikisha akamwambia Ewe Bilal r.a kanitafutie kuni(Mbao)ili apate kuchomwa moto Alqamah, Akasema Mama wa Alqamah hauwezi kuchukua moyo wangu kuona mwanangu anateseka, Akasema Bwana Mtume s.a.w adhabu ya Mwenye-enzi-Mungu ni kali kuliko hiyo na ni ya kuendelea, basi kama utataka asamehewe na Mollah wake itabidi Uridhie moyo wako na kama hukuridhia moyo wako hazitomfaa, sala zake wala funga zake wala utowaji wake wa sadaka midamu moyo wako umefungika juu yake.
Akasema Mama yake Alqamah Mwenye-enzi-Mungu ananishuhudia na Malaika wake na waislam wote walohudhuria hapa yakuwa mimi niko Radhi na mwanangu, Akasema Bwana Mtume s.a.w Ewe Bilal r.a nenda kamtizame Alqamah anaweza kusema (Laa-illah-illa-Allah)au hawezi, isije ikawa Mama yake Alqamah kasema kitu hakimo ndani ya moyo wake ila kanionea haya mimi, Akenda Bilal r.a akamsikia Alqamah anasema (Laa-illah-illa-Allah)akaingia ndani ya nyumba Bilal r.a na kuwaambia waliomo ndani kufungika kwa Mama yake Alqamah ndio kuliko fanya uzito wa kushindwa ulimi wa Alqamah kutamka shahada, mpaka aliporidhia mama yake ndio ulimi ukatamka na ukawa mwepesi, ikisha baada ya hapo Alqamah akafa siku ile ile.Sasa ikiwa Shahada imeshindikana nini habari ya kuipata hiyo pepo inakuaje? Endelea part-4

NANI KAMA MAMA?PART-4

Asalaam Aleiykum,

Nani kama Mama?
Leo unataraji pepo huku unamtuma mama yako akuletee chai, huku unapita ukisema anamkera mkeo au mumeo, Mama akiomba pesa ya chakula unamjibu huna wakati ukitoka unakwenda kuchapa matumizi kwa mambo ya kijinga, Nyie watoto wa kike haijambo kidogo mnajitahidi kuwafanyia hisani Mama zenu ila zidisheni unyenyekevu, Enyi watoto wa kiume nyie tahadharini sana na kuwatupa mama zenu na kuwasahau, yanakufikeni madhara na fimbo ya Mwenye-enzi-Mungu inakupigeni pasi na nyinyi kujijua, Unapita kujiuliza mbona mambo hayendi, mbona sina furaha, mbona nyumba yangu haikaliki kuna nini? mbona watoto hawanisikilizi, mbona kipato changu hakitoshi, kumbe hujijui umo katika kukanusha Maneno ya Mwenye-enzi-Mungu"Ni shukuru mimi na wazazi wako wawili"huyo ndio Mama ambaye leo umemtupa, leo humtizami, huwezi hata kumtembelea una harakati nyingi. Ewe mtoto umeambiwa muhudumie mama yako unasema huna uwezo eti unamajukumu mengi, nini habari yako wewe kama ghafla utafunga kauli huwezi kusema tena, Angalau mwenzio Alqamah alipata bahati Mama yake akamridhia, sasa nini hali yako wewe kama Mama yako akikutangulia bila ya kupata Radhi zake.
Sasa nini ufanye? vipi utamshukuru Mzee wako, itabidi tukitembelee kisa cha Nabii Mussa a.s "alipomuuliza Mollah wake nani atakua Rafiki yangu peponi?"Mwenye-enzi-Mungu akamwambia nenda katika njia mtu wa mwanzo utayekutana naye huyo ndie atayekua Rafiki yako peponi, Akatoka yule Msemezwa na Mollah wake Nabii Mussa a.s akenda kwenye hiyo njia akakutana na huyo mtu akamwambia leo nataka nikufate niwe na wewe kutwa nzima, yule mtu akamjibu sawa, wakatoka wakenda sokoni akanunua chakula wakarudi nyumbani walipofika walimkuta  
Bibi mtu mzima kakaa pembeni, yule kijana akatoa vile vitu akaanza kupika alipomaliza akachukua maji akamnawisha yule bibi halafu akaanza kumlisha ikisha akampa maji na kumrudisha kwenye kitanda, huku wakati wote Nabii Mussa a.s anamuangalia alipomaliza, Nabii Mussa a.s akamuuliza huyu bibi ni nani kwako, yule mtu akamjibu huyu ni Mama yangu, Nabii Mussa a.s akasema nilikua nakuona kila unachomfanyia huyu bibi unasema maneno, ni maneno gani ulokua unasema, akajibu kila nilipokua namfanyia kitu Mama yangu nilikua nikiomba Ewe Mollah nijaalie mimi kuwa Rafiki yangu Nabii Mussa a.s huko peponi. 
Nani kama Mama?
Huyo ndio Mama na hayo ndio malipo yake, hiyo ndio maana ya hiyo pepo ipo chini za nyayo za Mama zenu, "Ni Shukuru mimi na wazazi wako wawili"Kushukuru wazazi ni kuwatendea wema, kuwadekeza, kuwapa mapenzi, kusema nao kwa upole, usiwatolee jeuri, uwatizame kwa hali na mali, ukimuona anafanya kazi kuwa wa mwanzo kumsaidia, fanya kila uwezalo mpaka mama yako afurahi moyoni na akifurahi basi utaona matatizo yote yanaondoka utaipata furaha ya Raha mustarehe kama ulivokua tumboni nakukumbusha (Connection)bado ipo inaendelea mpaka mwisho wa Uhai wenu, na katika kiungo hichi ndipo inapokaa hiyo Radhi basi fanya jitihada usije ukaikosa au kuikata, Mwenye-enzi-Mungu wape Rehma zako za Usamehevu kwa wale wazee wetu walotangulia, wape afya njema kwa wale walobakia, na uwape umri mrefu wenye manufaa ya kukumbuka wewe daima-Amin

