Nani Mcha-Mungu?.
Naam itizame aya inofatia inasema nini na kwanini?mwanzo ilianza na mawalii wa Mwenye-enzi Mungu halafu hapa inataja hivi:

Ambao wameamini na wakafanya vitendo vya Taqwa:
Nini imani?
Kwa tulivo mimi na wewe imani ipo kwenye zile nguzo sita ndio maana utaona tumekubali tu lakini hatuijui nini Imani, kwa kuwa tupo kwenye nguzo, zikiyumba tunazini, zikitingishika tuna kula rushwa, tunasema uongo, tunadhulumu hizo ndizo nguzo zetu, na ukiulizwa unasema naamini vitabu vyake, naamini Mitume yake, naamini Malaika wake, lakini ni mdomo mtupu, hiyo si Imani ila huko ni kukubali kwa hiyo unakua huna mashiko yoyote, Jitizame mwenyewe usianze kubisha kabla ya kujitizama halafu ukigundua kama uko mweupe basi anza safari ya kujiunga na wacha Mungu kwa kuitafuta nini imani.
Sasa nini kafanya Mcha-Mungu hata akaitwa kaamini?
Mcha-Mungu kapiga kachumbe hakukubali kubakia na nguzo kenda (Deep) kwenye msingi, na nini kitokujulisha huo msingi wa Imani, hakuna chengine isipokua msingi wa hizo nguzo ni (Tawhid) hapo ndipo alipofika Mcha-Mungu na wewe unaitwa huko.
Qur'aan nzima inakuita katika msingi huo lakini kwa kuwa una pita juu juu hupati kitu unabakia kukusanya mahadithi wala hujui maana yake unakua (story teller) hebu jiulize umeshawahi wewe kuisoma Qur'aan ikakwambia (hakika katika kuutoa usiku na kuuwingiza mchana kuna dalili zetu) hebu pata japo siku moja upate kuuona usiku unavomalizika na asubuhi inapoingia tulia upate kujua nini kinatokea, au subiri uone magharibi ishaingia na mchana haujatoka vitu viwili hivo vimekutana ili upate kujua miujiza iliopo hapo.
Imani yako itageuka kabisa, au kama hayo makubwa japo pata kutawadha, maana yake sala ngumu, basi kutawadha hebu kamilisha udhu wako, hata udhu hupati , wazee wetu wakiibaadhi walikua wanatwambia udhu ni ibada unajua wana maana gani, waligundua kuwa maji yanafanyika kwa gas mbili yaani (Hydrogen na Oxygen) lakini hizi mbili zote zinapatikana hata hospital lakini kwanini haziwi maji, ni lazima kipatikane hichi cha tatu ukigundua nini hicho kitu cha tatu, basi udhu ukakamilika kikweli utajua kama udhu ni Ibada, au ni kutia maji tu kama unavofanya sasa hivi.
Basi kama umeshindwa na udhu jaribu kwenye chakula, hata kula umesahau jiulize una meno thalathini na nne (34), mbona unatafuna chakula mara tatu tu, hujiulizi kwanini.?
Mambo yako mengi sana yakukutupa katika msingi wa(Tauhid) na wala usione vibaya au ukawa na woga katika kujenga Imani yako hata Mitume waliomba wasukumwe katika msingi wa (Tauhid)wasukumwe vipi, "Anasema Nabii Ibrahim katika sura ya Baqara(aya-260) "Nioneshe vipi unavofufua wafu,Mollah wako akasema: kwani huamini, akasema nataka kuutosheleza moyo wangu,(nipate kuridhika)Akasema Mollah,chukua ndege wanne na wazoee(wahifadhi)ikisha uwachinje uwaweke kwenye juu ya kilima,kisha waite,watakujia mbio.
Huyo ndio Mtume na rafiki wa Mollah wake na yeye anataka kuuridhisha moyo na visa ni vingi kikumbuke pia kisa cha Nabii Musa a.s na wengine.
Sasa ikiwa wao wametaka matumaini ya msingi wa tauhid nini hali yako wewe wakati Quraan aya chungu nzima zina kwita ili zikuthibitishie imani yako, lakini umekua mkaidi hutaki kabisa kuchupa ukaanza safari ya ucha Mungu kwanini?.
Kwani hujaambiwa kwenye Quraan katika aya inosema na atazame mwanaadamu chakula chake, sisi ndio wenye kukisababisha,jee hivo ushapata kukila chakula hasa ikakujia fikira kama mimi nikikikosa kwa miezi mitatu chakula hichi nakufa, ushauliza swali hilo kwenye nafsi yako?
Lakini usende huko mbali wewe umesahau hata kula basi anza kwa kujiuliza kwanini umepewa meno 34 na unatafuna chakula mara tatu tu, sasa hayo meno 31 yako holiday,anza na mambo madogo madogo kama hayo ikisha makubwa yatafatia baadae.
Nakupa ahadi moja ukisha kuchupa msingini hutotaka kutoka tena. Ipitie aya ya (Fusilati 53)ukathibitishe maneno haya ninayo kwambia.
Neno la pili la aya hii linasema ikisha wakawa watu wa taqwa: Wafanyao vitendo vya Taqwa.
