Sunday, December 29, 2013

DAWA YA DHIKI PART 1

Asalaam Aleiykum,

Binaadamu yanatupata matatizo makubwa pale tunaposhindwa kutafautisha Baina ya Matatizo na Dhiki, Matatizo ni kitu cha nje, Matatizo ni majambo katika mambo ya Maisha, Lakini Dhiki ni yenye kuishi kwenye hiyo (Roho) yako, Na kaa ukijua mwenye Dhiki hana Raha ya Maisha, Ujaji wa Dhiki unakuja mfano uleule wa Matatizo, kama, yaweza kuwa Una Dhiki ya Mapenzi, au Dhiki ya utafutaji wako wa Riziki, mbona mambo hayendi, unaweza kuwa na Dhiki ya Moyo mambo yamekujaa na hujui utayatoa vipi, unaogopa kumhadithia mtu, kumbuka hayo yote yamo ndani ya (Nafsi) yako.
Sasa itabidi ujiulize ilikuaje hata ukafikia hali kama hiyo, huna haja ya Hadith wala kisa cha zamani eti ndio yakujulishe vipi umefika hapo, huna haja ya kwenda kwa Mmasai au kwa (Babu) ili upatiwe Dawa, kumbuka Dawa unayo mwenyewe, na kazi yangu mimi ni kukumbusha umeiweka wapi hiyo Dawa, ufanye nini utoke kwenye Dhiki, lakini utatokaje kabla ya kujua njia?
Ipi njia yenyewe, ni hiyo ya kuijua Dhiki ukaweza kuitafautisha na matatizo. Nini matatizo? Matatizo yanakuja kwa Kutamani, ikawa hichi unataka na kile unakitaka, unakua na (Ambitions) za kila aina, hivyo ndio kujitia kwenye matatizo. Nini Dhiki? Dhiki ni kuhitaji(Mahitaji)Unahitaji Raha, Unahitaji (Blissful life) Unahitaji Ku(Surrender)unahitaji utulivu, unahitaji (Normality)au tuite (Balance). kwanini sasa mambo yako yameharibika mpaka umefikia unaishi ndani ya Dhiki? sababu ziko na wewe mwenyewe ndiye muanzilishi, wewe ndie mtengenezaji wa hiyo Dhiki, na kabla hatujenda mbali wacha nikukumbushe kitu labda huwenda ukajua ama kweli Dhiki nimejitakia mwenyewe. Wacha nikujulishe Sheria ilopangwa na Mwenyewe aliyeumba Ulimwengu, Anasemaje kupitia Kwa Mja wake alompa Hekima Luqman a.s (Sura ya Luqman aya ya 16.
 يَـٰبُنَىَّ إِنَّہَآ إِن تَكُ مِثۡقَالَ حَبَّةٍ۬ مِّنۡ خَرۡدَلٍ۬ فَتَكُن فِى صَخۡرَةٍ أَوۡ فِى ٱلسَّمَـٰوَٲتِ أَوۡ فِى ٱلۡأَرۡضِ يَأۡتِ بِہَا ٱللَّهُ‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ لَطِيفٌ خَبِيرٌ۬
"Ewe Mwanangu Kwa hakika jambo lolote (Japo)liwe na uzito wa(Atom)chembe ya Hardali, likawa(Limetendeka au kufichwa)ndani ya Jabali au Mbinguni au Katika Ardhi, Mwenye Enzi Mungu atalileta (Na Kumlipa aliyelitenda),Hakika Mwenye Enzi Mungu ni Mwenye kujua (mambo) yalofichikana na (Mambo)yalodhahiri".
Kaanza kupewa Onyo mtoto sababu bado hajaingia kwenye Dhiki, Bado hajalimbikiza mali au mambo ya kidunia anaambiwa kaa ukijua chochote kile utendacho lazima ulipwe, na hiyo ndio sheria ya Mwenye Enzi Mungu lazima itekelezwe. Sasa vipi wewe umefikia katika hali hiyo ya Dhiki? Endelea part 2

DAWA YA DHIKI PART 2

Asalaam Aleiykum,

Kwenye hiyo aya imetajwa chochote ili usije kudhani labda vyengine havimo. Sasa Dhiki ina Pande mbili kama ilivo Shilingi, Upande wa kwanza una maandishi ya (kuhitaji)kuna kitu (Missing)lakini hukijui nini?, Na upande wa Pili kuna maandishi Dhiki ni Kapu la Dhanmbi, Dhiki haiji lazima kuna majanga unayatengeneza(Lazima unakwenda Shopping na kapu lako), na sasa matokeo yake kapu limejaa ndio maana unasikia (Dhiki).
Vipi unakua mpaka kufikia (Stage)hiyo, hapa nitaitaja mifano miwili mitatu na mengine utaongezea mwenyewe, na Mengine itakua (Surprise)lakini kwa kuwa ni sehemu ya Dhiki itabidi niitaje ili tupate faida yake. Vipi unaanza kuchuma Dhiki kwenye Nafsi yako? kumbuka huko nyuma umesoma kila kitu kinalipwa, sasa pengine unamtania mtu na yeye hapendi, hapo tayari ushachuma Dhiki, pia kumbuka Dhiki ni kitendo baina ya Nafsi kwa Nafsi, Ukiikera Nafsi na wewe malipo yake unapewa Dhiki, Unamsengenya mtu, mbali ya kuandikiwa Dhanmbi pia unapewa na Dhiki(Na mfano tizama kama ghafla atatokea huyo unomsengenya unakua vipi)hilo ndilo chumo la Dhiki, Unawatesa viumbe wenzio na wewe unapewa Dhiki, Unatamani Mke au Mume wa Mtu, huku kwa nyuma unapewa(Double dose)ya Dhiki na matatizo, Wewe Tajiri unaonea na kuwadhalilisha wafanyakazi wako, huku na wewe unapewa Dhiki huna Raha, Wewe kiongozi unaonea unaowaongoza huku unapewa Dhiki unakua huna Raha Kabisa, Hata ukimuona Nyoka maskini anakukimbia anaelekea shimoni kwake, ukaamua kumpiga akafa, basi na huku unapewa Dhiki kwani na yeye ana haki ya kuishi kama ulivo wewe.
Na Kubwa zaidi ni hili umeshakusanya Dhiki sasa zimekujaa (Tafrani)imekushika ghafla unaamua kumbe kuna kitu kinaitwa Sala, unaingia Dini kwa mikiki, sasa mahitajio yako yote ni (Pepo)ya (Express)tizama madhara ya Dhiki zako unavofanya katika Ibada zako, la kwanza inakua watu wote walosali miaka yote wanakua hawajui kusali, lazima uwafundishe tena, unakuja na hasira na jazba kubwa kabisa, unajua kwanin,i ni ile ile Dhiki inakutesa, kwanza ilikua katika Dunia sasa imehamia kwenye Akhera, ndio maana utaona matendo yako japokua mazuri lakini yamejaa chuki, mafundisho yako yanaweza kuwa yanafaa lakini kwa jinsi unavo yatoa yamejaa Dhiki, kwa hiyo inakua hasara juu ya hasara, Na unajua hayo yote ni kwa sababu gani? Ni kwa sababu unataka upate(Attention)Kwanini? kwa Sababu pengine mwanzo watu walikua wanakujua kwa sifa fulani na sasa unataka ujulikane kwa sifa ya (Ucha Mungu)hiyo ndio kazi ya Dhiki kwa Jumla, na wewe fanya Uchunguzi utayajua vizuri sana, chunguza Dhiki zako zinatokana na nini, lazima kuna (Source)fulani inayokusababishia hiyo Dhiki.
Jitizame mie mbona hivi nakerwa kazini hamaki zangu namalizia Nyumbani, kwanini upo katika hali kama hiyo, Unakerwa na watu wazima unawakasirikia watoto inakuaje hali hiyo, Sasa jiulize nini kinachokufanya usiwe katika hali ya kawaida alokupangia Mwenye Enzi Mungu wako, Basi ikiwa Mja umo katika hali ya Dhiki elewa unahitaji Dawa, Na Dawa gani utatumia ili Dhiki zikutoke.Endelea Part 3

