Thursday, November 1, 2012

SHAIRI LA MCHA MUNGU-PART-5

Asalaam Aleiykum,

Ikiwa utaamua kumpenda Mollah wako ukamtia moyoni basi hurejeshewa wewe mapenzi ukaruhusiwa kwa mapenzi hayo kuvipenda vyengine huku ukiridhiwa na Mollah wako na wala hakuna dhara itakayo kufika." Alikwenda kutembelewa Mcha Mungu Aitwaye bibi Rabbiya bint Adwiyya, yule mwenziwe alipofika aliomba Quraan ili asome kama ilivo kawaida yake, alipofika katika aya inayosema Hakika (shetani) ni adui aliye dhahiri, ikawa yale maandishi yamefunikwa, akamuuliza Ewe Rabbiya hili ulofanya ni kosa kufunika aya ya Quraan, kwanini umefanya hivi, akajibu bibi Rabbiya nimeujaza moyo wangu mapenzi ya Mollah wangu hata huyo Shetani akija na uadui wake basi hawezi kunipotosha, mimi simuogopi wala simchukii kwa kuwa hakuna tena nafasi katika moyo wangu hata wakukaa hiyo chuki".
Usije kumshangaa Bibi Rabbiya hata na wewe unafanya hayo hayo akikujia Mume kalewa humuogopi wala humchukii, akikujia mwanao jambazi humuogopi wala humchukii unaishi naye, tafauti yako na Bibi Rabbiya yeye kajaza mapenzi ya Mollah wake na wewe ni mweupe huna kitu moyoni, tahadhari sana nafasi hiyo isije kukaliwa na asiye kuwa Mollah wako.Usije ukawa katika kundi la wale wenye kulinda maasi,uovu na madhila hao wanakua na upofu wa moyo na wanabakia daima katika utumwa wa dunia.Na kumbuka jambo lolote linalopita shikioni likikaa moyoni linageuka kuwa jicho na ukipewa uweza wa kuona kwa kutumia moyo basi huko ni kufuzu kuliko kukubwa, pia napenda uelewe moyo ni jicho linalo kukurubisha zaidi kwa Mollah wako, na hiyo ndio (Communion)ilokufunga wewe na uhai, chochote ukitaka kujulishwa lazima kipitie huko moyoni, chunguza pumzi zako zinatokea wapi, zinakwenda wapi na kwenye nini, ukisha kujua hayo utaanza kulijua shairi la Mcha Mungu na kusudio lake.
Na yoyote yule mwenye kuusafisha Moyo wake kwa Tohara za Ibadah na kumkumbuka Mollah wake kwa wingi basi hufunguliwa jicho la moyo ukawa unaona na kujua mambo ya shani ya Mollah wako pasi na kizuizi, halifungani jicho hili na elimu yako ulo nayo wala ujuzi bali lenyewe hupokea moja kwa moja kutoka kwa Mjuzi aliyeumba.
"إِنَّمَا ٱلۡمُؤۡمِنُونَ ٱلَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ ٱللَّهُ وَجِلَتۡ قُلُوبُہُمۡ وَإِذَا تُلِيَتۡ عَلَيۡہِمۡ ءَايَـٰتُهُ ۥ زَادَتۡہُمۡ إِيمَـٰنً۬ا وَعَلَىٰ رَبِّهِمۡ يَتَوَكَّلُونَ "
Hakika wanaoamini kikweli ambao anapotajwa Mollah wao hujaa khofu katika nyoyo zao, na wanaposomewa aya zake huzidi imani,na kwa Mollah(wao) wakamtegemea (kwa yote).
"Nilipogundua mimi kwamba katika moyo wangu anaweza kukaa mwengine yoyote asiye kuwa wewe, nilifanya jitihada kuujaza uongofu wako mpaka akawa hawezi kukaa mwengine yoyote asiye kuwa wewe"."لما  علمت بأن قلبى فارغ----ممن سواك ملأته بهداك-----وملأت كلى منك حتى لم أدع ------منى مكاناً خالياً لسواك"
Abdulla Baja

No comments:

Post a Comment