Abdulla Baja

Thursday, November 1, 2012

SHAIRI LA MCHA MUNGU-PART-1

Asalaam Aleiykum.

furaha ilioje ukipata nafasi ya kuyasikia maneno ya Mcha Mungu hasa wakati kama huu umemaliza siku za furaha za Eid-Adh haa, Anasema nini Mcha Mungu.
"Nilipojua kwamba katika Moyo wangu kuna uwezekano wa kukaa asiye kuwa wewe Mollah wangu, Basi nilifanya mimi jitihada na mashindano makubwa ili kuhakikisha kuwa haingii akakaa mwengine yoyote asiye kuwa wewe Mollah wangu, niliendelea mimi kuujaza Moyo wangu uongofu wa kila jambo utokao kwako hata ikawa haikubakia nafasi yoyote ya kukaa asiye kuwa wewe Mollah wangu".
Anasema Mcha Mungu nilipojua au nilipogundua au uliponijia mimi (Uamsho) katika moyo wangu kwamba kuna uwezekano wa kukaa asiye kuwa wewe, hapo nilianza kufanya jitihada kubwa nilishindana sana kwa ajili yako Mollah wangu ili asije kuingia yoyote yule Moyoni mwangu, Katika maneno haya kuna siri kubwa Mcha Mungu anataka kutupa na sisi faida ili tupate huo (Uamsho)litutoke lepe lepe la usingizi ili tusikubali tena kumpisha kila ajae kukaa katika Mioyo yetu.
Nini maana ya neno Uamsho?
Katika matumizi ya lugha ya Wacha Mungu neno hili kama mengine yote yana maana mbili, Maana ya kwanza ni ile inotumika katika sauti za kila leo kama vile ukiambiwa Uamsho, wewe utafasiri kwa maana nyingi tu unavopenda, labda umelala umekuja kuamshwa, Pengine unaamshwa ukale daku mwezi wa Ramadhan, au tafsiri nyengine kuwa kuna watu washaamka na sasa wanakuamsha na wewe pengine unadhulumiwa au unatawaliwa na shetani wanakuzindua, sasa basi tena kutawaliwa simama  udai haki yako, wote huo unaweza kuita Uamsho, hiyo ni maana ya nje ya Uamsho. Ama katika maana ya ndani ya Uamsho inakua kama alivoitaja Mcha Mungu nilipojua (Awaken) vipi inakua muamko huu? Mfano utaupata katika usingizi wako wa kawaida, hebu jichunguze vipi inakua pale mwanzo ukiamka asubuhi, jitahidi usifungue macho utaona kitu cha mwanzo kinacho kujia ni (Awareness)kujijua mie nishaamka hapo hujijui mie fulani babaake fulani au mie fulani mke wa fulani, habari hizo hufatia baadae.
Kitu cha mwanzo kukushukia ni elimu ya kujijua mie ni macho na hapo Mcha Mungu husema (Alhamdullillah)ukitulia katika hali hiyo ndio utagundua kumbe kuamka ni (Process)kama vile inavoingia Alfajiri au Magharib, ndio Mcha Mungu akasema "(Nilipogundua kumbe katika moyo wangu anaweza kukaa asiye kuwa wewe)"na ukitaka kujua vipi anakaa asiye kuwa wewe basi ukiliacha lile sharti la usifungue macho, ukaja ukayafungua hapo utaanza kuona mtiririko wa asiye kuwa yeye unavo miminika, zinaanza kuingia (Information)zote unasahau hata kama ulikua umelala, unaanza kukumbuka viporo vyote ulobakisha jana, basi kabla hujaamia katika hizo kumbukumbu kitu cha mwanzo kinacho kujia ni hiyo elimu ya kujua, na huo ndio Uamsho, ambao watu wengine wanautilia mkazo tu ili usije ukalala tena au ukaja kulazwa, sasa ufanye nini endelea part 2 ujue taaluma hii ya uamsho inaishia wapi.