DAWA YA DHIKI PART 3

Asalaam Aleiykum,

Nini cha kufanya mpaka urejee katika hali ya kawaida, Unatakiwa uwe tayari na ujitaarishe kumeza kidonge ambacho ukikimeza tu, kinaanza kazi yake ya kukuponesha, na unakipata kidonge hicho kwenye Quraan sura ya Hashir aya ya 18 na 19.
يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ ٱتَّقُواْ ٱللَّهَ وَلۡتَنظُرۡ نَفۡسٌ۬ مَّا قَدَّمَتۡ لِغَدٍ۬‌ۖ وَٱتَّقُواْ ٱللَّهَ‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ خَبِيرُۢ بِمَا تَعۡمَلُونَ 
"Enyi Mloamini Mcheni Mwenye Enzi Mungu, Na kila Mtu aangalie, (Atizame)(Be Witness)anayoyatanguliza kwa ajili ya kesho, Na Mcheni Mwenye Enzi Mungu, Hakika (Yeye)anazo habari za mnayoyatenda"
Imetajwa kumcha Mungu kwenye aya hiyo mara mbili, Mara ya kwanza ni kuzinduliwa kuwa umeze kidonge cha Ucha Mungu, halafu uwe Shahidi kwa matendo yako, moja baada ya moja, kwa ajili ya kesho(Akhera)na kesho hapa hapa duniani utizame (Chain of Reaction)ukifanya sasa hivi tizama baadae itatokea nini(Be Witness)utajua kinatokea nini, Na ukianza kutizama matendo yako kidogo kidogo Dhiki inapotea kwani hiyo Dhiki imeingia moyoni kwako baada ya kugundua upo (Empty)nafasi iwazi.
Na kutajwa mara ya pili kuwa ukianza Kumcha Mollah wako ukawa shahidi wa vitendo vyako, Dhiki inapotea kwa ajili hutendi maovu, na kila wakati unakua kwenye kuelewa Mollah wako ni mwenye kukuona na hiyo ndio (Taqwa), na hicho ndio kitu kinachopungua katika maumbile yako, na kikipungua tu, unakaribisha Dhiki ikutawale ndio maana ukaambiwa kwenye aya inayofatia.

وَلَا تَكُونُواْ كَٱلَّذِينَ نَسُواْ ٱللَّهَ فَأَنسَٮٰهُمۡ أَنفُسَہُمۡ‌ۚ أُوْلَـٰٓٮِٕكَ هُمُ ٱلۡفَـٰسِقُونَ
"Wala msiwe kama wale walomsahau Mwenye Enzi Mungu, Na (Mwenye Enzi Mungu)Akawasahaulisha Nafsi zao, Hao ndio waasi wakubwa"
Kumsahau Mwenye Enzi Mungu ndio huko kukaribisha matendo ya Dhiki, Na ukimsahau Mwenye Enzi Mungu na yeye anakusahaulisha kuwa yeye yupo na dawa yako ya hiyo Dhiki ni Ucha Mungu, Nafsi inasahau kabisa ndio unaendelea kuteseka na unazama katika Bonde la maasi, usijione mbona mimi nasali na Dhiki bado ninazo,(No)Mwenye Enzi Mungu kakupa (Challenge)jitizame wewe Una Sali au unafanya mazoea(Hata kasuku akizoea Ata sali)itizame Sala yako kweli unaipeleka ipasavyo.
Basi hichi kidonge cha kwanza utakunywa kutwa Mara 5 nacho hicho cha (Taqwa), ukiitia moyoni mwako ukaitenda kwa (Ikhlasi)basi utakua ushaanza kupata ponesho la Dhiki, kwa Sababu penye Taqwa Dhiki haikai. Sasa kwanini inakaa? Sababu hitajio lako kubwa ni Taqwa, na wewe hilo umelitupa hulitaki, unalichukia au kama unafanya kwa ajili umemsikia Sheikh fulani kautaja Moto, na wewe unauogopa ndio unaanza kusali, lakini hupeleki Sala yako kwa ajili ya mapenzi ya Mollah wako, nakupa mfano huo ulotajwa utazame matendo yako hapo juu, jitizame ukitoa sadaka au kumsaidia mtu wewe unafanya kwa ajili  gani, la kwanza utagundua hufanyi kwa ajili ya Mollah wako sababu kwenye moyo wako hakuna linalotokezea, la Pili utaelewa unafanya kwa ajili ya kitu fulani, na la Tatu hakuna Hisia unafanya (Empty Heart)Na ukiona hivyo elewa Dhiki imejificha kwenye moyo wako, ndio maana Bwana Mtume s.a.w akaashiria mara tatu kwenye kifua chake na kusema (Taqwa)ipo humu, Nenda Moyoni ukagundue kinatokezea nini ili upate jawabu lako.
Na ukiipata Taqwa hapo unapewa kidonge cha Pili cha siri bila mwenyewe kujua unaona Dhiki imetoweka umekua mja wa furaha, ukiona Ndege anaimba wewe unacheka na dawa yenyewe ni hii (Alam-Nashrah aya ya 5)

فَإِنَّ مَعَ ٱلۡعُسۡرِ يُسۡرًا
"Basi Hakika baada ya Dhiki Faraji"
Faraji ndio maumbile yako, usikubali kabisa kuishi kwenye Dhiki, hama utoke kwenye Dhiki uende kwenye Taqwa, ukutane na faraj, faraji ndio afya, faraj ndio mapenzi, faraj ndio (Nature) yetu, usikubali kinyume cha hayo, Na Mollah wetu atatusaidia kuipata Faraj.


