Asalaam Aleiykum,
Hakuna jambo ambalo mwanaadamu anajihadaa kama kujinasib ana amini, ikisha ndani ya nafsi yake akawa anajua moyoni mwake hakuna hata chembe ya (Imani)Darsa yetu ya leo inagusa pahala penye uchokozi, tunakwenda kupachokoza pahala hapo ili upate kujua kumbe mimi siamini chochote, leo kamata kipimo chako ujue thamani ya Imani yako, halafu mwisho jiulize hivyo mimi naamini au nimejaa wasiwasi tu.
Ili kukufanyia urahisi wakujua tafauti ya Mtu alokua hana Imani na Mwenye Imani nimekuchagulia visa hivi viwili ili vitufungulie darsa yetu ya leo, visome kwa umakini halafu utajiamulia mwenyewe ingekua wewe kundi lipi ungetamani kujiunga nalo. Hebu jikumbushe visa hivi viwili vimetokea katika miji tafauti, kimoja kimetokea katika mji wa (Lindi)ambapo walimaliza waumini kadhaa wakiislam kusali ikisha wakakaa Barazani, akatokea Mtu mmoja kashika panga mkononi akauliza ghafla jee hapa pana Muislam yoyote, waliopo pale barazani kwa khofu wakatingisha vichwa kuashiria hakuna Muislam huku kila mtu anatetemeka kwa khofu, yule Mtu akashika njia akenda zake, baada ya nusu saa akatokea kwa mbali huku panga lake limejaa damu anakuja haraka haraka, Barazani hakukaa mtu, walisema walokaa pale huyo yule jamaa sasa anarudi tumekwisha anarudi kuulizia kama kuna mkiristo miongoni mwetu, kumbe maskini yule Mtu alivouliza mwanzo alikua anataka akachinjiwe Ngombe wake kwa sheria za kiislam, na hii mara ya pili anarudi ili kuwaomba watu wakachukue sadaka ya nyama alipofika karibu kaikuta baraza nyeupe. Hizo ndizo zilivo Imani zetu, tukiulizwa una Amini tunatingisha vichwa kuashiria ndio, kumbe moyoni hapana kitu, Sala zote mtu anakwenda kusali kwa kuogopa moto tu, na wala si kwa ajili ya Mwenye-enzi-Mungu wake, hivyo ndio wengi Imani zetu zilivyo.
Na kisa cha Pili hiki kimetokea katika mji wa Basra kule Iraq, siku moja Darweish mmoja alikua ameketi (Zawiyyan)kwenye nyumba ya Ghorofa moja, alikua amezama katika hali ya (Wajid)kapotea kwa Mollah wake kwa ajili ya Ibadah, Darweish yule akawa anazungumza na Mollah wake "Anasema""Ewe Mollah wangu nijaribu mimi kwa chochote katika mitihani yako ili nipate kujipima mimi mapenzi yangu juu yako wewe, na mimi nafahamu mtihani wako unakuja kwa njia tafauti pasi kuwa na sababu yoyote,naomba mimi hilo ili nipate kuridhika, anamaliza kauli yake hiyo huku chini wanapita vijana na (Rika)zao wanaimba kasida hii""Kama kweli mpenzi wa Mungu chupa ujiunge nasi"(KAMA KWELI MPENZI WA MUNGU CHUPA UJIUNGE NASI)hawajamaliza mara ya tatu maneno haya mara wanamuona Darweish anazunguka na majuba hewani kutokea Ghorofani kajiachia, alipofika chini vijana wote wakakimbia Darweish huyo akakusanya majuba yake akarejea ndani ya nyumba yake bila ya kuumia hata kiungo kimoja.
Hiyo ndio Imani,. Sasa ikiwa leo na wewe mpenzi wa Mungu basi chupa ujiunge nami ili tupate kuzijua Imani zetu zikoje ili kama dhaifu tupate kuzifanyia kazi. Kumbuka katika safari hii hatakiwi mwanasiasa, au msomi, au mfanyabiashara au mpiga porojo anotakiwa katika safari hii ni yule mpenzi wa Mungu mwenye kutaka kujua Imani yake, na huko upande wa pili kuna nini? na kwanini mimi simo kwenye kundi la wenye Imani?Endelea Part 2
No comments:
Post a Comment