SHAIRI LA MCHA MUNGU-PART-2

Asalaam Aleiykum,

Uamsho huu wa ndani au wa aina ya pili unatokana na Mollah wako, na Mtu au watu wakisha amshwa na Mollah wao inakua tabu tena kuwalaza hata ukitumia nguvu ukali hawalali tena, sababu wanakua washajua na siri ya kujua inakaa moyoni, ndio maana Mcha Mungu akautaja Moyo, na hakitajwi kitu chenye uzito kama moyo kikawa kitu cha upuuzi, lazima kuna faida kubwa kwa watakao kujua. Kwa fahamu zetu za haraka haraka tunafahamishwa moyo ni (Pump)inayo sukuma damu, ikisha tunaishia hapo hatutaki kwenda zaidi tukajua jee Moyo una siri gani kwetu sisi wanaadamu?.
Yapo mambo mengi yano pitikana katika Moyo ambayo wengi wetu hatuna habari nayo, Mcha Mungu aliposema "nilipogundua katika Moyo wangu anaweza kukaa asiye kuwa wewe" Haya ni maneno yalobeba siri kubwa ndani yake, na siri hii ina anza wiki tatu tu unapoanza kuumbwa katika(Umbo la kuonekana)mimba ikingia baada ya wiki tatu mpaka tano mapigo ya chombo hichi tayari yameshaanza kusikika na ambayo yataendelea mpaka mwisho wa umri(maisha)yako.
Kwa mtazamo wa nje moyo ni (Pump)inayosukuma damu, lakini kwa mtazamo wa Mcha Mungu anajua kuwa Moyo una kazi nyengine lakini mpaka uzinduke au upate(Uamsho)ndio unakutana  na hiyo siri ya utendaji wa kazi nyengine, na ukigundua siri hiyo ndio unakua, umefanikiwa, ushavuka na daima unakua Mcha Mungu lakini lazima siri hii akufunulie pazia Mollah mwenyewe na hapo inakua tabu tena kwa wewe kurejea katika ulimwengu wa maasi, shida za kidunia. Inakuaje chombo hichi chenye kudumu na sisi mpaka mwisho wa uhai wetu na hizo kazi za siri? Na siri gani alogundua Mcha Mungu hata akautaja Moyo?Wanasema wanasayansi kitu cha mwanzo kufanya kazi katika huo Moyo kinaitwa(Sino-Node)au(Electric-Conduction-System)huo ndio Moyo kitaaluma tunaishia hapo (Pump)inafanya kazi.
Lakini Mcha Mungu kakataa kuishia hapo, kaamua kwenda mbele zaidi kidogo ndio (akagundua kwenye moyo kuna nafasi ikiwa hakua makini nafasi hiyo yaweza kukaliwa na asiye kuwa Mollah wake, kuna wengine watashangaa mbona sasa anazungumza mambo mapya, mbona haya mageni, vipi moyo ukawa na kazi nyengine, naam hiyo ni kawaida walishangaa wenye kushangaa pale walipoambiwa maji ni (Gas)mbili na (formula)yake ni (HO2)lakini mshangao unakuja hapa, Mbona gas hizi mbili zipo lakini hazigeuki maji, Siri yake lazima ipatikane kitu cha tatu nayo hiyo (Elecricity)ndio kifanye hayo maji, Mcha Mungu yeye kaita (Rehma)Quraan-Anbiya-"وَجَعَلۡنَا مِنَ ٱلۡمَآءِ كُلَّ شَىۡءٍ حَىٍّ‌ۖ أَفَلَا يُؤۡمِنُونَ "
"Tukajaalia maji (Kwa)kila kilicho hai(Tulichokiumba), Jee hawaamini".
Naam hiyo iliyomo kwenye Moyo na kwenye maji lazima ipatikane sasa mnaulizwa jee hamuamini?, Kuwa mstahamilivu tuko tunamfata Mcha Mungu na maneno yake, usije ukahadaika na maneno ya Mcha Mungu ukaja kukwama kwenye maneno, bali chukua ujumbe uliomo kwenye maneno haya,"Nilipogundua katika huu Moyo wangu kwamba anaweza kukaa asiye kuwa wewe"jee unataka kujua undani wa maneno haya basi endelea-part-3