Sunday, December 22, 2013

UJUMBE WA MAREHEMU PART 1

Asalaam Aleiykum,

Nani Marehemu?
Yoyote yule alotangulia mbele ya haki ndiye Marehemu, Na yule Alobaki katika Ulimwengu huu mimi na wewe tunoishi kwa hivi sasa sisi sote ni (Rahima) wenye Rehma. Na wale walotangulia ni wenye Kurehemewa, na hilo ndio lililotufanya sisi kumwita alotangulia Akhera ni Marehemu.
Mwanaadamu yaweza kuwa una Baba au Mama katangulia kwa Mollah wake, Iwe Dada au kaka yako, awe Mwanao au ndugu yako, na iwe Rafiki ili kuipima Dini yako wakati huu ulonao, kujua kama unazo fikra za Akhera basi inapasa kujiuliza mara ngapi  kwa siku au miezi  unawakumbuka walo wako, Jiulize jee wanatakiwa kukumbukwa? Nafahamu uzuri unajitahidi kusoma magazeti hayakupiti, vitabu vya historia umevihifadhi wewe, unakumbuka mambo ya zamani, Mababa wa Taifa unawakumbuka wewe, unakumbuka waanzilishi wa chama chako, unamkumbuka mwanasayansi fulani, lakini ni mwiko kwako kuwakumbuka walio karibu na wewe kwa dua ya maombezi, jua hao kuna  mahusiano ya mazazi juu yako.
Vipi wewe huwakumbuki wale wenye ukuruba wa kidamu juu yako, kumbuka mara ya mwisho lini umempelekea Rehma za Dua, kwa sababu huko kuzungumza kwako ni Rehma, na ukipeleka maombi basi unakua umepeleka Rehma(Mfano)wa(Recycle). Usije kubisha unajua umekata mawasiliano miaka mingi ilopita, Imekusahaulisha nafsi yako na kuamini yule mtu keshaoza kaburini, Na wala hahitaji kukumbukwa, kitu kimoja nakukumbusha kilicho kufa na kuzikwa ni kiwiliwili chake tu, lakini Roho yake iko hai kwenye Ufalme wa Mwenye enzi Mungu, Na hufurahi Roho hiyo ikiwa utaikumbuka kwa kuitakia (Msamaha au kuiombea Makaazi mema). Na zile Roho ziloishi na kupita kwenye Ulimwengu huu kwa kujisalimisha kwa Mollah wao basi nazo hupewa Radhi za Mollah wao na kupata fursa ya kuwasiliana na walio karibu nao katika mahusiano ya Kiroho.
Na wale ambao wamepita katika Ulimwengu huu wakafanya Shari za kupindukia na wao pia hupewa nafasi za kuwaonesha walo wao mambo yanayo wakuta huko walipo ili wawakumbushe jamani wee huku kumoto, tutupieni Dua japo siku kati ya masiku. Sasa vipi mawasiliano haya yanafanyika, Vipi wanatuma ujumbe huo ili ikufike wewe msomaji, kwa kutaka tujue kama kweli (Communication)inafanyika wacha tumuulize Allamah Muhammad bin Sireen R.A atueleze kuhusu kadhia hii "Anasema yapo mawasiliano baina ya waliyo hai na walio kufa""Na chochote kile anacho kufahamisha maiti kwenye (Ndoto)basi ujue ni cha ukweli, sababu wao wako mbele ya haki na hawasemi uongo.
Kwa hiyo Ukimuona Maiti yako anakwambia "Ewe Mwanangu au Rafiki yangu huku mwenzio makwaju ya fimbo za moto yamenizidi au minyororo ya shaba za moto zinaniumiza, au chumba hichi cha moshi mzito sikiwezi kinaniadhibu sana basi jua maiti yako hiyo inahitaji dua zako, ndio maana ya kukuhadithia mambo hayo, sio kama anakutisha, fanya haraka umpelekee dua zako, muombee kwa Mollah wako asaa huwenda akapata shufaa, usisubiri mtu akakwambia inafaa au haifai, wewe peleka usiweke wakili baina yako na Mollah wako, alipokuumba hakuwepo yoyote kwanini sasa hivi azuke mtu kukufundisha wakati gani wa kuwasiliana na Mollah wako, Pengine huyo Maiti kaomba nipeni nafasi labda fulani, huwenda mwanangu fulani yeye kashika Ibada huwenda nikaipata shufaa, asaa Mollah wangu aweza kukubali maombi yake, nipeni nafasi, kule anapewa nafasi wewe huku unashangilia pengine mpira au harusi mambo hayo sasa. Endelea part 2

UJUMBE WA MAREHEMU PART 2

Asalaam Aleiykum,

Lazima Mtu atahadhari sana katika Ulimwengu huu, Aangalie vipi anaishi maisha yake, akumbuke kuna masiku mazito mbele yake wala si mchezo, Anaendelea Allamah wetu kutujuza yakwamba mawasiliano yapo ndio maana wakati mwengine mgonjwa akiwa taabani kazimia akija juu anasema nimewaona Bibi na Babu wamekuja nipokea, Anasema Allamah wetu"(Ukiona)au kuota Mtu alokufa anaingia kwenye nyumba basi jua ima maradhi yatakaa kwa muda mrefu au mgonjwa atakufa karibuni, Naam huo ndio Ujumbe wao kwa uchache wanaouleta ili kuwasiliana na wale walo hai.
Na yanaendelea Mawasiliano haya mpaka kwa vitendo vile vile ikiwa umewaachia watoto (Nyumba)za kuuzia ulevi wao wataendeleza, ikiwa umewaachia (Nyumba)za kuja watu (Beach)kustarehe wao wataziendeleza, ikiwa umewaachia mapesa ya Haramu na wao watayatumia kiharamu haramu kama inavotakiwa, lakini ikiwa ulikua Mja mwema utapata mfano huu katika Quraan (Kahf 82)
وَأَمَّا ٱلۡجِدَارُ فَكَانَ لِغُلَـٰمَيۡنِ يَتِيمَيۡنِ فِى ٱلۡمَدِينَةِ وَكَانَ تَحۡتَهُ ۥ كَنزٌ۬ لَّهُمَا وَكَانَ أَبُوهُمَا صَـٰلِحً۬ا فَأَرَادَ رَبُّكَ 
أَن يَبۡلُغَآ أَشُدَّهُمَا وَيَسۡتَخۡرِجَا كَنزَهُمَا رَحۡمَةً۬ مِّن رَّبِّكَ‌ۚ وَمَا فَعَلۡتُهُ ۥ عَنۡ أَمۡرِى‌ۚ
Na Ama (kuhusu)Ukuta, ulikua (kwa)ajili ya watoto wawili mayatima katika mji Ule, Na chini yake kulikuwa na Hazina yao, Na Baba yao alikuwa (Mja)Mwema, kwa hivyo, Mollah wako alitaka wafikie Baleghe yao na wajitolee hazina yao, hiyo ni Rehma inayotoka kwa Mollah wako, Na mie sikuyafanya haya kwa amri yangu.
Naam ukuta umejengwa na Mja mwema, chini ya Ukuta kawacha hazina ya Halali, Nani atakae hifadhi Mali yako ya halali hakuna ila Mollah wako Mlezi, hawezi kukutunzia Hotel zako za Maasi, hawezi kuinusuru Mali yako ya Haramu, hazipiti Rehma zake kabisa, sasa kwanini yakafanyika hayo, sababu huyo Baba(Mzee)alikua Mwema, yeye keshakufa lakini ujumbe wa Rehma ya Mollah wake unaendelea kufanya kazi yake(Shauri yenu na wale wanopita wakakwambieni haifai hata kuwataja)mnapata hasara kubwa, Na hayo hayakufanyika kwa Elimu ya yule Mja alofatana na Nabii Musa a.s bali ni kwa amri ya Mwenye Enzi Mungu, Na hapo ndio tunapoigusa Hadith ilosimuliwa Na Imam Nabhani katika kitabu chake kinachoitwa (Al-Anwar Muhammdiyah).Endelea part 3




