Saturday, November 24, 2012

BALAA ZA UJANANI PART-1

Asalaam Aleiykum,

Nakushukuru Mollah wangu kwa kunipa siku nyengine ya Uhai nikaweza kukutukuza kwa zawadi hii Adhim, Nakushukuru Mollah wangu nimeamka nikiwa Hai naweza kuvuta pumzi, Naweza kutembea, Naweza kuijua Familia yangu na nikiwa mzima wa Afya.
Leo hii Mollah wangu ungetaka ningekuwepo kaburini kama walivyo tangulia walopita kabla yangu, Lakini kutokana na uweza wako bado hujanihitaji Mollah wangu, Na hayo yote si kwa mahitajio yangu mimi , Mimi sina amri kwa hilo, hichi ni kitu ulonikirimu wewe pasi mimi kuomba, Umenipa uhai huu kwa ridhaa yako na mapenzi yako juu yangu, Basi kwa hilo sina budi mimi ila ni kukushukuru na kukumbuka kila wakati Mollah wangu.
Leo tena umenipa fahamu na uwezo nitaweza kula na kunywa, Nitaweza kuwaona wanangu na wote walo wangu na marafiki zangu, Nitaweza kutoka na kurudi kwa salama nyumbani kwangu bila ya khofu yoyote ile. "Ewe Mollah wangu hakika umenipa Uhai huu wakati mimi sikua na thamani yoyote ya kupewa zawadi hii, Umenidiriki nivute pumzi hizi bila ya tabu wakati mimi nikiwa katika hali ya kukuasi Mollah wangu katika ujana wangu, Na unaendelea kunikirimu Neema hii hali naendelea kukuasi hata sasa katika uzee wangu lakini wewe upo katika hali ya kunipa nafasi labda leo au kesho nitakukumbuka Mollah wangu ili upate kunisamehe".Umenipa mimi furaha na afya wakati ule nilipo kukimbia nikawa sikukumbuki hata sekunde moja, yote hayo Mollah wangu umenisubiria, sasa sina mimi ila kujawa na shukurani katika moyo wangu na nimeridhia lolote lile litakalo nifika basi najua pengine ni mambo niliyofanya Ujanani ni makosa yangu mwenyewe ya kushindwa kujichunga wakati wa Ujana wangu ndio yalo nifikisha hapa nilipo.
Nikipata maumivu ya mwili au kero za Akili basi najua hili nimelisababisha kwa makosa yangu ya kupotea katika njia yako ya uongofu, Na mimi mwenye kukumbuka yale yote nilotenda katika Ujana wangu kama ulivosema katika kitabu chako kitukufu sura ya Qiyama aya ya 13" بَلِ ٱلۡإِنسَـٰنُ عَلَىٰ نَفۡسِهِۦ بَصِيرَةٌ۬ ""Bali mwanaadamu ni shahidi juu ya nafsi yake"
Nilikua mimi mchapaji wa mtindi (ulevi),Nilikua mimi sitoki vilabuni,Nilikua mbele ya hadhara ya watu nikipanda kwenye kiti nacheza viuno huku wengine wakinipigia makofi na wengine wakinitizama kwa matamanio sote tukitenda makosa lakini mimi ndio nilikua sababu ya kosa hilo.Nilikua nikivuta madawa ya kulevya, Nilikua nikiiba Serekalini na nikiona kama jambo la kawaida,Nilijiunga na vikundi vya uzinifu na kwangu ikawa kama jambo la kawaida, nilikua nadhulumu watu na kuwapiga nikisahau kabisa kuwepo kwako Mollah wangu, Najua yote hayo yapo hayajafutika na mengine naendelea kuyatenda sijui hali yangu itakuaje wakati utakapofika wa sasa wewe kunihitaji Mollah wangu ili nije kukutana na wewe. Na wewe utaniuliza kwani Mjumbe wangu hakusema lolote kuhusiana na Kadhia hii ya Ujana?-Endelea part-2

No comments:

Post a Comment