SHAIRI LA MCHA MUNGU-PART-3

Asalaam Aleiykum,

Jaribu kujikumbusha mfano huu wa kugundua au kupata(Uamsho)unapokua mzima wa afya hushughuliki na mguu wala mkono, hupati tabu ya kukumbuka meno wala masikio lakini wacha kimoja katika viungo hivo vipate maradhi utaona hapo (Attention)yote Akili yote inahamia hapo, deko lote linakuwepo hapo kwenye huo mguu, umeshapata kujiuliza kwanini? tega jicho uzuri tupo katika kuuchambua Moyo tupate siri zake ili tujue vipi tuna(Falling in  love)vipi tunapata hisia, inakuaje mahusiano haya na hii jinsi yangu mimi mwanaadamu, nini habari ya kipande hichi changu cha nyama kilichopo kwenye kifua changu.
Mcha Mungu kagundua Moyo ni chombo cha mawasiliano ya njia ya (Communion)inapata mawasiliano yake (Direct)au(Pure)mawasiliano haya iwe yanatokea huko kusikojulikana au hapa Ulimwenguni, yawe ya siri au dhahiri chombo hichi kina uweza wa kuya hifadhi iwe kwa kuona au kusikia.Ndio utaona Bwana Mtume s.a.w akaambiwa katika sura ya (Najm)"مَا كَذَبَ ٱلۡفُؤَادُ مَا رَأَىٰٓ""Moyo haukusema uongo (Kwa)uliyoyaona".
Kwani na wewe kuna mengi unayaona huwezi kuyakataa, hebu tizama Mfano huu wa mtoto mdogo, Analia, Anacheka ana hamaki na Akili yake bado haijakua, vitu hivyo vimetokea wapi, hakuna pengine isipokua Moyoni, hapo ndipo panapo kaa mapenzi, hisia, chuki, hamaki,furaha na imani na chochote kile kilicho husiana na hiyo (Communion)ndio maana utaona mfano huu kama una mgonjwa una uguza umekaa naye siku zote anapo kufa wewe wa karibu huzuni zako haziwi sawa na yule aliye mbali, kwa aliye mbali akiwasili anakua na huzuni kubwa sababu ya hiyo (Communion)ndio maana walimwengu wakasema unacho kitia moyoni taabu kukitoa, ndio Mcha Mungu akasema "nilipogundua katika huu Moyo wangu kumbe anaweza kukaa asiye kuwa wewe" mkapewa mfano katika Quraan vipi kitu kinaweza kuingia kikenda kukaa moyoni ili iwe alama kwenu.Quraan Aaraf-204,
" وَإِذَا قُرِئَ ٱلۡقُرۡءَانُ فَٱسۡتَمِعُواْ لَهُ ۥ وَأَنصِتُواْ لَعَلَّكُمۡ تُرۡحَمُونَ"
"Na Ikisomwa Quraan isikilizeni, Nyamazeni ili mpate kurehemewa".  hapo yametajwa mambo mawili la kwanza kusikiliza na la pili kunyamaza,Isikilizeni ili ipate kuingia kwenye moyo, usizungumze kwani ukizungumza haitokaa moyoni ipe nafasi itulie, ulipoambiwa nyamaza sio kwenye Akili unaendelea kuzungumza utakosa faida ya huko Kurehemewa, na kusudio la kurehemewa hapo ni hilo la (Uamsho), hivo wewe hujawahi kutengeneza kitu, au unafanya mtihani, au umeulizwa swali hujui jawabu lake umekaa una fikiri halafu ghafla linakujia jawabu, limetokea wapi, "Nilipojua katika huu Moyo wangu anaweza kukaa asiye kuwa wewe"hiyo ndio maana ya sikizeni na nyamazeni kimya yakiingia maneno ya Quraan katika nyoyo zenu yaka kaa basi tena hugeuka Imani na huko ndiko kurehemewa kuna patikana kwa njia ya sauti.
Endelea-part-4