UJUMBE WA MAREHEMU PART 3

Asalaam Aleiykum,

Hakika palikuwepo Msichana wa kiyahudi, yeye alisilimu akaukubali Uislam kwa Ukamilifu na kuukamilisha Uislam wake, Baadae akafa katika Uislam, Alipokufa alikuja Baba yake na Mama yake kwa Bwana Mtume s.a.w wakamwambia Yaa Muhammad s.a.w sisi tunataka kufahamu nini hali ya mtoto wetu Akhera, hivyo kenda Peponi kwa ajili ya Uislam au Kenda Motoni.
Bwana Mtume s.a.w Akamuomba Mwenye enzi Mungu amteremshie (Ilham ya uthibitisho)Akawachuka wazee wale mpaka makaburini, wakasimama kwenye kaburi akaita Bwana Mtume s.a.w "Ewe Fulani Binti Fulani" Ikatoka sauti Kaburini, Naam Ewe Mjumbe wa Mwenye enzi Mungu, Akamuuliza Bwana Mtume s.a.w Ewe Msichana Wajibu wazee wako(Wanataka kujua hali yako)alisema nini wakati yeye yuko kwenye makaazi ya Salama ya (Barzaq)Akajibu yule Msichana Ewe Bwana Mtume s.a.w mimi simjibu Baba yangu wakati yeye bado Yahudi, Akasema Bwana Mtume s.a.w Kwanini? akajibu yule Msichana mimi nimemkuta Mollah wangu Bora kuliko baba yangu.
(Ewe Mollah wangu nilipogundua mimi katika Moyo wangu anakaa asiyekua wewe, basi nilifanya hima kuujaza uongofu wako, hata ikawa hakai asiyekua wewe) Nimemkuta Mollah wangu ana kheri zisomfano, Palepale wale wazee wakasema "Ewe Muhammad s.a.w Tunashuhudia Mwenye enzi Mungu ni mmoja na wewe ni mjumbe wake wa haki.
Naam nini hali yetu sisi tulosahau Dini yetu na wazee wetu wema walotangulia, inapaswa tuombe Dua hii "Ewe Mwenye kugeuza nyoyo, Zigeuze nyoyo zetu zisadikishe Dini yako"
Kasema Bwana Mtume s.a.w "Enyi watu Msiwahuzunishe Maiti zenu kwa matendo Mabaya" kwani Maiti ni wenye kutambua maasi ya walio hai. Ukenda kuzini au kudhulumu yeye anatetemeka huko aliko(Barzqh) mpaka Roho wenzie wanamuuliza vipi mbona hivyo, Anajibu alo wangu anakwenda kwenye maasi na akija kunyakuliwa Roho yake pale alipo kabla ya kutubu, mnajua kitamkuta nini?
(Al-Qariah-aya ya 10-11."وَمَآ أَدۡرَٮٰكَ مَا هِيَهۡ "
Ni nini kitakujulisha hiyo Haawiya,
"نَارٌ حَامِيَةُۢ"
"Ni Moto uwakao kwa ukali(Sana)" Ndio usiku unaota unasema "jana nimemuota Mama yuko pembeni mnyonge", asiwe mnyonge na kayaona Manyago yote, na yeye hana njia ya kukukataza ila anakujia kwa ishara ewe Mwanangu acha, basi tena umezama sana, Na ikiwa yeye ndiye mwenye matatizo atakujia na ishara chungu nzima za kukuonesha nitumie dua Mwanangu, niombee japo kidogo, na kama huzifahamu anaambiwa kiwapi, kama ulivo ishi wewe na yeye anaishi hivyo hivyo, basi wafanyieni Ihsani Maiti zenu kwa kuwakumbuka kwa dua japo mwaka mara moja, msiwatupe kabisa kabisa ikawa kama hawakupita katika Ulimwengu huu. Tizama mfano Mti wa Mbuyu au Nyumba ipo mwaka wa mia unaiona, vipi Maiti yako leo imekufa mwaka wa pili tu unaisahau. Wakumbukeni walo wenu na waso wenu kwa Dua, Na Mollah wenu atakukumbukeni kwa Rehma zake.

Sunday, December 15, 2013

TAFAUTI YA RAHA NA FURAHA PART 1

Asalaam Aleiykum,

Unaijua tafauti baina ya Furaha na Raha, vishawahi kukuta viwili hivi kwa wakati mmoja? Na kama huijui basi zinduka usingizini uelewe kuwa viwili hivi umbali wake kama Shamba na mjini, upeo wake mkubwa na inatakiwa kazi (Ya Ndovu na Mwanae)kuvikutanisha viwili hivi, Ikiwa Mja mwenye kutaka kufahamu na kutaka kujua ili unufaike kwa kuvipata vitu hivi viwili kwa wakati mmoja basi tuliza fahamu yako ili unufaike na darsa hii ya kukujulisha tafauti baina ya Raha na Furaha.
Kwanza kabisa napenda kukujulisha kwa hali ulokua nayo sasa hivi  ni vigumu kabisa kutafautisha nini Raha na nini Furaha, kwa hali ulonayo, inapokaa Raha furaha haionekani, vigumu Furaha kukufikia, na Inapokuwepo Furaha unakuwa ushaisahau Raha ndio maana Furaha ikimalizika unateseka sababu ni vigumu kwako kurejea katika hali ya Raha. Ukitaka kuyaelewa kwa uzuri mambo haya kwanza wacha nikuchukue katika Mji wa Furaha nikuoneshe mambo yake halafu nikupeleke kwenye mji wa Raha pia Ukashuhudie kukoje, halafu utaamua mwenyewe unataka kuishi katika Mji gani.
Hivi karibuni katika ziara zangu za nyumbani katika mji wa Mrima vijana waliniuliza swali niwape tafauti ya Raha na Furaha, Nikaanza kuwajibu kwamba Furaha ni kitu cha (Temproray)chenye kupita au kina kuja mara moja na kutoweka, hakidumu, na wewe ukichunguza utayagundua hayo, Furaha ni yenye kukaa kwenye Akili kwa muda, kwani si ushawahi kufanya harusi na ukiamka furaha zimekwisha, ukinunua kitu ukawa nacho muda mdogo tu furaha imekwisha, ukimuona rafiki yako wa siku nyingi unafurahi baada ya muda furaha imekwisha, iko mifano mingi furaha inavopita katika akili zetu kwa muda mchache, na zikitoweka furaha hizo tunakuwa wateja wakuzitafuta tena na tena mpaka 
tunasahau kuwa sisi tuna kitu muhimu tunacho ishi nacho nayo ni hiyo Raha ambayo mtu anatakiwa kwenda (Beyond)ili kuigundua tena hiyo Raha.
Kutaka kwenda kuigundua hiyo Raha itakubidi uteremke Bondeni, utoke juu Akilini uteremke taratibu moyoni kwenye raha za kudumu.
Endelea part 2 ujue nini Raha