Nini Taqwa?
Taqwa ni vitendo vya mapenzi, unapoigusa imani basi tambua inakugeuza unakua mtu wa mapenzi,mtu wa hisia, kila kitendo chako kinakua cha mapenzi yaani (Taqwa)tupu, kama nini huwezi kabisa kuwaona jirani zako na watoto wake wanalala na njaa wewe huku umeshiba na ukisha unasali naye ubavuni, Mcha-Mungu hawezi kuchukua itamkera usiku kucha, inakuingia huruma, ikikuingia huruma unaona imani, ukiona imani unataka kusaidia ukisaidia unafanya kwa mapenzi,ndio maana nikaiita (Taqwa)ni mapenzi,unatizama mayatima kwa mapenzi moyoni mwako,unakwenda kutizama wagonjwa kwa ajili ya mapenzi moyoni mwako,unasaidia watu kwa njia ya mapenzi hutaki malipo wala sifa au watu wengine wajue.
Sio kama sisi watu wa kawaida hisia inakuja siku moja tu kwenye umri mzima eti labda ufiwe na mwanao au mkeo,au afe mume hapo utaona mtu vipi anovosawajika kwa hisia za uchungu, napenda kukujulisha hisia kama hizo zinaweza kukujia wakati unasali,au umekwenda kumtizama mtu mzima mgonjwa nk, ukiona hisia kama hizo zinakujia katika vitu vidogo vidogo kama hivo basi jijue upo ukingoni na wakati wowote unaweza kuchupa.
Katika ulimwengu huu tunokwenda nao hatuna imani wala hisia ndio maana utaona unadhulumu, unakula rushwa, na mengi tuyafanyayo sababu moyo ushakufa hamna imani (Taqwa)mapenzi yatatokea wapi, ndio maana hata mkeo au mumeo ukimwambia unampenda inatokea mdomoni tu haifiki moyoni, wallahi kama itakua inatokea moyoni kweli kweli basi katika nyumba yako hayatokei matatizo kabisa wewe jaribu na utanikumbuka itoe katika moyo uone mambo yanavobadilika.
Nakwambia hivo sababu imani na mapenzi ni kitu kimoja chenye pande mbili,kwa hiyo mtu wa (Taqwa)anageuka yeye mwenyewe kuwa mapenzi,na akisha kugeuka hivo utaona mpaka vinyama vinampenda,analisha sisimizi akiwapa sukari,akiona ndege anawapa mtama,akiona maskini yeye wa mwanzo kukaa nao,hampiti mzee ila hutaka kumsaidia,vitendo vyote huwa mapenzi matupu,Mcha Mungu hawezi kutenda kinyume cha mapenzi,akicheka penzi tupu,akisema maneno ni kheri ilo jaa mapenzi, tahadhari msomaji usije ukatafsiri mapenzi haya katika fikra zako zilojaa kichwani mwako(kumbuka hayo ni matamanio).
Hiyo ndio Taqwa ilokusudiwa na tafauti yako na Mcha Mungu inakua hivi yeye akiswali anafanya hivo kwa ajili ya mapenzi ya Mollah wake,sala yake imejaa shukura na furaha na unyenyekevu wakuona Mollah wake kamuumba ikisha kamleta kuwa karibu na sasa anazungumza na Mollah wake.
Jitizame wewe unahangaika kumjulisha malaika wa thawabu kuwa sasa una sali hasara kubwa ilioje ikiwa tutabaki katika daraja hii.
Na aya inamalizia kwa kusema:

Wao wanabashiriwa mambo katika hii dunia:usije ukadhani (bishara)yenyewe kama utabiri laa, wanabashiriwa kwa kuondolewa pazia katika hii dunia wakawa wanajua mambo,wakawa wanaona mambo,ndio maana utakuta Mcha-Mungu anaweza kukwambia fulani mie nimebakisha siku tatu ukiniacha London au ukinipeleka Zanzibar nina siku tatu.
Naam kweli baada ya siku tatu utaona huyo kajiondokea na kama utahudhuria katika sakarati mauti yake basi utakuta yumo furahani anakwenda kukutana na Mollah wake, Na uzuri zaidi na huko endapo pia keshajua mapokezi yake yatakuje na wape anaondoka bila ya khofu wala huzuni,anaondoka huku anaaga.
Na ikiwa una shaka kwani hujaisoma ile aya inosema (na sisi tuko nae karibu zaidi lakini hamtuoni),basi hayo ndio Mcha-Mungu anobashiriwa akiwa hai, Na huo ndio (mwenendo)ulokwisha kupangwa wala si wenye kubadilika na huko ni kufuzu kuliko kukubwa kuwa kipenzi cha Mollah wako,kupanda daraja kulikoje ambako hushuki tena ukawa mtu wa chini,hizo ndio fadhila za Mcha-Mungu.
Naomba kwa Mollah wangu atufikishe katika daraja hizo ile tuwe karibu yake tupate ladha na nuru ya wacha Mungu.
Na Mollah wangu ndie ajuae zaidi
Mwenzenu.
Abdulla Baja
No comments:
Post a Comment