SHAIRI LA MCHA MUNGU-PART-4

Asalaam Aleiykum,

Sauti, jamani sauti ni nyenzo kali sana sababu inapenya moja kwa moja haina kizuizi, macho unaweza ukafunga au usitizame lakini sauti hata ukiziba masikio inapenya moyoni, ndio maana wakaambiwa enyi wanawake teremsheni sauti zenu kwa kuwa zinamtoa nyoka pangoni, zinakata maini msije mkazipandisha sababu zinakwenda kukaa moyoni. Na huu moyo una sifa zote mbili za kuona na kusikia, vipi kwa wewe mwanaadamu wa kawaida kadhia hii inatokea kwako, pengine unaona kwenye nchi yako au nyumbani kwako maasi yamekithiri lakini una yapuuza, basi elewa bado yangali machoni, lakini matendo hayo yakishuka moyoni unakua huwezi kustahamili tena, sababu yanakuumiza, sasa utachukua hatua moja katika mbili hizi kama shujaa utaamua kuanza kazi ya kuyaondosha, na kama dhaifu utaona unaanza kusema chini kwa chini, bali elewa yote hayo mawili ni hijaza ilotoka kwa Mollah wako wala usifanye kazi ya kuanza kuitoa moyoni kwako kwani utakua mmoja katika hao maelfu walopotea.
Ukipata uzinduo huo wa kujua kwa moyo sasa inabidi ujiunge na wafuasi wa aya hii:Quraan-As-saff-"11"
"تُؤۡمِنُونَ بِٱللَّهِ وَرَسُولِهِۦ وَتُجَـٰهِدُونَ فِى سَبِيلِ ٱللَّهِ بِأَمۡوَٲلِكُمۡ وَأَنفُسِكُمۡ‌ۚ ذَٲلِكُمۡ خَيۡرٌ۬ لَّكُمۡ إِن كُنتُمۡ تَعۡلَمُونَ"" Muamini Mwenye-enzi-Mungu na Mtume wake, na piganieni dini ya Mwenye-enzi-Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu, hayo ni bora kwenu, ikiwa mnajua."
Kwanza imeanza Imani lazima utumie huo Moyo kujaza mawili hayo, ikisha upigane kwa njia ya Mollah wako, kwanza kwa hiyo Mali yako uliyoichuma, jijue wakati wowote unaweza kufa ikarithiwa na wengine wakaifuja kwa njia ya dhanbi, basi anza mwenyewe kuitoa kwa mambo ya kheri,sio unachangia mambo ya harusi na chakacha na kukandamizwa waislam wenzio, wewe toa katika kuondosha mambo machafu, halafu na nafsi yako nenda moyoni kama alivo kwenda kugundua Mcha Mungu, nini kagundua Mcha Mungu. "Nilipogundua katika huu Moyo wangu anaweza kukaa asiye kuwa wewe, nilifanya jitihada za kujaza uongofu utokao kwako mpaka nika hakikisha hakai mwengine asiye kuwa wewe"Mcha Mungu kagundua Mapenzi yanakaa moyoni(kapewa taaluma hii)"Ukipenda nchi unaitia moyoni,ukipenda mali unaitia moyoni,ukimpenda mtu unamtia moyoni"kumbuka chochote kile unachokipenda lazima kikae moyoni na wewe kifanyie uchunguzi utakuja kugundua kama alivojua Mcha Mungu, Na wanasema wajuzi wa mambo ya lugha, huwezi kupenda viwili na mapenzi yakawa sawa, basi ukiona kitu hakimo moyoni fanya hima ukijaze katika moyo wako, na wewe ndio utachagua kitu gani kikae kwenye moyo wako.endelea part-5