TAFAUTI YA RAHA NA FURAHA PART 2

Asalaam Aleiykum,

Nini Raha?
Raha ni Maumbile yako yaloambatana na Roho, Roho ni kitu kisichopenda karaha wala mateso na mfano mkubwa jitizame au mtizame yoyote yule alofikwa na maradhi hali yake inakua vipi, yatizame macho yake uyaone yalivojaa huzuni. Neno Raha limehusiana na (Roho)na Raha ni hicho ulichonacho chenye kukufanya uishi kwenye Ulimwengu huu bila ya Bughudha yoyote, bila ya mateso yoyote, Raha kwa lugha ya kigeni ni hiyo (Blissful) Raha haina kikomo, maisha yako yote ni Raha, ila bado hujayajua, unazaliwa katika Raha ikisha wewe mwenyewe unapanda ngazi huyo unatoka moyoni kuelekea kwenye Akili, unalifata tunda halafu unalitafuna kwa hiyari yako tena kwa mbwembwe, na ukisha kula tunda hapo hapo Raha inakupotea, na si kama imeondoka laa bali unasahau.Raha ni (Nature)yako, kinachotakiwa ufanye kazi ya kuikumbuka tena.
Na sababu kubwa itakayokujulisha kuwa umetoka kwenye Raha na umekwenda kwenye furaha  bila ya kujijua ni pale (Mfano) umemuacha Mke au Mume umekwenda nje kwa (Kimada), ulikua nyumbani umo kwenye Raha mstarehe, unakwenda nje kutafuta furaha, zikisha furaha hizo unakua unazitaka tena,Sababu ni za muda na zishapita,  sasa ushakua (Confused)Furaha imekwisha na Raha huipati, unaanza kutaka kuijaza(Gap)sasa unakua mteja wa kuzitafuta Furaha, labda kwa huyu au kwa yule atakupa furaha, na hiyo ndio sababu kubwa mkaambiwa msikurubie hizo Furaha za nje, unatoka katika (Qadir)ya Mollah wako alokupangia ya Raha unakwenda kwenye uchaguzi wako wewe wa kutafuta Furaha, (Mfano)mwengine upo ofisini unapata Riziki yako kwa urahisi unaacha kazi yako na kuamua kuanza Biashara, Unatoka kwenye Raha unakwenda kwenye furaha, Wewe hayo maisha yako yalivo jione uko kwenye Raha, Unaamka na Afya yako, unakwenda kazini na kucheka na wenzako huna tatizo lolote kabisa mpaka unalala kiumbe wewe hakijakukuta chochote, hakuna Raha kama jambo hilo, unaupata usingizi bila ya vidonge, unakula bila ya matatizo, unahema pasi na maradhi yoyote, umekaa salama usalimini hizo ni Raha za pekee.(Angalia Mfano wa viumbe wenzio kama)Mkulima anavoishi kwenye Raha, hana haja ya TV wala Taa ameridhika na (Nature)yake, sasa jaribu kwenda wewe Shamba, ukiona vijidudu vinameremeta(Vinawaka waka taa)utaanza kupiga kelele (Mbu)wa Shamba wamebeba(Tochi). Mtizame Mchukuzi yoyote yule anafanya kazi yake karidhia uangalie usingizi wake, Tajiri na mapesa yake yote hawezi kuununua, Kila usiku Mkulima au Mchukuzi kwa jinsi anavopendwa na Mollah wake anapewa Mapumziko ya Raha, analala kama (Sultan kwenye Ufalme wa Mwenye Enzi Mungu na akitoka Usingizini anapewa nguvu mpya za siku ya Pili. Watizame watoto bado wako Moyoni hawana habari ya Furaha, ndio maana ukimkera analia akimaliza kasahau, wacha ukerwe wewe ionekane balaa yake, sababu uko kwenye furaha na huwezi kurudi kwenye Raha tena ndio unapanda hamaki, hutaki kusamehe, kumbe sio lile kosa bali ni tafrani zako za kuwa huishi kwenye Raha, Raha kuamka Mollah kakuchangania na Furaha,kwenye Nafsi una Raha, mfukoni una furaha, Kwenye Nafsi umebarikiwa utulivu, kwenye maumbile umepewa sehemu na mahala pa kupumzikia hizo ndio Raha, ikiwa umepewa japo chembe ya mapenzi basi jijue umepewa Raha, Na raha zikizidi ndio utakuta mpenzi (Anaandika barua sasa mimi mwenzio sili wala silali)na hilo ni kweli kabisa unajua kwanini hali wala halali, kwa sababu anaona Raha, keshafika kwenye Roho yake na Roho hailali wala kula,(Kwa hiyo ni kweli halali wala hali)usidhani ni muongo, huyo yuko kwenye Raha, hajali mali wala kufilisika na wewe ukiishi kwenye Raha utakua  mtu wa aina hiyo, utakua huna (Attachment)ya kitu chochote katika Ulimwengu huu, huna habari ya kulimbikiza mali wala kuwa na (Account)ilonona, hutaki majumba wala magari ya kifahari, na unajua jambo moja muhimu kabisa nalo ni (You Belong to no one, and no one Belong to you)ukiwa katika hali kama hiyo wewe unakua uko katika ile njia ya (Balance)Ulimwenguni hupo na Akhera hujafika, hapo ndipo inapoishi Raha, na ukiwepo pahala hapo unakua simwenye kutenda dhanmbi kabisa, unakua Mja wa Huruma, mpole na kazi zako ni za kheri tupu.
Na hapo unaambiwa kwenye sura ya Rumi aya ya 15
فَأَمَّا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ وَعَمِلُواْ ٱلصَّـٰلِحَـٰتِ فَهُمۡ فِى رَوۡضَةٍ۬ يُحۡبَرُونَ
Wale waloamini na kutenda mema watafurahishwa katika Bustani.
Endelea part 3

TAFAUTI YA RAHA NA FURAHA PART 3

Asalaam Aleiykum,

Kuamini kuko moyoni, kuamini ni Raha katika mamlaka yake, ndio maana utaona mtu atachukua kila kilicho chako lakini hawezi kuchukua Imani yako, kuamini ni Raha, ndio utakuta mtu yuko tayari kufa kwa Imani yake, Raha ilioje anauliwa kakamata kamba ya Mwenye Enzi Mungu, ndio maana unamuona mwenye Imani ya kweli anakua ni mwenye kutenda mema, anakua mwenye huruma, anakua mpole, ana mapenzi matupu, ni mwenye kusaidia wenzie na anayafanya hayo yote kwa kuona Raha kwa ajili ya Mwenye enzi Mungu wake, basi hao kabla hata ya kufunga Macho wanafunguliwa pazia na kuwaonesha furaha zinazo wasubiri huko wendako, kwa sababu wao kuishi kwao kote katika Ulimwengu huu walikua wameitambua Raha kwa njia ya siri, wakaridhi (Qadara)ya Mollah wao, wakaamua kumtii Mollah wao na kuyafata aliyoamrisha, ikawa wao wakiumwa au wakiwa wazima wanamkumbuka Mollah wao, wakilala au wakiamka wako karibu na Mollah wao, na kuwa karibu ya Mollah wako ni kuzipata Raha zisizo mfano, na kuwa karibu ya Shetani unapata furaha yake lakini ni yenye madhila makubwa, yenye shida kubwa, basi ukitaka kugundua hilo wewe endelea na (Picnic)zako, ukiamka furaha imetoweka, piga mtindi ukiamka unaumwa, nenda (Shopping)ukirudi umenuna pesa zishakwisha, cheza ngoma ukiamka magoti yanachemka, Imba usiku kucha , ukiamka sauti haipo tena, jaribu kufanya utafiti uyajue yepi ya furaha za muda mfupi, na yepi yenye Raha za kudumu ili uyakamate, ukihangaisha Akili yako utayajua hayo moja baada ya jengine, kumbuka Furaha ni ya Muda Mfupi, na Raha ni yenye kudumu.Uchaguzi unao wewe.