SHAIRI LA MCHA MUNGU-PART-5

Asalaam Aleiykum,

Ikiwa utaamua kumpenda Mollah wako ukamtia moyoni basi hurejeshewa wewe mapenzi ukaruhusiwa kwa mapenzi hayo kuvipenda vyengine huku ukiridhiwa na Mollah wako na wala hakuna dhara itakayo kufika." Alikwenda kutembelewa Mcha Mungu Aitwaye bibi Rabbiya bint Adwiyya, yule mwenziwe alipofika aliomba Quraan ili asome kama ilivo kawaida yake, alipofika katika aya inayosema Hakika (shetani) ni adui aliye dhahiri, ikawa yale maandishi yamefunikwa, akamuuliza Ewe Rabbiya hili ulofanya ni kosa kufunika aya ya Quraan, kwanini umefanya hivi, akajibu bibi Rabbiya nimeujaza moyo wangu mapenzi ya Mollah wangu hata huyo Shetani akija na uadui wake basi hawezi kunipotosha, mimi simuogopi wala simchukii kwa kuwa hakuna tena nafasi katika moyo wangu hata wakukaa hiyo chuki".
Usije kumshangaa Bibi Rabbiya hata na wewe unafanya hayo hayo akikujia Mume kalewa humuogopi wala humchukii, akikujia mwanao jambazi humuogopi wala humchukii unaishi naye, tafauti yako na Bibi Rabbiya yeye kajaza mapenzi ya Mollah wake na wewe ni mweupe huna kitu moyoni, tahadhari sana nafasi hiyo isije kukaliwa na asiye kuwa Mollah wako.Usije ukawa katika kundi la wale wenye kulinda maasi,uovu na madhila hao wanakua na upofu wa moyo na wanabakia daima katika utumwa wa dunia.Na kumbuka jambo lolote linalopita shikioni likikaa moyoni linageuka kuwa jicho na ukipewa uweza wa kuona kwa kutumia moyo basi huko ni kufuzu kuliko kukubwa, pia napenda uelewe moyo ni jicho linalo kukurubisha zaidi kwa Mollah wako, na hiyo ndio (Communion)ilokufunga wewe na uhai, chochote ukitaka kujulishwa lazima kipitie huko moyoni, chunguza pumzi zako zinatokea wapi, zinakwenda wapi na kwenye nini, ukisha kujua hayo utaanza kulijua shairi la Mcha Mungu na kusudio lake.
Na yoyote yule mwenye kuusafisha Moyo wake kwa Tohara za Ibadah na kumkumbuka Mollah wake kwa wingi basi hufunguliwa jicho la moyo ukawa unaona na kujua mambo ya shani ya Mollah wako pasi na kizuizi, halifungani jicho hili na elimu yako ulo nayo wala ujuzi bali lenyewe hupokea moja kwa moja kutoka kwa Mjuzi aliyeumba.
"إِنَّمَا ٱلۡمُؤۡمِنُونَ ٱلَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ ٱللَّهُ وَجِلَتۡ قُلُوبُہُمۡ وَإِذَا تُلِيَتۡ عَلَيۡہِمۡ ءَايَـٰتُهُ ۥ زَادَتۡہُمۡ إِيمَـٰنً۬ا وَعَلَىٰ رَبِّهِمۡ يَتَوَكَّلُونَ "
Hakika wanaoamini kikweli ambao anapotajwa Mollah wao hujaa khofu katika nyoyo zao, na wanaposomewa aya zake huzidi imani,na kwa Mollah(wao) wakamtegemea (kwa yote).
"Nilipogundua mimi kwamba katika moyo wangu anaweza kukaa mwengine yoyote asiye kuwa wewe, nilifanya jitihada kuujaza uongofu wako mpaka akawa hawezi kukaa mwengine yoyote asiye kuwa wewe"."لما  علمت بأن قلبى فارغ----ممن سواك ملأته بهداك-----وملأت كلى منك حتى لم أدع ------منى مكاناً خالياً لسواك"
Abdulla Baja