Sunday, December 8, 2013

HAKUNA SHEIKH-A-KAMA WEWE PART 1

Asalaam Aleiykum,

Baada ya kusoma sifa za Majina ya Mwenye Enzi Mungu nimeona kuna haja ya kurejea katika Darsa zetu za kawaida ili tuendelee kupata faida za kawaida za matunda ya dini yetu, leo hii tunaitizama Ihsan na fadhila kubwa tuloipata katika dini ya Kiislam kutoka kwa Mtume s.a.w pale alipo wacha kumchagua kiongozi wa kuindeleza Dini hii, alijua hii Dini ya Haki na italindwa na Mwenyewe alomtuma kuufikisha ujumbe huu, isionekane kwamba hakufanya uteuzi laa, alifanya uteuzi lakini ulikua wa Kisiasa kwani yeye alikua ni Mjumbe wa Mwenye Enzi Mungu na pia Mkuu wa Dola ya Kiislam, kama Mkuu wa Dola na kiongozi wa Waumini aliteua Magavana(Governor), lakini kwa upande mwengine kama Mjumbe wa Mwenye Enzi Mungu alikaa kimya na hivyo ndio walivofanya Wajumbe wote kabla yake.
Hakuchagua Khalifa au huyu awe Sheikh wenu, Hakuchagua Mchungaji wala kuwepo na Muangalizi, ila yeye alipewa na kufahamishwa maneno na Mwenye Enzi Mungu kuwajulisha Umma wake yakwamba Dini ni (Indivisual)mtu pekee, huna haja ya kushikiwa dini yako, na kama utayafahamu maneno hayo (In-deep understanding)basi kuanzia leo hutotaka mtu yoyote awe Sheikh wako au kuwa Imam wako, yatosha wewe Mwenyewe kuifanya kazi hiyo, na wala usitafute mtu wakukusomea dua na hivi na vile.
Utayafanya Maombi hayo kwa uchache au kwa wingi bila ya kutegemea yoyote, lakini cha msingi mpaka haya maneno yapasue akili yako huku ukiambiwa(Babu jinga inama ufikiri dini yako unashikiwa), kabla ya kuyagusa maneno hayo(Adhimu)Naomba nikumbushe kitu kuhusiana na Mtume s.a.w alivokua anapenda Usawa, Haki, na Uongofu, ndio  mpaka leo ukaona wale alokua nao pamoja wakati ule hawakuitwa wanafunzi wake, au wafuasi wake bali walikuwa wakiitwa (Masahaba zake)Marafiki zake.
Nani Rafiki?
Rafiki ni mtu ambaye yuko karibu na  akishirikiana na wewe katika mahusiano ya kiroho, Ikiwemo furaha na Misiba, kwenye shida na Raha zote, Rafiki ni Mwenye kukushauri katika mambo yote ya wema, na hana shaka wala wasiwasi juu yako kwenye jambo lolote la Ukweli, Kinyume na hayo anza kutilia wasiwasi Urafiki wenu.
Sasa twende tukahudhurie hayo maneno aloteremshiwa Bwana Mtume s.a.w ili tupate kujua vipi na wewe utakua Sheikh, wacha leo tuondoshe Viburi vya wale wanodhani Dini ni Mali yao, wacha tuwafichue wale wanotumia migongo ya wenzao kuwapanda na kuwadanganya na kuwadharau wenzao, kuendelea kuwabagua na kuwatenga, kuzidi kuwalaza ili wapate kuonekana wao ndio wenye kujua na wanayo mamlaka kamili ya uwezo wa kumpeleka mtu peponi, na maandalizi yote wanayo wao, napenda uelewe katika Uislam hakuna kitu kama hicho,na ukimgundua mtu ana nyendo kama hizo basi mkimbie haraka sana.
Endelea part 2 

HAKUNA SHEIKH-A-KAMA WEWE PART 2

Asalaam Aleiykum,

Al-Hujurat (13) يَـٰٓأَيُّہَا ٱلنَّاسُ إِنَّا خَلَقۡنَـٰكُم مِّن ذَكَرٍ۬ وَأُنثَىٰ وَجَعَلۡنَـٰكُمۡ شُعُوبً۬ا وَقَبَآٮِٕلَ لِتَعَارَفُوٓاْ‌ۚ إِنَّ أَڪۡرَمَكُمۡ عِندَ ٱللَّهِ أَتۡقَٮٰكُمۡ‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ۬ 
"Enyi Watu hakika tumekuumbeni Wanaume na Wanawake na tumekufanyeni Mataifa na Makabila(Mbali mbali)ili (Mpate)mjuane(Tu)Hakika ahishimiwaye sana(Mwenye cheo na daraja)miongoni mwenu mbele ya Mwenye enzi Mungu ni yule amchaye Mungu zaidi katika nyinyi,(Mwenye mapenzi na Mollah wake) Hakika Mwenye enzi Mungu ni mjuzi, na Mwenye habari."
Huna haja ya kujifanya fanya wewe una msimamo au ndio uko katika usawa, Mollah wako anajua kila kitu anazo habari zote mpaka katika kifua chako kuna kitu gani, huna haja ya kudanganya, wala usimwachie mtu akakudanganya kukwambia wewe ndio pekee unafanya sawa wengine wote sio sawa, kazi hiyo mwachie Mollah wako ndie atakae ifanyia uamuzi, unachotakiwa wewe uombe Imani ikujae kwenye nafsi yako, na Imani ikikujaa unakua huyumbi, unakua ushaupata ukweli, Na ukiujua ukweli hutaki tena kushikiwa Dini yako, unakua hutaki Sheikh yoyote, au mjanja yoyote wa maneno akusogelee, Bali wewe mwenyewe unageuka kuwa huo ukweli, na kila unapokuwepo unauwakilisha huo ukweli, na ukweli wenyewe ni huo Uislam na matendo yake.
Basi Mwenye kuujua ukweli ndio anaambiwa "Enyi Watu" tumekuumbeni Wanaume na Wanawake katika tafauti ya Maumbile tu, lakini katika jumuiko la (Roho)nyote sawa,  Tafauti yenu katika maumbile ambayo yana dhumuni maalum, ama katika mambo ya Nje Mwanamme yeye ndie Mwenye dhamana, na kuhusu mambo ya ndani Mwanamke anachukua madaraka kamili, kama Mwanamme anapigana vita ya Mpakani, Mwanamke anapigana vita ya Moyoni ambayo ndio nzito zaidi kuliko ya mpakani, Mpakani ukipigwa risasi kazi yako imekwisha, lakini ya moyoni kifo chake ni taratibu, machungu yake ni ya muda mrefu, ndio maana utakuta Mwanamke mstahamilivu anabeba mimba na huku mtoto anaumbwa ndani ya tumbo lake kwa muda wa miezi tisa, yote hayo Wanaume tunayajua na ukipata kuyajua hayo basi utafahamu kuwa sisi sote ni viumbe na inapaswa kuheshimiana.
Tukakujaalieni Mataifa na Makabila na hilo kama Muumin unalifahamu ni kwa ajili ya kujuana tu. 
 Kujuana(Knowing) Ipo kwenye Akili, na Akili ni nyenzo ya kutumika kwa mahitaji ya kuishi siku hadi siku, Lakini kipo cha zaidi ambacho kitu hicho nyote mnakutana kwenye (Level)moja, hakuna huyu Mweupe huyu Mweusi, huyu kabila fulani yule kabila hili, huyu ana cheo hichi yule ana utajiri huu, katika (Level) hiyo Muumin wa kweli ambaye kaamini kwa dhati huondosha Kiburi chake, anafahamu pahala hapa niache jeuri zangu, pahala hapa mimi si chochote,pahala hapa niwache kuwadanganya wenzangu, pahala hapa mimi sina madaraka yoyote  ya kumjua nani mwema na nani mbaya, Nani kashika dini na yupi kaichia, Na pahala hapo ndio sote tunapokutana kwenye Mamlaka ya (Kiroho)Na Mfano midogo ipo (Angalia sote tunakula uwe tajiri au maskini, sote tunavuta pumzi, sote tunalala, sote tunaongea, sote tunacheka, sote tunatembea, sote tuna ndoto zetu, sote tunaona na kusikia, sote tuna majina na mengi mengineyo)basi haikujii fikira ewe Mwanaadamu kwamba kuna pahala tunakutana, na pahala hapo ndipo pekee penye Mamlaka ya kujua kwamba kiumbe anatenda kheri au shari, nani mwenye msimamo na yupi hana, Sala yake inakubaliwa au haikubaliwi, dua yake imefika au haijafika, kwa hiyo asizuke mtu akakupeni habari yeye ni mwenye kujua dua au anajua njia za kukupeleka peponi, au yeye yupo kwenye kabila fulani au kikundi fulani ambacho ndicho kinakubalika hakuna kitu kama hicho kabisa, ndio maana aya ikasema dhumuni lake la huo Utaifa na ukabila ni kujuana tu, na wala halina kazi nyengine.
Endelea part 3



HAKUNA SHEIKH-A-KAMA WEWE PART 3

Asalaam Aleiykum

Hakika mbora wenu Mbele ya Mwenye Enzi Mungu ni yule Mwenye vitendo vya Mapenzi juu ya Mollah wake, ni yule mwenye Mapenzi na Mollah wake(Taqwa)Na Ukimpenda Mollah wako unakua si mwenye kumsahau hata dakika moja, na hiyo ndio alama kubwa ya mapenzi ya Mwenye Enzi Mungu, na ikiwa kweli umefika katika daraja ya Mcha Mungu basi kwenye masaa 24 isikupite hata dakika kumsahau Mollah wake, na ukishindwa kufanya hivyo basi wewe umo tu kwenye kundi la wale wenye kujitahidi.
Utakapofikia Daraja hiyo basi jua hakuna Sheikh kama wewe, hakuna Imam kama wewe, lakini ikiwa kinyume na hayo jijue wewe bado na wacha kuwapumbaza wenzako, wacha kuwapa (Boarding Pass)za pepo ya uongo wenzio, unafanya jambo la hatari litakuangamiza, Kwani aliye kipenzi cha Mwenye Enzi Mungu ni yule Amchaye, na Mcha Mungu wa kweli  ndio huyo mwenye kuishi na huo ukweli, ambaye keshakutana na mambo ya Mwenye enzi Mungu, kashaoneshwa Taa ya Mollah wake ambayo inamuongoza akiwa sokoni yeye yupo na Mollah wake, akiwa darasani yuo na Mollah wake, akiwa na family yupo na Mollah wake, akiwa kwenye halaiki za siasa yupo na Mollah wake, kila aendapo yeye ni mwenye Kumkumbuka Mollah wake, huku anakua kavaa taji la sifa ya upole na ukarimu, si mwenye kumbagua yoyote, unapomkuta Wallahi utaona Nuru ya Rahiim inammurika, huyo ndio anofaa kuwa Mwalimu wenu, huyo ndio anofaa kuwa Sheikh wenu, kuwa Imam wenu, kuwa kiongozi wenu, kinyume na hivyo itakua nyote mnapotea.
Hakika Mwenye enzi Mungu ni mjuzi(Wa hayo yote)na ni mwenye habari zote, anakujueni mnavopanga mipango yote ya njama za kujiona nyinyi bora, anafahamu mbinu zenu za kutaka kuwashikia wenzenu dini yao, eti dua lazima uombe wewe ndio iwe kubuli, hakuna kabisa kitu kama hicho katika Uislam.hakuna mwenye kuijua siri hiyo katika dini ndio katika aya ya (11 ya sura hiyo hiyo ya Hujurat)Inasema,
يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ لَا يَسۡخَرۡ قَوۡمٌ۬ مِّن قَوۡمٍ عَسَىٰٓ أَن يَكُونُواْ خَيۡرً۬ا مِّنۡہُمۡ وَلَا نِسَآءٌ۬ مِّن نِّسَآءٍ عَسَىٰٓ أَن يَكُنَّ خَيۡرً۬ا مِّنۡہُنَّ‌ۖ وَلَا تَلۡمِزُوٓاْ أَنفُسَكُمۡ وَلَا تَنَابَزُواْ بِٱلۡأَلۡقَـٰبِ‌ۖ بِئۡسَ ٱلِٱسۡمُ ٱلۡفُسُوقُ بَعۡدَ ٱلۡإِيمَـٰنِ‌ۚ وَمَن لَّمۡ يَتُبۡ فَأُوْلَـٰٓٮِٕكَ هُمُ ٱلظَّـٰلِمُونَ 
Enyi Mloamini Wanaume wasiwadharau Wanaume wenzao,Huwenda wakawa bora kuliko wao, Wala Wanawake wasiwadharau Wanawake wenzao, Huwenda wakawa bora kuliko wao,(Na)Wala msitukanane kwa Kabila, wala msiitane kwa majina mabaya,(Na)Jina Baya kabisa kuambiwa Mtu ni asi baada ya kuwa ni Muislam,(Na kufanya hivyo ni Dhanmbi)Na wasotubu basi hao ndio Madhalim,(Wamedhulumu nafsi zao kwa kuipinga amri ya Mollah wao).
Kama mna Imani ya kweli, basi sikieni maneno ya Mollah wenu, na kama husikilizi kaa peke yako ujiulize wewe uko kundi gani?Basi ikiwa unaendelea kumsikiliza Binaadamu mwenzako hilo ni shauri lako, Na huenda hao mnaowadharau mkawaona sio Masheikh wakawa bora kuliko nyinyi, Na wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao huwenda wakawa bora kuliko wao, wala msitukanane kwa kabila, au kikundi fulani wakajiona sisi bora kuliko wale, yote hayo ni maneno msihadaike na maneno hakuna anojua yupi bora, hakuna anoshushiwa (Wahyi)akaambiwa nyinyi ndio mnokwenda Peponi yote hayo ni maneno, usikubali kuyumbishwa na maneno mazuri, kumbuka nyuma ya maneno mazuri kuna ubaya ulojificha, fanya uchunguzi utalijua hilo.
Na hakuna jina baya kama ukipita ukamtangazia mwenzio yule asi, yule si Sheikh, yule kafiri, yule jinsi kadhaa wa kadhaa, ikiwa unayatenda hayo basi jijue wewe mwenyewe ndio asi mkubwa na unataka dawa ili upone, na wala usifikiri huo ni Ucha Mungu, huko ni kuingia hasarani, na unatakiwa utoke kwenye kundi hilo na utubu kwa dhanmbi zako hizo, Rejea kwa Mollah wako Uwe Mcha Mungu upate daraja ya watu wema, Uwe katika watendao mazuri, upate cheo cha hakuna Sheikh kama wewe, hakuna Imam kama wewe, na hicho ndio cheo kikubwa kukipata hapa Ulimwenguni, Na hicho ndio cheo cha Ucha Mungu ambacho sote tunatakiwa tupigane kukipata, na ukisha kukipata wewe utakua umeipata Nuru ya Mwenye enzi Mungu, lakini hivi sas kwa wakati huu bado umo kwenye kuiona Taa, ondoka katika taa ukaione Nur -ala-Nur, Na hayo ndio mafanikio makubwa ambayo sote tunayataraji kuyapata.
Tunamuomba Mollah wetu atuwezeshe kuipata Nur yake.

Sunday, December 1, 2013

MAJINA YA MWENYE ENZI MUNGU(SHAKUR)PART 1

Asalaam Aleiykum,

Hakuna Jina lenye Ibada yenye kumridhisha na Mollah na kumfurahisha Kiumbe kama jina hili la (Shakur)
Mwenye Kushukuru, Ndio Maana hata kwenye ufunguzi wa Sala Unaanza kwa kushukuru(Alhamdulillah)Namshukuru Mollah wa viumbe vyote, Hapana apasae kuabudiwa na kushukuriwa isipokua Mwenye enzi Mungu wa haki. Kila kilichomo katika matendo yako kinastahiki shukran kwa ajili ya Mollah wako, Yeye ndiye aliyekupa Uhai kwa Mapenzi yake, Una nini wewe cha kumlipa isipokua hiyo shukurani ya dhati itokayo kwenye Moyo wako.
Wewe Shukuru kwa wema na Ihsani aliyokufanyia kakupa Afya na Mali, Kakupa Majumba na Magari ushakaa na kuyafikiri hayo halafu ukajaa furaha Moyoni yenye kutambua katika wengi wa viumbe vyake Mollah kanichagua mimi kunipa haya nilonayo, Usipewe hayo basi mengine ambayo unachukulia kwa mzaha kama vile umetoka usingizini mara ngapi unakumbuka umetoa Shukurani kwa kuamka kwako na ukasema(Alhamdulillah).
Jee labda umemaliza kuozesha Mwanao umekumbuka kutoa Shukurani kwa Mollah wako na kusema nakushukuru Mollah wangu kazi yangu ya ulezi ulonipa nimeimaliza salama, Jee siku ulopata hicho cheo umekimbilia Msala peke yako ukamshukuru Mollah wako, usiogope najua umemshukuru (Boss)wako mie nakukumbusha tu Jina la (Shakur).
Sasa una Afya nzuri maradhi yametoweka jee unakumbuka kila wakati kumshukuru Mollah wako, au unasubiri mpaka uanze kuumwa tena ndio uanze (Toba Yarabi), Umekaa peke yako ikakujia kushukuru kwa ajili ya kuumbwa tu kwenye Ulimwengu huu, Ishakujia fikra kuwa hata utakapo kufa basi Mollah wako atakufufua tena akupe Uhai kwa Mapenzi yake, ushawahi kushukuru kwa jambo hilo.
Ushawahi kushukuru kwa ajili ya kupewa Elimu na Akili ya kuyajua mazuri yaliyomo kwenye Ulimwengu huu ukayafurahia. Basi elewa hakuna mwenye kustahiki kushukuriwa kwa haki isipokua Mollah wako aliye Mkarim.Isiwe unasubiri mpaka upate kitu kizuri ndio Ushukuru lazima kila siku iwe siku ya Shukura kutoka kwako kwa ajili ya kupewa kwako maisha haya unayoishi. Mollah wako si mwenye kuhitaji shukurani yako, lakini kila ukishukuru moyo wako unazidi kuelekea kwake Muumba wako na hiyo ndio Ibada kama inavosema aya ya 66 sura ya Zumar,
بَلِ ٱللَّهَ فَٱعۡبُدۡ وَكُن مِّنَ ٱلشَّـٰكِرِينَ 
"Bali Muabudu Mwenye Enzi Mungu na uwe Miongoni mwa wenye kushukuru"
Na ukaendelea kukumbushwa kwenye sura ya Baqarah aya ya 152 inasema:endelea part 2

MAJINA YA MWENYE ENZI MUNGU(SHAKUR)PART 2

Asalaam Aleiykum,

فَٱذۡكُرُونِىٓ أَذۡكُرۡكُمۡ وَٱشۡڪُرُواْ لِى وَلَا تَكۡفُرُونِ 
"Basi nikumbukeni,(Namie)Nitakukumbukeni, Na Mnishukuru wala msinikufuru"
Ukianza kulitumia jina la (Shakur) au mengine yote unakua unafanya vitendo viwili kwa wakati mmoja kwanza unakumbuka halafu unatumia maana ya hilo neno, kwa hiyo nikumbukeni, nani umkumbuke Mollah wako, nini ukumbuke (Ya Shakur) uwe mwenye kutoa shukurani, Nini kitatokea na yeye atakukumbuka na hakuna fadhila ilo bora, raha isokwisha kama kukumbukwa na Mollah wako.
Yeye Mollah wetu ni mwenye kutukumbuka kwa mapenzi yake, basi anastahiki Shukurani zetu hususan tukikumbuka pale ndugu na jamaa wakishakukufikia ardhini wewe unabaki na nani? Mshukuru Mollah wako yeye ndiye (Shakur). Mshukuru Mollah wako aliyekupa uwezo wa kufikiri, kuona kusikia, na kuzungumza, yeye yuko pamoja na wewe kila wakati kwa hiyo wajibu wako kumshukuru.
Mshukuru yule ambaye bila ya kunyoosha mikono anakupa kila zawadi katika Ulimwengu huu, kuanzia chakula, afya, pumzi na kila kitu, huyo ndiye anayestahiki kushukuriwa na kila kiumbe, kaa kila wakati ukikumbuka fadhila zake kwako zisizokua na kipimo basi kila ukikaa kumbuka yuko alokuumba na anastahiki kushukuriwa.
Na ukitumia Jina hili la (Shakur) litakupeleka kumjua Mollah wako kwa undani zaidi, na furaha ilioje kumjua Mollah wako kupitia sifa hii ya Shukurani.